Saturday, May 7, 2011

Tatizo ni mazalia ya mbu na sio kukosa chandarua tu!

Malaria haiwezi kutoweka kwa vyandarua vya msaada


KATIKA miaka ya 1960 ilikuwa ni jambo la kawaida kwa ofisa afya wa mji kutembelea kila kaya na kuhakikisha kuwa wakazi wa kila nyumba wako salama na imara kiafya. Mojawapo ya kazi zilizofanyika ilikuwa ni kunyunyiza dawa ya kuua mbu wa malaria.

Kwa maneno mengine, kabla na miaka michache baada ya Tanganyika kupata uhuru watumishi wa serikali ya kikoloni na serikali mpya ya Waswahili zote zilifuata utaratibu wa kuwaangamiza mbu kama njia ya kupambana na ugonjwa wa malaria.

Ninalikumbuka jambo hili vizuri kwa sababu ofisa afya aliyekuwa akija nyumbani kwetu alikuwa ni Kaburu, mzungu mwekundu, mnene mwenye malaika rangi ya njano mikononi na miguuni. Naye alikuwa ameoa mwanamke wa Kichagga na aliishi eneo la Njoro. Nadhani huyu ni yule kaburu mzuri maana alikuwa hana msamaha na yeyote aliyechangia kuhatarisha afya ya wanajamii wenzake kwa mfano kuacha madimbwi ya maji ovyo karibu na nyumba au kutupa makopo na vifuu shaghala baghala.

Nilikuwa nikimuona haraka haraka nilikimbilia ndani kuitungua kadi iliyoning'inia ukutani ili aiwekee 'tiki' kila alipohakikisha kila jambo liko kama inavyotakiwa ili kulinda afya za wakazi wa nyumbani kwetu.

Halmashauri za miji zilionyesha wakati huo sio tu dhamira bali vitendo vyenye uchungu na uchu wa kulinda afya za wakazi wake.
Kumbukumbu hii njema ya mtumishi wa serikali ambaye anajituma na anajitolea kwa hali na mali kuhakikisha kuwa jamii haipati madhara kutokana na uzembe wa mtu mmoja au watu wachache imedumu nami hadi wa leo.

Pengine ndiyo maana wakati mradi wa kupambana na malaria kwa kutumia chandarua unaanza, niliandika makala kueleza wasiwasi wangu kuwa mkakati huu lazima ushindwe kwa sababu ulikuwa unashughulikia dalili za ugonjwa na sio chanzo.

Kwa maana, wananchi hawawezi kuvaa neti na baadhi yetu kutokana na dhiki alizo nazo Mtanzania hulala huku wanapiga mateke ovyo na kurusha mikono kiasi wao wenyewe humpelekea mbu kile anachokitaka. Achilia mbali watoto wanaolala na njaa na kuhangaika kitandani kiasi cha kudondoka chini kila usiku. Na kwa makosa au kwa usahihi nikadai kuwa mradi wa chandarua kupitia ushairi wangu ni mradi wa 'wajanja' lakini hauna nia na dhamira ya kweli ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo la ugonjwa wa malaria nchini.

Inavyoelekea ni kwamba kuna miaka huko nyuma katika historia yetu watu walikuwa na wito na moyo wa kuitumikia jamii bila kutegemea kupata chochote toka jamii isipokuwa mishahara yao. Watu hawakudai shukrani achilia mbali kudai rushwa. Mtu alitimiza wajibu wake na kuendelea mbele bila kutazama tena nyuma.

Hivi leo watu wa namna hiyo ni nadra. Maana mfumo wetu wa kiuchumi na kijamii umejengwa kwa namna ambayo walio wengi wanataka wapate kitu bila wao kutoa mchango wowote kwa jamii.

Kuhusu kadri wengine wanavyomenyeka na huyo 'mnyonyaji' au 'mhamishaji' kupata utajiri bila ya kuifanyia jamii lolote la maana ndivyo mtu huyo anavyoonekana mjanja na bora zaidi.

Miradi ya kupambana na ugonjwa wa malaria kama ilivyo mingi mingine inasumbuliwa pia na tatizo hili la watu kunufaika na miradi hiyo bila lolote la maana kufanyika kwa wanaokusudiwa na mradi isipokuwa kwa nafuu ya muda mfupi.

Nafuu inayosababisha mradi huo uongezewe muda, urudiwe tena au mbadala ubuniwe ili watu waendelee kula.

Wakati umefika wa kuamua, ama, tuwe tunakubali miradi inayochangia kikwelikweli kutatua matatizo ya jamii au kuikubali miradi ambayo ni 'panadol' kwa matatizo ya jamii. Mingi ya miradi tuliyonayo hivi sasa ni 'panadol' na ni ajabu kama itatufikisha mbali. Kwani siku zote njia ya muongo fupi.

Hata hivyo, isije eleweka kwamba vyandarua vyenye dawa havihitajiki. Bado vitaendelea kuhitajika lakini kinachotakiwa hapa ni kuacha kuonyesha kama vyandarua hivyo ndio jawabu kamili la kutokomeza malaria nchini.

Kwa maneno mengine, vyandarua ni kijisehemu tu cha ufumbuzi wa kupunguza na hatimaye kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini. Na kazi yake kubwa ni kupunguza maambukizi ya malaria na sio kutokomeza ugonjwa huo.

Mbu wafuatwe walipoMapambano dhidi ya malaria yanaendelea takriban kwenye kila nchi iliyo katika ukanda wa ikweta. Mikakati mbalimbali imezaa matunda tofauti. Lakini wale waliofanikiwa zaidi ni wale ambao wameamua kuwafuata mbu wanakotokea au kwenye mazalio yao na sio wale wanaongoja mbu waingie kwenye makazi ya binadamu.

Baadhi ya nchi ambazo zimeonyesha mafaniko makubwa na ambako tunaweza kujifunza mikakati mipya dhidi ya malaria ni pamoja na Cuba, Costa Rica, Venezuela, Vietnam, Zanzibar na nchi kadhaa za Amerika ya Kusini na ya kati.

Hapa Afrika kwa sababu za kisiasa na njaa kali ya wataalamu wetu miradi mingi dhidi ya mbu ni ile ambayo ya kumpa ngao mwananchi dhidi ya kuumwa na mbu na sio ile ya kumuangamiza mbu.

Na hili limelazimishwa pamoja na sauti kadhaa zilizoiona mikakati kwa sura inayostahili kuonekana toka mwanzo, kwamba ni ile isiyo na uwezo wa kutokomeza malaria bali kutuliza kwa muda na pengine baadaye kutokea mlipuko mkubwa zaidi wa vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria.

Mkakati wa kufuata mbu wa malaria kwenye mazalio yake ni mkakati wenye faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuangamizwa kwa mbu na wadudu wengine wanaosababisha maradhi mengine, kupunguza gharama za ujenzi, kupunguza gharama za matibabu; kupunguza idadi ya vifo, kupunguza kuathirika watu kwa dawa za kupuliza kwenye majumba na kuleta utulivu na amani katika nyumba.

Ugonjwa wa malaria una athari nyingine mbaya isiyotajwa mara kwa mara. Nayo ni ile inayofanya watu wasiweze kuwajibika ipasavyo kikazi, kifamilia na kimaisha.
Nini kifanyike?

Ninapendekeza kuwa wakati umefika kwa wote wanaohusika kwenda kujifunza toka nchi zilizoorodheshwa hapo juu. Kwa hiyo ni muhimu kwa bajeti maalumu kuandaliwa kwa ajili ya mkakati mpya wa kupambana na malaria na ikiwezekana bila kutegemea misaada toka nchi fadhili.Watanzania lazima wamiliki vita dhidi ya malaria wao wenyewe badala ya ilivyo sasa ambapo inaonekana kuwa vita hivyo vinamilikiwa na watu wa nje.

Tujipange wakati tunasubiri taarifa kwa hao watakaokwenda kujifunza mapya nchi za nje ili tuanza kuwa na mipango, taasisi na nguvu-akili na nguvu-kazi ambayo kazi yake ni kupambana na mbu kwa namna yoyote.

Kuhakikisha kuwa kila nyumba angalau mara mbili kwa mwezi inafikiwa na taasisi husika ili mbu wauawe na mazalio yao yasambaratishwe.Pawe na kadi katika kila nyumba inayoonyesha dawa na kazi nyingine zilizofanyika katika matumizi ya kuwapiga vita mbu.Kushirikiana na wale wote ambao tayari wamejikita katika mikakati ya kumuangamiza mbu kama njia kuu ya kutokemeza malaria nchini mwao.

Miradi kama hii ya kupambana na mbu kwa kutumia vyandarua au kupambana na ukimwi iangalie uwezekano wa kupunguza mishahara na marupurupu wanayopata wakubwa na watumishi. Pale watu na taasisi ikitathminiwa na kuonekana kweli imefikia malengo yake na jamii na nchi imepiga hatua katika jambo hilo ndipo watu wapewe bonasi zao.

Ieleweke kwamba, miaka ya kuona fedha za wafadhili kuwa sio hela yenye uchungu imekwishapita. Ni lazima tuionee uchungu fedha ya wafadhili kama tunavyoionea uchungu fedha yetu.

Ninakumbuka kutokana na ukubwa wa misaada ya malaria inayotoka nje mara ya kwanza nilipoandika kuonya kwamba dawa sio chandarua bali kuangamiza mazalia ya mbu nilichukiwa na wakubwa wote toka chini hadi juu. Ninaami kwenye hili historia daima itkuwa upande wangu.
Neti ni mbwembwe tu na kitega uchumi cha wachache, lakini mwisho wa siku ili mbu wasiwe kero hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili ni kuangamiza mazalia yao pale Jangwani. Kama kipanya alivyosema,'labda pia tuwe tunapika na kupakua tukiwa ndani ya chandalua' ndio Tanzania bila malaria itawezekana.

Hili ni muhimu katika miaka hii ambayo imegundulika kuwa nchi zisizopata misaada au zinazopata misaada kidogo ndizo zinazoendelea kuliko zinazopata misaada mikubwa. Wafadhili wanatafakari na sisi tutafakari !

Taifa budi liwe na kumbukumbu

KATI ya masuala yaliyoibuka katika semina, warsha, mikutano na baadaye kutangazwa na vyombo vya habari wiki hii ni pamoja na ya madai ya taifa kukosa tabia na mfumo wa kuweka na kutumia kumbukumbu za masuala tofauti yakiwemo yale ya maazimio, sera, utekelezaji na kukwama katika mipango na mikakati ya miradi ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

Kihistoria, Tanzania inasifika kwa kufanya maamuzi mbalimbali yaligonga vichwa vya habari katika magazeti kote duniani. Kama ilivyo katika sanaa na sayansi ya maamuzi, baadhi ya maamuzi hayo yalikuwa hayana kasoro kubwa na mengine yalikuwa na kasoro mbalimbali ambazo zilikuwa sababu tosha ya kutofanikiwa kwa nia au mradi huu au ule.

Katika menejimenti tunatambua fika uamuzi unaweza usifanye kazi wakati Fulani, lakini uamuzi huo huo ukazaa matunda katika wakati tofauti.

Aidha, tunajua fika kuwa oganaizesheni hai ambayo ina kila nafasi ya kuendelea mbele siyo ile inayotupa au kusahau maamuzi na mipango yake ya zamani bali ni ile inayoyaweka katika kumbukumbu ambazo zinaweza kurejewa na kufanyiwa kazi na pengine safari hii kufanikiwa.

Yapo maamuzi na sera mbalimbali zilizopitishwa tokea tupate uhuru. Nyingi ya sera na maamuzi hayo yalikuwa na nia njema ya watunzi wake kuona wanachangia katika mabadiliko toka hali duni kwenda bora ya watu wao. Na bado yanahitajika kwa kuwa yanahusu maadui zetu wakubwa watatu: ujinga, maradhi na umaskini. Maadui ambao hadi wa leo bado tunapambana nao na dalili za ushindi zinaonekana kuwa ngumu na mbali kuliko tulivyotarajia.

Watanzania bado ni taifa maskini, kiwango cha wanaojua kusoma na kuandika hakipandi bali kinashuka; maradhi mapya yanazuka na hivyo kuongeza idadi ya maadui tunaotakiwa kupambana nao kwa rasilimali zile zile, hadi leo Watanzania walio wengi wana dhiki ya maji, lishe bora, mazingira salama na safi na nyumba na makazi yanayostahi na kuwapa watu kiburi cha kujiona ni taifa linalojua lilikotoka na linalokwenda na sio taifa la kideiwaka tu.

Matatizo yetu ni yale yale, lakini kila serikali mpya ikiingia madarakani ama kwa kujua au kutokujua inazungumza kwa namna ambayo inaonekana kama tatizo hilo halijawahi kushughulikiwa huko nyuma, hatujui nini kilichofanyika, kwanini wenzetu walikwama, gharama gani zilitumika na ni masomo gani ambayo tunastahili kuwa tumejifunza ili katika kulishughulikia tatizo hilo hilo katika awamu mpya tujue wapi pa kuanzia na kuishia.

Tuchukulie kwa mfano aibu ya kuwa taifa ambalo maelfu ya watoto wake wanakufa kutokana na utapiamlo hali Elimu ya Kujitegemea pamoja na faida zake nyingine ilitakiwa isaidie katika kuwapa watoto wetu lishe bora. Kukatisha jambo rahisi sana lakini kulianza upya kazi kweli.

Chukulia pia suala la nyumba bora na makazi. Miradi yake ilianzia kwa hisani ya Benki ya Dunia nadhani enzi za Marehemu Bryceson ambaye ametuachia kumbukumbu njema katika hili. Katika mikoa na kanda mbalimbali ilizuka mipango ya mashirika binafsi na halmashauri na taifa lenyewe kuhusiana na jinsi ya kupambana na umaskini kuwapatia watu wetu nyumba bora. Hivi leo mwaka 2010 inaibuka mipango mipya kama vile hakuna chochote kilichowahi kufanyika kuhusiana na eneo hili. Katika hali kama hii itakuwa kila siku tuna mwendo wa mbele nyuma.

Suala la Kilimo ambacho husemwa ni uti wa mgongo wa taifa limeshapitia vipindi vya maazimio, sera na mikakati mbalimbali. Lakini hakuna jipya hapa. Kinachotakiwa ni Watanzania kuwa na kilimo cha kisasa na hivyo kutosheleza mahitaji yao yote ya chakula na pia kuzalisha mazoa yatakayotuwezesha kuwa na viwanda vya msingi kama vile vya nguo, viatu, vinywaji, vyakula vya kusindika na kuhifadhi ziada kwa ajili ya matumzi wakati wa dhiki.

Ninaamini sababu zifuatazo [sio zote] kwa kiasi fulani zimechangia hali hii ya kuwa na taifa lisilo na kumbukumbu ya kazi zake zilizofanyika huko nyuma na hivyo kuonekana kama kwa kila jambo Watanzania eti wanaanza jambo jipya:

*Kukosa maktaba ya kumbukumbu za mipango, sera na miradi ya kitaifa hai na inayofanyiwa kazi wakati wote kuonesha viongozi wapya katika wizara, idara na sehemu nyingine za kazi wapi chombo chao kilipotoka, kilipofika na kinakotakiwa kwenda.

*Kutofuata kikamilifu misingi na kanuni bora za menejimenti na utawala;
*Uchelewaji wa mabadiliko na kubadilika kila inapohitaji;
*Kupiga vita mabadiliko na uvumbuzi wa njia mpya za kufanya kazi;
*Kiwango duni katika uvumbuzi na ugunduzi wa mambo na njia mpya;
*Matumizi duni ya teknolojia mpya inayoweza kurahisisha sio tu kuweka kumbukumbu bali pia kufunza na kuendeleza wahusika;
*Siasa mbovu zisizojenga kwenye yaliyofanywa na waliotangulia bali kujaribu kufanya jambo lolote hata kama lilikwishaanza huko nyuma lionekane kuwa ni kitu kipya;
*Udhaifu wa vyombo vya ufuatiliaji na udhibiti ikiwa idara ya utumishi wa umma na mkaguzi mkuu wa serikali na vingine kama hivyo.

Nini kifanyike?

Ili taifa liweze kuwa na kumbukumbu ya shughuli zake mbalimbali ipo haja ya kutumia teknolojia kuhakikisha kuwa maamuzi, maazimio, mipango, mikakati, malengo, sera, tathmini, mwitiko, nyaraka mbalimbali, miongozo ya uendeshaji idara, wizara, makampuni na kadhalika vilivyokuwepo zamani vinatafutwa na kuhifadhiwa pengine katika kitu kitakachoitwa maktaba au makumbusho ya maamuzi, sera, mipango,mikakati na mwitiko mbalimbai ya kitaifa, kiwizara, kimkoa, kiwilaya hadi ngazi ya chini kabisa inahifadhiwa.

Pamoja na kuhifadhiwa kuwepo na mtandao utakaomwezesha kiongozi au mwananchi yeyote kurejelea na kunasua chochote anachokitaka ili katika kuendeleza jambo fulani asiwe analazimika tena kugundua gurudumu jipya la maendeleo. Moja linatosha. Kazi ni kulisukuma lifike kileleni linakotakiwa.

Pili ni muhimu kutoa elimu ya menejimenti na uchumi kwa lugha ya Kiswahili ili hata yule mtendaji wa chini kabisa katika wizara, idara, mkoa, wilaya, tarafa, kata aweze kujua umuhimu wa maamuzi na uongozi wake katika kuiendeleza nchi na jamii yetu.

Hili likifanyika tutakuwa tunawawezesha viongozi na wananchi wengi zaidi kukumbuka kwamba 'njia hii tulishapita na kulikuwa na chatu mmeza watu na hatukwenda mbali, vipi hawa jamaa wanataka kutupitisha tena njia hii yenye hatari ile ile.
Chuo Kikuu cha Mzumbe kina uwezo kabisa kama kikiwezeshwa kutafsiri masomo haya ya uchumi na menejimenti kwa Kiswahili na pia kuwa na mtandao nchi nzima wa kuwafundisha viongozi wa juu na wa chini elimu hii muhimu katika uongozi.

Ipo haja pia ya kuainisha fursa, matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania, kwa maana, ya kuainisha masuala haya bayana halafu kuandalia mikakati ya kuyashughulikia. Hili litafanyika, hata hivyo, vizuri zaidi kama kila idara, wizara na kiongozi nchini watashirikishwa katika kujua matatizo na maadui wetu wa zamani na wapya ni wepi na tuwashughulikie vipi ili tushinde tena kwa haraka kuliko wengine wanavyodhania.

Tuna matatizo na fursa mbalimbali kama sio changamoto katika vita dhidi ya ukimwi, utapiamlo, malaria, unene wa kupindukia kwa wanaokula vizuri mno na magonjwa mengine ya kuambukizana.

Tuna changamoto pia katika suala la kila mwananchi kuwa na nyumba bora, maji safi, umeme na mazingira safi na salama. Tuna changamoto la usafiri na uchukuzi usiowakera au kuhatarisha maisha ya wanaotumia barabara.

Tuna changamoto karibu katika kila sekta ambazo zinahitaji kwa hakika kujua tulikotoka, tulipo na tunapokwenda. Na ni baada ya kuyajua hayo yote ndio tunapoweza kukaa na kuandaa pengine mipango na mikakati ya kimaendeleo ya aina mpya na inayorejelewa kila kipindi bila kuingiliwa na tashwishi za kisiasa au ubinafsi na hivyo kusababisha kutofanikiwa.


Nimalizie kwa kusema kwamba bila taifa na viongozi wake kuzingatia kwa makini kule tulikotoka, tulipo na tunapokwenda; kuthamini kilichofanywa na wengine huko nyuma; kujifunza kutokana na makosa ya wengine na kulikumbusha taifa kuwa linalotakiwa kufanyika sio jipya ila ni muendelezo wa lile ambalo hadi leo halijafanikiwa itakuwa ni kazi kweli kujikwamua hapa tulipo.

Hili inahitaji kuijuza historia kama ilivyo. Kupiga vita wanaokataa mabadiliko na uvumbuzi wa njia mpya za kufanya kazi na kuwa na serikali ya wachache, lakini inayochangiwa mawazo na fikra na wengi katika kutatua matatizo ya wananchi na kuzichangamkia fursa na changamoto za kimaendeleo ziliopo mbele yao pale walipo.

Waislamu wanahitaji kuwezeshwa kiuongozi na kiundeshaji taasisi zao

MAAZIMIO kadhaa ya kidini yameandaliwa na kutangazwa hususani Waraka wa Wakatoliki na Mwongozo wa Waislamu katika siku za hivi karibuni. Je, tumejiuliza asili yake ni nini? Maana viongozi wa dini hawawezi hivi hivi tu, kutokana na dhamana, heshima na uzito wao katika jamii kukurupuka tu na kufanya mambo kama haya.

Tujiulize hivi halipo 'ombwe' la utendaji wa kiuongozi, kisiasa na kiserikali ambalo imelazimika lijazwe ? Na wanaolijaza ni viongozi wa dini kwa heri au kwa shari? Kiuongozi ombwe hilo ni ile hali ya kuwa na aina ya uongozi ambao hauna mawasiliano ya kitarafu na wale wanaowaongoza na hivyo kushindwa kujua malengo, matamanio na matarajio yao.

Ombwe hilo pia linachangiwa pia na kiongozi kutojua wanasiasa wenzake na watendaji wa serikali wanachokifanya au wanachoshindwa kukifanya. Kisha kuwawajabisha pale inapostahili. Inadaiwa katika serikali na vyama watu hudhihirisha au kuficha Uislamu au Ukiristo wao kutokana na maslahi na anayegawa maslahi hayo, unafiki mtupu. Kiserikali ombwe hilo linasababishwa na makundi fulani ya watu kuwa huru zaidi kuliko makundi mengine na hivyo badala ya kujenga umoja hujenga mgawanyiko katika makundi.
Tunahitaji kukomaa kisiasa kwa kuacha kushawishika kwa yale moyo unayoyatamani na badala yake tushawishike na kufanya maamuzi kwa kutumia akili zetu, Kipaji pekee ndicho kinachomtofautisha wanadamu na wanyama. Tukikomaa kisiasa kwa kila tamko na kila kitendo, tutakachokifanya kwanza ni kutafakari, kisha kuchunguza chanzo au asili yake, halafu kuangalia athari zake na hatimaye kuangalia jinsi ya kuepusha mabaya.

Katika makala hii hoja yangu ni kuwa tafrani ya dini na serikali iliyopo leo inasababishwa na dini moja kuamini kuwa haisaidiwi na haipewi fursa sawa ya kuchanua na kukua kama dini zingine kwa sababu zisizojulikana—na amani na umoja vitakuwa mashakani hali hii isiporekebishwa. Pamoja na hoja hiyo kuu zipo hoja kadhaa ambazo zipo hapa chini ambazo nazo kwa kiasi fulani zimetufikisha hapa tulipo: Utendaji mbovu wa serikali katika elimu na afya. Ni dhahiri kwamba hivi sasa ni shule, vyuo na hospitali za kidini zinazoendeshwa na kufanya vizuri wakati zile za serikali ni hoi.

Ukichangia na 'MOU' ya Serikali na taasisi za dini za Kikiristo huu umekuwa ni mwiba wa samaki mkubwa kumezwa na Waislamu. Kujirahisisha, kujidhalilisha kwa wafadhili. Haiyamkiniki kwa serikali ya nchi huru na yenye katiba na misimamo yake mingine achilia mbali msingi wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, kukubali nchi za nje kutuamulia mambo ambayo yanaweza kutugawa. Uongozi dhaifu kwa Waislamu. Kutokana na wanasiasa na serikali kuingilia mambo ya Waislamu sasa nchi inavuna matunda yake. Inaaminika na wengi, kama Waislamu wangelipata viongozi bora (kielimu na kiutendaji na sio ombaomba na kuinyenyekea serikali) na mifumo huru ya kisasa ya uendeshaji wa dini yao, maendeleo yao yangelikuwa ya uhakika zaidi kuliko ilivyo sasa, na hivyo amani na umoja watu ‘ungegarantiwa’.

Uchumi huria na utandawazi. Miaka sio mingi iliyopita serikali ilitamalaki katika kila shughuli kuanzia elimu, afya hadi viwanda. Hivi leo soko huria na utandawazi kutokana na sera na mwelekeo wa serikali unaoelekea kuwaogopa au kuwapendelea watu wa dini moja zaidi kuliko dini nyingine. Hii ni pamoja na misaada kwa Waislamu kubatizwa misaada ya kigaidi wakati ile kwa wenzao inayotishia umoja na amani yetu imeendelea kuja na kukubalika. Vyanzo na ukubwa wa mitaji tofauti. Wakati baadhi ya dini nchini hazina mtaji wowote wa maana nyingine zina mitaji ndani na nje ya nchi ambayo sasa inawasaidia kununua viwanja, mashamba, majengo na kadhalika na kuanzisha miradi ambayo inawafanya wawe matajiri na wenye uwezo zaidi kisiasa na kijamii. Wakati wale wasiokuwa na mitaji wanaendelea kuwa maskini.

Mipango na Mikakati. Utafiti mdogo nilioufanya umeonyesha kwamba ndugu zetu wa Kiislamu ni dhaifu katika mipango na udhibiti wa shughuli zao. Hii ni tofauti kabisa na Wakatoliki ambao kila kinachoanzishwa kina mpango, mfumo na muungo wa 'oganaizesheni' yake. Kanuni za udhibiti wake na aina ya uongozi unaostahili kuendesha chombo husika. Katika miaka hii ni muhimu kwa taasisi za kiislamu kuwa na 'Rolling Strategic Planning' yake pamoja na matamko muafaka ya 'visheni' na 'misheni' zao. Usimamizi wa fedha.

Utafiti wangu umeonyesha pia kwamba taasisi nyingi za Kiislamu zina usimamizi duni wa mambo ya fedha. Kiongozi anaweza atoke anakotoka na kuchukua fedha yoyote bila kuwajibika kwa mtu yeyote. Fedha ni damu ya taasisi kama isiposimamiwa vizuri huleta madhara zaidi kuliko faida. Umaskini wa fedha na elimu. Waislamu wengi ni maskini kifedha na kielimu. Wanahitaji kuwezeshwa kwa njia moja au nyingine kwa faida yetu sote. Ushahidi wa hili upo katika uhalifu, magereza na mateja barabarani. Muundo na mfumo wa taasisi.

Zipo kanuni na miongozo mbalimbali kuhusu taasisi mbalimbali iwe ya elimu au ya afya au ya fedha na kadhalika. Muundo au mifumo ya lazima inayohitajika kuwepo ili mambo yaende vizuri. Kwa wenzetu kuna upungufu mkubwa na aghalabu taratibu na kanuni za menejimenti ya kisayansi havipo kabisa. Elimu na Uongozi. Wakati makanisani kuna watu ambao ni madaktari, maprofesa na mabingwa wa mambo mbalimbali hivi sivyo ilivyo kwa wenzetu. Inaelekea kama yoyote yule mwenye elimu hatakiwi kwenye safu za uongozi wa juu wa taasisi kiritimbifu inayosimamia mambo ya Waislamu kwa hivi leo. Kutokuwepo Umoja katika wingi.

Yapo madhehebu mbalimbali ya Kiislamu lakini inavyoelekea serikali hutambua mwakilishi mmoja, tofauti ilivyo kwa Wakiritsto ambavyo kila dhehebu lina uwakilishi wake. Hili lazima lishughulikiwe mara moja ili kuwapa Waislamu nafasi ya kujenga umoja wa madhehebu yao. Aidha kwa kuwa Uislamu hauna ubaguzi wa rangi wala kabila hatutarajii kwamba lazima kiongozi wao awe tu Mmatumbi hata kama mtu huyo hana elimu tosha ya dini na dunia. Kwani Wahindi au Waarabu bora zaidi hawawezi kuwa viongozi ?

Misaada toka nje. Wapo wanoamini kuwa misaada toka nje inatakiwa iwe na faida sawa kwa watu wa imani zote. Ikiwa inaonekana watu wa imani moja wananufaika zaidi na misaada sio ya ndani tu bali hata ya nje huwezi ukajenga umoja wa kitaifa. Mwamba ngozi kuvutia kwake. Katika jamii yoyote kila kundi hupenda kuvutia ngozi (manufaa) upande wao. Kazi kubwa ya serikali ni kuhakikisha kila upande una fursa sawa katika vuta hiyo. Serikali inapoonekana kulalia upande mmoja, ndipo matatizo yanapoanza. Mipaka kati ya serikali na taasisi za kidini.

Lazima pawe na mipaka kati ya uongozi wa serikali na wa dini. Na hili linaweza likafanyika vizuri zaidi kwa kuwa na Katiba mpya badala ya hii ya viraka tunayotumia sasa. Maana tunapozungumzia katiba mpya sio suala la kisiasa tu bali ni makubaliano rasmi kati ya viongozi na wananchi kuhusu serikali itegemee nini kutoka kwa wananchi, na wananchi wategemee nini kutoka kwa serikali katika kila jambo. Mawasiliano. Ni muhimu kwa viongozi na serikali kuwa na mawasiliano ya kudumu na viongozi wa makundi makubwa ya kijamii kiasi cha kuwa wakati wote 'wanaanalaizi' ni nini matarajio na kero za makundi hayo na viongozi wake.

Hili litatuwezesha kuepusha kuzuka kwa mitazamo na misimamo tofauti ambayo haichangii bali inajenga nyufa katika jamii yetu. Athari za haya ni nini ?Vipengee vyote nilivyoonesha hapo juu vinahitaji kuangaliwa upya kwa makini na kushughulikiwa kwa namna ambayo athari mbaya zinadhibitiwa. Athari hizo ni pamoja na chuki, wivu, ugomvi usiokwisha, kutishiwa kwa amani na umoja wetu, watu kutoaminiana na wanasiasa na viongozi wa dini 'waovu' kuitumia fursa hiyo kupanda mbegu za 'Kirwanda enzi zile' nchini mwetu.

Watanzania ni jamii ya aina yake ulimwenguni hapa. Karibu kila familia yetu ina Mkiristo na Mwislamu ndani. Baba wa Taifa aliweka misingi madhubuti ya umoja wa Kitaifa iliyojengwa juu ya haki, usawa na heshima kwa wote. Kiongozi wa aina yoyote anapopinda masuala haya ya haki, usawa na heshima ndiye atakayekuwa chanzo cha kuvunjika amani na umoja wetu. Na kiongozi yoyote wa serikali au kisiasa anayeshindwa kuwaambia viongozi wa dini: ' Ya Kaizari mpeni Kaizari, na ya Mungu mwachieni Mungu, ' ni tatizo.

Mwisho, ikumbukwe kwamba taasisi ni kama mwanadamu. Ni kiumbe kinachozaliwa, kukua, kubadilika na kuwa bora zaidi kupambana na mazingira yake kwa jinsi muda unavyokwenda. Kwa hiyo sio sahihi basi kusema kwamba taasisi tulizo nazo sasa zimetosha. Eti kukiwa na taasisi nyingi tutatjivuruga wenyewe. La hasha. Kwa mujibu kwa nadharia za kuzaliwa, kukua, kufa na vingine kuchukua mahala pake kushindwa au kufa kwa taasisi moja au nyingine sio kitu kibaya. Maana ni ushahidi wa kutosha kwamba taasisi hiyo muda wake ulikwisha na haikuwa inahitajika tena na binadamu.

Kuna taasisi tulizonazo leo ambazo lazima zitakufa na ni dhahiri kuna taasisi nyingi nyinginezo zinazoweza kuzuka sasa na zikaishi miaka mingi baada ya sisi kusahahulikwa kwamba tuliishi hapa duniani.

Waislamu wameponzwa na wanaendelea kuponzwa na ukiritimba wa BAKWATA na kwamba taasisi zinazoweza kuiga mifano ya kina Ismailia na Jamatini zao za kuzuia watu wao kushuka chini ya mstari wa umaskini, mabohora na hata Answari Sunna na Wahabi zinahitajika kuliko zilivyowahi kuhitajika huko nyuma ili kuwasaidia Waislamu kushiriki kikamilifu na kwa mapana na marefu katika vita dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi. Taasisi zinazoshindwa kuwafaa wengi kwa walio wachache kuzila na kuziua kwa manufaa yao binafsi sio taasisi Waislamu wanazostahili kuwa nao, maana taasisi zao zilistahili kuwa bora kabisa kuliko taasisi za dini nyingine hapa nchini.

Tuwakumbuke na kuwaenzi Waislamu wa miaka ya uhuru wa kisiasa ambao hawakusita kutumia mali na nafsi zao kupigania uhuru. Ili kuanzia leo tujenge uongozi wa kiislamu unaodhamiria kutumia mali na nafsi zao kuwakomboa Waislamu nchini na Afrika kwa ujumla.

Wavuti za Serikali Ziweje?

KWANZA tutofauatishe kati ya Tovuti na Wavuti. Tovuti ni mtandao wa kompyuta kadhaa duniani zinazowezesha watu kuwasiliana kielektroniki. Wakati ambapo Wavuti ni kurasa za mtu binafsi au taasisi au serikali kwenye mtandao huo.

Afrika kwa ujumla wake iko nyuma sana katika kuwakilishwa kwake kwenye tovuti. Maudhui nyingi zilizopo leo katika mtandao ni za Ulaya, Marekani, India, China na kwingineko na sio Afrika. Aidha Tanzania ina uwakilishi sawa na hamna katika lugha yake ya Kiswahili. Maudhui za nje zilizopo katika Kiswahili ni nyingi kuliko maudhui za Kiswahili kutoka Tanzania.

Hivi sasa Tanzania ina wavuti moja ya serikali ambayo imejumuisha wizara zote humo ndani yake. Tovuti hii kwa wengi inaonekana kutokuwa na tofauti na ubao wa matangazo. Kwa kiasi kikubwa wavuti hiyo hairuhusu mawasiliano tasihili kati ya wahusika wizarani na wananchi. Bado kwa walio wengi wakiwa na shida serikali inawabidi kuswaga mguu na kwenda huko na kupewa mihadi inayochukua muda kutimizwa hadi matatizo yao yashughulikiwe au yatupwe kwenye kaburi la sahau.

Tofauti na nchi kama Rwanda, Mauritius na Ghana viongozi wetu hawaonekani kwenda na wakati wala kulichangamkia suala la Teknohama kwa kuzingatia kwamba kuna faida nyingi za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kiteknolojia zinazoweza kupatikana kutokana na kuwa na mtazamo na msukumo wa kimaendeleo zaidi.

Pengine ni kwa sababu hii ndio maana nchi hizo ambazo zilikuwa nyuma ya Tanzania katika suala la Teknohama kwenye miaka ya 80 wakati sisi tunatawakali katika kuondoa kodi k atika uingizaji wa kompyuta leo zinatuonesha indiketa. Na kama tusipobadilika hatutaona hata moshi wa motokaa yao ya maendeleo ya Kiteknohama.

Swali hapa ni, je, serikali inaweza kulibadili hili na kuwa na mfumo wa wavuti unaoonekana kuwa na maana na faida kwa Watanzania na wasio Watanzania ?

Tatizo la kuwa na wavuti moja kwa wizara zote za serikali ni kuwepo kwa mlundikano wa maudhui zisizooana na zinazomkanganyisha na kumpotezea mtafutaji jambo na msomaji na hivyo kuongeza gharama kwa upande wake. Faida ya kuwa na wavuti kwa kila wizara ni kuwa unarahisisha utambulisho wa wizara, visheni na misheni yake na kazi zake. Vievile unarahisisha upatikanaji wa habari zinazohusu wizara na mawasiliano na utoaji huduma kwa wananchi na wote wanaohitaji huduma za wizara hiyo. Hali kadhalika, wavuti inaweza ikaonesha umuhimu au kutokuwepo na umuhimu wa kuwa na wizara fulani. Kwa kawaida, wizara ambayo hakuna mtu anayewasiliana nayo itagundulika kuwa ama inachapa kazi vizuri sana na hakuna aliye na malalamiko nayo au wizara hiyo ni boya ambalo linahitajika tu wakati wa dharura-pengine kisiasa.

Kwanini ni muhimu kuwa na Wavuti?

Zipo faida mbalimbali za kuwa na wavuti ambazo viongozi wetu wakizifahamau basi watachangamkia mara moja tenda ya kuhakikisha kuwa kila wizara inawakilishwa vilivyo katika tovuti. Faida hizo ni pamoja na:
. Kujulisha dunia kuwa upo. Katika dunia ya leo sio rahisi kujulikana kama upo kama huna uwakilishi katika mtandao. Bahati na manufaa mbalimbali zimeziendea taasisi na watu ambao wameonekana kuwepo mtandaoni. Wakati kuna taasisi na watu wengi tu ambao wamekosa mambo mbalimbali kutokana na kutokuwepo katika tovuti.
Aidha, yeyote aliye na tovuti ana fursa ya kujitangaza kwa haraka na kwa mapana zaidi kuliko yule asiye na wavuti.
. Mawasiliano. Wavuti nyingi hivi leo zinatoa fursa ya mawasiliano ya papo kwa hapo. Mathalani, BBC wanaweza wakawa hewani na wakati huo huo wanawasiliana na wasikilizaji wao kupitia wavuti yao.
. Shule au Chuo. Wavuti inaweza kuwa na huduma ya elimu au shule au chuo ambacho hutoa elimu au mafunzo mtandaoni. Yapo mambo mbalimbali yanayoibebesha serikali gharama kubwa leo lakini laiti yangeliweka mtandaoni serikali ingelihitaji watu wachache tu kuieneza elimu hiyo hadi vijijini.
. Chombo cha Habari. Wavuti ikitumika ipasavyo ni chombo cha habari cha uhakika, ndani na nje ya nchi. Kwa kutumia chombo hiki serikali inaweza kuepusha umbeya na uzushi ambao sikuhizi huanzia kwanza kwenye mtandao.
. Chemchemi ya fikra na mawazo huru. Wavuti huvuta na kukusanya mawazo ya kila aina -mazuri kwa mabaya na kuwapa viongozi mbalimbali fursa ya kujua mtazamo na msimamo wa wananchi na hivyo kuwaepusha kufanya maamuzi yatakayoharibu na badala yake kuwapa fursa ya kufanya maamuzi yatakayojenga nchi siku zote.
. Ukaguzi na uwajibikaji. Endapo serikali haina lolote la kuficha wavuti inaweza ikatumika kuwasilisha bajeti ya mapato na matumizi ya kila wizara siku zote katika mwaka mzima na hivyo watu kufuatilia bajeti hizo na kuzikosoa kabla mambo hayajaharibika.
. Mijadala. Hivi leo dunaini mijadala mingi ya kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa inafanyika katika tovuti kuliko katika sehemu nyingine zozote za mawasiliano ya umma. Watumiaji wengi wa tovuti ni watu waliosoma na wanaojua kile wanachokizungumza kuliko mbumbumbu.
. Kuongeza wingi wa taarifa na makala za lugha yako. Endapo wizara zote zitakuwemo katika tovuti na kisha machapisho yote ya Kiswahili toka enzi za Waarabu, Wajerumani na Waingereza na awamu zote za serikali baada ya uhuru kuwepo humo basi Tanzania itakuwa imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza wingi wa maudhui za Kiswahili katika mtandano na hivyo kurahisisha mambo mengi yanayohitajika na Watanzania wa rika na elimu mbalimbai kupatikana humo.
. Kurahisisha kazi. Wavuti pia hutumika kurahisisha kazi. Badala ya mtu kufuata na kujaza fomu toka wizarani mtu anaweza kujaza fomu hiyo kwenye mtandao na kusubiri majibu toka kwenye mtandano ili kufuatilia kinachotakiwa hapo baadaaye. Hili litapunguza urasimu na msongamano katika wizara na hivyo kuwapa watumishi wa wizara nafasi ya kushughulikia masuala mengine muhimu zaidi kitaifa. Hii ina maana kwamba wavuti ni chombo cha huduma kinachoaminika na kufanya kazi haraka zaidi kuliko vyombo vingi vinginevyo.
. Biashara. Kwa zile wizara zinazochangia uzalishaji mali nchini kuna fursa pia kwa wavuti kutumika kibiashara. Biashara kubwa ya nchi za nje inaweza ikafanyika katika tovuti na pakiwa na udhibiti wa kutosha pasiwe na nyufa zinazoruhusu rushwa na utapeli kama ilivyo leo.
. Kwenda sambamba na teknolojia. Kwa kuwa na wavuti jambo hili peke yake linasaidia kuwaamsha watendaji wa wizara na hivyo kutokuwa mbumbumbu na kubaki nyuma kiteknolojia. Ni kitu kinachowapa changamoto pia ya watumishi hao kutaka kujua zaidi na kujiendleleza katika masuala ya Teknohama. Hili linawasaidia pia kubadilika na kwenda na utandawazi kiasi ambacho ni rahisi kwao kuajiriwa na nchi au makamapuni ya nchi za nje kwa faida yao na faida ya nchi.
. Kutoa fursa za ajira kwa vijana. Ni dhahiri pia kwamba pale kila wizara itakapokuwa na wavuti yake basi nafasi kadhaa za ajira zitakuwa zimeundwa kwa ajili ya vijana wa Kitanzania na hivyo kuongeza fursa ya wao kujiboresha na kuweza kushindania nafasi za ajira katika soko la dunia. Kwa hali ilivyo sasa ni kwamba vijana wakikosa changamoto na shughuli zinazowaingizia kipato wanaweza kugeuza ustadi na ubingwa wao wa Teknohama kufanya mambo ya kipuuzi yasiyo na maana kwa nchi na watu wetu.
. Tathmini. Wavuti pia ni njia ya mtu au taasisi kujitathmini na kutathminiwa na wengine kama mtu huyo anafanya au taasisi hiyo inafanya jambo la maana lenye faida kwa walaji au watumiaji wa huduma au bidhaa zake. Usipokuwa na wavuti mtu au taasisi yenyewe na watu wengine wote wanabaki katika giza kuhusu suala hili.

Hivi sasa Tanzania ina Sera ya Teknohama, ina taasisi kadhaa za kuanza utekelezaji kamilifu wa sera hizo na ina vijana wenye hamasa na tashwishi kubwa ya kufanya Teknohama kuwa kitega uchumi muhimu kitaifa. Kinachokosekana ni utashi wa kisiasa. Pamoja na mambo mengine ili tuondokane na kulemaa huku kiteknolojia ni muhimu kwa viiongozi wetu kuamka na kuanza kwa mapana na marefu kuitangazia dunia nia na azma ya Tanzania kuwa nchi inayokubali, kukumbatia na kutaka kujiendeleza zaidi kwa kutumia Teknohama. Nina hakika vyombo vyote vya habari viko tayari kuisaidia serikali na wananchi katika hili. Kinachongojewa ni kwa serikali kuonesha ari na nia hiyo ya kutambua kuwa Teknohama ni kitega uchumi muhimu katika maendeleo ya Tanzania.

Wanafunzi na watoto wana haki kupinga uzembe katika ajali barabarani

TUKIO la wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibasila ni kumbukumbu inayosikitisha, kwani inahusu tabia iliyojijenga miongoni mwa watumishi mbalimbali wa umma. Tabia hiyo ni ile ya kufumbia macho na masikio matatizo ya wadogo na wanyonge hadi matatizo hayo yazae maafa. Ni mbegu inayopendwa na uongozi na mfumo wa serikali ambayo imebobea katika kupanga, lakini haifuatilii kwa makini na karibu utekelezaji wa mambo mbalimbali.

Ni uongozi ulio mbali na maisha, hali halisi na matatizo ya mwananchi wa kawaida. Ni uongozi unaoweza kukaa madarakani miaka mia moja na usilete mabadiliko yoyote. Ni uongozi uliopo madarakani kwa sababu ya udhaifu wa kielimu, kifedha, kikatiba na kimamlaka au kiuwezo wa kisiasa ya wananchi wengine? walio wengi ambao wangeliweza kuwa viongozi bora zaidi.

Ni zao la kuwa na wananchi walio wengi ambao ni mbumbumbu wa demokrasia na dhana ya kubadili serikali inayoshindwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi.


Ingawa insha hii itawazungumzia polisi, lakini wao ni mfano hai tu na iko mingine pengine mibaya zaidi...

Mathalani je, ni wizara gani inayoruhusu mashimo wazi barabarani na inayochangia watu kuumia na hususan kuvunjika miguu kila siku mijini ? Hawalioni hili. Nani awawajibishe?
Ni nani anayethubutu kutobadili nguzo za umeme zinazokaribia kuanguka au kutodhibiti waya za umeme zinazopita chini badala ya juu ?

Ni nani anayeruhusu petroli stesheni kwenye makazi ya watu wakati hathubutu kuwapigia faya simu bali anawabipu tu?


Ni wahandisi gani na wizara gani inayoruhusu ghorofa zinazojengwa kwa 'udongo'.... yaani kwa maana zege ambalo halijafikia kiwango kinachotakiwa na hakuna anayewawajibisha ?

Iweje tuna shule zisizo na vifaa wala mbinu za kukabiliana na janga la moto au kwa kuwa?hakuna mtoto wa mkubwa anayesoma huko?
?
Inakuwaje wakubwa wana mashangingi yanayogharimu Sh 200 milioni, lakini kuna hospitali zisizo na gari la kubeba wagonjwa (ambulance)?

Inakuwaje tunakuwa na magari ya faya yasiyo na maji?wala njia za uhakika za kuwasiliana nayo?


Vipi wananchi wanakunywa maji yasiyotiwa dawa na hakuna anayewajibika? Ni nani anayedhibiti kiwango kinachotakiwa? Nani anayedhibiti usalama wake na nani anafuatilia?


Tumejipanga vipi kuona kwamba hakuna silaha ikiwemo mabomu yasiyo mahala pake au tunasiasaisha mpaka hili? Nani anayekula au kusalimika kwa maneno matamu?
Ni nani anayewajibika na watoto wetu wakienda au kutoka shuleni? Kuwalinda dhibi ya udhalilishaji na ukora wa makonda na wapiga debe kulikuwa nguvu ya soda? Na wazazi wenyewe mbona hawana umoja kukataa kunyanyaswa kwa watoto nchini hapa?


Kwa kifupi utaona maswali haya yanaelekeza kidole karibu kila idara na wizara. Uwajibikaji wetu ni usanii na wimbo huo umekwishawachosha wengi.? Tusipobadilika kuanzia sasa tuachane na jina Tanzania na kujiita Nigeria maana ndiko tunakoelekea!


Katika nadharia ya uongozi au menejimenti wote tunafahamu kwamba kuna kazi kadhaa zinazopaswa kutekelezwa. Kazi hizo pamoja na kuwepo kwa mipango, mikakati?na utekelezaji wenyewe ni kazi za oganaizesheni, uratibu, usimamizi au uongozi?na udhibiti au ufuatiliaji wa mambo na kuchukua hatua za haraka kurekebisha mambo pale yanapoonekana hayaendi kama yalivyopangwa.


Serikali yetu na watumishi wake wanasifika kama magwiji wa mipango. Lakini utekelezaji aghalabu huwa tofauti na mipango kwa walio wengi. Aidha suala la oganaizesheni yaani kuhakikisha kuwepo kwa mifumo na taratibu zinazofanya kazi,iwe ni kwa watu au vifaa bado ni duni.? Suala la uongozi na usimamizi kwa maana ya watu wanaohakikisha mambo yanafanyika kama yalivyopangwa lina kasoro kubwa.? Udhibiti na ufuatiliaji mambo hufanyika mambo pale tu yanapoharibika na sio wakati wote. Na matokeo yake ndiyo hapa tulipofikishwa leo. Lithibitishe hili kwa yaliyotokea BoT.


Wote ni kama tunaamka asubuhi na kwenda makazini mwetu kama maroboti kila asubuhi bila kuwa na azma hata moja ya kuhakikisha nchi angalau inashinda na kuyaacha nyuma matatizo ya msingi.
?
Kwanini serikali yetu iitwe gari ambalo betri imekwisha na haliendi bila kusukumwa ? Na ni vipi tunakuwa na betri mpya ili ukiwasha stata tu gari linaondoka?


Kwanini serikali yetu iponzwe na watumishi wake na kuonekana ni serikali inayolala na huamka tu jambo likishatokea? Kwanini tusiwe na watu wanaoweza kutuepusha na mabalaa kama wanavyofanya wao wenyewe majumbani kwao, ili kuwalinda wake, watoto na mifugo yao? Au ukishakuwa kiongozi siku hizi haustahili tena kujali ya wengine? Huu ndio uongozi kweli? Je, kwa namna hii tutafika ?


Katika suala la oganaizesheni ni kwa kiasi gani tunafahamu yote yanayopaswa kufanyika ili kazi au mradi fulani ufanikiwe? Tunagawaje kazi na majukumu ? Nani au idara gani au wizara gani anahusika na nini ?

Tathmini yake inafanyikaje? Na OPRAS iliyobuniwa na kuvalishwa vichwani mwetu na wataalamu wa rasilimali watu toka nje inafaa katika mazingira yetu ya Tanzania au nayo ni sawa na kutaka abiria kwenye gari lenye abiria wengi waliosimama kuliko waliokaa na kufunga mikanda? Je, kuna uratibu na nani anafanya uratibu huo? Je, kuna taarifa za utendaji na zinawafikia wanaostahili kuzipata ili kufanya maamuzi ya kuhakikisha mambo yote yanakwenda sawasawa wakati wote? Je, tunapitia mara kwa mara muundo, mfumo na taratibu, rasilimali watu na nyinginezo na kuona kinachohitajika kubadilika ili utendaji usiyumbe?

Je, hili lingefanyika kwenye ile njia panda ya Chang'ombe na Mandela viongozi pengine hata wa juu wa serikali wasingelikuwa wanafahamu mahala pale pana matatizo gani kiasi cha kuitwa 'Machinjioni'? Je, wote tulikuwa vipofu kutokuona kwamba pale hakuna taa za barabarani na usalama wa barabarani hawapataki kwa sababu wanazojua wao wenyewe?

Tatizo kama nilivyokwishawahi kusema hapo awali halistahili kabisa kuacha kuendelea kuwa tatizo. Lakini kwa Tanzania tatizo huendelea kuwa tatizo mwaka nenda, mwaka rudi. Na watumishi?wanaohusika hustuka tu pale tatizo kubwa linapotokea au watu wanapoamua kulala majiani na magari ya wakubwa yakashidwa kupita.


Kiongozi ni mtatua au mtafuta ufumbuzi wa matatizo. Yule anayeshindwa kupata ufumbuzi wa matatizo hata yale ya kawaida ana walakini. Hana sifa ya uongozi. Hafai kuwa kiongozi.
Maana akiwepo au asipokuwepo hali itakuwa ileile.
?
Huwa ninajiuliza hivi kweli watoto wa vigogo na vizito nao wangelikuwa katika walalamikaji hali ingefikia hivi?

Hivi unaojali tu wake na watoto wao kweli unaweza kuitwa uongozi wa watu ?
?
Ninasikia baadhi ya wakubwa wakilalama viongozi wenzao wawe na huruma. Huruma itatoka wapi bwana wee wakati mmekwishajenga tabia ya mkubwa kutojali kabisa ya mdogo?

Hili huanzia tunapowapa watu hawa ukubwa. Baadhi yao, iwe mawaziri, wakuu wa mikoa, makatibu wakuu na kadhalika hupewa maofisi wakubwa wajifiche huko wasikutane tena na watu; hupewa magari ya kifahari kuwabeba wao, wake zao na watoto wao, katika maofisi yao wengine wana vyoo na hata lifti zao tu binafsi na huko nchi za nje tunaambiwa hoteli wanazofikia hazifanani na padiemu zao. Mtu wa namna hii kweli utamtegemea aelewe ugumu wa maisha kwa Mtanzania wa kawaida ?

Sifa moja ya uongozi ni kiongozi kujishusha na kuwa sawa na anaowaongoza. Kisha akajifunza maisha na matatizo yao. Aidha akajua ni nini matamanio au matarajio yao. Na baada ya hayo akasuka mipango na mikakati inayowawezesha wote kwa pamoja kufikia malengo ya taasisi au eneo na wakati huo kutimiza ndoto za washikadau wote.

Nimalizie kwa kubainisha kuwa mimi ni kati ya wale wasioamini kwamba kiongozi atakayeitoa nchi kwenye ujinga, maradhi na umaskini anaweza akatoka katika kizazi hiki kinachojenga makasri ndani na nje ya nchi. Kwa upande wangu ninaamini kwamba kiongozi atakayeitoaTanzania katika aibu ya kuwa nchi maskini wakati ina kila sababu ya kuwa nchi tajiri, atakuwa yule atakayeshuka chini na kwenda kuishi na watu vijijini, ili aonje adha ya maisha ya Watanzania walio wengi, ajifunze na akamate matarajio na matamanio yao na kisha arudi Ikulu kuipanga nchi upya.
Hawa sio kati ya wale viongozi wanaokataa hata tu kwenda kuishi Dodoma wakati sio kijiji bali ni mji. Wala sio wale wanaotaka kuishi kama matajiri wa Ulaya katika nchi ya maskini wakubwa duniani. Kiongozi huyo ni mtu atakayekubali kuwa maskini ili awatajirishe kwanza wale anaowaongoza. Na huyu sidhani ni mtu nitakayekaa na kumuona?wakati wa uhai wangu maana viongozi waliopo hawajui kwamba muda nao ni rasilimali adimu. Na tukiyangoja maendeleo kwa muda mrefu wote tutakuwa tumekwishakufa.

Kuzungumzia 'njaa' kama tatizo la nchi miaka hii ni kushindwa kuongoza

KWA MUJIBU wa vyanzo vinavyoaminika, Tanzania kichakula iko salama. Lakini usalama huo unategemea kuwa chakula kilichopo hakitakuwa kinauzwa nchi za nje na kupaacha nyumbani patupu.

Pamoja na hayo, hali ya hewa iliyojitokeza Ulaya na Asia mwaka huu inaashiria kwamba panaweza kuwa na tatizo la kupatikana mvua na chakula cha kutosha mwaka huu; pia hali ya ukame na ukosefu wa maji katika sehemu mbalimbali nchini kuongezeka.

Kusini mwa Tanzania, huko Msumbiji hivi sasa kuna mafuriko. Ingawa taarifa za hali ya chakula zinatutia moyo lakini haya yote hayaashirii kwamba mwaka huu utakuwa na chakula cha kutosha. Na hata kukiwa na chakula cha kutosha kwa kuwa milango ya Tanzania iko wazi usiku, haielekei kama chakula kitabakia hapo kilipo na sio kupelekwa nchi za nje na hivyo kusababisha uhaba wa chakula nchini.

Kwa maneno mengine, taarifa za hali nzuri ya chakula 2008/9 zimewafanya watu wajisahau na kutokumbuka kuwa kama majirani wana njaa, wakikichukua chakula hicho basi wao ndio watakaojikuta na njaa kali zaidi!

Kwa mujibu wa taarifa za usalama wa chakula Oktoba 2008-Machi 2009, pamoja na kuwa chakula kipo cha kutosha, mijini bado bei yake ni nje ya uwezo wa Watanzania walio wengi. Watu wanaweza kwa hiyo kuwa na njaa sio kwa sababu chakula hakipo lakini hawakimudu kutokana na bei yake kuwa kubwa mno.

Taarifa hiyo imeonya kwamba kwa upande wa mifugo kuna hatari ya Homa ya Bonde la Ufa na kwa upande wa mhogo upo uwezekano wa ugonjwa wa mchirizi wa rangi ya udongo unaoshambulia mihogo kutokea pia. Hili likitokea wanaokula mchicha, sukuma wiki na kisamvu watazidi kuongezeka. Protini itaadimika zaidi ukizingatia pia kwa hivi sasa ni wachache wanaomudu kununua samaki.

Hata hivyo, taarifa hii imeshindwa kuonesha ni kuwa nchi jirani zenye uhaba wa chakula na zitakazofungua milango yao kupokea chakula kutoka Tanzania kihalali au kwa haramu zinaweza kuongeza hali ya kutokuwa na usalama wa kutosha kwa upande wa chakula.

Utafiti wa kijuujuu uliofanywa maeneo ya Himo na vijiji jirani mkoani Kilimanjaro unaoenesha kwamba mahindi husafirishwa nje ya nchi kila usiku.

Himo imegeuka ni kituo kikubwa cha kuhifadhi bidhaa hiyo haramu kabla haijasafirishwa kwenda nje. Wenye nyumba pale Himo wanafukuza wapangaji ili kukodisha majengo yao kwa wasafirishaji haramu wa mahindi.

Nyumba moja sasa inakodishwa kwa kati ya 150,000/- na 300,000/- kwa usiku mmoja. Na hii imesababisha wenye nyumba kuona kodi za pango la wapangaji wa kawaida ni sawa na chakula cha kuku kwao!

Hili linaweza kukupa picha ya biashara nzuri ya ulanguzi wa mahindi na nafaka nyingine inayoendelea kaskazini mwa Tanzania. Lakini ni ishara nzuri kuwa baada ya muda sio mrefu kutakuwa na upungufu mkubwa wa chakula katika mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Singida na Dodoma.

Na sijui ni nini kitakachowazuia walanguzi wa Kaskazini mashariki ya Tanzania kuhamia maeneo mengine ya nchi kupanua biashara yao ya ulanguzi kwa ajili ya kupata faida kubwa zaidi.

Nina hakika Zimbabwe, Kongo, Burundi na Zambia nazo zina upungufu mkubwa wa chakula na hivyo ni rahisi pia kwa mikoa jirani na nchi hizo kuwa na njaa mwaka huu!

Huko Kenya, inaelekea mahindi yanahitajika sio tu kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa nchi hiyo bali pia kuna makundi kadhaa ya watu wanaoyasafirisha mahindi hayo kwenda Sudan ya Kusini, Somalia na Ethiopia.

Bei za nafaka nchini kutokana na hali hii haziwezekani tena kushuka wakati tunaelekea kwenye masika tarajiwa. Mvua ikinyesha patakuwa na afueni kutokana na mazao kama ndizi, viazi na mihogo. Isiponyesha hali itazidi kuwa mbaya.

Njaa na siasa

Huko nyuma, njaa ikija karibu na kipindi cha uchaguzi mkuu inakuwa ni neema na baraka kwa wanasiasa walioko madarakani.
Misaada ya chakula iliyokuwa inatolewa, aghalabu, ilikuwa ikigeuzwa kuwa tenda zenye maslahi makubwa kwa wachaguliwa wachache na chama kilichopo madarakani.

Je, mwaka huu, hali hii pia kama ikitokea inaweza ikatumika kisiasa kwa watu kujisahau na nafaka yote ikishapelekwa Kenya ndio watu washtuke kuwa tuna upungufu wa chakula na kuanza kuhaha kuomba msaada wa chakula ili ugeuzwe nyenzo ya kisiasa au wafadhili hivi sasa watakuwa wamekwishafunguka macho na kukataa mtego huu?

Kuanzia Iringa, Kilimanjaro hadi Dar es Salaam, nchi wakati fulani ilikuwa na maghala yaliyohifadhi tani kadhaa za vyakula katika kile kilichojulikana kama Mkakati wa Taifa wa Uhifadhi Nafaka. Je, mradi huo upo. Je, hivi leo tunajua tuna akiba kiasi gani ya chakula na hususan nafaka ili kama mvua zitakataa Machi mwaka huu tuwe na uhakika kwamba tunaweza kubangaiza hadi Machi 2010?

Hali ya maji nayo pia sio nzuri. Na sote tunajua kuwa maji yakikosekana basi kunazuka matatizo ya kila aina nchini ikiwemo umeme kukosekana muda mrefu, mitambo na mashine za uzalishaji mali kuzimwa; na huduma mbalimbali kuathirika kwa hilo.

Je, tuna mkakati gani wa kuwa na njia mbadala za kupata maji? Mvua zikinyesha, je, tutaweza kuvuna maji badala ya kuyaachia yaishilie tu baharini? Au ni nini kinachoweza kufanyika ili maji ya Ziwa Victoria, Tanganyika, Rukwa na Nyasa na mengineyo yawe na faida kwa Mtanzania achilia mbali kumhakikishia uhai wake hapa duniani?

Tanzania imekwishaamua kuwa nchi yenye kufuata mfumo wa soko huru kiuchumi. Na haipendezi kuona tena serikali inalazimika kuingilia kati mambo ya kibiashara. Lakini kwa kuwa chakula ni jambo linalogusa uhai wa mtu haiwezekani serikali kukaa pembeni na kuwaachia wajanja wachache kuwaingiza walio wengi katika mashaka ya njaa na uhitaji kutokana na tamaa ya faida ya haraka haraka.

Ni lazima serikali wakati wote iwe inajua hali halisi ya chakula sio kwa kubuni au kusikia bali kwa kutathmini hali halisi kama ilivyo nchini. Hata kama kuna akiba ya taifa, akiba hiyo isitumike kwa ajili ya tatizo la kujitakia.

Kwa hiyo ni lazima kuhakikisha nchi inafungua biashara ya chakula kwa namna ambayo watu wanakuwa huru kuuza ziada lakini wawe na nidhamu ya kubakiza chakula cha kutosha kila mwaka.

Uuzaji chakula nje unaweza ukawa ni njia ya kuliongezea taifa pato na hivyo kuwapa Watanzania fursa ya kuchagua vilivyo bora zaidi. Lakini uuzaji huo usifanyike kwa namna ambayo chakula kinauzwa bila watu kujua akiba iliyopo. Aidha isifanyike kwa njia ambazo zinaikosesha serikali pato linalotokana na kodi za uuzaji bidhaa nje. Pato ambalo lingejazia mapengo yanayojitokeza katika bajeti ya nchi.

Serikali ya awamu ya nne ina wizara saba ambazo zikishirikiana na kukawa na ushirikishwaji wa majeshi yetu tunaweza kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika muda mfupi kiasi tusichofikira.

Kuna takriban Wizara saba ambazo zikiwa na ushirikiano mzuri kazi ya kuleta mapinduzi ya kilimo inaweza isiwe ngumu kama tunavyofikiria, zikiwamo Wizara ya Fedha na Uchumi,
Viwanda, Biashara na Masoko; Kilimo, chakula na Ushirika; Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa;
Maji na Umwagiliaji; Maendeleo ya Ufugaji na Uvuvi na ile ya Maendeleo ya Miundombinu.

Wizara ya Ulinzi na JKT?
Kuna wanaoweza kuuliza hata nayo Wizara ya Ulinzi pia? Jibu ni ndio kwa sababu binafsi ninaamini jeshi letu bado linaweza kuwa na mchango mkubwa katika utengenezaji wa vifaa na zana za kilimo, umwagiliaji maji na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.

Ushirikiano wa karibu wa wizara hizo unahitaji kwa sababu shibe ndio changamoto ya kwanza kwa serikali yoyote ile. Ni rahisi mengine kufanyika ila lazima kwanza watu wawe wameshiba vinginevyo tutakuwa tunajidanganya.
Barua-pepe: sammy.makilla@columnist.com

Vikwazo kwa Demokrasia nchini KATIKA makala hii nitajaribu kudhihirisha vikwazo vikuu vya kukua na kuimarika kwa demokrasia nchini. Vikwazo nitakavyovizungumzia leo ni pamoja na kukosekana kwa katiba mpya; kuwepo kwa chama-dola kinachotamalaki kila nyanja ya maisha nchini; kuwa na Baraza la Mapinduzi linalopindua uhuru na haki za binadamu Zanzibar wakishiriana na wale wasiotambua wajibu wao katika mfumo wa vyama vingi na umaskini wa Vyama Mbadala. Kwa wale wanaotaka kujifunza zaidi juu ya vikwazo basi waone makala zilizoko katika http://demokrasiaafrika.blogspot.com.

Kuachia watu wawe na demokrasia ya kina na pana kunataka moyo. Ni jambo ambalo halitofautiani sana na kukubali binti anayependwa na kuaminika nyumbani kuolewa. Wazazi huwa na taabu sana kutokana na mazoea kuamini kuwa watapata amani na huduma waliyoizoea kutoka kwa mtu mwingine. Lakini wakati ukifika umefika. Hakuna njia ya kuzuia yanayopaswa kutokea. Maana wakati ni ukuta na ukiupiga kofi au ngumi utaumiza tu mkono wako mwenyewe. Demokrasia kama mwali lazima apewe wananchi. Hatuwezi kuendelea kumlazimisha kukaa ndani mwetu milele. Mliopo madarakani amueni Demokrasia Ruksa ! Ili hili lifanyike yapo mambo kadhaa yanayopaswa kufanyika kwanza.

Mambo hayo ni pamoja na: Kuandikwa Katiba Mpya. Katiba mpya sio jambo la kisiasa au kiserikali tu. Katiba mpya ni makubaliano mapya yaliyostahili kuwepo kati ya watawala na watawaliwa tangu siku ile nchi hii ilipoamua kuwa nchi ya siasa za vyama vingi. Tumechelewa. Na wakati ni huu. Afrika nzima inaitazama Tanzania kuona kama tumekua na kukomaa kisiasa au la. Tusikubali kutanguliwa na tutoto vya jana kisiasa katika hili. Umuhimu wa katiba mpya ni kwamba utamaliza kabisa matatizo mbalimbali yaliyojitokeza kutoka mfumo wa vyama vingi uanze. Baadhi yake ni pamoja na haki na uhuru wa watu kuzungumza, kukutana,

kuandamana na kuunda au kuua vyama; vyama kadhaa kujiunga na kuwa kimoja kwa hiari yao wenyewe; matumzi ya redio, magazeti na televisheni ya umma; haki ya kumiliki mali zilizozalishwa na wananchi wote kwa pamoja; nafasi za makundi ya vyama vyote ya vijana, wazee na wanawake tofauti na yale ya kichama na kadhalika. Katiba hiyo inatakiwa kuandikwa na wawakilishi wote wa wananchi ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi wetu wote kwa angalau miaka 50 ijayo. Hili sio jambo la kufanywa na wanasiasa au wanasheria wachache hasa ukizingatia tofauti za kijamii, kiuchumi na kisiasa zilizopo leo. Ni jambo linalohitaji ushirikishwi wa washika-dau wote wa Kitaifa.

Demokrasia nchini hapa haiwezi kabisa kukua na kuimarika kama tunaendelea kuwa na chama-dola ambacho kwa heri au shari kinaathiri maamuzi na utekelezaji wa mambo mbalimbali. Ikumbukwe wanasiasa ni watu. Na kila mmoja wao ana matarajio na matamanio yake. Ni rahisi kwa chama-dola kujikuta kinachanganya maslahi binafsi ya viongozi wake na maslahi ya umma. Mathalani, katika sakata la ufisadi linaloendelea hapa nchini kwa hivi sasa. Pengine viongozi wa kisiasa kweli wamenufaika kwa kiasi fulani lakini wananchi walio wengi wamekula hasara. Tatizo la chama-dola ni kuwa mawaziri wake aghalabu hujali tu maslahi ya chama na sio ya wananchi wote.


Kwa hiyo maamuzi hufanyika sio kwa manufaa ya Watanzania wote bali kwa sababu chama fulani kitanufaika na maamuzi hayo au vyama fulani vitaumizwa na maamuzi hayo. Katika bunge la chama-dola tatizo ni hilo hilo. Bunge la namna hiyo hujali zaidi maslahi ya chama chao badala ya maslahi ya wananchi. Hili linapotokea uwakilishwaji wa wananchi na wabunge wao huwa umeorojeshwa kiasi cha kuwa hauna maana wala mchango wowote wa maana katika maisha ya wananchi waliowapeleka wabunge hao bungeni.

Ukiritimba wa chama-dola huathiri hata uongozi wa mikoa na wilaya. Katika mikoa na wilaya nyingi kinachoogopa huko sio serikali yenyewe bali chama kinachotawala. Matokeo yake utakuta kuna unafiki zaidi kuliko kujitambua kwa viongozi hao na kubaini mchango unaotakikana toka kwao na jamii wanayoiongoza. Hali hii inajitokeza pia katika tawala za mikoa na uongozi vijijini na mijini. Pale chama tawala kinapofika mpaka huku nacho kikawa ni chama-dola basi hakuna lolote la maana kidemokrasia litakalopikwa na kuiva huko.

Ili demokrasia ya kweli iwepo ni muhimu kutenga kabisa shughuli au kazi na wajibu wa serikali mbali na ule wa chama tawala. Hili linawezekana linataka tu kutambua kuwa chama tawala ni sawa na chama mbadala kinginecho chochote ambacho nacho pia siku moja kinaweza kuwa chama tawala. Usawa huu unawalinda wote kwa kuhakikisha kuwa hakuna anayepora nguvu na mamlaka zaidi ya yale ya kuwa chama mara anapopewa kuongoza serikali. Aghalabu hili husaulika sana na vile vyama vinavyodhani vitakaa madarakani milele. Lile linaloitwa BARAZA LA MAPINDUZI visiwani Unguja na Pemba kwa sasa ndio tishio kubwa kuliko kitu kingine chochote kwa demokrasia na hususan Visiwani. Baraza hilo ambalo ni taasisi iliyopitwa na wakati linaendelea kuwepo bila kujua wajibu wake siasa za sasa za nchi.

Limeendelea kuishi katika ukale na kuongoza kutokana na historia badala ya kuongoza kulingana na visheni na misheni mpya katika mfumo wa vyama vingi. Zanzibar ambayo ina nafasi kubwa ya kushindana na nchi kama zile za UAE ikiwemo Dubai, Sharijah, Bahrain na kadhalika leo inakwaza kutokana na siasa za dhuluma na uonevu zinazoendeshwa visiwani humo na hasa zile zinazonuia kumnyang'anya mtu haki zake za kikatiba. Ni dhahiri kwamba baraza hilo ni kikwazo kwa mabadiliko ya kweli na ya dhati yanayoweza kuwa chachu muhimu ya kuwaondoa Wazanzibari wote kutokana na udhalili na uhitaji wao karibu katika kila nyanja ya maisha.

Na sio hilo tu vijana wengi wa Kizanzibari ambao leo wanakwepa nchi yao watakuwa na kila sababu ya kurudi au kwa namna moja au nyingine kuchangia vitu vya maana katika maendeleo ya nchi mama yao. Kwa kurubuni, kutapeli na kudhulumu haki za baadhi ya wanajamii uongozi uliopo hauoneshi ujanja bali upofu na uziwi juu ya kule dunia inakoelekea siku hizi. Ikumbukwe kwamba unaweza kubabaisha kundi fulani la watu leo na kesho lakini huwezi kubabaisha makundi yote ya watu wakati wote na unafiki na uzandiki wako usijulikane.

Na aghalabu hata yule unayemtuma kudhulumu anaweza akawa si wako ila kwa kukuogopa anatekeleza amri ya kafiri apate mradi wake. Na kwa siasa hizi ni rahisi kujikuta umezungukwa na wanafiki kuliko wacha Mungu na wapenda utu na haki za binadamu. Matokeo ya hili ni kuwa na wakubwa wanaovunja sheria lakini ukawalinda kutokana na upofu na uziwi ulio nao. Hakuna binadamu mwenye akili zake timamu na uwezo wa kuleta mabadiliko yeye mwenyewe anayeweza kukubali dhuluma na mabavu siku zote. Iko siku atajibu.

Na siku hiyo isije ikawa ya kusaga meno. Hakuna anayekubali siasa za kurudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kama ni motokari sasa watu watakuwekea mawe usishuke zaidi ya hapo ulipoteremka ukirudi nyuma. Unafiki mara nyingi ni dalili za uongozi dhaifu usio na dira ya kule unakoweza kuwafikisha wanaoongozwa. Katika kutapatapa na kuhangaika basi huishia kuvuruga na kuchafua na hivyo kuwatia wananchi umasikini na ukiwa zaidi. Maendeleo ya nchi hayawezi kamwe kuletwa na ubinafsi, choyo, jeuri, kiburi, ujibari na dharau kama hiyo ndio tabia ya viongozi.

Katika dunia hii hii imewahi kutokea utawala wa wezi katika nchi fulani pale wananchi walipodanganyika na walipojisahau na kushindwa kutimiza wajibu wao. Ni dhahiri pia katika miaka hii tunaweza kushuhudia uongozi wa wahuni, waongo, wababaishaji na hata watu wajinga pindi nasi tutakapojisahau na kudhani kwamba kila mtu anaweza kuwa kiongozi. Kikwazo kingine kikubwa kwa demokrasia ni ujinga wa watu juu ya Demokrasia Vijijini.Uchumi na siasa zetu zimekaa kwa namna ambayo wananchi vijijini bado kabisa kujua faida na manufaa ya mfumo wa vyama vingi. Walioko madarakani wametumia fursa hii kuonyesha tu kasoro na hasara za mfumo wa vyama vingi.

Na kutokana na kiwango chao cha elimu na kukosa huduma muhimu za mawasiliano kama vile magazeti wanayomudu kununua, redio na televisheni basi wanakuwa na uwezo duni wa kuchambua na kutathmini wanayoambiwa na viongozi wapita njia au wale wa kwao vijijini. Katika hili ni dhahiri ipo haja ya kuweka mkakati wa elimu na njia za kufikisha elimu kwa wananchi vijijini wakati wote ili wawe wanaendelea kufunguka macho na masikio juu ya manufaa ya demokrasia katika maisha yao ya kila siku.

Kilimo: Ili tufanikiwe budi kuwa na dhati, waadilifu na wakweli

KATIKA miaka ya 60 tulizungumzia kilimo kuwa uti wa mgongo wa taifa letu; miaka ya 80 tukateta juu ya kila mtu kuwa mkulima na kuusogeza pembeni mgawanyo wa kazi; katika miaka ya 90 tukajusuru kuanzisha mapinduzi ya kijani na chakula kama tatizo; na hivi sasa tunazungumzia juu ya KILIMO KWANZA.Je, kuna lililobadilika? Hapana, maana maneno ni yale yale na kinachohitajika kama kilivyokosekana katika miaka ya nyuma ni dhati ya vitendo na watu kujituma ili kuwezesha lile tutakalo litokee. Vinginevyo soda au bia ni ile ile na kilichobadilika labda ni rangi au umbo la chupa tu. Mambo hayaji kwa kutamani tu, lazima tuyafanyie kazi. Kwa hiyo katika enzi hizi za KILIMO KWANZA, kama hatutafuatia maneno na dhamira yetu kwa vitendo na nguvu za kimtaji, miundombinu, kizana/kiteknolojia na kifedha bado tutarudia papa hapa tulipo hii leo—yaani, nchi kubwa lakini mchango wake katika kilimo kwa dunia mdogo sana.Sikuhudhuria warsha kuhusu mustakabali wa kilimo nchini, lakini hata hivyo ninaamini waliokuwepo watakuwa wamezungumzia mengi mazuri na yanayoweza kuwafaa Watanzania kama yakitekelezwa. Ninaamini, kuwawezesha wakulima hususan kwa kuwa na njia bora na nafuu za usambazaji pembejeo na kuanzishwa kwa Benki ya Wakulima nchini yatakuwa yamepewa uzito unaostahili.Ninaamini pia kilimo kimezungumzwa kwa upana na marefu yake; na kwamba ufugaji wanyama, nyuki, ndege, samaki na uvuvi na viwanda vidogo vidogo vya usindikaji mazao ya kilimo ni mambo yaliyojumuishwa katika mazungumzo hayo.Pamoja na hayo nina wasiwasi kuwa tusiporejea nyuma na kuangalia historia yetu katika kilimo ilikuwaje na nini kilichotufikisha hapa tulipo, tutashindwa kupanga na kutekeleza yale yanayofaa kufanyika na tunaweza tukateleza tena kama ilivyofanyika huko nyuma na kuishia kuangukia pua.Historia yetu katika kilimo inatuonesha tulikuwa hatufanyi vibaya hadi pale tulipotaifisha mashamba miaka kama sita baada ya uhuru na kisha kufuatiwa na mradi wa kuwahamisha watu kutoka maeneo yao ya asili na kuwaweka kando ya barabara au sehemu zilizokuwa hazina rutuba kulinganisha na zile walizotoka.Huko nyuma mila na desturi za makabila yetu mengi yalidhibiti uharibifu wa mazingira ikiwemo kutunza vyanzo vya maji na nishati na kuzilinda maliasili nyingine kama wanyama au misitu au maji ya mito, maziwa au bahari. Aidha, sheria alizotuachia mkoloni na wazee wetu waliozisimamia mara baada ya uhuru zililinda mazingira na zilitulinda sote sio haba. Halmashauri za Maendeleo za Wilaya zilifanya kazi nzuri ambayo hakuna manispaa au halmashauri yoyote ya leo imeweza kuzifanya.Vyama vyetu vya ushirika kabla ya kuingiliwa na siasa vilifanya kazi nzuri ambayo hadi wa leo hakuna ushirika wa kisasa ulioweza kuifanya.Hapakuwa na walanguzi na mkulima alikuwa anahudumiwa na chama chake cha ushirika tangu mahitaji ya msingi hadi pembejeo, mikopo na misaada mbalimbali.Kuna makundi ya vijana kama Uvikiuta la jijini Dar es Salaam yaliyofadhiliwa na watu binafsi na mashirika na yakadhihirisha kuwa vijana wakipata sapoti siku za mwanzo wanaweza kuanzisha na kuendeleza mradi wa kilimo na ukawafaa na kuchangia heshima ya nchi na vijana wake.Wilaya na mikoa ilikuwa inajizatiti katika kilimo cha aina fulani na hivyo kuwafanya wakazi wake kuwa stadi na mabingwa katika kilimo, ufugaji au uvuvi wa aina fulani.Inawezekana kwamba utaifishaji mashamba, ukame, njaa na vita vya Uganda vilichangia katika matatizo yetu kwa kiasi fulani. Lakini ukweli unabaki pale pale 'kukisiasaisha' kilimo kwa hakika ndicho kilichokuwa mhusika mkuu wa kifo cha kilimo Tanzania. Matokeo yake ikawa ni mkulima kupunjwa kipato cha jasho lake huku viongozi wa kupachikwa kwenye ushirika wakawanyonya zaidi kama si kuwaibia na hatima ya yote mkulima wa Tanzania akapoteza kabisa matumaini kwamba kilimo kinaweza kumkomboa au kumnufaisha kwa njia yoyote ile. Kutokana na hayo hapo juu, ninaamini basi kazi yetu ya kwanza kama kweli tuna nia na dhamira ya kukifanya kilimo mkombozi wa Watanzania basi ni lazima kwanza kusahihisha makosa yetu ya huko nyuma na kuhakikisha 'miundo-mbinu' ya sekta mpya ya kilimo inajengwa kwa namna ambayo kweli itamnufaisha mkulima kuliko kunufaisha wanasiasa, walanguzi na watu wengine.Kama mwanafunzi wa masuala ya rasilimali watu ninaamini kabisa kwamba kazi au ajira yoyote inayomnufaisha mtu ina fursa kubwa ya kumuendeleza yeye na nchi kuliko ajira ambayo haikidhi mahitaji ya yule anayeshughulika nayo.

Sekta ya kilimo hadi leo inachukuliwa kama ni sekta ya maskini, watu wasiosoma na waliokosa ajira katika sekta zingine. Kazi kubwa ya kwanza kwa serikali, chama tawala na vyama mbadala nionavyo mimi itakuwa ni kubadili mtazamo huu wa watu. Ni lazima Watanzania wakiheshimu na kukienzi kilimo na waamini kuwa ni ajira kama ajira zingine.Baada ya mabadiliko hayo ya kifikira basi itakuwa ni rahisi kuifufua sekta hiyo na ikaanza kurudisha upya imani ya watu na hivyo kilimo kuanza kuchangia zaidi katika maendeleo ya nchi na watu wake.Kabla ya uchumi kuingiliwa na siasa zisizo na mbele wala nyuma mambo yetu mengi yalikwenda vizuri.

Ni kweli sekta kama za madini na utalii zinakuwa haraka sana lakini bado kwa mapana na marefu hata sekta hizo nazo kukua kwake kutetegemea sana mafanikio ya nchi katika uzalishaji mazao ya biashara na kilimo kwa upande mmoja na mazingira endelevu kwa upande mwingine. Kama hivyo ndivyo, ni rahisi basi kuona kwamba sekta za utalii na madini zinawajibika kukibeba kilimo kwanza kwa namna moja au nyingine.

Ili mradi sasa tumezinduka na kugundua makosa tuliyoyafanya huko nyuma basi tusione aibu kuondokana na maadili, sera, tabia, mifumo na taratibu mbalimbali ambazo hazijengi bali zinazobomoa utu na kujiamini kwetu kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii.
Mathalani, kuna sera ya ushirika wa wazalishaji mali ikiwemo kilimo. Hii ikiwezeshwa na serikali na ushirika huo ukawa wa kisasa na unaojiendesha wenyewe unaweza ukawa sawasawa na kampuni yoyote hapa nchini. Maana wanachama wa ushirika huo watalima pamoja, watauza ndani na nje kwa bei nzuri na watasimamia fedha zao wenyewe kupitia benki ya wakulima tarajiwa.Ninashauri pia kila wilaya na mkoa uwe na muda wa kuandaa mpango wake wa kimkakati wa kilimo na viwanda vya kilimo (District and Regional Agriculture and Agro-Industry Strategic Plan) ili kujali tofauti zilizopo kati ya wilaya na wilaya au mkoa na mkoa na hivyo kuwawezesha wakazi wa wilaya au mkoa husika kujikita kwenye eneo la kilimo litakalolipa haraka zaidi na kuwa chachu ya kuendeleza baadaye maendeleo mengine ya kilimo, ufugaji na uvuvi.

Ni muhimu kuangalia na kuainisha pia ni nini utakuwa mchango wa wizara, mkoa na wilaya katika kilimo. Vilevile wabunge, wenyeviti wa vijiji, serikali za mitaa na madiwani watakuwa na majukumu gani katika KILIMO KWANZA.

Na kubwa zaidi ni mifumo na taratibu rahisi za kutatua matatizo ya wakulima na kilimo kwa wakati ili nchi nzima iwe kama timu moja inayocheza kama timu na sio kila mtu na lwake.

Mipango na mikakati ikifanyika ipasavyo itatujulisha nini kinastahili kufanyiwa majaribio wapi na kupandwa wapi. Haya yatapaswa yaoanishwe na mahitaji ya utandawazi ambayo sasa yana mwelekeo wa kupambana na yale yote yanayochafua hali ya hewa na mazingira kwa ujumla. Mwisho wa siku, wakazi wa kila eneo wakishirikishwa wanaweza kutoa majibu mwafaka zaidi kwa changamoto zote zitakazoletwa na KILIMO KWANZA. Vitabu mbalimbali vilivyoandikwa na Mwalimu, TANU na CCM vipitiwe na kuchapishwa upya na kila kinachofaa kitafutiwe mahala katika azimio la KILIMO KWANZA.

Kama kuna jambo Nyerere alilosikitika kulifanya basi ni kushindwa kuifanya Tanzania ifanikiwe katika mapinduzi ya kilimo. Baba wa Taifa kwa maneno na vitendo vyake inaonesha dhahiri angehesabu katimiza wajibu wake kama nchi hii ingelikuwa nchi ya kijani. Katuachia sisi changamoto hiyo. Ili kumuenzi Baba wa Taifa Watanzania tunachotakiwa kukifanikisha ni kuleta mapinduzi hayo ya kilimo haraka iwezekanavyo. Ni kwa faida yetu, manufaa ya kizazi chetu na heshima ya Mtanzania na Mwafrika duniani kwamba naye anaweza kujilisha na asitegemee misaada ya chakula kutoka nje.

Sera ya Kilimo Kwanza aidha lazima iwe ni ya kazi kwa maarifa na zana za kisasa na inayozingatia maswali ya elimu isiyo na mwisho, utafiti endelevu na maendeleo ya rasilimali watu wakati wote.

Msiba mkubwa ambao Tanzania unao ni ule wa wanasiasa kujifanya wakubwa wa kila jambo na wanaojua kila kitu. Hivi leo mabwana na mabibi shamba vijijini hawana tofauti na wanavijiji wengine katika umasikini wao. Mabwana na mabibi shamba hawaendi vijijini ili kusaidia kuwatoa wanavijiji kwenye umaskini bali wao pia kutumbukia katika lindi la umaskini. Maana, ukweli ni kuwa elimu na maarifa yao peke yake havitoshi. Lazima mambo mengine muhimu katika kufanikisha kilimo nchini yafanyike. Lazima pawe na ofisi na shamba la kujifunzia, zana mbalimbali na sio tena jembe la mkono, gereji, madarasa ya kilimo, kitengo cha mbolea, nafaka na mali ghafi nyinginezo.

Lazima bwana shamba awe na usafiri wa kuaminika. Leo magari ya Wizara husika ni mengi mjini kuliko mashambani. Wakati toka mwanzo wizara yenyewe ilistahili kuwa vijijini.

Wakati mwingine hata elimu na maarifa mabwana shamba waliyonayo inakuwa imepitwa na wakati. Yaani, kwa maneno mengine hakuna bwana shamba anayestahili kumaliza shule. Na vyuo vikuu na vya kawaida tulivyoanzisha vinastahili kubeba mzigo huu wa kufikisha elimu na tafiti mpya kwa mabwana shamba na wakulima vijijini kwa njia rahisi ikiwemo matumizi ya teknohama.

Isitoshe upo umuhimu wa kuwepo kwa ushirika wa kweli wa uzalishaji mali katika kilimo unaosaidiwa na Benki ambayo kazi yake kubwa ni kuendeleza kilimo na uzalishaji chakula nchini.

*** Mwalimu wangu mmoja, hayati Prof. Joshua Nkululi aliniusia kwamba kuna mambo mengine yanatakiwa uweke malengo ya juu kabisa ili hata ukianguka ufikie angalau wastani.

Mathalani, ni kosa kuweka lengo letu la kilimo kuwa kujilisha badala ya kuwa ni kuzalisha mazao kabakaba kwa ajili ya uuzaji iwe ndani au nje ya nchi. Kwa kuwa mtazamo huu unaanza kwa kulitazama soko huku ikibainika fika kwamba pamoja na kuuza kinachozalishwa kwenye masoko ya ndani na nje bado kiasi cha kutosha kitapatikana kwa matumizi yetu wenyewe. Na ili mradi tuna utaratibu mzuri wa kuhifadhi chakula cha kutosha kwa miaka kadhaa dharura inapotokea haitatubabaisha sana.

Kwa hiyo tabia ya kuwasakama wakulima wanapouza mazao mikoa au nchi jirani na wanapotumia nafaka kwa uzalishaji pombe mimi siioni kama ni busara maana unawakwaza watu kimasoko na kibiashara. Ukihofia kufa njaa kwa kuwekeza au kufanya kitu fulani katika maisha sikuzote hutofanikiwa katika dunia hii. Uuzaji wa chakula nchini na masoko yake yawe huru kama vile uuzaji maji ya Bakhressa ulivyo au uuzaji petroli ya Oilcom ulivyo. Hakuna anayemkumbusha Bakhressa kubakia na maji ya kutosha na hakuna anayewakumbusha kina Islam na ndugu zake kubakia na petroli ya kutosha magari yao.

Kubwa zaidi ni hili la uwezo wetu sisi wenyewe wa kutengeneza mashine za msingi za kilimo kwa kutumia wahandisi wazawa na wale wasio na kazi huko Romania, Hungary, Serbia, Croatia na nchi kadhaa za Russia ya zamani.

Ni aibu miaka 50 baada ya uhuru Tanzania kushindwa kuwa angalau na trekta lake linalotengenezwa na teknolojia na mafundi wa kuazima na hasa kama trekta hilo ni kapawatila tu.

Kwa maneno, mengine, kilimo kwanza kitakuwa kilimo mwisho kama tusipokuwa na zana na mashine zetu wenyewe za kilimo. Na pengine hii kwa sasa ndio iwe eneo muhimu kuliko lote la uzalishaji viwandani kwa nchi yetu. Azma ikiwa kujitosheleza kwa zana za kisasa za kilimo ambazo mkulima wa kawaida atamudu kuzinunua. Na kisha kutengneza zana na mashine hizo kwa wingi ili kuuza kwa wenzetu Afrika na nchi zinazoendelea. Mengine tukiyaweka pembeni kwa muda, hili litatuhakikishia kukua uchumi endelevu unaotegemea teknolojia yetu wenyewe na hilo litasababisha sisi pia kujikomboa katika teknolojia na ufundi mwingine muhimu ukiwa pia vifaa na mashine tunavyostahili kuwa navyo kwa uchimbaji wa madini mbalimbali sisi wenyewe kwa kutumia teknolojia yetu au ya kuazima.

Tukifia hapo tutafikia kile kinachoitwa 'takeoff' kiuchumi au kwa maneno mengine gari litafika kileleni na upande wa pili ukiwa mteremko tutaviringika kirahisi tu hadi kwenye malengo yetu mengine ya kimaendeleo.

Aidha, wakati umefika wa chama tawala na serikali yake kuwachukulia wakulima wetu kama na wao pia ni wawekezaji. Tayari wana ardhi ambayo ina thamani na pengine mazao kadhaa ya kudumu humo. Hii inatosha kabisa kwa serikali kuziaminisha benki katika kutoa mikopo ifaayo kwa wakulima hatua kwa hatua ili ifikie mahala ikawa wazi kuwa wakulima wa Tanzania wanakopesheka. Wakikopa wanalipa. Fumba na kufumbua tutamtoa mkulima wa KItanzania toka kwenye umaskini, naye akapata ziada ya kuingia katika shughuli nyingine za kiuchumi na kuwaachia watu wachache tu kushughulika na sekta ya kilimo na bado taifa. likajiendesha kichakula na kibiashara.