Sunday, November 6, 2011

Tukubali ushoga au tuachane na nchi za Magharibi ?

ZIPO habari kwamba serikali ya Uingereza iko mbioni kuandaa utaratibu ambao nchi zinazokataa 'ushoga' , kwa maana ya mwanamme kujigeuza mwanamke na kuwa na haki ya kuolewa na kuwekwa ndani kama mke, zitakuwa zikinyimwa fedha za jamala ambazo kwa Waafrika walio wengi sio msaada ila ni sawa na kurudisha kile ambacho Waingereza na ndugu zao walikwiba, wanakwiba na wanaendelea kukwiba toka kwa Watanzania na Waafrika wengine kupitia ukoloni, ukoloni mambo leo na unyonyaji mkuu wa kibiashara na kiuchumi kimataifa.


Mama wa demokrasia duniani, Uingereza, anataka kwa mabavu kupandikiza ushoga katika nchi za Kiafrika ikiwemo Tanzania kwa kuwazaini Waafrika kwa pipi na shanga kama ilivyokuwa zamani wakati makampuni yake hayachoti tu dhahabu na madini yetu mengine bali pia hata fedha zetu kidogo zilizo katika hazina yetu.

Uingereza ndio nchi iliyoitawala Tanganyika tokea ilipomshinda Mjerumani ikisaidiwa na rafiki zake mwaka 1918-1961 bila kufikia hata nusu ya mafaniko yaliyofanywa na Mjerumani katika miaka yake 30 hivi ya kuitawala Tanganyika. Lakini ndiyo iliyofanikisha kujenga unyonyaji wa hali ya juu wa nchi hii, hadi hii leo ikiwmo kasumba ya viongozi na matajiri wetu kuwapeleka watoto wao kwenda kusomeshwa Uingereza.

Hili hata hivi linatufungua macho Watanzania kwa kutambua kwamba serikali ya Uingereza na Jumuiya ya Madola ni kama vile zinaamini kwamba zimeziweka mfukoni nchi maskini za Kiafrika na kwamba zinaweza kutumia udikteta kufosi kwenye makoo yao chochote kile wanachokitaka wao kwa kuwa ni matajiri na watu wa nchi zetu kwa kuwa maskini wakakubali kirahisi tu.

Hili huwa linawezekana kwa sababu Uingereza na Marekani huwa linawatumia watu waliosoma au kufanya kazi kwao kuja 'kuunyakua' uongozi wa nchi sio kwa sababu nyingine ila kuendeleza maslahi ya Uingereza na Marekani katika nchi husika. Katika wimbi la demokrasia katika nchi zetu hivi sasa tuwe macho sana na viongozi wa kupandikizwa kwa sababu ya nguvu ya fedha. Watu hao kwa kawaida hutumwa na mabepari wa dunia ambao ni kama asilimia 1 tu ya watu duniani kuja kukwiba utajiri wenu kwa kuunda genge la asilimia 0.005 ya mabepari na wanasiasa matapeli ndani ya nchi husika.

Kwa wasiojua dunia ya ubepari tuliyoikaribisha Tanzania ni mfumo ambao unaendeshwa na asilimia 1 tu ya matajiri duniani lakini ulio na sauti na nguvu sio tu juu ya serikali zao bali pia serikali za nchi zinazoendelea ambazo huzitegemea nchi zao. Asilimia hii moja ndiyo inayoipa nguvu asilimia nyingine kama 15-20 za mabepari wa kati wanaokuja kuwekeza katika nchi zetu na kuwanu nua viongozi na matajiri wachache nchini (labda asilimia 2-3), ili kudhulumu asilimia 97-98 ya raia wenzao kwa heri na shari.

Katika hili, mimi sina tatizo hata kidogo kuona wanawake, wazee, vijana, wafanyakazi, wakulima na makundi mengine katika jamii yakifanya uamuzi ya kuandamana na kuwapasha Waingereza na Wamarekani na wenzao kama wao kwamba hatutaki na hatukubali ushoga katika urithi, desturi, utamdauni na mila zetu za Kiafrika hapa Tanzania na kwingineko Afrika.

Ushoga kwa wale wanaoamini katika Quran Tukufu na Biblia ndiyo mambo yaliyosambaratisha nchi za Sodom na Gomorrah. Wakati kuna dalili za Marekani na nchi za Ulaya kuwa katika masahibu ya kila aina, zipo hisia kwamba Waingereza wanachotaka kukifanya ni sawa na mtu anayezama kutaka kufa na wale wanaoweza kuwasaidia na wanaotaka kumuokoa.

Ni kichekesho kwa Uingereza kuwa na msimamo kama huu katika karne ya 22, kama vile bado tupo kwenye karne za 19 au 20.

Inaonekana kama vile Uingereza na nchi nyingine tajiri bado zinaamini kwamba nchi za Kiafrika ni nchi zinazoongozwa na watu ambao uroho na tamaa yao ya misaada vinaweza kuwafanya wakubali lolote lile hata likiwa baya kwa mila, desturi, imani, utamaduni na utu wa watu wao.

Hivi leo uchumi wa Ulaya na Marekani upo kwenye misukosuko sio kwa sababu nyingine bali kwa sababu ya uchumi kukosa haya na aibu au kile kinachoitwa, 'economics without ethics', uchumi bila maadili. Na misaada toka nchi hizo nazo sasa inataka kugeuzwa kuwa ni 'aid without ethics' au misaada bila maadili. Vitu hivi tusivikubali. Na huu ni wakati wa kuwashauri Wazungu kuanza kitu kitakachoitwa uchumi na misaada yenye maadili kama masomo katika shule zao za viongozi na hasa wale wa kimataifa. (Ethiconomics na aideconomics) ili watuelewe na kutufahamu zaidi. Umaskini hauimanishi maskini kukubali kuuza roho, utu na imani yake kwa ajili ya kupewa misaada.

Lakini ni ajabu pia kwa sababu hivi sasa nchi za BRIC-Brazili, Russia, India, Uchina na bila kusahau nchi za Kiarabu, zile zilizokuwa katika ile iliyokuwa ikiitwa Urussi ya zamani, Malaysia, Indonesia, Korea Kusini, Vietnam, Japani na zile za Scandinavia nazo zinatuhitaji zaidi kuliko wao wanavyotuhitaji.

Ili kuwafunza jamaa hawa ningelishauri nchi za Kiafrika kama zilikuwa zikiwapa fursa 8 kati ya 10 Waingereza na wamarekani nchini mwao, sasa zigeuze kibao na kuyapa mataifa haya mapya na yanayokuwa kwa kasi zaidi asilimia 80 ya biashara, uwekezaji na ushirikiano kati yao na kuwabakizia wakongwe Uingereza na Marekani asilimia 20 tu, ili vitisho vyao viwe kazi bure huko tunakokwenda.

Mambo yetu Waafrika kwa kiasi kikubwa yameharibika kutokana na ukaribu na kukubali bila kujiuliza tamaduni za nje, hususan, za Kiingereza na Kimarekani. Ni dhahiri kwamba tungelikuwa tunaujali utamaduni wetu wenyewe na tukashirikiana zaidi na zaidi na nchi tofauti na hizi mbili, hivi leo labda hadithi ya Afrika isngelikuwa hii iliyopo hivi sasa.

Ni nchi za Magharibi na hususan Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Italia na Marekani ndizo zilizochangia na zinazoendelea kuchangia kudhoofisha utu, utamaduni, imani na udugu wetu kwa sababu wanazozijua vizuri kuliko sisi wenyewe. Kutokana na umaskini wetu tumeendelea kuwaganda huku wanatunyonga taratibu.

Huu ni wakati muafaka kwa viongozi wa dini na wafuasi wao nao kuja juu kiddedea na kuwaonyesha mabwana na mabibi zetu wa zamani kwamba Tanzania ya leo sio ya jana na sio nchi ya kuichezea tena!

Viongozi wa dini watumie fursa hii kuzungumza moja kwa moja na walipa kodi wa Uingereza wakiwemo Wakiristo, Waislamu na Wayahudi kuwaomba washinikize serikali ya Uingereza kuachana na wazo la kuinyima Tanzania msaada kwa sababu Tanzania haitakubali ushoga achilia mbali watu wa jinsia moja kufunga na kufungishwa ndoa.

Wakati huohuo, vyama vya siasa nchini hapa na vile vya Uingereza vianzishe vuguvugu la kudai demokrasia katika utoaji misaada na kuheshimiwa kwa haki za nchi maskini katika kulinda utu wa watu wake na mila na utamaduni wao.

Enzi za Uingereza na Marekani kutoa masharti ya kisenge na kiudhalimu kwa Waafrika ninaamini zimepita. Hivi sasa Afrika ina nafasi ya kuchagua na kukataa masharti ya kijinga na yanyochimbua mizizi na kuusambaratisha mashina yake ya utu na utamaduni wake bila sababu ya msingi. Kufuatia ujibari, jeuri na kiburi cha Marekani na Wayahudi, ingekuwa jambo zuri kama nchi za BRIC na marafiki wengine tajiri wa Afrika, zingeingilia kati na kuliziba pengo la bajeti ya UNESCO, kama Marekani itajitoa kuifadhili UNESCO eti kwa sababu Palestina imekubalika kama mwananchi kamili.

Kama mataifa haya makubwa yanaamini kweli katika demokrasia hayawezi kuwalazimisha viongozi wetu kufanya maamuzi kwa niaba yetu. Maana kufanya hivyo ni kuwafunza udikteta viongozi wetu.

Isitoshe baadhi yetu katiba zetu tayari hazikubali ushoga. Je, kwa masharti hayo ya Waingereza hawaoni moja kwa moja kwamba sio tu wanataka kuingilia sheria na katiba yetu, bali pia wanaonyesha dharau kwa serikali na watu wetu ya hali ya juu kabisa.

Wanachostahili kufanya mabwana hawa ni kuwezesha nchi zetu kuwapa fursa wananchi wao kupiga kura ya kukubali au kupinga kuingizwa au kulazimishwa kuufanya halali ushoga nchini mwao.

Kwa jinsi serikali yetu inavyojikuta mchafukoge katika masuala kama ya mkorogo katika suala la huduama za umeme, maji, afya na tiba, ustawi wa jamii na usafi; migodi na madini; ufisadi, EPA na wenzake; mawakala wanavyotumbua na kadhalika na tunavyoambiwa kuwa wanaCCM wenyewe hawaoni mtu wa kupambana na ufisadi ndani ya chama hicho hatujui ni kwa kiasi gani tunaweza kuwa na viongozi watakaoendelea kuonyesha ubabe na ufidhuli kwa wale wanaotutaka tuwe mashoga na wasenge katika dunia hii ieleekeayo kwenye maangamizi ya Sodom na Gomorrah.

Sunday, October 9, 2011

Tumuenzi vipi Mwalimu Nyerere miaka 12 baada ya kifo chake....

YAPO mengi tunayoweza kuzungumza kama njia za kumuenzi Baba wa Taifa, Julius K. Nyerere miaka 12 baada ya kifo chake. Binafsi ninaamini haya nitakayoyaorodhesha hapa chini yanaweza kuwa ni changamoto ambazo kwazo tunaweza kumuenzi kikwelikweli kiongozi huyo wa Afrika na siyo Tanzania pekee.

Kitu cha kwanza, ni kuirithi na kuiboresha visheni aliyokuwa nayo baba taifa kuhusu Tanzania na Afrika na nafasi yao katika dunia hii ya ubepari na utandawazi.

Mwalimu anatarajia kuwa viongozi wa nchi hii waliotangulia na wa sasa, watachangia sio haba kuleta umoja wa Afrika Mashariki na wa ule wa Afrika na kwamba katika maeneo hayo yote, Tanzania, itakuwa mstari wa mbele na sio vinginevyo. Tuliyoyaona hivi karibuni ni kinyume cha hivyo. Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuenzi na kufuata na pengine hata kutetea maslahi ya nchi kubwa duniani kama vile Marekani na Uingereza; na ya mwisho katika kuenzi na kutetea yale yanayohusu wananchi wa Afrika, lakini mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya viongozi fulani wa Afrika, hata kama viongozi wao wanawatendea isivyo haki wananchi wao. Siamini kama jambo hili linamfurahisha baba wa taifa huko aliko. Nyerere aliwaweka wananchi wa Afrika mbele na sio viongozi wao! Maana alijifunza mengi kutokana na viongozi wababe wa Nigeria, Uganda na Kongo.

Utu, uungwana, ubinadamu na kutopenda makuu ni baadhi ya sifa alizokuwa nazo baba wa taifa. Inatia mashaka kama sifa hizi bado zinaenziwa na viongozi wetu walioko madarakani na viongozi wastaafu. Na matokeo yake yanaonekana kila kona ya nchi, nayo ni yale wananchi kukosa imani na siasa na wanasiasa kiasi cha asilimia chini ya 30 ya wananchi wa Igunga wanaostahili kupiga kura kujitokeza katika zoezi hili. Hapa kuna mambo na wala sio jambo. Ni vizuri viongozi walioko na waliokuwepo enzi hizo wajichunguze, wachunguze wengine na wachunguzane ili kujua kama kile tunachowatendea wananchi wa Tanzania kinaleta jumla na majibu yanayokubalika au tunawapotezea tu wananchi wakati wao.

Azimio la Arusha lina mambo mengi ambayo kwayo Mwalimu Nyerere anaweza akaenziwa miaka mingi baada ya kizazi hiki kinachotawala na kitakachotawala baada ya kuondoka duniani. Mambo hayo ni pamoja na kuenzi elimu ya kujitegemea; kuzuia kukua kupindukia kwa tofauti kati ya walionacho na wasionacho kiutawala na kikodi na sio kimaguvu; kuwapa uhuru wakulima na wazalishaji mali wengine; kufufua kisomo cha watu wazima; kujenga siasa za demokrasia ya kijamii ambayo inawaruhusu watu kuwa na sauti kuliko serikali kuu; na kuwaendeleza vijana wa Kitanzania kushika nafasi zao wanazostahili kama viongozi wa dunia katika miaka ya ubepari na utandawazi.

Maendeleo vijijini. Baba wa taifa aliwajali sana wakulima na wanavijiji. Ingawa jaribio lake la kuanzisha vijiji vya kisasa kupitia ujamaa vijijini lilishindwa, siyo yeye aliyeshindwa bali ni Watanzania na hususan viongozi waliomfuatia. Wakati vijiji vya ujamaa vya Israel 'Kibutz' leo ni vijiji vya kisasa na kivutio cha utalii kikubwa nchini, swali ni, je, waliomfuatia Nyerere waliamini na wanaamini kwamba vijiji bado haviwezi kuendelezwa kwa faida ya wanavijiji na nchi kwa ujumla, maana maneno ni mengi kuliko vitendo pale suala la maendeleo vijijini linapozungumziwa. Ninaimani kwamba bado maendeleo vijijini ni ufunguo wa nchi hii kutoka nchi ya ulimwengu wa nne na kuwa nchi ya angalau ulimwengu wa tatu.

Madaraka mikoani. Mwalimu tofauti na viongozi waliomfuatia na waliopo alitambua kwamba kadri Watanzania wengi wanavyoelimika na kufunguliwa macho na teknolojia mpya basi watazidi kudai haki na uhuru wa kutawala mambo yao wenyewe. Kwa kulitambua hili ndio maana akaanzisha sera ya madaraka mikoani kwa maana kwamba sio mikoa tu bali pia wilaya, tarafa na vijiji na kata vingelikuwa na maamuzi ya mwisho kuhusu jinsi ya kuendesha kiuchumi na kijamii maeneo yao bila kuingiliwa bila sababu na serikali kuu. Hivi sasa, inaelekea kwamba pamoja na kubadili majina na mbwembwe za kila aina mipango na sera inayozingatia kiukweli madaraka mikoani hamna na mambo yanajiendea tu kwa kudra ya Mwenyezi Mungu. Hili lina hatari kubwa ya shinikizo la mabadiliko sasa kutoka kwa wananchi wenyewe, na hasa pale serikali itakapoendelea kuchelewa na kukosa msukumo wa sio tu kupanga bali kusimamia na kudhibiti zoezi zima la madaraka mikoani kwa faida ya wakazi wa miko na nchi nzima.

Mojawapo ya sifa kubwa aliyokuwa nayo Baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kuwachukulia wanawe wa kuzaa kama sehemu ya wanawe wa kutawala. Wakina Anna, Rose na Madaraka hawakuwazidi kitu watoto wengine wa Kitanzania. Kinachojitokeza sasa si hivyo. Na hili kila mtu analijua na hatuna sababu ya kuliongelea na hususan katika chama tawala ambapo tunaona dhahiri mashindano ya baadhi ya viongozi kuwarithisha watoto wao uongozi wa chama na pengine nchi bila kujali wana uwezo au hawana uwezo. Tungevuta hatua moja nyuma na kutafakari yale yanayotokea huko Uarabuni na jinsi nchi yetu inavyoweza kuathirika kama baadhi ya wazazi viongozi wataendelea na msimamo na mtazamo walio nao sasa.

Elimu. Nyerere alichukulia elimu kama haki ya kila mtoto wa Kitanzania. Alijua nchi ni masikini. Na wale waliopewa elimu kwake walifananishwa na wanavijiji kwenye vijiji vyenye njaa waliopewa chakula chote na kijiji ili kwenda kijiji cha mbali kutafuta chakula cha kuja kuwanusuru watu wake. Mtazamo na msimamo wetu hivi leo ni tofauti. Kwa Watanzania wengi hivi leo elimu ni ufunguo wa kuzidisha ubinafsi wao na kujionesha wao, watoto wao na familia zao ni bora kuliko za Watanzania wengine. Na elimu na malezi ya watoto leo yanaelekea pengine kutokana na sera ya ubinafsishaji kubinafsishwa zaidi kwa madhara makubwa baadaye kwa taifa na mustakabali wake.

Kiongozi anayeona giza tu katika handaki la elimu ana tatizo. Kwa kuwa anaona giza hawezi tena kuongoza watu wakaiona nuru.

Kwa kuwa elimu haina mwisho, tatizo sio wingi wa wenye digrii mbili, madaktari na maprofesa bali kile watu hao wanachopangiwa ili kuitoa Tanzania kwenye nchi ya ulimwengu wa nne na kuifanya nchi ya ulimwengu wa tatu.

Uchumi uwe mikononi mwa Watanzania. Kama kuna jambo ambalo Nyerere alisikitika kutokuliona basi pengine ni lile la kuona uchumi wa Tanzania ukiwa chini ya Watanzania wenyewe na sio chini ya wawekezaji na wageni toka nje tu. Kumuenzi Nyerere lazima viongozi na nchi iwe na mipango na sera zinazolenga 'kuutanzania' uchumi na maendeleo yetu kwa kiasi kikubwa zaidi.

Kubwa zaidi ni lile la elimu tunayoitoa kulenga kutatua matatizo ya Watanzania na sio vinginevyo. Ni kichekesho hivi leo kuwa na wasomi wasiojua kutengeneza kitu chochote tunachokitumia, wahandisi wasioweza kutengeneza barabara wala reli wala madaraja; wahandisi umeme wasioweza kujiunga wakatatua matatizo ya umeme ya Watanzania; wahandisi wa maji wanaoshindwa kutupa huduma ya kuridhisha ya maji; wahandisi wanaoshindwa kutujengea bandari na viwanja vya ndege vizuri na salama na vyenye kufanana na mazingira na utamaduni wetu na kadhalika.

Teknolojia, sayansi na kwenda na wakati. Nyerere alienzi sana sayansi na teknolojia na hususan kwa maendeleo vijijini. Ili kumuenzi ni lazima tuhakikishe kuwa teknolojia na sayansi zilizopo nchini hivi leo zinarahisishiwa kufika na kutumiwa huko vijijini kwa faida ya Wanavijiji na wakulima na nchi kwa ujumla.

Jamii na Kujitegemea. Sifa ambayo hakuna kiongozi mwingine wa Tanzania amewahi kuipata ni ile ya Nyerere kuwa kiongozi pekee aliyetambua kwamba hatuwezi kutegemea fedha kwa maendeleo yetu. Kwa maneno yake mwenyewe: Fedha sio msingi wa maendeleo! Ni kwa kutambua hili ndio maana mwalimu akawa anapigia debe sana mchango wa hali na mali toka kwa wananchi katika maendeleo yao wenyewe. Serikali inayojiweka katika nafasi kwamba inaweza kuwafanzia kila kitu Watanzania sio serikali inayowatakia mema Watanzania. Inakotupeleka ni kule ambako leo Ugiriki inakokanyaga. Je, huku ndiko tunakotaka kwenda?

Mali asili, madini na uwekezaji. Mwalimu angelitamani sana kuona maliasili yetu, madini na majaliwa mengine yanatumika kwa faida ya Watanzania wote na sio kwa faida ya wawekezaji wachache, mangimeza wa serikali na vibarakala wao. Hali ilivyo hivi leo, hili linaonekana kuwa mbali sana na viongozi wetu wote, wastaafu kwa waliopo wanaokena zaidi kujali kujinufaisha wao na jamaa zao na sio Watanzania wote kwa ujumla kwa hatari na mikosi mingi isiyostahili kabisa kuwepo.

Umoja wa Afrika wenye maslahi ya wananchi na
sio ya viongozi wabovu kulindana. Kama mwanzilishi wa Umoja wa Afrika siamini kama mwalimu alitaka AU iwe klabu ya viongozi wazuri kwa wabaya kulindana na kupeana muda zaidi kuwagandamiza Waafrika wenzao. Mtazamo na mategemeo ya mwalimu yalikuwa kuona nchi za Kiafrika zikitawaliwa na viongozi wenye uchungu na wananchi wao na wasiotumiwa na viongozi au nchi za nje kuwanyonya na kuwagandamiza watu wao. Mwalimu akifufuka leo atasikitika kukuta hata zile nchi zilizosaidiwa na Tanzania kuwa huru na viongozi waliosomeshwa hapa Tanzania wamo katika mkumbo wa uroho wa madaraka, udikteta na kuwanyonya, kuwatesa, kuwadhulumu na kuwagandamiza watu wao.

Kama kuna kitu kitakachomkasirisha Baba wa taifa ni kukuta Tanzania ya leo ina viongozi wa juu wa kitaifa wastaafu ambao pamoja na usomi wao kwa sababu za kibinafsi wanaoendeleza siasa za kichama na wanajiingiza kuvuruga umoja na amani ya taifa hili.

Sunday, September 25, 2011

Elimu: Jamii na serikali muhimu kushirikiana kwa maendeleo zaidi.

UUNGWANA, pamoja na mambo mengine ni kuona na kusifu kile ambacho mmojawetu ameweza kukifanikisha katika maisha yake kwa faida ya wanajamii wenzake. Mojawapo ni mchango wa serikali katika maendeleo ya elimu hususan ule ambao umechangiwa na uongozi wa awamu ya nne toka uingie madarakani 2005.

Hakuna kilicho kamili katika dunia hii. Ndio maana mafanikio katika sekta ya elimu nchini hivi sasa yanaibua mijadala mingi inayobainisha udhaifu na kasoro zilizopo, wingi wa mawazo na mapendekezo mbalimbali juu ya nini kifanyike na kadhalika.

Mafanikio yaliyopatikana katika elimu Tanzania hadi wa leo, yanaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa na zaidi ya watoto milioni 1.5 katika shule za msingi, milioni moja katika shule za sekondari na laki mbili au tatu katika vyuo vikuu kila mwaka. Kinachotakiwa ni kujipanga vizuri kwa kukuza ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wanajamii kwenye maeneo shule au vyuo vilivyoko.

Elimu kama zilivyo sekta nyingine inahitaji rasilimali watu bora zaidi; majengo na rasilimali zisizo hai, safi, nzuri na bora na zinaboreshwa kila siku; uongozi au menejimenti bora zaidi kila siku; mafanikio makubwa zaidi katika matokeo ya kazi za watumishi katika sekta husika na matokeo mazuri ya kimasomo kwa upande wa wanafunzi.


Katika baadhi ya nchi za Kiafrika kama ilivyo kwenye nchi nyingi zinazoendelea, tabia moja mbaya sana imekuwa ikikubalika bila kuhojiwa na tabia hiyo kwa kiasi kikubwa inachangia zaidi matatizo kuliko kupatikana kwa ufumbuzi wa matatizo. Inadumaza maendeleo ya watu na jamii, wakati mwingine hata wakubwa wa nchi bila kujua kinachoendelea.

Tabia hiyo siyo nyingine ila ni ile ya serikali na chama tawala kujifanya ndio taasisi pekee zenye uwezo wa kifedha, kiufundi, kiutaalamu, kimamlaka na kirasilimali kuwezesha jambo lolote kufanyika na kwamba eti wanajamii hawana uono au uwezo kama huo ambao chama tawala na serikali yake walio nao.

Huu ni uzushi, utapeli, ulaghai na uongo mtupu. Wanaostahili kuwa na uwezo, fedha na rasilimali ni wanajamii wenyewe kupitia kodi zao mbalimbali zinazowezesha kuwepo kwa serikali. Serikali kama yalivyo makundi mengine katika jamii ni kundi la watu wa matumizi na hata wakati mwingine matanuzi yasiyoisaidia kitu jamii.

Upo ulazima wa kuwaelimisha watu juu ya ukweli huu, uwezo, nguvu na rasilimali walizonazo na jinsi utofauti katika hili unavyoweza kuwaondoa wananchi kutoka hali ya uhitaji na unyonge na kuwaweka sio tu kwenye nafasi ya kujitosheleza katika mahitaji yao ya msingi bali pia katika nafasi nzuri na isiyoterereka ya kuhoji utendaji, ufanisi na ufanifu wa serikali, viongozi wake na wa chama tawala.

Ili uamsho huu uweze kufanya kazi na kuzaa matunda yanayotarajiwa ni muhimu kwa taasisi zisizo za kiserikali na wanaharakati wote kwa ujumla kuwa na programu za kuwaamsha wananchi kwa kuwabainishia kuwa wao ndio wenye uwezo wa kubadili maisha yao na vizazi vyao na sio vinginevyo. Na rasilimali zote za nchi zinastahili kuwa zao na zinazochangia kuleta mabadiliko tarajiwa.

Si haki nchi iuze almasi au dhahabu au ardhi yake kisha wananchi wadanganywe kwa pipi, halua, chandalua zenye dawa na kondomu!!!

Ili sekta ya elimu iweze kupata mafanikio ni lazima wazazi waambiwe, watambue na wakubali kwamba wao binafsi wana mchango mkubwa katika shule na vyuo vilivyopo. Na kwamba ili mchango huu uanze kupatikana na kufanya kazi ni lazima wawe na taasisi, uongozi, mifumo na taratibu zinazofanya kazi. Bila hivyo, itakuwa sio rahisi kwa uwezo na nguvu waliyonayo kuonekana dhahiri, kukubalika na kuheshimiwa na washikadau wengine ikiwemo serikali, wahisani na taasisi binafsi na za kidini.

Kwa mfano, hivi leo panahitajika haraka sana: 'Taasisi ya Wazazi wenye Wanafunzi Mashuleni na Vyuoni' kuliko wakati mwingine wowote huko nyuma ili kutetea na kulinda maslahi ya wazazi na watoto wao wanaosoma katika taasisi mbalimbali ikiwemo usalama kwenye taasisi hizo, ubora wa elimu, mafunzo na walimu au wahadhiri, ubora wa malazi, ubora wa vyakula, usalama wa maji na haki na uhalali wa ada na gharama nyingine zinazolipwa ili wazazi kupuka kutapeliwa na shule za msingi, shule za sekondari, vyuo na vyuo vikuu feki au vibabaishaji.

Jamii inaweza isiridhike na shule na vyuo vilivyopo na ikaamua kuwekeza na kuanzisha shule na vyuo vyake ambavyo vitakuwa bora zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. Jambo hili si jipya duniani. Baadhi yaWamarekani walipoanza kuchakachua elimu na kutoa elimu isiyohitajika na soko la ajira, jamii mbalimbali za KImarekani zilianza kuanzisha shule za msingi za kijamii na kisha wakaanzisha sekondari na vyuo vikiuu vya kijamii na hivi leo taasisi hizo ni kati ya zile zinazong'ara nchini Marekani.

Lakini ilimradi vile vilivyopo vinajikusuru, basi ni vizuri zaidi Taasisi kama hiyo ya wazazi wenye wanafunzi wanaosoma ikawepo ili kusimamia, kushinikiza na kutoa chachu ya mabadiliko, ukuaji na maendeleo kwa taasisi zote za elimu zilizopo.

Ni muhimu pia serikali kutambua kwamba haina ubavu, nguvu, rasilimali na mitaji ya kutosha kuweza kufanya kila kitu peke yake kwa yote yale wananchi wanayoyahitaji. Kwa namna moja au nyingine, lazima ikiri hadharani, kama ilivyofanya kwa kuinyima ukiritimba TANESCO, juu ya lile lililoonekana kushindwa kuendelea kwa serikali kulibeba achilia mbali kulifufua shirika hilo na hivyo kufungua milango kwa watu wa ndani na nje kuwekeza katika uzalishaji, usambazaji na uuzaji umeme kama soko huru linavyotushuritisha.

Ndivyo inavyotakiwa pia kwa serikali mapema iwezekanavyo

kutoa wito kwa wananchi kila inapowezekana kuwekeza, kuendesha, kusimamia na kusaidia shule zilizopo kwenye maeneo yao kwa faida ya nchi na watu wake. Kwa maneno mengine, serikali inapaswa kutamka bila kusita kwamba wazazi na wanajamii kwa ujumla wana sababu, uwezo na shuruti ya kusaidia kwa hali na mali, maendeleo ya shule za kata na nyinginezo ili kuboresha sio tu hali za shule husika bali pia utawala au menejimenti na matokeo ya mitihani ya shule husika kimkoa, kitaifa na kimataifa. Shule, kwa maneno mengine, 'sio shule za serikali tu' ni shule za wananchi au wanajamii wa maeneo husika.

Wanajamii ndio wanaoweza kusifanya zifanye vizuri na kufanikiwa au kuziangusha. Upo ushahidi wa kutosha kwamba ushiriki wa wanajamii katika usimamizi na uendeshaji wa shule huchangia sio haba kupunguza matatizo mbalimbali yanayokabili shule, walimu na wanafunzi.

Na kwamba mchango wa hali na mali wa wanajamii katika maeneo hayo unahitajika na unakubalika. Wanajamii wakishirikiana na walimu au wahadhiri na wakuu wa taasisi husika wanaweza 'wakakomisheni 'tafiti mbalimbali ili kuona nini kinachoendelea, kisichostahili kuwepo na ukubwa au upana wa pengo lililopo na mabadiliko yanayotakikana,ili kuongeza ubora katika sekta ya elimu kwenye maeneo mbalimbali.

Baadhi ya mambo ya kutafiti na kufanyia kazi ni pamoja na je, Idadi ya masomo yaliyopo ni sahihi? Mitaala na silabasi zilizopo zinakidhi haja zetu? Je, masomo hayo yana manufaa kimaisha? Je, yatamsaidia mwanafunzi wa leo kuja kujiajiri au kuajiriwa? Je, sio vyema wanafunzi
kuchagua masomo machache kuendana na kipaji, uwezo wa mwanafunzi na kile anachokipenda kuwa katika maisha yake hapo baadaye?

Aidha ni lazima kupata majibu kwa maswali kama, je, alama za kiwango cha kufaulu ni sahihi na cha haki?
Je, kurudia darasa kiwango cha kufaulu kisipofikiwa sio jambo zuri na kwa faida ya mwanfunzi kuliko kuwa na mwanafunzi anayeingia darasa la pili lakini hana uwezo wa mwanafunzi wa chekechea ?
Je, idadi ya wanafunzi darasani ni sawa? Je, idadi ya walimu waliopo katika shule ni sawa? Je, muundo na mifumo iliyopo inaruhusu viranja, viongozi na wasimamizi wa shule kufanya kazi bila uonevu au upendeleo? Je chakula, kifungua kinywa, maji na lishe ya wanafunzi inaendana na hali ya maisha leo? Je, majengo na huduma stahilivu yana viwango vinavyokubalika na vinaendelea kuboreshwa kila siku, au shule au vyuo havina sera ya uchakavu na majengo yao yanatisha na kusikitisha? Na, je, mtoto wa Kimalawi au Kizambia au Kikongo au Kirundi au Kinyarwanda achilia mbali Kiganda na Kikenya anaweza kujiunga na shule au vyuo vyote na wazazi wake wakaridhika kwa elimu na huduma za msingi atakazopata?

Je, unyapara na hususan ule wa ukaguzi katika sekta ya elimu sio kitu chema na kinachohitajika wakati wote?

Na ni kwa mikakati na mbinu gani zinazoweza kutumika ili kuboesha kipato cha walimu na maupurupu yao bila kuwalazimisha kutafuta njia za mikato na zisizo na tija kitaifa na kijamii?

Je, katika jiji kama Dar es salaam kupanga ratiba za masomo ya shule za msingi na sekondari kuanza saa 12 alfajiri na kukoma kwenye saa sita au saba hakutapunguza tatizo la kunyanyapaliwa wanafunzi na wenye daladala na hivyo kuathiri maendeleo ya darasani na kwenye mitihani ? Na je, kuwa na kalenda ya shule na vyuo vyote katika elimu kwa masomo, likizo, sikukuu mitihani, michezo, michuano ya michezo mbalimbali, safari za kimasomo, muda wa masomo kwa vitendo, ukarabati, ukaguzi, ununuzi na usambazaji wa vitabu ni jambo litakalosaidia maendeleo ya elimu au la?

Je, kupunguza masaa ya shule au kuyagawa kati ya mafunzo na michezo hakutachangia kumkuza mtoto kimwili na kiakili kwa mapana na marefu zaidi?

Je, wanajamii wenye elimu, ujuzi, maarifa na uwezo mbalimbali ambao sio walimu hawawezi kufanyiwa utaratibu wa kusaidia kufundisha pale kusiko na walimu wa kutosha?

Haya ni baadhi ya masuala ambayo yanaweza kuzungumzwa, kufanyiwa utafiti na makundi husika ya shinikizo katika elimu kuiwajibisha serikali iliyopo madarakani kufanya yale yanayohitajika na yanayowezekana bila ulegevu, uoga, uvivu, ubabaishaji, 'usiasaishaji', au ucheleweshaji wa aina yoyote? Ni kwa namna hii tu ndipo tutakapoweza kutoa majibu sahihi kwa changamoto zilizoko katika sekta ya elimu na mafunzo nchini kwa faida ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.Baba wa Taifa, J.K.Nyerere alituasa fedha si msingi wa maendeleo. Yapo yawezayo kufanywa kwa fedha na yapo yanayoweza kufanywa kwa utashi, akili, bidii, juhudi na nguvu za wanajamii husika.
Tukitegemea fedha kwa kila kitu hatutafika mbali.

Friday, September 16, 2011

Mikopo kwa wanafunzi na matumizi ya kadi za krediti

NIMEKUWA nikifuatilia sakata la mikopo kwa wanafunzi hapa nchini kwa muda sasa.
Majumuisho yangu yasiyo rasmi ni pamoja na kwamba taasisi iliyopo, muundo uliyo nayo, mifumo iliyopo, mipango iliyopo, taratibu zinazofuatwa-vyote vimeanzishwa kwa makosa na visingestahili kuwepo.

Serikali iliyopo madarakani kwa sababu ambazo inazijua yenyewe ilianzisha bodi ya mikopo ili isaidie kitu kingine lakini sio kuwasaidia wanafunzi wanaohitaji mikopo.

Wimbo wa serikali inatakiwa kujitoa kwenye masuala ya uchumi na biashara uliishia katikati, maana ulistahili kuendelea kwa kubainisha pia serikali inatakiwa kujitoa kwenye masuala yote ya kifedha na mikopo isiyoihusu serikali moja kwa moja.

Kinachoendelea hivi sasa ni kwamba serikali imejiingiza katika sekta ya Benki na mikopo bila kuwa na uwezo, vifaa, rasilimali watu,utaalamu wa kuendesha kwa makini na kibiashara na kwa faida shughuli ya mikopo kwa wanafunzi nchini. Upo uwezekano mkubwa kwamba hapo baadaye serikali italazimika kufuta mikopo yote vitabuni mwake kwani itakuwa ni mikopo mibovu.

Waliostahili kuifanya kazi hii walistahili kuwa benki mbalimbali nchini kwa ushirikiano na Mamlaka ya Kodi nchini (TRA), chama cha Waajiri nchini (ATE), chama kikuu cha wafanyakazi nchini (TFTU), mashirika ya hifadhi ya wafanyakazi mbalimbali nchini, makampuni mbalimbali ya bima nchini na waajiri waliopo na waajiri tarajiwa nchini.

Kilichotakiwa kufanyika ili serikali isijiingize katika matatizo, ili wajanja wachache wasitumie mwanya huo kujinufaisha wao wenyewe na jamaa zao na hali kadhalika wanafunzi na wazazi wao wasisumbuke ilikuwa ni kuvipa dhima vyombo hivyo kuanzisha KADI YA KREDITI kwa wanafunzi mbalimbali watarajiwa kwa namna ambayo ingelipunguza urasimu; umangimeza; kujuana, yaani, huyu mtoto wa nani na yule wa nani; ubabaishaji; usumbufu; matumizi ya fomu na makaratasi ambayo ni rahisi kupotea na wakati huo huo kuwezesha kuwaingiza wakopaji katika mifumo ya kompyuta ya serikali, benki husika, taasisi mbalimbali ikiwemo TRA na Mkaguzi Mkuu wa serikali na mkaguzi wa mikopo ya wanafunzi (kama yupo) kwa sababu za kiudhibiti na ufuatiliaji kuanzia mkopo unapochukuliwa hadi unapolipwa.

Nitatoa mfano,CRDB Benki kwa ruksa ya serikali inanunua dhamana za serikali (government bonds au treasury bills) toka hazina kwa kiasi cha mikopo inayohitajika na wanafunzi. Bila kubagua wanafunzi wote wanaoingia kwenye vyuo vya juu wanapewa krediti kadi ya CRDB Bank toka kitengo cha Mikopo Maalum kwa Wanafunzi kitakachokuwa kinajitegemea ndani ya benki hiyo. Ikumbukwe hii ni benki pekee ya wazawa nchi ambayo tunastahili kuibeba kwa hali na mali.

Benki hii kwa kushirikiana na taasisi husika haitafanya kazi hii bure. Italipwa. Na malipo yenyewe yatatokana na kuendesha shughuli nzima ya mikopo kwa wanafunzi kibiasharra kati ya benki na serikali kwa upande mmoja; na kwa upande wa pili kama huduma kati yake na wanafunzi wa vyuo vya juu waliopo na watarajiwa.

Kwa maneno mengine nia ya serikali kutoa huduma ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya juu itatimia kwa benki hiyo kuisaidia serikali katika jukumu lake.

Na kwa upande mwingine benki na taasisi ya fedha husika kwa kukabidhiwa kazi hiyo na kulipwa na serikali itakuwa imerejeshewa kufanya kile ambacho kwa kweli ndiyo kazi zake za kila siku. Wote kwa namna hii wataibuka ni washindi, ingawa serikali itakuwa mshindi zaidi kwa maana sasa itaondokana na aibu ya kuzodolewa kila siku na wazazi na wanafunzi kuhusu suala hili la mikopo kwa wanafunzi.
Benki tofauti na serikali kwa kiasi fulani, itakuwa na kumbukumbu zote za kila mkopo inayouhudumia na mkopaji na jinsi ya kumfuatilia toka mwanzo mpaka mwisho.

Kwa kushirikiana na TRA, mkaguzi mkuu wa serikali na mkaguzi wa elimu ya juu, benki itawatambua wanaostahili kukopa na wasiostahili kukopa. Wasiostahili kukopa watabebeshwa riba kubwa zaidi na muda wao kulipa kuwa mfupi zaidi, na wanaostahili kukopa riba ndogo na kupewa muda mrefu zaidi kulipa deni lao.

Jukumu la kuhudumia mkopo huo sasa halitakuwa tena la serikali bali la mwanafunzi na mzazi wake au mlezi wake wakishirikiana na benki husika. Akili au mkono mtu katika suala zima utakuwa na fursa ndogo sana ya kuharibu nia hii nzuri ya serikali kwa watu wake.

Kwa wasiojua, kadi ya krediti ni kadi kama ilivyo Tembo Card ya CRDB Bank au nyinginezo kama hii ambayo badala ya kuwa na fedha za mwenye kadi, ni benki husika inayomwekea kiwango fulani cha fedha anazoweza kutumia kama mkopo kwa shughuli zake binafsi ili mradi tu havuki ukomo aliowekewa (maana kadi yenyewe haitamruhusu kufanza hivyo). Kama zilivyo kadi nyingine kadi hii ya krediti inaweka kumbukumbu zote muhimu kwa njia ya kistaarabu na kwa namna ambayo sio rahisi kumbukumbu hizo kupotea. Kadi ya krediti itamruhusu mwanafunzi kulipia tuisheni au gharama za mafunzo; vitabu; mitihani; malazi; chakula; afya na tiba; usafiri; utafiti; mafunzo kwa vitendo na majukumu mengine mbalimbali ya kiuanafunzi.

Ili kuwawezesha wanafunzi kutumia vyema na ipasavyo hizi Kadi za Krediti CRDB Benki itaendesha mafunzo kwa kushirikiana na wahusika wengine kwa wanafunzi/ wakopaji wote. Baada ya hapo itakuwa ni mtihani kwa mtumiaji mwenyewe kuitumia kadi hiyo ya krediti kwa namna ambayo itampunguzia deni laki huko baadaye na hata kumnufaisha wakati wa masomo kwa kumuwezesha kuwa mjasiriamali na mtu anayejiajiri hata kabla hajamaliza chuo.

Wahisani au wafadhili wanaweza kukaribishwa ili wachangie kupunguza gharama za mikopo hiyo na kuwawezesha wanafunzi wanaostahili kukopa kutokulipa riba yoyote.

Katika miaka hii ni rahisi sana kuwa na viongozi ambao uwezo wao wa uamuzi, uchambuzi, uchaguzi, uteuzi na utekelezaji sahili na sahihi ni dhaifu kuliko wa baadhi ya wale wanaowaongoza. Kwa hiyo ni muhimu pale inapoonekana katika jambo au kazi fulani ambayo inawahusu raia walio wengi kujitokeza kwa viongozi zaidi ya viongozi ili kurekebisha mambo.

Mipango, utaratibu na utekelezaji mzima wa suala la mikopo kwa wanafunzi sio tu vinaonesha walakini mkubwa lakini kunaashiria dhuluma, ujanja, kutorejeshwa kabisa mikopo na matatizo yasiyo na mwisho. Ni kwa sababu hii ndio maana ninapendekeza kwamba shirika la Hakielimu liingilie kati ili kubadili mustakabali wa jambo lenyewe. Hata kama tumeanza vibaya jambo lililo muhimu zaidi ni kumaliza jambo lenyewe kwa kupatikana haki kwa wale wote wanaostahili haki, ikiwemo jamii ya walipa kodi nchini.

Hakielimu inaweza kuingilia kati kwa kujitolea kuanzisha kazi ya kuundwa makundi mbalimbali ya washikadau katika elimu na kisha kuwasapoti katika kurasimisha uundwaji na kuwepo kwa makundi hayo na pia mikutano yao ya awali.

Mathalni, tuna maprofesa na walimu wastaafu wengi tu ambao wakiwezeshwa wanaweza kuzungumzia mengi mazuri tu kuhusu utekelezaji wa masuala mbalimbali ya elimu hapa nchini kwa sekta ya umma na sekta binafsi. Makundi mengine ni pamoja na mainspekta wastaafu wa elimu, washauri na watafiti katika masuala ya elimu na mafunzo, waandishi wa masuala ya elimu na mafunzo, wakuu wa vyuo na walimu wakuu wastaafu; watumishi wa wizara ya elimu wastaafu; viongozi katika vyuo vikuu, vyuo vya kawaida, shule za sekondari, shule za msingi na wamiliki wa shule na vyuo mbalimbali.

Maamuzi mengi ambayo yanaishia kuwa bomu kwa kufanywa kidikteta na kwa maslahi ya watu au taasisi fulani sasa yatapatiwa changamoto na haitakuwa rahisi siku za mbele kuwa na maamuzi mengi mabovu katika elimu na taasisi za elimu kama ilivyo sasa.

Hasara za mfumo uliopo hivi sasa ni pamoja na: kuwepo urasimu na umangimeza unaoharibu zaidi ya kutengeneza; dhuluma na upendeleo katika utoaji mkopo; kuiongezea serikali gharama za uendeshaji na utoaji mikopo; unadra wa mikopo kulipwa kwa wakati; kutokuwepo mbeba dhamnana inayotolewa a serikali; kuzinyima benki na taasisi za fedha fursa za kiuchumi inazostahili; kuwa na watu wanaoajiriwa na kulipwa mishahara bila sababu ya msingi; kufedheheka serikali mbele ya macho ya wannanchi wake na dunia nzima; kuruhusu kulipwa mikopo wasiostahili na wanaostahili kutokulipwa na kadhalika.


Faida za kadi za krediti ni pamoja na kuondoa: matatizo yanayoletwa na akili na mkono wa binadamu; kuondoa urasimu; ;kuondoa upendeleo na dhuluma; kurahisisha zoezi zima la kukopa na kulipa mkopo; kudhibti wadaiwa na malipo husika; kukuza uchumi kwa kuongeza mzunguko wa fedha; kuhamisha jukumu la kujisimamia kifedha kwa wazazi na wanafunzi wenyewe; kuondoa gharama kwa kuwepo na taasisi na majengo maalum kwa shughuli hiyo na kuongeza haki na usawa katika medani ya maisha ya kitaifa nchini.

Uwekezaji kaika kilimo unufaishe vijiji na wanavijiji

Kuna kosa la kihistoria ambalo lilikwishatokea na linaloendelea kutokea kwa sababu serikali imeshindwa hadi wa leo kufanya tathmini halisi, halali na ya haki ya watu na utamaduni wao, mtaji wao wa kijamii, vijiji vyao na ardhi na mali asili walizonazo.

Aidha serikali imepindua kinyemela madaraka na mamlaka ya wananchi wanayostahili kuwa nayo kwa mujibu wa katiba juu ya uongozi na maamuzi ya nchi, ardhi na mali asili zao na kujiweka juu kwenye nafasi ya muamuzi mkuu na mmiliki wa ardhi badala ya wananchi kuwa ndio wanaofanya maamuzi na wanaomiliki kihalali ardhi na rasilimali nyinginezo katika nchi hii, kiasi kwamba serikali inaweza kuamua wakati wowote kuwapora wananchi ardhi yao na wananchi walipwe kidunchu tu au sawa na kutokulipwa na wakati mwingine hata kuporwa kimaguvu ardhi na mali asili zao nyingine na wale wanaoitwa wawakilishi wa serikali.

Isitoshe, ardhi na sekta ya kilimo ndiyo inayowagusa wananchi walio wengi Tanzania na maamuzi katika eneo hili ni lazima yawe na manufaa kwa wanavijiji walio wengi na sio wanamji na wawekezaji wawili watatu wa ndani na nje.

Kihistoria, haikanushiki pia kwamba japo katiba ya nchi hii inataka uwiano na ulinganifu katika maendeleo, hali llivyo leo ni kwamba bado watu wa mjini na sehemu za mijini zimekuwa zikipewa upendeleo mkubwa kuliko watu wa vijijini na maeneo ya vijijini. Uvumilivu, subira na ukawaida wa watu wa vijijini umechangia sana katika hili pengine kwa wao kuonekana wanaoridhika kirahisi au mabwege wasioweza kuwafanya wakubwa lolote. Lakini kuendelea na hali hii sio tu ni dhuluma na uonevu kwa watu wa
vijijini bali ni kukosa kuona mbali na mbele na kuamini kuwa siku zote watu wa vijijini watakuwa wavumilivu, wenye subira na mabwege na mafala kuhusu haki zao, matakwa na matarajio yao.

Hali kadhalika, matatizo mengi yanayotokea katika miji yetu hapa nchini hivi leo yanasababishwa na upendeleo huu wa miji dhidi ya vijiji iwe ni katika wingi wa watu wasiobebeka mjini, wizi, wingi wa magari na foleni, kukosekana huduma muhimu mijini na kadhalika.

Ndio maana tunasema kwamba bila ya sera ya Kilimo Kwanza na Uwekezaji katika kilimo kumnufaisha moja kwa moja mwanakijiji basi mapinduzi ya kilimo nchini yatakuwa ni sawa na kazi ya kupanda kilima kirefu chenye majabali yenye ncha kali na mijoka iliyojificha.

Katika siku za hivi karibuni kilimo kwanza ambayo ni sera iliyoanza siku nyingi lakini imeendelea kubadilishwa majina kama vile yapo matarajio yasiyokufa kwamba eti jina ndilo linaloweza kuifanya ifanikiwe imekuwa ikipigia debe nchi za nje kupewa ardhi ya Watanzania kwa ajili ya kilimo kama vile hakuna Watanzania wanaoweza kuingia kwenye ubia na wawekezaji toka nje kwa faida ya pande zote zinazohusika.
Nchi zinazozungumziwa sana ni ile ya Korea Kusini, Iran, Uturuki na zile za Kiarabu.

NInaamini kuzipa nchi hizi za nje ardhi ya Watanzania moja kwa moja kama vile ardhi hiyo haina wamiliki wake wa asili na haina thamani yoyote na Watanzania wahusika hawastahili wao wenyewe kufanya maamuzi juu ya ardhi yao ni kukiuka katiba na kwamba mamlaka na madaraka juu ya maamuzi ya matumizi ya rasilimali za nchi hii inayo wananchi wenyewe na serikali ni watendaji na watekelezaji wa maamuzi ya wananchi na sio vinginevyo. Kwa kila hali serikali na viongozi wake wamepituka uwezo ambao tumekasimu kwao.

Kutokujua au ujinga wa wananchi kuhusu haki zao katika ardhi, sio tu kiumilikaji na kiunufaikaji, ila katika kubwa zaidi kwamba wao ndio wanaostahili kuwa wamiliki wa rasilimali zao na maamuzi yote juu ya matumizi ya ardhi yanastahili kufanywa na jamii zao ndiko kulikochangia wajanja wachache kujinufaisha kwa kuwatumikia wakuu wa mikoa na wilaya sio tu kujimegea ardhi katika maeneo wasiyo na nasaba au ukuruba nayo, bali pia kuwauzia wawekezaji wao wakanufaika na wananchi wakaendelea kuwa maskini japo rasilimali yao imeuzwa na walistahili kunufaika na mauzo hayo.

Hakuna anayepinga nchi, kampuni na watu kutoka nje kuwekeza katika kilimo nchini. Tunachokipinga ni uwekezaji unaofanywa kwa namna ambayo kilimo vijijini mwetu na wakulima katika vijiji vyetu hawatasaidiwa kubadilika kitu na uwekezaji kama huo.

Uwekezaji tunaostahili kuupigia debe ni ule ambao nchi fulani duniani au kampuni fulani au mtu fulani anayekuja kuwekeza Tanzania ANAINGIA UBIA na mojawapo ya vijiji vyetu ili kuitumia ardhi ya kijiji kulima, kufuga, kuvua au kufanza mradi wowote ule huku wananchi wa kijiji husika na mwekezaji mwenyewe wakivuna na kugawana kinachopatikana kwa namna watakayokubaliana wenyewe kwa manufaa ya wote.

Kwa mtaji huu mwanakijiji atakuwa sio tu na soko la nguvu kazi yake; bali pia atanufaika na soko la nje, elimu, ujuzi na teknolojia atakayoleta mwekezaji huku wakizalisha mali ambayo itachangia kunyanyua hali ya maisha ya wanavijiji wahusika na kipato cha mwekezaji na nchi kadhalika.

Kabla ya nchi- wawekezaji kuruhusiwa kuwekeza katika kilimo hapa nchini ni muhimu benki ya wakulima iwe tayari imeanzishwa. Fedha zinazolipwa na nchi, kampuni na watu wanaowekeza katika kilimo zitawekwa katika benki hii zikigawanywa katika mafungu ya hisa za mwekezaji na kiasi fulani kutumika kuendeleza miundo mbinu na huduma muhimu vijijini na sio vinginevyo. Tathmini halali, halisi na haki ya thamani ya mtaji watu wa kijiji husika, utamaduni na urithi wao, ardhi yao, misitu yao na mali asili zao nyingine ikishafanyika Benki ya Wakulima itatoa hati ya uwekezaji au mkopo inayolingana na thamani ya rasilimali za kijiji. Thamani hii itakayokuwa katika shilingi ya Kitanzania itakuwa ni sehemu ya uwekezaji wa kijiji husika wenye thamani sawa na fedha zilizochangwa na mwekezaji katika kijiji chao.

Tunapaswa kukubali kuwa hii ndiyo njia pekee ya vijiji vyetu kulala maskini na kuamka matajiri kesho yake. Na kwamba serikali inawjibika kuwezesha na kurahisisha hili, kwani haina namna yoyote nyingine inayoweza kuondoa tofauti kati ya vijiji na miji na kupunguza matatizo ya miji yanayotokana na kusahaulika kimaendeleo kwa vijiji ila tu kwa mkakati na mbinu hii. Katika muktadha uliopo ni muhimu viongozi wetu wabadilike kimawazo ili nchi iweze kuendelea kijamii na kiuchumi. Mustakabali wa ustawi na mafanikio ya vijiji vyetu unategemea hili kuliko kitu kingine chochote duniani.

Hakuna kiongozi wa zamani au leo binafsi ambaye kwa kuwekeza mwenyewe katika kilimo na ufugaji anaweza akatutoa kutoka kwenye dunia ya tatu na kutupandisha hadi ya pili. Ni pale wakulima wote kwa pamoja wanapopewa fursa hii ndio hili litakuwa na nafasi angalau ya kuwezekana.

Sera za MKUKUTA wa I na wa II zimeshindwa kuchangia cha maana katika kuondoa umaskini wa Mtanzania kwa sababu hazikufanikiwa kuainisha kwa usahihi chanzo cha umaskini wetu. Na chanzo hicho sio kingine ila ardhi na mali asili nyingine za Tanzania kutokuwa na thamani halisi, halali na ya haki kiasi cha kuwanufaisha Watanzania kupitia umilikaji wao katika harakati zao za kujikomboa kiuchumi.
Bila umiliki huu, maamuzi na usimamizi wa ardhi na mali asili za wanajamii kufanywa na wananchi wenyewe rasmi haitakuwa rahisi nchi yetu kuondokana na umaskini wa kutupwa kwa walio wengi.

Tathmini ya haki, halisi na halali ikifanyika watu, urithi na utamaduni wao, vijiji vyao, maliasili zao, ardhi na rutuba yake, uoto, maji na ujumla wa mtaji wao wa kijamii ni vitu vyenye thamani sawa na fedha, mashine na mitambo yote itakayoletwa na mwekezaji yoyote yule.

Hii ina maana kwamba vijiji vyetu na jamii zake vina kitu cha thamani au rasilimali ya kuwekeza bila kutoa senti hata moja mfukoni mwao.

Ili kusahihisha kosa hilo la kihistoria hapo juu ninashauri kwamba sio vyema nchi, makampuni na watu kutoka nje kupewa ardhi ya Watanzania moja kwa moja bila ushirikishwaji na ubia wa vijiji na wanavijiji katika uzalishaji na uuzwaji na unufaikaji wa mazao husika.

Ni wataalamu wa tathmini ya mambo husika na sio wanasiasa wanaostahili kuamua kwamba kijiji na wanakijiji fulani kwa ujumla wao wana mali za thamani ya kiasi gani na muwekezaji akishawekeza mgawa wa mapato kutokana na shughuli za kilimo zitakazoendeshwa utakuwa vipi?

Saturday, September 10, 2011

Maafa yakishatokea ndipo tunapopata akili

USAFIRI na UCHUKUZI Tanzania uwe wa barabarani, angani au majini umezungukwa na kila aina ya mapungufu na kukosa ukaguzi na udhibiti wa kutosha.

Aghalabu tunakuwa na akili pale balaa linapotokea na roho zinapopotea. Wakubwa na mamlaka zao wamekaa zaidi mkao wa kufurahia ukubwa na vyeo vyao na wala sio kutekeleza kile ukubwa au cheo husika kinachowataka kutekeleza. Na hakuna anayewasema wala kuwachukulia hatua, maana pengine na wakubwa nao wamekaa mkao huohuo.


Maafa kama yaliyotokea mkondo wa Nungwi ni kitu kilichokuwa kikisubiriwa tu kitoke na Mungu aepushilie mbali yapo mengine kama hayo yanayotusubiri kwenye maziwa na bahari zetu, barabarani na angani kama tusipozinduka na kuanza kudhibiti kila kazi inayogusa maisha ya watu hapa nchini, ili kuwe na uhakika na usalama wa maisha ya watu na mali zao.

Ilivyo hivi leo ni kwamba mtu akiwa na fedha au cheo anaweza akafanya lolote hata kama kwa kufanya analolifanya anahatarisha maisha ya maelfu ya Watanzania wasio na kosa. Na sheria zilizopo ni sheria bibi au sheria nyanya ambazo hazimsaidii mzawa kwa lolote zaidi ya mamba kumwaga machozi yao na huruma za kisiasa ili watu wahurumiwe kwa kuonekana wana huruma wakati huruma yao ilikuwa inatakiwa ionekane kwa kuona mbali na mbele, kupanga na tathadhari kuchukuliwa kabla ya janga husika. Ambayo hii kwa hakika ndiyo kazi ya uongozi, yaani, kazi ya uongozi ni kuona mbali na mbele na kuwaepusha wananchi na matatizo yanayoweza kutokea aidha kutokana na uzembe wa watu au amri ya Mwenyezi Mungu.

Hakuna tume itakayoundwa na ikamsaidia mtu yeyote kama serikali na waendeshaji wake wasipojichunguza na kuangalia utendaji wao na kwa kiasi gani unakidhi changamoto za usalama na ulinzi wa raia na mali zao.

Wataalamu wanadhihirisha Watanzania ni wazuri sana kwa mipango na kupanga lakini ni wabovu katika utekelezaji wa kila jambo kwa sababu udhibiti, ukaguzi na ufuatiliaji mambo husika haupo au upo kwa kiwango cha chini sana.

Ieleweke kwamba, hatumlaumu yeyote kwa sasa lakini tukubaliane kwamba 'uswahili', yaani, ubabaishaji au kufanya kazi tu mkubwa anapokuwepo au kwa kubebembelezwa, au kule kufanya mambo kama vile mtu hutaki au kuamini kwamba kitakachotokea ni amri ya Mungu na huwezi kukizuia, sio tu utatugharimu maisha na mali nyingi sisi wenyewe bali utawafukuza pia watalii na wawekezaji watakapoona umezidi na hauvumiliki. Ni lazima tubadilike.

Ingelifaa sote, pamoja na tume husika tujiulize maswali yafuatayo:

.Je ni kweli au si kweli kwamba meli zilizo katika bahari ya Hindi na katika maziwa ya Tanganyika, Victoria na Nyasa ni chakavu na zimeshapita muda wake wa kuishi lakini tunazilazimisha kuendelea kubeba abiria?

.Je ni kweli au si kweli kwamba meli nyingi zinazosafiri kwenye bahari na Hindi pamoja na kuwepo kwa SUMATRA na maofisa bahari na forodha bado zinasafiri bila kuwa na vifaa tosha kama 'lifejackets' kuokoa maisha ya watu meli inapozama? Na kwamba ukaguzi na udhibiti kwa hili ni mdogo mno au sawa na haupo?

.Je ni kweli au si kweli kwamba moto ukitokea katika migodi, nyumba, shule, hospitali, meli, basi au treni ni watu wachache sana watakaonusurika kwa sababu hatua zinazolazimisha kuwepo na vizimia moto vya dharura haziheshimiwi na hazionekani kama ni muhimu. Na Uswahili unatawala kuliko utawala wa kisheria?

.Je ni kweli au si kweli, kwamba barabarani ukishakuwa tajiri au na cheo kikubwa unaweza ukavunja sheria na usifanzwe lolote?

.Je ni kweli au si kweli kwamba wenye mali au vyeo au wapambe wao wanamiliki magari mabovu yanayobeba kama mende mizigo usiku na hayaachi kufa njiani kila siku katikati ya barabara na kuua mamia ya Watanzania wanaoshtukizia wameshaingia nyuma yao.

.Je ni kweli au si kweli, kwamba mamia ya daladala jijini ni mbovu na hazifai kubeba abiria lakini kwa kuwa zinamilikiwa na wakubwa au jamaa zao zipo na zinaendelea kufanya kazi bila kubughudhiwa na mtu?

.Je ni kweli au si kweli, au reli zetu zimeoza na zinafaa kung'olewa na kuwekwa mpya ila kuhakikisha usalama wa wanaozitumia?

.Je ni kweli au si kweli kwamba balaa la maji au mafuriko au gharika ikitokea tutaangaza angaza macho tu kuiongojea nusura ya Mwenyezi Mungu na serikali yetu na tunaowalipa kodi hawataweza kutusaida kwa lolote!

.Je ni kweli au si kweli kwamba Tsunami ikitokea kwenye pwani Pemba, Unguja au Mrima kitakuwa ndio kiama kwa wakazi wengi wa maeneo ya huko maana hatuna lolote kitahadhari tulilowahi kulifanya huko wala tunalolifikiria kufanya hivi sasa?

.Je ni kweli au si kweli kwamba tufani au upepo mkubwa vikiikamia Tanzania hakuna miti wala zana maalum za kupunguza makali ya balaa litakalotuangukia?

.Je ni kweli au si kweli kwamba migodi na machimbo yetu mengi hayana usalama wa kutosha na waliomo humo wanapona tu kwa kudra ya Mwenyezi Mungu?

.Je ni kweli au si kweli kwamba baadhi ya vyakaula na vinywaji vinavyoruhusiwa kuingia nchini toka nchi za nje ni hatari kwa uzima na afya ya Watanzania?

.Je ni kweli au si kweli kwamba maji, vyakula na viliwa vingine katika mahoteli yetu uswahilini yasiyo na vyoo wala vilinda afya na siha havina tofauti na kula sumu. Na kwamba pakiwa na viwango vinavyodhibtiwa sio tu afya na usalama wa walaji vitahakikishwa bali tutajijengea heshima mbele ya watalii, wawekezaji na wageni kwa ujumla?

Katika miaka hii ya utandawazi, hatuna muda wa kupoteza. Ni muhimu kubadilika mara moja. Kazi kubwa kuliko nyingine zote za serikali ni kuhakikisha kuwa maisha na mali ya raia zake inalindwa. Serikali ikiterereka katika hili huo unakuwa ni mtihani mkubwa kwetu sote!

Na je ni kweli au si kweli kwamba ubabe na uzembe wa wenye vyombo vya usafiri na uchukuzi hapa nchini unatokana na thamani ya Mtanzania kuonekana ndogo kuliko ya ng'ombe au punda na fidia ya maisha ya Mtanzania anayepoteza kufa maisha kuwa vijisenti tuchache tu? Na kwamba fidia hiyo ingekuwa kubwa kiasi cha kumfilisi mmiliki wa chombo ajali ZINGEPUNGUA SAAANA!!!

Benki Kuu iwe na kapu la sarafu mchanganyiko

HALI ya kifedha na kiuchumi ya Marekani na misuguano ya kisiasa inayoendelea nchini humo haitupi moyo Watanzania kwamba panaweza kuwa na mabadiliko ya maana kiuchumi duniani hivi karibuni.

Marekani na nchi za Ulaya zenye matatizo makubwa zimekuwa zikiishi nje ya uwezo wao kifedha. Kwa maana ya kwamba serikali za nchi hizo zimekuwa zinatumia fedha nyingi kuliko fedha zinazoingiza kila mwaka, na hivyo kukuza mzunguko wa deni na riba serikali hizo zinazodaiwa kwa hasara ya wananchi wao. Wote tunajua hatari ya mtu anayedaiwa. Akiugua ghafla au kupatwa na janga fulani basi ndio wanaomdai wasahau tena kupata chochote kutoka kwake. Ndivyo zilivyo serikali ambazo baadhi yake nchi zetu zimewekeza na hivi leo zina matatizo makubwa ya kifedha. Hali ikiwa mbaya zaidi katika nchi hizo hawatatufikiria sisi kwanza bali wananchi wao kwa hasara yetu na nchi zetu. Ndio maana, wazo la kuwa na kapu la benki kuu lenye sarafu mbalimbali halitofautiani sana na kuweka mayai waliotaga kuku wetu wa kiuchumi katika makapu mbalimbali na sio kapu moja.

Ukizingatia pia kwamba hali ya kifedha ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya kwa baadhi ya wanachama wake ni muflisi, ipo haja ya Waafrika na hususan Watanzania kuzinduka na kukagua upya kama sarafu na vito vya thamani vilivyoko katika hazina yetu ndivyo vinavyoweza kutunusuru kama hali ya kiuchumi duniani itaendelea kuzorota au kuwa mbaya zaidi ya ilivyo hivi sasa.

Hivi karibuni, Gavana wa Benki kuu ya Shirikisho la Nigeria, Sanussi Lamido Sanussi, ametangaza kwamba benki kuu ya nchi hiyo kuanzia sasa itaweka akiba yeke ipatayo asilimia 10 katika fedha za Kichina au Yuan. Hiki ni kitendo cha kijasiri na kiume na ambacho kinastahili kuwa fundisho kwa nchi nyingine za kiafrika ambazo kwa miaka mingi sasa zimekuwa kama mateka kama sio watumwa wa dola ya Marekani au Faranga ya Kifaransa au Pauni ya Kiingereza.

Hili liliweza kuwa sawa wakati ambapo dalili zote zilionesha nchi hizo ni kubwa na zenye uchumi usioterereka na uliokuwa ukikua kwa kasi inayobashirika. Katika miaka hii ambayo, utegemezi wa nchi hizo kwa rasilimali na biashara toka nje umeendelea kuongezeka ni hatari sana kukubali hifadhi ya taifa kuwa katika sarafu ya nchi moja au mbili tu.

Jambo hili tofauti na huko nyuma inafaa lizungumzwe na wananchi wakiongozwa na wataalamu wa uchumi na mambo ya fedha badala ya kuishia kufanyiwa uamuzi na serikali au benki kuu peke yake. Ukiritimba huu wa maamuzi ndio uliosababisha dhahabu kupakuliwa toka Benki Kuu kiujanja na kuiacha Tanzania ikipata kipigo kushoto na kulia kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu yake na kupanda kwa bei ya mafuta.

Mazungumzo kama hayo yatatusaidia pia kuepuka kudanganywa na nchi zilizoendelea kwa kugaiwa kondomu na chandalue zenye dawa za bure huku nchi hizo zikihamisha vitu vyenye thamani mara elfu kumi kama sio zaidi kwa matani kwenda kuwatajirisha huko kwao na kuendelea kutuacha sisi masikini wa kutupwa na ombaomba.

Yuan inapigwa vita kwa madai kwamba China bado ni nchi ya kikomunisti na kidikteta, hoja ambayo inakataliwa na wengi kwamba sio kikwazo maana Wachina walio wengi wanaridhika na mfumo huo kwa kuwa umewaletea shibe na neema. Kuna maana gani ya kuwa huru, huku ni masikini unayetumika na wakubwa?

Hali kadhalika, kutokana na wingi wao ni vigumu kuwa na nchi isyodhibtiwa kwa karibu. Viongozi wa Kichina wanaonekana pia kuwa bado ni wanafunzi katika demokrasia na siasa za kiliberali na hivyo wanahitaji kupewa muda zaidi kuweza kuachia mambo yawe yanayojiendesha yenyewe.

Dai lingine ni kuwa fedha ya China inadhibitiwa na haiachiwi kutulia na kuamua thamani yake halisi ukilinganisha na fedha nyingine duniani. Jambo hili nalo linaeleweka na kwa yakini nchi zinazoendelea zinachagizwa kuiga vivyo hivyo, kwani ukiilazimisha sarafu yako kupimwa na sarafu zenye nguvu zaidi, daima ni wewe utakayeumia na sio wale wenye nguvu. Wachunguzi wanaamini katika hili pia China inahitaji muda ili kuhakikisha ughali wa vitu vinavyotengenezwa Ulaya kwa sababu ya mishahara mikubwa ya Wamarekani na Wazungu haiingilii biashara na faida ya Wachina ambao wanalipa mishahara midogo na kukubali kuishi kimasikini ili wenzao katika nchi zinazoendelea wapate bidhaa zisizokuwa ghali.

Ni lazima tuoanishe mahitaji yetu toka nje na sarafu za nchi tunazotakiwa kuwa nazo katika hazina ya benki kuu. Ninaamini masuala kama mitambo, magari na mashine, mafuta, wapewa kandarasi za ujenzi wa miundo mbinu, masoko ya mazao yetu, masoko tunayonunua teknolojia zetu mbalimbali, wanakotoka wawekezaji wetu wakubwa, wataalamu na rasilimali watu muhimu tunazohitaji vinaweza kutumika kuchagua kapu la sarafu Benki Kuu yetu inayostahili kuwa nazo wakati wowote kwa ajili ya kujikinga na kupanda na kushuka kwa uchumi wa dunia na thamani ya shilingi yetu.

Ni dhahiri katika kufikia uamuzi wa jambo hili kuna wengi watakaopinga. Lakini kwa watu kama hao tunawataka watofautishe maamuzi ya kifedha/kirasilimali na maamuzi ya ya kisiasa na mazoea. Pamoja na mapungufu yake kadhaa kisiasa na katika haki za binadamu bado ukweli unabakia pale pale kwamba hatuwezi kukwepa kufanza biashara au kuwa na miradi inayojengwa na Wachina hapa nchini. Kwalo hilo tu, litatuondolea adha ya shilingi kupungua ukilinganisha na dola, maana thamani kati ya yuan na shilingi inaweza ikabakia pale pale kwa faida yetu.

Kwa kuikubali yuan ya Uchina tutawarahisishia pia wawekezaji wa Kichina na Mashariki ya mbali kwa ujumla wanaotaka kuwekeza hapa nchini, kwani tayari yuan inakubalika kama sarafu ya uwekezaji sehemu mbalimbali duniani. Hii ina maana wawekezaji wazawa hapa nchini wanaweza kuuza hisa katika yuan kwa Wachina ili wawe wabia wao katika uwekezaji na hivyo kupata wawekezaji wazito zaidi kutoka huko, kuliko tunaowapata hivi leo ambao wameishia kushindana na Wamachinga Kariakoo.

Aidha tunaweza kukopa toka Uchina kwa kununua hawala za Kichina kwenye sarafu yao ya yuan/renminbi na hivyo kupunugza machungu ya riba kubwa kutokana na kushuka kwa thamani ya dola ukifananisha na shilingi ya Tanzania.

Wazo kubwa hata hivyo kwa wakati tulionao unaitaka Afrika Mashariki kuanzisha sarafu yake ndani ya sarafu zilizopo. Sarafu hiyo, tuseme, iitwe, Pauni au Dola ya Afrika Mashariki itaundwa kwa kuzihusisha sarafu muhimu duniani kama Pauni ya Uingereza, dola, yuan ya Uchina, Yen ya Japan, Kronor za Scandinavia, Escudo za Brazil, rupia za India na Euro ya Jumuiya ya nchi za Ulaya. Sarafu hii itaachiwa taratibu kama ilivyo kwa Euro Ulaya kuzing'oa sarafu binafsi za kila nchi na hivyo kurahisisha kuja kwa soko la kifedha la pamoja la Afrika Mashariki na masoko mengine yatakayofuatilia.

Ieleweke kwamba pale msiba unapotokea kwa mwenzio, kwako kunaweza kuwa harusi,kwa maana kweli unaoza mwana au kwa kuwa jirani yako alikuwa mchawi.

Uchumi wa dunia unapotatizika, sio lazima uchumi wetu nao pia uwe kwenye matatizo. Lakini hili linahitaji uangavu, uweledi wa mambo, uzuzi na ubunifu wa yale yasiyoyumkinika na ambayo wengi huchelea kuyafanza kwa kuhofia hasara kumbe kwa kuyafanya watanufaika na kunufaisha nchi na watu wao. Huu ni wakati kama huo, kwa kutumia fursa za kiutandawazi tunaweza kugeuza matatizo yetu yakawa ndiyo chanzo chetu cha kufanikiwa katika mengi ambayo huko nyumba tulishindwa. Maana maendeleo yote hutoka katika akili za mtu, lakini sio wale wanaoiba na wasiojua undani na usadifu wa wazo husika.