Sunday, July 28, 2013

Bomu linalosubiri kulipuka Afrika: Tofauti ya walionacho na wasionacho..

Kabla ya 2010 dunia ilijikita zaidi katika kushughulikia changamoto zilizosababishwa na athari au madhara yanayosababishwa na walimwengu kwa hali ya hewa na mazingira duniani. Kuanzia muongo wa pili wa karne ya ishirini na moja, hata hivyo, mtazamo na mwelekeo wa wanauchumi na wanajamii kwa ujumla umekuwa ukiegema zaidi upande wa namna au jinsi ambayo masuala ya kiuchumi na kijamii yanavyoweza kuhatarisha sio tu maisha ya mwanadamu, bali hata kuzidisha uwezekano wa athari mbaya dhidii ya mazingira na hali ya hewa kuongezeka. Katika makala ya leo tutajikita zaidi katika suala la kukua tofauti za kipato au kiuchumi kati ya wale wenye nacho na wasionacho. Tafiti zilizofanywa na Prof. Joseph E. Stiglitz wa Chuo Kikuu cha Columbia cha nchini Marekani, ni kazi nzuri inayokuja wakati muafaka katika kuitahadharisha dunia kuwa mfumo wa ubepari usiodhibtiwa budi utazipeleka nchi na dunia kubaya. Na kwamba upo umuhimu wa kujitoa kimasomaso kuja na sera ambazo hazitaipelekea Afrika kujikuta kwenye masahibu ambayo baadhi ya nchi za Ulaya na Asia leo zinalazimika kuyafungia kibwebwe. Mfano wa nchi ambazo zinajenga mfano mzuri wa kuigwa katika kudhibiti pendo kati ya walionacho na wasionacho ni nchi za Skandinavia. Nchi hizo hazina muujiza wowote ila tu ni kule kuanzisha kwao na kutunza mikakati na sera ambazo wanazitumia kuzuia kulipuka kwa tofauti kubwa katika kipato cha watu wa kima cha juu na wale wa chini. Sera hizi hubainika na wengi duniani kama mfumo wa ujamaa wa kidemokrasia. Laiti Tanzania isingetupa moja kwa moja siasa ya Ujamaa na Kujitegemea leo tusingekuwa na cha kuandika hapa. Hasara yetu ni sawa na ile ya mwogeshaji mwana, kumtupa mwana na maji machafu aliyeogeshewa. Nchi zinazoathirika zaidi ni zile zenye kukosa azma na sera kwa malengo ya kisiasa na kijamii yaliyo dhahiri na yanayokubalika kama dawa mujarabu kwa tofauti za kiuchumi na kipato katika jamii husika. Aidha, vijiji kusahaulika kimaendeleo kwa kukosa mipango ya kuvisaidia kupata uongozi au menejimenti bora ikiwemo ile ya rasilimali watu, usimamiaji uzalishaji mali, utafutaji mitaji na masoko Ujamaa, ubepari ni jambo jengine linaloendelea kuchangia kukua kwa tofauti za kipato hususan kati ya watu wa mijini na wale wa vijiini. Sera zozote zinazochania kumnyang'anya masikini hata kile kidogo alichonacho sio chachu ya kudumisha amani na umoja katika jamii husika. Katika nchi nyingi zilizoanza na kuendelea na ubepari tofauti hizi husababishwa kwa kiasi kikubwa kwa baadhi ya watu aidha kuzaliwa katika utajiri au ukubwa au nafasi zenyemlo na wengi wengine katika umaskini, hivyo kuwapa wale wa kwanza mtaji wa kiuzawa na vilevile kutokana na tofauti za kiajira na kielimu na uweledi wa kiteknolojia na utaalamu wa tasnia husika. Katika nchi zilizokuwa zikifuata ujamaa tofauti hizi zinazaliwa na watawala waliokuwa wajamaa kugeuka mabepari kwa kunufaika na mali zilizokuwa za umma huku wakigwaya kukiri kwa wananchi wao kuwa wao na nchi sasa ni ya kibepari na sio tena ya kijamaa; utumishi unaojali zaidi uswahiba na udugu na sio tija na ufanisi; utegemezi wa upendeleo, rushwa na teni pasenti kwa vyama tawala badala ya njia halali za mapato; wanasiasa kununuliwa na matajiri na fisadi; mabenki na taasisi nyingine za fedha kuwa chini ya wanasiasa wanaotawala; misaada toka nje kuwanufaisha watawala kuliko wananchi; kukosa uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa mipango, mikataba, siasa na sera za nchi husika; kusaini mikataba mibovu kwa faida ya chama na watu binafsi na sio kwa faida ya umma; kukosekana ushindani wa kweli wa kidemokrasia kisiasa na kiuchumi;kuwanyima fursa wapinzani wa kisiasa na watawala au watu wao kupewa fursa hizo; uwepo wa makampuni yasiyotozwa kodi tosha na ambayo yanaweza kuzaini umma na yenyewe kutengeneza mabilioni kama sio matrilioni katika muda mfupi tu bila udhibiti na ukaguzi wa uhakika toka kwa wanaohusika na ardhi na maliasili za nchi kuwafaa zaidi watawala, wageni na wenye nacho na sio mwananchi wa kawaida. Jambo jengine linachangia si haba kukuza pengo kati ya walio nacho na wasio nacho ni lile la kukosa vigezo vinavyokubalika katika ajira na ujira. Kwenye nchi nyingi waliosoma sana na wenye ujuzi mkubwa zaidi ndio hulipwa kidogo lakini wasiosoma bali wana vyeo wao wakafaidi ujira, masurufu na maduhuli makubwa zaidi. Nchi nyingi maskini kama vile Tanzania zina matatizo pia ya kushindwa kuwa na sera na mipango inayofanya kazi katka masuala ya matumizi na ugawanyaji pato la taifa kitaifa, kijamii mbalimbali na kati ya tasnia na makundi kazi mbalimbali katika jamii. Kosa lingine linalochangia kukua kwa pengo kati ya walionacho na wasio nacho ni kushindwa kuipa mali asili yetu kama ardhi, madini, mimea na watu wetu thamani stahilifu na inayoweza kuwanyanyua watu wetu kiuchumi na kimapato kwa njia moja au nyengine. Udhaifu katika menejimenti ya uchumi wa nchi na hasa uzalishaji mali na ujasiriamli ikiwemo, mathalani, fursa ya kuviongoza vijiji kiuchumi na kimapato zaidi nayo inachangia tatizo hili si haba. Kuna wanaodai kuwa vijiji na wanavijiji wakiboreshewa tu masuala ya menejimenti na utawala nchi inaweza kupunguza nusu ya umaskini wake kwa haraka zaidi kuliko inavyotarajiwa na hasa panapokuwa na uwekezaji unaolenga kutmia kile wanakiji walichonacho katika kuwasaidia kupata maendeleo makubwa zaidi. Siasa za WB, IMF ambazo leo zinakataliwa na Ulaya na Amerika wanaopitia matatizo yaleyale kama yetu zinahitaji pia kukataliwa waziwazi kwani zinachangia hatari ya kutuletea matatizo makubwa zaidi siku za usoni. Ipo haja ya kuangalia upya, baada ya nchi yetu sasa, kugundua mali asili mpya kama gesi, mafuta ya peteroli na madini salama kuvunwa ya aina mbalimbali ni kwa jinsi gani Tanzania inaweza kurejea tena kwenye mfumo mzuri uliodhibiti vilivyo tofauti ya kipato na kiutajiri kati ya watu wetu kama vile utoaji elimu bure; utoaji huduma za afya bure; kutoa ruzuku katika huduma muhimu kama zile za maji na umeme, usafirishaji na uchukuzi; kuwatunza maskini, yatima na wajane kwa kujitolea na nyenginezo kama hizo. Benki Kuu na vyombo vyetu vya fedha lazima zibadilike ili kuwa vyombo vya kupunguza pengo kati ya walichonachona wasionacho kwa namna moja au nyengine. Na kuu katika hili ni kuhakikisha kuna mifuko maalum ya kusaidia miradi kwa wanavjiji, vijana, wanafunzi wanaomaliza shule na wanatafuta kujiajiri na watu kama hao kwa kuiga mifano iliyofanikiwa ndani na nje ya nchi ili kzungusha pato la taifa na kutoa fursa kubwa zaidi ya uwekezaji wa wazawa nchini.

Tuesday, April 23, 2013

Migogoro ya Kiimani matunda ya kukosa uongozi jumuishi, bora na adilifu kijamii, kiuchumi, kidini na kisiasa

NCHI zote ambazo asili na utu wao unatawakali mbele ya vitu vingine duniani ndizo zilizotulia na zilizoepuka machafuko na migogoro ya kijamii na kiimani kwa kiasi kikubwa. Kuanzia Uarabuni, Uchina, India, Urussi, Vietnam, Malaysia, Indonedia, Ufilipino na kddhalika. Matatizo katika nchi hizi yanakuja pale mataifa haya yanapoanza kuzainiwa na kuacha kutanguliza asili, historia na utu wao kwanza na wakakubali kutanguliza kitu kingine mbele iwe dini au maslahi fulani au ukabila au ueneokijiografia au uchama na kadhalika. Utaifa, historia, desturi na utamaduni wa watu vinapopewa hadhi stahilifu husaidia sana na kuiepusha nchi kukwepa pepo za ushawishi na mbadaliko ya kimtazamo kutokana na kuingiliana na watu wa asili na tamaduni nyingine. Migogoro ya kiimani Afrika na hususan Tanzania ni matunda ya kuurudisha nyuma Utanzania na Uafrika wetu na kutanguliza maslahi ya kiitikadi na kibinafsi miongoni mwetu na hasa kati ya viongozi wetu. Hili nalo kwa maoni yangu linasababishwa na kushindwa kutambua kwamba uongozi bora ni jambo la ushirika kiushauri na la pamoja. Ukijenga ukiritimba katika uongozi mara nyingi unaharibu, badala ya kutengeneza. Kila jamii ina aina mbalimbali ya viongozi. Kuna viongozi wa kiseriikali, kisiasa, kiimani, kimila/kiutamaduni, kiuchumi/kibiashara, kiteknolojia na kadhalika. Pale viongozi wa kiutawala au wa kisiasa wanapoona kwamba wao ndio tu wanaostahili kuitawala jamii na sio viongozi wa aina nyingine, basi migogoro katika jamii hiyo haiishi na imani ya wananchi kwa viongozi wao hao hupungua kwa kiasi kikubwa. Katika hili yapo mengi ya kumuiga mwasisi wa taifa hili, Mwalimu J.K. Nyerere na moja kubwa ni kwamba hakusita kuwaita na kuwaambia waziwazi na bayana viongozi wa kiimaniya kwamba mpaka we0katika hili ni huu hapa na msivuke mstari huu. Maana Mwalimu aliutanguliza kwanza Uafrika na Utanzania wake kabla ya kitu kingine. Kuutanguliza Utanzania, Uafrika na utu wetu mbele ya kttu kingine ndiyo nguzo ya kwanza ya amani na umoja wetu. Athubutu mwingine kutwambia vingine. Ninaona katika hili, hivi leo kuna udhaifu mkubwa miongoni mwa viongozi wetu. Endapo tunataka kuondokana na migogoro inayolinyemelea taifa letu kwa hivi sasa ni lazima tuukubali ukweli huu hapo juu na kuanza kuandaa mifumo na miundo ambayo itawapa viongozi wote katika sehemu na ngazi zote nafasi ya kuchangia maendeleo ya nchi na watu wetu. Kinachoonekana kwa hivi sasa ni kwa viongozi wetu mbalimbali kuchomwa moyo zaidi na kujihusisha na vidonda na vipele na sio chanzo halisi cha gonjwa la kukosa sio tu amani bali upendo, ushirikiano na kuaminiana kati ya wanacnhi wetu kama ilivyokuwa kwenye awamu ya kwanza ya serikali ya Tanzania. Ieleweke hakuna Mtanzania mmoja aliyekuwa na akili kuliko Watanzania wote wakiwekwa pamoja na anayeamini hivyo sio tu anajidanganya ila yeye ni tatizo kubwa. Akili ni nywele na kila mtu ana zake. Taaluma, uwezo na kushindwa kujifunza kutokana na historia na watu wengine kwa ujumla ninaamini ni jambo moja linalochangia kuwepo kwa migogoro ya kiimani ambayo isingelikuwepo kwenye miaka ya sabini na themanini hapa nchini kutokana na dini kuwa mikononi mwa viongozi walioisoma jamii vyena ma waliojitahidi kutoa mchango wao katika kuifanya jamii yetu kuwa kitu kimoja. Hizo ni enzi ninazozikumbuka wakati wa viongozi kama Hemedi bin Juma, Kadinali Rugambwa, Askofu Moshi, Askofu Sangu na viongozi wa dini nyingine ndogo kwa kubwa waliojua kutenga kilichokua cha Kaizari na kilichokuwa cha Mungu. Leo tuna mamia ya watu wanajiona wao ni bora mara mia ya viongozi wao. Lakini tukumbuke pamoja na yote uongozi ni zawadi kwa wema au ubaya toka Kwa Mungu. Katika miaka hii kwa bahati mbaya sana kila sekta inaingiliwa na wanasiasa, matajiri na watu kama hao wanaotaka kuwatumia watu wengine kujitajirisha, kujenga umaarufu na wakati mwingine kuihadaa na kuigombanisha jamii kwa maslahi yao binafsi na sio maslahi ya walio wengi. Izingatiwe kwamba katika taifa lolote kuna asilimia ya watu 97 wanaofikiri kwa moyo na ni asilimia chini ya 3 wanaofikiri kwa akili. Ni asilimia hii 3 ndiyo ambayo aghalabu inayozusha matatizo ya kila aina. Huwa wanadhani wanajua, kumbe hawajui kitu. Wanajihadaa wao wenyewe na wale wanaowahadaa kwa hasara ya nchi na watu wake. Ipo haja ya kuwa na Taasisi ya Kuwafunza viongozi wote wawe wa kisiasa au kidini au kibiashara mahala pamoja juu ya nadharia na dhana na imani na kanuni za msingi zitakazochangia kutuunganisha badala ya kutugawa. Kwa namna hii, kila kiongozi nchini wa kundi lolote lile atajifunza lililo sawa kufanza na lisilo sawa kulifanza pale anapoteta au kufanya jambo lolote lile hadharani. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ingelipitia kwa mara nyingine tena uwepo wa 'World Conference of Religions for Peace' hapa nchini (taasisi muhimu sana inayopuuzwa kiasi cha kutisha) na kuona ni kwa namna taasisi hiyo inaweza kushikishwa na kuwezeshwa kufikia malengo na madhumuni yake ambayo kwa mapana na marefu ni hayo hayo au pengine zaidi ya hayo aliyogusia na anayoyahofia mheshimiwa Kikwete katika hotuba yake ya hivi karibuni. Kinachoonekana hapa nchini ni kwamba kuna watu na taasisi kabakaba ambazo zikiachwa kupuuzwa na zikashirikishwa katika changamoto na vilio vyetu mbalimbali vya kila siku, taasisi na watu hao wanaweza kutoa mchango wenye thamani na faida kubwa kwa nchi na watu wetu. Tuzinduaneni na tufanye kweli, lawana na hotuba zisizokwisha na zisizobadili kitu haziwezi kutufaa kwa lolote. Kisiasa ni muhimu kupitia upya na sera zinapendelea wanachama wa chama fulani na kubagua wa vyama vingine. Wanasiasa wakifanya hivyo, je, watu wa Mungu nao watahesabika wamefanya kosa na wao wakifanya ubaguzi kama huo? Wanasiasa wetu waelewe kuwa demokrasia na mfumo kamili, unapouwekea vikwazo upande mmoja, unachangia pia kuvuruga na kwignine usikokujua. Unafiiki na undumilakuwili ambao aghalabu unachangia mara kwa mara isijulikane kama hivi leo wanasiasa hapawanasema kweli au uongo hauwezi kutusaidia katika changamoto zilizo mbele yetu. Lazima viongozi wa dini na kisiasa wakubaliane kwamba nchi yetu haiwezi kujengwa juu ya misingi ya uongo, Kujitia uziwi na upofu unapoambiwa kweli, ubinafsi, kufikiri kwa moyo badala ya akili, kujigeuza kifaurongo, uzushi, kupakazina, umbeya, hadaa na uzaini wa kidizaini na kisanii bali katika misingi ya ukweli, uwazi, haki, usawa wa kisheria na uwajibikaji na vinginevyo ni kujidanganya kwa hasara ya walio wengi. Kwa kuanzia nawatafadhalisha viongozi wetu wote kujua ni mahala gani au wapi pa kusema yanayowahusu viongozi na wapi pa kumwaga mtama mbele ya kuku au bata wote. Ikiwa hivi tutakuwa na viongozi ambao mikono yao inafungwa na mikono ya viongozi wengine nchini na inakuwa ni rahisi kuwafuatilia na kuwadhibiti wanakosea na kuwatoa kwenye kundi la uongozi. Hatua hii italiepushia taifa madhara kama tunayoyaona kwingine Afrika. Mimi kama mwananchi wa kawaida nawatafadhalisha viongozi wetu kabla hawajafungua mdomo kutuambia chochote basi wazungumze wenyewe kwa wenyewe kwanza, wapime na kutathmini nini itakuwa atahri yake wanacnhi watakapofafanuliwa jambo hilo. Hatari kubwa ninayoiona kwa amani na umoja wa Tanzania sio kitu kingine ila midomo na kauli za viongozi wetu (kwa maana hiyo pana), kwamba kipo watakachokisema kitakachotuleta madhara makubwa kama ilivyo kwa watakachoacha kukisema nacho kikatuleta shari kubwa pia. Ninaamini viongozi wote kwa pamoja wana dhamana ya kulizungumzia hili na kujifunza kutoka kwa wengine itifakizinazoendana na matamshi yanayogusa sehemu kubwa ya watu wetu au taifa kwa ujumla wake. Viongozi wanapokuwa kitu kimoja katika kuongoza wale wanaostahili kuongozwa wana uwezo mkubwa zaidi wa kujenga amani na umoja kuliko vinginevyo. Mungu ibariki imani zetu, Mungu tubariki Tanzania na Afrika na tujalie kuutanguliza Utanzania na

Thursday, February 21, 2013

Mambo Yatakayonusuru Amani na Umoja Miaka hii na Ijayo..


AMANI na umoja hapa Tanzania una kila sababu ya kuendele kuwepo ili mradi tu mambo yafuatayo yanaheshimiwa,  hayawi tu sera bali yanakuwa vitendo vya kila siku na wote kwa pamoja tukawa tunakataa kwenda kinyume na kauli na ahadi za kitaifa kuhusu masuala husika.
                Kwanza viongozi na raia lazima kujiheshimu, kuheshimu wengine na kuheshimiana. Huwezi ukaendelea kuwadhalilisha wengine au kufanya vitendo vinavyohalalisha kudhalilishwa wengine na wewe ukaamini kuwa utaendelea kuheshimika. Kiongozi yeyote wa Tanzania atakayekubali Mtanzania yeyote kudhalilishwa ndani au nje ya nchi na yeyote yule awaye basi huwa mchangiaji katika hatima ya uvunjikaji amani na umoja wa nchi.
                Mtu mmoja mmoja, vikundi vya watu, wapangaji, wenye nyumba, wenye mji, wanamtaa, wanakijiji na wanamji kwa ujumla wao ni sehemu ya Tanzania. Kila mmoja wao ana wajibu na ana haki zake. Kitendo chochote kinachoruhusu au kuendelea kuruhusu mtu au watu fulani kununua na kuuza haki za wengine ni kitendo kinachonuiwa na kinachodhamiria kuvunja amani na umoja wetu. Kisikubalike
                Uhuru wa kweli kwa mtu mmoja mmoja na makundi au jumuiya ya watu pasina uhuru huo kuingilia uhuru wa wengine. Uhuru ndicho kitu kinachompa uwezo mwananchi au raia awaye kufanya maamuzi kwa kuangalia maslahi yake na kikundi chake bila ya kurubuniwa, kuzainiwa, kununuliwa au kushawishiwa kufanza hivyo kwa pesa au upendeleo wowote uwao. Nchi huru hujengwa na watu huru  haijengwi na watu wa kununuliwa au watumwa wa mtu fulani.
                Kama nchi, Tanzania tunapwaya mno katika medani za ukweli na uaminifu kama watu binafsi na dhamana tunazopewa kutunza na wenzeu. UOngo haujengi nchi, aghalabu uongo hubomoa na kausambaratisha watu, vyama na nchi. Ni muhimu katika uandikaji wa katiba yetu tukarejea suala la kuwa na maadili muhimu ya kitaifa. Maadili hayo pamoja na mambo mengine yahusu: ukweli  kama tabia inayokubalika na wote; uaminifu; usafi wa mazingira, miili na mioyo yetu; uchapakazi na uwajibikaji wa kiwango cha juu; tabia ya kujisomea na kujiendeleza baada ya kumaliza shule/vyuo; kujitolea kusaidia wengine; kujitegemea kama jamii kama hali inaruhusu na ndio njia peikee ya kutatua tatizo la kijamii na kujitahidi kuongoza kwa vitendo na sio porojo na maneno.
                Hali ilivyo hivi sasa ni kwamba kuna matajiri na wakubwa wengine wanaojiweka juu ya sheria na wengi wengine kuwa chini ya sheria. Amani na umoja wetu lazima kufa kama hapatakuwa na usawa mbele ya sheria kwa wote viongozi kwa raia.
                Tusikubali visingizio vya kihaki za kibinadamu na kisheria kukwamisha mapambano dhidi ya rushwa. Kwa vigezo na bishara zote mla rushwa na fisadi huonekana maili kumi toka pale alipo na wala sio siri. Tukiidharau rushwa na kukubali itutawale sisi kama taifa na sio sisi kuitawala rushwa tutakuwa tumeshindwa katika safari ya ustawi na maendeleo ya watu wetu kabla hata ya kuanza safari yenyewe.
Kujilinda na kuwa na maofisa habari na mawasiliano pia wahariri wa habari na waandishi ambao pamoja na  uchanga wao wanajifanya  ni watakatifu na wanajua kilicho bora zaidi kwa nchi na watu wake. Hali katika kufanya hivyo wakawa  ndio wanaopanda mbegu za ushetani na balaa kwa nchi na watu  wake .
-Kupigwa vita rushwa na ufisadi
                Kama hatutaenzi ahadi na amri mbalimbali ambazo ni sahihi na za haki basi kitaifa tutakuwa tunabomoa msingi wa amani na umoja wetu. Baada ya kusema hivyo, ni lazima kwa wakubwa wetu sio tu kuchungua mambo pale tatizo linapotokea bali pia kuchungua kwa makini, kina na mapana malalamiko yoyote nchini ambayo yanaashiria kuwepo tatizo kati ya mtu na mtu au watu na watu. Mambo haya yakichukuliwa kijuujuu yatatufiksha pabaya, kwani yana uwezekano mkubwa wa kuweka umoja na amani yetu rehani katika mikono ya wachache kwa wema au ila.
                Huko nyuma Watanzania walikuwa wepesi wa kuitana ndugu au komredi.  Kuzuka na kukua kwa matabaka kati yetu kumeanza kunyemelea na kuuharibu udugu na ujamaa huo. Ni muhimu kuangalia kwa kutumia njia zozote ziwezekanazo tunarudisha  upendo na kukubalika kwa makundi mbalimbali katika jamii na sio kama hivi sasa ambapo baadhi ya  watumishi wa umma wameanza kuonekana kama maadui na aghalabu wako juu ya sheria za nchi na maeneo mbalimbali. Udugu na mahusiano mema huzaa kile kinachoitwa mtaji wa kijamii. Mtaji huu usipokuweko mbio za manendeleo kwa jamii yoyote iwayo hatima yake ni kuishia sakafuni.
                Tuepuke tabia ya kuwadharau , kuwashusha h adhi na kuwakwaza wengine hadharani pasina sababu ya msingi ila kwa mtu kujipendekeza na kujionyesha kwa wenzake kwamba yeye ni mkereketwa na anayewashwa zaidi kuliko wenzako na hasa katika jambo muktalifuni na lisilokubalika  ukweli wake na watu alimu na wenye uadilifu. Tabia ya kuikweza na kujionyesha wewe safi na bora kuliko wengine hujenga  chuki na inda isiyo na tija. Aghalabu anayejikweza na kukwaza wenzake huonekana mbaya, mbinafsi, adui na huchukiwa na wenigi hata na wale anaodhania wanamshabikia na kumpenda. Maana leo ni yule, kesho aweza wageukia wao.
                Kumezuka tabia ya baadhi ya wanasiasa na matajiri kuwanunua  Watanzania wengine kwa sababu moja au nyingine.  Jambo hili sio tu linarudisha uhadimu kwa watu wetu kupitia mlango wa nyuma bali ni sababu moja kubwa inayochangia kuua na kuumaliza udugu na umoja wetu, kwa kuwa watu wanaonunuliwa ni rahisi sana kutumika kufanya lolote lile liwalo, liwe jema au baya mradi wanalipa deni lao.
                Katika miaka hii ya kugundulika kwa rasilimali mbalimbali nchini upo umuhimu wa kuwa na fomula ya kitaifa itakayogawa rasilimali na mapato yanayotokana nazo kwa namna ambayo kule inakopatikana wanaona wanastahili kupata wanachopata na wengine kugawiwa au kunufaika na kile kinachobakia, ikiwemo serikali na vyombo vyake pia.
                Upo uwezekano mkubwa wa amani na umoja wetu kudumu kama mambo niliyoorodhoshea hapo juu yatafanyiwa maamuzi sio kiimla bali kwa kuwashirikisha wahusika au wabia katika masuala mbalimbali na kufikia maamuzi ambayo yanachangia wote kujiona ni washindi na hakuna mshindwa.
                Kwenye jamii ya mpito kama ilivyo yetu aghalabu umoja hujengwa kwa kuwa na madaraja kati ya walionacho na wasio nacho. Aidha kila kinachoonekana kuwa ni kizuizi katika ukombozi wa wasionacho huwa kinang'olewa haraka kwa faida ya wote.
                Rasilimali zetu ni nyingi na za kutosha. Kinachokosekana ni uongozi, utu na  ubinadamu wa kuweza kutumia akili na maarifa tuliyopewa na Mola ili rasilimali hizo ziweze kutufaa sote bila ya wengine kutengwa na kusahauliwa. Hii ina maana katika sifa kubwa amabyo viongozi wetu kuanzia vijijini hadi kitaifa wangepaswa kuwa nayo ni ile ya kukosa kabisa ubainafsi wenye uharibifu.
                Hatuwezi kuwapata kina Nyerere wengine (watu waliokuwa wanajisahau wao wenywe na familia zao na kumtanguliza mbele Mtanzania kwanza) lakini tukiwa na maadili bora, kupata viongozi wenye kudhibiti ubinafsi wao kwa masalahi ya walio wengii ni kitu kinachowezekana kabisa. Kuna mifano mingi duniani inayoonesha kwamba nchi zilizochipukia na kuwa tajiri katika miaka ya hivi karibuni ziliongozwa na viongozi walionyima wao na kuwanufaisha watu wao kwanza, na sio waliowanyima na kuwakwaza watu wao ili wao wajinufaishe kwanza.
Tanzania katika nchi nyingi za Kiafrika ipo katika nafasi ya kipekee kuendelea kudumisha amani na umoja wa watu wake kama isipofuata msaragambo na kuiga yanayotokea katika nchi nyingine za Kiafrika na kwingineko duniani kwa kuwa na utaratibu wa wazi na usio na usiri katika kuzungumzia mambo mbalimbali yanayoonekana kuwa ni chanzo cha mtafaruku na maelewano kati ya Watanzania katika siku zijazo.
                Tabia ya mbuni haifai kwa nchi kama yetu, yaani, kuingiza kichwa chetu kwenye mchanga, kisha tukajifanya kama vile kwa kuwa hatuoni hatari inayokuja, basi tukifijificha hatari hiyo haitatugusa na eti tukabakia salama. Athari, hatari na matishio mbalimbali  kwa amani na umoja wetu lazima tupambane navyo ana kwa ana.



Elimu, Mitaala na Utatuaji Matatizo ya Watu na Nchi


Nia na madhumuni ya insha hii ni kujaribu kuwashawishi Watanzania kuona kwamba elimu yetu sasa hivi inaendeshwa kwa namna ambayo haina uhusiano kabisa na matatizo yanayokabili nchi na watu wetu.
                Ninavyoelewa mimi sababu kubwa ya kuwepo kwa elimu ni kusaidia kudumisha daraja la maarifa, nadharia, ujuzi na uzoefu wa waliotangulia na wanaowafatia katika jamii fulani.
                Jamii isiyoweza kurithisha toka kizazi kimoja kwenda kingine maarifa, elimu, teknolojia, mila, desturi na utamaduni wake kiujumla inayozikusanya muongo baada ya muongo sio jamii yenye uhakika wa kuwepo na kuendelea kuwepo katika siku zijazo.
                Urithishaji huu unajumlisha pia urithishwaji wa kizazi kimoja na kingine mbinu, njia na mikakati ya kushughulikia matatizo makubwa na madogo yanayokabili mtu mmoja mmoja na jamii nzima kwa ujumla.
                Inaaminika kwamba nusu ya matatizo ya jamii fulani huhesabika yamekwisha au yameishatatuliwa kama jamii hiyo itakuwa inawafunza vijana wake pamoja na elimu nyinginezo elimu ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikablili jamii husika.
                Mafunzo  haya hutolewa sio tu kinadharia bali pia kwa vitendo.  Unapotenganisha nadharia na vitndo katika elimu, basi jamii husika huwa inapoteza jambo muhimu sana katika wakati muafaka na sio rahisi kulipata jambo hilo tena katika siku zijazo.
                Kuna wanaoamini kwamba nusu ya matatizo ya Tanzania yanaweza kwisha kwa kuwa na mitaala inayolenga kutatua matatizo yake ya kijamii na kiuchumi.    
Matatizo ya kimaendeleo yanayowakabili Watanzania walio wengi ni pamoja na uadimu kama sio ukosefu wa maji, chakula na nyumba. Aidha kuna udhaifu katika elimu, tiba na afya kiasi kwamba watoto wa Kitanzania wanaendelea bado kusomeshwa nchi jirani na Ulaya au Asia; wakati huo huo wagonjwa wa Kitanzania wanaendelea kutibiwa
nje.
                Kuna tatizo la kukosa matunzo kwa wazee,  mayatima na watoto wa mitaani.      Vilevile yapo matatizo ya kiulinzi na usalama, uhalifu yanayotishia sio tu usalama wa raia mmoja mmoja bali amani na utulivu katika jamii ikiwemo kuongezeka kwa vitendo vya wivi na ubakaji pamoja na kuwa na sheria kali dhidi ya vitendo hivyo.
                Aidha yapo matatizo katika ujenzi na upanuzi au ujengaji upya wa barabara, reli, madaraja, uchimbaji madini, bandari, viwanja vya ndege na ujenzi wa uendelezaji wa miundombinu mingine.
                Kiutamaduni na Kiteknolojia tuna matatizo ya kuoanisha maendeleo ya teknolojia na mila na desturi zetu ili kupunguza gharama na kurahisisha ufanifu na ufanisi katika maeneo mengineyo ya maisha, kazi, sanaa, utunzi wa vitabu, filamu, michezo na burudani.
                Kijamii na kiuchumi matatizo makubwa ni katika ujasiriamali, mikopo na urudishaji wake, mipango, uratibu, uongozi, usimamizi na udhibiti wa mambo kiutawala, kimaandishi na kiteknolojia.  Hali kadhalika kuna masuala ya menejimenti na uendeshaji bora wa michezo, sanaa na uchumiwa utoaji au uuzaji huduma. Aidha kuna changamoto katika uchimbaji na utunzaji au uangalizi wa visima vya maji, bomba, pampu, mashamba ya kisasa, uvuvi na ufugaji wa kisasa, utunzaji na ulinzi wa wanyama pori, nege na viumbe wengine, matumizi bora na makubwa zaidi ya rasilimali nchi kavu, rasilimali kwenye baharini na kwenye maji kwa faida ya wengi na sio wachache.
                Elimu yetu kwa mapana na marefu sasa hivi imeelekezwa katika kujifunza vitu kama historia, sayansi kama sayansi, uraia, jiografia, hesabu, lugha na mambo kama hayo. Kwa maoni yangu masomo yote yanayotolewa hivi sasa iwe kwa shule za msingi au sekondari yanaweza kuangukia ndani ya masomo matatu makubwa: Maarifa ya Namba na Takwimu; Maarifa ya Kunadika na Mawasiliano na Maarifa ya Maisha, Sayansi na Mazingira.
                Fani hizo hapo juu zikipata msukumo wa kuwekwa kwenye mtandao kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza kama itakavyoandikwa na Watanzania wenyewe ni maeneo yanayoweza kutawaliwa kielimu vyema na mwanafunzi yeyote awaye.
                Hayo kwa upande wangu ndiyo yangelikuwa masomo ya msingi kuanzia chekechea hadi sekondari na yakawa ni lazima kuwepo kwenye kila mchepuo kwenye maeneo hayo.
                Masomo yanayotakiwa kupangwa kama ziada itakayotofautisha kati ya mchepuo wa mweleko fulani na mwingine ni mtatizo yalioorodheshwa hapo juu.
                Kwa mpangilio huo mwanafunzi, mathalani,  katika kundi la kwanza la matatizo ya uadimu na ughali wa maji, chakula, nyumba na kadhalika atakuwa akijishughulisha na kujifunza jinsi ambavyo matatizo hayo yanaweza kupunguzwa au kumalizwa nchini. Ni elimu inayomhakikisha kijana nafasi ya kujiajiri au kuajiriwa kwa sababu elimu hiyo itakazia nguvu zaidi katika vitendo na sio nadharia tu.
                Mchepuo mwingine unaweza ukaelekeza nguvu zake katika kujifunza na kurahisisha kuelewa matatizo ya elimu (elimu nayo pia huwa tatizo na lazima kufunzwa na kufanyiwa tafiti dahari ili kuboreshwa mara kwa mara),  tiba na afya  wataanza kugangana na mbinu, stadi na maarifa za ualimu au ufundishaji na uangalizi au utabibu mahospitalini na katika zahanati mbalimbali nzhini zisizo na watumishi wa kutosha.
                Wanafunzi wengine na hususan katika shule za msingi wataelekezwa kutokan na mapenzi na mwelekeo wao katika kujifunza na kulielewa tatizo la matunzo kwa wazee, wajane, mayatima na watoto wa mitaani ili waje kubobea sio tu katika nadharia bali vitendo vya kulipunguza au kuondosha kabisa tatizo hilo.
                Wale wanaopendelea mambo ya ujenzi na miundombinu wataanza kupigwa msasa toka shule za msingi kwa kujifunza juu ya umuhimu, kazi na faida za  nyumba, barabara, reli, madaraja, visima, bandari na viwanja vya ndege, vituo vya kisasa mipakani na usafiri na uchukuzi kiujumla. Kwa namna hii, mtoto hata akimaliza darasa la saba anaweza kuanza kufanya kazi katika eneo hilo na akawa anajiendeleza katika fani yake pasipokuwa na wasiwasi wa kuchanganya kimasomo au kimitaala. Maana elimu hapa inakuwa ikishughulika na tatizo lilipo, linaloeleweka na linaonekana na kila mtu katika jamii.
                Mcherpuo mmoja muhimu utakuwa ule wa kuwapa watoto kuanzia chekechea fursa ya kuonyesha vipaji vyao katika nyanja za sanaa, kuimba, kucheza ngoma na kukatika viuno, kuigiza, kuchekesha, uchezaji mpira wa vikapu na michezo mingine na mambo kama hayo. Kwa kuwa mtoto anaelekezwa kulekule anakokutaka inakuwa ni rahisi kijana wa Kitanzania kuanza kuonyesha vitu vyake akingali bado mdogo na hivyo kumpa nafasi ya kufanza makubwa zaidi hapo baadaye.
                Mabadiliko ya mitaala katika miaka hii pia lazima iwe na mchepuo wa uongozi, utawala, biashara na menejimenti ya vitu hivyo. Ni vizuri hili likaanzia shule za msingi kiasi kwamba mtoto wa Kitanzania akimaliza darasa la saba anakuwa sawa na mtoto wa Kimarekani aliyesomea B.B.A. au hata M.B.A. (unacheka?) nina hakika hili linawezekana kwa kuwa watoto wa Kitanzania kutokana na mzingira yao magumu wanaisoma na kuilewa dunia haraka kuliko watu wa nje katika hili.
                Mwanafunzi anayemaliza masomo katika mchepuo huu atakuwa na uwezo wa kusimamia biashara ya wazazi wake kwa namna bora zaidi kuliko wazazi  hao, na upo uwezekano mkubwa wa mchepuo huu kuzalisha viongozi bora zaidi kwa vyama, vijiji na taasisi nyingine kuliko hali ilivyo hivi sasa.
                Ninakubaliana na wale wote wanaodai kwamba ilikuwa ni makosa kuondoa elimu  ya ujamaa na kujitegemea mashuleni. Lakini kama ikirudishwa, ninashauri ingerudishwa kwa mapana na kina zaidi kwa kuzingatia ulazima wa kuoanisha matatizo ya jamii leo na elimu inayowapatia watu wake.
                Nionavyo mimi, Vyuo vya VETA vinastahili kuitia makali au kuinoa zaidi elimu vijana wetu watakayoipata shule za msingi na sio kuwa mahala pa kuanzia tu vitu vipya kwao. Nikiwa na maana kwamba shule zetu zote za msingi zinahitaji maabara na karakana za useremala, uashi, umakenika na ufundi mwingine ili ziwe kamili na sio nusunusu kama zilivyo leo. Hali ingelikuwa hivyo, leo tusingekuwa na shule za msingi zisizokuwa na madawati na vyoo vya kutosha, na zenye madarasa na majengo mengine yasiyofikia viwango.
Copyright © 2013 Sammy W.I. Makilla. All Rights Reserved.

Saturday, February 16, 2013

Ujamaa na Kujitegemea Bado una Nafasi Vijijini na mashuleni


KIHISTORIA watu wa mjini hawajawahi kuwa watu wanaotamani na kupenda ujamaa. Miji jinsi ilivyo imejengwa katika msingi wa ubinafsi na kila mtu na lweke. Na kwa miaka mingi ijayo hilo ndilo litakaloendelea kwa ubepari kuwa wenye sura mbaya na makucha makali zaidi.
 Mtu aneyeuchukia ujamaa eti kwa sababu tu Warussi wameutupa na wajamaa wa jana wameanza kukumbatia baadhi ya sera za kibepari ni mtu asiyejua maana halisi ya ubepari. Ni mtu anayehitaji kujitambua na kuijua jamii yake na hasa ile ya vijijini na shida na dhiki zao mbalimbali.
 Anakuwa hivyo kama anavyokuwa kwa sababu anadanganyika na mng'aro wa dhahabu ubepari unaonyesha kwa nje, bila kujua kilichoko ndani wala sio shaba achilia mbali madini ya fedha.
 Tumeshaufungulia mlango, na hakuna namna ambayo tutaweza kuuzuia. Labda, angalau tukubaliane na na kina Raila Oginga na wenzake (watangulizi maarufu katika ubepari) kuwa nchi zetu sasa zinastahili kuwa na sera na dira ya Ujamaa wa Kidemokrasia (Sosho-demokrasia), ha hivyo kupunguza ushetani na makali yaliyomo katika ubepari kwa faida ya wasionacho katika jamii yetu.
 Hata hivyo, hali ya maisha vijijini katika sehemu mbalimbali za Tanzania nilizotembelea na wanakoishi watu masikini na wa kawaida na sio viongozi au jamaa za viongozi kila feli, kila mtihani, kila tatizo na kila fursa inapiga mayowe ya kuwa pasipo ujamaa na kujitegemea miongoni mwa wanavijiji maisha huko tuendako yatakuwa magumu na yasiyo na huruma hata kidogo.
 Hili linakuwa hivyo, kwa kuwa nchi yetu bado haijawa na sera inayomfanya mwanakijiji anufaike na ardhi yake na kile kilichomo ndani yake kama viongozi wa juu wanavyonufaika.
 Aidha, pamoja na kuwepo kwa teknolojia ya habari na mawasiliano bado inawachukua wanavijiji muda mrefu kujua kinachotokea mkoani mwao achilia mbali nchini kwao na duniani kwa ujumla.
 Vilevile, pamoja na kuwa na vitu kama TASAF na NGOs mbalimbali zenye madhumuni na nia ya kuwasaidia wanavijiji kutatua matatizo yao bado  muundo na mifumo ya taasisi hizo imekaa kuwanufaisha zaidi watu wa mjini kuliko wa vijijini.
 Tafiti zinaonyesha kwamba jitihada za kuwaamsha na kuwafunza wanavijiji umuhimu wa ushirika zinaharibiwa na tamaa za viongozi wao na mabepari uchwara wsnaoishi au kuchanganyikana nao.
 Watu wanashangaa kusikia kwamba dhana na nadharia ya ushirikishwaji watu nchini  hapa pamoja na kuleta ufanisi wa aina fulani haikutoka kwenye ile ngazi ya chini kabisa katika ushirikishwaji watu kwa kutumia modeli ya ushirikishwaji watu iliyobuniwa na Mjapani kutoka Chuo Kikuu cha Kobe aitwaye Etsuko Okazaki. Hatua hiyo siyo nyingine ila ni ile ya uanasesere wa kuchezewa na wanasiasa na viongozi wa serikali za mkoa na kitaifa. Hatua za juu katika ngazi hiyo ya ushirikishwaji watu ni pamoja na tiba, kuarifiiwa, ushauri, kubembelewa, ubia, ukaimishwaji na nguvu ya umma.
 Matatizo yanayokabili vijiji vyetu nchini ni pamoja na tatizo la maji; dhikiya chakula na lishe bora; ukosefu wa nyumba bora kwa wananchi walio wengi na uzalishaji mali kwa njia dhaifu na zisizo na ufanifu na ufanisi  wa kutosha. Na kutokana na hili bado shughuli za kilimo, ufugaji pamoja na ule wa nyuki, uvuvi, uchimbaji madini na matumizi ya rasilimali ardhi na bahari kwa ujumla ni dhaifu na zisizowasaidia kitu wanavijiji katika kubadili ubora wa maisha yao na kuwa yenye heri na mafanikio zaidi.
 Matatizo mengine ni kutokuwepo kwa biashara zenye  manufaa zaidi kwa wanavijiji na mwelekeo wa kuchangia kuwafanza kwanza wazalishe kitu na ndio watumie; kutokuwepo huduma za uhakika zinazoweza kupunguza umaskini vijijini k.m. utaalii wa vijijini na wa kiutamaduni; matatizo ya mejengo, vifaa na walimu kwa shule nyingi vijijini; huduma dhaifu ya tiba na Afya vijijini; uadimu wa
umeme na nishati mbalimbali; na
Usafirishaji na Uchukuzi wenye matatizo kedekede na hivyo kusababisha hatari na hasara kwa wanavijiji walio wengi.
 Nichukulie tatizo moja tu nchini-maji. Tatizo hili, ninavyoamini, linaweza kutatuliwa kiurahisi ikiwa wanavijiji wenyewe wanajifunza na kubadilika na kuwa ndio viongozi wa maendeleo yao badala ya kuwategemea watu kutoka kwenye kata au tarafa au wilaya au mkoa au hata taifa kuja kuwasaidia.
 Wenyewe wakishaamua kusimama kidedea inakuwa ni rahisi kuamua,  kupanga na kutekeleza kile wanachokiamua. Na hili huwa ni rahisi zaidi pale wanakijiji wote kwa pamoja wanapokuwa kitu kimoja na sio baadhi yao kukubali kuzainiwa na wale wenye tamaa za uongozi na njaa yao binafsi.
 Huko nyuma nimewahi kupendekeza njia mbalimbali za wanavijiji kupata maji huko waliko vijijini pasina ya kutembea mbali au kuhangaika sana. Njia mojawapo ni kuchimba bwawa pale penye chanzo cha maji  na vilevile kwa ajili ya kutega maji ya mvua badala ya kuyaachia yote kwenda baharini. Njjia nyingine ni kuchimba kisima pale wataalamu wanapothibitisha kuwa maji hayapo mbali na uso wa dunia. Katika sehemu zenye maziwa jirani na wao upo umuhimu wa wahandisi wa Kitanzania kuamka na kuvumbua njia ambazo kwazo  kwa maziwa yaliyo na kina cha chini  wao wanaweza kuchimba  mtaro chini kwa chini na kuvuta maji hadi nchi kavu.  Wale wanaoishi pembeni na bahari huu ni wakati  wa baadhi yao kurudi shule na kujifuna kutoka kwa wenzetu jinsi wanavyobadili maji ya chumvi hadi maji hayo kutumika kunyweshwa mashamba na bustani na kusaidia pia katika matumizi ya nyumbani.
 Ukiyaangalia yote haya ni mambo yanayohitaji vichwa vilivyotulia na watu wanaokubali kwamba changamoto na fursa nyingi walizonazao zinalazimisha kuwepo kwa ushirikishwaji na kujitolea kwa namna moja au nyingine. Na kwamba bila ushirikiano wa walio wengi vijijini ippo hatari kubwa ya vijiji kubaki kama vilivyo hivi leo hata baada ya muongo mmoja ujao.
Maendeleo ya vijiji vyetu yamekwaza na viongozi wetu. Ambao kufatia Azimio la Zanzibar wamekuwa 'bize' kushughulika na mambo yote mengine na sio ujenzi na uendelezaji vijiji. Kwa namna moja au nyingine kwa miaka kadhaa sasa isipokuwa kwa vijiji viongozi wetu wanakotokea vijiji vingine vimeingizwa kwenye kabati kama sio kaburi la sahau.
 Jambo la kushangaza ni kwamba matatizo mengi yanayoikabili miji yetu hivi leo yanasababishwa uongozi kushindwa kutoa msaada na nyenzo (wakati mwingine vimilioni vichache tu) ili kuwawezesha wanavijiji kuhama kwenye umaskini wa kutupwa na kuwa watu wanaojitegemea.
 Kama kuna jambo moja ambalo ningeliwaomba wanaoendesha ukusanyaji maoni juu ya katiba mpya ni kutia shadidi katika kile kifungu kinachozungumziwa uwiano wa kimaendeleo kati ya sehemu moja na nyingine ili pawe na mikakati, sera na kanuni zilizo fasaha na wazi juu ya kushughulikia ujenzi na maendele oi ya vijiji vyetu. Ninazungumza hivyo nikiwa na uhakika kwamba nusu ya matatizo ya mjini yatakuwa yamekwisha kama vijiji vyetu vitatapatiwa angalau kwa kuanzia mahitaji yote ya msingi na ushirikiano kiungozi na kiutawala unaoweza kuwatoa wanavijiji pale walipo na kuwafikisha mahala ambapo sisi  sote wa mjini na vijijini tunaweza kujivunia.
 Jambo moja linalohitaji kupewa uzito wa kipekee hivi sasa ni kuangalia uwezekano wa kuwa na viongozi na watendaji bora wa vijiji bila kujali mtu anatokea wapi.
 Inashangaza kwamba pamoja na kuwa na vyuo vya maendeleo vijijini kasi ya maendeleo vijijini imezidi kwenda chini mwaka hata mwaka. Aidha, elimu inayotolewa na vyuo kama hivyo haiendani na wakati au wanaozalishwa na vyuo hivyo hawaendi kuwa viongozi  wa vijiji bali wanaselea humu humu mjini kama wahitimu katika masuala mengine. Kama ilivyo kwa vijiji basi mengi pia  ya kijamaa na kujitegemea yanaweza kufanzwa  shuleni na vyuoni kwa manufaa ya wanafunzi, wazazi wao na nchi  yao. Hata kama baada ya shule vijana wataamua kufata  ubepari na sio ujamaa.
 Ninaamini kwamba jambo litakalochochea  ari, mwamko na msukumo wa maendeleo kwa watu wa vijijini ni rasilimali watu. Wakati umefika huko vijijini wanavijiji kuwa na viongozi bora na sio bora viongozi.
 Ukweli ni kuwa hata tukiwa na viongozi wazuri kiasi gani katika ngazi za juu  lakini huko vijijini uongozi ukawa dhaifu kupita kiasi hatutaweza kuendelea kiwelikweli.   Jambo hili likiunganishwa na ufanyaji kazi kidhati kwa mashirika yanayosemekana kazi yake ni kusaidia maendeleo vijijini na kisha wanakijiji wakafunzwa namna za kukopesheka kama wawekezaji wanaokuja kupewa ardhi kwenye vijiji vyao wanavyopewa mikopo kiurahisi kwa kutumia ardhi hiyo hiyo, basi maendeleo ya vijiji vyetu hayatabakia katika ruia zetu tu! Aidha, bila kusita wala kutafuna maneno huu ni wakati  wa serikali zetu za mitaa na serikali  kuu kuhakikisha kwamba wale wanaoishi katika maeneo  mbalimbali hapa nchini  wananufaishwa na  na tathmini mpya ya mali asili na rasilimali zao nyingine na  kwamba mali hizo kuanzia sasa zitakuwa zinahesabika kama mtaji wao kieneo na kitaifa na hivyo kuwaruhsu kunufaika kihisa na kifedha na rasilimali kama hizo na isiwe tu wanaonufaika na hili ni viongozi  wa juu na wanasiasa nchini. 

Sunday, November 25, 2012

Kwanini Ushirika, Vijiji na Miradi ya Pamoja Inakwama ?


AGHALABU husemwa kwamba anayeumwa na nyoka akiona jani hustuka. Hii ndiyo hadithi ya shughuli za Ushirika, vijiji na miradi ya pmoja katika sehemu mbalimbali za nchi.
 Baada ya shughuli hizo kuingiliwa na siasa na wanasiasa na hatimaye kuchafuliwa kama sio kuharibiwa kwa kiasi kikubwa, Watanzania wengi walikatishwa tamaa na shughuli zozote zilizohitaji kufanzwa na mtu zaidi ya mmoja. Kila mmoja akawa ameamua kwenda kipweke pweke, hata pale ilipoonekana dhahiri kuwa jambo linalofanywa haliwezi kufanikiwa bila umoja au  ushirikiano wa namna moja au nyingine kati ya watu wawili au zaidi.
 Katika uchambuzi wake wa kisayansi kuhusu nadharia za ushirikishwaji umma nchini, Bi. Rebecca Maarsland (2006) alibainisha kwamba ushirika na ushirikishwaji watu Tanzania kumeathirika kwa kiasi kikubwa na mapambano  kati ya walio nacho na wasio nacho. Serikali ya awamu ya kwanza kwa nia njema kabisa iliamini na kutekeleza dhana ya ushirikishwaji umma kwa  lengo la kuwanasua  Watanzania na umaskini wa kupindukia. Hata hivyo. viongozi wa vikundi vya  ushirika walijikuta wakiwa na uwezo na fedha chungunzima na hapakuwa na njia nyingine ya kuutumia ila kwa kuingia katika siasa. Wanasiasa kwa upande wao walitegemea kodi iliyolipwa na wananchi nayo haikutosha pia kuwapa na fungu la kujiimarisha kisiasa. Hivyo, ushirika na viongozi wake wakawa ni tishio kwa viongozi wengine wa kisiasa. Mkwara ndipo ulipoanza. Wanasiasa na mangimeza hawakuwa tena na nia ya kuendeleza ushsirika bali kuua ushirika.
 Ushirikwa na ushirikishwaji ulistawi tu kati ya Uhuru na kabla ya kuanzishwa kwa CCM. Kuna wanaoamini kwamba hayo yalikuwa hivyo kwa sababu ni mtu mmoja tu aliyekuwa na nia ya kweli ya kuwasaidia Watanzania mafukara kupitia ushirika. Huyo hakuwa mwingine ila Mwalimu Nyerere. Inaelekea katika timu yake nzima ya uongozi hakuna aliyefahamu dhana ya ushirikishwaji achilia mbali kuamini katika nadharia hiyo  na kuitekeleza kwa vitendo.
 Wakati Tanzania ilisifika sana kimaneno kwa ushirika, yakini, ushirika wa kweli kwa vitendo  ulikuwepo Kenya japo kuwa wakati huo tukiwazomea kuwa wao ni wanyama au ubepari ni unyama ! Kweli ubepari ni unyama, lakini tofauti na ilivyo hivi leo Tanzania, Kenya wana kimbilio la kujihifadhi kama vyama vyao vya ushirika na vinawasaidia si haba. Tanzania hawana pa kukimbilia.
 Walioathirika sana ni wananchi ambao walifikia kuona ushirika ni baba na mama kwao. Ushirika ghafla ukawa ni wizi na unyonyaji wa masikini na wala sio mwokozi na kimbilio lao tena. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa kufa kwa ushirika nchini na imani ya wananchi kwa kitu kiitwacho ushirika. Hadi wa leo jeraha hilo kubwa halijapona.
 Nyerere alipowaachia viongozi wake wajenge na kuendeleza vijiji vya kijamaa ili nchi iwe na mfano unaong'aa kwa Afrika yote na dunia, maofisa wake walioona hiyo ni nafasi ya kuwakomoa wanavijiji tajiri na jeuri na hivyo wakawatoa kuliko na ardhi nzuri na yenye rutuba na kuwapeleka kwenye mawe na mchanga. Huo ukawa ni mwanzo wa kifo cha vijiji Tanzania, sambamba na  kufanikiwa kwa vijiji vya Uyahudi Kibutz  huko Uyahudi, ambavyo, hivi leo ni mfano kwa dunia nzima.
 Miji ilionekana kuwa na mameneja wazuri na hivyo kuiendesha miji yao vizuri  ikatuhumiwa kuwatajirisha na kuwapa kichwa mameneja na viongozi wake wengine, hivyo mkwara ukatafutwa na CCM  wa kumaliza nguvu pia halmashauri za mji nchini. Huo ukawa ni mwanzo wa kuwa na miji dhaifu na michafu Tanzania.

Kukosekana na ukweli na dhati pamoja na wanasiasa na mangimeza kuona miradi ya pamoja kama ni kazi ya kusadia masikini na watu walio nyuma kimaendeleo na sio kazi ya kuonesha uwezo wao kama viongozi ulichangia si haba....
 Utafiti usio rasmi nilioufanya unaonyesha kwamba hivi leo Watanzania hawana imani kabisa na kitu kinachoitwa ushirika wala miradi inayofanywa na watu wengi wasioshabihiana kwa mengi. Nalo hili kwa kiasi limechangiwa na siasa na sera za chama tawala ambacho  kwa makusudi ziliua moyo sio tu wa kujitegemea bali dhana nzima ya ushirika na ushirikishwaji nchini. Hata hivyo, ukweli haukanushiki kuwa ushirika na uendeshwaji wa vijiji kama makampuni ndio njia pekee ya kuwatoa kwenye umasikini watu walio wengi na hakuna njia nyingine rahisi kama mbadala.
 Nadharia mpya juu ya ushirika na ushirikishwaji watu zimeweza kutanabaisha kwamba kuna ngazi mbalimbali za ushirikishwaji watu na upelekaji madaraka kwenye ngazi za chini iwezekanavyo kwa faida ya walio wengi na sio wachache.
 Ukiipandikiza nadharia hii katika sehemu za mashambani au vijijini Tanzania utaona kwamba  katika miaka yetu yote ya kusumbuka na Ushirika na ushirikishwaji wananchi Tanzania haikuwa imekwenda popote. Ilikuwa chini kabisa katika modeli za nadharia ya ushsikishwaji watu na mgawanyo wa mamlaka au madaraka kwa wananchi.
 Kuna ngazi zipatazo nane katika nadharia hiyo ya ushirikishwaji. Ngazi hizo ni ile ya mwisho au ya chini kabisa, ambayo ndiyo ile iitwayo ya hila, ujanja, uzaini au kuchezea (manipulation)  ushirika na ushirikishwaji watu katika masuala mbalimbali. Katika hatua hii serikali kuu, serikali za mitaa, NGOs, makundi ya kiimani na mengineyo kwa kuwatumia watu iwe mjini au vijijini wanatafuta kunufaika wao kwanza na sio kuwastawisha walengwa. Ndio maana inaiitwa pia kuchezea watu au kucheza na maisha ya watu. Ni mzaha na utani mtupu. Kwa bahati mbaya hii ndiyo hatua ya chini na ya mwisho kabisa na masikini Watanzania hapo ndipo ushirika na ushirikishwaji wao ulipo kwa hivi leo.
 Ngazi ya saba ni ile ya kuganga (therapy) ambayo hutokea pale watu fulani wanapokuwa na tatizo basi tatizo hilo huhitaji ushirikishwaji wao ili kulitatua. Kwa hiyo ushiriki wao huanzia na kuishia hapo. Kwa mfano, kikizuka kipindukipindu ushirikishwaji huu huwa unatumika zaidi kuliko wa aina nyinigne yoyote.
 Ngazi ya sita ni ule ushirikishwaji wa kuarifiwa au kupewa habari au taarifa kwamba mnafanyiwa hili au lile. Wanaohusishwa zaidi ni viongozi wa kijiji au mtaa au sehemu husika. Kwa mfano, huu ndio mtindo maarufu zaidi unaotumiwa na TANAPA na washirika wake katika kulinda na kutunza hifadhi za wanyama kwa kuwashirikisha wananchi. Wananchi hawana sauti yoyote ya maana isipokuwa kugawia ambacho wenyewe tayari pia wamekwishajigawia.
 Tuliza au bembeleza ndio ngazi ya tano ambayo kama neno linavyoonyesha watu fulani wanabembelezwa kama sio kudekezwa au kutulizwa kwa kufanyiwa hili au lile halafu wenye mradi wakaendelea na shughuli zao kama kawaida bila kusumbuliwa na wanaowazunguka. Hilo hutokea sana katika miradi ya uchimbaji madini, gesi na mafuta.
 Kwenye ngazi ya nne sio tu watu wanabembelezwa na kutulizwa na kitu kidogo au miundombinu na zawadi hizi na zile bali pia wenye uwezo wanatafuta ushauri toka kwa wasio na uwezo. Mathalani, serikali kuomba ushauri wa raia, au mwneye mradi wa uchimbaji tanzanite kuomba ushauri wa watu wa Merelani. Lakini bado, watu wanakuwa hawana uwezo wa hali na mali katika mradi husika.
 Hatua yenye afadhali zaidi ni hatua ya tatu. Katika hatua hii ambayo inaitwa UBIA, raia au wananchi au wakazi wa sehemu husika wanakuwa ni wana hisa katika mradi husika. Mathalani, katika kilimo mwekezaji anapokubali kushirikiana na wanakijiji ili kuzalisha mazao fulani kwa ajili ya kuuza nchi za n je na kisha faida ikagawanywa kama ilivyokubaliwa katika mkataba ulioridhiwa na wanajiji wote kwa pamoja.
 Ngazi ya pili na ya kwanza ndio za juu kabisa katika ushirika na ushirikishwaji wananchi. Ya saba ni ile ya kukaimishiwa madaraka au mamlaka, mathalani, mkoa kuwa na gavana badala ya kiongozi wa kuteuliwa na kuruhusiwa kusimamia mambo yake ya kiuchumi na kijamii bila kuingiliwa nas erikali kuu katika utendaji shughuli zake za kila siku ili kuharakisha maendeleo ya mkoa na nchi nzima.
 Ngazi ya nane ni ile ya mamlaka au madaraka kuhodhiwa na wanakijiji au wanamtaa au wananchi wa eneo husika. Hii ndiyo ngazi ya juu kabisa katika ushirika na ushirikishwaji umma, ikiashiria pamoja na mambo mengine uhuru kamili wa watu kuendesha mambo yanayohusu maisha yao ya kila siku bila kuingiliwa na watu wanaokaa na kufanya kazi mbali kabisa na wao.
 Ni dhairi kuwa Tanzania  katika suala hili la ushirika na  ushirikishwaji umma ndio kama vile  tena tumeanza. Inasikitisha sana. Lakini ndio ukweli. Wenye niia ya kuufufua ushirika na moyo wa ushirikishwaji na kujitegemea kwa watu wetu ni lazima waanze kwanza kwa kazi ya kuwadhihirishia kwamba yaliyofanyika huko nyuma ni mkaosa na bado ushirika na mchango wao katika miradi ya kiuchumi na kijamii ni nunu yenye thamani kubwa na haiwezi  kuwa na ushindani wa aina n yingine.
 

Sunday, November 4, 2012

Tunajifunza kitu gani toka Utajiri wa Bakhressa ?


BIDHAA, viwanda na magari ya Bakhressa yanajulikana kuliko mwenyewe anavyojulikana. Somo la kwanza, umaarufu wa mtu unaotokana sio na kujisifia mwenyewe ila kile anachokizalisha na kukiuza au kukifanya na kukileta sokoni ni bora zaidi.
Moja kwa moja hili pamoja na mambo mengine ninayoyajua linanifanya kuamini kwamba bwana huyu amebahatika kuwa mtu mwenye kujitambua na anayejua anahitajiwa afanye nini katika dunia hii. Watu kama hawa huwa ni wachache sana duniani. Wengi wetu tupo, tupo tu, hata pale tunapopewa dhamana za juu katika makampuni au nchi. Na huwa tunaishi zaidi kwa kujinufaisha sisi na jamaa zetu na sio zaidi ya hapo. Wakati Bakhressa anaishi ili kuinufaisha nchi na sehemu kubwa ya Afrika na dunia. Haishi ili kuonekana ila anaishi ili anachokifanza kionekane na Mungu wake na dunia.
Ukubwa na utajiri sio ubwana bali ni utwana ni funzo jingine muhimu tunaloweza kujifunza tokana na utajiri wa mtu huyu mashuhuri asiyekimbiza sifa ila sifa zinazomkimbiza.
Taarifa za hivi karibuni zinazofichua utajiri wa Bakhressa na yeye kama mmojawapo wa matajiri wakubwa Afrika hazikuja kwa wengi kama kitu cha kushangaza. Watu walijua, wanajua, na wameendelea kujua kuwa Bakhressa ni tajiri asiye na makelele wala vishindo.
Kutokana na kutopenda sifa kwake ni kazi kweli kukutana au kukutanishwa naye. Lakini kutoka kwa watu wa karibu naye na uchambuzi binafsi wa maisha yake nimefanikiwa kuokota vitu viwili vitatu nitakavyowapatia.
Bwana huyu ni mchamungu nalo hili linaonekana wazi si katika vitendo na kauli zake tu bali pia katika bei ya bidhaa zake. Nina hakika uchamungu wake kwa kiasi fulani una mchango mkubwa katika utajiri alionao. Hii ni tofauti kabisa na viongozi na matajiri wetu walio wengi ambao wanadhani walichokipata na walichonacho kinatokana na akili na uwezo wao na sio mapenzi ya mungu.
Habari toka ndani zaidi zinasema kwamba bwana huyu huwa anaanza kazi baada tu ya swalati alfajiri na hatoki ofisini hadi saa nne usiku kama sio zaidi ya hapo. Hivi nani katika viongozi na matajiri wetu wengine anaweza akakipa kile anacholipwa mshahara au kinachomwingizia kipato zaidi ya masaa sita kwa siku? Ninaamini ni wachache sana. Na muda mwingi utakuwa unatumika kwa kujionyesha au kuzungumza mambo yasiyohusiana kabisa na kitu anachotakiwa kuwajibika.
Nikiikamata sifa hii hii, utagundua kuwa huyu bwana zaidi ya kusali sala 5 au zaidi kwa siku huwa hana muda na kitu kingine. Kwa hiyo, moja kwa moja gharama zake kimaisha ni ndogo mno, tofauti na viongozi na matajiri wetu wengi walivyo. Hana matanuzi, lakini si mchoyo wa zaka na sadaka na kodi ya serikali.
Kama ningeliikuwa shehe Saidi ninadhani ningeishia hapa. Ila nina hakika mtu wa kwanza kunikosoa atakuwa mhariri wangu. Makala yangu haitajaza nafasi iliyowekewa. Kwa hiyo, kwa kuwa kazi yetu ni kubwabwaja na hapa tunasifia sio mtu bali matunda ya mtu hebu tuendelee kidogo.
Huyu ni mmojawapo wa Watanzania wachache ambao wakati wanasiasa wetu wanapoteza muda kugombea nani atakuwa rais 2015/6; yeye yuko 'bize tu' na mananga kuhakikisha kwamba kila nyumba, kila duka, kila shule, kila hoteli na kila taasisi iwayo inakipata inachokihitaji kwa wakati.
Haiwezekani kila Mtanzania kuwa rais. Lakini inawwezekana kila mtu kuwa na mchango maalum wa kutoa kwa jamii ya Kitanzania. Bakhressa anaonesha kwa vitendo kuwa hili linawezekana. Na kwamba uongozi sio wa kisiasa tu, bali pia biashara ni uongozi na pengine bora zaidi.
Pamoja na kuwaachia wengine kukamata nafasi mbalimbali muhimu, bado ana muda na nguvu tosha ya kufuatilia na kudhibiti mambo pengine kutokana na uwezo wake binafsi au muundo wa kampuni au mfumo anaoutumia katika biashara zake.
Ili kuwa na huduma na bidhaa kama anazozalisha bwana huyu ni lazima uwe na rasilimali watu au wafanyakazi unaowajali na unaoangalia maslahi yao kwa kulhali. Wafanyakazi hao ndio wanaomuwezesha kufanikiwa katika mambo yake mbalimbali.
Tofauti na matangazo ya bidhaa za makampuni na watu wengine nchini upo ukweli kwa kiasi kikubwa kuhusu bidhaa za bwana huyu, hili likiwa na maana kwamba na yeye pia ni mkweli.

Wasifu wake unatufikisha wapi ?

Kwa kifupi tumeorodhesha sifa za Bakhresa kuwa ni pamoja na asiyetaka sifa binafsi; mchamungu; mkarimu; mpenda watu; mkweli; muadilifu; anatambua anachotakiwa kukifanya duniani; anaishi kutumikia wengine; mchapa kazi; ana iktisadi au mchache wa israfu na meneja au kiongozi daraja la kwanza.
Kwa maoni yangu,, bwana huyu ni kitabu kinachoishi cha menejimenti kinachostahili kutumiwa na viongozi wa kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiteknolojia na kiutamaduni ili Tanzania kupitia mfano wake iweze kuondokana na umaskini. Kama utajiri wake umetokana na Tanzania, basi kwanini Tanzania iwe maskini ikiwa angalau watu 1,000 tu watapatikana kuiga mfano wake?
Utajiri mkubwa wa bwana huyu umepatikana kutokana na mazao na bidhaa zinazotoka au zinazokuzwa hapahapa nchini. Vitu hivyo ni pamoja na nafaka, matunda, maji, maziwa, sukari na vitu kama hivyo. Nina hakika tungekuwa na sera nzuri za kodi, fedha na uchumi katika uchukuzi na usafirishaji pengine bwana huyu angetuwezesha pia kuwa na usafiri wa ndege, meli na mabasi ulio bora zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. Aanaonekana kuwa mbele zaidi ya wanasiasa na viongozi wetu kiuchumi na kiuongozi. Kiasi kwamba inabidi wamwekee breki hata pale breki hizo zinapokuwa sio kwa manufaa ya nchi na watu wake.
Je, viongozi wetu wa kisiasa wakizitazama sifa za kiongozi huyu wa kiuchumi na bila kuhofu wao ni vichuguu na yeye ni mlima Kilimanjaro hatuwezi kuambulia chochote hapa ?
Nina hakika mia kwa mia kwamba kama wilaya na mikoa yetu inaongozwa kama vile ni kampuni huru ndogo chini ya kampuni kubwa (nchi) na sio kama ofisi za chama tawala mapinduzi haya ya kiuchumi yaliyoasisiwa na Said Salim Bakhressa wa Tanzania ni kitu kinachoweza kupanuliwa zaidi na yakaishia sio kuifaa tu Tanzania bali Afrika na dunia nzima.
Sera inayohitajika hapa ni kuenzi vitu na watu wa ndani kwanza na sio kuchukuliwa na upepo wa uwekezaji ambao leo kwa mfano kwenye migodi ya dhahabu tunaona jinsi wanavyodanganya hata kwenye kile kidogo wanachotakiwa kutulipa. Kwa maneno mengine, ni muhali kwa nchi kujengwa na wawekezaji au watu kutoka nchi za nje bila kushirikishwa kikamilifu mzawa katika uleteaji nchi yake maendeleo ambaye na yeye pia ni mwanahisa.

Uchumi mikoani, wilayani

Kwa kukosa neno la kufaa pengine tunahitaji sera ya kuupelekea uchumi wetu mkoani na wilayani. Ukichukulia ule mfano wa kampuni niliouainisha hapo j uu ni kwamba kila wilaya na mkoa utaangalia rasilimali ilizonazo na kisha kuamua ni uzalishaji, huduma, biashara au shughuli gani zinazoweza kuukomboa mkoa au wilaya kiuchumi.
Hiki sio kitu kipya. Mikoa ya Nyanda za Juu kusini, mathalani iliaminika kwamba inaweza kulisha sio tu Tanzania bali Afrika Kusini na ya kati kwa nafaka za aina mbalimbali. Hata h ivyo, hadi wa leo miundombinu na mikakati ya kiuchumi na kibiashara inayoweza kufanikisha hilo bado haipo.
Kwa kifupi ni kwamba kuna mikoa na wilaya hapa nchini ambayo inaweza kutajirika na uvuvi tu au kilimo cha mboga na matunda tu au uchimbaji madini tu au sekta ya elimu (msingi, sekondari hadi vyuo) tu au mahospitali yanayopokea wagonjwa toka nchi za nje tu au kuwa na masoko na maduka ya mipakani na viwanja vya ndege, treni na mabasi tu au kwa utalii na huduma za hoteli tu. Hivi sasa tunajitawanya na kutapanya rasilimali chache tulizonazo ambazo badala ya kutusogeza mbele kimapato kunatukwamisha na kutuacha tusiojitosheleza hata kwa mahitaji yetu ya msingi.
Bakhressa hajajiingiza katika kila sekta ya uchumi. Amechagua. Na hizo alizochagua zimemfanya awe tajiri anayetambulika na dunia. Vivyo kila wilaya, kila mkoa, kila nchi (Tanganyika na Zanzibar ) inaweza kuchagua eneo moja la kiuchumi kama ndilo eneo lake la kuukimbia umaskini na kuanzia hapo ikawa hakuna kurudi nyuma tena ila kwa nchi nzima kuiga mfano wa Bakhressa-Inshallah!