Wednesday, June 15, 2011

Tatizo sio Posho ni haki na usawa katika kugawana keki ya taifa....

SISHANGAI kwanini baadhi ya wabunge hawajagutukia mtego uliopo katika kashikashi ya posho iwepo au isiwepo. Kwa tunaojaribu kuangali mbali na kuona mbele tunatambua kwamba tatizo hapa sio POSHO bali ni ile hali ya umaskini wa kutisha aliyonayo Mtanzania wa kawaida.


Kwa bahati mbaya waheshimiwa wabunge wetu wanachokiona ni kutaka kuporwa na pengine na wale 'walioneemeka kwa njia nyingine' hata kile ambacho bado wao wanakiona ni kidogo.

Wale waliokwishazunguka mijini na vijijini baada ya kubaini kwamba wanaweza kutumia matatizo na dhiki mbalimbali za wananchi kama mtaji wa kisiasa hawajachelewa kufanya hivyo.
Na wale wanaokurupuka na majibu ya haraka haraka bila shaka watajikuta wanajiumbua wenyewe na kubaki wameshangaa ni kitu gani kinachoendelea.

Wenzetu wasingelikuwa wanasumbuliwa na ule ugonjwa niliowahi kuusilimisha kwa jina la 'ndivyotunavyofikir' wangekuwa wajanja kidogo tu, wangelitambua wanaowawakilisha wanauliza na wanataka majibu ya ni nini taifa hili linalovuna na kinachovunwa kinagawanywa vipi ?

Ni vigumu kuandika makala kama hii bila kuegemea upande wa walalahoi na wasiofaidika na mfumo uliopo lakini nitajaribu kutokupendelea upande wowote kwa mara ya kwanza.

Mlipuko wa mawasiliano rahisi kati ya mtu na mtu kupitia simu za mkononi, redio, televisheni, tovuti, blogi, twitter na facebook mijini na vijijini vinawaarifu wananchi mambo mengi kupita hata uwezo wao wa kuyatafakari na kuyachambua. Lakini, kila mmoja akihabarika kiasi cha kuanza kuuuliza je hicho kinachovunwa na taifa ni
nani anayekipata, yuko wapi hapa nchini, anakipata wakati gani, na kwanini anapata yeye na sio wengine ?

Dakika moja tu inatosha kwa mtoto wa mkulima kule kijijini kufahamu kutoka kwa mwanawe kwamba senti anazomtumia inabidi zipungue kwa sababu uwezo wake wa kifedha sasa umeterereka. Gharama mbalimbali zimepanda na wa kulaumiwa ni serikali na chama tawala. Kwa maneno mengine, kazi ya kuwaumbua, kuwasingizia, kuwapakazia na kulaumu viongozi na serikali imekuwa rahisi kufikishwa hadi kijijini -ambako watu kwa kawaida walikuwa wamelala na wasioamin kwamba serikali inaweza kuwa na nia mbaya na wanachi wake achilia mbali kuwafanyia ubaya huku ikijua inawafanyia ubaya.


Je, kuna usawa na haki katika kile kinachopatikana kwa maana wananchi wote wana fursa sawa, wako huru kukifanya au kuna wanaojichagua na kufaidi wao tu. Na kama kuna matatizo, je, kuna wanaoyashughulikia matatizo hayo kwa wakati na kwa manufaa ya jamii husika.
Au kila kiongozi toka ngazi ya chini hadi juu yuko 'bize' na mambo mengine lakini sio matatizo ya wananchi. Na je, wale wanaotumwa kwenda kuwawakilisha wananchi je wanafanya hivyo au wanawakilisha watu au taasisi nyingine ?


Je, mfumo na miundo ya kiuchumi na kijamii iliyopo inaonesha kuwa na uwezekano wa kuwapa wananchi fursa ya kutatua matatizo yao na kujiendeleza wao wenyewe bila kuhadaiwa na siasa au wanasiasa au watu wengine ?

Hii ni miaka ambayo wananchi watakuwa wanauliza maswali yaliyokuwa hayaulizwi sana huko nyuma. Mathalani, wanaweza kuuliza je, hao wanaopata kilicho kikubwa na zaidi ya wengine kutoka kwenye keki ya taifa wanastahili kupata wanachokipata. Au wanakipata kitu wasichokitolea jasho, yaani, wasichokistahili kwa uhalali kabisa, kwa maana kuwepo kwao ni mzigo tu kwa wananchi na watu hao hawasaidii wananchi kuapta unafuu wowote katika maisha yao ?

Yaani, wanaopata zaidi wanakula haramu na jasho la wananchi bue kwa kupata zaidi au wanapendelewa au wanajipendelea bila kuwa na sababu yoyote ya kuridhisha? Utakumbuka wale tulioikuwa tunasoma sekondari za kulala au hata za siku ambazo kuna chakaula cha mchana au jioni. Katika dhambi kubwa niliyowahi kujisikia ni ile ya kujimegea mimi binafsi wali mwingi na mboga nyingi kuliko wanafunzi wenzangu tuliokuwa tunakula kwenye meza moja. Nilifanya hivyo baada ya kuguswa na kosa nililolifanya. Nikaugawa tena wali wangu kwa kuwapunguzia wenzangu na mimi kubakiwa na kiasi kidogo kuliko wao. Kuanzia hapo, palikuwa hapana swali ni nani anastahili kugawa chakula katika meza yetu.

Swali dada na hili ni lile la nani wanaopata kidogo au wanaokosa kabisa ? Na kama kukosa kwao kunatokana na wao kuwa duni, wajinga, wavivu na wasiojituma kwa kiasi hicho au kwa kuwa wamezidiwa tu ujanja na uelewa na wale waliotangulia kupata mitaji na wanaowaongoza?

Kwanini wanakosa ? Kwanini hawatosheki, hawaridhiki na hawashibi kwa yale mazuri viongozi na wanasiasa wanayoamini tayari wamekwishawafanyia toka kuwepo kwao madarkaani?

Na je, mfumo mapokeo tuliourithi na tulio nao hadi leona uloanzia toka tukiwa na watu milioni 9 (1960) unafaa baada ya miaka 50 ambako tunakadiriwa kuwa watu milioni 50 ? Au kwa maneno mengine, kama Karl Marx alivyohoji, je, mahesabu yetu ya 'production' na 'reproduction' na 'redistribution' ya mapato ya taifa yapo sawa na sio yameachiwa huru mno kiasi ambacho tunachezea bomu la tofauti kubwa ya kipato kati ya walionacho na wasionacho?

Tanzania inafikisha miaka 50 ya Uhuru wa benderea ikiwa na tofauti kubwa kati ya mtu wa kipato cha chini na yule wa kipato cha juu pengine kwa uwiano wa 1: 10,000. Hii sio tu ni hatari bali ni aibu na fedheha kwa nchi ambayo Mungu na kiongozi wake wa mwanzo alishawaonyesha ubaya wa tofauti kubwa namna hii kati ya walionacho na wasio nacho.

Na kama Wahenga walivyosema,' Mwenye shibe, hamjui mwenye njaa', jambo hilo sasa, yaani walionacho kushindwa kujua kwanini kuna umasikini na kwanini watu hawana fedha mifukoni mwao na majumbani mwao, limefikia hadi kwenye ngazi za juu za uongozi wetu? Majemadari wanaotakiwa kuwatoa Watanzania toka kwenye umasikini hawajui upana, urefu na kina cha umasikini nchini mwao na miongoni mwa watu wao!!

Upo uwezekano mkubwa kwa nchi hii na viongozi kujiabisha kuhusu hali ya maisha ya Mtanzania kutokana na kulewa na sifa za viongozi wa nje na wale wanaowatumia kisiasa kwa faida zao wanazozijua wao wenyewe.

Katika kupanga tufanye nini wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru tuwe waangalifu sana ili sherehe hizo zisiwe chanzo cha kujiaibisha na kujifedhehesha badala ya nafasi nzuri ya kurekebisha makosa yaliyopo na kuifanya siku hiyo siku ya kuzindua yale yatakayowapa wananchi matumaini na faraja.

Ni wakati muafaka kwa hiyo kuoanisha suala la 'posho ya wabunge' na lile la 'riziki ya kila siku ya mwananchi wa kawaida' na wawakilishi wetu kujiuliza kama hakuna uhusiano kati yake na hali halisi ya yule wanayemwakilisha bila kuzingatia dhiki na umaskini wake huko bungeni na kulipa hilo uzito unaostahili bila kuburuzwa na mtu au taasisi yoyote ambayo imeamua kufumbia macho jambo hili ?
Au kuna wanaowafunga macho kwa kitambaa cha khaki tena khaki nyeusi katika usiku mweusi wa hali halisi ya kiuchumi ya Mtanzania?

Je tunaweza kuongeza kinachovunwa? Kwa njia gani na mbinu zipi na mikakati ipi ya chapchapu ? Na hivi ukiwauliza Watanzania kwanini wao ni masikini na wewe una wajibu wa kuwatoa toka kwenye umaskini je, unawajibika kweli na je, unawatendea haki Watanzania masikini? Je, Taasisi ya Utafiti kuhusu umaskini hapa nchini imefikia wapi na yale ambayo imekwishayatafiti hadi wa leo yamefanyiwa kazi kiasi gani? Kwa maneno mengine, je, taasisi hiyo imekuwa na manufaa yaliyokusudiwa kwa Watanzania masikini au imewashibisha tu waliomo katika taasisi hiyo na nyingine kama hizo?

Na, je, ukiritimba katika masuala ya uongozi wa kijamii na uchumi ndio utakaotusaidia kutoka kwenye umasikini na matatizo yetu au tunaung'ang'ania tu kwa sababu ya mazoea na uoga wa kujaribu kilicho kipya?

Maana kuna wanaoamini kwamba serikali kuu inapswa kugawa madaraka ya maamuzi na utekelezaji sio tu kwa mikoa, wilaya, vyama vya kisiasa, mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali, makundi mbalimbali ya kijamii na watu mmoja mmoja kushiriki na kuchangia kikamilifu katika kuziona na kuzitumia fursa za kiuchumi na kijamii zilizopo nchini kuliko tulivyowahi kufanza huko siku za nyuma na vilevile kuyatafakari matatizo mbalimbali yanayowakabili Watanzania na kisha kuweka mkakati unaosadikisha kwamba 'utatuaji matatizo kila sekta, katika kila jamii' kila kona nchini ndiyo ajenda yetu ya kwanza kwa kila mpango tulionao na tutakaokuwa nao.
Tuiaminishe pia jamii yetu kwamba tukijipanga upya, kimkakati, kiakili na kwa hekina na busara zaidi tunaweza kupatia ufumbuzi sisi wenyewe matatizo na changamoto nyingi zinazotukabili.

Na pale msaada wa serikali, sekta binafsi na wasamaria wema inapohitajika inakuwa ni pale ambapo hatuna ujanja kwani kiakili, kiteknolojia na kirasilimali nyinginezo tumekwama na hatuna ujanja.

Nguvu na akili-jamii na ujasiriamali-kijamii ndio njia pekee ya kuinua ubora wa maisha ya Mtanzania.

Serikali yetu lazima ifike siku irudie maneno ya Mwalimu Nyerere kwamba, 'Serikali na Watanzania hatuna fedha. Na fedha na mtaji wetu ni akili, nguvu, maarifa, juhudi na bidii zetu wenyewe katika kutatua matatizo na changamoto mbalimbali zinazotukabili.'


Serikali ikiendelea kujifanya ndio bwana mkubwa, tajiri, ina mali, ina uwezo, ina nguvu na inaweza kila kitu na haishindwi na chochote lazima kuna siku tataibika na tutakwama.

Ninaamini ni Watanzania ndio wanaostahili kuwa BWANA MKUBWA, MATAJIRI, MFANO WA MUKTADIRI, KWA MAPENZI NA BARAKA ZA MWENYEZI MUNGU WANAWEZA KILA JAMBO, HAWASHINDWI NA LOLOTE na wingi, nguvu, matakwa na maslahi yao ndiyo yanayopasa kutawala na kuendesha nchi hii na sio vinginevyo. Demokrasia kwanza, mengine ni mazungumzo baada ya habari.

Tunaweza kumlaumu Mtanzania kuwa chanzo cha kukosa mahitaji yake ya msingi, maradhi, ujinga na umaskini wake lakini tusisahau kwamba upo uwezekano pia ikawa ni mundo na mifumo tuliyo nayo na ukiritimba wa serikali katika mipango, maamuzi na utekelezaji wake vikawa ndio sababu ya umasikini wa Mtanzania.

Katiba, wabunge na posho...

LABDA wabunge wanaotaka wasilipwe posho wameaona kile wanachokula hakilingani na kazi wanayowafanyia masikini wa Kitanzania katika jitihada zao za kutuondoa na umaskini, ujinga na maradhi.

Wametangulia Katiba katika kuleta mabadiliko ya kimsingi yanayohitajika, kwa maana ya kwamba, kipato cha kila kiongozi wa Kitanzania kwanza, kinatakiwa kinaoanishwa na mchango wake katika kupiga vita umaskini, ujinga na maradhi awali ya yote. Na kwa upande mwingine ipo haja kujenga miundo na mifumo inayomsaidia mwananchi kuondakana na umaskini badala ya miundo inayomwingiza mwananchi kwenye umaskini zaidi.

Wakati tunasubiri ujio wa Katiba mpya na namna itakayolishughulikia suala la keki ya taifa na inavyostahili kugawanywa kwa namna ambayo kila Mtanzania anakuwa na arri na motisha ya juu kuiondoa nchi hii kwenye daraja la tatu na umaskini mkubwa kwenda kwenye daraja la pili la kiuchumi kidunia lenye nafuu, utu na ubinadamu zaidi.

Saturday, June 11, 2011

Tofauti kati ya Uchumi-nchi na Uchumi-mtu

KUNA msemo ambao hudhalilisha sana matumizi ya takwimu katika taarifa mbalimbali unaosema kuna aina tatu za uongo (Ona kitabu cha Lies, Damn Lies and Statistics). Kuna uongo wa kawaida, halafu kuna uongo mweupeee na uongo wa tatu unaitwa TAKWIMU !

Katika kitabu hicho mwandishi anajaribu kuoensha kwamba uongo ulio mbaya na wa hatari zaidi ni takwimu kwa sababu wanaoziandaa takwimu huziandaa aghalabu kupotosha ukweli ulivyo; wanaozitangaza takwimu wanajua wanasema uongo lakini wanaamini katika uongo huo na wanaosikia uongo huo hawajui waamini lipi kati ya takwimu kadhaa zinazokuja kivyakevyake kila moja ikiwa na ajenda yake ya siri.

Uchumi-nchi ( Macroeconomics ) na uchumi-mtu ( Microeconomics) vyote huwasilishwa kinadharia katika takwimu zinazohusiana na maeneo husika. Mara nyingi sio rahisi kuchukua takwimu na hesabu za kila eneo kwa hiyo wakati mwingine watu huchagua kati ya maeneo kadhaa na kuwasilisha kile wanachoamini kinazungumza kwa faida ya wengine wote.

Ndio maana leo kuna Watanzania wanaoshindwa kuelewa na wanaoshangaa kwanini wakati nchi inaendelea kwa kasi kubwakutokana na takwimu zinazoonesha kuwa eti pato la Mtanzania sasa ni zaidi ya dola 500 kwa mwaka na kuwa pato la taifa linakuwa kwa asilimia sita kama sio zaidi ya hapo kuna Watanzania wasioliona hili na kulisifia na kuwasifia viongozi wao.

Ukiwauliza wataalamu wa uchumi kama sijakosea tatizo hili linaletwa na viongozi wetu kujikita zaidi katika masuala ya uchumi-nchi na kujisahau au kuwaachia wababaishaji kusimamia masuala ya uchumi-mtu.

Kwa tafsiri uchumi-nchi ni uchumi-jumla wa nchi ambao daima hutoa picha kubwa kiuchumi kwa nchi na hauangazii tu hali ya kiuchumi ya mtu mmoja mmoja. Japo chumi hizi mbili zinategemeana, zinaingiliana na kuoana sana lakini kila moja ina nafasi na wajibu wake katika jamii husika. Kwa upande mmoja, maendeleo ya nchi kiujumla huwa kivutio kwa wawekezaji, wabia wa kibiashara na kiuchumi na watalii na watu kama hao, wakati hilo halimpi sababu mwananchi mjini au kijijini kufarajika kwa sababu anaweza awe ananufaika na uchumi-nchi au kinyume cha hivyo.

Hali ilivyo kwa Tanzania ni asilimia ndogo sana ya Watanzania ndio wanaonufaika na takwimu na hali halisi ya uchumi-nchi . Hawa wanaonufaika ni pamoja na viongozi wa nchi wanaolipwa mishahara na marupurupu mazuri na wakati mwingine hawalipi kodi mbalimbali; wawekezaji na wafanyabiashara na wenye viwanda wanaoweza kuwabebesha walaji gharama zinazoongezeka katika biashara au viwanda vyao na hivyo kubakia pale pale kiuchumi hata kama mfumuko wa bei na gharama mbalimbali zimezidi kuongezeka mno katika kipindi kilichopita.

Wengine wanaonufaika na uchumi-nchi katika hali ambayo bei na mfumuko wa bei vimekuwa vikikuwa siku hadi siku ni wale waliomo katika mashirika ya kimatiafa, mashirika ya kiserikali na walanguzi wa kila aina na ukubwa.

Kwa hiyo uchumi-nchi unaoweza kuwa umekua au unakua lakini faida yote inaenda kwa wale wanaolipwa mishahara na marupurupu na posho nene, wawekezaji, wafanyabiashara, wenye viwanda, makampuni makubwa ya kitalii, waagizaji mafuta na peteroli, wenye viwanda, wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa, wafuasi wa chama kinachotawala na watu kama hao tu na sio kwa Mtanzania wa kawaida.

Katika hali kama hii nchi inakuwa kama timu ambayo wachezaji fulani kwa kuitwa wachezaji nyota basi wanalipwa mamilioni ya fedha huku wachezaji wenzao wakipata chini ya nusu ya kile wenzao wanachokipata. Kimya kimya wachezaji walio wengi (asilimia 90) wanaamua kuwaachia wachezaji wanaolipwa vizuri sana ndani ya timu wacheze wenyewe na timu ishinde. Eti timu inaachiwa kucheza bila kucheza kama timu. Wote kwa kuitazama Real Madrid na Chelsea tunajua ni kitu gani kitakachotokea.

Ili nchi kama timu ishinde inahitaji zaidi ya viwango vya kukua uchumi, wawekezaji, mipango na bajeti za serikali. Nchi inahitaji kwanza, watu waamini kwamba wamo katika safari moja na sio kila mtu ana safari yake. Pili, lazima tuwe na visheni moja ya kule tuendako sio kila mtu awe na dira au ndoto binafsi ya kule anakotaka kwenda. Tatu, lazima tujenge uchumi wetu kama timu moja, kama kitu kimoja na sio kinyume cha hiyvo. Nne, lazima akilini mwetu sote tuwe na picha ya kile tunachotaka kukijenga kama vile mfano wa nyumba inayotakiwa kujengwa. Na mwisho lakini sio jambo dogo akili zetu ziione nchi nzima, mikoa, wilaya, tarafa, kata, miji, vijiji na mitaa kama MFUMO MMMOJA mkubwa ulio na mifumo kadhaa midogo midogo nayo yote ikiingiliana kila wakati na kwamba mfumo mdogo mmoja mdogo ukiwa na tatizo basi mifumo mingine yote midogo na huo mkubwa utakuwa katika matatizo pia. Na mfumo huo mkubwa itambulike pia ni sehemu ya mfumo mkubwa kabisa wa dunia na ulimwengu kiujumla ambao kwa sasa watambulika kama utandawazi. Nasi tukiwa na jukumu la kujipanga kwa namna ambayo kwayo tunanufaika badala ya kuathirika vibaya na huo utandawazi.

Tumewahi kuzungumzia huko nyuma kuwa mahitaji muhimu ya binadamu ni pamoja na maji, chakula, mahitaji ya kijamii, mavazi, makazi/nyumba, afya na tiba, elimu na usalama wa watu na mali zao. Vitu hivi ndivyo vinavyostahili kutumika kama kigezo cha kuamua uchumi umekua au haujakua katika medani ya uchumi-mtu na wala sio takwimu za aina nyingine.

Tuwaulize wanauchumi wetu kama Tanzania ya mwaka jana wa bejeti walikuwa na hali bora zaidi au mbaya zaidi katika suala la upatikanaji maji, chakula,mahiraji ya kijamii kama huduma mbalimbali za usafiri ikiwemo wa daladala, usafi na umeme ? Majibu ya hili pengine yatawafungua macho waliofunga macho na walio katika usingizi wa kuridhika na kutosheka na hali kama ilivyo.

Je, wanauchumi wetu walio huru nchini wanasema kwamba Watanzania wameacha kuvaa mitumba kama Mwinyi na Mkapa walivyotuacha au bado tunaendea na mtumba.

Je, hivi leo ni rahisi kujenga na kumiliki nyumba kama ilivyokuwa mwaka jana au hali imezidi kuwa mbaya zaidi. Jibu kwa hili nalo litatuonesha kama tuna sababu ya kukenua meno au ya kufunga vinywa kwa hasira ya ukata na kutokuridhika.

Wanauchumi wetu waambaje katika masuala ya afya na tiba na kama shida na dhiki za kina mama na watoto na wagonjwa wengine katika mahospitali yetu zimeisha au bado zinaendelea. Ziada ya ndogondogo ikiwa je, wale mbu wa Muhimbili wametushinda au tumewadhinda ? Kama mbu hao wametushinda nina mashaka kama tumepiga hatua yoyote mbele ya maana na inayoonekana.

Hali hii ya kuutazama uchumi kutoka juu na kushindwa kuutazama toka chini utaendelea kujenga msimamo na mtazamo wa wale walioko madarakani kujijali zaidi wao wenyewe kwanza na wale wanaowaweka madarakani na kamwe 'haiwezekani' wao kuwa na mipango na sera zinazotoka chini kwenda juu, yaani, kumneemesha kwanza mnyonge kisha ndio vigogo na vizito waneemeke zaidi ya walivyoneemeka. Na hiki ndio chanzo cha wao kuona kwa miwani yenye lensi kubwa uchumi-nchi na kutazamia uchumi-mtu kwa miwani yenye lensi ndogo.

Isitoshe uchumi wowote unaojengwa kwa kutegemea zaidi rasilimali na uwekezaji nyonyaji-sana toka nje hauwezi kamwe kuleta maendeleo linganifu ya uchumi-nchi na uchumi-mtu. Na hili benki ya dunia na IMF wameliona na wanalitambua na ndio maana wanaishauri serikali kupitia upya mikataba na wawekezaji katika sekta ya madini na migodi.

Aidha, nchi inayoshindwa kucheza na kuoanisha mahesabu na takwimu kwa nadharia na vitendo katika masuala ya pande-toaji/ugavi (supply) na pande-mahitaji (demand) katika ngazi ya uchumi-mtu haiwezi kamwe kuwa na maendeleo endelevu na ambayo huwa nadra kuguswa vibaya au kuathirika na kile kinachotokea ndani na nje ya nchi. Hili kama alivyosema Shaaban Robert linahitaji KIASI. Vigogo na vizito wakpata zaidi ya KIASI na walalahoi wakikosa chini ya KIASI basi inakuwa muhali na vigumu sana kujenga pia mtaji wa kijamii ambao hutegemea watu na sio fedha katika nchi husika.

Tunafanya kosa kubwa sana kiuchumi na hususan kibajeti kwa kukosa kuwa na mipango na mikakati adhimu ya kulifanya soko la ndani lifanye kazi kubwa linaloweza kuifanya kwa kujishughulisha zaidi na soko la nje, tena kwa upande wa manunuzi ya vitu vya anasa kwa sana.

Katika kipindi tulichomo na hali tuliyo nayo kiuchumi tulitakiwa tutumie muda mkubwa zaidi na fedha nyingi zaidi za kukuza uchumi-mtu kwanza na sio vinginevyo. Bajeti ya hivi majuzi haioneshi kuwa rafiki wa Malengo ya Milenia (MDGs) ukitazama mgawo wa bajeti ulivyokwenda. Na wala hakuna panapoonesha ni kwa namna na njia gani Tanzania katika kipindi cha bajeti kijacho itajitahidi kuhakikisha wananchi wake wanapata angalau sehemu ya kuridhisha ya mahitaji yao ya msingi. Pengine kwa viongozi kuamini kuwa kwa kuwa uchumi-nchi unakuwa basi watu wana fedha tele mifukoni mwao, kitu ambacho si kweli.

Friday, June 3, 2011

Taarab asili ni Urithi usiostahili kupotea

KWENYE miaka ya hivi karibuni kumekuwa na jitihada zenye mwelekeo potofu katika vyombo vya habari mbalimbali kupotosha maana na dhana halisi ya taarabu na kile ambacho taarabu inastahili kuwa na kuitwa.

Baada ya Watanzania kugeukawavivu wa kila kitu ikiwemo kupiga ala za muziki na kutaka mteremko katika kila jambo wale waliozuka na mitindo inayotumia mashairi au tungo zenye vina na mizani au isivyo hivyo wakaona urahisi ni kuita miziki yao 'modern taarab'. Miziki hiyo ninakaata sio taarabu bali inastahili kuitwa mipasho, kiduku, rusha na roho au mnanda na vitu kama hivyo lakini sio kamwe taarabu.

Muziki wa taarabu una asili na fasili yake katika watu wa pwani na visiwani na maeneo ya mwambao wa Afrika Mashariki.
Umeathirika kwa kiasi kikubwa na muziki wa Mashariki ya Kati, India na kaswida za Kiislamu.

Sifa moja kubwa ya muziki wa taarabu tofauti na wengi wanavyofikiri sio maneno na mpangilio wake, bali ala za muziki huo na mipangilio yake na ule ufundi wa kila mwanataarabu kuwa bingwa au stadi katika kupiga chombo fulani. Taarabu isipokuwa na ala hizi sio taarabu ni igizo tu kwa kiasi fulani la kitu kama taarabu. Taarab kwa kawaida ni kitulizo cha fikra ndani ya nyumba na katika hadhara isiyoshawishiwa na usasa na umagharibi kiasi cha kupuuza maadili na mila za wahusika.

Ala za taarabu ni nyingi na swahiba wangu Ali Salehe ambaye sio tu shabiki wa taarabu bali ni mtunzi pia wa nyimbo za taarab anaweza baadaye kunipokea hapa na kuelezea zaidi kwanini tunastahili kuwekeza kwenye taarab asilia kama eneo la utamaduni linalostahili kuhifadhiwa na kuenziwa.

Taarabu kama walivyoiendelza kina Siti binti Sadi, Bi Kidude, Juma Bhalo na kina Sheikh Ilyas, Machapurala bila kuwasahau mamia ya wanawake na wanaume wa Kizanzibar na Kimrima waliochangia maendeleo ya tasnia hii adimu lakini iliyo na sifa ya kuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa mwambao ya Pwani ya Afrika Mashariki na usiostahili kuachiwa kupotea.

Taarabu ni muziki wa enzi na enzi. Ni sehemu ya utamaduni endelevu na hususan katika mikoa ya pwani ya Afrika Mashariki. Taarab ni ustaarabu, utaratibu, upole na uungwana. Taarabu ni kitulizo cha mawazo na gundi ya kuunganisha familia kama sio ukoo mzima. Sifa ambayo si mipasho, sio rusha roho sio mnanda unayo.

Taarab kiasili sio muziki wa kucheza bali wa kutazama, kusikiliza, kutafakari na kutunza. Huu ni muziki uliokuwa ukisikilizwa na watu wenye fikira, busara na hekima kuwapa muda wa kuwaza na kuwazua juu ya hili au lile. Muziki wa kupayuka, kujiona, msshauzi, kusemana, kutukanana, kuumbuana na wenye nyimbo ambazo hazina staha, usiri wala taadibu ya kuimbwa katika mafumbo hauwezi kuitwa taarab.

Ni muziki ambao kwa kawaida una ala takriban ya ishirini. Na kwa wapenzi halisi wa taarabu hufuatilia upigaji wa kila ala na ufundi au ugwiji wa yule anayetumia ala husika. Aidha, mashairi ya taarab hayaangalii tu mlingano wa vina na mizani bali maudhui na mantiki ya kile kilichomo tena kikiwe kwenye mafumbo kuweza kusomeka vyema na wanaosikiliza wimbo husika.

Ni muziki ambao hutungwa kwa mafumbo na kwa namna ambayo hauzui familia nzima, yaani, babu, bibi,baba,mama, kaka na dada wote kujumuika kwa pamoja bila kutokea chochote ambacho kinaweza kuwafanya washindwe kuzungumza au kutazamana. Taarab kiasili uliunga pamoja familia za wakazi wa mji husika. Tofauti na hiyo inayoitwa 'modern taarab' ambayo kwa kiasi kikubwa inazivunja familia katika kila mji na kijiji.

Siti bint Saad (1928) ndiye nyota wa kwanza wa taarab
ambaye kwa mara ya kwanza badala ya kuimba kwa Kiarabu aliimba kwa Kiswahili. Alifyatua mamia ya santuri za nyimbo India na wapenda muziki wa enzi hizo hakuna aliyekosa wimbo wake nyumbani.

Muziki wa taarab asili hauna tofauti na 'Classical Music' wa Ulaya au 'Country Music' wa Marekani. Miziki hiyo ilikuwepo, imekuwepo na itakuwepo bila kubadilika wala kuitwa kwa jina jingine wala kupigwa kwa namna nyingine tofauti na ilivyokuwa, ilivyo sasa na itakavyokuwa kesho.
Ni sehemu ya kudumu ya utamduni wa watu na sio kitu cha kupita na kusahaulika.

Aina hizo za miziki pamoja na kuzuka kwa miziki ya kila aina Ulaya na Marekani bado inatambulika kwa nembo na jina lake. Country ni country na classical ni classical. Hapajakuwepo muziki mwingine uliopewa umodern kuhusiana na miziki hii, hakuna kitu kama modern country au modern classic.

Rouget katika Music and Trance anafafanua kwamba neno taarab linatokana na neno la kiarabu 'tariba' likiwa na maana ya hisia za kusisimka, kudhihirisha au kutaka kufanya kitu fulani kama vile kuimba au kucheza taarab.

Taarab asili ilingia kwanza hapa Afrika Mashariki kupitia Zanzibar kunako miaka ya 1870. Aliileta Sultan Seyyid Barghash ambaye alileta kikundi cha wanamzuki toka Misri kukaa kwenye jumba lake la Kifalme.

Tofauti na viongozi wetu wa leo, Barghash aliwapeleka Wazanzibari kadhaa wakiongozwa na IbrahimMohammed kwenda kusomea muzki nchini Misri nao waliporudi waliunda kikundi cha kwanza pengine cha taarabu Afrika Mashariki kilichoitwa Zanzibar Taarab Orchestra.

Kunako 1905 kikundi cha pili cha taarabu kilizaliwa huko huko Unguja kikiitwa Ikwhani Safaa Musical Club. Kikundi hicho kipo hadi wa leo, lakini kama vilivyo vikundi vingine vya taarab 'hasa' havina msaada wowote wa maana toka kwa yeyote yule, kwani inavyoelekea wengi pamoja na viongozi wa serikali wametekwa na rusharoho na mipasho.

Taarab asili haistahili kuonekana kama ni taarab tu. Ni zaidi ya taarab. Hii ni hazina ya utamaduni katika mwambao wa Afrika Mashariki kuanzisa Lamu hadi Kilwa na Sofala.


Kama jitihada zinavyofanyika kukarabati na kutunza maeneo kama vile Mji Mkongwe Zanzibar, Bagamoyo na Kilwa ili iendelee kuwepo basi upo umuhimu pia wa wanaohusika katika serikali zetu kuhakikisha kuwa muziki wa taarab asili na wanamuziki wake wanakumbukwa na kuenziwa na kisha kizazi kipya kinajengwa ili kuendeleza muziki huu kwa faida ya vizazi vijavyo. Kwa maana, ukweli ni kwamba taarab asili ikipotea ndio utakuwa mwisho wa taarab hapa Afrika Mashariki.

Kwanini tuhifadhi taarab asilia

Kwa bahati mbaya wengi tumezoea kuchukulia vitu kama ardhi, fedha, nyumba, magari kuwa ndio rasilimali tu. Lakini muziki wa kiasili nao ni rasilimali muhimu kimaendeleo na kisaikolojia. Bila urithi wa namna hii tutakuwa ni taifa lipolipo tu ambalo si jambo zuri.

Pamoja na mambo mengine kuifufua, kuitunza na kuiendelza taarab asili ni jambo lenye faida kadhaa ikiwemo kuendeleza mila na utamaduni wetu; kuzileta familia pamoja mara kwa mara; kujenga maadili bora katika jamii; kuwa na muziki usioendana kinyume na maadili ya dini; kukuza na kuendeleza ushairi na Kiswahili; kuwa kivutio kwa wageni wa leo na kesho
na kuzienzi na kuendeleza ala asili za muziki na upigaji wake.

Ninatoa wito maalum pia kwa vyombo vya habari kuacha kuuchanganya umma juu ya muziki wa taarab. Tafadhali Bi Hindu, Dida, Mzee Chapuo, Bi Chau, Miriam wa Migomba, Kristina wa Mbezi kwa kuturahisisishia hili kwa kubaini kwamba Afrika Mashariki kuna taarab moja tu, nayo ni taarab asilia ambayo kwa kawaida hupigwa na vyombo vingi, hutumia mafumbo na usiri katika nyimbo zake na hauchezwi achilia mbali kunenguliwa na kutingishiwa mawowowo.

Miziki inayojiita modern taarab iitwe kwa majina yao yanayostahili kama ni kiduku basi kiduku, kama ni rusha roho basi rusha roho fulani, kama ni mipasho basi ni mipasho na kama ni mnanda uitwe mnanda
na miziki hii isiruhusiwe kutumia mgongo wa taarab kujijenga isipostahili.

Nikiri kuwa nilitaka sana nitembelee Lamu, Malindi, Mombasa, Tanga na Zanzibar kuzungumza na wakereketwa wenzangu wa taarabu asili kabla ya kuandika makala haya lakini haikuwezekana. Ninaamini, hata hivyo kupitia makala haya ujumbe unaweza kufika kwa kiasi fulani.

Ninawashauri wanaharakati wa kulinda na kuendeleza utamaduni wetu kuangalia uwezekano wa haya yafuatayo: Kusaidia juhudi binafsi zilizopo za kufufua na kuendeleza vikundi vya taarabu kupitia vilabu na vyuo vya upigaji ala za asili za taarab (mathalani juhudi za Bi Hamndani, Zanzibar) ; Kushirikiana na UNESCO kuhifadhi taarab asili kwa kutumia TEKNOHAMA;
Kuwatafuta wanataarab asil waliko na kuwaunganisha ili kuufufua na kuchochea kuwepo kwa muziki huo kiasili na kuongeza vionjo viwili vitatu vya kuvutia familia zaidi kuliko mtu mmoja mmoja.

Aidha, kusaidia vikundi vilivyopo lakini havina ala za kutosha za muziki toka Misri na Uarabuni; kuenzi Ushairi katika vyombo vya habari kukuza vipaji vya washairi chipukizi na
kuchukulia Taarab asili kama urithi usiostahili kupotea kwa msaada wa UNESCO na wapenda utamaduni wetu wengineo.


http://www.gmail.com
sammy.i.makilla@gmail.com