Monday, February 20, 2012

Wakatu umefika wa kuwa na Rais mwanamke?

HUU si wakati mbaya wa kuanza kuzungumzia kama nchi yetu baada ya
miaka hamsini ya utawala wa marais wanaume, haijfafikia sasa kumruhusu
mwanamke awe kiongozi wa Tanzania.

Ikumbukwe kuna juhudi mbalimbali zinazofanyika ili kuwapendelea
wanawake washike nafasi nyingi kadri iwezekanavyo bungeni, serikalini
na kwingineko. Na kilichobakia ni Ikulu nayo kuwa na rais mwanamke kwa
mara ya kwanza.

Ieleweke, hata hivyo, hatumtaki mwanamke kwa sababu tu ya uanawake
wake, na kuwa tofauti na mwanamme, bali tunamtaka mwanamke mwenye
akili, uwezo, jasiri na anayeweza kuwadhihirishia wanaume kuwa wao
katika miaka 50 ya mwanzo ya uhuru wetu walikuwa wakiichezea shilingi
yetu chooni, na ndiyo maana imeporomoka kiasi hicho.

Isitoshe, hii ni njia muafaka kabisa ya kuzima uchu, uroho, tamaa na
njaa ya ukubwa miongoni mwa wanaume katika vyama vyetu hivi leo ambao
badala ya kuwaondolea Watanzania matatizo yao mbalimbali wameanza
kugombania nani atakuwa rais 2015 kama vile wote bila aibu wala haya
wana mihadi na Mwenyezi Mungu, kwamba, hadi kufikia hapo atakuwa bado
kawaridhia fursa ya kupumua na kutanua katika dunia hii.

Kwa miaka zaidi ya hamsini sasa tumeona marais wanaume wakifanya kazi
kwa staili, kipaumbele na mikakati na mbinu zao mbalimbali. Kuna
wakati tulianza kwenda mbele, lakini bahati mbaya upepo wa shetani
ukatukumba tukaua ushirika, vyama vya kijamii, halmashauri za miji na
miundo mingine muafaka ya wakati huo na hivyo kupoteza zaidi ya miaka
20 ya kimaendeleo kwa makosa ya siasa zisizo na ushindani au
kudhibitiwa. Ninaamini, huko tunakokwenda ushindani utakuwa na
kudhibitiana na kudhibitiwa na kujidhibiti yatakuwa mambo ya kila siku
na ya kawaida. Na kwamba mwenye sifa na vigezo vya kutosha ndiye
atakayekuwa kiongozi na wababishaji na wasanii hawatakaa tena wapewe
nafasi. Ninaamini hadi kufikia hapo uigizaji sinema utakuwa umefikia
kiwango cha juu kabisa na watu kama hao kwenda kutafuta utajiri huu na
sio kuja kulazimisha kuwa viongozi na wakubwa wetu tena. Na mwanamke
atakayekuja kuwa rais hatakuwa msanii au muigizaji bali mtendaji,
mleta mabadiliko ya kweli na mwanamapinduzi ya kiuchumi na kijamii.

Sifa za wanawake kama viongozi

Wanaume kama walivyozoea kusema uongo kwa wake, wapenzi , watoto na
jamaa zao ndivyo walivyogeuka kuwa waongo wakubwa pia katika siasa na
serikali.

Fursa ya kuwa na rais mwanamke, ambao kimsingi ni wastu wasiopenda
uongo ingawa wapo wanaopenda uongo na umbeya pia, ni fursa ya kuanza
kusafisha serikali na vyama vya siasa huko tunakokwenda. Ili
tuondokane kabisa na tabia inayojijenga hivi sasa kwamba ukienda
kuajiriwa na gazeti, redio au televisheni fulani unaajiriwa ili kwenda
kuandika au kutangaza uongo. Watu kwa njaa ya ajira na malezi ya
watoto na watu tegemezi wanakubali kuuza utu na ubinadamu wao kwa
kujidhalilisha kuandika na kutangaza uongo mweupee, ili tu mtu apate
kujisetiri. Hii ni aibu kubwa kuliko mfano, lakini ndipo hapa ambapo
wanasiasa wanaume leo wametufikisha.

Aidha, wanawake ni viumbe wenye kiasi na kutosheka, tofauti na
wanaume. Hii ina maana kwamba mwanamke akishapata vitu vya msingi
anavyohitaji katika maisha yake kwa kawaida hawi na tamaa zaidi kama
inavyokuwa kwa wanaume. Kwa hiyo kujilimbikizia ni sifa ambayo
mwanamke hanayo sana, ila panapokuwa na kasosro za kiakili, kitamaa na
kimaumbile kwa mhusika.

Mwanamke pia ni mzuri katika iktisadi. Uwekevu ni tabia ya kuifanya
shilingi elfu kumi itoshe siku tatu badala ya siku moja. Wanawake
wanayo sifa hii, lakini ni wanaume wachache sana wanayo. Na ndiyo
maana ukianza kumsema mwanamme kuwa anatumia vibaya, mbadhirifu,
hatunzi fedha ni mwepesi kununa. Lakini huu ni ukweli mwanamme daima
mbadhirifu. Na tunayaona hatuhitaji kuambiwa.

Sifa nyingine ya wanawake ni ile ya kuwa waaminifu (ingawa wanaokuwa
kinyume cha hivyo, hukubuku kuzidi hata wanaume), na hivyo angala kuwa
na watendaji chini ya rais mwanamke kama huyo ambaye watu wengi
wataiga mfano wake na hivyo kurejesha imani zaidi kwa wananchi. Ambao
hivi leo, hawaamini wanasiasa na hususana wabunge wao, kutokana na
yale yanayoendelea ndani na nje ya majimbo yao.

Katika miaka kadhaa, niliyokuwa mkuu kwenye makampuni na idara
mbalimbali, ilitokea aghalabu kuwategemea na kuwaamini wasaidizi wangu
wanawake zaidi ya nilivyowaamini wanaume. Wanaume huwa na sababu elfu
za kukuelezea wameshindwa kufanya jambo fulani kwa sababu hii au ile.

Matatizo mengi yanayowakabili Watanzania leo, yanawagusa zaidi
wakinamama kuliko wanaume. Mathalani, unapoongelea suala la watoto na
malezi, tatizo hili linabebwa kwa zaidi ya asilimia 90 na wanawake.

Hili linaendana na tatizo la mayatima na watoto wa mitaani. Hakuna
mama anayependa kumuona mwanawe au mtoto wa mwenzie katika uyatima au
kukosa mlezi. Hili haliwaumi sana wanaume. Pengine, kuwepo kwa rais
mwanamke kutatoa msukumo zaidi kwa upande huu.

Marais wanaume na wanasiasa kwa ujumla na mangimeza kwa upande
mwingine wamejenga mazingira ya kuwapa matunzo, malezi na uangalizi
viongozi wazee wastaafu. Lakini wazee wa kawaida hakuna anayewajali.

Kuwepo kwa rais mwanamke na ule ukweli kwamba sio wanaume bali ni
wanawake wanaosumbuka zaidi katika kuwatunza wazee wetu, upo uwezekano
mkubwa kwamba sera nzuri na zenye kufanya kazi zitabuniwa na kiongozi
huyo, kutokana na kuelewa uzito na ugumu wa kuwatunza wazee na kuwapa
matumaini huku ukijua fika wanasubiri kwenda safari yao wasiorejea
tena!

Ahadi nyingi zilizotolewa na rais aliyeko madarakani zilihusu
urahisishaji upatikanaji maji mijini na vijijini. Ni dhahiri ahadi
zilizo nyingi hazitatimizwa. Na ukweli ni kuwa anayesumbuliwa sana na
dhiki hii sio mwanamme, ni mwanamke, iwe mjini au vijijini ambapo sasa
kuna tofauti ndogo sana kati yao.

Kwa kutambua uzito wa tatizo la maji kwa wanawake, kiongozi mwanamke,
atajitoa kwa hali na mali, kuona anawasaidia wemzake kugeuza dhiki na
tatizo hili kuwa historia isiyopendeza katika nchi hii.

Hivi leo ugumu wa maisha nchini umefanya tatizo la utafutaji na
upatikanaji kuni, mkaa na nishati nyinginezo kuwa ghali na gumu zaidi
katika kila familia. Na mhusika mkuu au muathirika mkuu hapa sio
mwingine ila ni mwanamke.

Ni dhahiri, rais mwanamke atafanya kila awezalo ili adha na kero ya
gharama na upatikanaji wa nishati kwa njia inayorahisisha maisha ya
mwanamke mijini na vijijini yawe ni mambo yatakayopigwa vita kwa
ukucha na jino na kwa wepesi wa radi au tetemeko la ardhi.

Hivi sasa vijana wengi wanakimbilia mjini na hivyo kuwaachia mama na
dada zao kazi zote za sulubu kiasi ambacho wanawake wengi vijijini
wanachoka na kupoteza uzuri wao wakiwa na miaka 30 tu. Hii si haki, ni
lazima rais ajaye ahakikishe kwamba tunawarahisishia wanawake maisha
huko vijijini kwa namna ambayo wanawake wanaendelea kuwa wabichi na
wenye mvuto hata wakiwa na miaka 40. Na hili ni jambo linalowezekana
kama wanawake watakataa kuendelea wabeba mifuko ya wanaume nchini, na
wao kumchagua mwanamke mwenzao kuwa rais wa kwanza mwanamke katika
kizazi hiki na wakati huu tulio nao. Maana ukweli ni mwanamke tu,
ndiye anayeweza kuamua rais ajaye awe mwanamke au mwanamme!

Picha nyingi tulizoziona wakati wa mgomo wa madaktari nchini,
hazikuonyesha wanaume bali wanawake. Na wanaume ni wale wababe
waliokuwa wakidiriki pamoja na kuugua kwao kusema kwamba madaktari
poa, waendelee tu na mgomgo wao mbona wanasiasa wanakwiba mchana
kweupe?

Ninahakika rais mwanamke siyo tu ataimarisha huduma na afya tofauti na
viongozi wa sasa, bali ataiwezesha nchi kuwa na huduma za kisasa na
kukomesha kabisa nchi kupoteza mabilioni kwa ajili ya kwenda tibia
watu nchi za nje, kwani mahospitali ya hapa nyumbani nayo yatakuwa
yanatibu pia wagonjwa kutoka nchi za nje katika wakati wake.

Tahadhari: Ili kumpata kiongozi bora na atakayekuwa mfano kwa wanawake
na wanaume ni vizuri kuepuka wanawake wenye uchama kupindukia; wenye
tabia ya kuzomea na kukashifu wenye mitazamo tofauti; wapigaji
vigelegel ovyo na wale wanaobebwa sio kwa sababu ya akili na uwezo wao
bali kwa sababu ya jinsia yao. Aidha, huu si wakati wa kuwa na
viongozi wanaopenda kwenda nchi za nje wasikojifunza lolote la
kuibadili nchi yao, bali wakati wa kuwa na kiongozi anayependa kwenda
vijijini na kujifunza mbinu na mikakati ya kuufuta umaskini huko huko
vijijini, na wakati huohuo kuwatunuku wanavijiji utajiri na neema, na
hivyo nchi yetu nzima kuwa tajiri na ustawi wa hali ya juu zaidi
kimaisha.

Friday, February 3, 2012

Wizara ya Afya, Uongozi na Muundo wake vinakwenda na wakati?

KWA UJUMLA pamoja na bajeti kubwa na misaada mbalimbali ambayo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hupata bado sekta hii sikuzote imekuwa katika tatizo hili au lile.

Tatizo hili la madaktari kugoma ni tatizo lililokuwa njiani na kila mtu akawa analiona, lakini wengi wakaamua kuficha kichwa chao mchangani kama vile mbuni afanyavyo anavyoona hatari i mbele yake. Hili ni kosa kwa sababu unatoa nafasi kwa nadhara makubwa zaidi kutokea.

Isitoshe hili ni moja tu kati ya matatizo ambayo wizara hiyo inakabiliana nayo. Yapo mengine mengi, makubwa kwa madogo ambayo kama petroli yanahitaji mtu kupita tu na kijinga cha moto na moto ukalipuka. Hivyo, kutafuta mchawi wa matatizo ya sekta ya afya kunakoishia kumtaja mtu mmoja au wawili sio kitu cha busara wala hekima na hakimsaidiii yoyote ndani au nje ya wizara husika.

Binafsi ninaamini kuna matatizo yafuatayo katika wizara husika: Utawala, uaminifu na uwezo wa mameneja wa mahospitali;
madaktari kufunguka macho zaidi juu ya haki zao zisizotekelezwa; manesi na wafnyakazi wasaidizi katika mahospitali mbalimbali kugeuzwa wafanyakazi maskini na ombaomba; wagonjwa kukosa mahitaji, ulinzi na maangalizi ya msingi.


Aidha ni makosa kwa upande wangu kwa wizara hiyo kubebeshwa idara kama ile
ya Ustawi wa jamii na makundi yake ambayo kwa maono yangu ni mzigo ambao nao unahitaji ubebaji wa aina yake ili kutendea haki sawa pande zote mbili, yaani Idara ya Afya na ile Idara ya Ustawi wa Jamii.

Vilevile, huu ni wakati wa kuangalia upya kama uoga wetu wa kuiachia mikoa na wilaya kuwa huru zaidi katika mipanga, mikakati, oganaizesheni na utekelezaji wa majukumu ya sekta ya afya nchini ni kitu kinachosaidia kupungua au kuongeza matatizo katika sekta hiyo.

Matatizo mengine ninayoyaona kwa upande wangu ni lile la ujira, maslahi na posho za watumishi wa ngazi za kati na chini katika wizara hiyo; kukosa utawala na menejimenti bora ya rasilimali watu katika sekta muhimu kama hii; muundo wa wizara uliopitwa na wakati;
kukosa aina yoyote ya ushindani kati ya wafanyakazi na kati ya mahospitali nchini; kukosa mifuko maalum kwa mahospitali na watumishi inayoweza kuchangia kuleta ahueni kwa njia moja au nyingine; udhibiti dhaifu wa rasilimali na hususan fedha wizarani na kukosekana na ubunifu na uvumbuzi katika sekta nzima ya afya nchini.


Ninaamini sina akili wala uwezo wa kutoa majawabu kwa changamoto zinazokabili wizara hii, kwani kitakwimu na kitaalamu sijajaliwa uwezo wa kufundwa na kuelewa kila jambo lipasalo. Nitajaribu tu kutoa mawazo ya kijuu juu ambayo kwayo waelewa zaidi wanaweza kujenga juu yake na hatimaye ufumbuzi wa matatizo ya kudumu au ya muda mrefu kwa wizara na changamoto zake yakapatikana.

Sekta hii ni nyeti. Inahitaji mameneja na watawala ambao wanaoana na kuiva vizuri na watumishi wa ngazi za juu na chini. Ukiwaweka watu wanaojiona ni wakubwa, bora na muhimu zaidi kuliko wengine basi misingi yote ya kuwa na wizara yenye mafanikio unakuwa umebomolewa fumba na kufumbua. Siingili kwa undani zaidi juu ya hili, lakini kwa wote wanaoelewa ukweli huu tutakuwa kwa uahkika katika frekwensi moja hapa.

Ikiwezekana majopo ya wataalamu husika yatastahili kuwashauri wakubwa wa nchi nani anafaa kwa nafasi ya uwaziri, unaibu waziri na nafasi za juu katika wizara na mahospitali kwa namna wazi na bora zaidi kuliko iliyopo hivi sasa. Kubwa la kuzingatiwa ni kuwa na watu wenye uwezo wa juu kiutendaji katika masuala ya utawala, uaminifu na uwezo wa kiumeneja katika mahospitali na sekta ya afya na tiba kwa ujumla.

Madaktari kutokana na yale yanayotokea kwingineko hivi duniani wameona mengi ambayo yamewasaidia kufunguka macho juu ya mambo mengi. Ni vizuri viongozi wa wizara wakajua kuwa wanayoyajua kuhusu sekta hiyo na mahospitali katika nchi zenye maisha bora ingawa maskini na
madaktari wetu nao wamefunguka macho zaidi juu ya haki zao zisizotekelezwa.

Aidha, manesi na wafnyakazi wasaidizi katika mahospitali mbalimbali wamechoka kugeuzwa wafanyakazi maskini na ombaomba katika nchi yao na kukosa uwezo wa kuwalisha na kuwasomesha vizuri watoto wao ila kwa kungojea bakshishi kutoka kwa wakubwa ambao ndio chanzo cha wadhifa wao kimshahara, kimaslahi na kihali ya maisha.

Katika nchi ambayo kuna tatizo kubwa la ajira na vifaa vinavyotakiwa na mahospitali vinaweza kutengenezwa na magenge ya seremakala au mawelda (wachomaji na waundaji vitu vya bati na chuma) toka Mwenge, Keko, Kawe na kwingineko nchini na wagonjwa kukosa mahitaji, samani, vifaa, ulinzi na maangalizi ya msingi, basi wanaosimamia wizara husika ni kama vile wapo wapo tu, na ni ile aina ya uongozi ambayo huachia matatizo kuendelea kuwa matatizo katika sehemu husika, hata ukiwaachia miaka hamsini kufanya kazi mahala hapo.

Aidha ni makosa kwa upande wangu kwa wizara hiyo kubebeshwa idara kama ile
ya Ustawi wa jamii na makundi yake ambayo kwa maono yangu ni mzigo ambao nao unahitaji ubebaji wa aina yake ili kutendea haki sawa pande zote mbili, yaani Idara ya Afya na ile Idara ya Ustawi wa Jamii.

Kwa maneno mengine ni makosa kuwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kama wizara moja badala ya kuwa ni wizara mbili. Ndio maana hivi leo utunzaji na usaidizi kwa wazee, watoto watundu wanaoishinda jamii na familia zao, mayatima, walemavu, albino, wajane, ombaomba na watu kama hao ni mambo yanayofanyika kiubabaishaubabaishaji tu na kuruhusu wajanja kujinufaisha kutokana na ombwe lililopo.

Vilevile, huu ni wakati wa kuangalia upya kama uoga wetu wa kuiachia mikoa na wilaya kuwa huru zaidi katika mipanga, mikakati, oganaizesheni na utekelezaji wa majukumu ya sekta ya afya nchini ni kitu kinachosaidia kupungua au kuongeza matatizo katika sekta hiyo.

Muundo mpya, majukumu mapya

Ninavyoamini ni kuwa wizara ya Afya ingeliachiwa tu kushughulikia majukumu ya upatikanaji dawa, uendeshaji mahospitali na uratibu wa shughuli za kinga, afya na tiba nchini na si zaidi ya hapo.

Shughuli na majukumu yote yanayosalia, kwa maoni yangu, yangestahili kupewa Taasisi huru ambazo utendaji wake sio utakuwa na ufanisi na ufanifu zaidi bali pia unaweza ukawa ungiza fedha zaidi kuliko ya zinavyotumia.

Pamoja na wizara kugawanywa katika sehemu zaidi ya mbili ningelipendekeza pia kwamba
hata wizara ya afya asilia yenyewe igawanywe katika:
Taasisi ya Hospitali za Ngazi ya Rufaa nchini; Taasisi ya Hospitali za Ngazi ya Mkoa nchini; Taasisi ya Hospitali za Ngazi ya Wilaya nchini;
Taasisi za Hospitali Binafsi na zahananti; Taasisi za Hospitali za Kijamii na Hospitali za Kiimani nchini; Taasisi ya Utafiti kwa Tiba Mbadala na Tiba za Kisunna na Taasisi Maalum ya Kuoanisha na Kuunganisha nguvu na uwezo wa taasisi za sekta za afya kwa ufanisi na ufanifu zaidi nchini.

Dhamira kuu ya uanzishwaji wa taaisisi kama hizo hapo juu zinatokana na ule ukweli kwamba wizara na hospitali zetu kwa hali ilivyo haziwwezi kujitosheleza katika mahitaji yao yote bila kuwa watundu, wabunifu, wavumbuzi na wanaoweza kupanua wigo wa wagonjwa wanaotibiwa hadi nje ya mipaka yetu. Hiki ni kitu kinachowezakana, kinataka tu serikali iliyo angavu na inayotoa fursa kwa wenye mawazo mapya kuonekana, kufnayiwa kazi, kutunzwa na kuenziwa.

Matatizo mengine ninayoyaona kwa upande wangu ni lile la ujira, maslahi na posho za watumishi wa ngazi za kati na chini katika wizara hiyo. Katika nchi kama Norway hivi leo kuna watu wachache wanaotaka uanasiasa au uwaziri kwa sababu kazi wanazozifanya zinawalipa vizuri zaidi kuliko uwaziri au ubunge.

Kwa kugeuza miguu juu na kichwa chini sera hii muhimu ya kipato cha mtu, leo tunaishiwa kuwa na watu wa ajabu wanaopewa nafasi za ubunge, baadhi yao wakifanya pati na kualika wasichana wenye sketi fupi tu kuliko wote kuhudhuria pati hizo !!! Hawa ndio wabunge wetu, na hii ni nchi yetu, na yote haya tumeyataka sisi wenyewe!

Wizara husika na mahospitali ni maeneo yanayohitaji idara nzito ya rasilimali watu. Ukikosa utawala na menejimenti bora ya rasilimali watu katika sekta muhimu kama hii; na kuwa na muundo wa wizara uliopitwa na wakati;
na ukakosa aina yoyote ya ushindani kati ya wafanyakazi na kati ya mahospitali na taasisi au idara zake nchini ni dhahiri unajenga mwanzo mzuri wa matatizo na shinikizo zisizokwisha wakati wote huko mbele ya safari. Ni muhimu kuvuta hatua moja nyuma na kuona ni kwa namna gani jambo hili linaweza kufikiriwa na kuzingatiwa na kisha kuingizwa katika mbinu na mikakati ya ujenzi wa wizara mpya yenye mtazamo chana unaojiandaa kabla kupambana na kila aina ya changamoto mbele yake.

Umefika wakati wa kujiuliza pia kama ni shahi kwa wizara na mahospitali mikoani na wilayani kukosa mifuko maalum kwa mahospitali na watumishi inayoweza kuchangiwa na wenye fedha na uwezo nchini iwe ni watu binafsi au mashirika au taasisi za kidini au vyama vya kisiasa !

Mifuko kama hii si haba inaweza kuchangia kuleta nyingine katika mahospitali na zahanati zetu katika maeneo mbalimbali ya taifa letu.

Ipo haja pia ya kuangalia kama tuna udhibiti imara au dhaifu wa rasilimali na hususan fedha wizarani. Aidha, kuona kama matumizi ya wizara hiyo ni yale ambayo kweli yanastahili kufanyika na wizara husika au ni matumizi ambayo hayastahili kuwa na nafasi katika wizara kama hiyo. Maana ukiwa na wizara inayotumia mabilioni kulipia matangazo ya biashara kwangu binafsi ni walakini mkubwa na unastahili kutazamwa na CAG kwa undani zaidi ya kawaida anayoifanya.

Wizara ambayo inaviza na kudumaza akili, uwezo, ubunifu na uvumbuzi katika rasilimali watu zake ni wizara inayojichimbia kabura lake wakati yenyewe ingali hai kwa kupenda. Na wizara ikiwa hivyo basi hilo huashiria kukosekana na kuadimika kwa ubunifu na uvumbuzi katika sekta nzima ya afya nchini.

Ni muhimu pia kujenga ushindani kati ya hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini na hata kati ya hospitali za rufaa kibiashara na kijamii pia. Na wale wanaokuwa bora kutunzwa kwa mujibu wa taratibu na kanuni zitakazokubaliwa na wadau wote. Bila ya ushindani, tutaendelea kuachia wasiostahili kuzawadiwa, na wanaostahili kuzawadiwa kutokupata lolote na hivyo kuwavunja moyo na imani.

Lazima wizara na hospitali za rufaa, mikoa na wilaya kuwa na mfuko maalum (Health and Medicare Foundation) wa fedha za kuchangia na msaada kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya hospitali na vilevile kuendesha tafiti mbalimbali ambazo zitawasaidia interns na waganga kufanya utafiti utaowangezea kipato chao kwa namna moja au nyingine.

Tunastahili pia kuuwatumia vijana wa Kitanzania wasio na ajira kutengeneza vitanda, magodoro, mipira ya wagonjwa na samani na vifaa vinavyohitajika mahospitalini na kwa hiyo tukaua ndege wawili kwa jiwe moja.

Huu ni wakati pia wa kuziwezesha na kuziipa hospitali za mipakani changamoto na uwezo wa kutibu wagonjwa toka nje ya mipaka yetu na kwa uwekezaji huu sekta ya afya na tiba isibaki kuwa ya matumizi tu, bali pia inayoiingia taifa pato la haja.
Kinachohitajika ni kuboresha majengo na mandhari ya hospitali husika, kuwapa madaktari na watumishi wengine motisha ya kutosha, na kisha kuweka vifaa vya kisasa katika mahospitali hayo na hivyo kuiingizia nchi fedha za kigeni na uwezo wa kupunguza gharama kwa wagonjwa wa ndani..