HUU si wakati mbaya wa kuanza kuzungumzia kama nchi yetu baada ya
miaka hamsini ya utawala wa marais wanaume, haijfafikia sasa kumruhusu
mwanamke awe kiongozi wa Tanzania.
Ikumbukwe kuna juhudi mbalimbali zinazofanyika ili kuwapendelea
wanawake washike nafasi nyingi kadri iwezekanavyo bungeni, serikalini
na kwingineko. Na kilichobakia ni Ikulu nayo kuwa na rais mwanamke kwa
mara ya kwanza.
Ieleweke, hata hivyo, hatumtaki mwanamke kwa sababu tu ya uanawake
wake, na kuwa tofauti na mwanamme, bali tunamtaka mwanamke mwenye
akili, uwezo, jasiri na anayeweza kuwadhihirishia wanaume kuwa wao
katika miaka 50 ya mwanzo ya uhuru wetu walikuwa wakiichezea shilingi
yetu chooni, na ndiyo maana imeporomoka kiasi hicho.
Isitoshe, hii ni njia muafaka kabisa ya kuzima uchu, uroho, tamaa na
njaa ya ukubwa miongoni mwa wanaume katika vyama vyetu hivi leo ambao
badala ya kuwaondolea Watanzania matatizo yao mbalimbali wameanza
kugombania nani atakuwa rais 2015 kama vile wote bila aibu wala haya
wana mihadi na Mwenyezi Mungu, kwamba, hadi kufikia hapo atakuwa bado
kawaridhia fursa ya kupumua na kutanua katika dunia hii.
Kwa miaka zaidi ya hamsini sasa tumeona marais wanaume wakifanya kazi
kwa staili, kipaumbele na mikakati na mbinu zao mbalimbali. Kuna
wakati tulianza kwenda mbele, lakini bahati mbaya upepo wa shetani
ukatukumba tukaua ushirika, vyama vya kijamii, halmashauri za miji na
miundo mingine muafaka ya wakati huo na hivyo kupoteza zaidi ya miaka
20 ya kimaendeleo kwa makosa ya siasa zisizo na ushindani au
kudhibitiwa. Ninaamini, huko tunakokwenda ushindani utakuwa na
kudhibitiana na kudhibitiwa na kujidhibiti yatakuwa mambo ya kila siku
na ya kawaida. Na kwamba mwenye sifa na vigezo vya kutosha ndiye
atakayekuwa kiongozi na wababishaji na wasanii hawatakaa tena wapewe
nafasi. Ninaamini hadi kufikia hapo uigizaji sinema utakuwa umefikia
kiwango cha juu kabisa na watu kama hao kwenda kutafuta utajiri huu na
sio kuja kulazimisha kuwa viongozi na wakubwa wetu tena. Na mwanamke
atakayekuja kuwa rais hatakuwa msanii au muigizaji bali mtendaji,
mleta mabadiliko ya kweli na mwanamapinduzi ya kiuchumi na kijamii.
Sifa za wanawake kama viongozi
Wanaume kama walivyozoea kusema uongo kwa wake, wapenzi , watoto na
jamaa zao ndivyo walivyogeuka kuwa waongo wakubwa pia katika siasa na
serikali.
Fursa ya kuwa na rais mwanamke, ambao kimsingi ni wastu wasiopenda
uongo ingawa wapo wanaopenda uongo na umbeya pia, ni fursa ya kuanza
kusafisha serikali na vyama vya siasa huko tunakokwenda. Ili
tuondokane kabisa na tabia inayojijenga hivi sasa kwamba ukienda
kuajiriwa na gazeti, redio au televisheni fulani unaajiriwa ili kwenda
kuandika au kutangaza uongo. Watu kwa njaa ya ajira na malezi ya
watoto na watu tegemezi wanakubali kuuza utu na ubinadamu wao kwa
kujidhalilisha kuandika na kutangaza uongo mweupee, ili tu mtu apate
kujisetiri. Hii ni aibu kubwa kuliko mfano, lakini ndipo hapa ambapo
wanasiasa wanaume leo wametufikisha.
Aidha, wanawake ni viumbe wenye kiasi na kutosheka, tofauti na
wanaume. Hii ina maana kwamba mwanamke akishapata vitu vya msingi
anavyohitaji katika maisha yake kwa kawaida hawi na tamaa zaidi kama
inavyokuwa kwa wanaume. Kwa hiyo kujilimbikizia ni sifa ambayo
mwanamke hanayo sana, ila panapokuwa na kasosro za kiakili, kitamaa na
kimaumbile kwa mhusika.
Mwanamke pia ni mzuri katika iktisadi. Uwekevu ni tabia ya kuifanya
shilingi elfu kumi itoshe siku tatu badala ya siku moja. Wanawake
wanayo sifa hii, lakini ni wanaume wachache sana wanayo. Na ndiyo
maana ukianza kumsema mwanamme kuwa anatumia vibaya, mbadhirifu,
hatunzi fedha ni mwepesi kununa. Lakini huu ni ukweli mwanamme daima
mbadhirifu. Na tunayaona hatuhitaji kuambiwa.
Sifa nyingine ya wanawake ni ile ya kuwa waaminifu (ingawa wanaokuwa
kinyume cha hivyo, hukubuku kuzidi hata wanaume), na hivyo angala kuwa
na watendaji chini ya rais mwanamke kama huyo ambaye watu wengi
wataiga mfano wake na hivyo kurejesha imani zaidi kwa wananchi. Ambao
hivi leo, hawaamini wanasiasa na hususana wabunge wao, kutokana na
yale yanayoendelea ndani na nje ya majimbo yao.
Katika miaka kadhaa, niliyokuwa mkuu kwenye makampuni na idara
mbalimbali, ilitokea aghalabu kuwategemea na kuwaamini wasaidizi wangu
wanawake zaidi ya nilivyowaamini wanaume. Wanaume huwa na sababu elfu
za kukuelezea wameshindwa kufanya jambo fulani kwa sababu hii au ile.
Matatizo mengi yanayowakabili Watanzania leo, yanawagusa zaidi
wakinamama kuliko wanaume. Mathalani, unapoongelea suala la watoto na
malezi, tatizo hili linabebwa kwa zaidi ya asilimia 90 na wanawake.
Hili linaendana na tatizo la mayatima na watoto wa mitaani. Hakuna
mama anayependa kumuona mwanawe au mtoto wa mwenzie katika uyatima au
kukosa mlezi. Hili haliwaumi sana wanaume. Pengine, kuwepo kwa rais
mwanamke kutatoa msukumo zaidi kwa upande huu.
Marais wanaume na wanasiasa kwa ujumla na mangimeza kwa upande
mwingine wamejenga mazingira ya kuwapa matunzo, malezi na uangalizi
viongozi wazee wastaafu. Lakini wazee wa kawaida hakuna anayewajali.
Kuwepo kwa rais mwanamke na ule ukweli kwamba sio wanaume bali ni
wanawake wanaosumbuka zaidi katika kuwatunza wazee wetu, upo uwezekano
mkubwa kwamba sera nzuri na zenye kufanya kazi zitabuniwa na kiongozi
huyo, kutokana na kuelewa uzito na ugumu wa kuwatunza wazee na kuwapa
matumaini huku ukijua fika wanasubiri kwenda safari yao wasiorejea
tena!
Ahadi nyingi zilizotolewa na rais aliyeko madarakani zilihusu
urahisishaji upatikanaji maji mijini na vijijini. Ni dhahiri ahadi
zilizo nyingi hazitatimizwa. Na ukweli ni kuwa anayesumbuliwa sana na
dhiki hii sio mwanamme, ni mwanamke, iwe mjini au vijijini ambapo sasa
kuna tofauti ndogo sana kati yao.
Kwa kutambua uzito wa tatizo la maji kwa wanawake, kiongozi mwanamke,
atajitoa kwa hali na mali, kuona anawasaidia wemzake kugeuza dhiki na
tatizo hili kuwa historia isiyopendeza katika nchi hii.
Hivi leo ugumu wa maisha nchini umefanya tatizo la utafutaji na
upatikanaji kuni, mkaa na nishati nyinginezo kuwa ghali na gumu zaidi
katika kila familia. Na mhusika mkuu au muathirika mkuu hapa sio
mwingine ila ni mwanamke.
Ni dhahiri, rais mwanamke atafanya kila awezalo ili adha na kero ya
gharama na upatikanaji wa nishati kwa njia inayorahisisha maisha ya
mwanamke mijini na vijijini yawe ni mambo yatakayopigwa vita kwa
ukucha na jino na kwa wepesi wa radi au tetemeko la ardhi.
Hivi sasa vijana wengi wanakimbilia mjini na hivyo kuwaachia mama na
dada zao kazi zote za sulubu kiasi ambacho wanawake wengi vijijini
wanachoka na kupoteza uzuri wao wakiwa na miaka 30 tu. Hii si haki, ni
lazima rais ajaye ahakikishe kwamba tunawarahisishia wanawake maisha
huko vijijini kwa namna ambayo wanawake wanaendelea kuwa wabichi na
wenye mvuto hata wakiwa na miaka 40. Na hili ni jambo linalowezekana
kama wanawake watakataa kuendelea wabeba mifuko ya wanaume nchini, na
wao kumchagua mwanamke mwenzao kuwa rais wa kwanza mwanamke katika
kizazi hiki na wakati huu tulio nao. Maana ukweli ni mwanamke tu,
ndiye anayeweza kuamua rais ajaye awe mwanamke au mwanamme!
Picha nyingi tulizoziona wakati wa mgomo wa madaktari nchini,
hazikuonyesha wanaume bali wanawake. Na wanaume ni wale wababe
waliokuwa wakidiriki pamoja na kuugua kwao kusema kwamba madaktari
poa, waendelee tu na mgomgo wao mbona wanasiasa wanakwiba mchana
kweupe?
Ninahakika rais mwanamke siyo tu ataimarisha huduma na afya tofauti na
viongozi wa sasa, bali ataiwezesha nchi kuwa na huduma za kisasa na
kukomesha kabisa nchi kupoteza mabilioni kwa ajili ya kwenda tibia
watu nchi za nje, kwani mahospitali ya hapa nyumbani nayo yatakuwa
yanatibu pia wagonjwa kutoka nchi za nje katika wakati wake.
Tahadhari: Ili kumpata kiongozi bora na atakayekuwa mfano kwa wanawake
na wanaume ni vizuri kuepuka wanawake wenye uchama kupindukia; wenye
tabia ya kuzomea na kukashifu wenye mitazamo tofauti; wapigaji
vigelegel ovyo na wale wanaobebwa sio kwa sababu ya akili na uwezo wao
bali kwa sababu ya jinsia yao. Aidha, huu si wakati wa kuwa na
viongozi wanaopenda kwenda nchi za nje wasikojifunza lolote la
kuibadili nchi yao, bali wakati wa kuwa na kiongozi anayependa kwenda
vijijini na kujifunza mbinu na mikakati ya kuufuta umaskini huko huko
vijijini, na wakati huohuo kuwatunuku wanavijiji utajiri na neema, na
hivyo nchi yetu nzima kuwa tajiri na ustawi wa hali ya juu zaidi
kimaisha.
Monday, February 20, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment