Tuesday, March 8, 2011

Mchungaji Ambilikile na Fursa ya Utalii wa Tiba Tanzania

KAMA Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile (76) angezuka kwenye nchi kama Italia au Spain au Bahama auBarbados au hata Kenya au Botswana au Afrika Kusini au Seychelles hapa Afrika, nadhani serikali katika nchi hizozingelijikusuru ndani ya muda mfupi tu kujenga mazingira ambayo yangeliwezesha tiba kuendelea na wananchi wa Kijiji cha Samunge, Sale, wilayani Ngorongoro kulala maskini na kuamka tajiri. Na wakati huo mkoa wa Arusha na nchi nzima kunufaika kiuchumi na kimatangazo duniani kwa bei sawa na bure.


Tunaposema serikali ijitoe katika kuendesha masuala ya uchumi hatuna maana ijiondoe pia hata katika ubunifu, kupanda mbegu, kustawisha na kukuza vitu kama hivi. Kufanya hivyo ninaamini ni makosa, tena makubwa sana. Na ni kuwatendea isivyo haki wananchi. Maana kama tunaweza kuwaachia watu wakachota fedha za EPA, lakini tunashindwa kutumia vijisenti vichache vya serikali kujenga miundombinu na kutoa huduma muhimu huko Samunge basi upo walakini mkubwa kiuongozi!


Inavyoelekea kama kawaida yetu sera na watendaji wetu serikalini hawana utambuzi wala hawajachangamka na kuitambua fursa ya
'mgeni aje mwenyeji apone.'


Kwa maneno mengine kama serikali ya mkoa wa Arusha na serikali kuu zikiweza kukisaidia kijiji hicho kwa hali na mali katika masuala muhimu ya miundo mbinu na huduma za dharura umaskini katika eneo hilo unaweza ukafutika ndani ya kipindi kisichozidi miezi mitatu.


Pengine kwa kuwa hao wanaotegemewa kuyafanya mambo hayo nao wamo katika misafara ya kuelekea huko huko Loliondo. Lakini ninaamini hata kama wasingelikwenda huko mambo yangelikuwa vivi hivi. Basi makala hii pia itumike kuwashtua angalau wale watakaokuwa na busara na hekima baada ya kwenda kuaguliwa huko warudi wanakorudi, wajipange na wafanye kile kinachohitjika ili baraka iliyojileta yenyewe isijegeuka baa au balaa ya mwaka.


Utalii kwa Watanzania walio wengi una maana ya kwenda kuona wanyama na vivutio vilivyozoeleka nchini. Lakini kuna utalii wa aina nyingi. Kuna utalii wa mambo ya kale au historia na kumbukumbu, utamaduni, michezo mbalimbali midodgo kwa mikubwa, mbio za magari, farasi,pikipiki na baiskeli, starehe, kamari, kuogelea na kulala ufukweni, kuwinda, kutembelea maeneo yenye maajabu nchini na mali asili.


Aina mpya za utalii zinazojitokeza sasa ni pamoja na utalii wa vijijini (watalii kuishi na kuwasaidia watu vijijini, jamii (wanajamii wenyewe kumiliki mahoteli, magari na biashara zingine za kitalii), elimu (wanafunzi na walimu kuja kuishi kwa muda nchini), utafiti na utoaji huduma maalum ikiwemo tiba asili, mbadala na ile ya miujiza.


Kwa yakini kila binadamu anachokifanya kikawa tofauti au adimu na nadra kuonekana kwingine huwa nacho ni kivutio cha utalii. Kwa maneno mengine, binadamu kutokana na akili aliyopewa na Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kutengeneza pia vivutio vipya vya utalii. Safari hii lakini Mwenyezi Mungu ameamua kukitengeneza mwenyewe kivutio kwa kupitia Mchungaji Ambilikile. HIvi dunia itatuona vipi kama tumepewa kivutio kama hiki halafu tukakosa akili na dhamira ya kunufaika nacho ?


Kilichotokea Arusha baada ya Mchungaji Ambilikile kuanza kuponesha watu kimiujiza ni fursa ambayo haijawahi tena kujitokeza Tanzania. Ni fursa ya papo kwa papo kujenga na kunufaika na utalii wa tiba inayotolewa kwa karama aliyopewa Mchungaji Ambikile.


Huko Ureno na Hispania ambako kuna mawaziri na watendaji wa sekta ya utalii ambao kila wakilala, wakila, wakiamka na wakitembea huwaza kitu kimoja tu-jinsi ya kupata fursa mpya za kukuza utalii nchini kwao, mambo haya yalishatokea na hivi leo maeneo husika ni mojawapo ya vivutio vikuu vya utalii katika nchi zao.


Kama tunavyochangamkia kutuma FFU wakati wa maandamano haya au yale, hii ilikuwa ni nafasi ya mwaka kutuma jeshi la wananchi na vikosi vya mangimeza kwenda kuhakikisha barabara zinatengenezwa; mahema yanawekwa; maboza ya maji yanapeleka maji kila kukichwa; mama ntilie wanapewa usafiri wa bure kwenda kuanzisha biashara ya muda; pia bidhaa na vifaa mbalimbali ambavyo wagonjwa watarajiwa na wageni wengine watakavyohitaji vinapelekwa ili kufanya biashara. Hili lingeweza kufanywa kwa ubia kati ya serikali ya mkoa na wananchi wa huko wakisaidiwa na serikali kuu na vyombo vyake.


Ukiona watu wako tayari kutumia vyombo vya dola kuharibu na kulemaza rasilimali muhimu kuliko zote katika nchi, yaani watu, badala ya kuvifanya vyombo hivyo kutoa mchango chanya katika maendeleo ya jamii na kiuchumi ni lazima ujiulize maswali mengi.


Na hata wale wenye uroho na uchu mkubwa wa vyeo na madaraka ambao wamo katika mkoa husika wanaposhindwa kuliona hili nao wakaingilia kuimba wimbo wa mbwa-mwitu, mbwa mwitu wa mchungaji wa Esopo badala ya ule wa Ambilikile jua hamna kitu hapo ndugu.


Wananchi wa Kijiji cha Samunge, kama Tanzania ingelikuwa na Benki na taasisi kama hizozinazoona mbali na mbele na zinazojali maendeelo ya kweli ya Watanzania wangelipewa mikopo chapuchapu kuongeza vyumba viwili-vitatu kwenye nyumba/viwanja vyao ili nao wanufaike kwa kupangisha vyumba hivyo kwa wageni na kutoa huduma za chakula na kadhalika.


Benki zingelisaidia pia upatikanaji wa maji, umeme na huduma mbalimbali zinazohitajika na watu wanaokwenda kutafuta tiba Semunge.


Tumewaona wanasiasa wakipeperushwa na helikopta huku na kule, lakini kwa kuwa tumeshakubali kuwa Watanzania wasiokuwa viongozi ni walaniwa wa kupanda mabasi yaendayo kwa fujo, treni mbovu na meli chakavu hakuna aliyewaza kuwa ujio wa Mchungaji Ambilikile nao unahitaji pia kuwe na kiwanja cha helikopta kama sio cha ndege karibu na pale anakotoa dawa. Kwa kuwa watu wamemuamini na wanapona nina hakika nauli ya kupanda helikopta kutoka Arusha hadi Semunge isingeliwashinda watu.


Lakini kinachotokea sasa ni kwamba kwa kuwa hakuna anayefikiria haya, basi jamaa zetu kama kawaida wametafuta njia ya mkato ma rahisi kama walivyozoea. Njia hiyo siyo nyingine, ila ni kuzuia wagonjwa wasielekeee Loliondo kwa muda.


Watu waliokata tamaa na ghafla kuwa na matumaini mapya ya kupona sasa wamewekwa njia panda. Wako njia panda kwa sababu wale wanaosimamia mambo yao wameshindwa kuitambua fursa hii ya kuwa na utalii wa Tiba huko Semunge, Ngorongoro.


Utalii ambao tukiuchangamkia mapato yake kwa sasa yakitoka mfukoni mwa Watanzania yangeweza kabisa kuzidi mara kadhaa mapato ya utalii yanayotokana na watalii kutoka nje hapo wilayaniNgorongoro.


Ni mambo kama haya yanaonesha tofauti kati ya serikali yenye watu wasiolala nawanaowaza saa zote juu ya maendeleo ya watu na serikali ambayo viongozi wake wamelala na wako madarakani kujishughulisha na uchungaji kondoo wa mali zao na wanapozinduliwa toka usingizini huanza kupiga mayowe ya mbwa mwitu, mbwa mwitu!


Ninaamini, huu ndio mwanzo. Wakenya, Waganda, Wanyarwanda, Warundi, Wakongomani, Wazambia na Wamalawi wako njiani. Isitoshe watu toka Uarabuni, Uchina, Ulaya na Marekani nao watakuja.


Kama tunakubaliana juu ya hilo hapo juu basi ni vyema watendaji wa serikali na hususan wanaobeba dhima ya kuujenga na kuuendeleza utalii nchini waamke. Wakishaamka, wahahe huku na huku kutafuta misaada toka kwa taasisi na watu husika ili kuona kama mawazo yangu ya Ki-Alinacha yanaweza kufanyiwa kazi.
Siwezi kushangaa kama ghafla nchi jirani zitaanza kuomba ruhusa ya kuingiza helikopta zenye wagonjwa Semunge. Hii itakuwa ni baraka na neema, lakini pia aibu ya mwaka kwa watendaji wetu nchini!


Na serikali inapashwa kuonesha njia katika hili. Vinginevyo itajikuta inapiga ngoma isiyo na wachezaji, maana watu wote wanakimbilia kwa manju wapya!

No comments:

Post a Comment