Saturday, June 11, 2011

Tofauti kati ya Uchumi-nchi na Uchumi-mtu

KUNA msemo ambao hudhalilisha sana matumizi ya takwimu katika taarifa mbalimbali unaosema kuna aina tatu za uongo (Ona kitabu cha Lies, Damn Lies and Statistics). Kuna uongo wa kawaida, halafu kuna uongo mweupeee na uongo wa tatu unaitwa TAKWIMU !

Katika kitabu hicho mwandishi anajaribu kuoensha kwamba uongo ulio mbaya na wa hatari zaidi ni takwimu kwa sababu wanaoziandaa takwimu huziandaa aghalabu kupotosha ukweli ulivyo; wanaozitangaza takwimu wanajua wanasema uongo lakini wanaamini katika uongo huo na wanaosikia uongo huo hawajui waamini lipi kati ya takwimu kadhaa zinazokuja kivyakevyake kila moja ikiwa na ajenda yake ya siri.

Uchumi-nchi ( Macroeconomics ) na uchumi-mtu ( Microeconomics) vyote huwasilishwa kinadharia katika takwimu zinazohusiana na maeneo husika. Mara nyingi sio rahisi kuchukua takwimu na hesabu za kila eneo kwa hiyo wakati mwingine watu huchagua kati ya maeneo kadhaa na kuwasilisha kile wanachoamini kinazungumza kwa faida ya wengine wote.

Ndio maana leo kuna Watanzania wanaoshindwa kuelewa na wanaoshangaa kwanini wakati nchi inaendelea kwa kasi kubwakutokana na takwimu zinazoonesha kuwa eti pato la Mtanzania sasa ni zaidi ya dola 500 kwa mwaka na kuwa pato la taifa linakuwa kwa asilimia sita kama sio zaidi ya hapo kuna Watanzania wasioliona hili na kulisifia na kuwasifia viongozi wao.

Ukiwauliza wataalamu wa uchumi kama sijakosea tatizo hili linaletwa na viongozi wetu kujikita zaidi katika masuala ya uchumi-nchi na kujisahau au kuwaachia wababaishaji kusimamia masuala ya uchumi-mtu.

Kwa tafsiri uchumi-nchi ni uchumi-jumla wa nchi ambao daima hutoa picha kubwa kiuchumi kwa nchi na hauangazii tu hali ya kiuchumi ya mtu mmoja mmoja. Japo chumi hizi mbili zinategemeana, zinaingiliana na kuoana sana lakini kila moja ina nafasi na wajibu wake katika jamii husika. Kwa upande mmoja, maendeleo ya nchi kiujumla huwa kivutio kwa wawekezaji, wabia wa kibiashara na kiuchumi na watalii na watu kama hao, wakati hilo halimpi sababu mwananchi mjini au kijijini kufarajika kwa sababu anaweza awe ananufaika na uchumi-nchi au kinyume cha hivyo.

Hali ilivyo kwa Tanzania ni asilimia ndogo sana ya Watanzania ndio wanaonufaika na takwimu na hali halisi ya uchumi-nchi . Hawa wanaonufaika ni pamoja na viongozi wa nchi wanaolipwa mishahara na marupurupu mazuri na wakati mwingine hawalipi kodi mbalimbali; wawekezaji na wafanyabiashara na wenye viwanda wanaoweza kuwabebesha walaji gharama zinazoongezeka katika biashara au viwanda vyao na hivyo kubakia pale pale kiuchumi hata kama mfumuko wa bei na gharama mbalimbali zimezidi kuongezeka mno katika kipindi kilichopita.

Wengine wanaonufaika na uchumi-nchi katika hali ambayo bei na mfumuko wa bei vimekuwa vikikuwa siku hadi siku ni wale waliomo katika mashirika ya kimatiafa, mashirika ya kiserikali na walanguzi wa kila aina na ukubwa.

Kwa hiyo uchumi-nchi unaoweza kuwa umekua au unakua lakini faida yote inaenda kwa wale wanaolipwa mishahara na marupurupu na posho nene, wawekezaji, wafanyabiashara, wenye viwanda, makampuni makubwa ya kitalii, waagizaji mafuta na peteroli, wenye viwanda, wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa, wafuasi wa chama kinachotawala na watu kama hao tu na sio kwa Mtanzania wa kawaida.

Katika hali kama hii nchi inakuwa kama timu ambayo wachezaji fulani kwa kuitwa wachezaji nyota basi wanalipwa mamilioni ya fedha huku wachezaji wenzao wakipata chini ya nusu ya kile wenzao wanachokipata. Kimya kimya wachezaji walio wengi (asilimia 90) wanaamua kuwaachia wachezaji wanaolipwa vizuri sana ndani ya timu wacheze wenyewe na timu ishinde. Eti timu inaachiwa kucheza bila kucheza kama timu. Wote kwa kuitazama Real Madrid na Chelsea tunajua ni kitu gani kitakachotokea.

Ili nchi kama timu ishinde inahitaji zaidi ya viwango vya kukua uchumi, wawekezaji, mipango na bajeti za serikali. Nchi inahitaji kwanza, watu waamini kwamba wamo katika safari moja na sio kila mtu ana safari yake. Pili, lazima tuwe na visheni moja ya kule tuendako sio kila mtu awe na dira au ndoto binafsi ya kule anakotaka kwenda. Tatu, lazima tujenge uchumi wetu kama timu moja, kama kitu kimoja na sio kinyume cha hiyvo. Nne, lazima akilini mwetu sote tuwe na picha ya kile tunachotaka kukijenga kama vile mfano wa nyumba inayotakiwa kujengwa. Na mwisho lakini sio jambo dogo akili zetu ziione nchi nzima, mikoa, wilaya, tarafa, kata, miji, vijiji na mitaa kama MFUMO MMMOJA mkubwa ulio na mifumo kadhaa midogo midogo nayo yote ikiingiliana kila wakati na kwamba mfumo mdogo mmoja mdogo ukiwa na tatizo basi mifumo mingine yote midogo na huo mkubwa utakuwa katika matatizo pia. Na mfumo huo mkubwa itambulike pia ni sehemu ya mfumo mkubwa kabisa wa dunia na ulimwengu kiujumla ambao kwa sasa watambulika kama utandawazi. Nasi tukiwa na jukumu la kujipanga kwa namna ambayo kwayo tunanufaika badala ya kuathirika vibaya na huo utandawazi.

Tumewahi kuzungumzia huko nyuma kuwa mahitaji muhimu ya binadamu ni pamoja na maji, chakula, mahitaji ya kijamii, mavazi, makazi/nyumba, afya na tiba, elimu na usalama wa watu na mali zao. Vitu hivi ndivyo vinavyostahili kutumika kama kigezo cha kuamua uchumi umekua au haujakua katika medani ya uchumi-mtu na wala sio takwimu za aina nyingine.

Tuwaulize wanauchumi wetu kama Tanzania ya mwaka jana wa bejeti walikuwa na hali bora zaidi au mbaya zaidi katika suala la upatikanaji maji, chakula,mahiraji ya kijamii kama huduma mbalimbali za usafiri ikiwemo wa daladala, usafi na umeme ? Majibu ya hili pengine yatawafungua macho waliofunga macho na walio katika usingizi wa kuridhika na kutosheka na hali kama ilivyo.

Je, wanauchumi wetu walio huru nchini wanasema kwamba Watanzania wameacha kuvaa mitumba kama Mwinyi na Mkapa walivyotuacha au bado tunaendea na mtumba.

Je, hivi leo ni rahisi kujenga na kumiliki nyumba kama ilivyokuwa mwaka jana au hali imezidi kuwa mbaya zaidi. Jibu kwa hili nalo litatuonesha kama tuna sababu ya kukenua meno au ya kufunga vinywa kwa hasira ya ukata na kutokuridhika.

Wanauchumi wetu waambaje katika masuala ya afya na tiba na kama shida na dhiki za kina mama na watoto na wagonjwa wengine katika mahospitali yetu zimeisha au bado zinaendelea. Ziada ya ndogondogo ikiwa je, wale mbu wa Muhimbili wametushinda au tumewadhinda ? Kama mbu hao wametushinda nina mashaka kama tumepiga hatua yoyote mbele ya maana na inayoonekana.

Hali hii ya kuutazama uchumi kutoka juu na kushindwa kuutazama toka chini utaendelea kujenga msimamo na mtazamo wa wale walioko madarakani kujijali zaidi wao wenyewe kwanza na wale wanaowaweka madarakani na kamwe 'haiwezekani' wao kuwa na mipango na sera zinazotoka chini kwenda juu, yaani, kumneemesha kwanza mnyonge kisha ndio vigogo na vizito waneemeke zaidi ya walivyoneemeka. Na hiki ndio chanzo cha wao kuona kwa miwani yenye lensi kubwa uchumi-nchi na kutazamia uchumi-mtu kwa miwani yenye lensi ndogo.

Isitoshe uchumi wowote unaojengwa kwa kutegemea zaidi rasilimali na uwekezaji nyonyaji-sana toka nje hauwezi kamwe kuleta maendeleo linganifu ya uchumi-nchi na uchumi-mtu. Na hili benki ya dunia na IMF wameliona na wanalitambua na ndio maana wanaishauri serikali kupitia upya mikataba na wawekezaji katika sekta ya madini na migodi.

Aidha, nchi inayoshindwa kucheza na kuoanisha mahesabu na takwimu kwa nadharia na vitendo katika masuala ya pande-toaji/ugavi (supply) na pande-mahitaji (demand) katika ngazi ya uchumi-mtu haiwezi kamwe kuwa na maendeleo endelevu na ambayo huwa nadra kuguswa vibaya au kuathirika na kile kinachotokea ndani na nje ya nchi. Hili kama alivyosema Shaaban Robert linahitaji KIASI. Vigogo na vizito wakpata zaidi ya KIASI na walalahoi wakikosa chini ya KIASI basi inakuwa muhali na vigumu sana kujenga pia mtaji wa kijamii ambao hutegemea watu na sio fedha katika nchi husika.

Tunafanya kosa kubwa sana kiuchumi na hususan kibajeti kwa kukosa kuwa na mipango na mikakati adhimu ya kulifanya soko la ndani lifanye kazi kubwa linaloweza kuifanya kwa kujishughulisha zaidi na soko la nje, tena kwa upande wa manunuzi ya vitu vya anasa kwa sana.

Katika kipindi tulichomo na hali tuliyo nayo kiuchumi tulitakiwa tutumie muda mkubwa zaidi na fedha nyingi zaidi za kukuza uchumi-mtu kwanza na sio vinginevyo. Bajeti ya hivi majuzi haioneshi kuwa rafiki wa Malengo ya Milenia (MDGs) ukitazama mgawo wa bajeti ulivyokwenda. Na wala hakuna panapoonesha ni kwa namna na njia gani Tanzania katika kipindi cha bajeti kijacho itajitahidi kuhakikisha wananchi wake wanapata angalau sehemu ya kuridhisha ya mahitaji yao ya msingi. Pengine kwa viongozi kuamini kuwa kwa kuwa uchumi-nchi unakuwa basi watu wana fedha tele mifukoni mwao, kitu ambacho si kweli.

1 comment:

  1. Naam, hivi kweli kumbe Uchumi unaweza ukaelezwa kwa ufasaha namna hii katika lugha yetu tamu ya Kiswahili? Je, bwana kama huyu hawezi kupewa msaada na serikali yetu ili atuandikie kitabu cha uchumi kwa kiswahili fasaha kama hivi ? Au wabugne wetu wamezoea tu kutetea posho yao lakini sio kuwasaidia wananchi wengine wenye mchango pengine mkubwa kuliko wao katika maisha ya Watanzania walio wengi?

    ReplyDelete