Friday, July 6, 2012

Demokrasia ni ufuataji sheria, utu, haki na usawa



TUKIO la kutekwa na kukomolewa kwa kipigo kikali, kiongozi wa chama cha madaktari nchini,  Daktari Steven Ulimboka, limezua mtafaruku mkubwa miongoni mwa wananchi nchini na hata kwenye safu za madaktari kimataifa. Pamoja na baadhi yetu kukerwa na hatua za madaktari wetu kuigomea serikali, wananchi wengi wamekerwa na kuhuzunishwa na kiteno hicho cha kinyama. Wengi wanaamini, huko siko sisi kama nchi ya kidemokrasia inayojali haki za binadamu na utawala wa kisheria, tunakostahili kuelekea.
    Binafsi, ninaamini kuna hatari kubwa sana kwa nchi na watu wake kuuachia mmea huu kuota na kustawi hapa nchini. Mmea huu sio mwingine ila ule wa wa mtu au kikundi cha watu kujichukulika sheria mikononi mwaka. Tuemyaona Kenya na tunajua Kenya kwa namna gani imo katika matatizo makubwa kutokana na watu wa nanmna hiyo.
    Kwa maoni yangu sisi kama nchi na taifa tunaweza kuchezea vitu vyote vingine lakini tusichezee maisha ya watu wetu, demokrasia, sheria, mali asili, mazingira, maji, hewa, chakula, ardhi, haki na usawa.
    Kwa faida ya wale ambao hadi wa leo wanadhani Tanzania sio nchi inayofuata na kujali demokrasia, kwanza, na pili wale wanaodhani kwamba wanaweza kuturejesha kwenye mfumo wa chama kimoja na udikteta, ninawakumbusha wapitie upya katiba ya sasa ya nchi na wapate maoni ya  vijana nchini hivi leo kutambua kwamba Watanzania hawako tayari tena kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja na udikteta.
    Ni jambo la kusikitisha kwamba wakati vyombo vya dola vikiwemo vile vya usalama kule Uchina vilikuwa vikitoa mchango wao katika ulinzi na uendelezaji miradi ya mashamba makubwa ya ufugaji kuku (zaidi ya milioni 3 kila shamba) ambayo yaanazalisha sio tu mamilioni ya mayai kila siku, bali pia huwa yanazalisha umeme na mbolea ya kutosha miji na mashamba husika na kadhalika, huku kwetu watu wetu walikuwa wakiweweseka kwa kuona sinema ya kutekwa nyara na kuumizwa mtu asiye na silaha wala asiye na ugomvi binafsi na wahusika.
    Kwa tafsiri nyepesi demokrasia ni utawala wa watu, kwa ajili ya watu na na unaosimamiwa na watu wenyewe. Haijawahi kusemekana kwamba demokrasia ni utawala wa kinyama kwa ajili ya wanyama na unaosimamiwa na wanyama wenyewe.
    Kwa hiyo pale wanapotokea watu wakawafanyia unyama  watu wengine katika jamii husika hatudhani hapo kuna demokrasia ya kweli. Kuna walakini mkubwa hapo na pengine mamlaka iliyopo kwa namna moja au nyingine  wanaweza wakawa wanahusika sio lazima kama serikali lakini kutokana na nafasi ya mtu na mtu huyo kujiweka juu ya sheria na katiba ya nchi kwa matashi yake. Ndio wenye  jambo au kitu cha kulinda tusichokijua, na sio mtu mwingine.
    Ukimya wa serikali katika hili unaongeza wasiwasi na tuhuma kama hizo, kama Profesa E. Lwaitama katika kipindi chake cha Hoja ya Lwaitama, alivyozungumza, upo uwezekano kwa serikali kutohusika moja kwa moja, na kwamba ni watu wachache walioamua kufanya walilolifanya wakidhania wanaifanyia nchi fadhila, na kumbe sivyo bali ni kinyume cha makusudio yao.
    Utawala wa kisheria nao una maana kwamba kati yetu sote kama raia wa nchi fulani hakuna anayestahili au sababu yoyote ya kuwa juu ya sheria na wengine wakawa chini ya sheria za nchi hiyo hiyo.  Aisha, haiwezekani kuwa na watu ambao kwa sababu hii au ile wanaweza kuvunja sheria, wakamteka mtu, kumpiga na kumtelekeza kama maiti porini tukahesabu kuwa tuna utawala wa kisheria. Sembuse demokrasia ?
    Kwa maneno mengine, usawa ni sehemu muhimu ya utawala wa kisheria. Na pale unapoona kuwa kama ilivyotokea katika Shamba la Wanyama la George Orwell, pakazuka watu au wanayama wanaojiona wana haki zaidi kuliko wenzao basi ndio unakuwa mwanzo wa matatizo yasiyokwisha katika taifa lolote lile.
    Utu kama sehemu ya demokrasia unajidhirisha kwa watu wanaotofautiana kimawazo na kifikira kutotumia mabavu au njia za kuumizana, kutiana ulemavu au kuuana ili kumaliza tofauti zao. Demokrasia si mabavu, si maguvu na wala si utumiaji wa mashaka wa vyombo vya dola.         Demokrasia ni kuzungumza au kuteta na kumaliza tofauti kati ya mtu na mtu, au kati ya makundi ya watu kwa mazungumzo mezani yenye hoja na ushawishi yakini na sio kwenye viwanja vya vita au misitu ya Pande.
    Utu vilevile, ni muono nje ya lensi nene au zenye giza kuhusu vitu vidogovidogo vinavyojidhirisha kama toauti kati ya watu na ambavyo havistahili kuwepo kama vigezo vya haki na sthaili kamilifu vinaangaziwa. Kwa maneno mengine, ni utu pia kuona kwamba katika kudai haki zetu, hakuna anayesimama katikati ili zisipatikane na vilevile na sisi wenyewe hatuwanyimi kwa ila bila sababu za kutosha haki wengine wanazostahili.
    Haki ya mtu na usalama wake ni sehemu muhimu ya katiba yetu. Na mtu hawezi kulazimishwa atoe haki, wakati yeye kwa upande wake naye anaona hatendewi haki au haki zake hakuna anayezijali.
    Mazingira yaliyosababisha kutekwa nyara na kuumizwa vibaya kiongozi wa  Madaktari Tanzania, Ndugu Steven Ulimboka kumetafisiwa kwa namna mbalimbali na watu mbalimbali na kuacha maswali makubwa kuhusu azma ya serikali kuwapeleka madaktari mahakamani na tukio hilo. Ikifikia wakati madaktari hawaiamini serikali, na serikali haiwaamini madaktari, sijui tutakuwa tunelekea wapi kama nchi na taifa. Mungu aepushie mbali.
    Kuna baadhi ya watu wanaoamini vilevile kwamba jambo hili linaweza kuhusishwa na vyama vya kisiasa na uwezekano wa matumizi ya makundi ya kibabe na kihuni yasiyo hata na itikadi kama wale wa Kenya. Ni dhahiri vidole vya Watanzania havitakoswa pa kuelekeza na ni muhimu sana serikali na wanasiasa wetu wakajisafisha kwa sabuni na dawa muhimu ili tuone kuwa kweli ni wasafi na sio tu wanajikosha.
    Wabunge na wanasiasa wengine katika miaka hii sio haki kabisa kulipwa kuliko watu wengine ila  kama na wao pia wana elimu na wasifu sawa na hao wengine.  Hii ina maana mbunge au waziri  au rais daktari mshahara wake utakuwa mkubwa kwa sababu hiyo; na  mbunge au waziri aliyemaliza shahada ya kwanza, mshahara wake hautapishana na wenzake kwenye tasnia mbalimbali. Lakini kubwa zaidi likiwa ni kuoanisha uzalishaji au utoaji huduma wake na kile anacholipwa na umma. Tofauti hii ya kipato inaleta dharau, jeuri na kiburi kisicho cha maana kwa wengine. Mtu anajivuna kitu gani, kama anajifaa mwenyewe na hana manufaa kwa wengine? Na iweje vyombo vya dola na usalama kujivunia kulinda wachache vikashindwa kuwalinda wengi ? Huu si uchochezi wala sio ukorofi bali ni mambo ya kuyaweka wazi na bayana ili kama kuna tulichokizoea kutokana na kawaida, basi kawaida isigeuke sheria mwaka nenda, mwaka rudi. Mabadiliko hayaepukiki katika jamii yetu hivi leo. Na wakati mwingine ni wa juu kukubali kujirudisha chini, ili kuwaridhisha wa chini.
    Jambo hili litasaidia kwa kiasi kikubwa na viongozi wanaojali kujiendeleza, kujikamilisha na kujikuza kwa kila hali ili wasiachwe na wakati wakajikuta wanakuwa ni viongozi wa kupiga vigelegele au kuzomea katika nchi inayohitaji watu wenye akili zinazochaji na kuzua mapya ili nchi iondokane na umaskini, ujinga na maradhi na sio kusinziasinzia. Huu ni wakati wa ushindani na kuchangamshana kitu ambacho wanasiasa wa zamani hawakukizoea, lakini watapaswa kujifunza.
    Uoga wa migomo, maandamano, mikutano, majadiliano na mikusanyiko ya watu katika enzi za demokrasia ni kitu kilichopitwa na wakati. Maana ukweli ni kuwa demokrasia haiwezi kamwe kujengwa bila ya kuwepo kwa vitu hivi. Nchi hustawi katika migongano na misuguano. Mradi haki inatendeka nchi huendelea. Haijawa na haitakuwa nchi kuendelea pasipo migogoro, migomo na misuguano. Na yote hufanyika bila mauaji haramu.
    Ni hasara kuwa na viongozi wanaoididimiza nchi na watu wake, halafu viongozi hao bado wakalipwa mishahara mikubwa ukilinganisha na watumishi wengine wa umma wanaostahili kulipwa kwa haki na  vizuri zaidi.
    Tuazimie kwa faida ya nchi na bila uchama kuhakikisha mmea huu ambao baadhi yetu wanajaribu kuupanda, yaani, mmea wa mauaji ya kisiasa au tofauti za kimsimamo na dhidi ya haki za binadamu, tunaung'oa mara moja bila kuchelewa. Maana kama hautaleta balaa upande huu, basi utakuja leta balaa upande ule.
    Turudi nyuma kidogo na kuwakumbuka Tom Mboya, Joseph Kariuki na Robert Ouko na pengine George Saitoti na wanasheria kadhaa wa huko Kenya na wengine kama wao ambao waliuawa kikatili kutokana tu na watu fulani kuwaona ni hatari kwa malengo yao ya kisiasa enzi za Kenyatta na Moi.
    Taifa lolote linapokubali mtu au chombo chochote cha kitaifa kikawa ni mali ya mtu au kikundi kimoja, kinaweka rehani amani na umoja wa nchi. Katika katiba mpya tuhakikishe kwamba haturuhusu vyombo hivi kuwa vya mtu au kikundi cha watu na kinakuwa chini ya kamati au timu ya kitaifa yenye uwakilishi mpana unaoruhusu udhibiti na ufuatiliaji wa katibu katika majukumu yake.
Serikali katika nchi yoyote ni kikundi cha watu wachache wanaopewa dhamana ya kuongoza na kulilinda taifa lakini si kutekeleza matakwa yao binafsi. Hilo likifanyika ni kosa. Na serikali kama hiyo inawajibika kujiuzulu.
    Katika nchi ya kidemokrasia ya kweli na yenye viongozi wanaofahamu umuhimu wa kuwajibika hadi hivi leo kuna safu za viongozi kadhaa ambao wangelikwisha kutangaza kuwajibika kwao kutokana na kitendo alichofanyiwa mwenzetu Ulimboka.
    Kilichotokea kwa Daktari  Ulimboka ni ushahidi tosha kwamba demokrasia yetu bado ni changa, haijakuwa, si wazi, haiwajibishi watu na viongozi hawawajibiki bado sababu ya kutegemea chombo au mtu fulani na pengine ina zaidi ya serikali moja zinaoenda sambamba nchini kwa wakati mmoja bila yoyote kujua serikali nyingine inafanya kitu gani. Kama hili ni kweli huo ni udhaifu mkubwa wa kisiasa, kiuongozi na kiutawala. Aidha ni kielelezo kwamba wapo baadhi yetu wapo tayari kugeuzwa au kujigeuza kuwa wanyama na mamluki kwa sababu tu ya njaa zetu na tofauti zetu za kisiasa na utumwa wetu kwa wlalio madarakani, kijamii na kiuendeshaji nchi jambo ambalo halikubaliki katika nchi inayofuata utawala wa kisheria. Maana watu kama  hao wanafanya hivyo kwa kujua kuna mkono utakaowalinda. Hali kadhalika huu ni wakati muhimu kuwakumbusha viongozi wetu na wananchi kwa ujumla nchini kwamba haki na usawa ni nguzo muhimu ya kidemokrasia na jamii ya kistaarabu. Tusikubali kuwa na nchi ambayo kuna watu kati yetu wenye haki na usawa zaidi mbele  ya katiba yetu iliyopo na itakayokuja na sheria zote za nchi. Katika jambo la uvunjaji haki za binadamu pasiwepo kabisa atakayekuwa juu ya sheria ikiwemo hata rais na mawaziri wake.
    Binafsi ninaiombea nchi yetu iwe inastawi katika kutofautiana kisiasa na kiuelewa, migogoro, migomo, maandamano na mikutano ambayo inawafungua viongozi na wananchi macho na sote tukabadilika kwa faida ya nchi yetu na watu wake. Nchi isiyokuwa na migogoro na misiguano huwa sawa  na  nusu mfu, na sio rahisi kuendelea. Ili mradi tu migogoro na misuguano hiyo isiishie kwenye kutoana roho kusikomsaidia yeyote kati yetu.

<<<<<<ends>>>>>>

No comments:

Post a Comment