Sunday, January 5, 2014
Rai kwa rasimu ya pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwanza, ninapoingeza Tume ya Warioba (Rasimu ya Katiba ya JMT) kwa kazi yao nzuri ambayo kila mtu ameiona na wakati huohuo kuwarai Watanzania wenzangu kumuenzi kiongozi huyu na timu yake, sasa na siku zijazo na kuhakikisha wanakuwepo kitwasira katika sebule kuu za taifa letu kwa ajili ya kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.
Kazi iliyobakia kwetu sisi wananchi ninaamini ni kama kung'arisha kitu ambacho utengenezaji wake umeshakamailika na imebakia tu mambo tudogotudogo hapa na pale kuikamilisha.
Katika makala haya nitaangazia mambo machache tu ambayo kwa uoni wangu wa haraka haraka nadhani yanahitaji kuangaliwa kwa undani zaidi wakati wa mikutano ya Bunge la Kuboresha Rasimu ya Katiba mpya.
Mapato yatakayotokana na gesi, petroli na madini yetu ni lazima yaelekezwe kwenye elimu. Sioni ibara ifuatayo kwanini isisomeke kama ifuatavyo, yaani kifungu
42. (b) kingelisomeka kama: "kupata elimu bora ya msingi na sekondari.....yaani.
Kuhusu Haki ya elimu lazima itangaze pia kwamba pamoja na yaliyomo hivi sasa ni
haki kwa taasisi yoyote ile inayotoa elimu kutoa elimu yoyote ile kwa lugha mwenye au wenye taasisi na walengwa wanayoitaka; katika kujenga usawa kati ya mikoa, kila mkoa utakuwa na angalau chuo kimoja kikuu cha umma; na kwamba elimu toka chekechea hadi sekondari itatolewa kwa gharama za pato la taifa hususan kutokana na utajiri weu wa madini na mali asili kwa faida ya wengi; na kwamba elimu itakayotolewa italenga siku zote kuwawezesha vijana wa nchi kutatua matatizo ya nchi na watu wao na hivyo kukuza ajira kwa kuboresha maisha ya waliio wengi.
Pamoja nayaliyomo katika ibara ya 44 ingelifaa yaongezwe pia kwamba ni jukumu la serikali kuu kuwajengea vijana mazingira ya kujiajiri wenyewe kwa kujifunza kuwa wabunifu, wavumbuzi na kujiingiza katika ujasiriamali na taifa kwa kutumia hazina yake itawajengea mazingira ya kuweza kukopeshwa na kupata nyenzo nyenginezo za kuwasaidia kujiajiri na kujitegemea....lengo likiwa ni kupunguza idadi ya mashine, magari na mitambo tunayonunua toka nje kwa sisi wenyewe kuvitengeneza hapa hapa nchini baadhi ya vitu hivyo.
Tunaijua hali ya nchi yetu na mapungufu yake, je, Tunu za kitaifa zilizoanishwa zinatutosha au ingelifaa pia tuongeze tunu nyengine kama:
utamaduni, mila na desturi chanya mbalimbali na usasaishaji wake;
ukweli; uaminifu; usafi; ubunifu na uvumbuzi na udhibiti kamilifu na bora wa majukumu na kazi kubwa kwa ndogo nchini.
Nina wasiwasi pia kama sifa anazostahili kuwa nazo mtu anayestahili kugombea urais kama zimeainishwa katika rasimu hii. Labda zimefutika kwenye nakala yangu, maana ukweli sikuziona. Je, tutapata kiongozi bora kama rais wa muungano bila ya kujua tunahitaji mtu wa aina au namna gani?
Ibara ya 32 inayozungumzia uhuru wa imani ya dini kwa baadhi ya watu inaonekana kuning'inia. Baadhi ya maswali yanayoulizwa ni je inajitosheleza bila kuzungumzia masuala kama: hakuna taasisi au chombo chochote kitakachopewa na katiba au sheria chini ya katiba hii ukiritimba juu waumini wa imani au dini yoyote ile iwayo; viongozi wa ksiasa na kiserikali hawataruhusiwa kwa namna yoyote ile kuwachagulia waumini viongozi wao; kwa imani zinazopenda serikali na wafadhili watasaidia kuwajengea waumini miundo na mifumo ya kuendesha mambo yao ili kuendana na wakati; serikali na wahisani wa ndani na nje wanastahili kusaidia kila imani kukamilisha masuala yao ya ibada kwa kuwa na taasisi na watu wanaochangia ukamilikaji wa ibada zao; na kwamba sio tu haitaonekana bali haitakubalika kwa kikundi chochote katika jamii kuishawishi serikali kuinyima imani fulani ya kidni kuwa na mifumo, miundo na rasilimali watu muhimu wanaohitajika kukamilisha imani yake.
Wale wanaosema kwamba suala la Mahakama ya Kadhi, mathalani, sio la muungano ni muhimu wafafanue kama katiba ya muungano ni katiba mama, au ni katiba za Tanganyika na Zanzibar ndio katiba mama?
Ni dhahiri kutokana na miaka mingi ya utawala wa mfumo wa chama kimoja, muda unahitajika pia kuwabadili kimawazo na kivitendo baadhi ya watendaji watakaokuwa wamezoea kuwa watumishi wa umma na wakati huo watumishi wa chama cha kisiasa....
Kwa yale mambo ambayo yanayonekana yanaweza kuwa chanzo cha kutokuelewana miongoni mwetu, fujo au ghasia au kusababisha 'tokomeza' nyingine kama yasiporekebishwa sasa hivi, ni vyema yaanze mara moja....
Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, bunge letu kwa kushirikiana na mabunge mengine ya Afrika Mashariki yatatunga sheria moja ili kuoanisha mitazamo yetu na kuvipa vyombo vya habari kutimiza wajibu wake kwa jamii zetu bila mikwaruzano na serikali isiyo ya lazima.
Kiujumla kuna vifungu kadhaa katika rasimu hiyo ambavyo kwa faida za baadaye za kisheria ni muhimu kupanuliwa zaidi ili kile kinacholengwa hatimaye kipatikane kiurahisi bila shida kwa walengwa wa katiba hii mpya.
Vifungu vingi vinavyohsu mamlaka, haki na wajibu wa wananchi na wale watakaowatawala ni lazima vifafanuliwe zaidi ili kuondokana na kosa kubwa linalotokea kwenye katiba yoyote mpya, nalo sio lingine ila lile la kuzusha migongano inayokuja kuleta ukinzani mgumu mbele ya mahakama panapokuja kuzuka tatizo ambalo misingi yake haikufafanuliwa ipasavyo.
Ingawa Tume ya Jaji Warioba imependekeza pawe na miaka minne hivi ya mpito, kwa upande wangu ninaona ingelifaa yale yanayowezekana kufanyika leo leo, yafanyike, na yale ambayo kwa namna fulani yanastahili kufanyiwa kazi zaidi ndiyo yacheleweshwe.
Rasimu imekaa kimya pia juu ya suala la madaraka mikoani au mikoa iliyo huru kiuchumi na haja ya kupunguza utititri wa wakuu wa wilaya nchini. NInaamini wajumbe wa bunge la katiba wataendelea kulishughulikia ili kupata muafaka wenye manufaa kwa Watanzania.
Je, ni muhimu Uchaguzi Mkuu ujao ufanyike 2015. NInadhani sio lazima. Kama nikiruhusiwa, ningelipendekeza kwamba Rais Jakaya Kikwete angeongezewa miaka miwili 2005-2007 ambacho kitaitwa kipindi cha mpito cha kukamilisha kazi ya katiba iliyosalia. Katika muda huu pengine Mheshimiwa Kikwete atambulike kama Rais wa muda wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kazi yake kubwa itakuwa kuzisaidia Tanganyika na Zanzibar kama nchi mbili katika muungano mpya kupata viongozi wanaofaa. Kwa maoni yangu Uchaguzi Mkuu wa Tanganyika, Zanzibar na ule wa Muungano wa Tanzania ungestahili kufanyika Januari 2007. Na kuanzia hapo mwaka wetuu wa kifedha ubadilishwe pia na kuanzia Januari na kuishia Disemba ili kupunguza matatizo yanayoendana na mwaka wa kifedha tunaotumia kwa hivi sasa.
Tutakachokikosa hapa zaidi ni kutokuwa na chaguzi zinazofanyika kwa miaka inayoishia 0 au 5.
Wengi waliofanya haraka ya kutaka kuikamilisha katiba na wakati huoo kuendesha uchaguzi mkuu kwingineko Afrika wamejikuta na matatizo mengi kuliiko walivyotegemea.
Ninaamini kama pendekezo langu litakubalika basi Tanzania itapata muda wa kutosha kufanya maandalizi na marekebisho muhimu yatakayozisaidia nchi zetu mbili na serikali ya muungano kuanza vizuri na kuepuka shinikizo na songombingo zisizo za lazima.
NI dhahiri kama teuzi kadhaa za watu muhimu; na kwamba mawaziri hawatatokana tena na wabunge; na kwamba kutakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na wagombea huru kwa nafasi mbalimbali ni jambo litakalohitaji muda wa kutosha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment