Friday, August 23, 2013

Reli ya Tanga- Taveta - Arusha igeuzwe Chuo Kikuu cha Ujenzi wa Reli nchini...

HOJA yangu binafsi leo ni kwamba Tanzania baada ya miaka hamsini ya uhuru haina sababu ya kutegemea nchi nyingine duniani katika ujenzi wa baadhi ya miundombinu yake na uwepo wa viwanda vinavozalisha mitambo na mashine muhimu katika maendeleo yake ya kiuchumi na kijamii na ujenzi wa nchi kwa ujumla. Vijana wengi niliowauliza walimaka: ' Na kufuatia uamuzi wa Kenya kujenga upya reli yake kati ya Mombsa na Malabo kwa msaada wa Wachina, huku Rwanda na Burundi nazo kupitisha mizigo yake kupitia Kenya, upo uwezekano mkubwa wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo kuwa ghalibure na hasara na mzigo usiobebeka kwa kizazi kijacho. Itakuwa ni busara na hekima kutumia njia mbadala za ujenzi wa reli zetu nchini na badala ya kuviongezea vizazi vijanvyo mzigo wa madeni kuvipunguzia zigo hilo ogepewa. Badala ya kuzungumzia serikali mbili, haya ndiyo mambo ambayo vijana wa Tanzania kuonesha wako mbele ya vijana wengine wa Kiafrika walikuwa wanapaswa kuzungumzia. Na sio kuzungumzia mikakati ya kuua kabisa matumaini ya umoja wa Afrika ili kuzima kiu na kushibisha njaa ya leo. Ujenzi wa reli kwa akili zetu wenyewe na rasilimali zetu wenyewe sio tu utaondosha baadhi ya matatizo yetu bali utawapa vijana wa nchi hii kuwa wajenzi wa reli waanzilishi hapa Afrika. Ili tuwe nchi bora na nchi mali lazima viongozi na wananchi wetu tuone mbali kuliko jirani wanaotuzunguka. Tunacheleweshwa mno!' Na kwamba uwekezaji mkubwa unaostahili kufanywa na nchi inayotaka kuendelea kikweli kweli ni katika vijana wake na sio tu ardhi , migodi na viwanda. Katika miaka hamsini ya mwanzo kutokana na kukosa watu waliosoma, shule na vyuo stahilifu, raia wanaojijua na sababu ya kuwepo kwao, wajasirimali, vijana wabunifu, mitaji, masoko, teknolojia muafaka na mitandao ya kusaidiana kufanikisha azma fulani palikuwa hapana njia ila kuvumilia tu kutegemea watu wengine watujengee nchi yetu huku sisi wenyewe tukijifunza. Hoja yangu inapewa nguvu na makali na ukweli kwamba tumeshajifunza kiasi cha kutosha sasa; tuna shule na vyuo stahilifu; na wapo wasomi nje na ndani ya nchi wanaotaka kuchangia kwa hali na mali kutatua matatizo ya watu na nchi yao pindi wanapowezeshwa na kurahisishiwa kufanza hivyo. Vijana wengi wa Kiafrika wamechoka kuona wanabwebwa na kudekezwa na kunyimwa kufanza mengi kama vile wao ni watoto na wazungu au wageni wengine ndio watu wazima. Wanataka kuonyesha utundu wao, kujaribu, kuthubutu na hatimaye kuweza kuanza kutoa mchango kwa maendeleo ya nchi na watu wake haraka iwezekanavyo. Wakati huko Chinana kwingineko Asia, vijana wa miaka 18 wanaanzisha miradi na kuwa na kampuni zao wenywe, hapa Tazania ndio kwanza tunamficha kijana shuleni asome, kisha afeli na kukata tamaa na maisha. Isitoshe hivi leo dunaini kuna mitandao na rasilimali za kielimu, kiujuzi na kimaarifa za kila aina kumuwezesha mwanadamu kuunda chochote anachokitaka; teknolojia zinatafutwa kwenye intaneti kirahisi; soko kwa ajili ya miundombinu ya namna hii bado bikra kabisa Afrika; kuna taasisi za kila aina kuwawezesha vijana kupata mtaji mradi tu wapate mdhamini; nchi ina vijana wabunifu ambao vipaji vyao vinahitaji kuengwaengwa na kuendelezwa kidogo tu, pasina ubabaishaji,unafiki, kumjua huyu ni wa nani na yule si wa nani, wala upendeleao; wengi wa vijana wetu leo ni watu wanaojitambua kuwa sababu ya kuwepo kwao sio starehe na anasa bali kubwa zaidi na la mwanzo kabisa ni kusaidia nchi yao kuondokana na umaskini, ujinga na mardhi, na hali kadhalika elimu na vipaji vya ujasiriamali na maarifa ya kiuchumi na kiteknohama vinachipua kama uyogakila kona nchini. La kujiuliza baada ya miaka hamsini ya uhuru ni je, elimu tunayoendelea kuitoa hapa nchini inasaidia nchi kwa kiasi gani kutatua matatizo ya nchi na watu wake? Nchi yetu ina matatizo mbalimbali yakiwemo yale ya usafiri na uchukuzi- ikiwemo uundaji na utengenezaji wa reli, meli, ndege, vyombo vingine vya usafiri na uchukuzi, bandari, barabara, viwanja vya ndege, chakula, maji, nishati nafuu na rahisi kutumika, na viwanda mama na viwanda vidogovidogo. Nchi yetu bado inahitaji pia nyumba bora kwa ajili ya wanacnhi wake na hasa vijijini; shule, hospitali, vijiji na miji safi na bora zaidi. Achilia upatikanaji kirahisi wa maji, umeme na huduma za usafi na utunzaji mazingira nchini.Aidha, tunahitaji kuzlisha mazao na bidhaa mbalimbali kwa kiwango cha kimataifa na vile vile ktuoa huduma zinazokubalika kimataifa ili tusipate ulazima wa kujitengenza na kuwa wasafi pale mgeni ajapo kututembelea kwa usafi na mazingira bora kuwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Nitazungumzia leo tatizo moja tu, lakini ninaamini fikra za ufumbuzi wa tatizo hilo zinaweza pia kutumika kwenye kutatua matatizo ya mahaa na aina nyingine kiurahisi kama itavyowezekana katika hili. Yeyote anayetembelea miji au vijij kando ya reli ya Tanga-Kahe- Taveta- Arusha kam vile vya Mkumbara, Hedaru, Pongwe, Magunga, Mombo, Korogwe, Makanya, Chekereni, Himo, Uchira, Kahe, Mtakuja, Kiyungi, Rongoi, Rundugai, KIA, USA River na kadhalika hakosi kuona nini hali ya sehemu na maeneo hayo ingekuwaje laiti Shirika husika la reli lingelikuwa bado linatoa huduma zake na hasa katika ubebaji mizigo na mifugo. Jambo hili tukilifanza kwa njia ya utegemezi na kusubiri h isani ya wafadhili litatuchukua miaka kama sio miongo kadhaa. Lakini jambo hili hili tukijifunga kibwebwe na kulianzishia shule au chuo cha ujenzi wa reli kwa kuitumia njia hiyohiyo ya reli ya Tanga-Moshi-Taveta na Arusha linaweza sio tu kufnyika haraka, lakini pia likawa ndio mwanzo wa Tanzania kuachana na kuzitegemea nchi nyingine katika uundaji wake wa magarimoshi na utengenezaji wa njia zake za reli. Chuo hiki kinaweza kuanza kwa vifaa vilevile ambavyo bado vipo kwenye maeneo ya shirika hilo kwenye mikoa husika. Kwa kutumia mabehewa ya zamani na mahema vijana wakaanza mwaka wa kwanza kwa kujifunza masomo ya msingi katika uhandisi wa njia za reli na uundaji garimoshi. Wakishajifunza sayansi, mahesabu na teknolojia za msingi vijana hao katika mwaka wa pili wanaanza kazi ya kulaza reli upya katika njia husika kwa kutumia viberenge huku wakisadiana mafundi wa kulipwa na kujitolea kutoka sehemu mbalimbali duniani ambako huko kwao hivi leo hawana ajira na wanangojea fursa kama hii kwa hamu sana. Mwaka unaofuata kwa kusaidiwa na serikali na watu wanaoipenda nchi yetu popote kule duniani vijana wanaanza kufufua au kukarabati mabehewa na vichwa vya treni huku mipango ikiandaliwa kimkakati kuwa na karakana au viwanda bora zaidi vya kufanyia kazi hiyo kwa kuwatumia wafanyakazi wa zamani katika sekta za reli ndani na nje ya nchi. Msaada huu utawezeshwa zaidi kwa kuwa na mawasiliano ya uhakika kati ya wahadhiri na wanafunzi chuoni hapo na mabingwa wa reli kimataifa kupitia simu za mkononi na nyenzo kama facebook. Badala ya facebook kuzipindua nchi zetu, sasa itatumika kuleta mapinduzi ya kujitegemea kiufundi na kitaalamu katika nchi zetu. Baada ya hapo huduma inaanza kwa uchukuzi wa mizigo na mifugo kwanza kabla usafirishaji binadamu haujaanza huku vijana wakijifunza menejimenti na utawala au uendeshaji bora wa sekta ya reli nchini na Afrika kwa ujumla. Hili likifanyika, wakati huo huo chuo kinaanza kujitangaza na kutafuta tenda za ujenzi wa reli katika nchi kama Kongo, Afrika ya kati, Chad, Zambia, Angola na kwingineko duniani ikiwemo India, Urussi, Amerika ambayo njia zake za reli zimechakaa kupita kiasi. Wakishamaliza mafunzo ya bashara na menejimenti kuu, sasa vijana watajimwaga kusomea masomo kama vile menejimenti ya operesheni, logistiki, uboreshaji safari za treni kwa kuwa na treni ziendazo kasi na kutumia umeme, utafiti na uvumbuzi muafaka katika kuendeleza na kuimarisha uchukuzi na usafirishaji kwa kutumia reli na masuala mengine ya kitaifa na kimataifa yatakayochangia katika kuifanya nchi kuwa mfano na kitovu cha ujenzi reli asili hapa Afrika. Vijana wanaopitia mchakato huu pindi wanapohitimu sio tu watapata vyeti vinayotambulika kimataifa, lakini, chuo na wabia wake kibiashara kinamwajiri papo kwa hapo. Inawezekana kweli kwamba nipo kwenye ndoto, lakini muamuzi mzuri wa hili ni kijana wa Tanzania asiyekuwa na ajira hivi sasa. Tumuulize, hli linawezekana au haliwezekani?

No comments:

Post a Comment