Tatizo Si Vyama Bali Vijana Kukosa Ajira na Tumaini
UPO msiba mkubwa Tanzania ambao sio mwingine ila ni ule wa viongozi na wananchi kujenga tabia ya kutangaza, kuamua au kutetea jambo fulani baada ya kumsikiliza mtu mmoja au chombo kimoja tu. Huu ni msiba mkubwa ambao unaweza kutufikisha kwenye gharika ya karne kitaifa katika muda sio mrefu kutoka sasa.
Aidha, pamoja na msiba huo ni ajali za kila siku ambako viongozi wetu hufikia kwenye majibu mepesi na ya kirahisi kwa masuala tata na magumu ya kitaifa na kijamii!
Mifano iko mingi. Tanzania inashinda kombe la chalenji kwa fluki basi nchi bila hata kukuza vipaji vyovyote vya maana wala maandalizi inaonekana tayari imepanda juu kisoka (hebu cheki taarifa ya FIFA ya hivi karibuni-mambo ni kinyume chake). TANESCO wanaomba kuongeza bei na wanaruhusiwa mara moja eti gharama zimepanda. Hakuna maelezo ya
wataalamu kwamba badala ya kupandisha bei TANESCO ingeweza ikapunguza gharama moja, mbili, tatu na isihitajike kupandisha bei umeme. Hakuna anayehangaisha akili ili kuangalia wizi na ubadhirifu TANESCO upo kiasi gani, jinsi gani watu wanajiandikia 'overtime' ya masaa 10 kwa kazi ya saa moja na kadhalika.
Tuliambiwa mgawo wa umeme sasa ni historia. [ Wengine leo wanadai wanahabari walinukuu kauli hiyo vibaya. Eti ni mgawo wa Kihistoriaa na sio mgawo utakuwa historia. ]
Inaonekana bado ni hadithi pevu na mpya kabisa. Kiasi kwamba wakati mwingine kuna watu wanaojiuliza kama viongozi wetu ni watu wazima au watoto wadogo? Inashangaza sana.
Kati ya muda ambao kiongozi anaambiwa kuwepo tatizo au fursa au changamoto fulani hadi anatoa kauli juu ya tatizo hilo kuna mambo kadhaa yanayotakiwa kufanyika. Kwanza, apate habari tofauti kutoka vyanzo mbalimbali. Asiwaamini tu maofisa na washauri wake. Apate watu wa kumfanyia kazi ya ziada pembeni ya wale wanaomzunguka. Atafakari ripoti zote
kwa kina. Akutane na wataalamu wa masuala husika na azungumze nao bila kutumia ukubwa wake kupata msimamo wao wa kweli. Kisha aangalie sasa kutokana na maelezo aliyo nayo anafaa kutangaza au kulizungmza jambo hadharani au la. Na kama ni kulitangaza litangazwe likiwa na mashiko yapi ya kiidhibati, kisheria na kiakili, kibusara na kihekima.
Kukurupuka tu baada ya kushauriwa na mtu au kikundi au taasisi moja mtu akajibu maswali mazito ya kitaifa au kimataifa hakika ni msiba usioelezeka nchini hapa. Na matokeo yake mara nyingi inakuwa ni mtu au nchi kujiiaibisha bila sababu ya maana.
Nikimsikiliza mwanasiasa mmoja machachari Tanzania nilibaki kinywa wazi alivyokuwa akielezea kiini cha tatizo la maandamano na vurugu huko Tunisia na Misri. Sina haja ya kurudia alichokisema, lakini upeo na uwezo wake kama kiongozi ulikuwa rahisi sana kuonekana kwa yeyote mwenye utambuzi na tafakuri kama mtu wa kawaida tu na wala sio lazima
awe mwalimu wa menejimenti na oganaizesheni na sayansi ya maamuzi. Hizi ndizo baadhi ya ajali za nchi yetu ambazo zinatokana na kutotambua umuhimu wa kutafuta katika rasilimali watu zetu kile kilicho bora zaidi kwa kila jambo na eneo.
Kinachotokea Afrika Kaskazini si majibu kwa ukame wa demokrasia na usawa katika ugawanyaji rasilimali za nchi ingawa hizi ni baadhi ya sababu.
Ukikumbuka historia ya ulimwengu kunako miaka ya 1960 na kizazi cha 'baby boomers' na 'mahippies' moja kwa moja unaona uhusiano kati ya matukio ya miaka hiyo na kile kitakachotokea katika muongo huu hapa Afrika.
Hali ya hewa na mazingira katika miaka ya 60 na 70 yamechangia Waafrika kuwa na watoto wengi ambao leo ni vijana. Baadhi ya vijana hawa wamezaliwa, wamesoma chekechea, shule ya msingi na sekondari, chuo kikuu na kuishia joblesi mitaani chini ya rais mmoja au wawili au chini ya chama kimoja tu cha kisiasa. Na hao waliokuwa madarakani hawana cha maana walichokifanya kama wenzetu wa Asia na Marekani Kusini kuinua nchi zao kiuchumi na kijamii.
Vijana hao ambao sasa wana miaka 20-40 wameona wazazi wao wakiwa na maisha bora kuliko waliyokuwa nayo wao leo; wameona jinsi viongozi wanavyozidi kujitajirisha; wameona viongozi wanavyowapa wanawake na watoto wao utajiri na nafasi katika utawala; na wameona jinsi nchi zao zinavyoporwa na kuibwa na viongozi wao wenyewe. Na wamefikia mahala wamechafukwa na roho, moyo na akili kiasi kwamba wako tayari wakipepewa na upepe mdogo tu kuwasha moto mkubwa unaoweza kuangamiza jamiii nzima.
Amani na umoja ambao kwa kawaida unakuwa ni wimbo wa vyama vikongwe vilivyotawala Waafrika sasa unakuwa ni wimbo unaowakinaisha na kutokuwaogopesha kabisa vijana.
Vijana wanajua fika amani wala umoja ni muhimu. Lakini kukosa ajira kwao ni kukosa umoja na kukosa riziki kwao ni kukosa amani. Na kukosa matumaini katika maisha ni kukosa mshikamano kabisa na jamii mtu aliyemo.
Hawa ni watu ambao wamekulia chini ya chama kimoja au rais mmoja toka walipozaliwa, kusoma chekechea, kusoma shule ya msingi, sekondari na hata chuo kikuu. Na sasa ni joblesi na watu wasio na matumaini chini ya chama au rais huyohuyo ! Na televisheni, redio, intaneti na simu za mkononi zinawafungua macho kila siku kuwa mtu au chama kimoja kikitawala kwa muda mrefu kinazeeka, kinachoka na kinaridhika na hali ilivyo hata kama kwa kufanya hivyo kuna mateso, dhiki na majonzi makubwa mioyoni mwa walio wengi.
Katika lugha ya kiutafiti tatizo hili la vijana limeelezwa na watu kadhaa kama David Bloom na wenzake kuwa ni tukio la kinchi linaloitwa 'demographic dividend' au mgawo wa ziada wa kimaendeleo unaoletwa na kuwa na watu wengi wenye umri wa kufanya kazi kuliko wasiofanya kazi. Ikiwa viongozi wanaliona hili na kulifanyia kazi ili nguvu na akili hizo zitumike
kuijenga na pengine kuitajirisha nchi basi nchi itakuwa na amani na maendeleo.
Wasipoliona jambo hili na kadri idadi kubwa ya vijana wanavyokuwa hawana kazi na hawachangii lolote la maana katika maendeleo yao binafsi, ya familia zao na ya nchi basi kulipuka na kusambaratika kwa nchi husika ni kitu kisichoepukika. Kwa maneno mengine, 'demographic dividend' hustahili kuwa kitu cha manufaa kwa nchi na watu wake, lakini
chini ya uongozi mbovu, unaoifilisi serikali yake yenyewe, uongozi unaofikiria kuneemeka wenyewe kwanza na sio wananchi na utawala usiojua unakwenda wapi na unafanya nini jambo hili hugeuka kuwa tani za fataki hatari kwa jamii na nchi nzima.
Baadhi ya dhiki na matatizo yanayowakera vijana wa Kiafrika ni pamoja na kushindwa kujikimu wenyewe na kutegemewa wazazi na watu wengine; kuiona nchi yao inakuwa shamba la bibi la wageni; kuona ndani ya serikali kuna wizi na ufisadi wa kutisha; kuona hakuna dalili zozote za uongezwaji au uzalishaji wa ajira mpya nchini; kubebeshwa zigo la gharama za elimu na afya na kudhulumiwa hata kile wanachotakiwa kupewa au kukopeshwa.
Matatizo mengine ni pamoja na dini na madhehebu mbalimbali kukosa dhamira ya kweli kufuta umaskini na kuwasaidia vijana mitaji, mafunzo na uwezeshwaji wa aina mbalimbali ili waweze kujiajiri; miradi mingi ya serikali ya kijamii kuwa ni ya kuwapa watu samaki badala ya kuwapa nyavu; nchi kushindwa kutumia fursa za kiuchumi zilzoletwa na intaneti na teknolojia mpya; viongozi na matajiri kuwapendelea watoto wao kwanza kwa kila kitu na suala la maendeleo na nafuu vijijini kwa vijana na wazee kuchimbiwa hali hai katika kaburi la sahau serikalini na katika vyama vya kisiasa.
Dini na madhehebu yaliyoanzisha shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu vilitarajiwa vitatoa elimu kwa bei nafuu zaidi na hasa ukizingatia kwamba dini hizo zinapewa sio tu ruzuku na serikali bali pia na nchi za nje. Kinyume chake, shule za kidini leo zinatisha kwa gharama kubwa, walimu duni na wachache, wababaishaji katika menejimenti ya shule, walaji wazuri
tu lakini wanaowalisha wanafunzi chakula sawa au pengine chakula duni zaidi ya kile cha wafungwa magerezani. Shule hizo za kidini zimegeuzwa ni vyuo vya kuvumilia shida na taabu za kila aina.
Mashirika binafsi na yale ya umma yanajali zaidi kutoa ajira kwa watoto wa wakubwa na matajiri lakini wasiokuwa na majina hawafikirii wala kupewa msaada wa kujiendeleza.
Wanaoshika nafasi za uongozi serikalini wanajli zaidi kuwanufaisha watoto, ndugu na jamaa zao na sio kila kijana wa Kitanzania.
Ili kukabiliana na hali hii ni vyema wananchi wakashinikiza viongozi na vyama vya kisiasa na serikali zao kuhakikisha vitendo sasa viwe vinatangulia kauli. Serikali na wanasiasa wafanye kazi kwanza kuleta nafuu kwa watu ndio maneno yafuate. Ieleweke kwamba hakuna kitu kinachomkatisha tamaa mwanadamu kama vile kupewa ahadi hewa au isiyotekelezwa. Hesabu za haraka haraka zinaonesha kuna ahadi zaidi ya 100 zilizotolewa na wagombea nafasi ya Urais nchini. Kama hivyo ndivyo ni hatari kuachia mambo kwenda kama kawaida bila kuwa na taarifa zinazotoka kila mwezi kuonesha ahadi hizo zinaendeleaje kutekelezwa. Na ahadi zenye uzito hapa ni zile ambazo kwa namna moja au nyingine zinakuwa na manufaa kwa vijana.
Tatizo la ahadi zetu nyingi ni kuwa zinachukua miaka mingi hadi kutimizwa. Tunapaswa kujiangalia na kupanga ahadi kutokana na muda unaohitajika. Ahadi ya kukipa kijiji maji ya kisima isichukue mwaka bali ichukue mwezi mmoja au miwili tu. Shule ikikosa madawati au viti lisiwe jambo la mwezi bali la wiki moja tu. Na pale ambapo jambo kweli linataka miezi kadhaa au miaka liwe ni jambo ambalo kila mtu anakubali kwamba haiwezekani vinginevyo.
Wanasiasa wetu kihistoria hawaheshimu muda. Lakini lazima tubadilike tuwe tunaheshimu na kuuchukulia muda kuwa ni rasilimali adimu kuliko zote duniani. Ahadi lazima zimfae yule anayeahidiwa. Tukishakufa ahadi wala maneno mazuri hayatusaidii kitu. Tutekeleze mambo mapema na kwa wakati ili watu wafaidi tunayoahidi wakiwa hai na sio wakishakuwa wafu. Na hili ndilo linalowatisha vijana. Wanaogopa kwamba hakuna ahadi itakayotimizwa wakati wakiwa hai. Au zikitimizwa watakuwa wazee na hawatafaidika tena na kitu chochote kutokana na uzee na kukosa nguvu na uwezo mwingineo.
Ni muhimu pia kwa vijana wa Tanzania kuanzia sasa kuwa na jumuiya ya kitaifa badala ya jumuiya za kichama ili kuepusha tunayona yakitokea Misri na kwingineko baadaye. Kwanza, kuwagawa vijana katika makundi mbalimbali ni kuwazuia kuwa na umoja wa kitaifa na nguvu na sauti zaidi katika maamuzi ya nchi. Lakini muhimu zaidi ni kuwa vijana wakiwa chini ya Muungano wa Vijana wa Tanzania na sio wa chama hiki au kile watajenga Uzalendo na Utanzania wao kuwa madhubuti zaidi kuliko vinginevyo.
Taasisi kama JKT iliundwa makusudi kuwaleta pamoja vijana wa Kitanzania na kuwafanya wote (masikini kwa tajiri,dini mbalimbali, kabila mbalimbali) kujiona wao ni Watanzania kwanza juu ya kitu kingine. Tukiiachia fursa hii kupotea tutakuja ijutia baadaye.
Nimalizie kwa kusema kwamba, Tanzania haijafikia zilipofikia nchi za Maghreb lakini hatuko mbali sana kama tusipoamka na kubadili muundo wa serikali, mifumo ya uendeshaji nchi, matumizi ya rasilimali za nchi na kuacha kuwatanguliza matajiri, wanasiasa na wageni mbele badala ya kumtanguliza Mtanzania mzawa kwanza.
Ni lazima pia tufanye mambo yetu tofauti na watu wengine. Utofauti huu peke yake ndiyo unaoweza kutufanya tuwe tofauti na pengine kufanikiwa kwa haraka zaidi kuliko Waafrika wengine. Tuna mbegu, ardhi na maji tosha kupanda na kuvuna nchi yenye amani, mshikamano na maendeleo kwa wote. Watakaosababisha mambo kuwa kinyume cha hivyo wamo miongoni mwetu na ni wale wasiojua nchi hii na watu wake wanatakiwa waelekee wapi!
Kila mtu anaafiki Tanzania ina viungo vyote nchi inayohitaji kuandaa pilau safi ya ustawi jamii; uchumi imara; lugha ya Kiswahili inayoweza kumfundisha Mtanzania kila kitu chini ya mbingu; ustaarabu; miji safi na yenye mvuto kwa walio ndani na nje; kilimo kinachotutosheleza na ziada kupatikana; viwanda maridhia kukidhi mahitaji yetu ya ndani na ya nje; utalii wenye vivutio aali na vingine vya kutengnezwa an watu; taasisi za elimu zinazovutia walimu na wanafunzi toka nje, hospitali zinazovutia madaktari na wagonjwa toka nje, migodi ya madini na mali asili zinazoweza kupunguza nusu ya umaskini wetu na masoko na biashara zinazoweza kutufanya wafanyabiashara bora Afrika na kwingineko -ila kinachokosekana ni wapishi wanaoweza kuikubali kazi yao ya upishi wakakaa jikoni kwa muda unaohitajika na sio kama viongozi wetu ambao wanausahau upishi wao na kukaa mezani chakula hicho kipikwe sijui na nani?
Sunday, February 6, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment