MAJUMA mawili yaliyopita, siku ya Jumanne, kulikuwa na habari za Kenya kujenga bandari na kiwanja cha ndege mpakani mwa Tanzania. Hili linatokea wakati ambapo mwaka mmoja haujapita toka makala haya kuhoji kuwepo kwa 'bodaposti' katika mipaka yetu ambazo zimefanana sana na vichaka bodaposti hizo zilizomo.
Makala haya yakashauri kwamba wakati umefika sasa kubadilisha bodaposti hizo zifanane na viwanja vya ndege vya kimataifa ili kuwapendezesha na kuwavutia zaidi watalii na wawekezaji kuja kusaidia kukuza na kuendeleza uchumi wetu. Kitu ambacho ni haki yao. Wakati Kenya walisoma, kuitafakari na kuifanyia kazi habari hiyo wenzetu bado wapo usingizini na hakuna kinachoendelea. Bado somo la utandawazi na ushindani usio na mipaka halijaeleweka hata kidogo kwa upande wao.
Kenya inatambua fika kwamba vivutio vikubwa vya utalii hapa Afrika Mashariki viko Tanzania. Walichokifanya ni kutumia akili yao kwani wanajua Watanzania hawatumii zao ila kwa yale yasiyochangia maendeleo yao bali kuyavuruga na kuharibu walichonacho. Nchi ya maneno mengi sana, lakini ya vitendo vifupi na vichache mno, ndivyo tunavyoitwa eti! Nani wa kubisha ?
Kiutalii tunakwenda wapi ?
Hivi kweli tunataka utalii uchangie kupunguza umaskini nchini ? Nina mashaka. Maana tungelikuwa na busara hiyo yale yaliyofanyika Arusha ambayo ni kitovu cha utalii yasingefanyika. Lakini hilo ni dogo tu. Tuje kwenye picha kubwa. Hivi kujitangaza Ulaya, Marekani na kwenye CNN na wengineo kama hako kutatusaidia kweli bila kujipanga hapa nyumbani ? Muhali sana.
Takwimu zinaonesha sekta ya utalii inakuwa haraka kuliko sekta za mazoea za siku za nyuma. Lakini kukua kwa utalii hapa nchini kutategemea sana jinsi tunavyoondokana na picha ya sisi kuwa nchi masikini. Kwa kadri tutakavyoonekana ni masikini (wa kujitakia) tutawaogopesha watu kuja kutalii nchi hii. Na kwa ujumla watu wasiotaka kubadilika na wanaotaka kuvuna pale wasipopanda kitu chochote. Ni lazima serikali ishiriki kikamilifu katika uendelezaji wa sekta hii ili iweze kufanya maajabu katika muda mfupi iwezekanavyo. Na njia mojawapo kama nilivyosema ni ile ya kuwa na mikakati sahihi ya kupunguza kama sio kuundoa kabisa umaskini wa kutupwa.
Tanroads na Wizara husika zijipange upya
Kama kweli tunataka utalii utusaie kupunguza umaskini ni lazima tujipange upya. Ninachokiona sasa ni kuwa wahusika wakuu kila mmoja anakwenda njia yake na analifanya lile analojua yeye. Hili nadhani ni kosa. Ninashauri wale wanaoishi kando ya barabara zetu, Tanroads, SUMATRA, Kituo cha Uwekezaji Tanznia, NSSF, PPF, Wizara ya Utalii, TANAPA, Wenye vyombo vya usafiri, Wasafirishaji Watalii, Wenye mahoteli wafanye kazi pamoja ili barabara zetu zisiwe kama mstari tu unaopita juu ya nchi baliziwe na vivutio vya aina mbalimbali vitakavyogeuza njia husika yenyewe kuwa ni kivutio cha utalii pia.
Tuchukulie mfano wa barabara mbili kuu Tanzania, yaani, ile ya Dar es Salaam-Arusha/Namanga na ile ya Dar es Salaam-Mbeya/Tunduma. Barabara hizi zimejengwa kizamani. Hazina mvuto kwa watalii ila vivutio vya asili na vile vichache watu binafsi walivyoviweka njiani. Lakini hebu tujiulize walichokifanya waliojenga hoteli pale Kitonga na pale Highway Korogwe kimeongeza ubora wa huduma za usaifi njia hizo kwa kiasi gani ? Na, je, mifano hii inaweza kuigwa kwenye mambo mengine ? Je, tunaweza kuwa na sehemu zenye huduma zote muhimu kama vile misikiti au mahala pa kusalia, zahanati, vituo vya mafuta, vyombo vya ulinzi na usalama, mahoteli, viwanja vya michezo mbalimbali,mabwawa ya kuogelea, vyoo safi, bafu, gesti, intaneti, simu, maduka, masoko na kadhalika kwa kila kilomita 70 hivi? Mathalani njia ya Dar-Arusha ukawa na vituo kama hivyo 5 na ile ya Dar-Mbeya kama 10 hivi ? Ninaamini kuwepo barabara kunakuwa na faida endapo watu wanafaidika na barabara hiyo na biashara na miji mipya inazuka. Kazi ya kwenda kuchimba dawa ikiisha hivi kuna mgeni atakayesita kusafiri na mabasi ya TABOA ?
Tujiulize, ni kwa namna gani tutaacha kujenga barabara zisizokuwa na kivutio chochote njia nzima? Maana zikibaki kama zilivyo zinakuwa hazijaongeza thamani wala maslahi yoyote ya maana kwa Mtanzania wa kawaida. Na utunzaje wake pia hapo baadaye unakuwa wa mashaka. Njia bora ni kuwa na ushirikiano na washikadau wote katika kuzifanya barabara zetu na maeneo zinakopita kuwa ni aina fulani ya kivutio cha utalii. Kiasi kwamba mtu anaposafiri kuelekea Arusha au Mbeya asitake kufika huko haraka na ikiwezekana alale siku mbili au tatu njiani kufaidi vivutio mbalimbali anavyokutana navyo njiani. Kwa namna hii pia utalii sasa utashuka hadi chini na kuwanufaisha masikini ili mradi tu twende nao sambamba katika kuhakiki viwango vya ubora vinavyokubalika njia nzima.
Utalii ni kama msichana. Jinsi anavyokuwa mzuri, msafi, mwenye kujua mapishi ya kila aina, mcheshi na mwenye kuvutia kwa kila hali ndivyo wanaume wengi wanavyojigonga gonga kwake kila kukichwa!
Humo mote barabara hizo kuu zinamopita inawezekana kuwa na programu kamambe ya kukuza utalii wa aina mbalimbali ukiwemo ule wa makumbusho, vyakula na vinywaji, miti na mali asili zingine. Aidha, utalii wa kielimu, mafunzo, mikutano na kiutafiti pia unawezekana na ile ya anasa au starehe, michezo na sanaa. Vilevile utalii wa usafi na mazingira bora, mazoezi, tiba na afya na kadhalika.
Kama hili litaendana na kuondokana na bodaposti za kale na badala yake kuwa na vituo vya mpakani sawa na viwanja vya ndege kwa ushirikiano kati ya wananchi, serikali na wawekezaji wa nje na ndani kilichofanywa na Kenya kinaweza kikawa ni hasara badala ya faida. Isipokuwa hakuna muda hata kidogo wa kusubiri. Kama walivyosema wahenga: " Chelewa, chelewa utamkuta mtoto si wako!"
Tanroads isifikirie kiuhandisi au kifundi tu. Ianze kujenga tabia ya kufikiria mambo kibiashara na kiuchumi. Upo uwezekano mkubwa sana wa barabara zetu kusaidia kupunguza umaskini endapo miradi kama iliyooneshwa hapo juu itatekelezwa inavyostahili na sio kiubabaishaji.
Sambamba na hili ni lile la kuwa na barabara moja kuu inayotambaa na bahari ya Hindi katika pwani ya Tanzania kiasi ambacho kwamba tunaweza pia kuwa na Utalii wa pwani ya Tanzania kwa meli, ndege na magari. Na katika yote haya nafuu ya kimaisha na kiuchumi ikapatikana kwa wakazi wa maeneo husika katika muda mfupi tu ujao. Mikoa yetu ya pwani kwa kiasi fulani ni masikini na iko nyuma kimaendeleo kwa sababu bahari, vilivyomo na fukwe zake ambazo ndio rasilimali zao kuu hazijatumika ipasavyo kuvutia watalii katika maeneo hayo.
Katika dunia inayobadilika kila siku ni kosa kubwa kufanya jambo bila kuhusisha mambo mengine yanayoendana na jambo hili. Huu ni mtazamo wa kuyafanya mengi kwa faida kubwa chini ya mwamvuli mmoja, kwa maana kwamba, mambo mengi kwa pamoja yanaweza kufanyika kwa faida kubwa zaidi na kwa manufaa ya wengi zaidi kwa wakati uleule.
Ipo kila sababu kama kweli tunataka kuitumikia nchi hii na watu wake kuifanya Tanroads, Wizara ya Mali Asili, Hazina, TASAF, Benki Kuu, mabenki mbalimbali, makampuni ya mafuta na simu za mkononi kuanza kufikiria kuwapa Watanzania nyavu za kuvua samaki wao wenyewe badala ya kuwadanganya na kipande cha samaki au nguru kila siku.
Wednesday, February 9, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment