Sunday, February 27, 2011

Mikoa Huru na Udikteta Chipukizi

UDIKTETA au ukiritimba au mtu kuhodhi mamlaka yote peke yake, iwe kisiasa au kiuchumi au kijamii huashiria kuwa huyo ni mtu au mtu mwenye kikundi cha watu wasiajiamini na wasiokuwa na uhakika na kile wanachokifanya. Aghalabu watu wa namna hii huwa hawajui wanakotoka wala wanakokwenda. Ni mwanzo wa kuficha maovu mengi kwa kuonesha mazuri machache ambayo pengine hayana faida wala manufaa kwa a ya kujichimbia kaburi lake yenyewe. Huanza kwa kutoamini wengine lakini huishia kwa kutojiamini wenyewe na kutoaminiana wenyewe kwa wenyewe na kuishia kujichanganya na kujimaliza wenyewe.

Udikteta huweza kuundwa na mtu mmoja au kikundi cha watu. Udikteta uliopo Tanzania hivi leo ni ule wa kichama. Udikteta huu unajidhirisha kwa chama hicho kutaka kuwa na watu na sauti katika kila jambo hata yale yasiyokihusu- kwa mfano, dini, utamaduni, mila na desturi, mawasiliano, maendeleo ya watu na jamii zao, ushirika, uzalishaji mali na majumuiko mengine ya kijamii kwa hofu hii au ile.
Kwa kuwa wanasiasa waliopo wanaamini kwamba kwa kuwa hawawezi kuitawala nchi bila ya kulazimisha mikoa, wilaya, vijiji na mitaa kuwa chini ya chama tawala basi miundo na mifumo ya kisiasa inayoundwa sio ile ya kufanya maeneo hayo kuwa huru bali maeneo hayo kutawaliwa moja kwa moja au kimzunguko na chama tawala na viongozi wake.
Ni dhahiri basi madaraka mikoani au kuwa na mikoa huru kiuchumi na kijamii sio jambo linaloweza kufanywa na wanasiasa wa chama tawala. Hili ni jambo linalostahili kuwemokwenye katiba na sheria za nchi kama sehemu moja ya kupanua na kuongeza kina cha watu kujitawala, kujiamulia mambo yao wenyewe na demokrasia kiujumla.
Chama tawala kina unafiki mkubwa ambao ni muhimu kuutambua na kuubainisha kwa wadau wa katiba. Kwa kuwa kinatambua nguvu yake inatokana na ujinga, umaskini na magonjwa mbalimbali ya watawaliwa inaelewa fika kuwa kupiga vita mambo hayo ni lazima wanajamii washirikiane ili kufanikiwa. Lakini, ushirikiano wa wananchi kijamii na kiuchumi kutawapa pia wanajamii nguvu na sauti sawa au zaidi ya wanasiasa. Kwa mantiki hii chama cha siasa kinachokubali makundi ya jamii au watu kuwa huru zaidi kiuchumi na kisisasa katika ngazi ya mtaa, kata, wilaya na mkoa huhofia pia kujimaliza kisiasa. Kwa sababu hii, maamuzi yote yanayohusiana na kuyapa makundi ya kijamii nguvu na uwezo zaidi hufanywa polepole mno. Jambo la siku moja huchukua mwezi; la mwezi, mwaka; la mwaka muongo; la muongo karne kama sio zaidi!
Hata hivyo, ili nchi na watu wake kuendelea hakuna njia ya mkato. Njia ni moja tu. Nayo ni ushirikishwaji wananchi katika uundwaji wa katiba na sheria za nchi zinazoendana na wakati tuliomo; ushirikishwaji watu katika maamuzi, mipango, uongozi, utekelezwaji na udhibiti wa masuala yote ya maendeleo na ustawi wa jamii huska ikiwemo kuwa na mikoa huru kiuchumi inayokuwa chini ya viongozi waliochaguliwa na wananchi au wakazi wa mkoa husika.
Kwa kifupi kuna mambo kadhaa yanayoonesha wazi kwamba ili serikali yoyote ifanikiwe ni lazima wananchi wake washiriki na wawe na sauti katika uongozi wa nchi:
. Kukubalika, heshima na uwezo wa serikali kuu huanza kwenye mitaa na jamii mikoani;
. Maendeleo ya kweli ya mkoa yanatokana na kile wananchi wake wanachozalisha na kumiliki na sio vitu vya wageni;
. Serikali zenye nguvu na uwezo za mikoa na mitaa hufanya kazi ya kulinda hazina ya mkoa na mali asili za eneo husika kwa faida ya wakazi wake na nchi nzima;
. Uongozi wa kitaifa hutekeleza miradi ya mikoa aghalabu nusu nusu kutokana na kukurupuka na kwenda kuzima moto unaowaka mkoa mwingine, hivyo kuhamisha fedha kwa ajili ya mkoa mmoja kwenda kuufaa mkoa mwingine isivyo haki;
. Wizi wa kura unaofanyika kirahisi chini ya uchaguzi wa kitaifa utapungua ikiwa kila mkoa unachagua viongozi na serikali yake kwanza wao wenyewe kabla ya uongozi wa kitaifa;
. Serikali huru za mikoa ni shule au chuo pekee kitakachowafundisha viongozi wa baadaye wa kitaifa kwa vitendo huko huko waliko mikoani.

Migogoro ya kisiasa inayotokea Afrika na hususan Tanzania kwa kiasi kikubwa ni kati ya wale wamanaoamini:
. wanasiasa kazi yao ni kutawala na wananchi ni kutawaliwa tu dhidi ya wale wanaoamini wananchi wanastahili kujitawala wenyewe;
. Wanasiasa wanaoamini viongozi wetu wanastahili kuishi kifahari na wale wanaoamini ni lazima wanasiasa wajishushe kwanza na kuwanyanyua watu wao kabla ya wao wenyewe kuwa na maisha mazuri na bora;
. Wanasiasa wanaodhani kuwa kazi ya vyombo vya habari vya umma na vile vya chama tawala ni kufuma na kusambaza urongo na wale wanaoamini hakuna mwenye haki ya kutengeneza na kuuzia wananchi uongo Afrika;
. wanasiasa wanastahili maisha mazuri na bora kuliko raia wengine na wale wanaoamini wananchi wanastahili maisha bora na mazuri kuliko ya wanasiasa;
. wanasiasa wana haki ya kuiba toka hazina za taifa na kuweka fedha toka nchi maskini katika nchi tajiri kwa hifadhi yao ya baadaye na wale wanaoamini huo ni ujinga na kama mwanasiasa ni mwananchi mzalendo hifadhi yake lazima itoke ndani ya jamii yake;
. wanasiasa wetu wanastahili kuwanyenyekea na kuwafuata wale wanasiasa matajiri kwa kila jambo wanalolisema au kutushauri hata likiwa halina maslahi kwa watu wetu;
. wanasiasa wanastahili kuwatumia polisi na pengine jeshi ili kuwasaga wananchi waende kule wao wanakotaka waende dhidi ya wale wanaoamini polisi na jeshi wanastahili kudhibiti wanasiasa kwenda kle wananchi wanakotaka nchi iende;
. wanasiasa wanahitaji kubaki madarakani milele ili walete maendeleo na wale wanaoshani wanahitaji muhula mmoja tu kufanya kazi hiyo;
. wanasiasa wa chama tawala ndio tu wapewe uongozi hata kama hawawezi kazi na wale wanaodhani wanaostahili kuongoza wananchi lazima wachaguliwe na wananchi wa eneo husika;
. wanasiasa wanaoamini wananchi wakielimishwa na wakiondokana na umasikini itakuwa vigumu wao kutawala dhidi ya wale wanaoamini itakuwa rahisi zaidi kwao kutawala;
. wanasiasa wanaoamini kuwa chama cha kisiasa lazima kiwaibie wananchi ili kiendelee kutawala na wanaoamini wananchi wenyewe wanaweza kukika chama uwezo wa kujiendesha;
. wanasiasa wanaoamini ni wanachama wa chama fulani tu wanaostahili kuwa na sauti na kuwa makundi mengine katika jamii hayastahili kuwezeshwa wala kuwa na nguvu iwe ya kisiasa, kijamii au kiuchumi na kadhalika.

Afrika imebadilika, na Afrika ya leo si ya jana. Wale wote wenye fikra pacha za kwanza hawana tena nafasi katika Afrika mpya. Kizungumkuti kinachokuja kitawagia kama ilivyofanyika huko Maghreb pembeni na kuwajaribu wala wenye fikra mbadala pacha hapo juu.

Na njia sahihi ya kufuata kuanzia sasa ni kuhakikisha kuwa tunapelekea madaraka kwa wananchi sio tu mikoani bali mpaka vijijini.

Mikoa Huru ya Ujerumani:
Kwa mfano mikoa ya Ujerumani ni pamoja na Baden-Württemberg, Bavaria (Bayern), Berlin,Brandenburg na Bremen. Kahalika kuna Hamburg, Hesse
(Hessen), Mecklenburg-Vorpommern, Lower Saxony (Niedersachsen), North Rhine-Westphalia (Nordrhein-Westfalen), Rhineland-Palatinate (Rheinland-Pfalz), Saarland, Saxony (Sachsen), Saxony-Anhalt (Sachsen-Anhalt), Schleswig-Holstein na Thuringia (Thüringen).

Mikoa yote hii isipokuwa kwa mkoa mmoja tu ina serikali za pamoja/mseto kati ya vyama viwili au zaidi. KIla mkoa una waziri wake mkuu, baraza lake la mawaziri, wawakilishi wake na taasisi zake na inakuwa huru kwa kiasi kikubwa kwenye masuala yote ya kiuchumi na kijamii. Yale ya ulinzi, usalama, fedha na siasa za nje hushughulikiwa zaidi na serikali ya kitaifa yenye makao yake makuu hivi leo Berlin. Mikoa hii imewezesha kuwa na ushindani wa ndani kwa ndani na hivyo kuipa nguvu Ujerumani katika utandawazi na ushindani wa nje kwa kujikita tu kwenye maeneo inayoamini hakuna anayeweza kuwapita. Wao si watu wa kufanya na kujaribu kila kitu kwa kubahatisha. Hutafuta uhakika kwanza kabla hawajawekeza kwenye jambo fulani.

No comments:

Post a Comment