Wednesday, August 17, 2011
Nini chanzo cha migogoro kati ya wananchi na wawekezaji
NI kitu cha aibu kwamba hata viongozi wetu wa juu hapa nchini wameamua kuingia kwenye mbio za PRIMITIVE ACCUMULATION, labda pengine kutokana na kisomo chao duni na kushindwa kupata nafasi kimataifa kujipatia kipato baada ya kustaafu.
Lakini wakati huo huo ni nafasi ya wazi kabisa kuona jinsi ubinafsi na umimi unavyojijenga toka juu kabisa serikali hadi chini kabisa. Kisha mtu ajiulize hawa ndio watu waliokusudiwa kweli kujenga taifa la kijamaa au Nyerere alizaliwa katika nchi tofauti kabisa.
Binafsi, haya yote ninayaona katika macho ya ubinadamu na uhalisia wa mambo-kwamba hakuna mtu anayezaliwa kuwa mjamaa na hakuna Mtanzania anayependa mwenzake apate, ili anataka apate yeye tu, hata kama hana uwezo, akili na nguvu za kukitumia hicho anachojilimbikizia.
Huu ndio utamaduni wetu, na hao ni viongozi wetu na kizazi chao. Je, sasa tufanye nini. Ninaamini ya kwamba maendeleo yetu yatakuwa sawa na kupanda mlima mkubwa zaidi ya Kilimanjaro kama tusiporudia kwenye mambo ya msingi katika siasa za waasisi wetu na hususan Mwalimu Nyerere.
Kwanza, badala ya viongozi tena wa chama tawala chenye historia kongwe ya vita dhidi ya ubinafsi na kujilimbikizia mijimali lazima watangulize wananchi na hususan wanavijiji wa Tanzania mbele.
Badala ya kujijenga hekalu mbadala wake ungelikuwa ni kuwajengea wanavijiji 5,000 katika kijiji fulani kila familia nyumba ya kisasa ya vyumba vitatu.
Tunalalamikia foleni na kufurika kwa watu mjini lakini sio siri kuwa vijiji vikiwa na maji ya bomba, umeme, barabara safi na kumbi za starehe na huduma zote muhimu nchini ni wachache watakaotaka kubakia mjini.
Ukileta neema zaidi ya wanavijiji kutumia matrekta madogo kwa makubwa badala ya kisigirima ndio kabisa watu wataanza kuhama kuelekea vijijini na hivyo kuipa miji nafasi ya kupumua na mingine kufa kifo cha kawaida.
Ili hili lifanyike ni lazima viongozi wa kisiasa waache kutanguliza tamaa zao binafsi, uroho wa mali na kujilimbikizia na kuweka vipaumbele kichwa chini miguu juu.
Tatizo la Watanzania ni umaskini mkubwa na kukosa ajira na kipato cha kutosha kujiendeleza kwa vijana na wakulima nchini.
Yapo mambo mengi ambayo tukikaa na kutafakari tunaweza kuyafanya kwa pamoja au mtu mmoja mmoja na fumba na kufumbua kila tatizo nchini likageuka ni fursa ya kiuchumi au ya kuisongesha mbele jamii yetu.
Kabla hatujafikia hapo ni lazima kwanza TUWATHAMINI WATU WETU, TUTATHMINI UPYA THAMANI YA ARDHI, MADINI NA MALI ASILI ZETU NA TUTHAMINI UPYA UTU, MILA NA UTAMADUNI WETU KAMA RASILIMALI WATU YA KWANZA NA MUHIMU KULIKO ZOTE KWA FAIDA YA SIKU ZETU ZA USONI-WATU WETU.
Kuanzia Arusha hadi Zanzibar haipiti siku bila kusikia habari kwamba kuna tatizo kati ya wananchi na wawekezaji kwenye eneo fulani. Habari hizi za kuwepo na kuendelea kuwepo kwa mgogoro fulani ni dalili kwamba kuna ugonjwa fulani ambao umeanza na unaendelea kuenea na mgonjwa hata hajaonwa na daktari.
Kwanini wananchi wachome hoteli ya Kitalii; kwanini wananchi wavamie mgodi na baadhi yao kuuawa; kwanini viongozi wa juu wa serikali wa sasa na wa zamani walalamikiwe kuhondhi maeneo wasiyoyaendeleza na waliyopewa bure au sawa na bure ?
Sipendi kujifanya kwamba nina majibu ya kila tatizo linaloisibu nchi hii na watu wake. Ninaamini wapo wengi tu wanaojua zaidi yangu, lakini kwa sababu moja au nyingine wameamua kulifumbia tatizo hili macho. Kati yao wakiwemo wataalamu wa mambo ya ardhi, wanasheria na wanasiasa.
Ndio maana ninaamua kuwaandikia watu wa kawaida kwa njia ya maswali yasiyo na majibu ili waamke na wafanye kile kinachoonekana. Na umma uliolala ukizinduliwa toka usingizini hauwezi kamwe kuwaachia viongozi waendelee kupiga usingizi huku matatizo yao mbalimbali yakiwa hayajapata ufumbuzi.
Katika migogoro hii inayowahusisha wananchi na wawekezaji wa nje na wa ndani, inafaa kuuliza maswali kadhaa ya msingi kama vile, je, matatizo hayo yalianza lini? Yanapungua au yanaongezeka kila mwaka?
Hivi ni kweli kwamba Watanzania wengi kwa sababu wanazozijua wao wenyewe hawapendi wawekezaji ? Au wawekezaji hao na wakubwa wanaowakaribisha kuwekeza hapa nchini na mangimeza wa serikali na kati ya viongozi wa serikali za vijiji na mitaa kuna mkono wa mtu, na wanachokifanya ambacho kinawaudhi na kuonekana ni dhuluma kwa wananchi?
Kama zilivyo nchi nyingi za Kiafrika ni mwekezaji na hususan mtu mwenye ngozi nyeupe ndiye anayethaminiwa lakini sio raia na hususan yule mwenye ngozi nyeusi au mzawa ? Daraja hizi mbili au tatu za thamani tofauti kwa binadamu zinaigharimu nini jamii na nchi yetu? Na, je, huu ni mkakati muafaka wa kuiwezesha nchi kuja kuondokana na umaskini na kuwepo nyuma kimaendeleo hapo kesho na kesho - kutwa?
Na swali ambalo ningeliita ni MAMA WA MASWALI YOTE: Je, serikali yetu inaipa ardhi, mali asili, madini, gesi, mashamba, vijiji na utamaduni wa watu wetu thamani halisi na ya haki?
Nionavyo mimi, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo na ile ya Zanzibar zimeshindwa kuvipa vitu hivi thamani halisi na ya haki na uhakika na ndio chanzo kikuu cha matatizo yanayoendelea kushoto na kulia nchini. Na huu ni mwanzo tu, utafiti wa kina na hatua za haraka visipochukuliwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingi za Kiafrika ni nchi ambayo wanasiasa na viongozi wake hujiweka wao mbele kwanza na wameamua kujipa wao thamani kuliko mtu au kitu kingine nchini. Na wao wakishathaminiwa kama sio kuogopwa, kutetemekewa na kunyenyekewa na wale wanaowaneemesha basi sio kitu watu wanaowaongoza wakionekana hawana thamani. Mifano iko mingi, tazama mkubwa mmoja anavyopita njiani na kusababisha kinamama kujifungua njiani; tazama anavyozungukwa na ulinzi wa kutia kufuru; tazama hekalu au kasri anayojijengea na familia yake (kama vile kizazi chake kitamudu kutunza); tazama wapinzani wanapoandamana na mamilioni yanayofujwa ili kuwadhibiti; tazama wizara zinavyosherekea kupita kwa bajeti zao na tazama misafara ya wakubwa wakienda nchi za nje au kutembelea mikoani.
Angalia pia wanavijiji wanavyouawa na korokoroni wa migodi ya dhahabu na undumilakuwili wa serikali; wananchi wanaoathirika na ajali kila mwaka na fidia wanayolipwa; viongozi wanavyowatumia ma-RC na ma-DC kujimegea maeneo makubwa makubwa ya ardhi kwenye mikoa wasiyo na nasaba wala udugu nayo na wananchi wanavyohamishwa na fidia ndogo wanayolipwa.
Hii ndiyo hali halisi ilivyo. Wananchi mikoani na wilayani hawana sauti juu ya mali zao walizorithi toka kwa wazee wao. Na mtu anaweza kuzuka huko aliko iwe makao makuu ya wilaya au mkoa au nchi akatangaza eneo fulani kuchukuliwa kama vile mtu anajigawia shamba la baba yake aliyefariki. Na mwananchi hatakiwi kulalama au kupiga kelele, maana eti, hili ni la manufaa kwa nchi na watu wake. Lakini sio kwa manufaa ya mwananchi mhusika. Hivi, jambo hili sio kichekesho cha wakati wetu kwa kweli?
Maisha ya Mtanzania hayana thamani kwa sababu mali alizonazo hazipewi thamani halali, halisi na ya haki. Hata kwa ardhi iliyo duni au mbaya kabisa kwa ekari moja mwananchi hatakiwi kukosa angalau chini ya shilingi milioni mbili (kama iko mbali na mji). Na kama ardhi hiyo iko kwenye eneo lenye maji na ina rutuba haiwezi kuwa na thamani ya chini ya milioni tano. Ukizungumzia ardhi ambayo imegundulika chini kuna madini au mafuta au maji au nguvu ya kutoa nishati ya umeme, haiwezi kamwe kuwa na thamani ya chini ya milioni 25 kwa ekari. Na hizi ni thamani za chini kabisa, lakini sio mbaya kuanzia.
Hata hivyo, kwa miaka hamsini toka tupate uhuru, viongozi wetu wakishapewa chao cha chambele kwa mbele na
kuondokana na umaskini wao wa kuzaliwa, wawekezaji wamekuwa wakihalalishiwa kuwadhulumu wanavijiji kwa ushirikiano usio mtakatifu kati ya viongozi wa juu, viongozi wa mikoa na wilaya na viongozi wa vijiji.
Wanasiasa, wanauchumi, wabunge, wataalamu wa ardhi na wanasheria wetu wana deni kubwa la Watanzania ambao babu na baba zao wamedhulumiwa na mfumo uliopo hivi leo kuhakikisha hata kabla katiba mpya haijaandikwa dhuluma hii inakomeshwa.
Ni jukumu lao pia kuona kwamba katiba mpya itakuwa na vifungu vyote muafaka vinavyowawezesha wananchi wao wenyewe, ardhi yao, madini yao na mali asili zao nyingine kuwa na thamani ambayo kama wanabadilishana na wawekezaji basi watoto na wajukuu zao watakuwa hawana tena sababu ya kufa maskini.
Mtaji wa Masikini
Mtaji wa Mtanzania masikini sio tu nguvu zake mwenyewe bali pia ardhi, misitu, bahari, madini, gesi,mkaa, mafuta na mali asili zake zote. Umaskini wetu kwa kiasi fulani unasababishwa na muasisi wa msemo huu na serikali yake na uongozi mzima unaoshindwa kuvipa thamani majaliwa ya watu na vitu vilivyooneshwa hapo juu kwa sababu wanazozijua wao wenyewe.
Remi Isaac na Jos van Der Sterren (2004) wameliona hili na ndicho wanachokiita chanzo cha msingi cha kimuundo na kimfumo cha umaskini wa nchi nyingi za Kiafrika.
Watu wanamiliki ardhi au mashamba; wana mifugo; wanaishi pembeni ya bahari na maziwa yenye samaki kabakaba; wana misitu yenye miti adimu; wana mila na utamaduni wao; na wana mali asili za kila aina chini ya ardhi yao, achilia mbali mazingira yao ambayo awali ya yote ni salama kuliko kwa wawekezaji, lakini serikali zao zinapofikia makubaliano na wawekezaji vitu hivi vyote
eti vinaonekana kukosa thamani kabisa. Wizi ulioje huu? Na kwanini usikome kuanzia sasa ?
Wananchi waelewe ardhi na mali asili zao ndio jambo muhimu kuliko kitu kingine chochote kwenye katiba yao. Katiba sio jambo la chama tawala kung'ang'ania madarakani au upinzani kuking'oa au wasomi wa sheria kunufaika na kupalilia nafasi zao bali ni ngao ya mnyonge na maskini. Katiba ni andiko takatifu linalomrejeshea raia wa kawaida uhuru wa kuamua wale wanaomtawala wana haki zipi na yeye raia kama mtawaliwa ana haki zipi. Lakini mamlaka na madaraka yote anayo yeye raia na kiongozi au viongozi ni waajiriwa wake na sio mabwana zake. Ni katika mustakabali huu ndipo umuhimu wa wananchi kushiriki katika mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya unapokuwa na umuhimu wa juu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Ardhi isipolindwa na isipotunufaisha kupitia katiba basi nchi inaweza ikaja uzwa na kongozi yoyote yule ajaye-awe tioka chama tawala au upinzani. Ni lazima wananchi waamue ni utajiri gani kama mtaji au mali ya msingi ambao ardhi, wao wenyewe, mali asili zao mbalimbali na utamaduni na mila zao wanastahili kuwa nayo na kuchangia katika miradi mbalimbali.
Mwekezaji aliyewekeza Geita, Bulyanhulu au Nyamongo alistahili kuambiwa kwamba ardhi yenye madini anayopewa ina thamani ya bilioni kadhaa na sio vijisenti kadhaa. Na wamiliki wake ni wakazi waliokuwepo. Kwa mtaji huu wakazi wa maeneo yote hayo hivi leo wangelikuwa ama ni wanahisa katika kampuni zinazochimba dhahabu huko kwa hivi sasa au wangekwishasepa na mamilioni yao na kwenda kuwekeza kwenye kile wanachokipenda na kukiamini zaidi kuliko uchimbaji madini.
Kadhalika badala ya wananchi kupewa maharagwe na sembe pembezoni mwa mbuga za wanyama kama kuna ardhi yao ilichukuliwa, basi wananchi hao walistahili kabisa kuwa na hisa katika TANAPA nchi nzima na kila mwaka wangelikuwa na haki ya kupata mgawo wao tokana na kinachoingizwa na shirika hilo.
Aidha, masikini ambao juzi walikuwa ndio wamiliki wa ardhi ya Mnazi Bay au Songosongo au Merelani au Liganga au Mchuchuma au Mwadui au Songea au Chunya na kwingineko kwenye gesi au uranium au mafuta au madini mengineyo au mali asili nyingine hivi leo sio tu wangelikumbukwa na wagumu wa kukumbuka watu kama TANESCO bali pia wangelikuwa ni watu wenye mali na nafasi zao kijamii. Lakini muundo na mfumo uliopo uliwadhulumu, umewadhulumu na unaendelea kuwadhulumu na pengine hivi leo hali zao ni mbaya zaidi kuliko zilivyokuwa kabla ya uwekezaji uliohalallishwa na kubarikiwa na watawala wetu wa nyakati hizi, bila kuwajali wananchi wanaotakiwa sio tu kuwaongoza bali kuwalinda, kuwawezesha na kuwaneemesha pia.
Katika hali kama hii, ninaamini, hata kwa mtu asiyekwenda shule, hawezi kushindwa kuelewa ni kwanini kuna migogoro kati ya wananchi na wawekezaji. Na sio tu yapo yaliyopo bali yapo mengi tu yatakayozuka kesho na kesho kutwa. Amani na umoja wetu utakuwa mashakani. Ni heri nusu ya shari kuliko shari kamili. Tujifunze kutokana na makosa yetu huko nyuma. Tujisahihishe. Ng'ombe wa maskini pengine anaweza asizae, lakini ardhi ya masikini lazima ima fa ima katika miaka hii IZAE tena izae kwa sana tu! Ni ardhi na vilivyomo ndani yake itakyotujenga au itakayotuangusha.
Mwekezaji ambaye si tapeli bali muadilifu, anayeona mbali na mbele na anayetaka kuwa sehemu ya maendeleo ya nchi yetu na watu wake ni yule ambaye atakubali kukaa nasi na kuona ni kwa jinsi na namna gani shughuli zake zinaweza kuoanishwa na mahitaji, matakwa, matamanio na ndoto za Watanzania kama kitu kimoja na sio vinginevyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment