KUNA tofauti kati ya bibi na nyanya. Bibi ni mama yake baba. Na nyanya ni mama yake mama. Bibi aghalabu huwa mkali na akilea hulea vyema na wajukuu wakawa watu bora. Nyanya ana tabia ya kudekeza na matokeo yake ni kuwaharibu wajukuu.
Mataifa bibi ni kama vile Australia, Uingereza na Singapore. Sifa yao kubwa ni kukithiri katika kulinda wananchi wao na kuingilia maisha yao ya kila siku. Wakati mataifa nyanya sifa yake kubwa ni kulegeza kama sio kudharau kabisa utawala wa sheria. Wakati wanakuwa na uhuru unaopindukia mipaka na hivyo kuingilia maisha na usalama wa wengine kwa njia moja au nyingine na aghalabu kwa ubaya na sio wema, wizi na sio uaminifu, uongo na sio ukweli, na ubabaishaji sio uchapakazi.
Mathalani, viongozi fulani kwa kutumia kofia ya chama au taasisi ya serikali huweza kufanya maamuzi yanayowanufaisha wachache na kuwagharimu wengi isivyo haki au halali.
Yeyote anayepewa chochote au kuhongwa na viongozi kama hawa lazima atawasifu na kuwapenda. Lakini watu kama hao wanashindwa kuelewa kwamba wao wanaponufaika asilimia zaidi ya 99.9999 ya Waanzania wanakuwa wameibiwa, wamedhulumiwa au wamenyonywa kijanja janja tu. Tumeona hayo Igunga, Dodoma na kwingineko.
Katika kulea na kutokuukwaza utawala wa kisheria hayumkiniki Tanzania kuwa nchi salama kwa watalii kama sheria zetu za barabarani ni dhaifu kiasi hiki. Jiulize ni mtalii gani atakayevinjari jiji kama Dar es salaam akijua fika daladala, bajaji, pikipiki, maguta, mikokoteni na kadhalika havina njia wala sheria na wakati wowote anaweza kugongwa na isijulikane kagongwa na nini au nani?
Bila utawala wa kisheria unaodhibiti maingiliano kati ya watu mitaani ni vigumu nchi kustaarabika.
Uongozi wowote unaoshindwa kufanya kazi (mathalani Wizara ya Madini na Nishati) kwa kulitia taifa katika matatizo yasiyokwisha na kushindwa kupata ufumbuzi wa maana na unaofanya kazi kwa matatizo ya wananchi hujiingiza katika kuridhishana na kupongezana wenyewe kwa wenyewe. Hutafuta kufanikisha mambo yao kwa siasa za bei sawa na bure. Au kwa maneno mengine siasa za ubabaishaji na maneno matupu yasiyomnufaisha mwananchi wa kawaida. Sera zinazoongeza tofauti na wivu kati ya walionacho na wasio nacho. Sera zinazojenga tofauti kuu ambazo hatimaye huchangia sana kuwa chanzo cha mifarakano katika jamii.
La kutisha ni upofu uliopo katika wizara, mikoa na wilaya kwa viongozi wa maeneo yao kutoona alama za nyakati kwa kubaini ukweli kuhusu umaskini wa kutisha wa wananchi mijini na vijijini. Nusu bilioni sio kitu kidogo kufanya sherehe, tena kwa wizara ambayo haina ufanisi wala ufanifu katika mambo yake, bali imelitia hasara taifa kwa kila hali.
Umefika wakati kwa viongozi wetu kujijua wao wenyewe na dhima walyo nayo kwa masikini wa nchi hii na kisha kuijua na kuikubali hali halisi ya umaskini Tanzania na kujiepusha kutapanya fedha katika masuala ambayo haimpi nafuu wala usalama wa maisha Mtanzania wa kawaida. Kinyume cha hivyo, ni kwa viongozi wetu kukubaliana na kile kilichomo katika biblia katika maneno kama, "masikini watakuwa nanyi daima!' na kisha kuhalalisha wao kupata na masikini kukosa kama ilivyo kwa hivi sasa lakini kwa maafa ya kizazi kijacho.
Inavyoelekea kuna viongozi Wizarani, Ikulu, mikoani na wilayani ambao wanataka kuendeleza kile tusichokitaka kiendelee, ambacho sio kingine, ila viongozi na matajiri nchini hapa kuishi kifahari na kwa raha wakati bahari ya masikini, yaani, wananchi walio wengi wakiendelea kuishi katika umasikini na uhitaji wa kutisha.
Pengine ni kwa sababu hii ndio maana nchi kama Tanzania zinaitwa 'mataifa nyanya'. Yanalea vibaya, yanadekeza na kuharibu kizazi kipya. Yanajifanya ndio baba ndio mama na yatawatimizia wote mahitaji yao, wakati ukweli ni kuwa hayawezi na jamii ni muhimu iwe na kiwango fulani cha kujiegemea kwa kutumia nguvu zao na mitaji yao asili. Na leo hii, tuna kizazi cha Watanzania wanaotaka tuishi kama vile tayari wao kwa kuwa viongozi basi eti nchi hii iko kwenye neema. Wamechemsha hapo. Na hawa sio viongozi wanaoweza kuleta mabadiliko ya kweli vijijini kuliko na masikini wengi.
Zipo gharama kwa kila fursa. Ukitumia nusu bilioni kujipongeza basi kuna wanafunzi wanaokosa mikopo, vijana wanaokosa ajira na vijiji vinakosa ama maji au dawa au pembejeo.
Matatizo yetu kwa kiasi fulani yanachangiwa na mifumo mbalimbali kukosa kumbukumbu, kuingiliana, kusuguana na kutegeana kwa hila katika hili au lile ili mtu au kikundi cha watu binafsi kifanikishe maslahi yake hata kama kwa kufanya wananchi walio wengi wanaumia. Bila mihimili ya taifa, yaani, serikali, bunge, mahakama na vyombo vya habari kuwa na viongozi na watumishi wanaojiona sawa kwa kila hali na sio watumiwaji wa wengine sio rahisi kufanikisha azma zetu mbalimbali za maendeleo kijamii, kidemokrasia na kiuchumi.
Kazi za kiongozi wa nchi ambayo inatambua ilikotoka, ilipo na inakotaka kwenda kwa faida ya watu wake wote sio kutetea kama kipofu maslahi ya kundi lolote lile iwe la kisiasa au vinginevyo kuendelea kuwepo achilia kushikilia madaraka fulani. Kama nchi ikiwa na kiongozi wa namna hiyo wakati ambapo mabadiliko katika jamii husika na utandawazi unadai vinginevyo basi huo ndio mwanzo wa kuuana wenyewe kwa wenyewe.
Kazi za kiongozi yeyote katika kipindi hiki ni:
kuhakikisha haki inatendeka kwa wote bila uonevu; kusimamia usawa na kupiga vita ubaguzi;
kuwafanza watu waamini na kuipenda serikali yake
na kujua na kudhibiti tabia za walio chini yake na katikati yake na wananchi
ili kuepusha matapeli na makuwadi wa kisiasa kuiingiza serikali mkenge.
Aidha ni kazi ya kiongozi kuhakikisha shibe ya watu wake wote bila ubaguzi; kuona maji yanatiririka kila mji kila kijiji wakati wote; wagonjwa wanaangaliwa vyema na kutibiwa; wazee, wajane, watoto, mayatima na watu dhaifu wanalindwa kwa hali na mali. Kazi kama hii, kamwe, haiwezi rais ambaye sio imara na madhubuti na wakati huo huo ni mwenyekiti wa chama cha kisiasa nchini.
Nchi ikiwa na miundo na mifumo inayofanya kazi, hata kiongozi dhaifu huweza kuonekana bora. Lakini kinyume cha hivyo, hata kiongozi mzuri anaweza kuonekana kanyaboya na mbabaishaji.
Awamu ya nne ilianza na baraza kubwa sana la mawaziri. Limepunguzwa katika kipindi cha pili cha awamu hiyo. Lakini bado kuna wanaoamini uratibu umekuwa mgumu kama ilivyotabiriwa. Viongozi na watumishi wanakanyagana. Bado tunaamini Tanzania inaweza kuongozwa vizuri tu kwa kuwa na wizara kati ya 12-15. Ziada hapo bora kuwa wakala au programu au taasisi maalum.
Udhaifu hujidhirisha pale viongozi au watumishi wa chini wanapofanya maamuzi bila idhini ya mkuu wao wa kazi; watumishi wa serikali wanapopokea amri kutoka kwa matajiri na sio viongozi wa serikali; baadhi ya watu wanaponufaika na rasilimali za taifa za ziada wanazopata isivyo halali na kisha watu hao kuwaabudu wale wanaowagia ngawira hiyo haramu; pale haramu inapogeuzwa halali; uzito wa kufanya maamuzi magumu pale mwanakundi haramu anapofanya kosa; kiongozi au mkuu wa kazi anapoamini kila kitu kinakwenda sawa kwa sababu ya kusifiwa kiuongo na walio chini yake; kiongozi au mkuu wa kazi anapodanganywa na kufichwa ukweli na kisha kuamini uongo ndio ukweli; taarifa kamili na zisizochujwa kutomfikia kiongozi au mkuu wa kazi.
Aidha udhaifu huonekana pale ambapo walio chini ya mkuu huyo wanapowatumia ndugu, watoto, jamaa na watu wa karibu naye kwa kuwapa kilicho haramu ili wahalalishiwe uharamu au dhuluma yao kwa wananchi walio wengi; serikali husika inapofadhiliwa na matajiri wenye malengo binafsi na sio ukombozi wa masikini; kushindwa kutofautisha maslahi binafsi na yale ya nchi; kushindwa kuelewa hali ya wale wanaoongozwa (kitu kilichonfanya Harun Al-Rashid kutowaamini moja kwa moja walio chini yake, na mara kadhaa kujifanya mtu mwingine na kuranda mitaa usiku ili ajue hali ya watu wake na matatizo yao).
Kundi la watendaji au watekekelzaji walioko kati ya viongozi na wananchi ni kundi nyeti sana. Linaweza kuijenga nchi au kuiangusha nchi. Na kama kuna gamba liliostahili kuvuliwa awali ya yote basi lilikuwa ni kulidhibiti kundi hili ambalo kwa siri au dhahiri linaamua kupora wananchi, bunge na hata serikali yenyewe nafasi na mamlaka yake na kujianzishia serikali nje ya serikali. Huu ndio ukweli wa mambo, kama hatuajauona sasa tufungue macho na kuliona. Kama ofisa wa nchi anajiona ana uwezo kuliko Waziri Mkuu na Bunge na Ikulu inaogopwa kuliko rais anavyoogopwa basi kuna walakini mkubwa mahala fulani.
Sunday, August 28, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment