Thursday, August 11, 2011

Tumebinafsisha visivyostahili kubinafsishwa




BAADA ya zaidi ya miaka 15 ya kubinafsisha vitu mbalimbali Tanzania sio vyote vilivyobinafsishwa vimekidhi matarajio yetu.

Wakati mashirika ya umma yanabinafsishwa watu walitarajia kuona uzalishaji ukiongezeka, ajira zikiwa za kumwaga na umaskini nchini ukipungua. Hivi leo kilichoonekana kuleta matumaini na mategemeo makubwa hakibebeki. Kizito. Kigumu. Na mbele kinachoonekana ni giza tu.

Ingawa kuna mafanikio kwa baadhi ya kampuni zilizobinafsishwa, zipo nyingi ambazo leo ndio sababu ya malalamiko na kilio chetu kikubwa.

Inavyoelekea, hatua la kubinafsisha ilifanywa haraka kutokana na msukumo wa IMF/WB ambao hawakutupa muda wa kuangalia kasoro mbalimbali zilizojitokeza na kisha kuainisha sababu hizo na kuzihakiki na kuona nini na sio tu kubinafsisha kungeweza kuliokoa jahazi letu la maendeleo.

Ninaamini kwamba jambo lolote katika nchi zetu za Kiafrika linalogusa maisha ya walio wengi linahitaji tahadhari kubwa katika uamuzi wa kutaifisha au kubinafsisha. Ni kweli, tunataka Serikali ifanye kazi za kiserikali na uendeshaji kampuni na biashara ufanywe na watu mbalimbali nchini na toka nje, lakini kuna mengine kwa kuzingatia saikolojia ya binadamu sio vizuri kuvibinafisha bila kuwa na mibadala sheria na kanuni zinazoweza kutumika kurekebisha mambo pale yanapoharibika.

Hali inazidi kuwa ngumu zaidi kutokana na Tanzania kutoka kwenye ujamaa na kuingia kwenye ubepari. Viongozi waliojikuta hawana lolote wanachakarika huku na huko ili nao saa kumi na mbili jioni waneemeke na watajirike. Wanachoshindwa kuelewa ni kwamba unaweza ukachuma eneo fulani, mathalani siasa, lakini ukijiingiza kwenye biashara unakwenda na maji.

Pupa hii ya viongozi wa serikali na vyama vya kisiasa, hata hivyo, ndio iliyoiingiza nchi mahala ilipofikia, kiasi cha benki kuu kusafishwa na mafisadi, mikataba bomu kutawala baraza la mawaziri na sasa hata vitu kama UDA kuuzwa kinyemelea ili kuwawezesha wakubwa kuishi maisha ya ukubwa kama ilivyokuwa zamani.

Mojawapo ni eneo la petroli na dizeli au mafuta yanayotumiwa na magari na vyombo mbalimbali vya usafiri na uchukuzi. Kwa maoni yangu, ni vyema shughuli ya uagizaji wa mafuta toka nje au uchimbaji wake hapa ndani ukafanywa kwa ubia kati ya Serikali na kampuni au nchi za nje. Serikali katika nafasi yake ina uwezo wa kununua kwa bei za sasa na za baadaye na kisha kuhifadhi mafuta kwa wingi wa kutosha kuiepusha nchi kuyumba kutokana na kupanda bei ya mafuta au kupungua kwake katika vipindi vifupi kutokana na hali ya uzalishaji mafuta hayo na bei yake katika wakati husika.

Uuzaji mafuta ndani ya nchi unaweza ukafanywa na watu binafsi na kwa kuwa Serikali ndiyo mwagizaji mkuu ni rahisi kuratibu na kupanga bei wakati wowote. Tunachohitaji ni mameneja waadilifu na wazuri ambao hawataingiiwa na wanasiasa katika kazi zao.

Ni muhimu pia kwa serikali na hususan TASAF kuingia maeneo ya mjini na kusaidia kuwawezesha wananchi kuanzisha miradi ya kijamii ikiwemo ya usambazaji na uuzaji rejareja wa petroli ili kupunguza makali ya sekta hii kushikwa mia kwa mia na watu binafsi.

TAFICO ilianzishwa ili Watanzania wapate kitoweo cha bei nafuu. Haieleweki ni katika mazingira gani shirika hili linalohitajika kufa na kupona na wananchi liliuzwa. Lakini sinema inayoendelea leo, iwe ile ya Samaki wa Magufuli au Samaki toka Ujapani zinazohofiwa kuwa na mianzi ya 'yuraniamu' ni matokeo ya uongozi na nchi ambayo imeshindwa kutunza kitu ambacho kingetunza nchi na watu wake na pengine hata kulinda lishe na afya yao. Haliingii kichwani kwa mtu wa pwani au maziwani kushindwa kibiashara kazi ya uvuvi. TAFICO lilikufa tu kwa sababu wakubwa waliliingilia kisiasa kama yalivyokuwa mashirika mengine yaliyokufa. Mashirika mengi yaliuawa na hayakujifia yenyewe. Na baadhi ya walioua mashirika hayo wapo hai, lakini kwa kuwa walikula na wakubwa na wenye nchi hakuna wa kuwagusa.

Eneo jlingine ambalo ni hatari kwa usalama wa raia na maslahi yao ya kiuchumi ni lile la maji. Serikali haiwezi kukaa pembeni na ikamkabidhi mtu toka nje au ndani ya nchi mashirika yetu ya usambazaji na uuzaji maji na hasa kwa miradi mikubwa ya miji kama Arusha, Tanga, Dar es salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Zanzibar.

Maji ni uhai. Lakini maji pia ni kifo. Hasa yakiwa mikononi mwa watu wasioaminika na wasio na uchungu na maisha ya Mtanzania.

Wote tunafahamu jinsi ambavyo DMT na baadaye UDA lilivyoendeshwa kistaarabu na kwa utu wa hali ya juu. Ilikuwa makosa kugeuza upungufu wa mameneja na watumishi wa shirika hilo kuwa ndio sababu ya kulinyonga shirika hilo. UDA bado linahitajika na ikipatikana fomula ya kuwapata mameneja wazuri hata kama ni kutoka nje; uwekezaji wa wanajamii na mchango wa Benki Kuu na benki nyingine bado jiji hili linaweza kwa mara nyingine kupata usafiri unaoaminika na unaothamini na kuheshimu abiria kuliko ilivyo sasa.

Daladala hivi leo ni mfafhaiko mtupu. Ni jinamizi ambalo kila mtoto wa shule akiliota hawezi kamwe kufaulu vyema. Ni jinamizi ambalo kila mfanyakazi akilifikiria hawezi kuwa na ubunifu au uvumbuizi wa aina yoyote ile.

Haya yote yanatokea kisaikolojia kwa kuwa mtu binafsi anajali yeye apate lakini sio mwingine apone achilia mbali kupata. Haileweki barabara za kasi zinazozungumwa kama ni stori ya Alinacha au ni kitu cha kweli? Palikuw ana porojo ya kutumia reli inayooza yenyewe kwa usafiri wa jiji, lakini Watanzania wanaamini hivi leo wanasiasa wao ni wapiga porojo tu na hakuna kitakachofanyika. Tuombe iwe kinyume cha hivyo.

Watu wengi wanauliza kwamba, hivi serikali yetu ilikuwa na njaa na umasikini kiasi gani kiasi cha kubinafsisha sekta ya uchimbaji madini kwa hasara. Ni dhahiri kuwa tathmini ya utajiri huo haukufanywa ipasavyo na wala haukuzingatia thamani ya ardhi yetu, watu wetu na mali asili zetu.

Haifahamiki ni kwa nini tuliweka Chuo cha Utafiti na Madini hapa Dar es salaam wala kitivo cha jiolojia pale Mlimani wakati wataalamu wake inavyoelekea upo uwezekano mkubwa kwamba hawakushirikishwa kabisa katika uamuzi huu ambao leo ni msiba na majonzi kwa taifa.

Hivi leo unaweza ukiwa na dhamana kukodi sio kununua mitambo ya kila aina duniani. Kukodisha mitambo ni nafuu kuliko kuinunua. Na hili lingefanyika Watanzania leo wangekuwa wanachimba dhahabu yao wenyewe. Isitoshe hivi kuwapa watu maeneo 3-5 kwa mpigo kuchimba madini ilikuwa ni akili au ujinga? Au ndio kuukata kwa wenzetu waliobahatika?

Kuhusu benki, CRDB Bank ni benki pekee iliyobinafsishwa na kuwa na manufaa kwa Watanzania.. Nyingine zimebinafsishwa kihasara na leo hatujui twende wapi wala tukamlilie nani.

Ukitaka kujua nchi iliyochanganyikiwa basi ni Tanzania. Hivi leo eti tunaanza tena kutafutana kuanzisha Benki za wananchi kama vile Community Bank, Benki ya Akinamama, Benki ya Wakulima, Benki ya Wanawake, Benki ya walimu na kadhalika. Hivi hatukuliona hili kabla? Au ni kwa sababu Mtanzania bahili kutoa teni pasenti basi ilibidi tuwauzie wazungu wanaokubali teni pasenti ?

Shirika letu la Ndege nalo limekumbwa na ila hiyohiyo. Kama baba na mwanao unamjua hana uwezo wa kufanya kitu fulani nawe una uwezo wa kuwekeza, basi ni vizuri uajiri mtu mwenye uwezo afanye kazi hiyo na mwanao akae pembeni na kwa kuwa unampenda umpe posho ya kila mwezi au sio?

Aidha, ni vyema kwamba tumeshindwa kuliuza shirika la simu (TTCL), ingawa tumelinyofoa hapa na pale, lakini hili ni shirika ambalo halistahili kuuzwa kwa kuona faida ambayo Tigo, Vodacom na Airtel wanaipata.

Katika tafiti zangu zinazoendelea nimegundua kwamba pamoja na kubinafsisha ulinzi na usalama nchini kwa kiasi fulani usalama nchini umepungua. Sio mimi ninayesema hivyo. Watalii. Pengine ipo haja ya kufanya utafiti kuyakinisha hili. Na utafiti huo usifanyike kijuujuu na kuacha kuona maana pana ya usalama toka kwenye macho ya mgeni au mtalii na sio mwenyeji.

Kwa mtalii, ukosefu wa usalama ni pamoja na kutokuwa na kinga za kuridhisha dhidi ya hali ya hewa, moto, maji na vitu kama hivyo. Kama ilivyo kwa hatari mbalimbali ambazo ulegevu wa sheria zetu za barabarani unamtia mashaka mtalii kutembea mjini kwa kuhofia kugongwa na daladala, bajaji, pikipiki au baiskeli au hata na watembeaji kwa miguu kwa sababu nchi haina nidhamu katika maingiliano ya watu majirani. Aidha kukosekana kwa treni na kubakia magari kama njia kuu ya usafiri ni kitu kinachoupa usafiri na uchukuzi wetu maksi sifuri kiusalama.

Ukosefu wa usalama kwa mtalii ni pamoja na kuwepo kwa nzi mahotelini, mbu vyumbani na maji yasiyoaminika hata kwa kunawia na kuogea.

Nitaliongelea hili peke yake katika makala zangu zijazo. Itosheleze tu kusema kuwa usalama ni zaidi ya mtu kuibiwa, kupigwa au kuuawa.

Ukitembelea mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na Serikali kule Masama au West Kilimanjaro, Mbeya, Iringa na kwingineko utatamani kulia. Ninaamini kwamba bado serikali kwa kushirikiana na Chuo Kikuu chetu cha Kilimo cha Sokoine, Mashirika ya utafiti wa tija katika mazao, mifugo na samaki basi yanaweza kugeuzwa kwa namna ambayo yakaendelea kuwa ni shule kwa wakulima, wavuvi na wafugaji wetu wadogo ili wawe wakubwa kesho na keshokutwa.

Silo la kuhifadhia nafaka nazo ninasikia lakini sina uhakika kwamba baadhi yake zimebinafsishwa. Kama ni hivyo, hili nalo ni kosa. Hivi miaka elfu ngapi baada ya Nabii Yusufu kuikoa Misri, sisi Tanzania tunashindwa kuwa na chakula cha kututosha kwa angalau hiyo miaka 7 tu?

Baadhi ya nyumba na majengo ya serikali yamebinafsishwa sawa na kutolewa bure. Pengine kwa kuwa walionufaika ni kina mama zetu wakubwa, watoto wetu, ndugu, jamaa na marafiki. Lakini tukumbuke hizo ni mali za serikali na kufanya hivyo ni kuwadhulumu watu wengine. Dhuluma inayoendelea kupandwa juu ya dhuluma nyingine ambayo inaweza kuwa sababu ya kuchangia nchi hii kukosa mwelekeo na dhamira ya kweli katika kuwaondoa watu wetu kwenye umaskini.

Tumetaifisha viwanda vingine, lakini kinachoendelea ni kwa waliowekeza kuuza mitambo yote na kisha kugeuza viwanda hivyo kuwa bohari zao za biashara na ubebaji mizigo. Hiki ndicho tulichoazimia. Na kwa nini hatua huzichukulia. Au mikataba iliwaruhusu watu kama hao kufanya lolote lile watakalo?

Hivi leo, eti tunazungumzia kuanzisha viwanda kama vile hatukuwa navyo kabisa. Mbona tunachezeana akili na 'intelligence' yetu ya kuzaliwa jamani? Au wote tunaonekana kuwa na akili fupi kiasi hicho, kiasi cha kutokumbuka mambo ambayo yametokea katika miaka isiyozidi ishirini tu iliyopita? Ninapendekeza kabla ya kugusa kodi ya Mtanzania kila aliyebinafsishiwa kiwanda achunguzwe kwanza na akionekana kafanya ndivyo sivyo arudishe majengo, mitambo na vifaa vingine ili wanajamii chini ya uongozi wa nguvu ya umma waweze kuvifufua viwanda vyetu. Hatuwezi kukubali kuibiwa kila upande, juu, chini, kulia, kushoto na kadhalika, tutakwisha, tutasambaratika kama nchi.
Lazima tuwe na dhamira ya kukaa kuwa soko la wengine. Ndio tuagize tusivyovitengeneza, lakini tutengeneze vyetu navyo viende kwenye masoko ya nje.
Ni kukosa tafakuri na usononi wa maendeleo ya watu na nchi yetu, kuzungumzia nchi haina ajira za kutosha wakati majengo ya viwanda tulivyovijenga hivi leo yanatumiwa na wahuni wachache kufanya kile wanachokijua wao wenyewe.

Changamoto zinazobakia kwetu baada ya kutambua tumebinafsisha vilivyokuwa havistahili kubinafsishwa, ni kujipanga kimkakati na kuanza kuwa na visheni na dira mpya ya kimaendeleo. Mambo yatakayotulazimisha pamoja na mengineyo, kutokutegemea nchi za nje kwa mahitaji yetu yote. Na kilele chake kitafikiwa pale sisi kama taifa tutakapojenga uwezo wa kujitosheleza kwa vitu vyote vinavyohitajika kila siku au mara kwa mara na hususan katika uzalishaji mali, usafiri na huduma mbalimbali. Bila hivyo, ndege ya maendeleo ya Tanzania haiwezi kutembea kwenye 'runaway' achilia mbali kuruka juu. Viongozi watainigia, watatoka, wataingia -watakula na kuondoka na nchi itabaki palepale kimaendeleo au kiumaskini!

No comments:

Post a Comment