YAPO mengi tunayoweza kuzungumza kama njia za kumuenzi Baba wa Taifa, Julius K. Nyerere miaka 12 baada ya kifo chake. Binafsi ninaamini haya nitakayoyaorodhesha hapa chini yanaweza kuwa ni changamoto ambazo kwazo tunaweza kumuenzi kikwelikweli kiongozi huyo wa Afrika na siyo Tanzania pekee.
Kitu cha kwanza, ni kuirithi na kuiboresha visheni aliyokuwa nayo baba taifa kuhusu Tanzania na Afrika na nafasi yao katika dunia hii ya ubepari na utandawazi.
Mwalimu anatarajia kuwa viongozi wa nchi hii waliotangulia na wa sasa, watachangia sio haba kuleta umoja wa Afrika Mashariki na wa ule wa Afrika na kwamba katika maeneo hayo yote, Tanzania, itakuwa mstari wa mbele na sio vinginevyo. Tuliyoyaona hivi karibuni ni kinyume cha hivyo. Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuenzi na kufuata na pengine hata kutetea maslahi ya nchi kubwa duniani kama vile Marekani na Uingereza; na ya mwisho katika kuenzi na kutetea yale yanayohusu wananchi wa Afrika, lakini mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya viongozi fulani wa Afrika, hata kama viongozi wao wanawatendea isivyo haki wananchi wao. Siamini kama jambo hili linamfurahisha baba wa taifa huko aliko. Nyerere aliwaweka wananchi wa Afrika mbele na sio viongozi wao! Maana alijifunza mengi kutokana na viongozi wababe wa Nigeria, Uganda na Kongo.
Utu, uungwana, ubinadamu na kutopenda makuu ni baadhi ya sifa alizokuwa nazo baba wa taifa. Inatia mashaka kama sifa hizi bado zinaenziwa na viongozi wetu walioko madarakani na viongozi wastaafu. Na matokeo yake yanaonekana kila kona ya nchi, nayo ni yale wananchi kukosa imani na siasa na wanasiasa kiasi cha asilimia chini ya 30 ya wananchi wa Igunga wanaostahili kupiga kura kujitokeza katika zoezi hili. Hapa kuna mambo na wala sio jambo. Ni vizuri viongozi walioko na waliokuwepo enzi hizo wajichunguze, wachunguze wengine na wachunguzane ili kujua kama kile tunachowatendea wananchi wa Tanzania kinaleta jumla na majibu yanayokubalika au tunawapotezea tu wananchi wakati wao.
Azimio la Arusha lina mambo mengi ambayo kwayo Mwalimu Nyerere anaweza akaenziwa miaka mingi baada ya kizazi hiki kinachotawala na kitakachotawala baada ya kuondoka duniani. Mambo hayo ni pamoja na kuenzi elimu ya kujitegemea; kuzuia kukua kupindukia kwa tofauti kati ya walionacho na wasionacho kiutawala na kikodi na sio kimaguvu; kuwapa uhuru wakulima na wazalishaji mali wengine; kufufua kisomo cha watu wazima; kujenga siasa za demokrasia ya kijamii ambayo inawaruhusu watu kuwa na sauti kuliko serikali kuu; na kuwaendeleza vijana wa Kitanzania kushika nafasi zao wanazostahili kama viongozi wa dunia katika miaka ya ubepari na utandawazi.
Maendeleo vijijini. Baba wa taifa aliwajali sana wakulima na wanavijiji. Ingawa jaribio lake la kuanzisha vijiji vya kisasa kupitia ujamaa vijijini lilishindwa, siyo yeye aliyeshindwa bali ni Watanzania na hususan viongozi waliomfuatia. Wakati vijiji vya ujamaa vya Israel 'Kibutz' leo ni vijiji vya kisasa na kivutio cha utalii kikubwa nchini, swali ni, je, waliomfuatia Nyerere waliamini na wanaamini kwamba vijiji bado haviwezi kuendelezwa kwa faida ya wanavijiji na nchi kwa ujumla, maana maneno ni mengi kuliko vitendo pale suala la maendeleo vijijini linapozungumziwa. Ninaimani kwamba bado maendeleo vijijini ni ufunguo wa nchi hii kutoka nchi ya ulimwengu wa nne na kuwa nchi ya angalau ulimwengu wa tatu.
Madaraka mikoani. Mwalimu tofauti na viongozi waliomfuatia na waliopo alitambua kwamba kadri Watanzania wengi wanavyoelimika na kufunguliwa macho na teknolojia mpya basi watazidi kudai haki na uhuru wa kutawala mambo yao wenyewe. Kwa kulitambua hili ndio maana akaanzisha sera ya madaraka mikoani kwa maana kwamba sio mikoa tu bali pia wilaya, tarafa na vijiji na kata vingelikuwa na maamuzi ya mwisho kuhusu jinsi ya kuendesha kiuchumi na kijamii maeneo yao bila kuingiliwa bila sababu na serikali kuu. Hivi sasa, inaelekea kwamba pamoja na kubadili majina na mbwembwe za kila aina mipango na sera inayozingatia kiukweli madaraka mikoani hamna na mambo yanajiendea tu kwa kudra ya Mwenyezi Mungu. Hili lina hatari kubwa ya shinikizo la mabadiliko sasa kutoka kwa wananchi wenyewe, na hasa pale serikali itakapoendelea kuchelewa na kukosa msukumo wa sio tu kupanga bali kusimamia na kudhibiti zoezi zima la madaraka mikoani kwa faida ya wakazi wa miko na nchi nzima.
Mojawapo ya sifa kubwa aliyokuwa nayo Baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kuwachukulia wanawe wa kuzaa kama sehemu ya wanawe wa kutawala. Wakina Anna, Rose na Madaraka hawakuwazidi kitu watoto wengine wa Kitanzania. Kinachojitokeza sasa si hivyo. Na hili kila mtu analijua na hatuna sababu ya kuliongelea na hususan katika chama tawala ambapo tunaona dhahiri mashindano ya baadhi ya viongozi kuwarithisha watoto wao uongozi wa chama na pengine nchi bila kujali wana uwezo au hawana uwezo. Tungevuta hatua moja nyuma na kutafakari yale yanayotokea huko Uarabuni na jinsi nchi yetu inavyoweza kuathirika kama baadhi ya wazazi viongozi wataendelea na msimamo na mtazamo walio nao sasa.
Elimu. Nyerere alichukulia elimu kama haki ya kila mtoto wa Kitanzania. Alijua nchi ni masikini. Na wale waliopewa elimu kwake walifananishwa na wanavijiji kwenye vijiji vyenye njaa waliopewa chakula chote na kijiji ili kwenda kijiji cha mbali kutafuta chakula cha kuja kuwanusuru watu wake. Mtazamo na msimamo wetu hivi leo ni tofauti. Kwa Watanzania wengi hivi leo elimu ni ufunguo wa kuzidisha ubinafsi wao na kujionesha wao, watoto wao na familia zao ni bora kuliko za Watanzania wengine. Na elimu na malezi ya watoto leo yanaelekea pengine kutokana na sera ya ubinafsishaji kubinafsishwa zaidi kwa madhara makubwa baadaye kwa taifa na mustakabali wake.
Kiongozi anayeona giza tu katika handaki la elimu ana tatizo. Kwa kuwa anaona giza hawezi tena kuongoza watu wakaiona nuru.
Kwa kuwa elimu haina mwisho, tatizo sio wingi wa wenye digrii mbili, madaktari na maprofesa bali kile watu hao wanachopangiwa ili kuitoa Tanzania kwenye nchi ya ulimwengu wa nne na kuifanya nchi ya ulimwengu wa tatu.
Uchumi uwe mikononi mwa Watanzania. Kama kuna jambo ambalo Nyerere alisikitika kutokuliona basi pengine ni lile la kuona uchumi wa Tanzania ukiwa chini ya Watanzania wenyewe na sio chini ya wawekezaji na wageni toka nje tu. Kumuenzi Nyerere lazima viongozi na nchi iwe na mipango na sera zinazolenga 'kuutanzania' uchumi na maendeleo yetu kwa kiasi kikubwa zaidi.
Kubwa zaidi ni lile la elimu tunayoitoa kulenga kutatua matatizo ya Watanzania na sio vinginevyo. Ni kichekesho hivi leo kuwa na wasomi wasiojua kutengeneza kitu chochote tunachokitumia, wahandisi wasioweza kutengeneza barabara wala reli wala madaraja; wahandisi umeme wasioweza kujiunga wakatatua matatizo ya umeme ya Watanzania; wahandisi wa maji wanaoshindwa kutupa huduma ya kuridhisha ya maji; wahandisi wanaoshindwa kutujengea bandari na viwanja vya ndege vizuri na salama na vyenye kufanana na mazingira na utamaduni wetu na kadhalika.
Teknolojia, sayansi na kwenda na wakati. Nyerere alienzi sana sayansi na teknolojia na hususan kwa maendeleo vijijini. Ili kumuenzi ni lazima tuhakikishe kuwa teknolojia na sayansi zilizopo nchini hivi leo zinarahisishiwa kufika na kutumiwa huko vijijini kwa faida ya Wanavijiji na wakulima na nchi kwa ujumla.
Jamii na Kujitegemea. Sifa ambayo hakuna kiongozi mwingine wa Tanzania amewahi kuipata ni ile ya Nyerere kuwa kiongozi pekee aliyetambua kwamba hatuwezi kutegemea fedha kwa maendeleo yetu. Kwa maneno yake mwenyewe: Fedha sio msingi wa maendeleo! Ni kwa kutambua hili ndio maana mwalimu akawa anapigia debe sana mchango wa hali na mali toka kwa wananchi katika maendeleo yao wenyewe. Serikali inayojiweka katika nafasi kwamba inaweza kuwafanzia kila kitu Watanzania sio serikali inayowatakia mema Watanzania. Inakotupeleka ni kule ambako leo Ugiriki inakokanyaga. Je, huku ndiko tunakotaka kwenda?
Mali asili, madini na uwekezaji. Mwalimu angelitamani sana kuona maliasili yetu, madini na majaliwa mengine yanatumika kwa faida ya Watanzania wote na sio kwa faida ya wawekezaji wachache, mangimeza wa serikali na vibarakala wao. Hali ilivyo hivi leo, hili linaonekana kuwa mbali sana na viongozi wetu wote, wastaafu kwa waliopo wanaokena zaidi kujali kujinufaisha wao na jamaa zao na sio Watanzania wote kwa ujumla kwa hatari na mikosi mingi isiyostahili kabisa kuwepo.
Umoja wa Afrika wenye maslahi ya wananchi na
sio ya viongozi wabovu kulindana. Kama mwanzilishi wa Umoja wa Afrika siamini kama mwalimu alitaka AU iwe klabu ya viongozi wazuri kwa wabaya kulindana na kupeana muda zaidi kuwagandamiza Waafrika wenzao. Mtazamo na mategemeo ya mwalimu yalikuwa kuona nchi za Kiafrika zikitawaliwa na viongozi wenye uchungu na wananchi wao na wasiotumiwa na viongozi au nchi za nje kuwanyonya na kuwagandamiza watu wao. Mwalimu akifufuka leo atasikitika kukuta hata zile nchi zilizosaidiwa na Tanzania kuwa huru na viongozi waliosomeshwa hapa Tanzania wamo katika mkumbo wa uroho wa madaraka, udikteta na kuwanyonya, kuwatesa, kuwadhulumu na kuwagandamiza watu wao.
Kama kuna kitu kitakachomkasirisha Baba wa taifa ni kukuta Tanzania ya leo ina viongozi wa juu wa kitaifa wastaafu ambao pamoja na usomi wao kwa sababu za kibinafsi wanaoendeleza siasa za kichama na wanajiingiza kuvuruga umoja na amani ya taifa hili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment