Sunday, September 25, 2011

Elimu: Jamii na serikali muhimu kushirikiana kwa maendeleo zaidi.

UUNGWANA, pamoja na mambo mengine ni kuona na kusifu kile ambacho mmojawetu ameweza kukifanikisha katika maisha yake kwa faida ya wanajamii wenzake. Mojawapo ni mchango wa serikali katika maendeleo ya elimu hususan ule ambao umechangiwa na uongozi wa awamu ya nne toka uingie madarakani 2005.

Hakuna kilicho kamili katika dunia hii. Ndio maana mafanikio katika sekta ya elimu nchini hivi sasa yanaibua mijadala mingi inayobainisha udhaifu na kasoro zilizopo, wingi wa mawazo na mapendekezo mbalimbali juu ya nini kifanyike na kadhalika.

Mafanikio yaliyopatikana katika elimu Tanzania hadi wa leo, yanaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa na zaidi ya watoto milioni 1.5 katika shule za msingi, milioni moja katika shule za sekondari na laki mbili au tatu katika vyuo vikuu kila mwaka. Kinachotakiwa ni kujipanga vizuri kwa kukuza ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wanajamii kwenye maeneo shule au vyuo vilivyoko.

Elimu kama zilivyo sekta nyingine inahitaji rasilimali watu bora zaidi; majengo na rasilimali zisizo hai, safi, nzuri na bora na zinaboreshwa kila siku; uongozi au menejimenti bora zaidi kila siku; mafanikio makubwa zaidi katika matokeo ya kazi za watumishi katika sekta husika na matokeo mazuri ya kimasomo kwa upande wa wanafunzi.


Katika baadhi ya nchi za Kiafrika kama ilivyo kwenye nchi nyingi zinazoendelea, tabia moja mbaya sana imekuwa ikikubalika bila kuhojiwa na tabia hiyo kwa kiasi kikubwa inachangia zaidi matatizo kuliko kupatikana kwa ufumbuzi wa matatizo. Inadumaza maendeleo ya watu na jamii, wakati mwingine hata wakubwa wa nchi bila kujua kinachoendelea.

Tabia hiyo siyo nyingine ila ni ile ya serikali na chama tawala kujifanya ndio taasisi pekee zenye uwezo wa kifedha, kiufundi, kiutaalamu, kimamlaka na kirasilimali kuwezesha jambo lolote kufanyika na kwamba eti wanajamii hawana uono au uwezo kama huo ambao chama tawala na serikali yake walio nao.

Huu ni uzushi, utapeli, ulaghai na uongo mtupu. Wanaostahili kuwa na uwezo, fedha na rasilimali ni wanajamii wenyewe kupitia kodi zao mbalimbali zinazowezesha kuwepo kwa serikali. Serikali kama yalivyo makundi mengine katika jamii ni kundi la watu wa matumizi na hata wakati mwingine matanuzi yasiyoisaidia kitu jamii.

Upo ulazima wa kuwaelimisha watu juu ya ukweli huu, uwezo, nguvu na rasilimali walizonazo na jinsi utofauti katika hili unavyoweza kuwaondoa wananchi kutoka hali ya uhitaji na unyonge na kuwaweka sio tu kwenye nafasi ya kujitosheleza katika mahitaji yao ya msingi bali pia katika nafasi nzuri na isiyoterereka ya kuhoji utendaji, ufanisi na ufanifu wa serikali, viongozi wake na wa chama tawala.

Ili uamsho huu uweze kufanya kazi na kuzaa matunda yanayotarajiwa ni muhimu kwa taasisi zisizo za kiserikali na wanaharakati wote kwa ujumla kuwa na programu za kuwaamsha wananchi kwa kuwabainishia kuwa wao ndio wenye uwezo wa kubadili maisha yao na vizazi vyao na sio vinginevyo. Na rasilimali zote za nchi zinastahili kuwa zao na zinazochangia kuleta mabadiliko tarajiwa.

Si haki nchi iuze almasi au dhahabu au ardhi yake kisha wananchi wadanganywe kwa pipi, halua, chandalua zenye dawa na kondomu!!!

Ili sekta ya elimu iweze kupata mafanikio ni lazima wazazi waambiwe, watambue na wakubali kwamba wao binafsi wana mchango mkubwa katika shule na vyuo vilivyopo. Na kwamba ili mchango huu uanze kupatikana na kufanya kazi ni lazima wawe na taasisi, uongozi, mifumo na taratibu zinazofanya kazi. Bila hivyo, itakuwa sio rahisi kwa uwezo na nguvu waliyonayo kuonekana dhahiri, kukubalika na kuheshimiwa na washikadau wengine ikiwemo serikali, wahisani na taasisi binafsi na za kidini.

Kwa mfano, hivi leo panahitajika haraka sana: 'Taasisi ya Wazazi wenye Wanafunzi Mashuleni na Vyuoni' kuliko wakati mwingine wowote huko nyuma ili kutetea na kulinda maslahi ya wazazi na watoto wao wanaosoma katika taasisi mbalimbali ikiwemo usalama kwenye taasisi hizo, ubora wa elimu, mafunzo na walimu au wahadhiri, ubora wa malazi, ubora wa vyakula, usalama wa maji na haki na uhalali wa ada na gharama nyingine zinazolipwa ili wazazi kupuka kutapeliwa na shule za msingi, shule za sekondari, vyuo na vyuo vikuu feki au vibabaishaji.

Jamii inaweza isiridhike na shule na vyuo vilivyopo na ikaamua kuwekeza na kuanzisha shule na vyuo vyake ambavyo vitakuwa bora zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. Jambo hili si jipya duniani. Baadhi yaWamarekani walipoanza kuchakachua elimu na kutoa elimu isiyohitajika na soko la ajira, jamii mbalimbali za KImarekani zilianza kuanzisha shule za msingi za kijamii na kisha wakaanzisha sekondari na vyuo vikiuu vya kijamii na hivi leo taasisi hizo ni kati ya zile zinazong'ara nchini Marekani.

Lakini ilimradi vile vilivyopo vinajikusuru, basi ni vizuri zaidi Taasisi kama hiyo ya wazazi wenye wanafunzi wanaosoma ikawepo ili kusimamia, kushinikiza na kutoa chachu ya mabadiliko, ukuaji na maendeleo kwa taasisi zote za elimu zilizopo.

Ni muhimu pia serikali kutambua kwamba haina ubavu, nguvu, rasilimali na mitaji ya kutosha kuweza kufanya kila kitu peke yake kwa yote yale wananchi wanayoyahitaji. Kwa namna moja au nyingine, lazima ikiri hadharani, kama ilivyofanya kwa kuinyima ukiritimba TANESCO, juu ya lile lililoonekana kushindwa kuendelea kwa serikali kulibeba achilia mbali kulifufua shirika hilo na hivyo kufungua milango kwa watu wa ndani na nje kuwekeza katika uzalishaji, usambazaji na uuzaji umeme kama soko huru linavyotushuritisha.

Ndivyo inavyotakiwa pia kwa serikali mapema iwezekanavyo

kutoa wito kwa wananchi kila inapowezekana kuwekeza, kuendesha, kusimamia na kusaidia shule zilizopo kwenye maeneo yao kwa faida ya nchi na watu wake. Kwa maneno mengine, serikali inapaswa kutamka bila kusita kwamba wazazi na wanajamii kwa ujumla wana sababu, uwezo na shuruti ya kusaidia kwa hali na mali, maendeleo ya shule za kata na nyinginezo ili kuboresha sio tu hali za shule husika bali pia utawala au menejimenti na matokeo ya mitihani ya shule husika kimkoa, kitaifa na kimataifa. Shule, kwa maneno mengine, 'sio shule za serikali tu' ni shule za wananchi au wanajamii wa maeneo husika.

Wanajamii ndio wanaoweza kusifanya zifanye vizuri na kufanikiwa au kuziangusha. Upo ushahidi wa kutosha kwamba ushiriki wa wanajamii katika usimamizi na uendeshaji wa shule huchangia sio haba kupunguza matatizo mbalimbali yanayokabili shule, walimu na wanafunzi.

Na kwamba mchango wa hali na mali wa wanajamii katika maeneo hayo unahitajika na unakubalika. Wanajamii wakishirikiana na walimu au wahadhiri na wakuu wa taasisi husika wanaweza 'wakakomisheni 'tafiti mbalimbali ili kuona nini kinachoendelea, kisichostahili kuwepo na ukubwa au upana wa pengo lililopo na mabadiliko yanayotakikana,ili kuongeza ubora katika sekta ya elimu kwenye maeneo mbalimbali.

Baadhi ya mambo ya kutafiti na kufanyia kazi ni pamoja na je, Idadi ya masomo yaliyopo ni sahihi? Mitaala na silabasi zilizopo zinakidhi haja zetu? Je, masomo hayo yana manufaa kimaisha? Je, yatamsaidia mwanafunzi wa leo kuja kujiajiri au kuajiriwa? Je, sio vyema wanafunzi
kuchagua masomo machache kuendana na kipaji, uwezo wa mwanafunzi na kile anachokipenda kuwa katika maisha yake hapo baadaye?

Aidha ni lazima kupata majibu kwa maswali kama, je, alama za kiwango cha kufaulu ni sahihi na cha haki?
Je, kurudia darasa kiwango cha kufaulu kisipofikiwa sio jambo zuri na kwa faida ya mwanfunzi kuliko kuwa na mwanafunzi anayeingia darasa la pili lakini hana uwezo wa mwanafunzi wa chekechea ?
Je, idadi ya wanafunzi darasani ni sawa? Je, idadi ya walimu waliopo katika shule ni sawa? Je, muundo na mifumo iliyopo inaruhusu viranja, viongozi na wasimamizi wa shule kufanya kazi bila uonevu au upendeleo? Je chakula, kifungua kinywa, maji na lishe ya wanafunzi inaendana na hali ya maisha leo? Je, majengo na huduma stahilivu yana viwango vinavyokubalika na vinaendelea kuboreshwa kila siku, au shule au vyuo havina sera ya uchakavu na majengo yao yanatisha na kusikitisha? Na, je, mtoto wa Kimalawi au Kizambia au Kikongo au Kirundi au Kinyarwanda achilia mbali Kiganda na Kikenya anaweza kujiunga na shule au vyuo vyote na wazazi wake wakaridhika kwa elimu na huduma za msingi atakazopata?

Je, unyapara na hususan ule wa ukaguzi katika sekta ya elimu sio kitu chema na kinachohitajika wakati wote?

Na ni kwa mikakati na mbinu gani zinazoweza kutumika ili kuboesha kipato cha walimu na maupurupu yao bila kuwalazimisha kutafuta njia za mikato na zisizo na tija kitaifa na kijamii?

Je, katika jiji kama Dar es salaam kupanga ratiba za masomo ya shule za msingi na sekondari kuanza saa 12 alfajiri na kukoma kwenye saa sita au saba hakutapunguza tatizo la kunyanyapaliwa wanafunzi na wenye daladala na hivyo kuathiri maendeleo ya darasani na kwenye mitihani ? Na je, kuwa na kalenda ya shule na vyuo vyote katika elimu kwa masomo, likizo, sikukuu mitihani, michezo, michuano ya michezo mbalimbali, safari za kimasomo, muda wa masomo kwa vitendo, ukarabati, ukaguzi, ununuzi na usambazaji wa vitabu ni jambo litakalosaidia maendeleo ya elimu au la?

Je, kupunguza masaa ya shule au kuyagawa kati ya mafunzo na michezo hakutachangia kumkuza mtoto kimwili na kiakili kwa mapana na marefu zaidi?

Je, wanajamii wenye elimu, ujuzi, maarifa na uwezo mbalimbali ambao sio walimu hawawezi kufanyiwa utaratibu wa kusaidia kufundisha pale kusiko na walimu wa kutosha?

Haya ni baadhi ya masuala ambayo yanaweza kuzungumzwa, kufanyiwa utafiti na makundi husika ya shinikizo katika elimu kuiwajibisha serikali iliyopo madarakani kufanya yale yanayohitajika na yanayowezekana bila ulegevu, uoga, uvivu, ubabaishaji, 'usiasaishaji', au ucheleweshaji wa aina yoyote? Ni kwa namna hii tu ndipo tutakapoweza kutoa majibu sahihi kwa changamoto zilizoko katika sekta ya elimu na mafunzo nchini kwa faida ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.Baba wa Taifa, J.K.Nyerere alituasa fedha si msingi wa maendeleo. Yapo yawezayo kufanywa kwa fedha na yapo yanayoweza kufanywa kwa utashi, akili, bidii, juhudi na nguvu za wanajamii husika.
Tukitegemea fedha kwa kila kitu hatutafika mbali.

No comments:

Post a Comment