Friday, December 16, 2011

CUF na hatima ya upinzani Tanzania...

WATANZANIA mnamo mwaka 1990 waliupokea mfumo wa vyama vingi kwa matumaini makubwa ya mageuzi na mabadiliko chanya katika mfumo wao wa kisiasa, kijamii na kiuchumi. Awali CUF kilihofiwa kuwa chama chenye udini, akheri, ni dhahiri inaweza kuwa au isiwe hivyo, ila kilicho wazi ni kuwa CUF baada ya muafaka ni chama cha Kizanzibari zaidi na sio cha Kitanzania, achilia mbali kuwa cha Kitanganyika.


Watu wengi waliamini mfumo wa vyama vingi utaleta ushindani wa kweli katika siasa, uchumi, teknolojia, utamaduni na rasilimali ziendazo kwa wanajamii ili kila mtu na kila jamii ipate kilicho bora kabisa na sio kitu hafifu, dhaifu na vilivyochakachuliwa.

Hata hivyo, ushindani katika sekta nyingine ulitegemea sana kuwepo na mafanikio ya ushindani wa dhati na wa kweli katika siasa. Ushindani huo katika siasa hadi hivi wa leo haujafika, haujaonekana na kwa siasa zilizopo ndani na nje ya chama tawala haionekani kama utapatikana kwenye awamu hii.

La kusikitisha ni kuwa siasa za mfumo wa vyama vingi Tanzania zimeiga neno kwa neno siasa za Kimarekani zinazotawaliwa na wenye fedha, na wasio na fedha kuwa wasindikizaji kama sio wanunuliwaji. Na kinachopandwa hakiashirii mema kwa nchi hii na watu wake hapo baadaye.

Kubwa tunalojifunza hapa ni kwamba kutokana na kukwamishwa kuwepo kwa ushindani wa kweli wa kisiasa ndani na nje ya bunge, viongozi wetu wanawapotezea wananchi muda na nafasi nyingi na nyinginezo za kuondokana na umaskini wao kwa kutumia fursa na changamoto ambazo aghalabu huzaliwa tu katika mfumo wenye ushindani wa kweli kisiasa. Hili linapaswa lionekane na lieleweke na wote, waliomo kwenye upinzani na wanaoongoza chama tawala hivi sasa ili maamuzi yanayofaa yafanywe kwa faida ya nchi na watu wake.


Ilitegemewa kuwa vyama vya upinzani vingekuwa vingi, lakini kuna viwili au vitatu vitakavyoungana na kukipa changamoto ya kutosha chama tawala. Kiasi ambacho chama tawala kisingeweza kufanya maamuzi yoyote ya maana kiurahisi bila ushirikiano na vyama vingine na kuwaelimisha na kuwaridhisha wabunge au wawakilishi wake kwenye mazungumzo mbalimbali.

Kinachoonekana leo, hata hivyo, ni kuongezeka vyama vya siasa visivyo na kichwa wala miguu, huku vile vilivyokuwepo vikizidi kudhoofika kwa njia moja au nyingine.

Zipo sababu mbalimbali zinazotolewa kuhusu udhaifu wa upinzani. Baadhi ya viongozi wa vyama tawala wanaamini kwamba vyama hivyo vimeanzishwa kwa shinikizo la IMF na Benki ya dunia, na hili pengine linaathiri mahusiano ya chama tawala na vyama hivyo kwa chama tawala kuona ndicho pekee chenye ridhaa na uhalali kwa wananchi lakini sio vya upinzani.

Aidha, vyama vingi vya upinzani pamoja na sheria ya kuvilazimisha kuwa na wanachama angalau 200 katika angalau mikoa 10 ni vyama vilivyokosa mizizi ya kweli mijini na vijijini na vinaishi kwa kubangaizabangaiza tu. Wakati hili linatokea chama tawala kwa kushika funguo za hazina na kuwa katika nafasi ya kufanya maamuzi kadhaa kwa manufaa yake, hakina dhiki kama hiyo, ila pale kinapoingizwa mkenge kama ilivyotokea kwenye suala la rada.

Kutokana na chama tawala na viongozi wake kuwa na uwezo wa kifedha (ambao hatuna uhakika na chimbuko lake, maana hakionekani kuwa na miradi ya maana ya kukiingizia kipato na wanachama wake wengi sio walipa ada wala watoa michango mikubwa) kimetumia njaa na umaskini wa vyama vya upinzani kwa manufaa yake kwa njia mbalimbali, ambazo hatuna sababu ya kuingilia kwa undani zaidi hapa. Pamoja na hayo kutokana na siasa kuitwa mchezo mchafu tumeshuhudia mambo ambayo yanatia mashaka kuhusu ukweli na uhalali wake katika maeneo mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimaendeleo kwa ujumla.

Kisiasa kwa mfano tumeona baadhi ya vyama vikisingizia vingine udini, wakati ndivyo vinavyolea udini kwa mlango wa nyuma; tumeona uoza na ufisadi ukiswafishwa na kuitwa utakatifu; tumeona wabunge wakizomewa na kukashifiwa kwa kuwa na msimamo fulani; tumeona wabunge wakitumiwa kwa manufaa ya chama na serikali na siyo ya wananchi; tumeona watu wakisingiziwa uongo na wengine kujiita na kutaka kuonekana watakatifu na kadhalika; na juu ya yote tumewaona wanafiki na wasioitakia nchi yetu mema wakijifanya wao ndio wenye uchungu mkubwa kabisa na nchi yetu kuliko watu wengine.

CUF na Zanzibar....

Baada ya kukerwa na ugomvi wa ndugu wa Unguja na Pemba, sisi sote tulivuta pumzi na kushukuru Mungu na tukafata wahenga waliyosema: ' Ndugu wakigombana, chukua kisegerema chako uende kulima; na ndugu wanapopatana, chukua kapu lake ukavune!'

Hebu turudi nyuma kidogo, hata hivyo, je, CUF kiliundwa makusudi na mahsusi kwa ajili ya muafaka wa Zanzibar? Au nini kilichotokea?

Pamoja na ukweli kwamba cham hicho kilistahili kuwa na wanachama 200 katika kila mkoa angalau kwa mikoa 10 Tanzania bara na visiwani ni vipi chama hicho kikamezwa kabisa na Wazanzibari? Kiasi kwamba kama chama hicho hakikuhusiswa na Uzanzibari na Upemba kilikuwa kikihusishwa na Uislamu kwa heri au shari ?

Je, katika hali ambayo tunayo leo, yaani, kuwepo sio tu muafaka bali pia serikali ya Umoja wa Kizanzibari, ukweli hauonekani kwamba chama cha CUF hakikuwa chama cha Tanzania bali cha Kizanzibari?

Iweje baada ya viongozi wa Kizanzibari kupewa ubunge na vyeo mbalimbali katika serikali yao ya Umoja wa kitaifa harakati zao za kisiasa kama upinzani unaotarajiwa kuwa imara katika kuikabili CCM bara kudhoofu na kuwa hoi bin taabani?

Katika matukio ya kitaifa na hususan Bungeni, tumeona watunga sheria wa CUF kwa heri au shari wakiunga mkono au kupinga moja kwa moja lolote lile ambalo Chama tawala liliunga mkono au kupinga ?

Na hivi Hazina, Tume ya Uchaguzi na Msajili wa vyama vya siasa wanastahili kulipa CUF na CCM kama chama kimoja au vyama viwili kwa hali kama hii?

Wamasheria wanasemaje kuhusu CUF hapa Tanzania kama ni chama cha Upinzani au chama tawala au chama kilicho katikati ya hayo ?


Na Watanzania waliohadaiwa na wapanda mabasi ya muafaka wakidhani wanapelekwa kwenye upinzani imara na wa kweli wana kila haki ya kushuka na kupanda basi jengine.

Vijana wa chama ambacho kimefikia kuwauza bila wao wenyewe kujua wanauzwa ili viongozi wachache wa chama hicho wapate ukubwa na sio maendeleo ya watu na nchi yao sio laiki yao kukaa kimya labda wakose kiongozi wa kuwafungua macho na kuwaongoza kwenda kule wanakosatahili kuelekea na sio vinginevyo.

Maana ya kuwa na upinzani nchini haiwezi kubadilika. Upinzani unahitajika kama njia muhimu ya kisiasa kwa wanasiasa wa mrengo fulani kupimwa kiuwezo, kufuatiliwa, kudhibitiwa na kutathminiwa kimatendo na kimatokeo kama na wanasiasa wenzao na wananchi kwa ujumla kama wanaweza au hawawezi kazi waliyoiomba.

Huu ni mfumo ambao ukiutumia vibaya unaweza ukairuhusu nchi kutawaliwa na kuendeshwa na chuya na pumba wakati nafaka zimetupwa jalalani. Au kwa upande mwingine mfumo wa vyama vingi ni mfumo unaoweza pia kuchangia sio haba nchi kuwa na viongozi safi, wenye uwezo, wenye nia ya kujenga nchi na watu wao na wenye mitazamo na dira za kimaendeleo zinazohitajika kufikisha nchi na watu wake kule wanakotaka kwenda.

Upinzani hauwezi kustawi kama katika nchi husika bado watu wana wasiwasi kwamba upinzani ni uasi, vita na uhaini. Ni lazima watu na hasa vijijini waliko wananchi wengi wakubali kwamba mfumo wa vyama vingi ni kitu kizuri na anayeutega au kudhoofisha ni adui wa nchi na watu wake. Na kwamba upinzani si ubaya, si uasi na sio vita wala uhaini. Na kwamba vita na uhaini hutokea pale demokrasia inapohujumiwa na wale walioko madarakani kukataa kushindwa na kuwanyima washindi haki yao kwa njia halali au haramu.

Juu ya yote upinzani hauwezi kujengwa na wazee ambao daima wanalilia kupewa nishani ili watambuliwe kwa kile kisichotambulika wala kueleweka. Upinzani wa kweli utajengwa na vijana waliofunguka macho na wanaotambua kwamba nchi hii haiwezi kujengwa kwa kuigeuza shamba la bibi kama sio la nyanya, ila kwa mikoa na wilaya za nchi hii kujiendesha kama makampuni huru yenye visheni na misheni ya kile kinachostahili kuzalishwa, kuundwa au kuhudumiwa kwa ufanifu na ufanisi wa hali ya juu kwa kasi ambayo itatuwezesha kuuaga ulimwengu wa tatu kwa haraka zaidi kuliko tunavyotarajia.

No comments:

Post a Comment