Friday, December 16, 2011

Tusipoangalia demokrasia yetu inaweza kuwa wizi….

SI MTU mwingine ila baba wa ukomunisti, Karl Marx ambaye miaka zaidi ya 120 alitahadharisha kwamba demokrasia kama ilivyokuwa katika nchi za Magharibi ni mfumo wenye udhaifu, mapungufu na kasoro nyingi.

Alionya kwamba demokrasia isipodhibitiwa na wananchi wenyewe ikaachiwa kwa wajanja wachache katika jamii inaweza kugeuka wizi wa mchana kweupe na wa kutisha ambao umehalalishwa na una nguvu za kisheria.

Kiasi ambacho jambo likishaamuliwa huwezi kulipinga kwa kutumia sheria ila kwa njia nyingine.

Alidai wale wanaoitwa wawakilishi wa wananchi wanaweza kuamua kupiga kura ya 'ndiyo' ili kuifagia na kuisafisha hazina au Benki Kuu ya nchi ikawa nyeupe na isibakiwe hata na shilingi moja kwa ajili ya matumizi yao binafsi.

Nina wasiwasi kama huko sio kwa mfumo tulionao leo, wa demokrasia ya chama kimoja iliyojificha ndani ya mfumo wa vyama vingi kama sio tunakokwenda.

Hakuna anayepinga wabunge kupata posho na maslahi zaidi na hata kufanya israfu na kufuru ndogondogo. Kwa mfano, wabunge wenzao wa Kenya wameidhinisha bunge lao kununua viti vipya vya bunge kwa mabilioni ya fedha za Kenya. Kiti kimoja kitakuwa chanunuliwa kwa takriban shilingi milioni tatu. Piga hesabu kwa viti zaidi ya mia tatu bungeni uone mambo hayo. Tofauti na Tanzania viti hivyo havitoki nje vitatoka magereza ya Kenya ambako kuna maseremala wenye hadhi ya kimataifa. Lakini huu ni uwakilishi wa walio nacho kuwawakilisha wasio nacho, ambao wanaamini ili kufanya kazi zao vizuri na kwa starehe lazima anasa na starehe nazo ziingizwe hadi bungeni kwa namna moja au nyingine. Na matajiri kumbukeni hawatopenda wawakilishi wenu waonekane kuteseka au kuwa na maisha ya dhiki au kufanya kazi katika mazingira magumu, kwa hiyo mkiwaruhusu au msipowaruhusu wao watawafadhili bila shida. Ili kuepukana na aibu hii na fedheha ya kufadhiliwa na wenye pesa basi gharama hizo huonekana ni za lazima na zisizoepukika.



Maswali ya kujiuliza

Swali kuu la kujiuliza ni kigezo au vigezo gani vinavyotumika kihistoria na kimapokeo na katika mazingira na hali halisi au muktadha uliopo hivi leo ? Swali hili linazaa maswali yafuatayo:

. Wabunge wetu wana umuhimu na utakatifu gani wa kustahili kulipwa vizuri kuliko madaktari, wahadhiri, wahandisi, walimu, manesi na watu wengine kama hao?
. Hivi kweli hiki tunachokiona katika luninga, yaani, bunge la kusifia na kujisifia na kujipalilia na bunge la NDIIIIYO.... ndicho Watanzania watakachokubali kwacho wabunge kulipwa kihalali na sio kidhulumati ?
. Hivi bunge letu kazi yake ni kutatua matatizo ya wananchi na kuwawezesha wananchi wetu au kazi yake ni kuwapatia fursa wabunge ya kutumbua na kutanua?
. Je, badala ya kuwa na bunge moja tukawa pia na bunge la makundi ya kimaslahi, yaani, bunge la pili muda wa vikao hautafupishwa kiasi wabunge wakashughulikia matatizo yetu badala ya swahifa na swahifa za maneno na porojo?
. Hivi kila mkoa ukiwa na waziri wake mkuu, mawaziri na wawakishi wake nao wakashughulikia moja kwa moja mipango na bajeti zao bunge au mabunge ya kitaifa hayatahitaji tu wiki moja kila baada ya miezi mitatu kuzungumzia mambo makubwa ya kitaifa badala ya utaratibu wa sasa unaotudumaza badala ya kutukuza?
. Hivi na wanaopiga porojo, wanaolala, wanaozomea na kupiga vigelegele nao wanastahili posho hii?

. Mfumo wetu wa bunge hivi unalandana na ule wa kikoloni au kibepari ambao umejengwa katika hoja kuwa watu ni matajiri na sio masikini au vipi?

. Huko Malasyia viongozi wakiwemo wabunge walijipa miaka kadhaa ili kwanza wawatoe wananchi kutoka kwenye umaskini wa kutisha na kisha ndio wabunge wakaanza kulipwa vizuri na kutanua, je, wabunge wetu wanapoanza kwa kutanua kuna uwezekano wowote kweli kwa sisi kukombolewa kiuchumi na kijamii? Wanakubaliana na falsafa ya wabunge wa Malaysia au hawajaona ndani? Ukizingatia hulka au saikolojia ya binadamu, tuna ubavu wa kuifikia Malaysia hata 2100 kwa namna za posho kama hizi za wabunge wetu ?
. Kuna uwiano gani kati ya kile wabunge wanachofanikisha kiuchumi na kijamii kwa wananchi na kile wanacholipwa ?
. Je, uwezo wetu wa kukusanya kodi na kipato chetu cha kila mwaka unaturuhusu kulipa posho hii?
. Je, mabilioni ya fedha yatakayolipwa kwa namna hii hayawezi kuwekezwa kwanza katika mradi utakaozalisha ili posho hiyo itokane na kinachozalishwa na sio kuiingizia hazina shimo jipya la kuchotwa fedha kila mwaka? Hivi wabunge wetu wana akili za uwekezaji au wanazisikia tu na wanataka wawe nazo wananchi lakini si wao wenyewe?
. Je, kwanini mhadhiri, mwalimu, polisi, daktari na nesi nao wasipate posho kama hii? Hasa ukizingatia mazingira magumu wanayofanya kazi na majukumu watumishi hawa waliyonayo kwa wananchi wenzao ?
. Je, uwezo wetu wa kiakili unatufanya tujali faida au manufaa makubwa zaidi kwa idadi iliyo kubwa zaidi au kinyume cha hayo?
. Ni miradi mingapi mbadala ambayo ingesaidia watu wenye kipato cha chini kuondokana na umaskini inakwamishwa kwa hatua hii?

Sababu za baadhi ya wabunge kuridhika na hili

Wabunge nao ni binadamu na mahitaji yao yanaongezeka kutokana na ukubwa walio nao na tamaa zao za kifahari licha ya umaskini wa watu wao; wanataka kulimbikiza ili kushinda uchaguzi ujao; uwakilishi unakuwa fursa ya wao kunyanyuka kiuchumi kama sio kutajirika kirahisi zaidi na mfumo uliopo unatumika kuwanunua bila kujua ili wawasaliti wanaowawakilisha na kutetea walioko mamlakani hata katika yale yanayowahujumu wawakilishwa wao. Aidha katika mfumo ambao wizi wa kura umehalalishwa kinyemela na mbunge hachaguliwi ila kwa kugawa fedha kwanza, wawakilishi hulazimika baadaye kulipa madeni ya watu au kudunduliza tena kile kilichokuwa akiba yao walichokitumia ili wapate kura za wananchi.

Kwanini wabunge wanajisahau
. Wabunge ni binadamu na katika mfumo unaostawi kwa ubinafsi wa kichama na umimi, ubinafsi hauonekani ni kitu kibaya;
. Wabunge walio wengi hawaingii bungeni kutetea maslahi ya wengine ila kulinda na kuendeleza maslahi yao binafsi na jamaa zao;
. Katika mfumo ambao umekwaza na unakinza fani na tasnia nyingine (k.m. mishahara njiwa kwa wahadhiri, walimu, manesi na madaktari ) kimshahara au kiujira, kimasurufu na kimaslahi matokeo yake ni wengi kukimbilia siasa hata kama hawapendi siasa na wanaziona ni uchafu kwa sababu ya fedha au kipato na siyo kwa sababu ya wito;
. Wabunge hawachaguliwi tena kama wawakilishi na watetezi wa wanajamii fulani bali kama watumishi wa chama fulani;
. Mawasiliano kati ya wanaowawakilisha na wabunge huisha mara baada ya mbunge kuchaguliwa;
. Mbunge hafanyi kazi zake ili wananchi wake waneemeke na kutajirika bali kukisaidia chama chake kurudi tena madarakani;
. Nguvu ya serikali na vyombo vya serikali hutumika kukijenga chama tawala na kuvidhoofisha vyama vingine na kutokana na udhaifu wa vyama vingi wabunge kuamini kuwepo kwao kisiasa kunategemea chama tawala kushinda;
. Baadhi ya vyama vingine nyongeza ya posho inapotolewa asilimia kubwa haiendi mfukoni kwa mwakilishi bali kwa chama husika, yaani, nyongeza ya posho ni mlango mzuri wa kustawisha udokozi wa vilivyo vya serikali ili kuwajenga wanasiasa na vyama vyao, na;
. Wawakilishi walio wengi hawaujui umaskini wa wanaowawakilisha. Na wengi huishi katika ukale badala ya kuangalia hali halisi iliyopo hivi leo majimboni mwao.
Majibu ya maswali hayo hapo juu na mengine kama hayo nina hakika ndiyo yatakayoamua hatima ya wabunge na wanasiasa wetu na mustakabali wa nchi yetu bila kujali masuala ya itikadi, msimamo, mtazamo, chama na serikali iliyopo madarakani.


Tanzania tuitakayo

Tanzania tuitakayo haiwezi kupatikana kwa kuwa na wabunge walioshiba na wasiyemjua mwenye njaa, na wakuu wa mikoa wanaokokota badala ya kuongoza mikoa; kwani wao bado waamini wana njaa pia; kwa kutanguliza mbele ubinafsi badala ya jamii; na bwabwaja wa kuzungumza lakini wachache wa vitendo; na vyama na wanasiasa ambao wanajilinganisha na matajiri na kuishi kama wao kama sio kuwapita; na wanaotetea maslahi ya chama au serikali badala ya wananchi wao; na wenye fedha wanaoingia bungeni ili kutajirika zaidi na sio kuwanyanyua wanaowawaklisha; na watu wanaokubali kutumiwa na wengine kwa manufaa ya wengine na sio ya watu wao; na watu wasiojua nchi ilipo na inapotakiwa kwenda.

Ninaelewa maswali hayo hapo juu sio rahisi kuyajibu achilia mbali kuyajibu kwa haraka sana. Ila yanadhihirisha kitu kimoja, muswaada wa katiba si 'blue' wala 'green' wala 'white' paper ya serikali unahitaji muda na wasaa kuusoma na kuutafakari. Na kwamba kama wanaharakati, kazi yetu moja kubwa ni kuitumia katiba ama kuondoa vipengele vyote vinavyowapendelea kiujira na kimaslahi wale wasiozalisha na kuwakamua wanaozalisha kwa upande mmoja na kuviingiza vipengele vipya vyote vinavyohitajika ili kuondokana na dhuluma hii ya kiujira na kimapato ilioyoanzishwa na wakoloni, kulelewa na watawala wetu wa jana na sasa na likachukuliwa kama msahafu au biblia na lisilogusika au kurekebishwa na watawala wetu wa leo. Muktadha huu si msahafu, si biblia na mapinduzi hayaepukiki ili tuwe na Tanzania yenye usawa, haki, utu na ubinadamu zaidi. Tanzania mtu anayelipwa kwa kigezo cha kile alichokisomea na kuhitimu na sio kwa kubebwa kisiasa bila hoja na sababu za msingi. Mungu tusaidie!

No comments:

Post a Comment