NI DHAHIRI suala la kuishi au kuhama mabondeni, hususan Jangwani, ni
suala 'lililosiasaishwa' na haiwezekani chama kilichoko madarakani na
serikali kuwahamisha wakazi wa maeneo haya kwa nguvu kama nguvu
inavyotumika sehemu zingine kutokana na kuhitajika kwa mtaji wa kisiasa.
Haiwezekani pia kidira, kisera, kifedha, kiteknolojia na kiuwezo kwa Dar es
salaam ambayo ni pua na mdomo na bahari kuwa na miundo mbinu
itakaloliwezesha jiji litapike maji yote ya mvua yaende baharini kama tu
imeshidwa kutapisha maji taka na ya matumizi ya kawaida kwenda baharini.
Ugumu wa hili umedhirishwa na kauli zinazopingana juu ya kuhama au
kutokuhama mabondeni zinazotolewa na viongozi wa serikali na chama
tawala. Haiwezekani katika muda mfupi na siamini kama suala hilo limo
katika kipaumbele cha serikali. Je, kiuhalisia kinachobakia kushauri ni kitu
gani ? Nitajaribu ingawa ninajua ni mtihani mkubwa kufanya hivyo katika
makala yangu leo. Ila kama kawaida tutarajie amri zisizotekelezeka na ahadi zisizotimizwa.
Kipindi cha pili cha awamu ya nne kilianza kwa bishara njemba katika
angalau za masula ya nyumba na makazi, lakini kadri muda unavyokwenda
imedhihirika kuwa hizo zilikuwa ni nguvu za soda tu.
Biashara hizo zilitokana kwanza na kuteuliwa kwa mwanamke aliyeswahi
kushika wadhifa wa juu katika shilrika la masula ya nyumba na makazi na
kauli zake za mwanzo ambazo zilionekana kama angelikuwa na uhuru wa
kufanya yale anayofikiria kichwani kwake leo angalau tungelianza angalau
kuona ishara za kuwa na mipngo miji katika nchi ambayo kwa mapana na
marefu na kwa ujumla yake ilikwishazika kabisa suala la mipango miji na
ujenzi uaoangalia na kutahadhari na yanayoweza kutokea kesho na kesho
kutwa.
Jambo moja linalochangia udhaifu katika utawala na menejimenti yetu ya
nyumba na makazi ni sheria za kubembelezana na kuvumiliana. Na siku hizi
umezuka mtindo kuwa pakijengwa kijiwe cha chama tawala mahala fulani,
basi mahala hapo panahesabika kuwa sehemu ambayo hata kama sheria
zimevunjwa, hazikuvunjwa!
Hizi ni siasa za kutafuta kupendwa na umaarufu, huku mtu akijua fika kwa
kuruhusu kinachofanyika kiendelee kufanyika basi mwisho wake ni zahama,
dhiki na vifo kwa wale wanouhurumiwa na kvumililiwa. Ninaamini wakati
umefika kwa nchi yetu kujenga heshima ya kuwa na utawala wa kisheria
ambao haushawishiwi vinginevyo na wanasiasa kwa malengo yao binafsi.
Pamoja na ujenzi wa nyumba mabondeni ipo mifano mingi ya kimaafa
maafa tu inayosubiri cheche moja tu, moto au bomu kulipuka.
Mifano hiyo ni pamoja na vituo vya zima moto na upatikanaji maji kuwa mbali
na maeneo ambayo janga la moto linaweza likazuka.
Manispaa mbalimbali za maji zimeruhusu au kuachia watu kujenga kuta au
vizuizi vya aina mbalimbali ambavyo vinaweza vikachangia si haba ukubwa
wa maafa na hasa yale ya maji na mafuriko.
Tembelea sehemu mbalimbali za jiji la Dar es salaam na utakuta makumi
kama sio mamia ya vituo vya petroli ambavyo vimejenga kando ya masoko
au ndani ya makazi ya watu.
Watalii mbalimbali hivi sasa wanahofia kuja Tanzania kutokana na
kukosekana usalama wa kutosha mabarabarani . Jambo linalosababishwa
na malori, daladala, bajaji, pikipiki, mikokoteni na vyombo vingine vya
uchukuzi kutofuata sheria zilizopo na kukosa uungwana na ustaarabu katika
maingiliano ya watu njiani.
Aidha, kumekuwa na kauli kadhaa za kisheria zisizotekelezwa juu ya hili au
lile, mojawapo likiwa ni amri inayokataza watu kuishi mabondeni toka zama
za Mzee Makamba alipokuwa mkuu wa mkoa wa jijimkoa.
Nchi haiwezi kamwe kujengwa kwa siasa za kujipendekeza, kutaka
kuonekana wema na wazuri na wengine wabaya na unafiki mwingine kama
huo. Ni lazima tufike mahala ambapo sheria zetu zinalinda na kutunza roho
za watu, kisha utamaduni, imani na mali za watu . Mengine ni uzandiki wa
kisiasa ulio na melngo binafsi dhidi ya yale yanayostahili kuwa ya umma.
Ninaamini, wakati tunatoa michango yetu kuhusu katiba yetu mpya itulinde
vipi tokana na wale tunaowapa ukubwa tutahakikisha kuwa ulinzi na
usalama wa roho za watu, utamaduni na mali zao unapewa uzito
unaostahili.
Kama azma yetu basi itakuwa ni hivyo ni dhahiri kubainisha hapa kwamba
huwezi ukalinda na kuthamini maisha ya wananchi wako kama wewe kama
serikali na mkusanyaji mkuu wa kodi na mirabaha unashindwa kuwapatia
wananchi unaowaongoza mahitaji yao ya msingi. Mahitaji hayo ya msingi ni
pmoja na nyumba na makazi bora na salama.
Nyumba kama hitaji la msingi
Kichekesho kwa wazungu na wageni wengi wanaotembelea nchi hii ni pale
wanapokuta kuwa kila Mtanzania ana mradi wa kujenga nyumba. Pengine
hawaelewi umasikini na kudunduliza kwetu na jinsi tunavyozaliana kwa
wingi, lakini bado ukweli unabakia pale pale wengi wanatushangaa
wanapoona badala ya kujenga vitu vya kututajirisha tunajenga vitu vya
kutumasikinisha.
Ukiweka siasa pembeni, nyumba ni hitaji la msingi la kila mwanadamu.
Inasemekana baada ya chakula na maji basi nyumba ni muhimu kuliko kitu
kingine. Kutokana na ukweli huu, serikali iliyokuwa makini haiwezi
kulichukulia suala hili kimzahaha mzaha au kuliona ni mzigo na kulisukuma
ili libebwe na watu wengine. Bila watu kuwa na nyumba bora na salama hata
kama watajishughulisha na mengi mazuri katika uzalishaji na ujenzi wa
nchi, fumba na kufumbua, siku moja vyote vinaweza kuoshwa au kufagiliwa
mbali na maafa ya aina hii au ile.
Serikali inayoona mbali na mbele, kwa hiyo, huwa inachukulia suala la
mipango na mikakati ya nyumba na makazi kama jiwe la msingi la
maendeleo la taifa na watu husika. Inafanya hivyo, kwa kuzingatia kuwa vita
vyote vingine vinavyokabili watu wake vikiwemo vile vya ujinga, njaa, maradhi
na umaskini ni vita vitakavyokuwa rahisi sana kuibuka kidedea kama
washindi wasioshindika.
Katika muktadha huu, hoja yangu hapa ni kwamba tusianze kumwaga
machozi ya mamba huku tukijua fika kwamba siasa zetu za kujipendekeza
zimechangia si haba kuwapotezea Watanzania wenzetu ambao kama sheria
zingelikuwa zinawalinda na rasilimali za nchi zinatumika kuwanufaisha wao
na sio vinginevyo hivi leo wasingelikuwa marehemu.
Ninasema hivyo, kwa kudhihirisha kuwa ulegevu na urojorojo wa seriikali
yetu ambayo kwa kushangaza sana inakuwa na nguvu ya kupambana na
waandamanaji toka vyama vya upinzani au wafuasi wa dini fulani
wanapotaka kuandamana au kuwasekwa ndani na kuwashtaki waandishi wa
habari kwa kutumia sheria za kidhalimu na kikoloni na zilizopitwa na wakati
kwa sababu tu waandishi hao wa habari wameandika kisichowafurahisha
wanasiasa walioko madarakani unachangia si haba nchi hii kuwa na
matatizo ya kila namna, kutokuendelea na kupiga maktaimu wakati watawala
wakidanganywa na takwimu na taarfifa za wapambe wao kwamba mambo ni
saaafii.
Mradi wa kuondokana na makazi ya mabondeni
Mathalani, kama serikali yetu ingelikuwa haifanyi kazi kisanii, basi mara tu
baada ya kutangaza marufuku ya kujenga na kuishi mabondeni
nilichotegemea kuona ni serikali hiyo kujenga nyumba za angalau chumba
kimoja na ukumbi kwa familia husika katika maeneo mengine na kisha
kupitia benki na taasisi nyingine za fedha, misaada na ukopeshaji kurejesha
gharama zake kwa kuwalipisha wananchi masikini kwa kiwango
wanachoweza kulipa hadi deni lao liishe. Je, tunakumbuka mikopo ya miaka
25 hadi 50 ya Benki ya Dunia kwa watanzania miaka ya huko nyumba.
Serikali yetu kwa kutumia utajiri, madini, mali asili zetu na kodi zetu hivi
inashindwa kufanya jambo kama hili au haina nafasi na watu wake ambao ni
maskini? Utaratibu huu utaendana hata na matarajio ya katiba ya kiutawala iliyopo na
utaanza kujenga kutoa fursa sawa kiustawi ili kuleta uwiano na usawa wa
kimaendeleo miongoni mwa Watanzania.
Hitaji la nyumba na makazi kama hitaji la msingi likishatoshelezwa, kinachobakia ni kwa wananchi kujiingiza katika ushindani mbalimbali wa kujiendeleza kielimu, kikazi, kibiashara, kihuduma, kisanaa, kimichezo na kadhalika na kuwa bora zaidi nchini na
duniani.
Kwa maneno mengine, safari ya kweli na dhati kuelekea kwenye
maendeleo ya Watanzania inakuwa ndio imeanza na sio vinginevyo.
Nyumba zilizo kwenye maeneo safi, bora na salama zitachangia sio haba
kuwapa mamilioni ya Watanzania utulivu wa akili na kiroho. Ni kitu
kitakachorahisisha miingiliano ya kijamii na kupatikana kwa huduma za
utumaji na upokeaji barua kupitia makasha nyumbani na sio ofisi za posta
mbali na waishipo watu. Hali kadhalika, kuishi kwenye makazi salama, mandhari nzuri
na yanayopendeza vitawapa Watanzania moyo wa amani, utu, huruma na mapenzi zaidi.
Na kubwa zaidi litawapa Watanzania nafasi kubwa zaidi ya kujiheshimu na
kujithamini na sio kujiona wao sio lolote sio chochote.
Nyumba bora na salama zitawapa watoto wa kimaskini nafasi ya kusoma
katika mazingira bora zaidi na kufanya vizuri zaidi katika shule na vyuo.
Nyumba bora na salama na zenye nafasi zitawapa watoto wa makini fursa
ya kuwa watundu, wenye kujaribu na wazua ujasiriamali wa kila aina siku
zote daima.
Nyumba bora, salama katika miji ambayo utawala wa kisheria sio tu
unasemekana kuwepo bali kufuatwa kwa herufi na silabi na zenye
kuhudumiwa ipasavyo na huduma zote muhimu za kijaami unaweza
kuifanya Tanzania fumba na kufumbua kuwa chaguo la watalii duniani na
mapato ya utalii peke yake yakatuwezesha kujivua nguo za mitumba ya
umaskini na kuvaa nguo mpya za raia wanaoheshimiwa, kujiheshimu na
kutoa mchango wao muhimu katika maendeleo ya dunia yao na wakati wao.
Kubwa zaidi ni lile la kwamba kuanzia hapo hayo hapo juu
yatakapozingatiwa watu wetu sio tu itakuwa ni rahisi kupata huduma zote
muhimu binadamu anazohitaji, bali kubwa zaidi maisha na mali zao
zitakuwa salama wakati wote.
Thursday, December 22, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment