Thursday, February 21, 2013

Mambo Yatakayonusuru Amani na Umoja Miaka hii na Ijayo..


AMANI na umoja hapa Tanzania una kila sababu ya kuendele kuwepo ili mradi tu mambo yafuatayo yanaheshimiwa,  hayawi tu sera bali yanakuwa vitendo vya kila siku na wote kwa pamoja tukawa tunakataa kwenda kinyume na kauli na ahadi za kitaifa kuhusu masuala husika.
                Kwanza viongozi na raia lazima kujiheshimu, kuheshimu wengine na kuheshimiana. Huwezi ukaendelea kuwadhalilisha wengine au kufanya vitendo vinavyohalalisha kudhalilishwa wengine na wewe ukaamini kuwa utaendelea kuheshimika. Kiongozi yeyote wa Tanzania atakayekubali Mtanzania yeyote kudhalilishwa ndani au nje ya nchi na yeyote yule awaye basi huwa mchangiaji katika hatima ya uvunjikaji amani na umoja wa nchi.
                Mtu mmoja mmoja, vikundi vya watu, wapangaji, wenye nyumba, wenye mji, wanamtaa, wanakijiji na wanamji kwa ujumla wao ni sehemu ya Tanzania. Kila mmoja wao ana wajibu na ana haki zake. Kitendo chochote kinachoruhusu au kuendelea kuruhusu mtu au watu fulani kununua na kuuza haki za wengine ni kitendo kinachonuiwa na kinachodhamiria kuvunja amani na umoja wetu. Kisikubalike
                Uhuru wa kweli kwa mtu mmoja mmoja na makundi au jumuiya ya watu pasina uhuru huo kuingilia uhuru wa wengine. Uhuru ndicho kitu kinachompa uwezo mwananchi au raia awaye kufanya maamuzi kwa kuangalia maslahi yake na kikundi chake bila ya kurubuniwa, kuzainiwa, kununuliwa au kushawishiwa kufanza hivyo kwa pesa au upendeleo wowote uwao. Nchi huru hujengwa na watu huru  haijengwi na watu wa kununuliwa au watumwa wa mtu fulani.
                Kama nchi, Tanzania tunapwaya mno katika medani za ukweli na uaminifu kama watu binafsi na dhamana tunazopewa kutunza na wenzeu. UOngo haujengi nchi, aghalabu uongo hubomoa na kausambaratisha watu, vyama na nchi. Ni muhimu katika uandikaji wa katiba yetu tukarejea suala la kuwa na maadili muhimu ya kitaifa. Maadili hayo pamoja na mambo mengine yahusu: ukweli  kama tabia inayokubalika na wote; uaminifu; usafi wa mazingira, miili na mioyo yetu; uchapakazi na uwajibikaji wa kiwango cha juu; tabia ya kujisomea na kujiendeleza baada ya kumaliza shule/vyuo; kujitolea kusaidia wengine; kujitegemea kama jamii kama hali inaruhusu na ndio njia peikee ya kutatua tatizo la kijamii na kujitahidi kuongoza kwa vitendo na sio porojo na maneno.
                Hali ilivyo hivi sasa ni kwamba kuna matajiri na wakubwa wengine wanaojiweka juu ya sheria na wengi wengine kuwa chini ya sheria. Amani na umoja wetu lazima kufa kama hapatakuwa na usawa mbele ya sheria kwa wote viongozi kwa raia.
                Tusikubali visingizio vya kihaki za kibinadamu na kisheria kukwamisha mapambano dhidi ya rushwa. Kwa vigezo na bishara zote mla rushwa na fisadi huonekana maili kumi toka pale alipo na wala sio siri. Tukiidharau rushwa na kukubali itutawale sisi kama taifa na sio sisi kuitawala rushwa tutakuwa tumeshindwa katika safari ya ustawi na maendeleo ya watu wetu kabla hata ya kuanza safari yenyewe.
Kujilinda na kuwa na maofisa habari na mawasiliano pia wahariri wa habari na waandishi ambao pamoja na  uchanga wao wanajifanya  ni watakatifu na wanajua kilicho bora zaidi kwa nchi na watu wake. Hali katika kufanya hivyo wakawa  ndio wanaopanda mbegu za ushetani na balaa kwa nchi na watu  wake .
-Kupigwa vita rushwa na ufisadi
                Kama hatutaenzi ahadi na amri mbalimbali ambazo ni sahihi na za haki basi kitaifa tutakuwa tunabomoa msingi wa amani na umoja wetu. Baada ya kusema hivyo, ni lazima kwa wakubwa wetu sio tu kuchungua mambo pale tatizo linapotokea bali pia kuchungua kwa makini, kina na mapana malalamiko yoyote nchini ambayo yanaashiria kuwepo tatizo kati ya mtu na mtu au watu na watu. Mambo haya yakichukuliwa kijuujuu yatatufiksha pabaya, kwani yana uwezekano mkubwa wa kuweka umoja na amani yetu rehani katika mikono ya wachache kwa wema au ila.
                Huko nyuma Watanzania walikuwa wepesi wa kuitana ndugu au komredi.  Kuzuka na kukua kwa matabaka kati yetu kumeanza kunyemelea na kuuharibu udugu na ujamaa huo. Ni muhimu kuangalia kwa kutumia njia zozote ziwezekanazo tunarudisha  upendo na kukubalika kwa makundi mbalimbali katika jamii na sio kama hivi sasa ambapo baadhi ya  watumishi wa umma wameanza kuonekana kama maadui na aghalabu wako juu ya sheria za nchi na maeneo mbalimbali. Udugu na mahusiano mema huzaa kile kinachoitwa mtaji wa kijamii. Mtaji huu usipokuweko mbio za manendeleo kwa jamii yoyote iwayo hatima yake ni kuishia sakafuni.
                Tuepuke tabia ya kuwadharau , kuwashusha h adhi na kuwakwaza wengine hadharani pasina sababu ya msingi ila kwa mtu kujipendekeza na kujionyesha kwa wenzake kwamba yeye ni mkereketwa na anayewashwa zaidi kuliko wenzako na hasa katika jambo muktalifuni na lisilokubalika  ukweli wake na watu alimu na wenye uadilifu. Tabia ya kuikweza na kujionyesha wewe safi na bora kuliko wengine hujenga  chuki na inda isiyo na tija. Aghalabu anayejikweza na kukwaza wenzake huonekana mbaya, mbinafsi, adui na huchukiwa na wenigi hata na wale anaodhania wanamshabikia na kumpenda. Maana leo ni yule, kesho aweza wageukia wao.
                Kumezuka tabia ya baadhi ya wanasiasa na matajiri kuwanunua  Watanzania wengine kwa sababu moja au nyingine.  Jambo hili sio tu linarudisha uhadimu kwa watu wetu kupitia mlango wa nyuma bali ni sababu moja kubwa inayochangia kuua na kuumaliza udugu na umoja wetu, kwa kuwa watu wanaonunuliwa ni rahisi sana kutumika kufanya lolote lile liwalo, liwe jema au baya mradi wanalipa deni lao.
                Katika miaka hii ya kugundulika kwa rasilimali mbalimbali nchini upo umuhimu wa kuwa na fomula ya kitaifa itakayogawa rasilimali na mapato yanayotokana nazo kwa namna ambayo kule inakopatikana wanaona wanastahili kupata wanachopata na wengine kugawiwa au kunufaika na kile kinachobakia, ikiwemo serikali na vyombo vyake pia.
                Upo uwezekano mkubwa wa amani na umoja wetu kudumu kama mambo niliyoorodhoshea hapo juu yatafanyiwa maamuzi sio kiimla bali kwa kuwashirikisha wahusika au wabia katika masuala mbalimbali na kufikia maamuzi ambayo yanachangia wote kujiona ni washindi na hakuna mshindwa.
                Kwenye jamii ya mpito kama ilivyo yetu aghalabu umoja hujengwa kwa kuwa na madaraja kati ya walionacho na wasio nacho. Aidha kila kinachoonekana kuwa ni kizuizi katika ukombozi wa wasionacho huwa kinang'olewa haraka kwa faida ya wote.
                Rasilimali zetu ni nyingi na za kutosha. Kinachokosekana ni uongozi, utu na  ubinadamu wa kuweza kutumia akili na maarifa tuliyopewa na Mola ili rasilimali hizo ziweze kutufaa sote bila ya wengine kutengwa na kusahauliwa. Hii ina maana katika sifa kubwa amabyo viongozi wetu kuanzia vijijini hadi kitaifa wangepaswa kuwa nayo ni ile ya kukosa kabisa ubainafsi wenye uharibifu.
                Hatuwezi kuwapata kina Nyerere wengine (watu waliokuwa wanajisahau wao wenywe na familia zao na kumtanguliza mbele Mtanzania kwanza) lakini tukiwa na maadili bora, kupata viongozi wenye kudhibiti ubinafsi wao kwa masalahi ya walio wengii ni kitu kinachowezekana kabisa. Kuna mifano mingi duniani inayoonesha kwamba nchi zilizochipukia na kuwa tajiri katika miaka ya hivi karibuni ziliongozwa na viongozi walionyima wao na kuwanufaisha watu wao kwanza, na sio waliowanyima na kuwakwaza watu wao ili wao wajinufaishe kwanza.
Tanzania katika nchi nyingi za Kiafrika ipo katika nafasi ya kipekee kuendelea kudumisha amani na umoja wa watu wake kama isipofuata msaragambo na kuiga yanayotokea katika nchi nyingine za Kiafrika na kwingineko duniani kwa kuwa na utaratibu wa wazi na usio na usiri katika kuzungumzia mambo mbalimbali yanayoonekana kuwa ni chanzo cha mtafaruku na maelewano kati ya Watanzania katika siku zijazo.
                Tabia ya mbuni haifai kwa nchi kama yetu, yaani, kuingiza kichwa chetu kwenye mchanga, kisha tukajifanya kama vile kwa kuwa hatuoni hatari inayokuja, basi tukifijificha hatari hiyo haitatugusa na eti tukabakia salama. Athari, hatari na matishio mbalimbali  kwa amani na umoja wetu lazima tupambane navyo ana kwa ana.



Elimu, Mitaala na Utatuaji Matatizo ya Watu na Nchi


Nia na madhumuni ya insha hii ni kujaribu kuwashawishi Watanzania kuona kwamba elimu yetu sasa hivi inaendeshwa kwa namna ambayo haina uhusiano kabisa na matatizo yanayokabili nchi na watu wetu.
                Ninavyoelewa mimi sababu kubwa ya kuwepo kwa elimu ni kusaidia kudumisha daraja la maarifa, nadharia, ujuzi na uzoefu wa waliotangulia na wanaowafatia katika jamii fulani.
                Jamii isiyoweza kurithisha toka kizazi kimoja kwenda kingine maarifa, elimu, teknolojia, mila, desturi na utamaduni wake kiujumla inayozikusanya muongo baada ya muongo sio jamii yenye uhakika wa kuwepo na kuendelea kuwepo katika siku zijazo.
                Urithishaji huu unajumlisha pia urithishwaji wa kizazi kimoja na kingine mbinu, njia na mikakati ya kushughulikia matatizo makubwa na madogo yanayokabili mtu mmoja mmoja na jamii nzima kwa ujumla.
                Inaaminika kwamba nusu ya matatizo ya jamii fulani huhesabika yamekwisha au yameishatatuliwa kama jamii hiyo itakuwa inawafunza vijana wake pamoja na elimu nyinginezo elimu ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikablili jamii husika.
                Mafunzo  haya hutolewa sio tu kinadharia bali pia kwa vitendo.  Unapotenganisha nadharia na vitndo katika elimu, basi jamii husika huwa inapoteza jambo muhimu sana katika wakati muafaka na sio rahisi kulipata jambo hilo tena katika siku zijazo.
                Kuna wanaoamini kwamba nusu ya matatizo ya Tanzania yanaweza kwisha kwa kuwa na mitaala inayolenga kutatua matatizo yake ya kijamii na kiuchumi.    
Matatizo ya kimaendeleo yanayowakabili Watanzania walio wengi ni pamoja na uadimu kama sio ukosefu wa maji, chakula na nyumba. Aidha kuna udhaifu katika elimu, tiba na afya kiasi kwamba watoto wa Kitanzania wanaendelea bado kusomeshwa nchi jirani na Ulaya au Asia; wakati huo huo wagonjwa wa Kitanzania wanaendelea kutibiwa
nje.
                Kuna tatizo la kukosa matunzo kwa wazee,  mayatima na watoto wa mitaani.      Vilevile yapo matatizo ya kiulinzi na usalama, uhalifu yanayotishia sio tu usalama wa raia mmoja mmoja bali amani na utulivu katika jamii ikiwemo kuongezeka kwa vitendo vya wivi na ubakaji pamoja na kuwa na sheria kali dhidi ya vitendo hivyo.
                Aidha yapo matatizo katika ujenzi na upanuzi au ujengaji upya wa barabara, reli, madaraja, uchimbaji madini, bandari, viwanja vya ndege na ujenzi wa uendelezaji wa miundombinu mingine.
                Kiutamaduni na Kiteknolojia tuna matatizo ya kuoanisha maendeleo ya teknolojia na mila na desturi zetu ili kupunguza gharama na kurahisisha ufanifu na ufanisi katika maeneo mengineyo ya maisha, kazi, sanaa, utunzi wa vitabu, filamu, michezo na burudani.
                Kijamii na kiuchumi matatizo makubwa ni katika ujasiriamali, mikopo na urudishaji wake, mipango, uratibu, uongozi, usimamizi na udhibiti wa mambo kiutawala, kimaandishi na kiteknolojia.  Hali kadhalika kuna masuala ya menejimenti na uendeshaji bora wa michezo, sanaa na uchumiwa utoaji au uuzaji huduma. Aidha kuna changamoto katika uchimbaji na utunzaji au uangalizi wa visima vya maji, bomba, pampu, mashamba ya kisasa, uvuvi na ufugaji wa kisasa, utunzaji na ulinzi wa wanyama pori, nege na viumbe wengine, matumizi bora na makubwa zaidi ya rasilimali nchi kavu, rasilimali kwenye baharini na kwenye maji kwa faida ya wengi na sio wachache.
                Elimu yetu kwa mapana na marefu sasa hivi imeelekezwa katika kujifunza vitu kama historia, sayansi kama sayansi, uraia, jiografia, hesabu, lugha na mambo kama hayo. Kwa maoni yangu masomo yote yanayotolewa hivi sasa iwe kwa shule za msingi au sekondari yanaweza kuangukia ndani ya masomo matatu makubwa: Maarifa ya Namba na Takwimu; Maarifa ya Kunadika na Mawasiliano na Maarifa ya Maisha, Sayansi na Mazingira.
                Fani hizo hapo juu zikipata msukumo wa kuwekwa kwenye mtandao kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza kama itakavyoandikwa na Watanzania wenyewe ni maeneo yanayoweza kutawaliwa kielimu vyema na mwanafunzi yeyote awaye.
                Hayo kwa upande wangu ndiyo yangelikuwa masomo ya msingi kuanzia chekechea hadi sekondari na yakawa ni lazima kuwepo kwenye kila mchepuo kwenye maeneo hayo.
                Masomo yanayotakiwa kupangwa kama ziada itakayotofautisha kati ya mchepuo wa mweleko fulani na mwingine ni mtatizo yalioorodheshwa hapo juu.
                Kwa mpangilio huo mwanafunzi, mathalani,  katika kundi la kwanza la matatizo ya uadimu na ughali wa maji, chakula, nyumba na kadhalika atakuwa akijishughulisha na kujifunza jinsi ambavyo matatizo hayo yanaweza kupunguzwa au kumalizwa nchini. Ni elimu inayomhakikisha kijana nafasi ya kujiajiri au kuajiriwa kwa sababu elimu hiyo itakazia nguvu zaidi katika vitendo na sio nadharia tu.
                Mchepuo mwingine unaweza ukaelekeza nguvu zake katika kujifunza na kurahisisha kuelewa matatizo ya elimu (elimu nayo pia huwa tatizo na lazima kufunzwa na kufanyiwa tafiti dahari ili kuboreshwa mara kwa mara),  tiba na afya  wataanza kugangana na mbinu, stadi na maarifa za ualimu au ufundishaji na uangalizi au utabibu mahospitalini na katika zahanati mbalimbali nzhini zisizo na watumishi wa kutosha.
                Wanafunzi wengine na hususan katika shule za msingi wataelekezwa kutokan na mapenzi na mwelekeo wao katika kujifunza na kulielewa tatizo la matunzo kwa wazee, wajane, mayatima na watoto wa mitaani ili waje kubobea sio tu katika nadharia bali vitendo vya kulipunguza au kuondosha kabisa tatizo hilo.
                Wale wanaopendelea mambo ya ujenzi na miundombinu wataanza kupigwa msasa toka shule za msingi kwa kujifunza juu ya umuhimu, kazi na faida za  nyumba, barabara, reli, madaraja, visima, bandari na viwanja vya ndege, vituo vya kisasa mipakani na usafiri na uchukuzi kiujumla. Kwa namna hii, mtoto hata akimaliza darasa la saba anaweza kuanza kufanya kazi katika eneo hilo na akawa anajiendeleza katika fani yake pasipokuwa na wasiwasi wa kuchanganya kimasomo au kimitaala. Maana elimu hapa inakuwa ikishughulika na tatizo lilipo, linaloeleweka na linaonekana na kila mtu katika jamii.
                Mcherpuo mmoja muhimu utakuwa ule wa kuwapa watoto kuanzia chekechea fursa ya kuonyesha vipaji vyao katika nyanja za sanaa, kuimba, kucheza ngoma na kukatika viuno, kuigiza, kuchekesha, uchezaji mpira wa vikapu na michezo mingine na mambo kama hayo. Kwa kuwa mtoto anaelekezwa kulekule anakokutaka inakuwa ni rahisi kijana wa Kitanzania kuanza kuonyesha vitu vyake akingali bado mdogo na hivyo kumpa nafasi ya kufanza makubwa zaidi hapo baadaye.
                Mabadiliko ya mitaala katika miaka hii pia lazima iwe na mchepuo wa uongozi, utawala, biashara na menejimenti ya vitu hivyo. Ni vizuri hili likaanzia shule za msingi kiasi kwamba mtoto wa Kitanzania akimaliza darasa la saba anakuwa sawa na mtoto wa Kimarekani aliyesomea B.B.A. au hata M.B.A. (unacheka?) nina hakika hili linawezekana kwa kuwa watoto wa Kitanzania kutokana na mzingira yao magumu wanaisoma na kuilewa dunia haraka kuliko watu wa nje katika hili.
                Mwanafunzi anayemaliza masomo katika mchepuo huu atakuwa na uwezo wa kusimamia biashara ya wazazi wake kwa namna bora zaidi kuliko wazazi  hao, na upo uwezekano mkubwa wa mchepuo huu kuzalisha viongozi bora zaidi kwa vyama, vijiji na taasisi nyingine kuliko hali ilivyo hivi sasa.
                Ninakubaliana na wale wote wanaodai kwamba ilikuwa ni makosa kuondoa elimu  ya ujamaa na kujitegemea mashuleni. Lakini kama ikirudishwa, ninashauri ingerudishwa kwa mapana na kina zaidi kwa kuzingatia ulazima wa kuoanisha matatizo ya jamii leo na elimu inayowapatia watu wake.
                Nionavyo mimi, Vyuo vya VETA vinastahili kuitia makali au kuinoa zaidi elimu vijana wetu watakayoipata shule za msingi na sio kuwa mahala pa kuanzia tu vitu vipya kwao. Nikiwa na maana kwamba shule zetu zote za msingi zinahitaji maabara na karakana za useremala, uashi, umakenika na ufundi mwingine ili ziwe kamili na sio nusunusu kama zilivyo leo. Hali ingelikuwa hivyo, leo tusingekuwa na shule za msingi zisizokuwa na madawati na vyoo vya kutosha, na zenye madarasa na majengo mengine yasiyofikia viwango.
Copyright © 2013 Sammy W.I. Makilla. All Rights Reserved.

Saturday, February 16, 2013

Ujamaa na Kujitegemea Bado una Nafasi Vijijini na mashuleni


KIHISTORIA watu wa mjini hawajawahi kuwa watu wanaotamani na kupenda ujamaa. Miji jinsi ilivyo imejengwa katika msingi wa ubinafsi na kila mtu na lweke. Na kwa miaka mingi ijayo hilo ndilo litakaloendelea kwa ubepari kuwa wenye sura mbaya na makucha makali zaidi.
 Mtu aneyeuchukia ujamaa eti kwa sababu tu Warussi wameutupa na wajamaa wa jana wameanza kukumbatia baadhi ya sera za kibepari ni mtu asiyejua maana halisi ya ubepari. Ni mtu anayehitaji kujitambua na kuijua jamii yake na hasa ile ya vijijini na shida na dhiki zao mbalimbali.
 Anakuwa hivyo kama anavyokuwa kwa sababu anadanganyika na mng'aro wa dhahabu ubepari unaonyesha kwa nje, bila kujua kilichoko ndani wala sio shaba achilia mbali madini ya fedha.
 Tumeshaufungulia mlango, na hakuna namna ambayo tutaweza kuuzuia. Labda, angalau tukubaliane na na kina Raila Oginga na wenzake (watangulizi maarufu katika ubepari) kuwa nchi zetu sasa zinastahili kuwa na sera na dira ya Ujamaa wa Kidemokrasia (Sosho-demokrasia), ha hivyo kupunguza ushetani na makali yaliyomo katika ubepari kwa faida ya wasionacho katika jamii yetu.
 Hata hivyo, hali ya maisha vijijini katika sehemu mbalimbali za Tanzania nilizotembelea na wanakoishi watu masikini na wa kawaida na sio viongozi au jamaa za viongozi kila feli, kila mtihani, kila tatizo na kila fursa inapiga mayowe ya kuwa pasipo ujamaa na kujitegemea miongoni mwa wanavijiji maisha huko tuendako yatakuwa magumu na yasiyo na huruma hata kidogo.
 Hili linakuwa hivyo, kwa kuwa nchi yetu bado haijawa na sera inayomfanya mwanakijiji anufaike na ardhi yake na kile kilichomo ndani yake kama viongozi wa juu wanavyonufaika.
 Aidha, pamoja na kuwepo kwa teknolojia ya habari na mawasiliano bado inawachukua wanavijiji muda mrefu kujua kinachotokea mkoani mwao achilia mbali nchini kwao na duniani kwa ujumla.
 Vilevile, pamoja na kuwa na vitu kama TASAF na NGOs mbalimbali zenye madhumuni na nia ya kuwasaidia wanavijiji kutatua matatizo yao bado  muundo na mifumo ya taasisi hizo imekaa kuwanufaisha zaidi watu wa mjini kuliko wa vijijini.
 Tafiti zinaonyesha kwamba jitihada za kuwaamsha na kuwafunza wanavijiji umuhimu wa ushirika zinaharibiwa na tamaa za viongozi wao na mabepari uchwara wsnaoishi au kuchanganyikana nao.
 Watu wanashangaa kusikia kwamba dhana na nadharia ya ushirikishwaji watu nchini  hapa pamoja na kuleta ufanisi wa aina fulani haikutoka kwenye ile ngazi ya chini kabisa katika ushirikishwaji watu kwa kutumia modeli ya ushirikishwaji watu iliyobuniwa na Mjapani kutoka Chuo Kikuu cha Kobe aitwaye Etsuko Okazaki. Hatua hiyo siyo nyingine ila ni ile ya uanasesere wa kuchezewa na wanasiasa na viongozi wa serikali za mkoa na kitaifa. Hatua za juu katika ngazi hiyo ya ushirikishwaji watu ni pamoja na tiba, kuarifiiwa, ushauri, kubembelewa, ubia, ukaimishwaji na nguvu ya umma.
 Matatizo yanayokabili vijiji vyetu nchini ni pamoja na tatizo la maji; dhikiya chakula na lishe bora; ukosefu wa nyumba bora kwa wananchi walio wengi na uzalishaji mali kwa njia dhaifu na zisizo na ufanifu na ufanisi  wa kutosha. Na kutokana na hili bado shughuli za kilimo, ufugaji pamoja na ule wa nyuki, uvuvi, uchimbaji madini na matumizi ya rasilimali ardhi na bahari kwa ujumla ni dhaifu na zisizowasaidia kitu wanavijiji katika kubadili ubora wa maisha yao na kuwa yenye heri na mafanikio zaidi.
 Matatizo mengine ni kutokuwepo kwa biashara zenye  manufaa zaidi kwa wanavijiji na mwelekeo wa kuchangia kuwafanza kwanza wazalishe kitu na ndio watumie; kutokuwepo huduma za uhakika zinazoweza kupunguza umaskini vijijini k.m. utaalii wa vijijini na wa kiutamaduni; matatizo ya mejengo, vifaa na walimu kwa shule nyingi vijijini; huduma dhaifu ya tiba na Afya vijijini; uadimu wa
umeme na nishati mbalimbali; na
Usafirishaji na Uchukuzi wenye matatizo kedekede na hivyo kusababisha hatari na hasara kwa wanavijiji walio wengi.
 Nichukulie tatizo moja tu nchini-maji. Tatizo hili, ninavyoamini, linaweza kutatuliwa kiurahisi ikiwa wanavijiji wenyewe wanajifunza na kubadilika na kuwa ndio viongozi wa maendeleo yao badala ya kuwategemea watu kutoka kwenye kata au tarafa au wilaya au mkoa au hata taifa kuja kuwasaidia.
 Wenyewe wakishaamua kusimama kidedea inakuwa ni rahisi kuamua,  kupanga na kutekeleza kile wanachokiamua. Na hili huwa ni rahisi zaidi pale wanakijiji wote kwa pamoja wanapokuwa kitu kimoja na sio baadhi yao kukubali kuzainiwa na wale wenye tamaa za uongozi na njaa yao binafsi.
 Huko nyuma nimewahi kupendekeza njia mbalimbali za wanavijiji kupata maji huko waliko vijijini pasina ya kutembea mbali au kuhangaika sana. Njia mojawapo ni kuchimba bwawa pale penye chanzo cha maji  na vilevile kwa ajili ya kutega maji ya mvua badala ya kuyaachia yote kwenda baharini. Njjia nyingine ni kuchimba kisima pale wataalamu wanapothibitisha kuwa maji hayapo mbali na uso wa dunia. Katika sehemu zenye maziwa jirani na wao upo umuhimu wa wahandisi wa Kitanzania kuamka na kuvumbua njia ambazo kwazo  kwa maziwa yaliyo na kina cha chini  wao wanaweza kuchimba  mtaro chini kwa chini na kuvuta maji hadi nchi kavu.  Wale wanaoishi pembeni na bahari huu ni wakati  wa baadhi yao kurudi shule na kujifuna kutoka kwa wenzetu jinsi wanavyobadili maji ya chumvi hadi maji hayo kutumika kunyweshwa mashamba na bustani na kusaidia pia katika matumizi ya nyumbani.
 Ukiyaangalia yote haya ni mambo yanayohitaji vichwa vilivyotulia na watu wanaokubali kwamba changamoto na fursa nyingi walizonazao zinalazimisha kuwepo kwa ushirikishwaji na kujitolea kwa namna moja au nyingine. Na kwamba bila ushirikiano wa walio wengi vijijini ippo hatari kubwa ya vijiji kubaki kama vilivyo hivi leo hata baada ya muongo mmoja ujao.
Maendeleo ya vijiji vyetu yamekwaza na viongozi wetu. Ambao kufatia Azimio la Zanzibar wamekuwa 'bize' kushughulika na mambo yote mengine na sio ujenzi na uendelezaji vijiji. Kwa namna moja au nyingine kwa miaka kadhaa sasa isipokuwa kwa vijiji viongozi wetu wanakotokea vijiji vingine vimeingizwa kwenye kabati kama sio kaburi la sahau.
 Jambo la kushangaza ni kwamba matatizo mengi yanayoikabili miji yetu hivi leo yanasababishwa uongozi kushindwa kutoa msaada na nyenzo (wakati mwingine vimilioni vichache tu) ili kuwawezesha wanavijiji kuhama kwenye umaskini wa kutupwa na kuwa watu wanaojitegemea.
 Kama kuna jambo moja ambalo ningeliwaomba wanaoendesha ukusanyaji maoni juu ya katiba mpya ni kutia shadidi katika kile kifungu kinachozungumziwa uwiano wa kimaendeleo kati ya sehemu moja na nyingine ili pawe na mikakati, sera na kanuni zilizo fasaha na wazi juu ya kushughulikia ujenzi na maendele oi ya vijiji vyetu. Ninazungumza hivyo nikiwa na uhakika kwamba nusu ya matatizo ya mjini yatakuwa yamekwisha kama vijiji vyetu vitatapatiwa angalau kwa kuanzia mahitaji yote ya msingi na ushirikiano kiungozi na kiutawala unaoweza kuwatoa wanavijiji pale walipo na kuwafikisha mahala ambapo sisi  sote wa mjini na vijijini tunaweza kujivunia.
 Jambo moja linalohitaji kupewa uzito wa kipekee hivi sasa ni kuangalia uwezekano wa kuwa na viongozi na watendaji bora wa vijiji bila kujali mtu anatokea wapi.
 Inashangaza kwamba pamoja na kuwa na vyuo vya maendeleo vijijini kasi ya maendeleo vijijini imezidi kwenda chini mwaka hata mwaka. Aidha, elimu inayotolewa na vyuo kama hivyo haiendani na wakati au wanaozalishwa na vyuo hivyo hawaendi kuwa viongozi  wa vijiji bali wanaselea humu humu mjini kama wahitimu katika masuala mengine. Kama ilivyo kwa vijiji basi mengi pia  ya kijamaa na kujitegemea yanaweza kufanzwa  shuleni na vyuoni kwa manufaa ya wanafunzi, wazazi wao na nchi  yao. Hata kama baada ya shule vijana wataamua kufata  ubepari na sio ujamaa.
 Ninaamini kwamba jambo litakalochochea  ari, mwamko na msukumo wa maendeleo kwa watu wa vijijini ni rasilimali watu. Wakati umefika huko vijijini wanavijiji kuwa na viongozi bora na sio bora viongozi.
 Ukweli ni kuwa hata tukiwa na viongozi wazuri kiasi gani katika ngazi za juu  lakini huko vijijini uongozi ukawa dhaifu kupita kiasi hatutaweza kuendelea kiwelikweli.   Jambo hili likiunganishwa na ufanyaji kazi kidhati kwa mashirika yanayosemekana kazi yake ni kusaidia maendeleo vijijini na kisha wanakijiji wakafunzwa namna za kukopesheka kama wawekezaji wanaokuja kupewa ardhi kwenye vijiji vyao wanavyopewa mikopo kiurahisi kwa kutumia ardhi hiyo hiyo, basi maendeleo ya vijiji vyetu hayatabakia katika ruia zetu tu! Aidha, bila kusita wala kutafuna maneno huu ni wakati  wa serikali zetu za mitaa na serikali  kuu kuhakikisha kwamba wale wanaoishi katika maeneo  mbalimbali hapa nchini  wananufaishwa na  na tathmini mpya ya mali asili na rasilimali zao nyingine na  kwamba mali hizo kuanzia sasa zitakuwa zinahesabika kama mtaji wao kieneo na kitaifa na hivyo kuwaruhsu kunufaika kihisa na kifedha na rasilimali kama hizo na isiwe tu wanaonufaika na hili ni viongozi  wa juu na wanasiasa nchini.