Thursday, February 21, 2013

Mambo Yatakayonusuru Amani na Umoja Miaka hii na Ijayo..


AMANI na umoja hapa Tanzania una kila sababu ya kuendele kuwepo ili mradi tu mambo yafuatayo yanaheshimiwa,  hayawi tu sera bali yanakuwa vitendo vya kila siku na wote kwa pamoja tukawa tunakataa kwenda kinyume na kauli na ahadi za kitaifa kuhusu masuala husika.
                Kwanza viongozi na raia lazima kujiheshimu, kuheshimu wengine na kuheshimiana. Huwezi ukaendelea kuwadhalilisha wengine au kufanya vitendo vinavyohalalisha kudhalilishwa wengine na wewe ukaamini kuwa utaendelea kuheshimika. Kiongozi yeyote wa Tanzania atakayekubali Mtanzania yeyote kudhalilishwa ndani au nje ya nchi na yeyote yule awaye basi huwa mchangiaji katika hatima ya uvunjikaji amani na umoja wa nchi.
                Mtu mmoja mmoja, vikundi vya watu, wapangaji, wenye nyumba, wenye mji, wanamtaa, wanakijiji na wanamji kwa ujumla wao ni sehemu ya Tanzania. Kila mmoja wao ana wajibu na ana haki zake. Kitendo chochote kinachoruhusu au kuendelea kuruhusu mtu au watu fulani kununua na kuuza haki za wengine ni kitendo kinachonuiwa na kinachodhamiria kuvunja amani na umoja wetu. Kisikubalike
                Uhuru wa kweli kwa mtu mmoja mmoja na makundi au jumuiya ya watu pasina uhuru huo kuingilia uhuru wa wengine. Uhuru ndicho kitu kinachompa uwezo mwananchi au raia awaye kufanya maamuzi kwa kuangalia maslahi yake na kikundi chake bila ya kurubuniwa, kuzainiwa, kununuliwa au kushawishiwa kufanza hivyo kwa pesa au upendeleo wowote uwao. Nchi huru hujengwa na watu huru  haijengwi na watu wa kununuliwa au watumwa wa mtu fulani.
                Kama nchi, Tanzania tunapwaya mno katika medani za ukweli na uaminifu kama watu binafsi na dhamana tunazopewa kutunza na wenzeu. UOngo haujengi nchi, aghalabu uongo hubomoa na kausambaratisha watu, vyama na nchi. Ni muhimu katika uandikaji wa katiba yetu tukarejea suala la kuwa na maadili muhimu ya kitaifa. Maadili hayo pamoja na mambo mengine yahusu: ukweli  kama tabia inayokubalika na wote; uaminifu; usafi wa mazingira, miili na mioyo yetu; uchapakazi na uwajibikaji wa kiwango cha juu; tabia ya kujisomea na kujiendeleza baada ya kumaliza shule/vyuo; kujitolea kusaidia wengine; kujitegemea kama jamii kama hali inaruhusu na ndio njia peikee ya kutatua tatizo la kijamii na kujitahidi kuongoza kwa vitendo na sio porojo na maneno.
                Hali ilivyo hivi sasa ni kwamba kuna matajiri na wakubwa wengine wanaojiweka juu ya sheria na wengi wengine kuwa chini ya sheria. Amani na umoja wetu lazima kufa kama hapatakuwa na usawa mbele ya sheria kwa wote viongozi kwa raia.
                Tusikubali visingizio vya kihaki za kibinadamu na kisheria kukwamisha mapambano dhidi ya rushwa. Kwa vigezo na bishara zote mla rushwa na fisadi huonekana maili kumi toka pale alipo na wala sio siri. Tukiidharau rushwa na kukubali itutawale sisi kama taifa na sio sisi kuitawala rushwa tutakuwa tumeshindwa katika safari ya ustawi na maendeleo ya watu wetu kabla hata ya kuanza safari yenyewe.
Kujilinda na kuwa na maofisa habari na mawasiliano pia wahariri wa habari na waandishi ambao pamoja na  uchanga wao wanajifanya  ni watakatifu na wanajua kilicho bora zaidi kwa nchi na watu wake. Hali katika kufanya hivyo wakawa  ndio wanaopanda mbegu za ushetani na balaa kwa nchi na watu  wake .
-Kupigwa vita rushwa na ufisadi
                Kama hatutaenzi ahadi na amri mbalimbali ambazo ni sahihi na za haki basi kitaifa tutakuwa tunabomoa msingi wa amani na umoja wetu. Baada ya kusema hivyo, ni lazima kwa wakubwa wetu sio tu kuchungua mambo pale tatizo linapotokea bali pia kuchungua kwa makini, kina na mapana malalamiko yoyote nchini ambayo yanaashiria kuwepo tatizo kati ya mtu na mtu au watu na watu. Mambo haya yakichukuliwa kijuujuu yatatufiksha pabaya, kwani yana uwezekano mkubwa wa kuweka umoja na amani yetu rehani katika mikono ya wachache kwa wema au ila.
                Huko nyuma Watanzania walikuwa wepesi wa kuitana ndugu au komredi.  Kuzuka na kukua kwa matabaka kati yetu kumeanza kunyemelea na kuuharibu udugu na ujamaa huo. Ni muhimu kuangalia kwa kutumia njia zozote ziwezekanazo tunarudisha  upendo na kukubalika kwa makundi mbalimbali katika jamii na sio kama hivi sasa ambapo baadhi ya  watumishi wa umma wameanza kuonekana kama maadui na aghalabu wako juu ya sheria za nchi na maeneo mbalimbali. Udugu na mahusiano mema huzaa kile kinachoitwa mtaji wa kijamii. Mtaji huu usipokuweko mbio za manendeleo kwa jamii yoyote iwayo hatima yake ni kuishia sakafuni.
                Tuepuke tabia ya kuwadharau , kuwashusha h adhi na kuwakwaza wengine hadharani pasina sababu ya msingi ila kwa mtu kujipendekeza na kujionyesha kwa wenzake kwamba yeye ni mkereketwa na anayewashwa zaidi kuliko wenzako na hasa katika jambo muktalifuni na lisilokubalika  ukweli wake na watu alimu na wenye uadilifu. Tabia ya kuikweza na kujionyesha wewe safi na bora kuliko wengine hujenga  chuki na inda isiyo na tija. Aghalabu anayejikweza na kukwaza wenzake huonekana mbaya, mbinafsi, adui na huchukiwa na wenigi hata na wale anaodhania wanamshabikia na kumpenda. Maana leo ni yule, kesho aweza wageukia wao.
                Kumezuka tabia ya baadhi ya wanasiasa na matajiri kuwanunua  Watanzania wengine kwa sababu moja au nyingine.  Jambo hili sio tu linarudisha uhadimu kwa watu wetu kupitia mlango wa nyuma bali ni sababu moja kubwa inayochangia kuua na kuumaliza udugu na umoja wetu, kwa kuwa watu wanaonunuliwa ni rahisi sana kutumika kufanya lolote lile liwalo, liwe jema au baya mradi wanalipa deni lao.
                Katika miaka hii ya kugundulika kwa rasilimali mbalimbali nchini upo umuhimu wa kuwa na fomula ya kitaifa itakayogawa rasilimali na mapato yanayotokana nazo kwa namna ambayo kule inakopatikana wanaona wanastahili kupata wanachopata na wengine kugawiwa au kunufaika na kile kinachobakia, ikiwemo serikali na vyombo vyake pia.
                Upo uwezekano mkubwa wa amani na umoja wetu kudumu kama mambo niliyoorodhoshea hapo juu yatafanyiwa maamuzi sio kiimla bali kwa kuwashirikisha wahusika au wabia katika masuala mbalimbali na kufikia maamuzi ambayo yanachangia wote kujiona ni washindi na hakuna mshindwa.
                Kwenye jamii ya mpito kama ilivyo yetu aghalabu umoja hujengwa kwa kuwa na madaraja kati ya walionacho na wasio nacho. Aidha kila kinachoonekana kuwa ni kizuizi katika ukombozi wa wasionacho huwa kinang'olewa haraka kwa faida ya wote.
                Rasilimali zetu ni nyingi na za kutosha. Kinachokosekana ni uongozi, utu na  ubinadamu wa kuweza kutumia akili na maarifa tuliyopewa na Mola ili rasilimali hizo ziweze kutufaa sote bila ya wengine kutengwa na kusahauliwa. Hii ina maana katika sifa kubwa amabyo viongozi wetu kuanzia vijijini hadi kitaifa wangepaswa kuwa nayo ni ile ya kukosa kabisa ubainafsi wenye uharibifu.
                Hatuwezi kuwapata kina Nyerere wengine (watu waliokuwa wanajisahau wao wenywe na familia zao na kumtanguliza mbele Mtanzania kwanza) lakini tukiwa na maadili bora, kupata viongozi wenye kudhibiti ubinafsi wao kwa masalahi ya walio wengii ni kitu kinachowezekana kabisa. Kuna mifano mingi duniani inayoonesha kwamba nchi zilizochipukia na kuwa tajiri katika miaka ya hivi karibuni ziliongozwa na viongozi walionyima wao na kuwanufaisha watu wao kwanza, na sio waliowanyima na kuwakwaza watu wao ili wao wajinufaishe kwanza.
Tanzania katika nchi nyingi za Kiafrika ipo katika nafasi ya kipekee kuendelea kudumisha amani na umoja wa watu wake kama isipofuata msaragambo na kuiga yanayotokea katika nchi nyingine za Kiafrika na kwingineko duniani kwa kuwa na utaratibu wa wazi na usio na usiri katika kuzungumzia mambo mbalimbali yanayoonekana kuwa ni chanzo cha mtafaruku na maelewano kati ya Watanzania katika siku zijazo.
                Tabia ya mbuni haifai kwa nchi kama yetu, yaani, kuingiza kichwa chetu kwenye mchanga, kisha tukajifanya kama vile kwa kuwa hatuoni hatari inayokuja, basi tukifijificha hatari hiyo haitatugusa na eti tukabakia salama. Athari, hatari na matishio mbalimbali  kwa amani na umoja wetu lazima tupambane navyo ana kwa ana.



No comments:

Post a Comment