Nia na madhumuni ya insha hii ni kujaribu kuwashawishi
Watanzania kuona kwamba elimu yetu sasa hivi inaendeshwa kwa namna ambayo haina
uhusiano kabisa na matatizo yanayokabili nchi na watu wetu.
Ninavyoelewa
mimi sababu kubwa ya kuwepo kwa elimu ni kusaidia kudumisha daraja la maarifa,
nadharia, ujuzi na uzoefu wa waliotangulia na wanaowafatia katika jamii fulani.
Jamii
isiyoweza kurithisha toka kizazi kimoja kwenda kingine maarifa, elimu,
teknolojia, mila, desturi na utamaduni wake kiujumla inayozikusanya muongo
baada ya muongo sio jamii yenye uhakika wa kuwepo na kuendelea kuwepo katika
siku zijazo.
Urithishaji
huu unajumlisha pia urithishwaji wa kizazi kimoja na kingine mbinu, njia na
mikakati ya kushughulikia matatizo makubwa na madogo yanayokabili mtu mmoja
mmoja na jamii nzima kwa ujumla.
Inaaminika
kwamba nusu ya matatizo ya jamii fulani huhesabika yamekwisha au
yameishatatuliwa kama jamii hiyo itakuwa inawafunza vijana wake pamoja na elimu
nyinginezo elimu ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikablili jamii husika.
Mafunzo haya hutolewa sio tu kinadharia bali pia kwa
vitendo. Unapotenganisha nadharia na
vitndo katika elimu, basi jamii husika huwa inapoteza jambo muhimu sana katika
wakati muafaka na sio rahisi kulipata jambo hilo tena katika siku zijazo.
Kuna
wanaoamini kwamba nusu ya matatizo ya Tanzania yanaweza kwisha kwa kuwa na
mitaala inayolenga kutatua matatizo yake ya kijamii na kiuchumi.
Matatizo ya kimaendeleo yanayowakabili Watanzania walio
wengi ni pamoja na uadimu kama sio ukosefu wa maji, chakula na nyumba. Aidha
kuna udhaifu katika elimu, tiba na afya kiasi kwamba watoto wa Kitanzania
wanaendelea bado kusomeshwa nchi jirani na Ulaya au Asia; wakati huo huo
wagonjwa wa Kitanzania wanaendelea kutibiwa
nje.
Kuna
tatizo la kukosa matunzo kwa wazee,
mayatima na watoto wa mitaani. Vilevile
yapo matatizo ya kiulinzi na usalama, uhalifu yanayotishia sio tu usalama wa
raia mmoja mmoja bali amani na utulivu katika jamii ikiwemo kuongezeka kwa
vitendo vya wivi na ubakaji pamoja na kuwa na sheria kali dhidi ya vitendo
hivyo.
Aidha
yapo matatizo katika ujenzi na upanuzi au ujengaji upya wa barabara, reli,
madaraja, uchimbaji madini, bandari, viwanja vya ndege na ujenzi wa uendelezaji
wa miundombinu mingine.
Kiutamaduni
na Kiteknolojia tuna matatizo ya kuoanisha maendeleo ya teknolojia na mila na
desturi zetu ili kupunguza gharama na kurahisisha ufanifu na ufanisi katika
maeneo mengineyo ya maisha, kazi, sanaa, utunzi wa vitabu, filamu, michezo na
burudani.
Kijamii
na kiuchumi matatizo makubwa ni katika ujasiriamali, mikopo na urudishaji wake,
mipango, uratibu, uongozi, usimamizi na udhibiti wa mambo kiutawala,
kimaandishi na kiteknolojia. Hali
kadhalika kuna masuala ya menejimenti na uendeshaji bora wa michezo, sanaa na
uchumiwa utoaji au uuzaji huduma. Aidha kuna changamoto katika uchimbaji na
utunzaji au uangalizi wa visima vya maji, bomba, pampu, mashamba ya kisasa,
uvuvi na ufugaji wa kisasa, utunzaji na ulinzi wa wanyama pori, nege na viumbe
wengine, matumizi bora na makubwa zaidi ya rasilimali nchi kavu, rasilimali
kwenye baharini na kwenye maji kwa faida ya wengi na sio wachache.
Elimu
yetu kwa mapana na marefu sasa hivi imeelekezwa katika kujifunza vitu kama
historia, sayansi kama sayansi, uraia, jiografia, hesabu, lugha na mambo kama hayo.
Kwa maoni yangu masomo yote yanayotolewa hivi sasa iwe kwa shule za msingi au
sekondari yanaweza kuangukia ndani ya masomo matatu makubwa: Maarifa ya Namba
na Takwimu; Maarifa ya Kunadika na Mawasiliano na Maarifa ya Maisha, Sayansi na
Mazingira.
Fani
hizo hapo juu zikipata msukumo wa kuwekwa kwenye mtandao kwa lugha ya Kiswahili
na Kiingereza kama itakavyoandikwa na Watanzania wenyewe ni maeneo yanayoweza
kutawaliwa kielimu vyema na mwanafunzi yeyote awaye.
Hayo
kwa upande wangu ndiyo yangelikuwa masomo ya msingi kuanzia chekechea hadi
sekondari na yakawa ni lazima kuwepo kwenye kila mchepuo kwenye maeneo hayo.
Masomo
yanayotakiwa kupangwa kama ziada itakayotofautisha kati ya mchepuo wa mweleko
fulani na mwingine ni mtatizo yalioorodheshwa hapo juu.
Kwa
mpangilio huo mwanafunzi, mathalani,
katika kundi la kwanza la matatizo ya uadimu na ughali wa maji, chakula,
nyumba na kadhalika atakuwa akijishughulisha na kujifunza jinsi ambavyo
matatizo hayo yanaweza kupunguzwa au kumalizwa nchini. Ni elimu inayomhakikisha
kijana nafasi ya kujiajiri au kuajiriwa kwa sababu elimu hiyo itakazia nguvu
zaidi katika vitendo na sio nadharia tu.
Mchepuo
mwingine unaweza ukaelekeza nguvu zake katika kujifunza na kurahisisha kuelewa
matatizo ya elimu (elimu nayo pia huwa tatizo na lazima kufunzwa na kufanyiwa
tafiti dahari ili kuboreshwa mara kwa mara),
tiba na afya wataanza kugangana
na mbinu, stadi na maarifa za ualimu au ufundishaji na uangalizi au utabibu
mahospitalini na katika zahanati mbalimbali nzhini zisizo na watumishi wa
kutosha.
Wanafunzi
wengine na hususan katika shule za msingi wataelekezwa kutokan na mapenzi na
mwelekeo wao katika kujifunza na kulielewa tatizo la matunzo kwa wazee, wajane,
mayatima na watoto wa mitaani ili waje kubobea sio tu katika nadharia bali
vitendo vya kulipunguza au kuondosha kabisa tatizo hilo.
Wale
wanaopendelea mambo ya ujenzi na miundombinu wataanza kupigwa msasa toka shule
za msingi kwa kujifunza juu ya umuhimu, kazi na faida za nyumba, barabara, reli, madaraja, visima, bandari
na viwanja vya ndege, vituo vya kisasa mipakani na usafiri na uchukuzi
kiujumla. Kwa namna hii, mtoto hata akimaliza darasa la saba anaweza kuanza
kufanya kazi katika eneo hilo na akawa anajiendeleza katika fani yake
pasipokuwa na wasiwasi wa kuchanganya kimasomo au kimitaala. Maana elimu hapa
inakuwa ikishughulika na tatizo lilipo, linaloeleweka na linaonekana na kila
mtu katika jamii.
Mcherpuo
mmoja muhimu utakuwa ule wa kuwapa watoto kuanzia chekechea fursa ya kuonyesha
vipaji vyao katika nyanja za sanaa, kuimba, kucheza ngoma na kukatika viuno,
kuigiza, kuchekesha, uchezaji mpira wa vikapu na michezo mingine na mambo kama
hayo. Kwa kuwa mtoto anaelekezwa kulekule anakokutaka inakuwa ni rahisi kijana
wa Kitanzania kuanza kuonyesha vitu vyake akingali bado mdogo na hivyo kumpa
nafasi ya kufanza makubwa zaidi hapo baadaye.
Mabadiliko
ya mitaala katika miaka hii pia lazima iwe na mchepuo wa uongozi, utawala,
biashara na menejimenti ya vitu hivyo. Ni vizuri hili likaanzia shule za msingi
kiasi kwamba mtoto wa Kitanzania akimaliza darasa la saba anakuwa sawa na mtoto
wa Kimarekani aliyesomea B.B.A. au hata M.B.A. (unacheka?) nina hakika hili
linawezekana kwa kuwa watoto wa Kitanzania kutokana na mzingira yao magumu
wanaisoma na kuilewa dunia haraka kuliko watu wa nje katika hili.
Mwanafunzi
anayemaliza masomo katika mchepuo huu atakuwa na uwezo wa kusimamia biashara ya
wazazi wake kwa namna bora zaidi kuliko wazazi
hao, na upo uwezekano mkubwa wa mchepuo huu kuzalisha viongozi bora
zaidi kwa vyama, vijiji na taasisi nyingine kuliko hali ilivyo hivi sasa.
Ninakubaliana
na wale wote wanaodai kwamba ilikuwa ni makosa kuondoa elimu ya ujamaa na kujitegemea mashuleni. Lakini
kama ikirudishwa, ninashauri ingerudishwa kwa mapana na kina zaidi kwa
kuzingatia ulazima wa kuoanisha matatizo ya jamii leo na elimu inayowapatia
watu wake.
Nionavyo
mimi, Vyuo vya VETA vinastahili kuitia makali au kuinoa zaidi elimu vijana wetu
watakayoipata shule za msingi na sio kuwa mahala pa kuanzia tu vitu vipya kwao.
Nikiwa na maana kwamba shule zetu zote za msingi zinahitaji maabara na karakana
za useremala, uashi, umakenika na ufundi mwingine ili ziwe kamili na sio
nusunusu kama zilivyo leo. Hali ingelikuwa hivyo, leo tusingekuwa na shule za
msingi zisizokuwa na madawati na vyoo vya kutosha, na zenye madarasa na majengo
mengine yasiyofikia viwango.
Copyright
© 2013 Sammy W.I. Makilla. All Rights Reserved.
No comments:
Post a Comment