Saturday, February 16, 2013

Ujamaa na Kujitegemea Bado una Nafasi Vijijini na mashuleni


KIHISTORIA watu wa mjini hawajawahi kuwa watu wanaotamani na kupenda ujamaa. Miji jinsi ilivyo imejengwa katika msingi wa ubinafsi na kila mtu na lweke. Na kwa miaka mingi ijayo hilo ndilo litakaloendelea kwa ubepari kuwa wenye sura mbaya na makucha makali zaidi.
 Mtu aneyeuchukia ujamaa eti kwa sababu tu Warussi wameutupa na wajamaa wa jana wameanza kukumbatia baadhi ya sera za kibepari ni mtu asiyejua maana halisi ya ubepari. Ni mtu anayehitaji kujitambua na kuijua jamii yake na hasa ile ya vijijini na shida na dhiki zao mbalimbali.
 Anakuwa hivyo kama anavyokuwa kwa sababu anadanganyika na mng'aro wa dhahabu ubepari unaonyesha kwa nje, bila kujua kilichoko ndani wala sio shaba achilia mbali madini ya fedha.
 Tumeshaufungulia mlango, na hakuna namna ambayo tutaweza kuuzuia. Labda, angalau tukubaliane na na kina Raila Oginga na wenzake (watangulizi maarufu katika ubepari) kuwa nchi zetu sasa zinastahili kuwa na sera na dira ya Ujamaa wa Kidemokrasia (Sosho-demokrasia), ha hivyo kupunguza ushetani na makali yaliyomo katika ubepari kwa faida ya wasionacho katika jamii yetu.
 Hata hivyo, hali ya maisha vijijini katika sehemu mbalimbali za Tanzania nilizotembelea na wanakoishi watu masikini na wa kawaida na sio viongozi au jamaa za viongozi kila feli, kila mtihani, kila tatizo na kila fursa inapiga mayowe ya kuwa pasipo ujamaa na kujitegemea miongoni mwa wanavijiji maisha huko tuendako yatakuwa magumu na yasiyo na huruma hata kidogo.
 Hili linakuwa hivyo, kwa kuwa nchi yetu bado haijawa na sera inayomfanya mwanakijiji anufaike na ardhi yake na kile kilichomo ndani yake kama viongozi wa juu wanavyonufaika.
 Aidha, pamoja na kuwepo kwa teknolojia ya habari na mawasiliano bado inawachukua wanavijiji muda mrefu kujua kinachotokea mkoani mwao achilia mbali nchini kwao na duniani kwa ujumla.
 Vilevile, pamoja na kuwa na vitu kama TASAF na NGOs mbalimbali zenye madhumuni na nia ya kuwasaidia wanavijiji kutatua matatizo yao bado  muundo na mifumo ya taasisi hizo imekaa kuwanufaisha zaidi watu wa mjini kuliko wa vijijini.
 Tafiti zinaonyesha kwamba jitihada za kuwaamsha na kuwafunza wanavijiji umuhimu wa ushirika zinaharibiwa na tamaa za viongozi wao na mabepari uchwara wsnaoishi au kuchanganyikana nao.
 Watu wanashangaa kusikia kwamba dhana na nadharia ya ushirikishwaji watu nchini  hapa pamoja na kuleta ufanisi wa aina fulani haikutoka kwenye ile ngazi ya chini kabisa katika ushirikishwaji watu kwa kutumia modeli ya ushirikishwaji watu iliyobuniwa na Mjapani kutoka Chuo Kikuu cha Kobe aitwaye Etsuko Okazaki. Hatua hiyo siyo nyingine ila ni ile ya uanasesere wa kuchezewa na wanasiasa na viongozi wa serikali za mkoa na kitaifa. Hatua za juu katika ngazi hiyo ya ushirikishwaji watu ni pamoja na tiba, kuarifiiwa, ushauri, kubembelewa, ubia, ukaimishwaji na nguvu ya umma.
 Matatizo yanayokabili vijiji vyetu nchini ni pamoja na tatizo la maji; dhikiya chakula na lishe bora; ukosefu wa nyumba bora kwa wananchi walio wengi na uzalishaji mali kwa njia dhaifu na zisizo na ufanifu na ufanisi  wa kutosha. Na kutokana na hili bado shughuli za kilimo, ufugaji pamoja na ule wa nyuki, uvuvi, uchimbaji madini na matumizi ya rasilimali ardhi na bahari kwa ujumla ni dhaifu na zisizowasaidia kitu wanavijiji katika kubadili ubora wa maisha yao na kuwa yenye heri na mafanikio zaidi.
 Matatizo mengine ni kutokuwepo kwa biashara zenye  manufaa zaidi kwa wanavijiji na mwelekeo wa kuchangia kuwafanza kwanza wazalishe kitu na ndio watumie; kutokuwepo huduma za uhakika zinazoweza kupunguza umaskini vijijini k.m. utaalii wa vijijini na wa kiutamaduni; matatizo ya mejengo, vifaa na walimu kwa shule nyingi vijijini; huduma dhaifu ya tiba na Afya vijijini; uadimu wa
umeme na nishati mbalimbali; na
Usafirishaji na Uchukuzi wenye matatizo kedekede na hivyo kusababisha hatari na hasara kwa wanavijiji walio wengi.
 Nichukulie tatizo moja tu nchini-maji. Tatizo hili, ninavyoamini, linaweza kutatuliwa kiurahisi ikiwa wanavijiji wenyewe wanajifunza na kubadilika na kuwa ndio viongozi wa maendeleo yao badala ya kuwategemea watu kutoka kwenye kata au tarafa au wilaya au mkoa au hata taifa kuja kuwasaidia.
 Wenyewe wakishaamua kusimama kidedea inakuwa ni rahisi kuamua,  kupanga na kutekeleza kile wanachokiamua. Na hili huwa ni rahisi zaidi pale wanakijiji wote kwa pamoja wanapokuwa kitu kimoja na sio baadhi yao kukubali kuzainiwa na wale wenye tamaa za uongozi na njaa yao binafsi.
 Huko nyuma nimewahi kupendekeza njia mbalimbali za wanavijiji kupata maji huko waliko vijijini pasina ya kutembea mbali au kuhangaika sana. Njia mojawapo ni kuchimba bwawa pale penye chanzo cha maji  na vilevile kwa ajili ya kutega maji ya mvua badala ya kuyaachia yote kwenda baharini. Njjia nyingine ni kuchimba kisima pale wataalamu wanapothibitisha kuwa maji hayapo mbali na uso wa dunia. Katika sehemu zenye maziwa jirani na wao upo umuhimu wa wahandisi wa Kitanzania kuamka na kuvumbua njia ambazo kwazo  kwa maziwa yaliyo na kina cha chini  wao wanaweza kuchimba  mtaro chini kwa chini na kuvuta maji hadi nchi kavu.  Wale wanaoishi pembeni na bahari huu ni wakati  wa baadhi yao kurudi shule na kujifuna kutoka kwa wenzetu jinsi wanavyobadili maji ya chumvi hadi maji hayo kutumika kunyweshwa mashamba na bustani na kusaidia pia katika matumizi ya nyumbani.
 Ukiyaangalia yote haya ni mambo yanayohitaji vichwa vilivyotulia na watu wanaokubali kwamba changamoto na fursa nyingi walizonazao zinalazimisha kuwepo kwa ushirikishwaji na kujitolea kwa namna moja au nyingine. Na kwamba bila ushirikiano wa walio wengi vijijini ippo hatari kubwa ya vijiji kubaki kama vilivyo hivi leo hata baada ya muongo mmoja ujao.
Maendeleo ya vijiji vyetu yamekwaza na viongozi wetu. Ambao kufatia Azimio la Zanzibar wamekuwa 'bize' kushughulika na mambo yote mengine na sio ujenzi na uendelezaji vijiji. Kwa namna moja au nyingine kwa miaka kadhaa sasa isipokuwa kwa vijiji viongozi wetu wanakotokea vijiji vingine vimeingizwa kwenye kabati kama sio kaburi la sahau.
 Jambo la kushangaza ni kwamba matatizo mengi yanayoikabili miji yetu hivi leo yanasababishwa uongozi kushindwa kutoa msaada na nyenzo (wakati mwingine vimilioni vichache tu) ili kuwawezesha wanavijiji kuhama kwenye umaskini wa kutupwa na kuwa watu wanaojitegemea.
 Kama kuna jambo moja ambalo ningeliwaomba wanaoendesha ukusanyaji maoni juu ya katiba mpya ni kutia shadidi katika kile kifungu kinachozungumziwa uwiano wa kimaendeleo kati ya sehemu moja na nyingine ili pawe na mikakati, sera na kanuni zilizo fasaha na wazi juu ya kushughulikia ujenzi na maendele oi ya vijiji vyetu. Ninazungumza hivyo nikiwa na uhakika kwamba nusu ya matatizo ya mjini yatakuwa yamekwisha kama vijiji vyetu vitatapatiwa angalau kwa kuanzia mahitaji yote ya msingi na ushirikiano kiungozi na kiutawala unaoweza kuwatoa wanavijiji pale walipo na kuwafikisha mahala ambapo sisi  sote wa mjini na vijijini tunaweza kujivunia.
 Jambo moja linalohitaji kupewa uzito wa kipekee hivi sasa ni kuangalia uwezekano wa kuwa na viongozi na watendaji bora wa vijiji bila kujali mtu anatokea wapi.
 Inashangaza kwamba pamoja na kuwa na vyuo vya maendeleo vijijini kasi ya maendeleo vijijini imezidi kwenda chini mwaka hata mwaka. Aidha, elimu inayotolewa na vyuo kama hivyo haiendani na wakati au wanaozalishwa na vyuo hivyo hawaendi kuwa viongozi  wa vijiji bali wanaselea humu humu mjini kama wahitimu katika masuala mengine. Kama ilivyo kwa vijiji basi mengi pia  ya kijamaa na kujitegemea yanaweza kufanzwa  shuleni na vyuoni kwa manufaa ya wanafunzi, wazazi wao na nchi  yao. Hata kama baada ya shule vijana wataamua kufata  ubepari na sio ujamaa.
 Ninaamini kwamba jambo litakalochochea  ari, mwamko na msukumo wa maendeleo kwa watu wa vijijini ni rasilimali watu. Wakati umefika huko vijijini wanavijiji kuwa na viongozi bora na sio bora viongozi.
 Ukweli ni kuwa hata tukiwa na viongozi wazuri kiasi gani katika ngazi za juu  lakini huko vijijini uongozi ukawa dhaifu kupita kiasi hatutaweza kuendelea kiwelikweli.   Jambo hili likiunganishwa na ufanyaji kazi kidhati kwa mashirika yanayosemekana kazi yake ni kusaidia maendeleo vijijini na kisha wanakijiji wakafunzwa namna za kukopesheka kama wawekezaji wanaokuja kupewa ardhi kwenye vijiji vyao wanavyopewa mikopo kiurahisi kwa kutumia ardhi hiyo hiyo, basi maendeleo ya vijiji vyetu hayatabakia katika ruia zetu tu! Aidha, bila kusita wala kutafuna maneno huu ni wakati  wa serikali zetu za mitaa na serikali  kuu kuhakikisha kwamba wale wanaoishi katika maeneo  mbalimbali hapa nchini  wananufaishwa na  na tathmini mpya ya mali asili na rasilimali zao nyingine na  kwamba mali hizo kuanzia sasa zitakuwa zinahesabika kama mtaji wao kieneo na kitaifa na hivyo kuwaruhsu kunufaika kihisa na kifedha na rasilimali kama hizo na isiwe tu wanaonufaika na hili ni viongozi  wa juu na wanasiasa nchini. 

No comments:

Post a Comment