Sunday, July 28, 2013

Bomu linalosubiri kulipuka Afrika: Tofauti ya walionacho na wasionacho..

Kabla ya 2010 dunia ilijikita zaidi katika kushughulikia changamoto zilizosababishwa na athari au madhara yanayosababishwa na walimwengu kwa hali ya hewa na mazingira duniani. Kuanzia muongo wa pili wa karne ya ishirini na moja, hata hivyo, mtazamo na mwelekeo wa wanauchumi na wanajamii kwa ujumla umekuwa ukiegema zaidi upande wa namna au jinsi ambayo masuala ya kiuchumi na kijamii yanavyoweza kuhatarisha sio tu maisha ya mwanadamu, bali hata kuzidisha uwezekano wa athari mbaya dhidii ya mazingira na hali ya hewa kuongezeka. Katika makala ya leo tutajikita zaidi katika suala la kukua tofauti za kipato au kiuchumi kati ya wale wenye nacho na wasionacho. Tafiti zilizofanywa na Prof. Joseph E. Stiglitz wa Chuo Kikuu cha Columbia cha nchini Marekani, ni kazi nzuri inayokuja wakati muafaka katika kuitahadharisha dunia kuwa mfumo wa ubepari usiodhibtiwa budi utazipeleka nchi na dunia kubaya. Na kwamba upo umuhimu wa kujitoa kimasomaso kuja na sera ambazo hazitaipelekea Afrika kujikuta kwenye masahibu ambayo baadhi ya nchi za Ulaya na Asia leo zinalazimika kuyafungia kibwebwe. Mfano wa nchi ambazo zinajenga mfano mzuri wa kuigwa katika kudhibiti pendo kati ya walionacho na wasionacho ni nchi za Skandinavia. Nchi hizo hazina muujiza wowote ila tu ni kule kuanzisha kwao na kutunza mikakati na sera ambazo wanazitumia kuzuia kulipuka kwa tofauti kubwa katika kipato cha watu wa kima cha juu na wale wa chini. Sera hizi hubainika na wengi duniani kama mfumo wa ujamaa wa kidemokrasia. Laiti Tanzania isingetupa moja kwa moja siasa ya Ujamaa na Kujitegemea leo tusingekuwa na cha kuandika hapa. Hasara yetu ni sawa na ile ya mwogeshaji mwana, kumtupa mwana na maji machafu aliyeogeshewa. Nchi zinazoathirika zaidi ni zile zenye kukosa azma na sera kwa malengo ya kisiasa na kijamii yaliyo dhahiri na yanayokubalika kama dawa mujarabu kwa tofauti za kiuchumi na kipato katika jamii husika. Aidha, vijiji kusahaulika kimaendeleo kwa kukosa mipango ya kuvisaidia kupata uongozi au menejimenti bora ikiwemo ile ya rasilimali watu, usimamiaji uzalishaji mali, utafutaji mitaji na masoko Ujamaa, ubepari ni jambo jengine linaloendelea kuchangia kukua kwa tofauti za kipato hususan kati ya watu wa mijini na wale wa vijiini. Sera zozote zinazochania kumnyang'anya masikini hata kile kidogo alichonacho sio chachu ya kudumisha amani na umoja katika jamii husika. Katika nchi nyingi zilizoanza na kuendelea na ubepari tofauti hizi husababishwa kwa kiasi kikubwa kwa baadhi ya watu aidha kuzaliwa katika utajiri au ukubwa au nafasi zenyemlo na wengi wengine katika umaskini, hivyo kuwapa wale wa kwanza mtaji wa kiuzawa na vilevile kutokana na tofauti za kiajira na kielimu na uweledi wa kiteknolojia na utaalamu wa tasnia husika. Katika nchi zilizokuwa zikifuata ujamaa tofauti hizi zinazaliwa na watawala waliokuwa wajamaa kugeuka mabepari kwa kunufaika na mali zilizokuwa za umma huku wakigwaya kukiri kwa wananchi wao kuwa wao na nchi sasa ni ya kibepari na sio tena ya kijamaa; utumishi unaojali zaidi uswahiba na udugu na sio tija na ufanisi; utegemezi wa upendeleo, rushwa na teni pasenti kwa vyama tawala badala ya njia halali za mapato; wanasiasa kununuliwa na matajiri na fisadi; mabenki na taasisi nyingine za fedha kuwa chini ya wanasiasa wanaotawala; misaada toka nje kuwanufaisha watawala kuliko wananchi; kukosa uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa mipango, mikataba, siasa na sera za nchi husika; kusaini mikataba mibovu kwa faida ya chama na watu binafsi na sio kwa faida ya umma; kukosekana ushindani wa kweli wa kidemokrasia kisiasa na kiuchumi;kuwanyima fursa wapinzani wa kisiasa na watawala au watu wao kupewa fursa hizo; uwepo wa makampuni yasiyotozwa kodi tosha na ambayo yanaweza kuzaini umma na yenyewe kutengeneza mabilioni kama sio matrilioni katika muda mfupi tu bila udhibiti na ukaguzi wa uhakika toka kwa wanaohusika na ardhi na maliasili za nchi kuwafaa zaidi watawala, wageni na wenye nacho na sio mwananchi wa kawaida. Jambo jengine linachangia si haba kukuza pengo kati ya walio nacho na wasio nacho ni lile la kukosa vigezo vinavyokubalika katika ajira na ujira. Kwenye nchi nyingi waliosoma sana na wenye ujuzi mkubwa zaidi ndio hulipwa kidogo lakini wasiosoma bali wana vyeo wao wakafaidi ujira, masurufu na maduhuli makubwa zaidi. Nchi nyingi maskini kama vile Tanzania zina matatizo pia ya kushindwa kuwa na sera na mipango inayofanya kazi katka masuala ya matumizi na ugawanyaji pato la taifa kitaifa, kijamii mbalimbali na kati ya tasnia na makundi kazi mbalimbali katika jamii. Kosa lingine linalochangia kukua kwa pengo kati ya walionacho na wasio nacho ni kushindwa kuipa mali asili yetu kama ardhi, madini, mimea na watu wetu thamani stahilifu na inayoweza kuwanyanyua watu wetu kiuchumi na kimapato kwa njia moja au nyengine. Udhaifu katika menejimenti ya uchumi wa nchi na hasa uzalishaji mali na ujasiriamli ikiwemo, mathalani, fursa ya kuviongoza vijiji kiuchumi na kimapato zaidi nayo inachangia tatizo hili si haba. Kuna wanaodai kuwa vijiji na wanavijiji wakiboreshewa tu masuala ya menejimenti na utawala nchi inaweza kupunguza nusu ya umaskini wake kwa haraka zaidi kuliko inavyotarajiwa na hasa panapokuwa na uwekezaji unaolenga kutmia kile wanakiji walichonacho katika kuwasaidia kupata maendeleo makubwa zaidi. Siasa za WB, IMF ambazo leo zinakataliwa na Ulaya na Amerika wanaopitia matatizo yaleyale kama yetu zinahitaji pia kukataliwa waziwazi kwani zinachangia hatari ya kutuletea matatizo makubwa zaidi siku za usoni. Ipo haja ya kuangalia upya, baada ya nchi yetu sasa, kugundua mali asili mpya kama gesi, mafuta ya peteroli na madini salama kuvunwa ya aina mbalimbali ni kwa jinsi gani Tanzania inaweza kurejea tena kwenye mfumo mzuri uliodhibiti vilivyo tofauti ya kipato na kiutajiri kati ya watu wetu kama vile utoaji elimu bure; utoaji huduma za afya bure; kutoa ruzuku katika huduma muhimu kama zile za maji na umeme, usafirishaji na uchukuzi; kuwatunza maskini, yatima na wajane kwa kujitolea na nyenginezo kama hizo. Benki Kuu na vyombo vyetu vya fedha lazima zibadilike ili kuwa vyombo vya kupunguza pengo kati ya walichonachona wasionacho kwa namna moja au nyengine. Na kuu katika hili ni kuhakikisha kuna mifuko maalum ya kusaidia miradi kwa wanavjiji, vijana, wanafunzi wanaomaliza shule na wanatafuta kujiajiri na watu kama hao kwa kuiga mifano iliyofanikiwa ndani na nje ya nchi ili kzungusha pato la taifa na kutoa fursa kubwa zaidi ya uwekezaji wa wazawa nchini.

No comments:

Post a Comment