NI CHINI ya asilimia 5 ya Watanzania wanaolalamikia tatizo la Umeme nchini. Asilimia 95 ya Watanzania hawana sababu ya kulalamika kwa sababu miaka 50 baada ya Uhuru hawana wala hawamo katika mpango wa kupata umeme.
Kwa hiyo, mgao wa umeme unaoendelea, na jinsi tatizo hilo lilivyopata wapiga makelele mbalimbali toka ndani na nje ya nchi, upo uwezekano mkubwa kwamba ufumbuzi wake uanweza ukawa pia ni ufumbuzi wa asilimia 95 ya Watanzania waliosahaulika nao kupata umeme. Kama laana yao kwa asilimia 5 ya wanaonufaika na matunda ya uhuru wa nchi hii itasitishwa.
Inavyoelekea bado tatizo la umeme linaloikumba Tanzania kwa hivi sasa halijaweleka na wote, yaani, viongozi na wananchi. Katika hali kama hii ni vigumu kuona mwanga upande wa pili wa pango, hususan, kuhusiana na uwezekano wa suala hilo kupata ufumbuzi bila kuchelewa mambo yakaharibika zaidi kuliko ilivyo sasa, kisiasa na kiuchumi.
Maana tatizo letu kama nchi nyingi za Kiafrika ni lile la kushindwa kuwa na miundo na mifumo inayofanya kazi kwa sababu mbalimbali zikiwemo zile za nchi kuongozwa kwa kufuata mipango, ahadi na misaada kutoka nje. Na kushindwa kabisa kujikwanyua toka kwenye makucha ya ubepari mamboleo, matapeli wa kimataifa na mabwana wa watwana. Uongozi wowote unaojenga tabia ya ombaomba, hujenga nchi ya ombaomba. Nyumba au uongozi wowote unaojivuna na unaothamini watu wake kikwelikweli hukataa kujenga tabia ya ombaomba. Watazame ombaomba mitaani Dar es salaam na familia zao ujiulize kama watu hawa kweli wanaweza kuja kubadilika baadaye. Haiwezekani. Badala yake ,hujenga tabia ya kupenda kujitegemea, kukinaishwa na kusaidiwa na kujivunia kama wenzetu wa Korea ya Kaskazini walivyofanya kunako miaka ya 1950 pale walipotengeneza trekta lao wenyewe la kwanza na badala ya kwenda mbele, gia zote zikawa ni za rivasi tu.
Kiongozi yeyote anayewadharau raia wake: kwa kuwaita wavivu, wezi, wategaji, wababaishaji atambue sio raia wake wenye tatizo bali ni yeye mwenye tatizo. Kwa kifupi, mdharau chake na kuthamini wengine na vya wengine hawezi kamwe kuwa kiongozi wa kutumaniwa wala kutegemewa kuleta mabadiliko ya kimsingi katika jamii husika. China au Korea Kusini au Brazl au India au Malaysia -ingelifanya hivyo, isingekua hapo ilipo leo.
Kuwathamini kupindukia watu toka nje na kutowathmini ipasavyo raia wako mwenyewe ni mwanzo wa jengo la nchi lisilo na msingi madhubuti.
Haya ni mambo yaliyotufikisha hapa tulipo ambapo leo pamoja na kuwa na wasomi wa masuala ya umeme na nishati, hawatumiki kwa ajili hiyo, na wanaofanya maamuzi juu ya masulala hayo ni wanasiasa ambao bila shaka ni mbumbumbu katika masuala hayo na uelewa wao unategemea maelezo wanayopata kutoka kwa wanaojua wanachokizungumza.
Aidha, kutokana na hayo hapo juu imekuwa vigumu kwetu kupambanua kati ya yale ambayo tunatakiwa tuyafanye sisi wenyewe ima-fa-ima na yale ambayo kwa sababu fulani fulani tunalazimika kuomba msaada au ushirikiano toka kwa wengine.
Hakuna asiyetambua kwamba, ili tuendelee nchi yetu inahitaji : chakula, maji; hewa safi; mazinigira salama; afya bora na usalama kwa watu wetu; umeme au nishati mbadala; reli ya kisasa; barabara zinazopitika bila usumbufu wakati wote; makazi bora kwa watu; usafiri wa anga na majini; masoko yanayofikika ndani na nje ya nchi; ushauri mzuri kwa waliotutangulia; utafiti na kuyaelezea kwa urahisi masuala mbalimbali ili yaeleweke na wengi nchini na elimu inayosaidia kutatua matatizo yetu au kutumia fursa za maendeleo zilizopo ndani ya mipaka yetu na nje ya mipaka yetu.
Tujihusishe na hili suala la umeme tu na hayo mengine tuyaache hadi wakati mwingine. Inshallah. Kuna vitu ambavyo 'piga-ua' ni lazima Watanzania waiunde au watengeneze wao wenyewe kwa kutumia watu wetu waliosoma na wasiosoma ili mradi ni wabunifu, watundu na wanaoweza kujaribu bila kukatishwa tamaa na kushindwa katika maisha yao yote. Hata wakishindwa mara ngapi! Na mimi siamini kama tukiwatumia wasomi wetu, wataalamu wetu, mameneja wetu, wanajeshi wetu na vijana wetu kikamilifu tuna sababu ya kushindwa zaidi ya mara mbili tatu tu! Tunashindwa kwa sababu hatuwatumii watu wetu ipasavyo! Tunashindwa kwa sababu wanasiasa wetu wamejifanya pia wao ndio wataalamu na magwiji wa uchumi na maendeleo ya jamii.
Lakini kama tutawatumia maprofesa wetu wa vyuo vikuu na wanafunzi wao katika taaluma ya umeme na nishati sio tu tunaweza kupata ufumbuzi wa muda mfupi bali wa kudumu wa matatizo yetu.
Ni kitu cha kuhuzunisha kuwa pengine kutokana na viongozi wetu wa vyuo vikuu kujikita zaidi kwenye siasa badala ya uchumi na uzalishaji mali, mahala kama Chuo Kikuu cha Dar es salaam, chenye idara ya Uhandisi wa umeme hakina mifano yoyote inayofanya kazi kama vile mashamba ya upepo wa umeme au ya solar energy au uzalishaji umeme kwa njia nyingine mikoani - na inayoweza kulipiwa na kufadhalilwa na kupanuliwa kukidhi mahitaji yetu ya umeme.
Msiba mmoja mkubwa kwa taifa letu ni lile la kuwa na elimu na wasomi wanaojengwa ili na wao kutegemea vitu na mitambo inayozalishwa nje kwa maendeleo ya watu na nchi yetu.
Ni kwa njia hii tu ndiyo tutaweza kupata maendeleo ya kweli, ya kudumu na endelevu na sio kwa kutegemea kila kitu kitoke kwa wengine.
Vitu hivyo ni pamoja na mashine na mitambo kwa ajili ya uzalishaji umeme; utekaji, uvutaji na usmbazaji na umwagiliaji maji; uchimbaji madini; ujenzi wa bandari; ujenzi wa reli; ujenzi wa viwanja vya ndege; ujenzi wa barabara; ujenzi wa madaraja; miundombinu ya mawasiliano; na zana au vifaa mbalimbali vinavyohitajika katika ujenzi wa majengo na makazi katika nchi.
Msingi wa nchi yoyote usipoanzia katika mambo hayo hapo juu, nchi haiwezi kamwe kuuacha umaskini, achilia kuwa na maendeleo endelevu. Mpango na mkakati wowote unaoshindwa kuibua mambo haya, kisha kuyatafakari, kuyainisha na kuyapa kipaumbele katika maendeleo ya nchi ni mpango au mkakati unaofaa kutupwa jalalani pindi unapogundulika kwamba upo na unagharamiwa na kodi za wananchi. Ni mpango unaoihukumu nchi kubaki kwenye makucha ya wakoloni, mabepari na mabeberu kwa faida zao na wala sio kwa faida ya nchi na watu wake. Ni mapango unaowalazimisha watu wa nchi fulani wawe ombaomba, huku rasilimali za nchi zikichotwa kwenda kuwafanya watoa sadaka matajiri na matajiri zaidi. Ni mpango na mkakati unaomfanya raia wa nchi hii kuwa mtumwa wa wakoloni wa zamani na vibarakala wao na utandawazi na mumiani wake.
Kwa maneno mengine matatizo yetu mengi, likiwemo hilo la umeme ni matatizo yanayoweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka na kudumu kwa kutumia vyema rasilimali watu yetu na rasimali watu toka nje pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali zetu nyingine.
Hili linaweza kufaulu tu katika nchi ambayo haijvunii na haiwalindi mafisadi kama sehemu ya uongozi wake; inayotambua maendeleo yetu kama rasilimali zetu zinatumika vizuri, yanaweza kugharamiwa na watakaopata ujuzi na uzoefu katika mipango yetu mbalimbali ya maendeleo nchini, wakati watakapokwenda kuwafanyia Waafrika wengine kazi kama hii. Fisadi wa Kitanzania, ni mwizi anayejiibia shati lake mwenyewe. Fisadi wa kimataifa, haibi cha ndani, hukwapua cha nje kuja kuwafaa wenzake walio nyumbani na sio vinginevyo. Na uwezo wa kutajirika kwa kutumia rasilimali za wengine, ikiwa ni pamoja na umeme, kutokana na nchi zinazotuzunguka Watanzania tunao, isipokuwa hatuna uongozi unaoona wala kuelewa hili.
Vilevile, hili huweza kufanyika tu katika nchi ambayo chama tawala hakiendeshi nchi kana kwamba ni wabunge wake tu na wanachama wake wenye uwezo wa kuwa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu wakuu, wakurugenzi, mamaneja, majaji, mabalozi na wafanyakazi nchi za nje na wasimamizi wa taasisi mbalimbali. Bali kinaendesha nchi kwa kutumia akili, uwezo na michango ya Watanzania wote bila kujali ni wafuasi wa chama tawala au la.
Miaka hamsini baada ya Uhuru dunia imeipa fursa kubwa nchi yetu ya kuchagua na kuwakaribisha wataalamu tofauti toka sehemu mbalimbali duniani wenye ujuzi na uzoefu wa kila aina kuanzia watengnenezaji baiskeli hadi waunda satelaiti na roketi. Hawa ni binadamu wenzetu amabo leo ni 'jobless' pamoja na utaalamu au elimu na uzoefu wao, walioko huko Marekani, Ulaya Magharibi, Ulaya Mashariki, Marekani ya Kusini na Asia. Watu ambao tukiwapatia nyumba, gari na mshahara wa kukidhi mahitaji yao ya msingi wapo tayari kuja nchini hapa kusaidiana na sisi kuifanya nchi yetu iendelee kwa kasi na haraka zaidi. Kinachotakiwa ni kutambua hili na kujipanga kulishughulikia kwa namna ambayo litakuwa ni la faida kwetu sote, kwao na sisi kadhalika. Ni rahisi, kulizungumza hili kwa maneno, lakini ukweli ni kwmba kwa uoga, uziwi na upofu wa viongozi wetu hususan kuhusiana na yale yanayoandikwa na magazeti ni GUMU KAMA GAMBA LA KOBE.
Ila kwa bahati nzuri, kutokana na kukua kwa demokrasia nchini hapa upo uwezekano kwamba hili likifumbiwa macho na watawala, haliwezi kuachwa kuokotwa na wapinzani na wanaharakati wengine wenye mapenzi ya dhati ya nchi yao na uchungu na umasikini wa wananchi wenzao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment