Saturday, September 10, 2011

Benki Kuu iwe na kapu la sarafu mchanganyiko

HALI ya kifedha na kiuchumi ya Marekani na misuguano ya kisiasa inayoendelea nchini humo haitupi moyo Watanzania kwamba panaweza kuwa na mabadiliko ya maana kiuchumi duniani hivi karibuni.

Marekani na nchi za Ulaya zenye matatizo makubwa zimekuwa zikiishi nje ya uwezo wao kifedha. Kwa maana ya kwamba serikali za nchi hizo zimekuwa zinatumia fedha nyingi kuliko fedha zinazoingiza kila mwaka, na hivyo kukuza mzunguko wa deni na riba serikali hizo zinazodaiwa kwa hasara ya wananchi wao. Wote tunajua hatari ya mtu anayedaiwa. Akiugua ghafla au kupatwa na janga fulani basi ndio wanaomdai wasahau tena kupata chochote kutoka kwake. Ndivyo zilivyo serikali ambazo baadhi yake nchi zetu zimewekeza na hivi leo zina matatizo makubwa ya kifedha. Hali ikiwa mbaya zaidi katika nchi hizo hawatatufikiria sisi kwanza bali wananchi wao kwa hasara yetu na nchi zetu. Ndio maana, wazo la kuwa na kapu la benki kuu lenye sarafu mbalimbali halitofautiani sana na kuweka mayai waliotaga kuku wetu wa kiuchumi katika makapu mbalimbali na sio kapu moja.

Ukizingatia pia kwamba hali ya kifedha ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya kwa baadhi ya wanachama wake ni muflisi, ipo haja ya Waafrika na hususan Watanzania kuzinduka na kukagua upya kama sarafu na vito vya thamani vilivyoko katika hazina yetu ndivyo vinavyoweza kutunusuru kama hali ya kiuchumi duniani itaendelea kuzorota au kuwa mbaya zaidi ya ilivyo hivi sasa.

Hivi karibuni, Gavana wa Benki kuu ya Shirikisho la Nigeria, Sanussi Lamido Sanussi, ametangaza kwamba benki kuu ya nchi hiyo kuanzia sasa itaweka akiba yeke ipatayo asilimia 10 katika fedha za Kichina au Yuan. Hiki ni kitendo cha kijasiri na kiume na ambacho kinastahili kuwa fundisho kwa nchi nyingine za kiafrika ambazo kwa miaka mingi sasa zimekuwa kama mateka kama sio watumwa wa dola ya Marekani au Faranga ya Kifaransa au Pauni ya Kiingereza.

Hili liliweza kuwa sawa wakati ambapo dalili zote zilionesha nchi hizo ni kubwa na zenye uchumi usioterereka na uliokuwa ukikua kwa kasi inayobashirika. Katika miaka hii ambayo, utegemezi wa nchi hizo kwa rasilimali na biashara toka nje umeendelea kuongezeka ni hatari sana kukubali hifadhi ya taifa kuwa katika sarafu ya nchi moja au mbili tu.

Jambo hili tofauti na huko nyuma inafaa lizungumzwe na wananchi wakiongozwa na wataalamu wa uchumi na mambo ya fedha badala ya kuishia kufanyiwa uamuzi na serikali au benki kuu peke yake. Ukiritimba huu wa maamuzi ndio uliosababisha dhahabu kupakuliwa toka Benki Kuu kiujanja na kuiacha Tanzania ikipata kipigo kushoto na kulia kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu yake na kupanda kwa bei ya mafuta.

Mazungumzo kama hayo yatatusaidia pia kuepuka kudanganywa na nchi zilizoendelea kwa kugaiwa kondomu na chandalue zenye dawa za bure huku nchi hizo zikihamisha vitu vyenye thamani mara elfu kumi kama sio zaidi kwa matani kwenda kuwatajirisha huko kwao na kuendelea kutuacha sisi masikini wa kutupwa na ombaomba.

Yuan inapigwa vita kwa madai kwamba China bado ni nchi ya kikomunisti na kidikteta, hoja ambayo inakataliwa na wengi kwamba sio kikwazo maana Wachina walio wengi wanaridhika na mfumo huo kwa kuwa umewaletea shibe na neema. Kuna maana gani ya kuwa huru, huku ni masikini unayetumika na wakubwa?

Hali kadhalika, kutokana na wingi wao ni vigumu kuwa na nchi isyodhibtiwa kwa karibu. Viongozi wa Kichina wanaonekana pia kuwa bado ni wanafunzi katika demokrasia na siasa za kiliberali na hivyo wanahitaji kupewa muda zaidi kuweza kuachia mambo yawe yanayojiendesha yenyewe.

Dai lingine ni kuwa fedha ya China inadhibitiwa na haiachiwi kutulia na kuamua thamani yake halisi ukilinganisha na fedha nyingine duniani. Jambo hili nalo linaeleweka na kwa yakini nchi zinazoendelea zinachagizwa kuiga vivyo hivyo, kwani ukiilazimisha sarafu yako kupimwa na sarafu zenye nguvu zaidi, daima ni wewe utakayeumia na sio wale wenye nguvu. Wachunguzi wanaamini katika hili pia China inahitaji muda ili kuhakikisha ughali wa vitu vinavyotengenezwa Ulaya kwa sababu ya mishahara mikubwa ya Wamarekani na Wazungu haiingilii biashara na faida ya Wachina ambao wanalipa mishahara midogo na kukubali kuishi kimasikini ili wenzao katika nchi zinazoendelea wapate bidhaa zisizokuwa ghali.

Ni lazima tuoanishe mahitaji yetu toka nje na sarafu za nchi tunazotakiwa kuwa nazo katika hazina ya benki kuu. Ninaamini masuala kama mitambo, magari na mashine, mafuta, wapewa kandarasi za ujenzi wa miundo mbinu, masoko ya mazao yetu, masoko tunayonunua teknolojia zetu mbalimbali, wanakotoka wawekezaji wetu wakubwa, wataalamu na rasilimali watu muhimu tunazohitaji vinaweza kutumika kuchagua kapu la sarafu Benki Kuu yetu inayostahili kuwa nazo wakati wowote kwa ajili ya kujikinga na kupanda na kushuka kwa uchumi wa dunia na thamani ya shilingi yetu.

Ni dhahiri katika kufikia uamuzi wa jambo hili kuna wengi watakaopinga. Lakini kwa watu kama hao tunawataka watofautishe maamuzi ya kifedha/kirasilimali na maamuzi ya ya kisiasa na mazoea. Pamoja na mapungufu yake kadhaa kisiasa na katika haki za binadamu bado ukweli unabakia pale pale kwamba hatuwezi kukwepa kufanza biashara au kuwa na miradi inayojengwa na Wachina hapa nchini. Kwalo hilo tu, litatuondolea adha ya shilingi kupungua ukilinganisha na dola, maana thamani kati ya yuan na shilingi inaweza ikabakia pale pale kwa faida yetu.

Kwa kuikubali yuan ya Uchina tutawarahisishia pia wawekezaji wa Kichina na Mashariki ya mbali kwa ujumla wanaotaka kuwekeza hapa nchini, kwani tayari yuan inakubalika kama sarafu ya uwekezaji sehemu mbalimbali duniani. Hii ina maana wawekezaji wazawa hapa nchini wanaweza kuuza hisa katika yuan kwa Wachina ili wawe wabia wao katika uwekezaji na hivyo kupata wawekezaji wazito zaidi kutoka huko, kuliko tunaowapata hivi leo ambao wameishia kushindana na Wamachinga Kariakoo.

Aidha tunaweza kukopa toka Uchina kwa kununua hawala za Kichina kwenye sarafu yao ya yuan/renminbi na hivyo kupunugza machungu ya riba kubwa kutokana na kushuka kwa thamani ya dola ukifananisha na shilingi ya Tanzania.

Wazo kubwa hata hivyo kwa wakati tulionao unaitaka Afrika Mashariki kuanzisha sarafu yake ndani ya sarafu zilizopo. Sarafu hiyo, tuseme, iitwe, Pauni au Dola ya Afrika Mashariki itaundwa kwa kuzihusisha sarafu muhimu duniani kama Pauni ya Uingereza, dola, yuan ya Uchina, Yen ya Japan, Kronor za Scandinavia, Escudo za Brazil, rupia za India na Euro ya Jumuiya ya nchi za Ulaya. Sarafu hii itaachiwa taratibu kama ilivyo kwa Euro Ulaya kuzing'oa sarafu binafsi za kila nchi na hivyo kurahisisha kuja kwa soko la kifedha la pamoja la Afrika Mashariki na masoko mengine yatakayofuatilia.

Ieleweke kwamba pale msiba unapotokea kwa mwenzio, kwako kunaweza kuwa harusi,kwa maana kweli unaoza mwana au kwa kuwa jirani yako alikuwa mchawi.

Uchumi wa dunia unapotatizika, sio lazima uchumi wetu nao pia uwe kwenye matatizo. Lakini hili linahitaji uangavu, uweledi wa mambo, uzuzi na ubunifu wa yale yasiyoyumkinika na ambayo wengi huchelea kuyafanza kwa kuhofia hasara kumbe kwa kuyafanya watanufaika na kunufaisha nchi na watu wao. Huu ni wakati kama huo, kwa kutumia fursa za kiutandawazi tunaweza kugeuza matatizo yetu yakawa ndiyo chanzo chetu cha kufanikiwa katika mengi ambayo huko nyumba tulishindwa. Maana maendeleo yote hutoka katika akili za mtu, lakini sio wale wanaoiba na wasiojua undani na usadifu wa wazo husika.

No comments:

Post a Comment