KAMA jiji hili ambalo ndilo lenye Ikulu na wizara na idara zote muhimu nchini linataka liondokane na uchafu, harufu mbaya mpaka misikitini na makanisani, kinyesi kinachozibuliwa wakati wa mvua barabarani na mandhari za kuchukiza sasa ni wakati wa kuirudisha kazi ya usafi wa jiji kwa wanajamii kwa kiasi fulani badala ya kutoa tenda na kukodisha mchakato wote kwa watu wasio na uwezo na wasiokidhi mahitaji na matakwa ya usafi wa jiji hili.
Serikali kuu na serikali za mitaa zitatakiwa kutoa ushirikiano maalum ili kufanikisha azma hii.
Tofauti na mambo mengine, ningelipendekeza kazi hii ipewe umuhimu wa juu hata machoni kwa watu wa nje wanaotaka kuisadia nchi yetu katika masuala ya utunzaji mazingira na usafi.
Kinachopendekezwa hapa ni kuachana na utitiri wa magari na matrekta mabovu katika kazi ya kukusanya na kusomba taka kuzipeleka huko zinakotupwa. Badala yake kutoa ajira pana na za kudumu kwa kina vijana wetu wenye matoroli, maguta, pikipiki, vipawatila, bajaji, mikokoteni na wilibaroo kufanya kazi ya kukusanya taka mitaani na kwenda kutupwa kwenye eneo maalum litakalokuwa na shimo kubwa la kutupwa taka zilizotenganishwa kiaina na kiufundi na kisha kuchakatwa hadi kuzalishwa bidhaa mpya inayoweza kutumika majumbani, viwandani na mashambani.
Umuhimu wa serikali kuu na serikali za mitaa ni katika kupatikana kwa maeneo maalum ya kuchimbwa mashimo hayo mitaani au kwenye kata; ujenzi wa miundo mbinu rahisi ya kukokotosha taka kuwa bidhaa hitajika; kuwaandaa vijana kimafunzo tayari kwa kazi za kutenganisha taka na kuzibeba kwenda kwenye maeneo husika; na kuhakikisha bajeti ya usafi toka serikalini na misaada ya wafadhili inaelekezwa kwenye mambo haya badala ya kuliwa na wajanja wachache huko walipo.
Italazimu pia kwa viongozi na maofisa wote wa jiji na katika wizara husika, ambao wameomba kupewa hisa na chochote na wawekezaji katika miradi mipya tarajiwa ya kurejelea taka kupewa ruhusa maalum na serikali kuu ya kuwekeza kwenye makampuni bila kutoa chochote !
Aidha wanajamii kwa kushirikiana na serikali kuu na za mitaa watapaswa kuwa na kisima cha maji kilichochimbwa kwenye eneo au kina ambacho maji hayakauki kamwe ili kuhakikisha mji unakuwa na mandhari nzuri na ya kuvutia wakati wote. Maji hayo pia yatatumika kusaidia kazi za kupooza na kulainisha bidhaa katika kituo kikuu cha kubadili taka kuwa mali na utajiri. Ndoto ya kuwa na mifumo mizuri ya kuvuna mvua itakuwa ziada ambayo si mbovu katika hili.
Kila nyumba italazimika kupatiwa pipa pacha nne au kwa maneno mengine pipa ambalo lina sehemu nne: moja kwa ajili ya kutupwa chupa na glasi: la pili kwa ajili ya kutupwa karatasi: la tatu kwa ajili ya kutupwa mabaki ya vyakula na la mwisho kwa ajili ya kutupwa taka ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu na taka mchanganyiko nje ya hizo hapo juu.
Vijana wakusanyaji watafunzwa jinsi ya kuzihamisha taka hizo toka mapipa hayo kwenda mifuko maalum ambayo itachukua taka kwa mpangilio huo huo huo na kuzipeleka kwenye kituo kikuu cha taka kwenye mtaa au kata kwa ajili ya kurejelewa upya kuzalisha kinachowezekana kuzalishwa.
Zitakapofikishwa kituoni hapo taka zitakuwa tayari zimetenganishwa kwa utaratibu huo hapo juu na hivyo kuingizwa kwenye moja kwa moja kwenye eneo zitakazofanyiwa kazi ili kuzalisha umeme au kutoa bidhaa fulani itakayotumika kama bidhaa mpya tena madukani au sokoni. Mabaki ya vyakula yanatarajiwa kutengenezwa kuwa mbolea asili isiyo na dawa yoyote ambayo itauzwa kwenye mifuko maalum kwa wakulima na watunza bustani.
Watumishi wizara ya ardhi wataaswa kwamba ili kuleta uwiano kati ya klutenda dhambai na mema- nchini ni muhimu kwao pamoja na kuuza maeneo wazi kwa mabwanyenye wetu wapya, sasa kutoa maeneo kwa ajili ya uchimbaji mashimo makubwa ya uhifadhi wa taka zitakazochakatwa na kuwa bidhaa mpya au kuzalisha umeme kwa ajili ya faida ya wakazi walio wengi jijini.
Wataalamu wa vyama vya siasa vyenye vijiwe mjini wataombwa wautumie utaalamu huo ili kugeuza vijana wetu toka 'majoblesi alwatani', wababaishaji na kupe wenye sifa za kimataifa kubadilika kwa kukopeshwa mitaji ya kununua toroli, maguta na vifaa kama hivyo ili kuwa wakusanyaji na wabebaji taka watakaoipa heshima mpya jiji la Dar es salaam.
Wataalamu wa kupiga raia mabomu, kuvunja maandamano na mikutano wataombwa kuutumia utaalamu wao ili kuhamasisha kazi ya usombaji taka kila wakati ili pasiwe na taka hata moja mahala popote jijini kwa kasi ile ile ya upigaji mabomu ya machozi wakati wa maandamano ya upinzani, wafuasi wa dini fulani au wafanyakazi au wanafunzi.
Mameneja wa migodi wataaombwa kuazimisha magreda na makatapila kuja kuchimba mashimo hayo katika mitaa au kata mbalimbali jijini kama walivyofanikisha zoezi la uchimbaji mashimo huko Geita, North Mara na Bulyanhulu,kutegemeana na kiwango cha uzalishaji taka katika maeneo husika.
Badala ya kuwa na magari mabovu yanayosafiri umbali mrefu kuokota na kutupa taka sasa vitoroli, mikokoteni, bajaji, guta na pikipiki zitatengenezwa kwa njia ambayo kwazo zitakuwa zikipeleka taka kwenye maeneo hayo yenye mashimo na miundo mbinu maalum ya kupokea taka zilizotenganishwa na kuanza kuzifanyia mchakato ili zitoe bidhaa za aina mbalimbali na kuzalisha umeme na vitu vingine vitakavyowezekanika.
Taka zinazohitaji kutupwa mbali zitachukuliwa na magari makubwa maalum machache lakini yenye kiwango cha kimataifa kwenda kutupwa mbali kabisa na makazi ya watu na wakati mwingine hata kwenda kufukia mashimo yaliyotokana na kuchimbwa madini yetu katika mikoa ya kaskazini na kusini.
Ukiutazama mtiririko huu mzima utagundua kuwa pendekezo hili lina shabaha ya kugeuza taka kuwa mali kwa namna kadhaa. Kwanza, vijana ambao wana tatizola ajira itabidi sasa wakimbie ajira wao wenyewe. Taka zitageuka fumba na kufumbua mali, maana kila mzigo kutegemeana na aina yake utakuwa ukilipwa fedha nzuri tu mara ukifika kwenye kituo kikuu cha kuchakata taka kwenye mtaa au kata.
Aidha magari mabovu ya kusomba taka amabyo wakati mwingine badala ya kusafisha mji huuchafua yatatoweka. Takataka hizo zitazaa bidhaa ambazo wafanyabiashara na wanunuzi watanufaika kwani zina uwezekano mkubwa wa kuwa za bei rahisi zaidi kuliko nyinginezo. Kisha mbolea itakayozalishwa itakwenda kuzistawisha bustani za Ikulu na Mnazi mmoja na maeneo mengine mjini na hivyo kulipa jiji mandhari ya kukata na shoka kwa uzuri wake. Hali kadhalika, sio tu tatizo la kukatikakatika umeme jijini litakuwa historia bali mradi huu utahakikisha hata nyumba mbavu za mbwa zilizo mabondeni zinapata umeme wa kutosha na wa uhakika kila siku.
Vilevile visima vitakavyoendana na mradi huu vitawahakikishia wakazi wa kila mtaa na kata upatikanaji maji masafi ya uhakika wakati wote, wakati wanasubiri maajabu yatakayofanywa na DAWASCO miaka mitano au kumi ijayo kama bado wako hai. Hili linawezekana, cheza nafasi yako na timiza wajibu wako. Miaka hamsini baada ya uhuru hutakiwi kushindwa na jambo hili.
Wakati ninaandika makala haya watafiti wanaonisaidia wameleta habari kwamba kuna watu tayari wameanza kujituma wenyewe na kuanzisha miradi kama hii. Kama hili ni kweli basi wilaya, mkoa na wizara husika zichangamkie mara moja jambo hili. NIna hakika likipata kuungwa mkono nao ni kitu kinachowezekana na kitakalolifanya jiji la Dar es salaam kuwa jiji la kuigwa na miji mingine sio tu Tanzania bali Afrika nzima.
lle tabia ya kujifanya kuwa serikali inaweza kufanya kila kitu si kitu kizuri. Na katika miaka hii ni kitu kilichopitwa na wakati na kuwazaini wananchi huku tukijua fika tunasema uongo. Kweli Watanzania hawana fedha, yaani, ni maskini. Lakini Watanzania wana kitu kimoja ambcho thamani yake wakati mwingine ni kubwa kuliko fedha. Kitu hicho sio kingine ila akili na nguvu zao. Pakiwa na uongozi unaoona mbali na mbele na unaojua kutumia akili na nguvu hizo na kuwekeza fedha kidogo Watanzania kama watu wengine wana nafasi ya kufanya maajabu mbalimbali duniani.
Friday, November 25, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment