Sunday, November 25, 2012
Kwanini Ushirika, Vijiji na Miradi ya Pamoja Inakwama ?
AGHALABU husemwa kwamba anayeumwa na nyoka akiona jani hustuka. Hii ndiyo hadithi ya shughuli za Ushirika, vijiji na miradi ya pmoja katika sehemu mbalimbali za nchi.
Baada ya shughuli hizo kuingiliwa na siasa na wanasiasa na hatimaye kuchafuliwa kama sio kuharibiwa kwa kiasi kikubwa, Watanzania wengi walikatishwa tamaa na shughuli zozote zilizohitaji kufanzwa na mtu zaidi ya mmoja. Kila mmoja akawa ameamua kwenda kipweke pweke, hata pale ilipoonekana dhahiri kuwa jambo linalofanywa haliwezi kufanikiwa bila umoja au ushirikiano wa namna moja au nyingine kati ya watu wawili au zaidi.
Katika uchambuzi wake wa kisayansi kuhusu nadharia za ushirikishwaji umma nchini, Bi. Rebecca Maarsland (2006) alibainisha kwamba ushirika na ushirikishwaji watu Tanzania kumeathirika kwa kiasi kikubwa na mapambano kati ya walio nacho na wasio nacho. Serikali ya awamu ya kwanza kwa nia njema kabisa iliamini na kutekeleza dhana ya ushirikishwaji umma kwa lengo la kuwanasua Watanzania na umaskini wa kupindukia. Hata hivyo. viongozi wa vikundi vya ushirika walijikuta wakiwa na uwezo na fedha chungunzima na hapakuwa na njia nyingine ya kuutumia ila kwa kuingia katika siasa. Wanasiasa kwa upande wao walitegemea kodi iliyolipwa na wananchi nayo haikutosha pia kuwapa na fungu la kujiimarisha kisiasa. Hivyo, ushirika na viongozi wake wakawa ni tishio kwa viongozi wengine wa kisiasa. Mkwara ndipo ulipoanza. Wanasiasa na mangimeza hawakuwa tena na nia ya kuendeleza ushsirika bali kuua ushirika.
Ushirikwa na ushirikishwaji ulistawi tu kati ya Uhuru na kabla ya kuanzishwa kwa CCM. Kuna wanaoamini kwamba hayo yalikuwa hivyo kwa sababu ni mtu mmoja tu aliyekuwa na nia ya kweli ya kuwasaidia Watanzania mafukara kupitia ushirika. Huyo hakuwa mwingine ila Mwalimu Nyerere. Inaelekea katika timu yake nzima ya uongozi hakuna aliyefahamu dhana ya ushirikishwaji achilia mbali kuamini katika nadharia hiyo na kuitekeleza kwa vitendo.
Wakati Tanzania ilisifika sana kimaneno kwa ushirika, yakini, ushirika wa kweli kwa vitendo ulikuwepo Kenya japo kuwa wakati huo tukiwazomea kuwa wao ni wanyama au ubepari ni unyama ! Kweli ubepari ni unyama, lakini tofauti na ilivyo hivi leo Tanzania, Kenya wana kimbilio la kujihifadhi kama vyama vyao vya ushirika na vinawasaidia si haba. Tanzania hawana pa kukimbilia.
Walioathirika sana ni wananchi ambao walifikia kuona ushirika ni baba na mama kwao. Ushirika ghafla ukawa ni wizi na unyonyaji wa masikini na wala sio mwokozi na kimbilio lao tena. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa kufa kwa ushirika nchini na imani ya wananchi kwa kitu kiitwacho ushirika. Hadi wa leo jeraha hilo kubwa halijapona.
Nyerere alipowaachia viongozi wake wajenge na kuendeleza vijiji vya kijamaa ili nchi iwe na mfano unaong'aa kwa Afrika yote na dunia, maofisa wake walioona hiyo ni nafasi ya kuwakomoa wanavijiji tajiri na jeuri na hivyo wakawatoa kuliko na ardhi nzuri na yenye rutuba na kuwapeleka kwenye mawe na mchanga. Huo ukawa ni mwanzo wa kifo cha vijiji Tanzania, sambamba na kufanikiwa kwa vijiji vya Uyahudi Kibutz huko Uyahudi, ambavyo, hivi leo ni mfano kwa dunia nzima.
Miji ilionekana kuwa na mameneja wazuri na hivyo kuiendesha miji yao vizuri ikatuhumiwa kuwatajirisha na kuwapa kichwa mameneja na viongozi wake wengine, hivyo mkwara ukatafutwa na CCM wa kumaliza nguvu pia halmashauri za mji nchini. Huo ukawa ni mwanzo wa kuwa na miji dhaifu na michafu Tanzania.
Kukosekana na ukweli na dhati pamoja na wanasiasa na mangimeza kuona miradi ya pamoja kama ni kazi ya kusadia masikini na watu walio nyuma kimaendeleo na sio kazi ya kuonesha uwezo wao kama viongozi ulichangia si haba....
Utafiti usio rasmi nilioufanya unaonyesha kwamba hivi leo Watanzania hawana imani kabisa na kitu kinachoitwa ushirika wala miradi inayofanywa na watu wengi wasioshabihiana kwa mengi. Nalo hili kwa kiasi limechangiwa na siasa na sera za chama tawala ambacho kwa makusudi ziliua moyo sio tu wa kujitegemea bali dhana nzima ya ushirika na ushirikishwaji nchini. Hata hivyo, ukweli haukanushiki kuwa ushirika na uendeshwaji wa vijiji kama makampuni ndio njia pekee ya kuwatoa kwenye umasikini watu walio wengi na hakuna njia nyingine rahisi kama mbadala.
Nadharia mpya juu ya ushirika na ushirikishwaji watu zimeweza kutanabaisha kwamba kuna ngazi mbalimbali za ushirikishwaji watu na upelekaji madaraka kwenye ngazi za chini iwezekanavyo kwa faida ya walio wengi na sio wachache.
Ukiipandikiza nadharia hii katika sehemu za mashambani au vijijini Tanzania utaona kwamba katika miaka yetu yote ya kusumbuka na Ushirika na ushirikishwaji wananchi Tanzania haikuwa imekwenda popote. Ilikuwa chini kabisa katika modeli za nadharia ya ushsikishwaji watu na mgawanyo wa mamlaka au madaraka kwa wananchi.
Kuna ngazi zipatazo nane katika nadharia hiyo ya ushirikishwaji. Ngazi hizo ni ile ya mwisho au ya chini kabisa, ambayo ndiyo ile iitwayo ya hila, ujanja, uzaini au kuchezea (manipulation) ushirika na ushirikishwaji watu katika masuala mbalimbali. Katika hatua hii serikali kuu, serikali za mitaa, NGOs, makundi ya kiimani na mengineyo kwa kuwatumia watu iwe mjini au vijijini wanatafuta kunufaika wao kwanza na sio kuwastawisha walengwa. Ndio maana inaiitwa pia kuchezea watu au kucheza na maisha ya watu. Ni mzaha na utani mtupu. Kwa bahati mbaya hii ndiyo hatua ya chini na ya mwisho kabisa na masikini Watanzania hapo ndipo ushirika na ushirikishwaji wao ulipo kwa hivi leo.
Ngazi ya saba ni ile ya kuganga (therapy) ambayo hutokea pale watu fulani wanapokuwa na tatizo basi tatizo hilo huhitaji ushirikishwaji wao ili kulitatua. Kwa hiyo ushiriki wao huanzia na kuishia hapo. Kwa mfano, kikizuka kipindukipindu ushirikishwaji huu huwa unatumika zaidi kuliko wa aina nyinigne yoyote.
Ngazi ya sita ni ule ushirikishwaji wa kuarifiwa au kupewa habari au taarifa kwamba mnafanyiwa hili au lile. Wanaohusishwa zaidi ni viongozi wa kijiji au mtaa au sehemu husika. Kwa mfano, huu ndio mtindo maarufu zaidi unaotumiwa na TANAPA na washirika wake katika kulinda na kutunza hifadhi za wanyama kwa kuwashirikisha wananchi. Wananchi hawana sauti yoyote ya maana isipokuwa kugawia ambacho wenyewe tayari pia wamekwishajigawia.
Tuliza au bembeleza ndio ngazi ya tano ambayo kama neno linavyoonyesha watu fulani wanabembelezwa kama sio kudekezwa au kutulizwa kwa kufanyiwa hili au lile halafu wenye mradi wakaendelea na shughuli zao kama kawaida bila kusumbuliwa na wanaowazunguka. Hilo hutokea sana katika miradi ya uchimbaji madini, gesi na mafuta.
Kwenye ngazi ya nne sio tu watu wanabembelezwa na kutulizwa na kitu kidogo au miundombinu na zawadi hizi na zile bali pia wenye uwezo wanatafuta ushauri toka kwa wasio na uwezo. Mathalani, serikali kuomba ushauri wa raia, au mwneye mradi wa uchimbaji tanzanite kuomba ushauri wa watu wa Merelani. Lakini bado, watu wanakuwa hawana uwezo wa hali na mali katika mradi husika.
Hatua yenye afadhali zaidi ni hatua ya tatu. Katika hatua hii ambayo inaitwa UBIA, raia au wananchi au wakazi wa sehemu husika wanakuwa ni wana hisa katika mradi husika. Mathalani, katika kilimo mwekezaji anapokubali kushirikiana na wanakijiji ili kuzalisha mazao fulani kwa ajili ya kuuza nchi za n je na kisha faida ikagawanywa kama ilivyokubaliwa katika mkataba ulioridhiwa na wanajiji wote kwa pamoja.
Ngazi ya pili na ya kwanza ndio za juu kabisa katika ushirika na ushirikishwaji wananchi. Ya saba ni ile ya kukaimishiwa madaraka au mamlaka, mathalani, mkoa kuwa na gavana badala ya kiongozi wa kuteuliwa na kuruhusiwa kusimamia mambo yake ya kiuchumi na kijamii bila kuingiliwa nas erikali kuu katika utendaji shughuli zake za kila siku ili kuharakisha maendeleo ya mkoa na nchi nzima.
Ngazi ya nane ni ile ya mamlaka au madaraka kuhodhiwa na wanakijiji au wanamtaa au wananchi wa eneo husika. Hii ndiyo ngazi ya juu kabisa katika ushirika na ushirikishwaji umma, ikiashiria pamoja na mambo mengine uhuru kamili wa watu kuendesha mambo yanayohusu maisha yao ya kila siku bila kuingiliwa na watu wanaokaa na kufanya kazi mbali kabisa na wao.
Ni dhairi kuwa Tanzania katika suala hili la ushirika na ushirikishwaji umma ndio kama vile tena tumeanza. Inasikitisha sana. Lakini ndio ukweli. Wenye niia ya kuufufua ushirika na moyo wa ushirikishwaji na kujitegemea kwa watu wetu ni lazima waanze kwanza kwa kazi ya kuwadhihirishia kwamba yaliyofanyika huko nyuma ni mkaosa na bado ushirika na mchango wao katika miradi ya kiuchumi na kijamii ni nunu yenye thamani kubwa na haiwezi kuwa na ushindani wa aina n yingine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment