Monday, April 25, 2011

Dini, Vyama vya Siasa na Katiba mpya

NINAAMINI ya kwamba huu ni muda mzuri wa kuzungumzia kichwa hicho hapo juu cha makala haya, siku ya leo, wakati wenzetu Wakiristo wanapokuwa wakiadhimisha sikukuu yao muhimu ya Pasaka.

Katika miezi ya karibuni hapa Tanzania kumekuwa na vuta nikuvute kati ya dini mbili kubwa, yaani, Wakatoliki na Waislamu kwa upande mmoja na kwa upande mwingine vyama vya CCM na CHADEMA na wale wanaoabudu ukubwa, maslahi
na manufaa yao binafsi kutaka kuwachanganya Watanzania kwa kuweka misalaba, mwezi na nyota katika bendera za vyama vya kisiasa isivyo rasmi.

Jambo ambalo ninaliona sio linalosasaisha mfumo wa vyama vingi, siasa na uongozi wetu bali linaloturudisha nyuma kimaendeleo kwa miaka kadhaa. Maana madhara ya hili yanaweza kuiangamiza nchi fumba na kufumbua na amani na umoja tunaouimba vikafunikwa na vilio, usononi na damu kwa miaka mingi ijayo. Na badala ya kujengea watoto na wajukuu wetu taifa lenye umoja na amani tukawajengea taifa la mauaji na balaa zisizokwisha kama ilivyo kwa nchi ambazo tayari zimeshajitupa katika tope la moto la volkano ya kuchanganya dini na siasa.

Inafaa kwa viongozi wetu wa kisiasa, kibiashara, kidini na kijamii kutumia muda huu kutafakari ni kwa namna gani tunaweza kuendeleza utaifa, umoja na amani yetu pamoja na tofauti zetu mbalimbali na kutokubali kuwa kama NIgeria ambapo Waislamu huamua kumpigia kura mgombea urais eti tu kwa sababu ni wa dini yao na wakiristo nao kadhalika huamua kumpigia mgombea urais kwa misingi kama hiyo hiyo.

Washikadau wote wa katiba mpya ni lazima watambue umuhimu wa kifungu kinachohusu dini katika katiba. Maana michango yao bila shaka ndiyo itakayosaidia kupata aina ya kifungu au ibara muafaka na mujarabu kuhusu dini katika katiba mpya ambacho kitatulinda sote na vizazi vijavyona kikawa hakipendelei au hakionei dini hii au ile.

Ingelifaa pamoja na mambo mengine ibara husika iwe na mambo yapi ya dini ni muhimu kuwa katika katiba ;ufafanuzi uwepo kuhusu uhusiano wa vyama vya siasa na dini; uhusiano wa serikali na vyama vya siasa na yale yote ambayo kwa kuangalia nyakati tulizo nazo yanaweza kuwa vichochezi vya matatizo au chachu na changamoto ya kujenga nchi yetu iwe na umoja na amani wakati wote, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, bila dini kuwa sababu ya kuvunjika kwake.

Ni wakati mzuri pia wa kuwafichua wale wanaoingia katika siasa na serikali kwa malengo ya kidini kama ilivyo kwa wale wanaoingia katika siasa na serikali na kuogopa kuwatendea haki watu wa dini zao eti kwa kuwa wao ni viongozi na wanahofia kujikwaza kwa kufanza hivyo. Kiongozi yeyote akishindwa kuwa mkali kama Baba wa Taifa alivyokuwa mkali kwenye jambo hili, atambue kuwa ndiye atakayekuwa chanzo cha mwanzo wa mwisho wa amani na umoja wa Watanzania.

Uwazi katika mahusiano ya viongozi wa dini na wanasiasa ni kitu cha kufa au kupona, maana ni pale 'vichaa wa kisiasa' wanapofunga ndoa na 'vichaa wa kidini' ndipo mambo katika jamii husika yanapokwenda arijojo na kuvunda.

Hakuna Mtanzania anayependa kusumbuliwa na umaskini, maradhi na ujinga. Na kwamba jukumu na wajibu wa kila dini pamoja na kuokoa roho za wafuasi wao ni kuipa akili na miili yao afueni hapa duniani. Na katika hili dini zote zinastahili kushindana katika kumsaidia Mtanzania bila kujali ni wa dini gani. Dini zipo kwa ajili ya kuwafaa masikini zaidi kuliko viongozi na matajiri.

Uhuru wa kuabudu pamoja na kila dini kuwa na taasisi zote zinazosaidia waumini wao kutekeleza imani yao kwa mujibu wa dini, vitabu na mafundisho yao husika ni jambo muhimu. Hili liendane pia pamoja na makubaliano juu ya taratibu za kiimani katika shule, vyuo, maofisini na mahala pengine pa kazi ili pasiwe na anyenyimwa uhuru wa kuabudu kwa kisingizio kimoja au kingine. Aidha, pawe pia na usawa katika sikukuu za kidini na upambaji katika maofisi ya serikali, umma na binafsi.

Hiki kiwe kipindi pia cha kukata mzizi wa fitina kuhusu kuchanganya dini na siasa au siasa na dini. Watanzania tufikie mahala pa kuamua na kukubali mipaka ya viongozi wa kila sekta au la tunakaribisha matatizo yasiyokuwa na mwisho. Mathalani, kwa kuruhusu viongozi wa kiuchumi (wafanyabiashara) kuingia katika siasa tumeona jinsi ufisadi na rushwa zilivyokithiri. Na ni pale ambapo viongozi wa dini walipoanza kuingilia moja kwa moja kisiasa badala ya kuwaongoza, kuwaelimisha, kuwarekebisha na kuwataadibu wanasiasa basi wanasiasa wanaotafuta urahisi wa mambo wameamua kabisa kuwanunua baadhi ya viongozi wa dini kwa maslahi binafsi na sio ya wafuasi wao wala ya nchi na watu wake. Hivi leo dini zetu na viongozi wake wamebaki kulalama bila kujijua wao wenyewe ndio tatizo, maana kondoo wao, wakiwemo wanasiasa wakubwa kwa wadogo hawana wachungaji. Hakika unaweza 'ukamtumikia kafiri kupata mradi wako,' lakini vilevile 'unaweza ukamtumikisha kafiri ili upate mradi wako.'

Siasa wakati mwingine huitwa mchezo mchafu na kiongozi yeyote wa dini anayejiingiza humo asisahau kuna siku lazima atapakwa matope kama sio kinyesi. Kwa ushauri wangu, Tanzania haitajengwa na wanasiasa tu (na hasa kukiwa na 'levo graundi') na kwamba madaktari, walimu, wakulima, wanamichezo, wasanii, wafanyakazi, wataalmu mbalimbali, wafanyabiashara, watoa huduma kila mmoja wetu ana mchango mkubwa anaoweza kutoa kwa nchi yetu na watu wake. Kazi ya katiba mpya iwe ni kuhakikisha kwamba sio wanasiasa tu wanaolipwa vizuri bali kila mtu katika nafasi yake na ikiwezekana wanaoingia katika siasa wasilipwe mishahara tofauti na ile ya elimu na utaalamu wao. Kwa maneno mengine wanaostahili kulipwa vizuri zaidi ni wale wanaowaletea wananchi na nchi maendeleo na siyo kinyume chake.

Mantiki ya hili ikiwa ni kwanini tuwalipe wanasiasa na viongozi mishahara mikubwa wakati wao wanashindwa kuwatoa watu wetu toka kwenye umaskini. Kwanini nusu ya mishahara na marupurupu yao yasikatwa na kutumika kupunguza umaskini nchini ? Bila shaka kuna watakaosema pia na viongozi wa dini nao wapunguze maisha ya kifahari yanayowalazimisha kuchaji ada na gharama nyingine katika huduma wanazotoa ambazo haziendani na hali ya Watanzania walio wengi.

Sio siri kwamba kama nilivyokwishawahi kusema huko mwanzoni katika dunia ya leo ni kitu kianchowezekana kwa mwizi kujiunga na jeshi la polisi sio kwa jukumu na wajibu wa kulinda raia na mali zao bali kwa ajili ya kuiba na kuwa tajiri bila ya kutuhumiwa na mtu kwa kuwa ni polisi.

Ndivyo ilivyo pia kwa vyombo vya kidini. Ni rahisi hivi leo mtu kuwa padri au shehe sio kwa sababu kwamba ni mcha-Mungu na anataka kumtumikia Mungu kikwelikweli bali kwa ajili ya kustarehe au kuwaibia wafuasi wao wasio na mashaka nao na kujinufaisha wao binafsi na wale wanaokula nao.

Dini na madhehebu za dini ni lazima ziwe na uwezo wa kimtaji, kijasiriamali, kijamii, kiuongozi au kiutawala, kifedha na kimiradi kujiendesha vyenyewe. Maana hatari kubwa katika demokrasia na uwajibikaji uongozi huletwa pale serikali na vyama vya siasa navyo vinapotoa sadaka kwa viongozi wa dini kwa minajili ya kuwanunua viongozi hao. Tukumbuke ufakiri ni nusu ya ukafiri, na dini maskini ina hatari ya kuwa na viongozi na wafuasi wengi makafiri.

Isitoshe Wakiristo wana nchi na mashirika kabakaba ya kigeni yanayowasaidia na yanayoendelea kuwasaidia. wakati Waislamu wana ndugu zao wa Kiislamu ambao nao wapo tayari kuwasaidia na kinachotakiwa ni uongozi bora, adilifu na wenye nia ya kweli kuendeleza dini na wafuasi wao na sio wabadhirifu, wababaishaji, ombaomba na kina saidia.

Upo umuhimu wa kujiuliza hivi kutokana na madai ya maisha na matumizi ya kifahari kwa baadhi ya viongozi wa dini sio muhimu kuwa na mabaraza ya Wazee Waadilifu wa kidini kusimamia mifuko mbalimbali ya kidini. Aghalabu wengi wao wakiwa ni viongozi safi wa kidini waliostaafu. Maana kadri dini zetu zinavyoongozwa na vijana vishawishi mbalimbali vinaweza kuwateka vijana hao na wakatumia mali za kanisa na misikiti kwa faida yao badala ya manufaa kwa wafuasi wenye matatizo ya kweli yanayohitaji misaada hiyo.

Ni muhimu pia kwa serikali kutoruhusu uuzaji holela wa mali za dini au wakfu na ni lazima izisaidie dini kuhakikisha kuwa mali hizo zinalindwa na zinakuwa na manufaa kwa wanaimani kizazi baada ya kizazi.

Dini lazima ziwe na viongozi waliosomea sio tu dini bali elimu mbalimbali ikiwemo uongozi au menejimenti ya taasisi na uwezo wa kuwatumia na kuwasimamia wataalamu mbalimbali wenye imani tofauti kuendesha mambo yao kwa faida badala ya wasiojua kuyaendesha mambo hayo kihasara. Dini yenye viongozi dhaifu, mbumbumbu wa menejimenti na oganaizesheni, wababaishaji na wasioachangia maendeleo ya kweli ya taasisi zao kwa kawaida ndio chimbuko ya dini au madhehebu zenye migogoro na vita visivyokwisha.

Dua za wale wanaoigeuza serikali na wanasiasa kuwa Mungu wao, Mola huzipuuza. Mola ambaye pia huitwa mlipiza kisasi hugeuza ubaya, mbaya anaomtakia asiyekuwa mbaya yakamfika huyo muomba dua. Kumbuka kisa cha Firauni na Musa na watoto wao wa kwanza.

Waumini wana kazi kubwa ya kudai uongozi bora na safi katika dini zao kama njia mojawapo ya kujenga demokrasia ya kweli nchini. Dini inapokuwa na viongozi bora na safi haiwezi kuyumba ovyo. Hata viongozi wa serikali huisikiza, wanasiasa huwatafuta na wafadhili wa ndani na nje huona wepesi wa kuzisadia dini kama hizo katika mambo mbalimbali. Dini inapokuwa na viongozi wasiokwenda shule, wababaishaji, wapenda anasa, wanafiki, waongo na wanaotumiwa na wanasiasa kiurahisi hukosa heshima na kuaminika na haiwezi kufanya lolote la maana kwa wafuasi wake. Na aghalabu huwa ni dini ya mwisho kimaendeleo katika jamii husika. Asalam aleykum warahamatullahi taallah wabarakat.

Tuesday, April 19, 2011

Wazee chemchemiya maji matamu, lakini hakuna wa kunywa

WAKATI mwingine wale tuliosoma au kwenda shule, huwa tunafanya kosa moja kubwa. Kosa hilo sio jingine ila ni lile la kudhania kwamba tunajua kila kitu. Kwa kuamini hivyo, huwa tunafanya makosa na kudhulumu nafsi zetu na za wenzetu wakati mwingine bila kujua.

Hapo zamani za kale akina sungura vijana waliitisha mkutano mkubwa wa wanasungura wote kuzungumzia mustakabali au hatima ya jamii yao. Ilionekana dhahiri katika kikao hicho kuwa vijana walikuwa wanakerwa sana na wazee kushika nyadhifa mbalimbali za juu na wao kupewa zile za chini tu. Ni dhahiri walikuwa wakitamani kushika nyadhifa hizo za juu wao wenyewe. Hilo ndilo walilolitaka.


Lakini hawakulizungumzia moja kwa moja, bali walitaja sababu tofauti zaidi. Wengine wakadai kwamba wazee wanakula zaidi kuliko vijana, wengine wazee hawaoni wala hawasikii hoja zote vizuri; wengine wakadai wazee ni wazito kufanya maamuzi; wengine wakadai wazee wana huruma kupita kiasi, ili mradi kila mmoja alitoa sababu iliyochangia, kuonyesha kuwa wazee kwa kweli walikuwa hawawafai tena.

Mwishowe, ikaamuliwa kwamba wazee wote wauawe ili udhia uishe. Na sungura wote isipokuwa mmoja tu aliyekuwa na mapenzi ya kipekee kwa baba na mama yake hakutii amri hiyo. Kwa maneno mengine unaweza kusema aliwasaliti wenzake. Lakini akilini mwake alichowaza ni kuwa wazee wameona, kusikia, kutembea, kupitia na kukutana na mambo mengi. Pengine siku moja wakibakia wao vijana tu patazuka jambo ambalo hakuna hata mmoja wao atakuwa na wazo ni namna gani walitatue. Kwa hiyo hakuwaua wazee wake, bali alikwenda kuwaficha mahala salama. Akawa anawahudumia wakati wote wakiwa mafichoni bila kuchoka.

Kufanya hadithi yetu kuwa fupi palizuka tatizo ambalo lilikuwa halijawahi kutokea toka sungura vijana wale wazaliwe. Yule aliyewaficha wazazi wake aliwaendea na tatizo hilo nao kama vijana wa siku hizi wasemavyo wakamwambia mbona 'ishuu yenyewe simpoo tu! '

Tatizo hilo lilimalizwa na ajuza na sahibu wa sungura kijana mjanja kuliko wote, ikadhihirisha wenzake wote walikuwa wajinga. Kijana sungura hakuonekana msaliti tena, bali mkombozi sasa.

Katika jamii yetu ya Kitanzania tuna wazee wachache ambao katika ujana wao wamepitia kazi au shughuli mbalimbali za kiuchumi, kijamii, kiteknolojia, kisayansi, kiutamaduni, kiafya na tiba, kibiashara, kibenki, kielimu na kadhalika.

Sikutaja wanasiasa kwa makusudi. Wao aghalabu wanakumbukwa tena sana. Na hivyo hawachangii kilio cha mada yangu. Ninapenda kuwazungumzia wale ambao pamoja na elimu, ujuzi na uzoefu walionao hakuna mwenye habari nao iwe mambo yanakwenda vizuri au vibaya. Ingawa wenye dhamana leo wanaamini kwamba hawawahitaji, wazee hao wangezungumza saa chache tu kwa juma na viongozi hao kuna mambo mengi ambayo yangelikwenda vizuri zaidi kuliko yanavyokwenda sasa. Na pengine wazee wangeliwafungua macho pia juu ya kutatua matatizo fulani na kutumia fursa zilizopo kuneemesha idara, wizara au shirika au kampuni kwa hatua ndogo chache tu.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, japo serikali inawatumia wazee vizuri sana katika siasa, lakini serikali hiyo hiyo imeshindwa kuwatumia wazee wataalamu kwa namna yoyote ya kujenga serikali bora zaidi. Lakini kama kuna taasisi ambayo ingelinufaika sana na hekima na busara za wazee taasisi hiyo isingelikuwa nyingine ila serikali, wizara, mikoa na wilaya.

Binafsi ninaamini ipo haja ya kuwatumia wazee hawa wenye utaalamu katika masuala ya elimu, kilimo, uhandisi, usalama, afya, usafiri na uchukuzi, ujenzi wa nyumba na barabara na kadhalika kama washauri maalum kupitia mabaraza ya wazee ya kisekta.

Katika masuala ya usafiri ( ATC, TRL, TAZARA, UDA) , mawasiliano (TTCL), Nishati na Umeme (TANESCO, SONGAS, SOLAR), benki na taasisi za fedha, shule, vyuo, hospitali, mashirika ya kibiashara, viwanda na mengine kama hayo kujifunza kutoka kwa wazee wetu waliokwishafanya kazi au shughuli kama hizi tunazofanya leo huko nyuma.

Nina hakika kuwa wale wazee waliokuwa wakifanya kazi kwenye mashirika ya ATC, TAZARA, TRC, UDA na KAMATA wakitafutwa na mameneja vijana wa leo, wakakaa pamoja na kushauriana hapataharibika kitu. Na kuna uwezekano mkubwa sana wa wazee hao kuwa dawa ya baadhi ya matatizo yanayokabili mashirika hayo sasa.

Ninaamini ndivyo itakavyokuwa kwa TANESCO, TIPER, na kwa wale wote wanaovinjari leo njia na mbinu mbadala za kuipatia Tanzania nishati ya umeme, mafuta na masuala ya nishati mbadala yanaweza kufanikiwa sio haba kwa kutumia uzoefu, busara na hekima za wazee. Bila shaka itasaidia mashirika hayo kutotugeuza abiria na wenye magari mabuzi yao ya kuchuna.

Hakuna sababu ya kampuni kama TTCL hivi leo kuendeshwa kihasarahasara; lakini kama tunadharau ushauri wa wazee wastaafu waliowahi kufanya kazi katika shirika hilo ni vpi tutalinusuru? Wazee hawa wanaweza wasiwe na la kuchangia katika masuala kama yale ya TEKNOHAMA na simu za mkononi, lakini ninaamini wakishirikishwa katika vikao muhimu baada ya muda watakuwa wanajua wanachokizungumza maana wana elimu na ufundi katika hayo, tena wa miaka mingi tu!

Kwenye kila Wizara, mkoa, wilaya na idara kuna mzee mmoja au wawili ambao wako hai nao wanaona mengi tu yanayokwenda mrama au ovyo ovyo! Hebu basi tujaribu kuwatafuta walikojificha na kupata mawili kutoka kwao ili tuboreshe utendaji kazi wetu na kuifanya dhana ya serikali inayowajibika kwa wananchi wake kuwa ni vitendo na sio maneno.

Upo ugonjwa mkubwa katika ofisi za serikali unaoletwa na ile tabia ya watu kuamini kuwa kiwango chao cha utendaji kazi walichofikia ndio cha juu kabisa na kwamba hawawezi kufanya zaidi ya hapo. Kumbe kwa kubadili muundo tu wa idara au taasisi iwayo na kisha kuleta maadili, mifumo, taratibu na kanuni mpya za kazi watumishi wa umma wanaweza wakafanya maajabu ya kuifanya serikali iheshimiwe na kupendwa zaidi na wananchi wake. Nani wa kusaidia hapa kama wazee waliopitia wizara husika?

Tatizo la mashirika ya umma ni kwamba, unaweza ukaliendesha kihasara, lakini kwa kuwa kuna gharama nyingi zisizolipiwa na pengine kuna ruzuku kila mwaka utadhani shirika lina ufanisi na ufanifu, kumbe sivyo!

Binadamu wachache wanataka kuijua historia yao kwa kina, lakini bila historia hiyo ni vigumu sisi wa leo kuelewa tunakotoka na tunakokwenda. Na hakuna mwalimu mzuri wa historia kama mzee aliyepitia na kuyaonja hayo yaliyomo katika historia.

Wazee wameptia mitihani mingi ambayo kwa kuwashirikisha katika mipango na maamuzi yetu wanaweza kutuokoa na kuingia hasara na gharama zisizo za lazima.

Hivi leo tunazungumzia kuboresha sekta za elimu na afya na masilahi ya walimu, madaktari na manesi. Lakini ni nani aliyekwenda kukutana na walimu, madaktari na manesi wazee wenye umri zaidi ya miaka 70 kupata ushauri wao. Na ni kitu gani wao walichokifanya huko nyuma tukaendesha taasisi za elimu na afya kwa ufanisi na ufanifu zaidi? Ni watu gani muhimu zaidi katika sekta ya elimu na afya? Walimu, Madaktari, manesi, wakuu wa taasisi au wakaguzi au wote ni muhimu na kila mmoja ana nafasi yake? Haya ni maswali yanayoweza kujibiwa vema zaidi na vikongwe hawa katika sekta ya elimu na afya.

Wazee katika nafasi mbalimbali walishawahi kujifunza kutokana na makosa yao wenyewe ya wakubwa wao na ya wadogo wao. Kukaa nao kwa siku mbili tatu kunaweza kuisaidia sekta fulani kuepuka kurejea makosa yale yale katika miaka hii ya 2000.

Wazee wengi hawakusoma falsafa, sosholojia wala saikolojia. Lakini maisha na uzoefu wao umewapa elimu ambayo ni vigumu mtu kuipata katika vyuo vikuu vingi duniani. Bado tu hatujaona 'nishi' hii ya wazee kuwa washauri na wataalamu wakubwa katika kusaidia kutatua matatizo yetu?

Masuala mengi ya jamii, uchumi, uzalishaji mali, utoaji huduma, biashara, ajira au kazi na kujiajiri, fedha, ushuru, mitaji, kodi, utamaduni, michezo, sanaa, uandishi, utangazaji na mambo kama hayo yanaweza kunufaika sio haba na kutafuta busara na hekima za wazee katika mpangilio unaoinufaisha taasisi husika na wazee wanaochangia kunufaika kwa taasisi hiyo.

Nimalizie kwa kukumbusha kuwa, ni wazee tu waliokwishapitia na kuona machungu ya kustaafu na kupata masilahi duni ya kustaafu. Nani wa kutushauri huko NSSF, NPF, LAPF, NHIF kama wao. Siamini wanataka sisi wazee wa kesho tupitie misukosuko kama yao. Kuna msemo wa Kiswahili unaosema: “Akili ni nywele, kila mtu ana zake.” Na wewe unaweza kuutafsiri utakavyo. Lakini kubwa kwa upande wangu ni kwamba, hakuna nyumba, mtaa, kata, tarafa, wilaya, mkoa au taifa lenye watu wanaojua kila kitu na wenye majibu ya kila swali na ufumbuzi wa kila tatizo. Ni kutokana na ukweli huu ndio inakuwa ni busara tupu na hekima kuwashirikisha watu wengi kadri iwezekanavyo katika kupanga na kuamua masuala yanayogusa sehemu kubwa ya jamii husika. Vinginevyo ni kuchimbana, vioja, vituko, kashfa na lawama zisizokwisha!

Tutazame Upya Uwekezaji katika madini

Hapo zamani za miaka ya 60 benki ya dunia ilivutiwa sana na azma ya Mwalimu Julius Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania katika kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi.

Kutokana na ushawishi wa Mwalimu wakuu wa benki hiyo waliisaidia sana Tanzania kwa mikopo ya riba nafuu na wakati mwingine hata mikopo isiyo na riba na sadaka za kusaidia hili au lile.

Pengine Watanzania wakati hu0 hawakuwa tayari kiuchumi na kwa hiyo sehemu kubwa ya mikopo na misaada hiyo haikutumika vizuri. Miaka karibu 50 baadaye Watanzania bado wanakabiliana na maadui wale wale wa miaka ya 1960. Tatizo ni nini ?

Sina jibu la moja kwa moja. Lakini yapo mengi yanayosemwa kama sababu ya sisi kuendelea kuwa watu wa dhiki na ombaomba. Kwanza, wengi wanadhani tumeshajenga tabia kama ombaomba mwingine yeyote kuwa hatuwezi kujikimu sisi wenyewe bila kusaidiwa.

Wengine wanaamini kuwa nchi haijapata aina ya viongozi wa kuitoa toka kwenye umasikini. Viongozi wanaopatikana hawaaangalii mbali wala mbele na wengi wao wanataka kula tu hata kama hawachangii chochote katika pato la taifa.

Wengine wanasema kuwa sisi ni Waafrika na kama Waafrika tupo katika hesabu ya waliolaniiwa kuwachotea maji na kuwakatia na kuwabebea kuni Wazungu, Waarabu, Wahindi na sasa Wachina na Wajapani.

Wengine wanasema ni kwa sababu kama ilivyo katika mitaa yetu aghalabu wenye uwezo, ari na sababu ya kuongoza hawako katika uongozi na wasiokuwa na uwezo wala sababu ya kuongoza ndio viongozi. Na kama sivyo basi viongozi ni wanasesere wa matajiri na wakubwa wa nje.

Baadhi ya watu wanadai kuwa wanasiasa na vyombo vya habari wameingilia fani za watu wengine na kujifanya wao ndio mabingwa na wataalamu zaidi kuliko wenye fani. Mwanasiasa anajua udaktari kuliko daktari, na mwandishi wa habari anajua sheria kuliko mwanasheria.

Wengine wanasema kwa kuwa elimu yetu inatolewa kwa kizungu hao wanaoweza kusoma kwa kizungu sio hao wanaoweza kuiletea nchi maendeleo ya kweli.
Na wanachagiza tutoe mfano ya nchi angalau moja ambayo inatumia lugha ya kuazima iliyoendelea hapa duniani. Wao wanasema hakuna labda pale wazungu wenye Kiingereza wanapotawala kila nyanja ya uchumi.


Ili mradi kila mtu ana sababu yake. Mimi sikatai wala sikubali yote haya. Kwa upande wangu nizungumzie leo juu ya sera mbovu za kiuchumi zinazoruhusu watu kuchuma nchini mwetu na kuwa matajiri na sisi tukabakia masikini kama sio mafukara zaidi baada ya watu hao kuchuma na kuondoka kurudi makwao.

Afrika isipokuwa kwa nchi kama Botswana , Namibia na Afrika Kusini ni mfano mbaya wa uongozi usioweza kubadilisha maisha ya wananchi wake lakini ukaendelea kung'ang'ania kubakia madarakani. Ni mfano mbaya pia kwa kuwa hakuna mfumo wa kuchuja na kuwaondoa viongozi na watendaji wabovu wa serikali wasiochangia kwa kadri inavyokubalika maendeleo ya kiuchumi wa nchi na hivyo kuiacha serikali wakati wote ikiwa na watu bora na wachapa kazi zaidi.

Mfumo unaotaka kuendelea kuwepo madarakani uko tayari kuuza heshima, haki, maendeleo na uhuru wa watu ili mradi upate unachokitaka. Sio mfumo endelevu iwe katika maendeleo ya kisiasa, kijamii, kiutamaduni, kitekelojia wala kiuchumi. Maana ni mfumo unaobakia kwa kufanya ujanja ujanja na wala sio kuleta tofauti yoyote ya maana katika maisha ya watu.

Hata hivyo ni nchi chache katika Afrika zilizojaliwa karibu viungo vyote muhimu vya kuondokana na umasikini na kukosa maendeleo kama ilivyojaliwa Tanzania .
Mtego ni kuwa kwenye miti hapana wajenzi, na mbomoa nchi yetu sio mwananchi bali viongozi !!!

Tatizo letu la kukosa maendeleo ni kwamba hakuna kiongozi hata mmoja hivi leo anayeweza kusimama mbele ya watu na kusema yeye ni mfano wa kuigwa.
Hakuna anayeonesha mfano ili aigwe, watu wabadilike na nchi isonge mbele.

Viongozi wengi wanadai ili wao walete maendeleo kwa wananchi haraka ni muhimu kwao wao kugharamiwa kuliko maelfu kama sio mamilioni ya wananchi wote wakiwekwa kwa pamoja. Leo 2009 gharama zote Watanzania walizobeba kwa niaba ya viongozi wao hazijawaletea maendeleo. Swali linakuja, je, mfumo huu wa viongozi kula kuliko wananchi ukibadilishwa ili angalau wananchi nao wale sawa na viongozi kama sio kuwazidi nchi haitaendelea ?


Hali ilivyo sasa ni kwamba pato kubwa la taifa linaliwa na walio juu na walio chini wanapata kidogo kama hawakosi kabisa. Lakini ni nani miongoni mwao anayethubutu kusema sitaki gari la milioni 200 bali nitachukua la milioni 20 tu? Ni nani anayeweza kusema kwa kuwa sisi ni nchi masikini badala ya kukaa kwenye mahoteli ya kifahari tutajenga hosteli katika kila nchi tuliyo na ubalozi ili kupunguza gharama za kukaa kwenye mahoteli ya bei mbaya? Ni nani anayethubutu kusema mimi safari hii siendi nje acha watu wachache tu waende ili kupunguza gharama kwa walipa kodi? Haya yote hayayumkiniki kwa kuwa mfumo uliopo tayari umekwishatangaza kuwa maisha ya kiongozi mmoja ni bora kuliko maisha ya Watanzania laki moja.

Vilevile ni ukweli usiofiichika kuwa hakuna ambalo unaweza kumfundisha tembo mzee. Viongozi wetu wengi ni 'recycled materials' na uzuzi, ubunifu na utundu wa kujaribu mapya kwao ni sifuri. Mabadiliko hayaji kamwe katika mazingira ya namna hii.

Isitoshe tabia yetu sisi Watanzania ni kwamba tuko radhi 'mgeni' atajirike kuliko mwenzetu atajirike. Nisingelipenda kusema zaidi juu ya hili bali wasomaji wenyewe wanaweza kushuhudia hili kwa visa mbalimbali wanavyokutana navyo katika maisha yao ya kila siku.

Ninadhani wengi wenu mmeshawasikia watu wakilalama iweje Mhindi au Mwarabu au Mzungu au Mchina fulani kuja nchini hapa na Marlboro na baada ya miaka 2-3 anakuwa tajiri mkubwa?

Kuna maswali mengine kama vile hivi serikali inapozungumzia juu ya ubia kati yake na wananchi ubia huo unachukua umbo au muundo upi?

Tuchukue suala hili la kwamba tumewaruhusu wageni kuchimba dhahabu nchini mwetu (bila kuwashindanisha Wakanada na Wachina au waingereza na wakorea kama vile bado dunia hii inatawaliwa tu na nchi za magharibi na hivyo kukubali masharti na mkataba wa kijinga) na wao kutulipa mrahaba sawa na hakuna eti tu kwa sababu sisi hatuna mashine na utaalamu unaohitajika. Wakiimanisha kwamba thamani ya Watanzania wote pamoja, mali asili zao na serikali yao ikiwekwa pamoja haifikii ile ya utaalamu wao na mashine zao.

Laiti kama huo ubia unaozungumziwa ungelichukua sura ya ya serikali, mabenki na vyombo mbalimbali vya fedha kutmbua kwanza watu wetu wana thamani kuliko kitu kingine duniani na kisha kutoa ushauri na kuwapa mtaji-mbegu wawekezaji wazawa nchi hii leo isingelikuwa hapa ilipo.

Kama benki ya dunia iliweza kutoa mikopo na misaada ili kujenga uchumi wa Tanzania iweje leo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vyombo vyake ishindwe kuwadhamini wazawa wapate elimu na maarifa ya uchimbaji madini na kisha kununua kwa mikopo ya muda mrefu kupitia Benki ya dunia mitambo na vifaa mbalimbali vinavyohitajika katika uchimbaji madini? Au hili nalo ni ushahidi kwamba viongozi wetu ni wale wale ambao wako tayari mgeni atajirike kuliko mwenyeji aukate?

Hivi sasa sio kazi kupata masomo yote kuhusu 'geology' au uchimbaji madini na kisha kuyatafsiri yawe katika Kiswahili na kuyaweka katika mtandao ili kila anayetaka kujifunza juu ya uchimbaji madini asipate shida kutafuta masomo hayo.

Kuna tunaoamini kwamba kwa kufuata mkakati ule ule wa miaka ya 1960 tunaweza kabisa kuwawezesha Watanzania wenyewe kuwa sio tu wamiliki wa machimbo ya dhahabu bali pia wamiliki wa viwanda na huduma mbalimbali zinazochangia katika mkufu mzima wa uchimbaji na uuzaji madini ndani na nje ya nchi. Tatizo ni kuwa hakuna mwamko wala moyo wa kizalendo na kisiasa katika kufanya hili.

Endapo Tanzania itakuwa na sauti katika soko la madini na vito ni wazi tutakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kujinasua na umasikini na ombaomba.

Hili pia litatuwezesha kutumia madini kuwekeza katika sekta mbadala
kama vile elimu kwa wanafunzi toka nje,

tiba na afya kwa wagonjwa toka nje, teknolojia, ujenzi wa nyumba na makazi mapya,
kuanzisha makampuni ya umeme yatakayofanikisha kupatikana nishati hiyo kwa wote. Aidha kwa rasilimali hizo hizo itakuwa ni rahisi kupata Watanzania watakaowekeza katika nchi za nje. Hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo ya kweli bila kuwekeza katika nchi nyingine. Tujifunze toka China na venezuela ili nasi tukae mkao wa kula katika dunia ya utandawazi.

Vikwazo kwa demokrasia nchini

KATIKA makala hii nitajaribu kudhihirisha vikwazo vikuu vya kukua na kuimarika kwa demokrasia nchini.

Vikwazo nitakavyovizungumzia leo ni pamoja na kukosekana kwa katiba mpya; kuwepo kwa chama-dola kinachotamalaki kila nyanja ya maisha nchini; kuwa na Baraza la Mapinduzi linalopindua uhuru na haki za binadamu Zanzibar wakishirikiana na wale wasiotambua wajibu wao katika mfumo wa vyama vingi na umaskini wa vyama mbadala. Kwa wale wanaotaka kujifunza zaidi juu ya vikwazo basi waone makala zilizoko katika http://demokrasiaafrika.blogspot.com.

Kuachia watu wawe na demokrasia ya kina na pana kunataka moyo. Ni jambo ambalo halitofautiani sana na kukubali binti anayependwa na kuaminika nyumbani kuolewa. Wazazi huwa na taabu sana kutokana na mazoea kuamini kuwa watapata amani na huduma waliyoizoea kutoka kwa mtu mwingine.

Lakini wakati ukifika umefika. Hakuna njia ya kuzuia yanayopaswa kutokea. Maana wakati ni ukuta na ukiupiga kofi au ngumi utaumiza tu mkono wako mwenyewe.

Demokrasia kama mwali lazima apewe mwananchi. Hatuwezi kuendelea kumlazimisha kukaa ndani mwetu milele. Mliopo madarakani amueni Demokrasia Ruksa!

Ili hili lifanyike yapo mambo kadhaa yanayopaswa kufanyika kwanza. Mambo hayo ni pamoja na:

Kuandikwa Katiba Mpya. Katiba mpya sio jambo la kisiasa au kiserikali tu. Katiba mpya ni makubaliano mapya yaliyostahili kuwepo kati ya watawala na watawaliwa toka siku ile nchi hii ilipoamua kuwa nchi ya siasa za vyama vingi.

Tumechelewa. Na wakati ni huu. Afrika nzima inaitazama Tanzania kuona kama tumekua na kukomaa kisiasa au la. Tusikubali kutanguliwa na tutoto twa jana kisiasa katika hili.

Umuhimu wa katiba mpya ni kwamba utamaliza kabisa matatizo mbalimbali yaliyojitokeza toka mfumo wa vyama vingi uanze. Baadhi yake ni pamoja na haki na uhuru wa watu kuzungumza, kukutana, kuandamana na kuunda au kuua vyama; vyama kadhaa kujiunga na kuwa kimoja kwa hiari yao wenyewe; matumzi ya redio, magazeti na televisheni ya umma; haki ya kumiliki mali zilizozalishwa na wananchi wote kwa pamoja; nafasi za makundi ya vyama vyote ya vijana, wazee na wanawake tofauti na yale ya kichama na kadhalika.

Katiba hiyo inatakiwa kuandikwa na wawakilishi wote wa wananchi, ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi wetu wote kwa angalau miaka 50 ijayo. Hili sio jambo la kufanywa na wanasiasa au wanasheria wachache hasa ukizingatia tofauti za kijamii, kiuchumi na kisiasa zilizopo leo. Ni jambo linalohitaji ushirikishwi wa washika-dau wote wa Kitaifa.

Demokrasia nchini hapa haiwezi kabisa kukua na kuimarika kama tunaendelea kuwa na chama-dola, ambacho kwa heri au shari kinaathiri maamuzi na utekelezaji wa mambo mbalimbali.

Ikumbukwe wanasiasa ni watu. Na kila mmoja wao ana matarajio na matamanio yake. Ni rahisi kwa chama-dola kujikuta kinachanganya maslahi binafsi ya viongozi wake na maslahi ya umma. Mathalani, katika sakata la ufisadi linaloendelea hapa nchini kwa hivi sasa. Pengine viongozi wa kisiasa kweli wamenufaika kwa kiasi fulani, lakini wananchi walio wengi wamekula hasara.

Tatizo la chama-dola ni kuwa mawaziri wake aghalabu hujali tu maslahi ya chama na sio ya wananchi wote. Kwa hiyo maamuzi hufanyika sio kwa manufaa ya Watanzania wote, bali kwa sababu chama fulani kitanufaika na maamuzi hayo au vyama fulani vitaumizwa na maamuzi hayo.

Katika bunge la chama-dola tatizo ni hilo hilo. Bunge la namna hiyo hujali zaidi maslahi ya chama chao badala ya maslahi ya wananchi. Hili linapotokea uwakilishwaji wa wananchi na wabunge wao huwa umeorojeshwa kiasi cha kuwa hauna maana wala mchango wowote wa maana katika maisha ya wananchi waliowapeleka wabunge hao bungeni.

Ukiritimba wa chama-dola huathiri hata uongozi wa mikoa na wilaya. Katika mikoa na wilaya nyingi kinachoogopwa huko sio serikali yenyewe bali chama kinachotawala. Matokeo yake utakuta kuna unafiki zaidi kuliko kujitambua kwa viongozi hao na kubaini mchango unaotakikana toka kwao na jamii wanayoiongoza.

Hali hii inajitokeza pia katika tawala za mikoa na uongozi vijijini na mijini. Pale chama tawala kinapofika mpaka huku nacho kikawa ni chama-dola basi hakuna lolote la maana kidemokrasia litakalopikwa na kuiva huko.

Ili demokrasia ya kweli iwepo ni muhimu kutenga kabisa shughuli au kazi na wajibu wa serikali mbali na ule wa chama tawala. Hili linawezekana linataka tu kutambua kuwa chama tawala ni sawa na chama mbadala kinginecho chochote ambacho nacho pia siku moja kinaweza kuwa chama tawala. Usawa huu unawalinda wote kwa kuhakikisha kuwa hakuna anayepora nguvu na mamlaka zaidi ya yale ya kuwa chama mara anapopewa kuongoza serikali. Aghalabu hili husaulika sana na vile vyama vinavyodhani vitakaa madarakani milele.

Lile linaloitwa BARAZA LA MAPINDUZI visiwani Unguja na Pemba kwa sasa ndio tishio kubwa kuliko kitu kingine chochote kwa demokrasia na hususan huko visiwani.

Baraza hilo ambalo ni taasisi iliyopitwa na wakati linaendelea kuwepo bila kujua wajibu wake siasa za sasa za nchi. Limeendelea kuishi katika ukale na kuongoza kutokana na historia badala ya kuongoza kulingana na visheni na misheni mpya katika mfumo wa vyama vingi. Zanzibar ambayo ina nafasi kubwa ya kushindana na nchi kama zile za UAE ikiwemo Dubai, Sharijah, Bahrain na kadhalika leo inakwaza kutokana na siasa za dhuluma na uonevu zinazoendeshwa visiwani humo na hasa zile zinazonuia kumnyang'anya mtu haki zake za kikatiba.

Ni dhahiri kwamba, baraza hilo ni kikwazo kwa mabadiliko ya kweli na ya dhati yanayoweza kuwa chachu muhimu ya kuwaondoa Wazanzibari wote kutokana na udhalili na uhitaji wao karibu katika kila nyanja ya maisha. Na sio hilo tu vijana wengi wa Kizanzibari ambao leo wanakwepa nchi yao watakuwa na kila sababu ya kurudi au kwa namna moja au nyingine kuchangia vitu vya maana katika maendeleo ya nchi mama yao.

Kwa kurubuni, kutapeli na kudhulumu haki za baadhi ya wanajamii uongozi uliopo hauonyeshi ujanja bali upofu na uziwi juu ya kule dunia inakoelekea siku hizi.

Ikumbukwe kwamba, unaweza kubabaisha kundi fulani la watu leo na kesho, lakini huwezi kubabaisha makundi yote ya watu wakati wote na unafiki na uzandiki wako usijulikane. Na aghalabu hata yule unayemtuma kudhulumu anaweza akawa si wako ila kwa kukuogopa anatekeleza amri ya kafiri apate mradi wake. Na kwa siasa hizi ni rahisi kujikuta umezungukwa na wanafiki kuliko wacha Mungu na wapenda utu na haki za binadamu.

Matokeo ya hili ni kuwa na wakubwa wanaovunja sheria, lakini ukawalinda kutokana na upofu na uziwi ulio nao.

Hakuna binadamu mwenye akili zake timamu na uwezo wa kuleta mabadiliko yeye mwenyewe anayeweza kukubali dhuluma na mabavu siku zote. Iko siku atajibu. Na siku hiyo isije ikawa ya kusaga meno na usononi usio na mwisho.

Hakuna anayekubali siasa za kurudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kama ni motokari sasa watu watakuwekea mawe usishuke zaidi ya hapo ulipoteremka ukirudi nyuma.

Unafiki mara nyingi ni dalili za uongozi dhaifu usio na dira ya kule unakoweza kuwafikisha wanaoongozwa. Katika kutapatapa na kuhangaika, huishia kuvuruga na kuchafua na hivyo kuwatia wananchi umaskini na ukiwa zaidi.

Maendeleo ya nchi hayawezi kamwe kuletwa na ubinafsi, choyo, jeuri, kiburi, ujibari na dharau kama hiyo ndio tabia ya viongozi. Katika dunia hii hii imewahi kutokea utawala wa wezi katika nchi fulani pale wananchi walipodanganyika na walipojisahau na kushindwa kutimiza wajibu wao. Ni dhahiri pia katika miaka hii tunaweza kushuhudia uongozi wa wahuni, waongo, wababaishaji na hata watu wajinga pindi nasi tutakapojisahau na kudhani kwamba kila mtu anaweza kuwa kiongozi.

Kikwazo kingine kikubwa kwa demokrasia ni Ujinga wa watu juu ya Demokrasia Vijijini.
Uchumi na siasa zetu zimekaa kwa namna ambayo wananchi vijijini bado kabisa kujua faida na manufaa ya mfumo wa vyama vingi. Walioko madarakani wametumia fursa hii kuonesha tu kasoro na hasara za mfumo wa vyama vingi. Na kutokana na kiwango chao cha elimu na kukosa huduma muhimu za mawasiliano kama vile magazeti wanayomudu kununua, redio na televisheni basi wanakuwa na uwezo duni wa kuchambua na kutathmini wanayoambiwa na viongozi wapita njia au wale wa kwao vijijini.

Katika hili ni dhahiri ipo haja ya kuweka mkakati wa Elimu na njia za kufikisha elimu kwa wananchi vijijini wakati wote, ili wawe wanaendelea kufunguka macho na masikio juu ya manufaa ya demokrasia katika maisha yao ya kila siku.

Barua-pepe: sammy.makilla@columnist.com

Tuesday, April 5, 2011

UNESCO kuokoa makabila, mila na utamaduni

INASEMEKANA kwamba uchumi au bora zaidi mapato yanayopotea kwa Watanzania kutokana na kufinywa au kubanwa utamaduni, mila, historia na lugha za kikabila ni sawa na mapato yanayopatikana hivi sasa nchi nzima.

Katika dunia hii ya utandawazi ajabu ni kuwa japo dunia inakuwa kijiji lakini majukumu ya usimamizi na uongozi katika nchi yanazidi kushuka chini hadi kwenye jamii, vijiji na watu wenye asili moja.

Kutokana na sababu za kisiasa huko nyuma viongozi wetu walilazimika kuua uongozi wa kimila, kupuuza lugha za makabila na kupiga vita tamaduni za watu mbalimbali kuhifadhiwa na kuendelezwa.

Sababu kubwa iliyotolewa wakati huo ilikuwa ni kulinda amani na umoja wa Watanzania na kwamba kama tungeliachiwa kushabikia makabila yetu kupita kiasi basi tungeweza kusababisha ukabila nchini.

Hata hivyo, ujio wa siasa za mfumo wa vyama vingi umezua makabila mapya. Makabila hayo ya 'kichama' yanaelekea kuwa hatari zaidi kwa umoja na amani yetu kuliko makabila ya kimapokea.

Katika nchi hii ilifikia mpaka mahala ikakubalika bila kuandikwa mahala kwamba watu kutoka makabila makubwa au yenye neema zaidi hayastahili kabisa kutoa viongozi. Na hadi wa leo katika baadhi ya vyama vyetu vya kisiasa ni mwiko mtu kutoka kabila kubwa kuchaguliwa kama kiongozi au kuteuliwa kuwa mgombea nafasi zaidi ya ubunge.

Katika kufanya hivyo, hakuna aliyeangalia hasara au faida za kutawaliwa na wale wanaotoka makabila makubwa kiutafiti na kiutaalamu na hakuna mahala popote tunapoelezwa faida na hasara za kutawaliwa na watu kutoka makabila madogo na uwezo wao kiuongozi.

Lakini ni dhahiri zipo sababu na zinajulikana ingawa zinafichika na miaka 50 baada ya uhuru tunaweza kutathmini kwa uhakika faida au hasara za kuongozwa na watu kama waliowahi kutuongoza.

Tanzania ina zaidi ya makabila 130 na makabila yote haya ni shule kama sio vyuo. Maarifa, busara, hekima na urithi mbalimbali umo humo na kama yanayostahili yakifanyika basi itakuwa ni rahisi na hasa mikoa itakapokuwa ikijiendesha kama maeneo huru kiuchumi kupata maendeleo kwa kasi na haraka zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.

Ili kufikia huko kwanza tuangalie jinsi makabila yetu ya asili yanavyoweza kuhifadhi lugha zao kwa kuwa na kamusi za lugha hizo na kisha vitabu vya kufundishia lugha hizo. Kwa mantiki hii kila kijana toka kabila lolote Tanzania ataweza kujifunza lugha ya kabila lolote analolitaka. Kwa mfano, Mkwere akitaka kuolewa na Mhaya anaweza kujifunza Kihaya na mwenzie akajifunza KIkwere na hivyo kuendelea kudumisha mila pia na umoja wetu.

Sambamba na hilo hapo juu ni muhimu kuwa na majumba ya makumbusho mawili matatu kwa kila kabila kutegemeana na ukubwa na upana wa utamaduni na mila zao. Kwa hiyo badala ya kuwa na jengo moja la makumbusho jijini Dar es salaam, tutakuwa na majumba ya makumbusho zaidi ya 390 ya makabila yetu.

Katika hizo makumbusho tatu za kikabila ile ya kwanza itajihusisha zaidi na hifadhi na zana zilizotumika kurithishaa maarifa, mafunzo, kazi na huduma mbalimbali za kijamii; ya pili itahusu masuala ya uzazi, ndoa na kifo na ya tatu itahusu masuala ya uongozi, uchumi, biashara na mahusiano na makabila au watu wengine.

Majumba haya ya makumbusho 390 yakijengwa vizuri na panapostahili na kutoa huduma ya kuwaridhisha wananchi na watalii watakaokwenda kuyatembelea peke yake yana uwezo wa kuingiza mabilioni ya shilingi kila mwaka.

Watanzania binafsi nao watakaotaka kuanzisha majumba yao binafsi ya makumbusho katika eneo moja la asili, historia na utamaduni wetu nao waungwe mkono na wasaidiwe kufanikisha azma yao hiyo.

Kazi hii inaweza kuanza kwa kuwa na majumba hayo ya makumbusho kama wavuti kwenye tovuti kwa kuanzia na baadaye rasilimali zikishapatikana majengo hayo yatajengwa.

Nimekuwa nikijiuliza kutokana na ujio wa watoto na vijana toka vijijini wanaofikia kwangu kwa ajili ya kazi au kujiendeleza kimasomo na uelewa wao wa Kiswahili kama kweli tuanwatendea haki watoto wanaoishi vijijini ambako ni lugha asili inayotumika zaidi kuliko Kiswahili.

Ninaamini wakati umefika wa kupanua na kuwa na kina kirefu zaidi cha maarifa yetu kwa kuwa na MAGAZETI NA REDIO ZA KIJAMII katika kila eneo - kabila. Magazeti na Redio zitakazowafunza wanaoelewa lugha hizo mambo kwa haraka na wepesi zaidi kuliko ilivyo sasa. Sio tu watoto na hata watu wazima watapata fursa ya kujifunza majina ya vitu, miti, ndege, wanyama, samaki na kadhalika kirahisi kwa lugha zao kwa kutumia redio na magazeti hayo.
Taifa lolote lina madaraja matatu ya mizizi. Daraja la kwanza ni mizizi ya lugha za kikabila, daraja la pili ni mizizi ya lugha kadhaa zinazokurubiana au kufanana na kusikilizana na daraja la tatu ni mizizi ya lugha kuu kitaifa. Mizizi hii ikiwa imara na watu wana maarifa ya kutosha toka makabila yao inakuwa ni rahisi kupanda madaraja mengine hadi kufikia upeo wa kupata wahandisi na wanasayansi wanaoweza kuelezea lolote lile kwa lugha yao kikabila.

Vyombo hivyo vya habari kwa lugha-zetu-za-kwanza vitasaidia pia kufundisha, kukuza, kuendeleza na kusasaisha lugha, ngoma, muziki, maigizo, michezo, vinywaji, vyakula, utengenezaji filamu, nyumba na makazi asili, hadithi, simulizi mbalimbali kama vivutio vitakavyouzika kwa watu wa ndani na wa nje ikiwemo watalii pia.

Ifahamike tofauti na Mheshimiwa Kabwe anavyosema kuwa lugha ya Kiswahili imezimeza lugha za kikabila, mimi ninaamini lugha ya Kiswahili imezuia kuzisaidia lugha za kikabila kwa njia kuu mbili. Kwanza, kwa kuzuiwa kutumika kama lugha ya kufundishia toka chekechea hadi chuo kikuu lugha hiyo imeshindwa kuzisaidia lugha za kikabila. Pili, kwa kuwa Kiswahili kimekosa fedha za kufanyia tafiti lugha za kikabila ili kujifunza kutoka huko imeshindwa pia kuzisaidia lugha hizo kujiweka kwenye nafasi bora zaidi kuliko iliyo nayo sasa. Fursa hizi zingelikuwepo, Kiswahili kingelikuwa na kupanuka Afrika nzima na makabila yetu kama walivyo Waskotishi na Wawelshi huko Uingereza tukajivunia lugha zetu zote mbili. Yaani, tukajivunia Kiswahili kwa sisi kuikitumia nacho kutumika dunia nzima na wakati huo huo lugha zetu za kikabila kutumika kwenye maeneo yanayostahili tukidhihirisha ulimwengu uzuri na ubora wa kuwa na vingi vinavyofumwa kuwa kitu kimoja. Hii ndiyo visheni niliyo nayo na ninaamini ni ya wengi pia, nako ndiko tunakostahili kwenda.

Lakini utamaduni, mila na historia za kila kabila zinahitaji usimamizi na uongozi. Itakuja kuonekana huko tunakokwenda kwamba uko umuhimu wa kurejesha tena nafasi ya uchifu au uongozi wa makabila kwa njia moja au nyingine. Ninasema kuurejesha lakini nikiamini pamoja na kusemekana uchifu ulifutwa kuna makabila ambayo bado kiukoo, kimila na kijamii yameendelea kuwatukuza na kuwaheshimu watu fulani miongoni mwao kama machifu wao. Mmojawao ninaamini alikuwa rafiki yangu, hayati Adam Lusekelo kwa upande wa Wanyakyusa wa Mwakaleli.

Usimamizi au ungozi huu wa machifu, kikabila utasaidia sana kurejesha maadili, adabu na nidhamu kwa wananchi na hasa watoto na vijana wetu; kupunguza ubinafsi na umimi kwa kiasi kikubwa kwani sasa jamii au kabila litapewa umuhimu juu ya mtu binafsi; na vile vile kujenga umoja kati ya watu wa hali, asili na imani mbalimbali.

Muhimu katika suala la kuenzi utamaduni wetu ni pamoja pia na kutunza na kuhifadhi vile vitu au dhana zisizoshikika kwa mikono. Vitu ambavyo tunavizungumza na kuvifanya kila siku lakini sio vitu vinavyoshikika lakini navyo vina thamani na vinaweza kuwa na maana kwa vizazi vijavyo na kuwa vivutio vya utalii leo na kesho pia. Yaani, jinsi tunavyozungumza, tuanvyotembea, tunavyojumuika na wenzetu, mazishi na kilio, uzazi au ndoa na nderemo na imani au hisia zetu mbalimbali na jinsi tunavyoonekana kwa wengine. Kwa mfano, huko nje, iwe Ulaya au Marekanim hadi juzi Watanzania walikuwa wanaaminika na kuonekana ni watu wapole, waungwana na wataratibu sana katika mambo yao. Hili nalo kama ni jambo zuri tunastahili pia kulienzi.

Saturday, April 2, 2011

CCM na hatima ya Tanzania

HIVI majuzi Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Peter Pinda, alizungumzia umuhimu wa wana-CCM wenzake kutambua umuhimu na faida za kuzungumzia mambo yanayowahusu pale panapostahili na sio ovyo ovyo vichochoroni.

Nyuma kidogo ya hapo, gazeti hili lilichapisha makala iliyokuwa na kichwa: ' Dalili za chama chenye hatari ya kusambaratika,' na baadhi ya yaliyokaririwa huko bila kificho yalidhamiriwa kuihatarisha CCM kwamba kule inakokwenda sio kuzuri. Tumefarijika na Waziri Mkuu kuliona hilo na kulimaizi waziwazi na kwamba kwa sasa faida na manufaa ya Watanzania kuwa na vyama vinavyojiendesha kiakili, kistadi na kimkakati sio kitu kisichofahamika tena. Na yeyote anayebisha hili ni mtu aliyezoea tu kubisha na asiyekubali ukweli unapojidhihirisha.


Kweli idadi ya Watanzania imeongezeka. Lakini na matatizo yao vilevileyanaongezeka. Ajira ni chache (tofauti na redio ya CCM inavyodai); uzalishaji mali Tanzania sekta zote bado duni mno; umeme tatizo sugu; maji usiseme pamoja na ahadi kabakaba; taasisi babaishaji kawaida; rushwa palepale; mfumuko wa bei mtindo mmoja; kilimo kwanza bila zana zetu wenyewe usanii; viwanda vyetu vimelemazwa na tatizo la nishati na ubunifu; na maradhi kama sio 'babu' hata viongozi wenyewe wangelikuwa hatarini; na matatizo ya kawaida ya wananchi yanaachiwa kuwa matatizo mwaka nenda, mwaka rudi. Uhalisia huu wa mambo unashadidia umuhimu wa CCM kujizaa upya na kuwa na mkakati maridhawa wa kupambana nayo.

Sifa za kiongozi bora ni jambo lililoanishwa vyema na Guru wa Menejimenti, hayati Peter Drucker katika kitabu chake cha The Effective Executive.

Kiongozi bora kama alivyoainisha Prof. Drucker ni mtu mwenye sita zifuatazo: anajua atatoa mchango gani kwa taasisi au chama chake; anaujua na kuupanga muda ili utumike kuiendeleza taasisi yake na sio vinginevyo; anavifahamu vipaumbele vyake na hufanya kazi kwa kuvizingatia; anatambua uwezo na udhaifu wa walio chini yake na jinsi ya kuwahamasisha ili uwezo na mazuri yao yashinde udhaifu wao na juu ya yote ni mtekelezaji mambo na sio mropokaji au mwimbaji upuuzi kila wakati.

Ni vyema katika kutathmini nafasi yao kisiasa hivi leo nchini CCM ijipime na kuona kama kweli ina viongozi wa aina hiyo hapo juu na wanaolingana na majukumu yaliyoainishwa hapo juu na Profesa Drucker.

Nina wasiwasi pia hivi leo kwa Mkutano Mkuu kuwa ndio chombo cha juu kabisa cha chama sio jambo zuri. Na vilevile utaratibu wa kofia mbili nao ninaona katika miaka hii una kasoro kubwa na walakini. Maana, matokeo yake ndiyo hayo kwamba viongozi wa zamani kwa kukosa nafasi yoyote ya uongozi katika chama wanaishia kuwa wakosoaji, wambeya na wazushi wa hili au lile. Ninauliza pia kwa hiyo, je, haiwezekani kuwa na Baraza la Wazee wa CCM kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ambalo litaendeshwa kama chombo huru ndani ya chama lakini kikiwa ni chombo cha ushauri na ukosoaji ndani ya chama tu na sio la kiutendaji? Hili halitasaidia, kuwapa nafasi viongozi wa zamani ambao hawana kazi, na sasa wanaongezeka kila siku ifutikayo kwenye kalenda?

Kitaifa hili ni pacha na suala la kuwa na Bunge la Juu pia kwa minajili ya kuwaleta pamoja viongozi wa zamani na wanataaluma na makundi mbalimbali ya kijamii ili bunge hilo liweze kusaidiana na bunge la wawakilishi wa wananchi. Bunge ambalo litasaidia pia kupunguza idadi kama sio kuwaondoa kabisa wabunge wa kuteuliwa kwnye bunge la sasa.


Ninaamini katika kuangalia uwezekano wa hayo hapo juu, CCM itawapa wastaafu wake na wanaharakati wengine fursa ya kuwa na maeneo yao ya kumwaga sera na kuunga au kupinga kauli au uamuzi wowote unaofanywa na viongozi waliopo madarakani kwa njia muafaka na ya kistaarabu zaidi. Katika miaka hii ni kosa kwa kikundi chochote katika jamii kujifanya kuwa kina akili, busara na hekima kuliko wananchi wote wakiwekwa pamoja.

Mfano unaooneshwa na CCM hadharani hivi leo unawatia wananchi mashaka, tena mashaka makubwa sana. Wengi wanajiuliza kama chama tawalal kinashindwa kusimamia vyema mambo yake ya ndani, je, kitayamudu vipi yale ya kitaifa, tena kwenye nyakati ambazo mihogo michungu imeota kila kona ya shamba?

Jambo lingine ambalo chama tawala kinafaa kujiuliza ni kwamba bila kuwa na mpango-mkakati uliotungwa kwa kuwashirikisha viongozi wote toka ngazi ya shinda hadi taifa, je, kitaweza kuhimivili vishindo vya huko tunakokwenda.

Tukiacha maneno ya kiswahili ambayo huwa ynnatuchanganya saa zingine tujiulize je, leo CCM ikiulizwa nini VISHENI (VISION) yake itakuwa na la kujibu kitaalamu na sio kiuswahili ? Na, je, MISHENI (mission) ya CCM katika Tanzania ni nini? Kweli, CCM imerithi yaliyoachwa na waasisi wake, lakini, je ni yote yanayofaa katika miaka hii au kuna yaliyopitwa na wakati na hawastahili kusita kuyatupa kwenye kapu la takataka za historia?

Kwa maneno mengine uwepo wa mpango-mkakati utaisadia sana CCM kujiuliza na kujibu maswali kama vile: chama propa na jumuiya zake zinataka kuwa kitu gani baada ya miaka 3-4 toka sasa; pengo lililopo kati ya matarajio na pale ilipo hivi sasa likoje; nini ulikuwa udhaifu dhidi ya uwezo au nguvu zake jana, leo na itakavyokuwa kesho; ni fursa na hatari zipi zilizo mbele yake; na ni mbinu au mikakati gani ifanyike ili kuwe na fikra,mwono, mtazamo, msimamo na vitendo chanya vya kuvipa ushindi chama dhidi ya majaribio mbele yake na kikafaulu kuwapeleka Watanzania kule wanakotaka kuwa baada ya miaka 3-4!

Aidha ni muhimu kwa mipango ya utekelezaji, utekelezaji wenyewe, ufuatiliaji na udhibiti wake vioanishwe na mipango mikakati ya jamii kuanzia ngazi ya mtaa, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi taifa kwa kuwa chama ni sehemu tu katika ulimwengu wa nchi na mambo yake.

Kweli jumuiya za chama hicho zimefanya uchaguzi na sasa zina viongozi wake, isipokuwa ninaamini kilichofanyika ni kutanguliza gari la farasi mbele na farasi kuja nyuma. Ushuhuda wa hili ni kauli na vitendo vya viongozi wa taasisi hizo zinazotia mashaka kama viongozi wake wamefundwa na wanaijua, kuikubali na kuitekeleza visheni ya chama, kama chama kinayo visheni hiyo hivi leo! Na swali kubwa ni je tunachagua viongozi wetu kutokana na nani mtoto wa nani au ni maarufu kiasi gani au kutokana na uwezo wake kama kiongozi ? Umaarufu na uwezo wa kuongoza ni vitu viwili tofauti.

Uongozi unaoshirikisha watu kidunchu au usioshirikisha watu kabisa katika mipnagona maamuzi yake siku zote hujikuta ikiwajibika kujipanga na kujieleza upya tena na tena na mwishowe kuwa imo katika biashara ya ahadi na maneno kwa wingi lakini hakuna cha manufaa kwa wananchi kinachofanyika. Hali ikifikia hivyo, maswali ya wananchi huzidi kuongezeka. Na wale wanaojiingiza papo kwa papo na kutoa majibu ya mkato fumba na kufumbua huwa ni wababe na mashujaa wanaostahili kuungwa mkono.

Fursa ya kipekee imejitokeza tokea mwaka 1977 wakati CCM ilipoundwa. Fursa itakayokipa jina, heshima na kumbukumbu milele chama tawala na kukipa nafasi maalum katika historia ya Tanzania. Nayo siyo nyingine ni ile ya ujasiri wa viongozi wake ambao pia ni viongozi wa serikali kutamka na kubaini kwa ulimi, moyo na kalamu: ' Wananchi ndio bwana, tajiri yetu na sisi ni watumishi wao. ' Na kisha badala ya kujitia kimbelembele na kupora ukubwa wasioustahili kuwaachia Watanzania kuunda Baraza la Kikatiba la Mwaka 2011 ambalo litapatikana kwa makundi ya kimaslahi mbalimbli nchini kuwachagua wajumbe wake kuwawakilisha katika mchakato mzima wa kupata katiba. Tume haistahili na sio sahihi kuundwa na rais ambaye ni mbia katika mchakato wa katiba. Tume inastahili kuundwa na baraza hili la kikatiba. Na masual yote ya kuanzia na kufikia hatima ya mchakato wa katiba mpya unastahili kusimamiwa na baraza hili na sio vinginevyo.

Ni muhimu CCM wazisome alama za nyakati. Na mambo ya wakubwa yasiachiwe watoto. Na hakuna kosa kubwa kama lile la viongozi wa CCM kujiona wao ni 'wakubwa na wana shughuli nyingi sana' na eti hawana muda wa kushiriki kwenye makongamano yanayoitishwa na wale tunaoamini ndio mabingwa na wataalamu wa hali ya juu katika masuala ya katiba hapa nchini. Hili linaonesha mushkeli mkubwa kwa viongozi wa chama hicho, uendeshaji wake na kama kina nia ya kweli ya kuwaachia wananchi wa Tanzania kuwa na katiba mpya au wanawadanganya Watanzania ili wakubali kuweka viraka tu kwenye katiba iliyopo.

CCM ina kila sababu ya kubakia kwenye ligi daraja la kwanza kisiasa nchini endapo itakuwa na visheni na misheni inayoeleweka na wote -viongozi kwa wafuasi; itakapowatumia na kutumia ushauri wa wataalamu badala ya ushauri wa watoto wa mjini; haitakuwa kazi kwa wachezaji wapya kuingia kwenye timu hiyo kama vile wachezaji wanaotaka kutoka itakavyokuwa rahisi kwao kutoka; viongozi wataacha umimi, ubinafsi na uchama hata usipostahili; viongozi watakapokuwa kwa ajili ya wote na sio wachache; itakapotambua uaula wa mambo na kuyafanya kwa wakati; viongozi watakapotumia muda walionao kujenga badala ya kujibomoa au kuwabomoa wengine; na itakapotambua akili ni nywele na kila mtu ana zake! Na mzungu wa kula hafunzwi mwana. Na CCM ikijiganga huku ikijua au ikiwa haijui kuwa inaumwa na gonjwa la 'ndivyofunavyofikiri' kama vile yule mtu anayekwenda kunywa kikombe kwa babu -tofauti kubwa itaonekana kwa faida ya nchi hii na watu wake!