Monday, April 25, 2011

Dini, Vyama vya Siasa na Katiba mpya

NINAAMINI ya kwamba huu ni muda mzuri wa kuzungumzia kichwa hicho hapo juu cha makala haya, siku ya leo, wakati wenzetu Wakiristo wanapokuwa wakiadhimisha sikukuu yao muhimu ya Pasaka.

Katika miezi ya karibuni hapa Tanzania kumekuwa na vuta nikuvute kati ya dini mbili kubwa, yaani, Wakatoliki na Waislamu kwa upande mmoja na kwa upande mwingine vyama vya CCM na CHADEMA na wale wanaoabudu ukubwa, maslahi
na manufaa yao binafsi kutaka kuwachanganya Watanzania kwa kuweka misalaba, mwezi na nyota katika bendera za vyama vya kisiasa isivyo rasmi.

Jambo ambalo ninaliona sio linalosasaisha mfumo wa vyama vingi, siasa na uongozi wetu bali linaloturudisha nyuma kimaendeleo kwa miaka kadhaa. Maana madhara ya hili yanaweza kuiangamiza nchi fumba na kufumbua na amani na umoja tunaouimba vikafunikwa na vilio, usononi na damu kwa miaka mingi ijayo. Na badala ya kujengea watoto na wajukuu wetu taifa lenye umoja na amani tukawajengea taifa la mauaji na balaa zisizokwisha kama ilivyo kwa nchi ambazo tayari zimeshajitupa katika tope la moto la volkano ya kuchanganya dini na siasa.

Inafaa kwa viongozi wetu wa kisiasa, kibiashara, kidini na kijamii kutumia muda huu kutafakari ni kwa namna gani tunaweza kuendeleza utaifa, umoja na amani yetu pamoja na tofauti zetu mbalimbali na kutokubali kuwa kama NIgeria ambapo Waislamu huamua kumpigia kura mgombea urais eti tu kwa sababu ni wa dini yao na wakiristo nao kadhalika huamua kumpigia mgombea urais kwa misingi kama hiyo hiyo.

Washikadau wote wa katiba mpya ni lazima watambue umuhimu wa kifungu kinachohusu dini katika katiba. Maana michango yao bila shaka ndiyo itakayosaidia kupata aina ya kifungu au ibara muafaka na mujarabu kuhusu dini katika katiba mpya ambacho kitatulinda sote na vizazi vijavyona kikawa hakipendelei au hakionei dini hii au ile.

Ingelifaa pamoja na mambo mengine ibara husika iwe na mambo yapi ya dini ni muhimu kuwa katika katiba ;ufafanuzi uwepo kuhusu uhusiano wa vyama vya siasa na dini; uhusiano wa serikali na vyama vya siasa na yale yote ambayo kwa kuangalia nyakati tulizo nazo yanaweza kuwa vichochezi vya matatizo au chachu na changamoto ya kujenga nchi yetu iwe na umoja na amani wakati wote, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, bila dini kuwa sababu ya kuvunjika kwake.

Ni wakati mzuri pia wa kuwafichua wale wanaoingia katika siasa na serikali kwa malengo ya kidini kama ilivyo kwa wale wanaoingia katika siasa na serikali na kuogopa kuwatendea haki watu wa dini zao eti kwa kuwa wao ni viongozi na wanahofia kujikwaza kwa kufanza hivyo. Kiongozi yeyote akishindwa kuwa mkali kama Baba wa Taifa alivyokuwa mkali kwenye jambo hili, atambue kuwa ndiye atakayekuwa chanzo cha mwanzo wa mwisho wa amani na umoja wa Watanzania.

Uwazi katika mahusiano ya viongozi wa dini na wanasiasa ni kitu cha kufa au kupona, maana ni pale 'vichaa wa kisiasa' wanapofunga ndoa na 'vichaa wa kidini' ndipo mambo katika jamii husika yanapokwenda arijojo na kuvunda.

Hakuna Mtanzania anayependa kusumbuliwa na umaskini, maradhi na ujinga. Na kwamba jukumu na wajibu wa kila dini pamoja na kuokoa roho za wafuasi wao ni kuipa akili na miili yao afueni hapa duniani. Na katika hili dini zote zinastahili kushindana katika kumsaidia Mtanzania bila kujali ni wa dini gani. Dini zipo kwa ajili ya kuwafaa masikini zaidi kuliko viongozi na matajiri.

Uhuru wa kuabudu pamoja na kila dini kuwa na taasisi zote zinazosaidia waumini wao kutekeleza imani yao kwa mujibu wa dini, vitabu na mafundisho yao husika ni jambo muhimu. Hili liendane pia pamoja na makubaliano juu ya taratibu za kiimani katika shule, vyuo, maofisini na mahala pengine pa kazi ili pasiwe na anyenyimwa uhuru wa kuabudu kwa kisingizio kimoja au kingine. Aidha, pawe pia na usawa katika sikukuu za kidini na upambaji katika maofisi ya serikali, umma na binafsi.

Hiki kiwe kipindi pia cha kukata mzizi wa fitina kuhusu kuchanganya dini na siasa au siasa na dini. Watanzania tufikie mahala pa kuamua na kukubali mipaka ya viongozi wa kila sekta au la tunakaribisha matatizo yasiyokuwa na mwisho. Mathalani, kwa kuruhusu viongozi wa kiuchumi (wafanyabiashara) kuingia katika siasa tumeona jinsi ufisadi na rushwa zilivyokithiri. Na ni pale ambapo viongozi wa dini walipoanza kuingilia moja kwa moja kisiasa badala ya kuwaongoza, kuwaelimisha, kuwarekebisha na kuwataadibu wanasiasa basi wanasiasa wanaotafuta urahisi wa mambo wameamua kabisa kuwanunua baadhi ya viongozi wa dini kwa maslahi binafsi na sio ya wafuasi wao wala ya nchi na watu wake. Hivi leo dini zetu na viongozi wake wamebaki kulalama bila kujijua wao wenyewe ndio tatizo, maana kondoo wao, wakiwemo wanasiasa wakubwa kwa wadogo hawana wachungaji. Hakika unaweza 'ukamtumikia kafiri kupata mradi wako,' lakini vilevile 'unaweza ukamtumikisha kafiri ili upate mradi wako.'

Siasa wakati mwingine huitwa mchezo mchafu na kiongozi yeyote wa dini anayejiingiza humo asisahau kuna siku lazima atapakwa matope kama sio kinyesi. Kwa ushauri wangu, Tanzania haitajengwa na wanasiasa tu (na hasa kukiwa na 'levo graundi') na kwamba madaktari, walimu, wakulima, wanamichezo, wasanii, wafanyakazi, wataalmu mbalimbali, wafanyabiashara, watoa huduma kila mmoja wetu ana mchango mkubwa anaoweza kutoa kwa nchi yetu na watu wake. Kazi ya katiba mpya iwe ni kuhakikisha kwamba sio wanasiasa tu wanaolipwa vizuri bali kila mtu katika nafasi yake na ikiwezekana wanaoingia katika siasa wasilipwe mishahara tofauti na ile ya elimu na utaalamu wao. Kwa maneno mengine wanaostahili kulipwa vizuri zaidi ni wale wanaowaletea wananchi na nchi maendeleo na siyo kinyume chake.

Mantiki ya hili ikiwa ni kwanini tuwalipe wanasiasa na viongozi mishahara mikubwa wakati wao wanashindwa kuwatoa watu wetu toka kwenye umaskini. Kwanini nusu ya mishahara na marupurupu yao yasikatwa na kutumika kupunguza umaskini nchini ? Bila shaka kuna watakaosema pia na viongozi wa dini nao wapunguze maisha ya kifahari yanayowalazimisha kuchaji ada na gharama nyingine katika huduma wanazotoa ambazo haziendani na hali ya Watanzania walio wengi.

Sio siri kwamba kama nilivyokwishawahi kusema huko mwanzoni katika dunia ya leo ni kitu kianchowezekana kwa mwizi kujiunga na jeshi la polisi sio kwa jukumu na wajibu wa kulinda raia na mali zao bali kwa ajili ya kuiba na kuwa tajiri bila ya kutuhumiwa na mtu kwa kuwa ni polisi.

Ndivyo ilivyo pia kwa vyombo vya kidini. Ni rahisi hivi leo mtu kuwa padri au shehe sio kwa sababu kwamba ni mcha-Mungu na anataka kumtumikia Mungu kikwelikweli bali kwa ajili ya kustarehe au kuwaibia wafuasi wao wasio na mashaka nao na kujinufaisha wao binafsi na wale wanaokula nao.

Dini na madhehebu za dini ni lazima ziwe na uwezo wa kimtaji, kijasiriamali, kijamii, kiuongozi au kiutawala, kifedha na kimiradi kujiendesha vyenyewe. Maana hatari kubwa katika demokrasia na uwajibikaji uongozi huletwa pale serikali na vyama vya siasa navyo vinapotoa sadaka kwa viongozi wa dini kwa minajili ya kuwanunua viongozi hao. Tukumbuke ufakiri ni nusu ya ukafiri, na dini maskini ina hatari ya kuwa na viongozi na wafuasi wengi makafiri.

Isitoshe Wakiristo wana nchi na mashirika kabakaba ya kigeni yanayowasaidia na yanayoendelea kuwasaidia. wakati Waislamu wana ndugu zao wa Kiislamu ambao nao wapo tayari kuwasaidia na kinachotakiwa ni uongozi bora, adilifu na wenye nia ya kweli kuendeleza dini na wafuasi wao na sio wabadhirifu, wababaishaji, ombaomba na kina saidia.

Upo umuhimu wa kujiuliza hivi kutokana na madai ya maisha na matumizi ya kifahari kwa baadhi ya viongozi wa dini sio muhimu kuwa na mabaraza ya Wazee Waadilifu wa kidini kusimamia mifuko mbalimbali ya kidini. Aghalabu wengi wao wakiwa ni viongozi safi wa kidini waliostaafu. Maana kadri dini zetu zinavyoongozwa na vijana vishawishi mbalimbali vinaweza kuwateka vijana hao na wakatumia mali za kanisa na misikiti kwa faida yao badala ya manufaa kwa wafuasi wenye matatizo ya kweli yanayohitaji misaada hiyo.

Ni muhimu pia kwa serikali kutoruhusu uuzaji holela wa mali za dini au wakfu na ni lazima izisaidie dini kuhakikisha kuwa mali hizo zinalindwa na zinakuwa na manufaa kwa wanaimani kizazi baada ya kizazi.

Dini lazima ziwe na viongozi waliosomea sio tu dini bali elimu mbalimbali ikiwemo uongozi au menejimenti ya taasisi na uwezo wa kuwatumia na kuwasimamia wataalamu mbalimbali wenye imani tofauti kuendesha mambo yao kwa faida badala ya wasiojua kuyaendesha mambo hayo kihasara. Dini yenye viongozi dhaifu, mbumbumbu wa menejimenti na oganaizesheni, wababaishaji na wasioachangia maendeleo ya kweli ya taasisi zao kwa kawaida ndio chimbuko ya dini au madhehebu zenye migogoro na vita visivyokwisha.

Dua za wale wanaoigeuza serikali na wanasiasa kuwa Mungu wao, Mola huzipuuza. Mola ambaye pia huitwa mlipiza kisasi hugeuza ubaya, mbaya anaomtakia asiyekuwa mbaya yakamfika huyo muomba dua. Kumbuka kisa cha Firauni na Musa na watoto wao wa kwanza.

Waumini wana kazi kubwa ya kudai uongozi bora na safi katika dini zao kama njia mojawapo ya kujenga demokrasia ya kweli nchini. Dini inapokuwa na viongozi bora na safi haiwezi kuyumba ovyo. Hata viongozi wa serikali huisikiza, wanasiasa huwatafuta na wafadhili wa ndani na nje huona wepesi wa kuzisadia dini kama hizo katika mambo mbalimbali. Dini inapokuwa na viongozi wasiokwenda shule, wababaishaji, wapenda anasa, wanafiki, waongo na wanaotumiwa na wanasiasa kiurahisi hukosa heshima na kuaminika na haiwezi kufanya lolote la maana kwa wafuasi wake. Na aghalabu huwa ni dini ya mwisho kimaendeleo katika jamii husika. Asalam aleykum warahamatullahi taallah wabarakat.

No comments:

Post a Comment