WAKATI mwingine wale tuliosoma au kwenda shule, huwa tunafanya kosa moja kubwa. Kosa hilo sio jingine ila ni lile la kudhania kwamba tunajua kila kitu. Kwa kuamini hivyo, huwa tunafanya makosa na kudhulumu nafsi zetu na za wenzetu wakati mwingine bila kujua.
Hapo zamani za kale akina sungura vijana waliitisha mkutano mkubwa wa wanasungura wote kuzungumzia mustakabali au hatima ya jamii yao. Ilionekana dhahiri katika kikao hicho kuwa vijana walikuwa wanakerwa sana na wazee kushika nyadhifa mbalimbali za juu na wao kupewa zile za chini tu. Ni dhahiri walikuwa wakitamani kushika nyadhifa hizo za juu wao wenyewe. Hilo ndilo walilolitaka.
Lakini hawakulizungumzia moja kwa moja, bali walitaja sababu tofauti zaidi. Wengine wakadai kwamba wazee wanakula zaidi kuliko vijana, wengine wazee hawaoni wala hawasikii hoja zote vizuri; wengine wakadai wazee ni wazito kufanya maamuzi; wengine wakadai wazee wana huruma kupita kiasi, ili mradi kila mmoja alitoa sababu iliyochangia, kuonyesha kuwa wazee kwa kweli walikuwa hawawafai tena.
Mwishowe, ikaamuliwa kwamba wazee wote wauawe ili udhia uishe. Na sungura wote isipokuwa mmoja tu aliyekuwa na mapenzi ya kipekee kwa baba na mama yake hakutii amri hiyo. Kwa maneno mengine unaweza kusema aliwasaliti wenzake. Lakini akilini mwake alichowaza ni kuwa wazee wameona, kusikia, kutembea, kupitia na kukutana na mambo mengi. Pengine siku moja wakibakia wao vijana tu patazuka jambo ambalo hakuna hata mmoja wao atakuwa na wazo ni namna gani walitatue. Kwa hiyo hakuwaua wazee wake, bali alikwenda kuwaficha mahala salama. Akawa anawahudumia wakati wote wakiwa mafichoni bila kuchoka.
Kufanya hadithi yetu kuwa fupi palizuka tatizo ambalo lilikuwa halijawahi kutokea toka sungura vijana wale wazaliwe. Yule aliyewaficha wazazi wake aliwaendea na tatizo hilo nao kama vijana wa siku hizi wasemavyo wakamwambia mbona 'ishuu yenyewe simpoo tu! '
Tatizo hilo lilimalizwa na ajuza na sahibu wa sungura kijana mjanja kuliko wote, ikadhihirisha wenzake wote walikuwa wajinga. Kijana sungura hakuonekana msaliti tena, bali mkombozi sasa.
Katika jamii yetu ya Kitanzania tuna wazee wachache ambao katika ujana wao wamepitia kazi au shughuli mbalimbali za kiuchumi, kijamii, kiteknolojia, kisayansi, kiutamaduni, kiafya na tiba, kibiashara, kibenki, kielimu na kadhalika.
Sikutaja wanasiasa kwa makusudi. Wao aghalabu wanakumbukwa tena sana. Na hivyo hawachangii kilio cha mada yangu. Ninapenda kuwazungumzia wale ambao pamoja na elimu, ujuzi na uzoefu walionao hakuna mwenye habari nao iwe mambo yanakwenda vizuri au vibaya. Ingawa wenye dhamana leo wanaamini kwamba hawawahitaji, wazee hao wangezungumza saa chache tu kwa juma na viongozi hao kuna mambo mengi ambayo yangelikwenda vizuri zaidi kuliko yanavyokwenda sasa. Na pengine wazee wangeliwafungua macho pia juu ya kutatua matatizo fulani na kutumia fursa zilizopo kuneemesha idara, wizara au shirika au kampuni kwa hatua ndogo chache tu.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, japo serikali inawatumia wazee vizuri sana katika siasa, lakini serikali hiyo hiyo imeshindwa kuwatumia wazee wataalamu kwa namna yoyote ya kujenga serikali bora zaidi. Lakini kama kuna taasisi ambayo ingelinufaika sana na hekima na busara za wazee taasisi hiyo isingelikuwa nyingine ila serikali, wizara, mikoa na wilaya.
Binafsi ninaamini ipo haja ya kuwatumia wazee hawa wenye utaalamu katika masuala ya elimu, kilimo, uhandisi, usalama, afya, usafiri na uchukuzi, ujenzi wa nyumba na barabara na kadhalika kama washauri maalum kupitia mabaraza ya wazee ya kisekta.
Katika masuala ya usafiri ( ATC, TRL, TAZARA, UDA) , mawasiliano (TTCL), Nishati na Umeme (TANESCO, SONGAS, SOLAR), benki na taasisi za fedha, shule, vyuo, hospitali, mashirika ya kibiashara, viwanda na mengine kama hayo kujifunza kutoka kwa wazee wetu waliokwishafanya kazi au shughuli kama hizi tunazofanya leo huko nyuma.
Nina hakika kuwa wale wazee waliokuwa wakifanya kazi kwenye mashirika ya ATC, TAZARA, TRC, UDA na KAMATA wakitafutwa na mameneja vijana wa leo, wakakaa pamoja na kushauriana hapataharibika kitu. Na kuna uwezekano mkubwa sana wa wazee hao kuwa dawa ya baadhi ya matatizo yanayokabili mashirika hayo sasa.
Ninaamini ndivyo itakavyokuwa kwa TANESCO, TIPER, na kwa wale wote wanaovinjari leo njia na mbinu mbadala za kuipatia Tanzania nishati ya umeme, mafuta na masuala ya nishati mbadala yanaweza kufanikiwa sio haba kwa kutumia uzoefu, busara na hekima za wazee. Bila shaka itasaidia mashirika hayo kutotugeuza abiria na wenye magari mabuzi yao ya kuchuna.
Hakuna sababu ya kampuni kama TTCL hivi leo kuendeshwa kihasarahasara; lakini kama tunadharau ushauri wa wazee wastaafu waliowahi kufanya kazi katika shirika hilo ni vpi tutalinusuru? Wazee hawa wanaweza wasiwe na la kuchangia katika masuala kama yale ya TEKNOHAMA na simu za mkononi, lakini ninaamini wakishirikishwa katika vikao muhimu baada ya muda watakuwa wanajua wanachokizungumza maana wana elimu na ufundi katika hayo, tena wa miaka mingi tu!
Kwenye kila Wizara, mkoa, wilaya na idara kuna mzee mmoja au wawili ambao wako hai nao wanaona mengi tu yanayokwenda mrama au ovyo ovyo! Hebu basi tujaribu kuwatafuta walikojificha na kupata mawili kutoka kwao ili tuboreshe utendaji kazi wetu na kuifanya dhana ya serikali inayowajibika kwa wananchi wake kuwa ni vitendo na sio maneno.
Upo ugonjwa mkubwa katika ofisi za serikali unaoletwa na ile tabia ya watu kuamini kuwa kiwango chao cha utendaji kazi walichofikia ndio cha juu kabisa na kwamba hawawezi kufanya zaidi ya hapo. Kumbe kwa kubadili muundo tu wa idara au taasisi iwayo na kisha kuleta maadili, mifumo, taratibu na kanuni mpya za kazi watumishi wa umma wanaweza wakafanya maajabu ya kuifanya serikali iheshimiwe na kupendwa zaidi na wananchi wake. Nani wa kusaidia hapa kama wazee waliopitia wizara husika?
Tatizo la mashirika ya umma ni kwamba, unaweza ukaliendesha kihasara, lakini kwa kuwa kuna gharama nyingi zisizolipiwa na pengine kuna ruzuku kila mwaka utadhani shirika lina ufanisi na ufanifu, kumbe sivyo!
Binadamu wachache wanataka kuijua historia yao kwa kina, lakini bila historia hiyo ni vigumu sisi wa leo kuelewa tunakotoka na tunakokwenda. Na hakuna mwalimu mzuri wa historia kama mzee aliyepitia na kuyaonja hayo yaliyomo katika historia.
Wazee wameptia mitihani mingi ambayo kwa kuwashirikisha katika mipango na maamuzi yetu wanaweza kutuokoa na kuingia hasara na gharama zisizo za lazima.
Hivi leo tunazungumzia kuboresha sekta za elimu na afya na masilahi ya walimu, madaktari na manesi. Lakini ni nani aliyekwenda kukutana na walimu, madaktari na manesi wazee wenye umri zaidi ya miaka 70 kupata ushauri wao. Na ni kitu gani wao walichokifanya huko nyuma tukaendesha taasisi za elimu na afya kwa ufanisi na ufanifu zaidi? Ni watu gani muhimu zaidi katika sekta ya elimu na afya? Walimu, Madaktari, manesi, wakuu wa taasisi au wakaguzi au wote ni muhimu na kila mmoja ana nafasi yake? Haya ni maswali yanayoweza kujibiwa vema zaidi na vikongwe hawa katika sekta ya elimu na afya.
Wazee katika nafasi mbalimbali walishawahi kujifunza kutokana na makosa yao wenyewe ya wakubwa wao na ya wadogo wao. Kukaa nao kwa siku mbili tatu kunaweza kuisaidia sekta fulani kuepuka kurejea makosa yale yale katika miaka hii ya 2000.
Wazee wengi hawakusoma falsafa, sosholojia wala saikolojia. Lakini maisha na uzoefu wao umewapa elimu ambayo ni vigumu mtu kuipata katika vyuo vikuu vingi duniani. Bado tu hatujaona 'nishi' hii ya wazee kuwa washauri na wataalamu wakubwa katika kusaidia kutatua matatizo yetu?
Masuala mengi ya jamii, uchumi, uzalishaji mali, utoaji huduma, biashara, ajira au kazi na kujiajiri, fedha, ushuru, mitaji, kodi, utamaduni, michezo, sanaa, uandishi, utangazaji na mambo kama hayo yanaweza kunufaika sio haba na kutafuta busara na hekima za wazee katika mpangilio unaoinufaisha taasisi husika na wazee wanaochangia kunufaika kwa taasisi hiyo.
Nimalizie kwa kukumbusha kuwa, ni wazee tu waliokwishapitia na kuona machungu ya kustaafu na kupata masilahi duni ya kustaafu. Nani wa kutushauri huko NSSF, NPF, LAPF, NHIF kama wao. Siamini wanataka sisi wazee wa kesho tupitie misukosuko kama yao. Kuna msemo wa Kiswahili unaosema: “Akili ni nywele, kila mtu ana zake.” Na wewe unaweza kuutafsiri utakavyo. Lakini kubwa kwa upande wangu ni kwamba, hakuna nyumba, mtaa, kata, tarafa, wilaya, mkoa au taifa lenye watu wanaojua kila kitu na wenye majibu ya kila swali na ufumbuzi wa kila tatizo. Ni kutokana na ukweli huu ndio inakuwa ni busara tupu na hekima kuwashirikisha watu wengi kadri iwezekanavyo katika kupanga na kuamua masuala yanayogusa sehemu kubwa ya jamii husika. Vinginevyo ni kuchimbana, vioja, vituko, kashfa na lawama zisizokwisha!
Tuesday, April 19, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment