INASEMEKANA kwamba uchumi au bora zaidi mapato yanayopotea kwa Watanzania kutokana na kufinywa au kubanwa utamaduni, mila, historia na lugha za kikabila ni sawa na mapato yanayopatikana hivi sasa nchi nzima.
Katika dunia hii ya utandawazi ajabu ni kuwa japo dunia inakuwa kijiji lakini majukumu ya usimamizi na uongozi katika nchi yanazidi kushuka chini hadi kwenye jamii, vijiji na watu wenye asili moja.
Kutokana na sababu za kisiasa huko nyuma viongozi wetu walilazimika kuua uongozi wa kimila, kupuuza lugha za makabila na kupiga vita tamaduni za watu mbalimbali kuhifadhiwa na kuendelezwa.
Sababu kubwa iliyotolewa wakati huo ilikuwa ni kulinda amani na umoja wa Watanzania na kwamba kama tungeliachiwa kushabikia makabila yetu kupita kiasi basi tungeweza kusababisha ukabila nchini.
Hata hivyo, ujio wa siasa za mfumo wa vyama vingi umezua makabila mapya. Makabila hayo ya 'kichama' yanaelekea kuwa hatari zaidi kwa umoja na amani yetu kuliko makabila ya kimapokea.
Katika nchi hii ilifikia mpaka mahala ikakubalika bila kuandikwa mahala kwamba watu kutoka makabila makubwa au yenye neema zaidi hayastahili kabisa kutoa viongozi. Na hadi wa leo katika baadhi ya vyama vyetu vya kisiasa ni mwiko mtu kutoka kabila kubwa kuchaguliwa kama kiongozi au kuteuliwa kuwa mgombea nafasi zaidi ya ubunge.
Katika kufanya hivyo, hakuna aliyeangalia hasara au faida za kutawaliwa na wale wanaotoka makabila makubwa kiutafiti na kiutaalamu na hakuna mahala popote tunapoelezwa faida na hasara za kutawaliwa na watu kutoka makabila madogo na uwezo wao kiuongozi.
Lakini ni dhahiri zipo sababu na zinajulikana ingawa zinafichika na miaka 50 baada ya uhuru tunaweza kutathmini kwa uhakika faida au hasara za kuongozwa na watu kama waliowahi kutuongoza.
Tanzania ina zaidi ya makabila 130 na makabila yote haya ni shule kama sio vyuo. Maarifa, busara, hekima na urithi mbalimbali umo humo na kama yanayostahili yakifanyika basi itakuwa ni rahisi na hasa mikoa itakapokuwa ikijiendesha kama maeneo huru kiuchumi kupata maendeleo kwa kasi na haraka zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.
Ili kufikia huko kwanza tuangalie jinsi makabila yetu ya asili yanavyoweza kuhifadhi lugha zao kwa kuwa na kamusi za lugha hizo na kisha vitabu vya kufundishia lugha hizo. Kwa mantiki hii kila kijana toka kabila lolote Tanzania ataweza kujifunza lugha ya kabila lolote analolitaka. Kwa mfano, Mkwere akitaka kuolewa na Mhaya anaweza kujifunza Kihaya na mwenzie akajifunza KIkwere na hivyo kuendelea kudumisha mila pia na umoja wetu.
Sambamba na hilo hapo juu ni muhimu kuwa na majumba ya makumbusho mawili matatu kwa kila kabila kutegemeana na ukubwa na upana wa utamaduni na mila zao. Kwa hiyo badala ya kuwa na jengo moja la makumbusho jijini Dar es salaam, tutakuwa na majumba ya makumbusho zaidi ya 390 ya makabila yetu.
Katika hizo makumbusho tatu za kikabila ile ya kwanza itajihusisha zaidi na hifadhi na zana zilizotumika kurithishaa maarifa, mafunzo, kazi na huduma mbalimbali za kijamii; ya pili itahusu masuala ya uzazi, ndoa na kifo na ya tatu itahusu masuala ya uongozi, uchumi, biashara na mahusiano na makabila au watu wengine.
Majumba haya ya makumbusho 390 yakijengwa vizuri na panapostahili na kutoa huduma ya kuwaridhisha wananchi na watalii watakaokwenda kuyatembelea peke yake yana uwezo wa kuingiza mabilioni ya shilingi kila mwaka.
Watanzania binafsi nao watakaotaka kuanzisha majumba yao binafsi ya makumbusho katika eneo moja la asili, historia na utamaduni wetu nao waungwe mkono na wasaidiwe kufanikisha azma yao hiyo.
Kazi hii inaweza kuanza kwa kuwa na majumba hayo ya makumbusho kama wavuti kwenye tovuti kwa kuanzia na baadaye rasilimali zikishapatikana majengo hayo yatajengwa.
Nimekuwa nikijiuliza kutokana na ujio wa watoto na vijana toka vijijini wanaofikia kwangu kwa ajili ya kazi au kujiendeleza kimasomo na uelewa wao wa Kiswahili kama kweli tuanwatendea haki watoto wanaoishi vijijini ambako ni lugha asili inayotumika zaidi kuliko Kiswahili.
Ninaamini wakati umefika wa kupanua na kuwa na kina kirefu zaidi cha maarifa yetu kwa kuwa na MAGAZETI NA REDIO ZA KIJAMII katika kila eneo - kabila. Magazeti na Redio zitakazowafunza wanaoelewa lugha hizo mambo kwa haraka na wepesi zaidi kuliko ilivyo sasa. Sio tu watoto na hata watu wazima watapata fursa ya kujifunza majina ya vitu, miti, ndege, wanyama, samaki na kadhalika kirahisi kwa lugha zao kwa kutumia redio na magazeti hayo.
Taifa lolote lina madaraja matatu ya mizizi. Daraja la kwanza ni mizizi ya lugha za kikabila, daraja la pili ni mizizi ya lugha kadhaa zinazokurubiana au kufanana na kusikilizana na daraja la tatu ni mizizi ya lugha kuu kitaifa. Mizizi hii ikiwa imara na watu wana maarifa ya kutosha toka makabila yao inakuwa ni rahisi kupanda madaraja mengine hadi kufikia upeo wa kupata wahandisi na wanasayansi wanaoweza kuelezea lolote lile kwa lugha yao kikabila.
Vyombo hivyo vya habari kwa lugha-zetu-za-kwanza vitasaidia pia kufundisha, kukuza, kuendeleza na kusasaisha lugha, ngoma, muziki, maigizo, michezo, vinywaji, vyakula, utengenezaji filamu, nyumba na makazi asili, hadithi, simulizi mbalimbali kama vivutio vitakavyouzika kwa watu wa ndani na wa nje ikiwemo watalii pia.
Ifahamike tofauti na Mheshimiwa Kabwe anavyosema kuwa lugha ya Kiswahili imezimeza lugha za kikabila, mimi ninaamini lugha ya Kiswahili imezuia kuzisaidia lugha za kikabila kwa njia kuu mbili. Kwanza, kwa kuzuiwa kutumika kama lugha ya kufundishia toka chekechea hadi chuo kikuu lugha hiyo imeshindwa kuzisaidia lugha za kikabila. Pili, kwa kuwa Kiswahili kimekosa fedha za kufanyia tafiti lugha za kikabila ili kujifunza kutoka huko imeshindwa pia kuzisaidia lugha hizo kujiweka kwenye nafasi bora zaidi kuliko iliyo nayo sasa. Fursa hizi zingelikuwepo, Kiswahili kingelikuwa na kupanuka Afrika nzima na makabila yetu kama walivyo Waskotishi na Wawelshi huko Uingereza tukajivunia lugha zetu zote mbili. Yaani, tukajivunia Kiswahili kwa sisi kuikitumia nacho kutumika dunia nzima na wakati huo huo lugha zetu za kikabila kutumika kwenye maeneo yanayostahili tukidhihirisha ulimwengu uzuri na ubora wa kuwa na vingi vinavyofumwa kuwa kitu kimoja. Hii ndiyo visheni niliyo nayo na ninaamini ni ya wengi pia, nako ndiko tunakostahili kwenda.
Lakini utamaduni, mila na historia za kila kabila zinahitaji usimamizi na uongozi. Itakuja kuonekana huko tunakokwenda kwamba uko umuhimu wa kurejesha tena nafasi ya uchifu au uongozi wa makabila kwa njia moja au nyingine. Ninasema kuurejesha lakini nikiamini pamoja na kusemekana uchifu ulifutwa kuna makabila ambayo bado kiukoo, kimila na kijamii yameendelea kuwatukuza na kuwaheshimu watu fulani miongoni mwao kama machifu wao. Mmojawao ninaamini alikuwa rafiki yangu, hayati Adam Lusekelo kwa upande wa Wanyakyusa wa Mwakaleli.
Usimamizi au ungozi huu wa machifu, kikabila utasaidia sana kurejesha maadili, adabu na nidhamu kwa wananchi na hasa watoto na vijana wetu; kupunguza ubinafsi na umimi kwa kiasi kikubwa kwani sasa jamii au kabila litapewa umuhimu juu ya mtu binafsi; na vile vile kujenga umoja kati ya watu wa hali, asili na imani mbalimbali.
Muhimu katika suala la kuenzi utamaduni wetu ni pamoja pia na kutunza na kuhifadhi vile vitu au dhana zisizoshikika kwa mikono. Vitu ambavyo tunavizungumza na kuvifanya kila siku lakini sio vitu vinavyoshikika lakini navyo vina thamani na vinaweza kuwa na maana kwa vizazi vijavyo na kuwa vivutio vya utalii leo na kesho pia. Yaani, jinsi tunavyozungumza, tuanvyotembea, tunavyojumuika na wenzetu, mazishi na kilio, uzazi au ndoa na nderemo na imani au hisia zetu mbalimbali na jinsi tunavyoonekana kwa wengine. Kwa mfano, huko nje, iwe Ulaya au Marekanim hadi juzi Watanzania walikuwa wanaaminika na kuonekana ni watu wapole, waungwana na wataratibu sana katika mambo yao. Hili nalo kama ni jambo zuri tunastahili pia kulienzi.
Tuesday, April 5, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment