Tuesday, April 19, 2011

Tutazame Upya Uwekezaji katika madini

Hapo zamani za miaka ya 60 benki ya dunia ilivutiwa sana na azma ya Mwalimu Julius Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania katika kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi.

Kutokana na ushawishi wa Mwalimu wakuu wa benki hiyo waliisaidia sana Tanzania kwa mikopo ya riba nafuu na wakati mwingine hata mikopo isiyo na riba na sadaka za kusaidia hili au lile.

Pengine Watanzania wakati hu0 hawakuwa tayari kiuchumi na kwa hiyo sehemu kubwa ya mikopo na misaada hiyo haikutumika vizuri. Miaka karibu 50 baadaye Watanzania bado wanakabiliana na maadui wale wale wa miaka ya 1960. Tatizo ni nini ?

Sina jibu la moja kwa moja. Lakini yapo mengi yanayosemwa kama sababu ya sisi kuendelea kuwa watu wa dhiki na ombaomba. Kwanza, wengi wanadhani tumeshajenga tabia kama ombaomba mwingine yeyote kuwa hatuwezi kujikimu sisi wenyewe bila kusaidiwa.

Wengine wanaamini kuwa nchi haijapata aina ya viongozi wa kuitoa toka kwenye umasikini. Viongozi wanaopatikana hawaaangalii mbali wala mbele na wengi wao wanataka kula tu hata kama hawachangii chochote katika pato la taifa.

Wengine wanasema kuwa sisi ni Waafrika na kama Waafrika tupo katika hesabu ya waliolaniiwa kuwachotea maji na kuwakatia na kuwabebea kuni Wazungu, Waarabu, Wahindi na sasa Wachina na Wajapani.

Wengine wanasema ni kwa sababu kama ilivyo katika mitaa yetu aghalabu wenye uwezo, ari na sababu ya kuongoza hawako katika uongozi na wasiokuwa na uwezo wala sababu ya kuongoza ndio viongozi. Na kama sivyo basi viongozi ni wanasesere wa matajiri na wakubwa wa nje.

Baadhi ya watu wanadai kuwa wanasiasa na vyombo vya habari wameingilia fani za watu wengine na kujifanya wao ndio mabingwa na wataalamu zaidi kuliko wenye fani. Mwanasiasa anajua udaktari kuliko daktari, na mwandishi wa habari anajua sheria kuliko mwanasheria.

Wengine wanasema kwa kuwa elimu yetu inatolewa kwa kizungu hao wanaoweza kusoma kwa kizungu sio hao wanaoweza kuiletea nchi maendeleo ya kweli.
Na wanachagiza tutoe mfano ya nchi angalau moja ambayo inatumia lugha ya kuazima iliyoendelea hapa duniani. Wao wanasema hakuna labda pale wazungu wenye Kiingereza wanapotawala kila nyanja ya uchumi.


Ili mradi kila mtu ana sababu yake. Mimi sikatai wala sikubali yote haya. Kwa upande wangu nizungumzie leo juu ya sera mbovu za kiuchumi zinazoruhusu watu kuchuma nchini mwetu na kuwa matajiri na sisi tukabakia masikini kama sio mafukara zaidi baada ya watu hao kuchuma na kuondoka kurudi makwao.

Afrika isipokuwa kwa nchi kama Botswana , Namibia na Afrika Kusini ni mfano mbaya wa uongozi usioweza kubadilisha maisha ya wananchi wake lakini ukaendelea kung'ang'ania kubakia madarakani. Ni mfano mbaya pia kwa kuwa hakuna mfumo wa kuchuja na kuwaondoa viongozi na watendaji wabovu wa serikali wasiochangia kwa kadri inavyokubalika maendeleo ya kiuchumi wa nchi na hivyo kuiacha serikali wakati wote ikiwa na watu bora na wachapa kazi zaidi.

Mfumo unaotaka kuendelea kuwepo madarakani uko tayari kuuza heshima, haki, maendeleo na uhuru wa watu ili mradi upate unachokitaka. Sio mfumo endelevu iwe katika maendeleo ya kisiasa, kijamii, kiutamaduni, kitekelojia wala kiuchumi. Maana ni mfumo unaobakia kwa kufanya ujanja ujanja na wala sio kuleta tofauti yoyote ya maana katika maisha ya watu.

Hata hivyo ni nchi chache katika Afrika zilizojaliwa karibu viungo vyote muhimu vya kuondokana na umasikini na kukosa maendeleo kama ilivyojaliwa Tanzania .
Mtego ni kuwa kwenye miti hapana wajenzi, na mbomoa nchi yetu sio mwananchi bali viongozi !!!

Tatizo letu la kukosa maendeleo ni kwamba hakuna kiongozi hata mmoja hivi leo anayeweza kusimama mbele ya watu na kusema yeye ni mfano wa kuigwa.
Hakuna anayeonesha mfano ili aigwe, watu wabadilike na nchi isonge mbele.

Viongozi wengi wanadai ili wao walete maendeleo kwa wananchi haraka ni muhimu kwao wao kugharamiwa kuliko maelfu kama sio mamilioni ya wananchi wote wakiwekwa kwa pamoja. Leo 2009 gharama zote Watanzania walizobeba kwa niaba ya viongozi wao hazijawaletea maendeleo. Swali linakuja, je, mfumo huu wa viongozi kula kuliko wananchi ukibadilishwa ili angalau wananchi nao wale sawa na viongozi kama sio kuwazidi nchi haitaendelea ?


Hali ilivyo sasa ni kwamba pato kubwa la taifa linaliwa na walio juu na walio chini wanapata kidogo kama hawakosi kabisa. Lakini ni nani miongoni mwao anayethubutu kusema sitaki gari la milioni 200 bali nitachukua la milioni 20 tu? Ni nani anayeweza kusema kwa kuwa sisi ni nchi masikini badala ya kukaa kwenye mahoteli ya kifahari tutajenga hosteli katika kila nchi tuliyo na ubalozi ili kupunguza gharama za kukaa kwenye mahoteli ya bei mbaya? Ni nani anayethubutu kusema mimi safari hii siendi nje acha watu wachache tu waende ili kupunguza gharama kwa walipa kodi? Haya yote hayayumkiniki kwa kuwa mfumo uliopo tayari umekwishatangaza kuwa maisha ya kiongozi mmoja ni bora kuliko maisha ya Watanzania laki moja.

Vilevile ni ukweli usiofiichika kuwa hakuna ambalo unaweza kumfundisha tembo mzee. Viongozi wetu wengi ni 'recycled materials' na uzuzi, ubunifu na utundu wa kujaribu mapya kwao ni sifuri. Mabadiliko hayaji kamwe katika mazingira ya namna hii.

Isitoshe tabia yetu sisi Watanzania ni kwamba tuko radhi 'mgeni' atajirike kuliko mwenzetu atajirike. Nisingelipenda kusema zaidi juu ya hili bali wasomaji wenyewe wanaweza kushuhudia hili kwa visa mbalimbali wanavyokutana navyo katika maisha yao ya kila siku.

Ninadhani wengi wenu mmeshawasikia watu wakilalama iweje Mhindi au Mwarabu au Mzungu au Mchina fulani kuja nchini hapa na Marlboro na baada ya miaka 2-3 anakuwa tajiri mkubwa?

Kuna maswali mengine kama vile hivi serikali inapozungumzia juu ya ubia kati yake na wananchi ubia huo unachukua umbo au muundo upi?

Tuchukue suala hili la kwamba tumewaruhusu wageni kuchimba dhahabu nchini mwetu (bila kuwashindanisha Wakanada na Wachina au waingereza na wakorea kama vile bado dunia hii inatawaliwa tu na nchi za magharibi na hivyo kukubali masharti na mkataba wa kijinga) na wao kutulipa mrahaba sawa na hakuna eti tu kwa sababu sisi hatuna mashine na utaalamu unaohitajika. Wakiimanisha kwamba thamani ya Watanzania wote pamoja, mali asili zao na serikali yao ikiwekwa pamoja haifikii ile ya utaalamu wao na mashine zao.

Laiti kama huo ubia unaozungumziwa ungelichukua sura ya ya serikali, mabenki na vyombo mbalimbali vya fedha kutmbua kwanza watu wetu wana thamani kuliko kitu kingine duniani na kisha kutoa ushauri na kuwapa mtaji-mbegu wawekezaji wazawa nchi hii leo isingelikuwa hapa ilipo.

Kama benki ya dunia iliweza kutoa mikopo na misaada ili kujenga uchumi wa Tanzania iweje leo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vyombo vyake ishindwe kuwadhamini wazawa wapate elimu na maarifa ya uchimbaji madini na kisha kununua kwa mikopo ya muda mrefu kupitia Benki ya dunia mitambo na vifaa mbalimbali vinavyohitajika katika uchimbaji madini? Au hili nalo ni ushahidi kwamba viongozi wetu ni wale wale ambao wako tayari mgeni atajirike kuliko mwenyeji aukate?

Hivi sasa sio kazi kupata masomo yote kuhusu 'geology' au uchimbaji madini na kisha kuyatafsiri yawe katika Kiswahili na kuyaweka katika mtandao ili kila anayetaka kujifunza juu ya uchimbaji madini asipate shida kutafuta masomo hayo.

Kuna tunaoamini kwamba kwa kufuata mkakati ule ule wa miaka ya 1960 tunaweza kabisa kuwawezesha Watanzania wenyewe kuwa sio tu wamiliki wa machimbo ya dhahabu bali pia wamiliki wa viwanda na huduma mbalimbali zinazochangia katika mkufu mzima wa uchimbaji na uuzaji madini ndani na nje ya nchi. Tatizo ni kuwa hakuna mwamko wala moyo wa kizalendo na kisiasa katika kufanya hili.

Endapo Tanzania itakuwa na sauti katika soko la madini na vito ni wazi tutakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kujinasua na umasikini na ombaomba.

Hili pia litatuwezesha kutumia madini kuwekeza katika sekta mbadala
kama vile elimu kwa wanafunzi toka nje,

tiba na afya kwa wagonjwa toka nje, teknolojia, ujenzi wa nyumba na makazi mapya,
kuanzisha makampuni ya umeme yatakayofanikisha kupatikana nishati hiyo kwa wote. Aidha kwa rasilimali hizo hizo itakuwa ni rahisi kupata Watanzania watakaowekeza katika nchi za nje. Hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo ya kweli bila kuwekeza katika nchi nyingine. Tujifunze toka China na venezuela ili nasi tukae mkao wa kula katika dunia ya utandawazi.

No comments:

Post a Comment