Tuesday, April 19, 2011

Vikwazo kwa demokrasia nchini

KATIKA makala hii nitajaribu kudhihirisha vikwazo vikuu vya kukua na kuimarika kwa demokrasia nchini.

Vikwazo nitakavyovizungumzia leo ni pamoja na kukosekana kwa katiba mpya; kuwepo kwa chama-dola kinachotamalaki kila nyanja ya maisha nchini; kuwa na Baraza la Mapinduzi linalopindua uhuru na haki za binadamu Zanzibar wakishirikiana na wale wasiotambua wajibu wao katika mfumo wa vyama vingi na umaskini wa vyama mbadala. Kwa wale wanaotaka kujifunza zaidi juu ya vikwazo basi waone makala zilizoko katika http://demokrasiaafrika.blogspot.com.

Kuachia watu wawe na demokrasia ya kina na pana kunataka moyo. Ni jambo ambalo halitofautiani sana na kukubali binti anayependwa na kuaminika nyumbani kuolewa. Wazazi huwa na taabu sana kutokana na mazoea kuamini kuwa watapata amani na huduma waliyoizoea kutoka kwa mtu mwingine.

Lakini wakati ukifika umefika. Hakuna njia ya kuzuia yanayopaswa kutokea. Maana wakati ni ukuta na ukiupiga kofi au ngumi utaumiza tu mkono wako mwenyewe.

Demokrasia kama mwali lazima apewe mwananchi. Hatuwezi kuendelea kumlazimisha kukaa ndani mwetu milele. Mliopo madarakani amueni Demokrasia Ruksa!

Ili hili lifanyike yapo mambo kadhaa yanayopaswa kufanyika kwanza. Mambo hayo ni pamoja na:

Kuandikwa Katiba Mpya. Katiba mpya sio jambo la kisiasa au kiserikali tu. Katiba mpya ni makubaliano mapya yaliyostahili kuwepo kati ya watawala na watawaliwa toka siku ile nchi hii ilipoamua kuwa nchi ya siasa za vyama vingi.

Tumechelewa. Na wakati ni huu. Afrika nzima inaitazama Tanzania kuona kama tumekua na kukomaa kisiasa au la. Tusikubali kutanguliwa na tutoto twa jana kisiasa katika hili.

Umuhimu wa katiba mpya ni kwamba utamaliza kabisa matatizo mbalimbali yaliyojitokeza toka mfumo wa vyama vingi uanze. Baadhi yake ni pamoja na haki na uhuru wa watu kuzungumza, kukutana, kuandamana na kuunda au kuua vyama; vyama kadhaa kujiunga na kuwa kimoja kwa hiari yao wenyewe; matumzi ya redio, magazeti na televisheni ya umma; haki ya kumiliki mali zilizozalishwa na wananchi wote kwa pamoja; nafasi za makundi ya vyama vyote ya vijana, wazee na wanawake tofauti na yale ya kichama na kadhalika.

Katiba hiyo inatakiwa kuandikwa na wawakilishi wote wa wananchi, ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi wetu wote kwa angalau miaka 50 ijayo. Hili sio jambo la kufanywa na wanasiasa au wanasheria wachache hasa ukizingatia tofauti za kijamii, kiuchumi na kisiasa zilizopo leo. Ni jambo linalohitaji ushirikishwi wa washika-dau wote wa Kitaifa.

Demokrasia nchini hapa haiwezi kabisa kukua na kuimarika kama tunaendelea kuwa na chama-dola, ambacho kwa heri au shari kinaathiri maamuzi na utekelezaji wa mambo mbalimbali.

Ikumbukwe wanasiasa ni watu. Na kila mmoja wao ana matarajio na matamanio yake. Ni rahisi kwa chama-dola kujikuta kinachanganya maslahi binafsi ya viongozi wake na maslahi ya umma. Mathalani, katika sakata la ufisadi linaloendelea hapa nchini kwa hivi sasa. Pengine viongozi wa kisiasa kweli wamenufaika kwa kiasi fulani, lakini wananchi walio wengi wamekula hasara.

Tatizo la chama-dola ni kuwa mawaziri wake aghalabu hujali tu maslahi ya chama na sio ya wananchi wote. Kwa hiyo maamuzi hufanyika sio kwa manufaa ya Watanzania wote, bali kwa sababu chama fulani kitanufaika na maamuzi hayo au vyama fulani vitaumizwa na maamuzi hayo.

Katika bunge la chama-dola tatizo ni hilo hilo. Bunge la namna hiyo hujali zaidi maslahi ya chama chao badala ya maslahi ya wananchi. Hili linapotokea uwakilishwaji wa wananchi na wabunge wao huwa umeorojeshwa kiasi cha kuwa hauna maana wala mchango wowote wa maana katika maisha ya wananchi waliowapeleka wabunge hao bungeni.

Ukiritimba wa chama-dola huathiri hata uongozi wa mikoa na wilaya. Katika mikoa na wilaya nyingi kinachoogopwa huko sio serikali yenyewe bali chama kinachotawala. Matokeo yake utakuta kuna unafiki zaidi kuliko kujitambua kwa viongozi hao na kubaini mchango unaotakikana toka kwao na jamii wanayoiongoza.

Hali hii inajitokeza pia katika tawala za mikoa na uongozi vijijini na mijini. Pale chama tawala kinapofika mpaka huku nacho kikawa ni chama-dola basi hakuna lolote la maana kidemokrasia litakalopikwa na kuiva huko.

Ili demokrasia ya kweli iwepo ni muhimu kutenga kabisa shughuli au kazi na wajibu wa serikali mbali na ule wa chama tawala. Hili linawezekana linataka tu kutambua kuwa chama tawala ni sawa na chama mbadala kinginecho chochote ambacho nacho pia siku moja kinaweza kuwa chama tawala. Usawa huu unawalinda wote kwa kuhakikisha kuwa hakuna anayepora nguvu na mamlaka zaidi ya yale ya kuwa chama mara anapopewa kuongoza serikali. Aghalabu hili husaulika sana na vile vyama vinavyodhani vitakaa madarakani milele.

Lile linaloitwa BARAZA LA MAPINDUZI visiwani Unguja na Pemba kwa sasa ndio tishio kubwa kuliko kitu kingine chochote kwa demokrasia na hususan huko visiwani.

Baraza hilo ambalo ni taasisi iliyopitwa na wakati linaendelea kuwepo bila kujua wajibu wake siasa za sasa za nchi. Limeendelea kuishi katika ukale na kuongoza kutokana na historia badala ya kuongoza kulingana na visheni na misheni mpya katika mfumo wa vyama vingi. Zanzibar ambayo ina nafasi kubwa ya kushindana na nchi kama zile za UAE ikiwemo Dubai, Sharijah, Bahrain na kadhalika leo inakwaza kutokana na siasa za dhuluma na uonevu zinazoendeshwa visiwani humo na hasa zile zinazonuia kumnyang'anya mtu haki zake za kikatiba.

Ni dhahiri kwamba, baraza hilo ni kikwazo kwa mabadiliko ya kweli na ya dhati yanayoweza kuwa chachu muhimu ya kuwaondoa Wazanzibari wote kutokana na udhalili na uhitaji wao karibu katika kila nyanja ya maisha. Na sio hilo tu vijana wengi wa Kizanzibari ambao leo wanakwepa nchi yao watakuwa na kila sababu ya kurudi au kwa namna moja au nyingine kuchangia vitu vya maana katika maendeleo ya nchi mama yao.

Kwa kurubuni, kutapeli na kudhulumu haki za baadhi ya wanajamii uongozi uliopo hauonyeshi ujanja bali upofu na uziwi juu ya kule dunia inakoelekea siku hizi.

Ikumbukwe kwamba, unaweza kubabaisha kundi fulani la watu leo na kesho, lakini huwezi kubabaisha makundi yote ya watu wakati wote na unafiki na uzandiki wako usijulikane. Na aghalabu hata yule unayemtuma kudhulumu anaweza akawa si wako ila kwa kukuogopa anatekeleza amri ya kafiri apate mradi wake. Na kwa siasa hizi ni rahisi kujikuta umezungukwa na wanafiki kuliko wacha Mungu na wapenda utu na haki za binadamu.

Matokeo ya hili ni kuwa na wakubwa wanaovunja sheria, lakini ukawalinda kutokana na upofu na uziwi ulio nao.

Hakuna binadamu mwenye akili zake timamu na uwezo wa kuleta mabadiliko yeye mwenyewe anayeweza kukubali dhuluma na mabavu siku zote. Iko siku atajibu. Na siku hiyo isije ikawa ya kusaga meno na usononi usio na mwisho.

Hakuna anayekubali siasa za kurudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kama ni motokari sasa watu watakuwekea mawe usishuke zaidi ya hapo ulipoteremka ukirudi nyuma.

Unafiki mara nyingi ni dalili za uongozi dhaifu usio na dira ya kule unakoweza kuwafikisha wanaoongozwa. Katika kutapatapa na kuhangaika, huishia kuvuruga na kuchafua na hivyo kuwatia wananchi umaskini na ukiwa zaidi.

Maendeleo ya nchi hayawezi kamwe kuletwa na ubinafsi, choyo, jeuri, kiburi, ujibari na dharau kama hiyo ndio tabia ya viongozi. Katika dunia hii hii imewahi kutokea utawala wa wezi katika nchi fulani pale wananchi walipodanganyika na walipojisahau na kushindwa kutimiza wajibu wao. Ni dhahiri pia katika miaka hii tunaweza kushuhudia uongozi wa wahuni, waongo, wababaishaji na hata watu wajinga pindi nasi tutakapojisahau na kudhani kwamba kila mtu anaweza kuwa kiongozi.

Kikwazo kingine kikubwa kwa demokrasia ni Ujinga wa watu juu ya Demokrasia Vijijini.
Uchumi na siasa zetu zimekaa kwa namna ambayo wananchi vijijini bado kabisa kujua faida na manufaa ya mfumo wa vyama vingi. Walioko madarakani wametumia fursa hii kuonesha tu kasoro na hasara za mfumo wa vyama vingi. Na kutokana na kiwango chao cha elimu na kukosa huduma muhimu za mawasiliano kama vile magazeti wanayomudu kununua, redio na televisheni basi wanakuwa na uwezo duni wa kuchambua na kutathmini wanayoambiwa na viongozi wapita njia au wale wa kwao vijijini.

Katika hili ni dhahiri ipo haja ya kuweka mkakati wa Elimu na njia za kufikisha elimu kwa wananchi vijijini wakati wote, ili wawe wanaendelea kufunguka macho na masikio juu ya manufaa ya demokrasia katika maisha yao ya kila siku.

Barua-pepe: sammy.makilla@columnist.com

No comments:

Post a Comment