NIMEKUWA nikifuatilia sakata la mikopo kwa wanafunzi hapa nchini kwa muda sasa.
Majumuisho yangu yasiyo rasmi ni pamoja na kwamba taasisi iliyopo, muundo uliyo nayo, mifumo iliyopo, mipango iliyopo, taratibu zinazofuatwa-vyote vimeanzishwa kwa makosa na visingestahili kuwepo.
Serikali iliyopo madarakani kwa sababu ambazo inazijua yenyewe ilianzisha bodi ya mikopo ili isaidie kitu kingine lakini sio kuwasaidia wanafunzi wanaohitaji mikopo.
Wimbo wa serikali inatakiwa kujitoa kwenye masuala ya uchumi na biashara uliishia katikati, maana ulistahili kuendelea kwa kubainisha pia serikali inatakiwa kujitoa kwenye masuala yote ya kifedha na mikopo isiyoihusu serikali moja kwa moja.
Kinachoendelea hivi sasa ni kwamba serikali imejiingiza katika sekta ya Benki na mikopo bila kuwa na uwezo, vifaa, rasilimali watu,utaalamu wa kuendesha kwa makini na kibiashara na kwa faida shughuli ya mikopo kwa wanafunzi nchini. Upo uwezekano mkubwa kwamba hapo baadaye serikali italazimika kufuta mikopo yote vitabuni mwake kwani itakuwa ni mikopo mibovu.
Waliostahili kuifanya kazi hii walistahili kuwa benki mbalimbali nchini kwa ushirikiano na Mamlaka ya Kodi nchini (TRA), chama cha Waajiri nchini (ATE), chama kikuu cha wafanyakazi nchini (TFTU), mashirika ya hifadhi ya wafanyakazi mbalimbali nchini, makampuni mbalimbali ya bima nchini na waajiri waliopo na waajiri tarajiwa nchini.
Kilichotakiwa kufanyika ili serikali isijiingize katika matatizo, ili wajanja wachache wasitumie mwanya huo kujinufaisha wao wenyewe na jamaa zao na hali kadhalika wanafunzi na wazazi wao wasisumbuke ilikuwa ni kuvipa dhima vyombo hivyo kuanzisha KADI YA KREDITI kwa wanafunzi mbalimbali watarajiwa kwa namna ambayo ingelipunguza urasimu; umangimeza; kujuana, yaani, huyu mtoto wa nani na yule wa nani; ubabaishaji; usumbufu; matumizi ya fomu na makaratasi ambayo ni rahisi kupotea na wakati huo huo kuwezesha kuwaingiza wakopaji katika mifumo ya kompyuta ya serikali, benki husika, taasisi mbalimbali ikiwemo TRA na Mkaguzi Mkuu wa serikali na mkaguzi wa mikopo ya wanafunzi (kama yupo) kwa sababu za kiudhibiti na ufuatiliaji kuanzia mkopo unapochukuliwa hadi unapolipwa.
Nitatoa mfano,CRDB Benki kwa ruksa ya serikali inanunua dhamana za serikali (government bonds au treasury bills) toka hazina kwa kiasi cha mikopo inayohitajika na wanafunzi. Bila kubagua wanafunzi wote wanaoingia kwenye vyuo vya juu wanapewa krediti kadi ya CRDB Bank toka kitengo cha Mikopo Maalum kwa Wanafunzi kitakachokuwa kinajitegemea ndani ya benki hiyo. Ikumbukwe hii ni benki pekee ya wazawa nchi ambayo tunastahili kuibeba kwa hali na mali.
Benki hii kwa kushirikiana na taasisi husika haitafanya kazi hii bure. Italipwa. Na malipo yenyewe yatatokana na kuendesha shughuli nzima ya mikopo kwa wanafunzi kibiasharra kati ya benki na serikali kwa upande mmoja; na kwa upande wa pili kama huduma kati yake na wanafunzi wa vyuo vya juu waliopo na watarajiwa.
Kwa maneno mengine nia ya serikali kutoa huduma ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya juu itatimia kwa benki hiyo kuisaidia serikali katika jukumu lake.
Na kwa upande mwingine benki na taasisi ya fedha husika kwa kukabidhiwa kazi hiyo na kulipwa na serikali itakuwa imerejeshewa kufanya kile ambacho kwa kweli ndiyo kazi zake za kila siku. Wote kwa namna hii wataibuka ni washindi, ingawa serikali itakuwa mshindi zaidi kwa maana sasa itaondokana na aibu ya kuzodolewa kila siku na wazazi na wanafunzi kuhusu suala hili la mikopo kwa wanafunzi.
Benki tofauti na serikali kwa kiasi fulani, itakuwa na kumbukumbu zote za kila mkopo inayouhudumia na mkopaji na jinsi ya kumfuatilia toka mwanzo mpaka mwisho.
Kwa kushirikiana na TRA, mkaguzi mkuu wa serikali na mkaguzi wa elimu ya juu, benki itawatambua wanaostahili kukopa na wasiostahili kukopa. Wasiostahili kukopa watabebeshwa riba kubwa zaidi na muda wao kulipa kuwa mfupi zaidi, na wanaostahili kukopa riba ndogo na kupewa muda mrefu zaidi kulipa deni lao.
Jukumu la kuhudumia mkopo huo sasa halitakuwa tena la serikali bali la mwanafunzi na mzazi wake au mlezi wake wakishirikiana na benki husika. Akili au mkono mtu katika suala zima utakuwa na fursa ndogo sana ya kuharibu nia hii nzuri ya serikali kwa watu wake.
Kwa wasiojua, kadi ya krediti ni kadi kama ilivyo Tembo Card ya CRDB Bank au nyinginezo kama hii ambayo badala ya kuwa na fedha za mwenye kadi, ni benki husika inayomwekea kiwango fulani cha fedha anazoweza kutumia kama mkopo kwa shughuli zake binafsi ili mradi tu havuki ukomo aliowekewa (maana kadi yenyewe haitamruhusu kufanza hivyo). Kama zilivyo kadi nyingine kadi hii ya krediti inaweka kumbukumbu zote muhimu kwa njia ya kistaarabu na kwa namna ambayo sio rahisi kumbukumbu hizo kupotea. Kadi ya krediti itamruhusu mwanafunzi kulipia tuisheni au gharama za mafunzo; vitabu; mitihani; malazi; chakula; afya na tiba; usafiri; utafiti; mafunzo kwa vitendo na majukumu mengine mbalimbali ya kiuanafunzi.
Ili kuwawezesha wanafunzi kutumia vyema na ipasavyo hizi Kadi za Krediti CRDB Benki itaendesha mafunzo kwa kushirikiana na wahusika wengine kwa wanafunzi/ wakopaji wote. Baada ya hapo itakuwa ni mtihani kwa mtumiaji mwenyewe kuitumia kadi hiyo ya krediti kwa namna ambayo itampunguzia deni laki huko baadaye na hata kumnufaisha wakati wa masomo kwa kumuwezesha kuwa mjasiriamali na mtu anayejiajiri hata kabla hajamaliza chuo.
Wahisani au wafadhili wanaweza kukaribishwa ili wachangie kupunguza gharama za mikopo hiyo na kuwawezesha wanafunzi wanaostahili kukopa kutokulipa riba yoyote.
Katika miaka hii ni rahisi sana kuwa na viongozi ambao uwezo wao wa uamuzi, uchambuzi, uchaguzi, uteuzi na utekelezaji sahili na sahihi ni dhaifu kuliko wa baadhi ya wale wanaowaongoza. Kwa hiyo ni muhimu pale inapoonekana katika jambo au kazi fulani ambayo inawahusu raia walio wengi kujitokeza kwa viongozi zaidi ya viongozi ili kurekebisha mambo.
Mipango, utaratibu na utekelezaji mzima wa suala la mikopo kwa wanafunzi sio tu vinaonesha walakini mkubwa lakini kunaashiria dhuluma, ujanja, kutorejeshwa kabisa mikopo na matatizo yasiyo na mwisho. Ni kwa sababu hii ndio maana ninapendekeza kwamba shirika la Hakielimu liingilie kati ili kubadili mustakabali wa jambo lenyewe. Hata kama tumeanza vibaya jambo lililo muhimu zaidi ni kumaliza jambo lenyewe kwa kupatikana haki kwa wale wote wanaostahili haki, ikiwemo jamii ya walipa kodi nchini.
Hakielimu inaweza kuingilia kati kwa kujitolea kuanzisha kazi ya kuundwa makundi mbalimbali ya washikadau katika elimu na kisha kuwasapoti katika kurasimisha uundwaji na kuwepo kwa makundi hayo na pia mikutano yao ya awali.
Mathalni, tuna maprofesa na walimu wastaafu wengi tu ambao wakiwezeshwa wanaweza kuzungumzia mengi mazuri tu kuhusu utekelezaji wa masuala mbalimbali ya elimu hapa nchini kwa sekta ya umma na sekta binafsi. Makundi mengine ni pamoja na mainspekta wastaafu wa elimu, washauri na watafiti katika masuala ya elimu na mafunzo, waandishi wa masuala ya elimu na mafunzo, wakuu wa vyuo na walimu wakuu wastaafu; watumishi wa wizara ya elimu wastaafu; viongozi katika vyuo vikuu, vyuo vya kawaida, shule za sekondari, shule za msingi na wamiliki wa shule na vyuo mbalimbali.
Maamuzi mengi ambayo yanaishia kuwa bomu kwa kufanywa kidikteta na kwa maslahi ya watu au taasisi fulani sasa yatapatiwa changamoto na haitakuwa rahisi siku za mbele kuwa na maamuzi mengi mabovu katika elimu na taasisi za elimu kama ilivyo sasa.
Hasara za mfumo uliopo hivi sasa ni pamoja na: kuwepo urasimu na umangimeza unaoharibu zaidi ya kutengeneza; dhuluma na upendeleo katika utoaji mkopo; kuiongezea serikali gharama za uendeshaji na utoaji mikopo; unadra wa mikopo kulipwa kwa wakati; kutokuwepo mbeba dhamnana inayotolewa a serikali; kuzinyima benki na taasisi za fedha fursa za kiuchumi inazostahili; kuwa na watu wanaoajiriwa na kulipwa mishahara bila sababu ya msingi; kufedheheka serikali mbele ya macho ya wannanchi wake na dunia nzima; kuruhusu kulipwa mikopo wasiostahili na wanaostahili kutokulipwa na kadhalika.
Faida za kadi za krediti ni pamoja na kuondoa: matatizo yanayoletwa na akili na mkono wa binadamu; kuondoa urasimu; ;kuondoa upendeleo na dhuluma; kurahisisha zoezi zima la kukopa na kulipa mkopo; kudhibti wadaiwa na malipo husika; kukuza uchumi kwa kuongeza mzunguko wa fedha; kuhamisha jukumu la kujisimamia kifedha kwa wazazi na wanafunzi wenyewe; kuondoa gharama kwa kuwepo na taasisi na majengo maalum kwa shughuli hiyo na kuongeza haki na usawa katika medani ya maisha ya kitaifa nchini.
Friday, September 16, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment