Kuna kosa la kihistoria ambalo lilikwishatokea na linaloendelea kutokea kwa sababu serikali imeshindwa hadi wa leo kufanya tathmini halisi, halali na ya haki ya watu na utamaduni wao, mtaji wao wa kijamii, vijiji vyao na ardhi na mali asili walizonazo.
Aidha serikali imepindua kinyemela madaraka na mamlaka ya wananchi wanayostahili kuwa nayo kwa mujibu wa katiba juu ya uongozi na maamuzi ya nchi, ardhi na mali asili zao na kujiweka juu kwenye nafasi ya muamuzi mkuu na mmiliki wa ardhi badala ya wananchi kuwa ndio wanaofanya maamuzi na wanaomiliki kihalali ardhi na rasilimali nyinginezo katika nchi hii, kiasi kwamba serikali inaweza kuamua wakati wowote kuwapora wananchi ardhi yao na wananchi walipwe kidunchu tu au sawa na kutokulipwa na wakati mwingine hata kuporwa kimaguvu ardhi na mali asili zao nyingine na wale wanaoitwa wawakilishi wa serikali.
Isitoshe, ardhi na sekta ya kilimo ndiyo inayowagusa wananchi walio wengi Tanzania na maamuzi katika eneo hili ni lazima yawe na manufaa kwa wanavijiji walio wengi na sio wanamji na wawekezaji wawili watatu wa ndani na nje.
Kihistoria, haikanushiki pia kwamba japo katiba ya nchi hii inataka uwiano na ulinganifu katika maendeleo, hali llivyo leo ni kwamba bado watu wa mjini na sehemu za mijini zimekuwa zikipewa upendeleo mkubwa kuliko watu wa vijijini na maeneo ya vijijini. Uvumilivu, subira na ukawaida wa watu wa vijijini umechangia sana katika hili pengine kwa wao kuonekana wanaoridhika kirahisi au mabwege wasioweza kuwafanya wakubwa lolote. Lakini kuendelea na hali hii sio tu ni dhuluma na uonevu kwa watu wa
vijijini bali ni kukosa kuona mbali na mbele na kuamini kuwa siku zote watu wa vijijini watakuwa wavumilivu, wenye subira na mabwege na mafala kuhusu haki zao, matakwa na matarajio yao.
Hali kadhalika, matatizo mengi yanayotokea katika miji yetu hapa nchini hivi leo yanasababishwa na upendeleo huu wa miji dhidi ya vijiji iwe ni katika wingi wa watu wasiobebeka mjini, wizi, wingi wa magari na foleni, kukosekana huduma muhimu mijini na kadhalika.
Ndio maana tunasema kwamba bila ya sera ya Kilimo Kwanza na Uwekezaji katika kilimo kumnufaisha moja kwa moja mwanakijiji basi mapinduzi ya kilimo nchini yatakuwa ni sawa na kazi ya kupanda kilima kirefu chenye majabali yenye ncha kali na mijoka iliyojificha.
Katika siku za hivi karibuni kilimo kwanza ambayo ni sera iliyoanza siku nyingi lakini imeendelea kubadilishwa majina kama vile yapo matarajio yasiyokufa kwamba eti jina ndilo linaloweza kuifanya ifanikiwe imekuwa ikipigia debe nchi za nje kupewa ardhi ya Watanzania kwa ajili ya kilimo kama vile hakuna Watanzania wanaoweza kuingia kwenye ubia na wawekezaji toka nje kwa faida ya pande zote zinazohusika.
Nchi zinazozungumziwa sana ni ile ya Korea Kusini, Iran, Uturuki na zile za Kiarabu.
NInaamini kuzipa nchi hizi za nje ardhi ya Watanzania moja kwa moja kama vile ardhi hiyo haina wamiliki wake wa asili na haina thamani yoyote na Watanzania wahusika hawastahili wao wenyewe kufanya maamuzi juu ya ardhi yao ni kukiuka katiba na kwamba mamlaka na madaraka juu ya maamuzi ya matumizi ya rasilimali za nchi hii inayo wananchi wenyewe na serikali ni watendaji na watekelezaji wa maamuzi ya wananchi na sio vinginevyo. Kwa kila hali serikali na viongozi wake wamepituka uwezo ambao tumekasimu kwao.
Kutokujua au ujinga wa wananchi kuhusu haki zao katika ardhi, sio tu kiumilikaji na kiunufaikaji, ila katika kubwa zaidi kwamba wao ndio wanaostahili kuwa wamiliki wa rasilimali zao na maamuzi yote juu ya matumizi ya ardhi yanastahili kufanywa na jamii zao ndiko kulikochangia wajanja wachache kujinufaisha kwa kuwatumikia wakuu wa mikoa na wilaya sio tu kujimegea ardhi katika maeneo wasiyo na nasaba au ukuruba nayo, bali pia kuwauzia wawekezaji wao wakanufaika na wananchi wakaendelea kuwa maskini japo rasilimali yao imeuzwa na walistahili kunufaika na mauzo hayo.
Hakuna anayepinga nchi, kampuni na watu kutoka nje kuwekeza katika kilimo nchini. Tunachokipinga ni uwekezaji unaofanywa kwa namna ambayo kilimo vijijini mwetu na wakulima katika vijiji vyetu hawatasaidiwa kubadilika kitu na uwekezaji kama huo.
Uwekezaji tunaostahili kuupigia debe ni ule ambao nchi fulani duniani au kampuni fulani au mtu fulani anayekuja kuwekeza Tanzania ANAINGIA UBIA na mojawapo ya vijiji vyetu ili kuitumia ardhi ya kijiji kulima, kufuga, kuvua au kufanza mradi wowote ule huku wananchi wa kijiji husika na mwekezaji mwenyewe wakivuna na kugawana kinachopatikana kwa namna watakayokubaliana wenyewe kwa manufaa ya wote.
Kwa mtaji huu mwanakijiji atakuwa sio tu na soko la nguvu kazi yake; bali pia atanufaika na soko la nje, elimu, ujuzi na teknolojia atakayoleta mwekezaji huku wakizalisha mali ambayo itachangia kunyanyua hali ya maisha ya wanavijiji wahusika na kipato cha mwekezaji na nchi kadhalika.
Kabla ya nchi- wawekezaji kuruhusiwa kuwekeza katika kilimo hapa nchini ni muhimu benki ya wakulima iwe tayari imeanzishwa. Fedha zinazolipwa na nchi, kampuni na watu wanaowekeza katika kilimo zitawekwa katika benki hii zikigawanywa katika mafungu ya hisa za mwekezaji na kiasi fulani kutumika kuendeleza miundo mbinu na huduma muhimu vijijini na sio vinginevyo. Tathmini halali, halisi na haki ya thamani ya mtaji watu wa kijiji husika, utamaduni na urithi wao, ardhi yao, misitu yao na mali asili zao nyingine ikishafanyika Benki ya Wakulima itatoa hati ya uwekezaji au mkopo inayolingana na thamani ya rasilimali za kijiji. Thamani hii itakayokuwa katika shilingi ya Kitanzania itakuwa ni sehemu ya uwekezaji wa kijiji husika wenye thamani sawa na fedha zilizochangwa na mwekezaji katika kijiji chao.
Tunapaswa kukubali kuwa hii ndiyo njia pekee ya vijiji vyetu kulala maskini na kuamka matajiri kesho yake. Na kwamba serikali inawjibika kuwezesha na kurahisisha hili, kwani haina namna yoyote nyingine inayoweza kuondoa tofauti kati ya vijiji na miji na kupunguza matatizo ya miji yanayotokana na kusahaulika kimaendeleo kwa vijiji ila tu kwa mkakati na mbinu hii. Katika muktadha uliopo ni muhimu viongozi wetu wabadilike kimawazo ili nchi iweze kuendelea kijamii na kiuchumi. Mustakabali wa ustawi na mafanikio ya vijiji vyetu unategemea hili kuliko kitu kingine chochote duniani.
Hakuna kiongozi wa zamani au leo binafsi ambaye kwa kuwekeza mwenyewe katika kilimo na ufugaji anaweza akatutoa kutoka kwenye dunia ya tatu na kutupandisha hadi ya pili. Ni pale wakulima wote kwa pamoja wanapopewa fursa hii ndio hili litakuwa na nafasi angalau ya kuwezekana.
Sera za MKUKUTA wa I na wa II zimeshindwa kuchangia cha maana katika kuondoa umaskini wa Mtanzania kwa sababu hazikufanikiwa kuainisha kwa usahihi chanzo cha umaskini wetu. Na chanzo hicho sio kingine ila ardhi na mali asili nyingine za Tanzania kutokuwa na thamani halisi, halali na ya haki kiasi cha kuwanufaisha Watanzania kupitia umilikaji wao katika harakati zao za kujikomboa kiuchumi.
Bila umiliki huu, maamuzi na usimamizi wa ardhi na mali asili za wanajamii kufanywa na wananchi wenyewe rasmi haitakuwa rahisi nchi yetu kuondokana na umaskini wa kutupwa kwa walio wengi.
Tathmini ya haki, halisi na halali ikifanyika watu, urithi na utamaduni wao, vijiji vyao, maliasili zao, ardhi na rutuba yake, uoto, maji na ujumla wa mtaji wao wa kijamii ni vitu vyenye thamani sawa na fedha, mashine na mitambo yote itakayoletwa na mwekezaji yoyote yule.
Hii ina maana kwamba vijiji vyetu na jamii zake vina kitu cha thamani au rasilimali ya kuwekeza bila kutoa senti hata moja mfukoni mwao.
Ili kusahihisha kosa hilo la kihistoria hapo juu ninashauri kwamba sio vyema nchi, makampuni na watu kutoka nje kupewa ardhi ya Watanzania moja kwa moja bila ushirikishwaji na ubia wa vijiji na wanavijiji katika uzalishaji na uuzwaji na unufaikaji wa mazao husika.
Ni wataalamu wa tathmini ya mambo husika na sio wanasiasa wanaostahili kuamua kwamba kijiji na wanakijiji fulani kwa ujumla wao wana mali za thamani ya kiasi gani na muwekezaji akishawekeza mgawa wa mapato kutokana na shughuli za kilimo zitakazoendeshwa utakuwa vipi?
Friday, September 16, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment