Saturday, May 7, 2011

Kilimo: Ili tufanikiwe budi kuwa na dhati, waadilifu na wakweli

KATIKA miaka ya 60 tulizungumzia kilimo kuwa uti wa mgongo wa taifa letu; miaka ya 80 tukateta juu ya kila mtu kuwa mkulima na kuusogeza pembeni mgawanyo wa kazi; katika miaka ya 90 tukajusuru kuanzisha mapinduzi ya kijani na chakula kama tatizo; na hivi sasa tunazungumzia juu ya KILIMO KWANZA.Je, kuna lililobadilika? Hapana, maana maneno ni yale yale na kinachohitajika kama kilivyokosekana katika miaka ya nyuma ni dhati ya vitendo na watu kujituma ili kuwezesha lile tutakalo litokee. Vinginevyo soda au bia ni ile ile na kilichobadilika labda ni rangi au umbo la chupa tu. Mambo hayaji kwa kutamani tu, lazima tuyafanyie kazi. Kwa hiyo katika enzi hizi za KILIMO KWANZA, kama hatutafuatia maneno na dhamira yetu kwa vitendo na nguvu za kimtaji, miundombinu, kizana/kiteknolojia na kifedha bado tutarudia papa hapa tulipo hii leo—yaani, nchi kubwa lakini mchango wake katika kilimo kwa dunia mdogo sana.Sikuhudhuria warsha kuhusu mustakabali wa kilimo nchini, lakini hata hivyo ninaamini waliokuwepo watakuwa wamezungumzia mengi mazuri na yanayoweza kuwafaa Watanzania kama yakitekelezwa. Ninaamini, kuwawezesha wakulima hususan kwa kuwa na njia bora na nafuu za usambazaji pembejeo na kuanzishwa kwa Benki ya Wakulima nchini yatakuwa yamepewa uzito unaostahili.Ninaamini pia kilimo kimezungumzwa kwa upana na marefu yake; na kwamba ufugaji wanyama, nyuki, ndege, samaki na uvuvi na viwanda vidogo vidogo vya usindikaji mazao ya kilimo ni mambo yaliyojumuishwa katika mazungumzo hayo.Pamoja na hayo nina wasiwasi kuwa tusiporejea nyuma na kuangalia historia yetu katika kilimo ilikuwaje na nini kilichotufikisha hapa tulipo, tutashindwa kupanga na kutekeleza yale yanayofaa kufanyika na tunaweza tukateleza tena kama ilivyofanyika huko nyuma na kuishia kuangukia pua.Historia yetu katika kilimo inatuonesha tulikuwa hatufanyi vibaya hadi pale tulipotaifisha mashamba miaka kama sita baada ya uhuru na kisha kufuatiwa na mradi wa kuwahamisha watu kutoka maeneo yao ya asili na kuwaweka kando ya barabara au sehemu zilizokuwa hazina rutuba kulinganisha na zile walizotoka.Huko nyuma mila na desturi za makabila yetu mengi yalidhibiti uharibifu wa mazingira ikiwemo kutunza vyanzo vya maji na nishati na kuzilinda maliasili nyingine kama wanyama au misitu au maji ya mito, maziwa au bahari. Aidha, sheria alizotuachia mkoloni na wazee wetu waliozisimamia mara baada ya uhuru zililinda mazingira na zilitulinda sote sio haba. Halmashauri za Maendeleo za Wilaya zilifanya kazi nzuri ambayo hakuna manispaa au halmashauri yoyote ya leo imeweza kuzifanya.Vyama vyetu vya ushirika kabla ya kuingiliwa na siasa vilifanya kazi nzuri ambayo hadi wa leo hakuna ushirika wa kisasa ulioweza kuifanya.Hapakuwa na walanguzi na mkulima alikuwa anahudumiwa na chama chake cha ushirika tangu mahitaji ya msingi hadi pembejeo, mikopo na misaada mbalimbali.Kuna makundi ya vijana kama Uvikiuta la jijini Dar es Salaam yaliyofadhiliwa na watu binafsi na mashirika na yakadhihirisha kuwa vijana wakipata sapoti siku za mwanzo wanaweza kuanzisha na kuendeleza mradi wa kilimo na ukawafaa na kuchangia heshima ya nchi na vijana wake.Wilaya na mikoa ilikuwa inajizatiti katika kilimo cha aina fulani na hivyo kuwafanya wakazi wake kuwa stadi na mabingwa katika kilimo, ufugaji au uvuvi wa aina fulani.Inawezekana kwamba utaifishaji mashamba, ukame, njaa na vita vya Uganda vilichangia katika matatizo yetu kwa kiasi fulani. Lakini ukweli unabaki pale pale 'kukisiasaisha' kilimo kwa hakika ndicho kilichokuwa mhusika mkuu wa kifo cha kilimo Tanzania. Matokeo yake ikawa ni mkulima kupunjwa kipato cha jasho lake huku viongozi wa kupachikwa kwenye ushirika wakawanyonya zaidi kama si kuwaibia na hatima ya yote mkulima wa Tanzania akapoteza kabisa matumaini kwamba kilimo kinaweza kumkomboa au kumnufaisha kwa njia yoyote ile. Kutokana na hayo hapo juu, ninaamini basi kazi yetu ya kwanza kama kweli tuna nia na dhamira ya kukifanya kilimo mkombozi wa Watanzania basi ni lazima kwanza kusahihisha makosa yetu ya huko nyuma na kuhakikisha 'miundo-mbinu' ya sekta mpya ya kilimo inajengwa kwa namna ambayo kweli itamnufaisha mkulima kuliko kunufaisha wanasiasa, walanguzi na watu wengine.Kama mwanafunzi wa masuala ya rasilimali watu ninaamini kabisa kwamba kazi au ajira yoyote inayomnufaisha mtu ina fursa kubwa ya kumuendeleza yeye na nchi kuliko ajira ambayo haikidhi mahitaji ya yule anayeshughulika nayo.

Sekta ya kilimo hadi leo inachukuliwa kama ni sekta ya maskini, watu wasiosoma na waliokosa ajira katika sekta zingine. Kazi kubwa ya kwanza kwa serikali, chama tawala na vyama mbadala nionavyo mimi itakuwa ni kubadili mtazamo huu wa watu. Ni lazima Watanzania wakiheshimu na kukienzi kilimo na waamini kuwa ni ajira kama ajira zingine.Baada ya mabadiliko hayo ya kifikira basi itakuwa ni rahisi kuifufua sekta hiyo na ikaanza kurudisha upya imani ya watu na hivyo kilimo kuanza kuchangia zaidi katika maendeleo ya nchi na watu wake.Kabla ya uchumi kuingiliwa na siasa zisizo na mbele wala nyuma mambo yetu mengi yalikwenda vizuri.

Ni kweli sekta kama za madini na utalii zinakuwa haraka sana lakini bado kwa mapana na marefu hata sekta hizo nazo kukua kwake kutetegemea sana mafanikio ya nchi katika uzalishaji mazao ya biashara na kilimo kwa upande mmoja na mazingira endelevu kwa upande mwingine. Kama hivyo ndivyo, ni rahisi basi kuona kwamba sekta za utalii na madini zinawajibika kukibeba kilimo kwanza kwa namna moja au nyingine.

Ili mradi sasa tumezinduka na kugundua makosa tuliyoyafanya huko nyuma basi tusione aibu kuondokana na maadili, sera, tabia, mifumo na taratibu mbalimbali ambazo hazijengi bali zinazobomoa utu na kujiamini kwetu kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii.
Mathalani, kuna sera ya ushirika wa wazalishaji mali ikiwemo kilimo. Hii ikiwezeshwa na serikali na ushirika huo ukawa wa kisasa na unaojiendesha wenyewe unaweza ukawa sawasawa na kampuni yoyote hapa nchini. Maana wanachama wa ushirika huo watalima pamoja, watauza ndani na nje kwa bei nzuri na watasimamia fedha zao wenyewe kupitia benki ya wakulima tarajiwa.Ninashauri pia kila wilaya na mkoa uwe na muda wa kuandaa mpango wake wa kimkakati wa kilimo na viwanda vya kilimo (District and Regional Agriculture and Agro-Industry Strategic Plan) ili kujali tofauti zilizopo kati ya wilaya na wilaya au mkoa na mkoa na hivyo kuwawezesha wakazi wa wilaya au mkoa husika kujikita kwenye eneo la kilimo litakalolipa haraka zaidi na kuwa chachu ya kuendeleza baadaye maendeleo mengine ya kilimo, ufugaji na uvuvi.

Ni muhimu kuangalia na kuainisha pia ni nini utakuwa mchango wa wizara, mkoa na wilaya katika kilimo. Vilevile wabunge, wenyeviti wa vijiji, serikali za mitaa na madiwani watakuwa na majukumu gani katika KILIMO KWANZA.

Na kubwa zaidi ni mifumo na taratibu rahisi za kutatua matatizo ya wakulima na kilimo kwa wakati ili nchi nzima iwe kama timu moja inayocheza kama timu na sio kila mtu na lwake.

Mipango na mikakati ikifanyika ipasavyo itatujulisha nini kinastahili kufanyiwa majaribio wapi na kupandwa wapi. Haya yatapaswa yaoanishwe na mahitaji ya utandawazi ambayo sasa yana mwelekeo wa kupambana na yale yote yanayochafua hali ya hewa na mazingira kwa ujumla. Mwisho wa siku, wakazi wa kila eneo wakishirikishwa wanaweza kutoa majibu mwafaka zaidi kwa changamoto zote zitakazoletwa na KILIMO KWANZA. Vitabu mbalimbali vilivyoandikwa na Mwalimu, TANU na CCM vipitiwe na kuchapishwa upya na kila kinachofaa kitafutiwe mahala katika azimio la KILIMO KWANZA.

Kama kuna jambo Nyerere alilosikitika kulifanya basi ni kushindwa kuifanya Tanzania ifanikiwe katika mapinduzi ya kilimo. Baba wa Taifa kwa maneno na vitendo vyake inaonesha dhahiri angehesabu katimiza wajibu wake kama nchi hii ingelikuwa nchi ya kijani. Katuachia sisi changamoto hiyo. Ili kumuenzi Baba wa Taifa Watanzania tunachotakiwa kukifanikisha ni kuleta mapinduzi hayo ya kilimo haraka iwezekanavyo. Ni kwa faida yetu, manufaa ya kizazi chetu na heshima ya Mtanzania na Mwafrika duniani kwamba naye anaweza kujilisha na asitegemee misaada ya chakula kutoka nje.

Sera ya Kilimo Kwanza aidha lazima iwe ni ya kazi kwa maarifa na zana za kisasa na inayozingatia maswali ya elimu isiyo na mwisho, utafiti endelevu na maendeleo ya rasilimali watu wakati wote.

Msiba mkubwa ambao Tanzania unao ni ule wa wanasiasa kujifanya wakubwa wa kila jambo na wanaojua kila kitu. Hivi leo mabwana na mabibi shamba vijijini hawana tofauti na wanavijiji wengine katika umasikini wao. Mabwana na mabibi shamba hawaendi vijijini ili kusaidia kuwatoa wanavijiji kwenye umaskini bali wao pia kutumbukia katika lindi la umaskini. Maana, ukweli ni kuwa elimu na maarifa yao peke yake havitoshi. Lazima mambo mengine muhimu katika kufanikisha kilimo nchini yafanyike. Lazima pawe na ofisi na shamba la kujifunzia, zana mbalimbali na sio tena jembe la mkono, gereji, madarasa ya kilimo, kitengo cha mbolea, nafaka na mali ghafi nyinginezo.

Lazima bwana shamba awe na usafiri wa kuaminika. Leo magari ya Wizara husika ni mengi mjini kuliko mashambani. Wakati toka mwanzo wizara yenyewe ilistahili kuwa vijijini.

Wakati mwingine hata elimu na maarifa mabwana shamba waliyonayo inakuwa imepitwa na wakati. Yaani, kwa maneno mengine hakuna bwana shamba anayestahili kumaliza shule. Na vyuo vikuu na vya kawaida tulivyoanzisha vinastahili kubeba mzigo huu wa kufikisha elimu na tafiti mpya kwa mabwana shamba na wakulima vijijini kwa njia rahisi ikiwemo matumizi ya teknohama.

Isitoshe upo umuhimu wa kuwepo kwa ushirika wa kweli wa uzalishaji mali katika kilimo unaosaidiwa na Benki ambayo kazi yake kubwa ni kuendeleza kilimo na uzalishaji chakula nchini.

*** Mwalimu wangu mmoja, hayati Prof. Joshua Nkululi aliniusia kwamba kuna mambo mengine yanatakiwa uweke malengo ya juu kabisa ili hata ukianguka ufikie angalau wastani.

Mathalani, ni kosa kuweka lengo letu la kilimo kuwa kujilisha badala ya kuwa ni kuzalisha mazao kabakaba kwa ajili ya uuzaji iwe ndani au nje ya nchi. Kwa kuwa mtazamo huu unaanza kwa kulitazama soko huku ikibainika fika kwamba pamoja na kuuza kinachozalishwa kwenye masoko ya ndani na nje bado kiasi cha kutosha kitapatikana kwa matumizi yetu wenyewe. Na ili mradi tuna utaratibu mzuri wa kuhifadhi chakula cha kutosha kwa miaka kadhaa dharura inapotokea haitatubabaisha sana.

Kwa hiyo tabia ya kuwasakama wakulima wanapouza mazao mikoa au nchi jirani na wanapotumia nafaka kwa uzalishaji pombe mimi siioni kama ni busara maana unawakwaza watu kimasoko na kibiashara. Ukihofia kufa njaa kwa kuwekeza au kufanya kitu fulani katika maisha sikuzote hutofanikiwa katika dunia hii. Uuzaji wa chakula nchini na masoko yake yawe huru kama vile uuzaji maji ya Bakhressa ulivyo au uuzaji petroli ya Oilcom ulivyo. Hakuna anayemkumbusha Bakhressa kubakia na maji ya kutosha na hakuna anayewakumbusha kina Islam na ndugu zake kubakia na petroli ya kutosha magari yao.

Kubwa zaidi ni hili la uwezo wetu sisi wenyewe wa kutengeneza mashine za msingi za kilimo kwa kutumia wahandisi wazawa na wale wasio na kazi huko Romania, Hungary, Serbia, Croatia na nchi kadhaa za Russia ya zamani.

Ni aibu miaka 50 baada ya uhuru Tanzania kushindwa kuwa angalau na trekta lake linalotengenezwa na teknolojia na mafundi wa kuazima na hasa kama trekta hilo ni kapawatila tu.

Kwa maneno, mengine, kilimo kwanza kitakuwa kilimo mwisho kama tusipokuwa na zana na mashine zetu wenyewe za kilimo. Na pengine hii kwa sasa ndio iwe eneo muhimu kuliko lote la uzalishaji viwandani kwa nchi yetu. Azma ikiwa kujitosheleza kwa zana za kisasa za kilimo ambazo mkulima wa kawaida atamudu kuzinunua. Na kisha kutengneza zana na mashine hizo kwa wingi ili kuuza kwa wenzetu Afrika na nchi zinazoendelea. Mengine tukiyaweka pembeni kwa muda, hili litatuhakikishia kukua uchumi endelevu unaotegemea teknolojia yetu wenyewe na hilo litasababisha sisi pia kujikomboa katika teknolojia na ufundi mwingine muhimu ukiwa pia vifaa na mashine tunavyostahili kuwa navyo kwa uchimbaji wa madini mbalimbali sisi wenyewe kwa kutumia teknolojia yetu au ya kuazima.

Tukifia hapo tutafikia kile kinachoitwa 'takeoff' kiuchumi au kwa maneno mengine gari litafika kileleni na upande wa pili ukiwa mteremko tutaviringika kirahisi tu hadi kwenye malengo yetu mengine ya kimaendeleo.

Aidha, wakati umefika wa chama tawala na serikali yake kuwachukulia wakulima wetu kama na wao pia ni wawekezaji. Tayari wana ardhi ambayo ina thamani na pengine mazao kadhaa ya kudumu humo. Hii inatosha kabisa kwa serikali kuziaminisha benki katika kutoa mikopo ifaayo kwa wakulima hatua kwa hatua ili ifikie mahala ikawa wazi kuwa wakulima wa Tanzania wanakopesheka. Wakikopa wanalipa. Fumba na kufumbua tutamtoa mkulima wa KItanzania toka kwenye umaskini, naye akapata ziada ya kuingia katika shughuli nyingine za kiuchumi na kuwaachia watu wachache tu kushughulika na sekta ya kilimo na bado taifa. likajiendesha kichakula na kibiashara.

No comments:

Post a Comment