BILA shaka toka nchi hii ianze kuukumbatia ubepari, soko huria na utandawazi tumeanza kuona mabadiliko makubwa sana katika tabia za watoto na vijana wa KItanzania.
Taifa la watu waliokuwa wema, wapole, wenye huruma, heshima na adabu limeanza kuwa kitu tofauti kabisa. Na hakuna anayeonekana kutaka kukemea huku kukengeuka. Sio vyombo vyetu vya habari au dini zetu wala sio serikali isiyokuwa na dini.
Aghalabu wengi hushtuka kutokana na utovu wa adabu, ukosefu wa heshima na hulka za kiajabuajabu ambazo inadaiwa ni kwenda na wakati.
Kwa namna fulani hali hii inatokana na kukua kwa kasi kwa ubinafsi na watu kujiamini kuwa wanaweza wakajitosheleza kwa kila kitu na wakawalea watoto wao bila msaada wa mtu mwingine.
Matokeo yake hivi leo sio tu kwamba watoto hao wanakuwa kero na maudhi kwa watu wengine lakini hata kwa wazazi wao wenyewe.
Pengine huu ni wakati muafaka wa kuvuta hatua moja nyuma na kujiuliza kama malezi haya ya leo kweli ndiyo yatakayolifikisha taifa letu pale tunapotaka liende ?
Nina wasiwasi mkubwa kama malezi haya kweli ndiyo yanayowafaa watoto wetu. Na kamwe waoto hawawezi kulaumiwa bali ni wazazi wao, viongozi wao wa dini, jamii yao, wanasiasa wao, na taifa lao.
Wazazi ndio wanaoshika usukani hata kama sio moja kwa moja. Na wao wanapochelea kuikosoa serikali na viongozi wao kwamba wanapeleka upogo kizazi kijacho hawatakuwa na kuwamlaumu ila kujilaumu wenyewe.
Pengine upofu huu unatokana na uchu wa viongozi wa dini kupata waumini ndivyo sivyo ili mradi sadaka inayopatikana ni kubwa na wao wanaishi maisha ya kifahari? Au pengine upofu huu unatokana na kukosa chama huru cha wazazi na viongozi wa wazazi wasio wanasiasa. Au pengine upofu huu unatokana na ubinafsi na tamaa ya kuonekana tofauti na watu wengine.
Potelea mbali sababu iwayo, lakini ukweli unabakia palepale kwamba kauli na vitendo vyetu leo ndivyo vinavyosaidia kurithisha tabia, hulka na mienendo ambayo sisi wazazi tulio wengi tunaonekana kuirithia.
Kauli na vitendo vya mzazi wa Kitanzania leo vimetawaliwa na vinatafiriwa na umimi na ubinafsi wa hali ya juu iwe nyumbani, kazini, njiani au michezoni. Na kiongozi mmoja alilipalilia hili kwa kiasi kikubwa pale alipowaambia Watanzania kuwa: ' Kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe!'
Lakini tunachoshindwa kujua sisi wazazi ni kuwa mtoto huzaliwa hana tabia yenye uhakika. Na tabia ni matokeo ya kuzungukwa na wazazi wake na jamii yake na yale yanayomtokea katika maisha yake. Na kama shamba lako halina magugu (kwa maana huna watoto wenye tabia mbaya) lakini aghalabu utakuwa umezungukwa na mashamba yenye magugu (majirani wenye watoto kisirani) na hivyo hatimaye magugu pia huingia shambani kwako kwa kushtukizia na kwa athari mbaya zaidi. Maana, wanao ni weupe na hawana wanalolijua.
Hebu, tuangalie sampuli kadhaa za wazazi na jinsi wanavyoathiri viongozi wa kesho na keshokutwa. Tuanze na huyu masikini aliyeko barabarani na ana watoto kadhaa. Watoto hao hawaendi shule bali wanamsaidia mzazi wao kazi. Kwa kuwa kazi ya baba au mama ni ombaomba, wanamsaidia kuomba kama mzazi wao. Hebu fikiria wewe mwenyewe je huyu atakuwa Mtanzania wa aina gani akiwa mtu mzima?
Baadhi ya wazzazi tunalia machozi ya mamba. Tunajifanya tuna uchungu sana na mayatima. Tunaanzisha vituo vya kulea mayatima. Lakini ukiangalia kwa undani vituo hivyo havina dhati ya kuwalea mayatima hao bali kumpatia mwenye kituo utajiri wa haraka haraka. Hivi kweli watoto waliotoka katika mateso ya uyatima au mama wa kambo wakakutana na kadhia kama hii watakuwa na utu gani. Na kwa nini yatima alelewe kwenye kituo. Kuna yatima wangapi Tanzania? HIvi haiwezekani kwa watu wenye uwezo kuwachukua na kuwalea mayatima hawa majumbani mwao ili wawe na maisha yaliyofanana na ya watoto wenye wazazi wawili? Hatujui dini yako inasemaje, wlala thawabu utakazopata au madhambi utakayofutiwa, lakini kitendo hiki kitahakikisha kuwepo kwa taifa bora zaidi kuliko hali ikiwa kinyume cha hivyo.
Aina nyingine ya wazazi ni wale wa tabaka la chini kimaisha. Wazazi hawa aidha wanafanya kazi au wana biashara fulani au ni wakulima. Lakini kutokana na ugumu wa maisha baba anaamua kuwa mlevi, wengine wanazidisha starehe ili wasahau maumivu na wengine wanakwepa majukumu yao kama wazazi. Si uongo, ulevi noma. Familia nyingi zinasambaratika kutokana na baba na balaa zaidi hata mama kuwa walevi. Je, matangazo kwenye redio na televisheni yanatosha kuwafanya wazazi hawa wapunguze idadi ya sigara na chupa za bia wanazosaidia serikali kuongeza bajeti yake?
Umewahi kukutana na mtoto wa mlevi au baba asiyejua majukumu yake kwa familia yake ? Nguo chakavu na chafu, kapauka (hana mafuta ya kujipaka), midomo mikavu (hakupata kifungua kinywa asubuhi), hana begi labda mfuko wa marlboro na kadhalika. Ikionesha dalili kwamba hakuna kitu kinachoitwa ustawi wa jamii hapa nchini na kama kipo basi hakifanyi kazi. Kimekufa. Je, taasisi hiyo inasaia kujenga chuki, husuda na roho mbaya miongoni mwa watoto kama hawa au inajenga amani na umoja wa kesho?
Kuna wazazi wa lile tabaka la pili ambao juzi na jana walikuwa na hali nzuri kiasi, wana nyumba, gari na wanakula milo 3 kwa siku. Lakini toka peteroli na bei ya vyakula ianze kupaa juu kuliko roketi na shilingi kuzidi kuporomoka maamuzi magumu yanabidi kufanyika. Kuweka gari peteroli na kula ugali kwa matembere au....
La ajabu, katika familia hizi tofauti na wenzetu kwingineko Afrika Mashariki pamoja na jamaa hawa kuwa na intaneti hakuna anayewafundisha wanawe ujasiriamali, ubunifu na uzuzi wa mambo mapya. Tunalea 'Kisukuma' baba linafanya kazi zote na wake na watoto wake kazi yao ni kula tu. Na jinsi mtu anavyolisha watu wengi ndivyo anavyozidi kuwa maarufu.
Lakini ni dhahiri kuwa vijana wa miaka 14 sio watoto tena. Hawa ni watu wanaoweza kufunzwa jinsi ya kushiriki moja au mawili ya faida kwao na wazazi wao leo na kesho. Tunapojenga utegemezi wa kupita kiasi mwishowe ni kuwa na nyumba zinazofanana na zile za Uswahilini pale Kariakoo. Utamkuta baba na mama, watoto wo wa kiume wanne na sita wa kike. Na hao watoto sita wa kike wote wamezalia nyumnbani na wajuku wanalelewa na bibi na babu. Kazi kweli! Uzazi wa namna hii ni chanzo kikubwa cha umasikini wa uzeeni. Na kama serikali ina nia ya kweli ya kuwasaidia wazee basi ianze kwa kuwapunguzia wazazi wa namna hii mzigo kama huu.
Ni wazazi hawa pia wanaotujali kwa kutuletea kizazi kipya na bidhaa zao. IKiwemo muziki wa kuiga au wa kinyani toka Marekani, kuvaa suruali inayoacha nusu ya makalio nje au sketi na vigauni ambavyo vinaacha sentimeta chache tu kuona sehemu nyeti-kwa kisingizio cha kwenda na wakati. Na baba na mama nyumbani wanawaunga mkono watoto wao. Mwisho wa yote humjui mzazi ni nani na mtoto ni yupi. Wote ngoma sawa. Balaa na mikosi ikianza kila mtu anaanza kumlaumu Muumba, maana hata kuomba tena hawajui. Uhuru huu usiokuwa na mipaka sio uhuru unaowasaidia vijana wetu wala taifa letu. Ya ngoswe muachieni ngose. Nina hakika tukiuenzi Uafrika wetu na kutunza adabu na heshima yetu basi tutakuwa na bidhaa bora zaidi na zinakubalika kimataifa kuliko ilivyo sasa. Msaada wa vyombo vya habari katika hili ni muhimu sana.
Halafu, tuna wazazi wa tabaka la tatu au matajiri wakubwa au vizito. Hawa wanaajiri, hawaajiriwi. Wana viwanda, biashara kubwa au shule au vyuo au hospitali na kadhalika. Kutokana na wingi wa mali hata watoto wao wa miaka 10 huchukua magari na kuingia nayo barabarani. Kwa kuwa sina utajiri wa kiasi hicho, labda niulize tu hivi mzazi kumfanya mwanawe aamini utajiri wake ni utajiri wa mwanawe pia kunamsaidia au kunambomoa kijana wake. Aidha, kwa viongozi au vigogo wa kisiasa wanaojua kazi moja tu ya kufundisha watoto wao-siasa, je, kutaka mwanao awe kama wewe kunamsaidia au kunamdumaza mwanao. Na je, ulicho wewe ndicho anachoweza kuwa yeye ? Baadhi ya wazazi ndio wanaomiliki televisheni. Tuwaulize wanaridhika kwa wajukuu zao kuona kile kinachooneshwa ?
Awe ni mtoto wa masikini au tajiri, mwenye wazazi au yatima, mwenye akili au mjinga, mweupe au mweusi, Mkiristo au Mwislamu hawa wote ni watoto wetu na hii ni nchi yetu na haya ndiyo malezi yetu. Swali la mwisho ni je hii amani na huu umoja tunaojivunia sana hapa Afrika watavirithi kwa malezi haya ?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment