Maonyesho kama yale ya Sabasaba kama yakiangaliwa upya na eneo kubwa zaii kupatikana yanaweza kuwa ni kivutio kikubwa cha utalii, wawekezaji na biashara kubwa kubwa duniani.
Katika kujipanga upya huko, kwanza, eneo jipya litafutwe ambako kutajengwa uwanja mpya utakaofaa uitwe Dar es salaam Internationl Expo -Tanzania.
Maonyesho haya yawe ni ya kimataifa. Yaani, bidhaa, tekhonhama na mitambo mbalimbali itakayooneshwa hapo iwe ni ile inayoweza kununuliwa na nchi zote zinazotuzunguka.
Uwanja huu unastahili kuwa ni wa ubora wa kimataifa na ingelikuwa ni vyema upatiwe kiwanja kipya ambacho kitaweza kuwa ni kijiji cha kudumu kwa maonyesho ya expo mbalimbali.
Wakati huo huo, kila mkoa unastahili kuwa na maonyesho yake ya sabasaba wakati ule ule yale ya Dar es salaam yanapofanyika.
Katika kufanya hivyo tutadhihirishia umma kwamba Dar es salaam sio Tanzania, na Tanzania sio Dar es salaam. Ajira zitaongezeka na kusambaa kwa sababu sasa patahitajika makundi 30 ya wawakilishi kwa kila Kampuni nchini kwenda katika mikoa 30 ya Tanzania. Kubwa zaidi, mikoa inayolala kwa kukosa kujua kuwepo kwa bidhaa na vifaa vya aina ambazo zinaweza kuwafanya waondokane na umaskini wao haitakaa ilale tena maana sabasaba kila mwaka itaizindua. Ndivyo inavyostahili pia kuwa kwa maonyesho ya nanenane. Yasiendelee kufanyika kisiasa bali yawe kweli ni maonyesho ya Expo-Kilimo International. Hali kadhalika mikoa nayo iwe na maonyesho yao kwa kadri ya uwezo, changamoto na matarajio yao.
Maonyesho yote haya yajikite kwanza na awali ya yote katika matatizo ya Watanzania, yawe ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni au kiteknolojia.
Kazi yake kubwa iwe ni kuoesha kipya kilichovumbuliwa na Watanzania na watu wengine ambacho kinaweza kuwa ufumbuzi wa tatizo au shida fulani. Kwa hiyo, miaka inavyokwenda matatizo ya Biashara, Kilimo na Viwanda yatakuwa yakipatiwa majibu yake katika maonyesho hayo.
Ni muhimu kwa maeneo kuwamakubwa zaidi na shughuli nzima iwe ni kivutio sio tu kwa wananchi wa kawaida, bali wawekezaji nawatalii pia. Hii iwe sawa na sherehe kubwa ya wiki nzima kitaifa ambako Watanzania watakuwa wakitafakari majibu ya matatizo yao na changamoto ambazo bado zinawakabili kuelekea kwenye dunia ya pili baada ya kugura ile ya kwanza.
Dhana nzima ya mashindano haya inapotezwa kwa kuangalia eti banda gani ni zuri na linalopendeza zaidi. Ninaamini wakati umefika kuvibadili vigezo vya ushindi na kuwachagua washindi kutokana na jinsi ambavyo banda husika limejitahidi kupata jibu sahihi kwa tatizo fulani linalowakabili Tanzania. Kwa mfano, bado tunanunua pampu za maji toka nje, je, zawadi si apewe aliyetengeneza pampu hiyo hapa nchini -iwe Mtanzania au mgeni!
Tuna tatizo la kupata zana za uchimbaji madini na hususan kwa wachimbaji wadogo, je, kwanini zawadi hiyo asipewe mtu atakayevumbua zana au mashine za kuchimba madini hapa nchini?
Tuna tatizo la uzalishaji na upatikanaji umeme, je, kwanini mzawadiwa asiwe ni Mtanzania au mgeni aliyekuja kuwekeza nchini na akaweza kuzalisha umeme kwa njia mbadala na umeme huo ukawa wa gharama nafuu zaidi.
Tuna matatizo ya kuzalisha magari, malori na mabasi yetu wenyewe kwanini zawadi zisiende kwa wale wa kwanza kabisa kutengeneza gari la Kitanzania hata kama teknolojia nzima itaazimwa au kuibwa nje?
Hivi atakayetengeneza trekta dogo la Kitanzania kwa kuazima teknolojia ya nje na ikawezekana trekta hilo kuuzwa kwa chini ya shilingi milioni mbili huyu si ndiye anayestahili kuwa mshindi kwenye Sabasaba Expo ijayo?
Watoto mashuleni hawana madeski, vitabu na vifaa vya kujifunzia vya kila aina. Je, kwanini zawadi wasipate wale watakaokuja na ufumbuzi wa matatizo hayo.
Mahospitali yetu yanafungwa na huduma kusimama kila kona nchini. Je, ushindani utakaofaa si ule wa utengenezaji wa zana na vifaa mbalimbali vya mahospitali hapa nchini ili viuzwe kwingineko kwa bei nafuu kuliko vinavyotoka nchi za nje? Maana, ukiwa na teknolojia duni katika hospitali au chuo ndivyo pia shule yenye inavyokuwa duni na ovyo kihali na kimazingira. Teknolojia ya kisasa inalazimisha usasa kwa kiwango cha juu ikiwemo usafi, mandhari na mazingira bora zaidi.
Mambo mengi yako ndani ya uwezo wetu. Kinachotakiwa ni kuona kwamba keki ya taifa inagawika kwa namna ambayo wajasiriamali na wazalishaji mali mbalimbali nao wanapata kitu cha uhakika ili kuleta mabadiliko tuliyokusudia nchini.
Nia na sababu ya kuwepo kwa maonyesho ya sabasaba ilikuwa ni kuiwezesha nchi kuwa na kipimamaendeleo kitakachoonesha jana tulikuwa wapi na leo tumefikia wapi. Lakini tukiwa mwaka nenda, mwaka rudi tunaonesha vilevile vya juzi basi kuna walakini mkubwa hapo. Utandawazi na makuzi ya teknolojia hayaturuhusu kuwa goigoi na wenda pole kiasi hicho.
Kiwanja kipya cha sabasaba lazima kiwe kikubwa kweli kiasi cha
kuwa na uwanja wa ndege mdogo, kituo cha treni, kituo cha basi, mabohari na vingine kama hivyo. Hili likifanyika foleni za kutisha zitakuwa historia maeneo ya Temeke. Na ili kuanza kutekeleza azma njema ya kutenga maeneo ya biashara na makazi ya wau au maofisi ni vyema kama uwanja wa Sabasaba hivi sasa utafanywa kuwa ni TEMEKE PUBLIC SHOPPING PLAZA AND SUPERMARKETS.
Uwanja mpya lazima uwe pia na hoteli ya hadhi ya kitalii kwa maana ya nyota 5 kwenda mbele. Uwanja wa golfu wa kisasa kabisa na vilevile uwanja wa mbio za langalanga (Formula 1) ili kutumika kwa uwanja huo mara kwa mara uwe ni kitu cha uhakika.
Wakati wa maonesho ni vyema uwanja huo ukawa na redio stesheni na TV ya maalum kwa ajili ya mawasiliano. Kwa upande mwingine kutakuwa na eneo la Tovuti au Intaneti ambako wafanyabiashara na wajasiriamali wa kila aina na rika watapata fursa ya kujifunza kufanya kazi zao kwa kutumia Teknohama.
Katika kufanya mabadiliko haya makubwa ni muhimu
kuwashirikisha watu wa nje kama Wajerumani, Wajapani na Wachina waliokubuhu katika mambo ya 'expo'.
Friday, July 8, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment