Sunday, July 24, 2011

Umeme: Mipango, mikakati na nishati mbadala muhimu

Katika miaka hii ambayo hali ya hewa inaendelea kubadilika na hatuna ahadi wala uhakika na mvua na kwa hiyo maji yanayotiririka katika mito na mabwawa tuliyoandaa kuzalisha umeme ni makosa makubwa kuendelea kutegemea umeme wa tabaini zinazoendeshwa na maji.
Hali yetu kama nchi sasa ni afadhali ukilinganisha na Somalia. Lakini upo uwezekano mkubwa wa ukame ulioikumba nchi hii iliyo kaskazini ya Tanzania na Kenya pia kuikumba nchi yetu.

Kutokana na ukweli huu, wale wanaoshika nafasi za uongozi nchini wanapaswa kuona mbali na mbele zaidi kuliko mwananchi wa kawaida.

Tatizo letu kwa hiyo siyo tu tatizo la ukame na kukosa mvua na maji ya kuzalisha umeme bali pia ni upungufu wa mipango na mikakati ya upatikanaji nishati ya uhakika na isiyoathirika na hali ya hewa kwa kadri inavyobadilika.

Tatizo pacha ni lile la serikali kudharau na kupuuza ushauri wa watu mbalimbali kuhusiana na muundo, kazi na nafasi ya shirka la umeme la taifa (TANESCO) katika kutafuta jawabu kamili na la kuridhisha la tatizo la umeme nchini.Shirika ambalo hivi leo limebatizwa na kuitwa 'TANZANIA ELELCTRIC SUFFOCATION COMPANY'- Ni dhahiri kwamba shirika ambalo miaka 50 baada ya uhuru limeweza kuwapatia asilimia 5 tu ya Watanzania umeme halina akili wala uwezo wa kufanya makubwa zaidi ya hayo ambayo tayari limekwishayafanya. Limefikia upeo wa uwezo na ubunifu wake.

Uendeshaji wa mashirika ya umma umefanana na ule wa mzazi ambaye alimshonea mwanaye suti akiwa na miaka 10 na leo mtoto huyo ambaye ana miaka 20 eti anatakiwa kuvaa suti ileile aliyoivaa akiwa na miaka 10. Watanzania tulikuwa milioni 9 mwaka 1960. Tuliyoyafanya wakati huo hayawezi kufanywa miaka hamsini baadaye na tukiwa takriban Watanzania milioni hamsini.

Baadhi ya watu wameshawahi shirika hilo livunjwe katika sehemu nne. Uzalishaji umeme, usambazaji umeme, utengenezaji vifaa vya umeme na uunganishaji na uhudumiaji miundo-mbinu ya umeme. Na sio lazima kufanya kazi zote hizi, bali shirika/serikali iruhusu Watanzania binafsi, wanajamii na wawekezaji kuendesha shughuli hizo kwa ufanisi na ufanifu zaidi.

Wapo pia waliopendekeza kwamba kila mkoa uwe na shirika lake la umeme, badala ya kuwa na shirika la umeme la taifa, kwa kutumia rasilimali za mkoa na ubia na wawekezaji wa ndani na nje. Hawa waliamini katika falsafa ya Schumacher kwamba 'Kidogo ni kizuri na chema zaidi,' au kwa Kiingereza: 'Small is Beautiful.' Kilal mkoa ungelitafuta chanzo chake binafsi cha uzalishaji umeme bila ya kutegemea tu maji. Hili lingeliendana pia na kifungu cha katiba kinachohusiana na kuwepo na ulinganifu katika maendeleo ya taifa-kitu ambacho kimeshindikana kabisa katika sekta hii ya nishati.

Niliposikiliza mahojiano ya Mh. Jakaya Kikwete na BBC akiwa ziarani Afrika Kusini sikuweza kuacha kuona kwamba majibu yake hayakuwa yenye kuonesha imani na matumaini kwamba tatizo la umeme liko ndani ya mikono ya Watanzania . Kilichojitokeza ni kwamba ni serikali ndiyo tu iliyokuwa ikitarajiwa kulitatua tatizo hilo. Aidha, serikali ilikuwa inapaswa kulipa fedha zote za ununuzi wa mitambo ya uzalishaji umeme papo kwa hapo. Kitu ambacho sio sahihi.

Ninaamini, Watanzania wakihamasishwa kama walivyokatwa kodi na haki zao mbalimbali ili kuanzisha mashirika ya umma (yaliyokuja kubinafsishwa bila wao kulipwa chochote) wana sababu, uwezo na nia ya kuchangia kumaliza tatizo la umeme lakini kwa sharti kuwa wanakuwa nao ni wamiliki wa mashirika yatakayoanzishwa kama sehemu ya ufumbuzi wa tatizo hili.

Vilevile, watengenezaji wa mitambo ya umeme wako tayari kukodisha mitambo yao na vile vile kuuza mitambo hiyo kwa mtu kulipia kidogo kidogo hadi deni liishe.

Hata hivyo kinachoonekan hapa ni kuwa mtazamo wa ndani kwa suala hili haupo na badala yake tuna mtazamo wa nje tu. Ikiwa ni pamoja na kuamini kuwa ni lazima tupate msaada au tukope kutoka nje ili tatizo la umeme liishe hapa nchini. Au wakati mwingine, pengine ni ujanja wa kununua vikubwa vikubwa kwa gharama kubwa ili watu wapate chambele au teni pasenti yao.

Sikubaliani kabisa na wale wanaoamini kwamba tatizo la umeme limesababishwa na ufisadi na eti kuna wauza majenereta walioihona serikali ili biashara yao ya majenereta ichanganye vilivyo. Japo kuwa majenereta yanauzwa kwa fujo hivi leo, lakini adha na gharama za uendeshaji majenereta ikiwemo kwa taasisi za serikali pia, kama vile gharama za dizeli au petroli; kelele; uchafu wa mazingira; nguvu kazi ya ziada katika kuzihudumia
ni mambo yanayoitia hoja hiyo hapo juu mashakani.

Uwekezaji katika sekta hii ya umeme unawezekana kabisa kutokea ndani ya nchi. Kwa maana kwamba, kama serikali ilivyoanzisha mashirika kwa kutumia kodi za wananchi upo uwezekano wa wananchi na wawekezaji kuchangia asilimia fulani na wawekezaji wa nje wakachangia asilimia fulani. Inapendekezwa ili makampuni ya umeme yawe ni ya Watanzania basi Watanzania wamiliki asilimia 51-60 na wawekezaji toka kwingineko asilimia 40-49.


Ufumbuzi wa tatizo la umeme, hali kadhalika, utakuwa mgumu bila kufahamu mchango wa siasa katika udhairu, kudumaa na kuserereka kwa TANESCO pamoja na misaada yote ambayo shirika hili limekuwa likipata toka kwa wafadhili wa nje na malipo ya gharama kubwa za umeme kuliko nchi nyingine yoyote Afrika. Wapo wanaodai kwamba shirika hilo liligeuzwa shamba la bibi na baadhi ya wanasiasa. Kwa maneno machache, shirika hilo, halijawahi kuendeshwa kibiashara bila kuingiliwa na wanasiasa. Pamoja na mifano mingi ya uwezo mdogo wa mameneja wa Kitanzania kusimamia miradi mikubwa hazijafanyika jitihada za dhati kumpata meneja toka nje mwenye uwezo na dhati ya kutusaidia Watanzania tuondokane na tatizo hili la umeme. Netsolution, kwa kiasi kikubwa, ilikuwa ni 'dili' lililonufaisha watu binafsi na sio nchi na watu wake.

Vilevile, wanasiasa Tanzania wamejenga tabia ya kuingilia kila fani na kazi nchini na kujifanya wao ni wataalamu zaidi kuliko wataalamu wenyewe. Toka mgao huu wa umeme pamoja na kuwa na vyuo vikuu vinavyotoa shahada mbalimbali za masuala ya umeme hapajawahikuendeshwa warsha au kongamano au angalau semina yoyote iliyowashsirikisha ili michango yao kuhusu ufumbuzi wa tatizo la umeme nchini lipatikane. Hii ni kasoro kubwa sana nchi mwetu, na isipoangaliwa itatuumiza katika kila sekta na nyanja ya maendeleo kwa miaka mingi ijayo.

Kama walivyo wanafunzi wa masomo mengine, wanafunzi wa shahada za uhandisi Tanzania hawapewi fursa za kutosha kutumia elimu yao kwa utafiti na uvumbuzi kwa majibu ya matatizo yetu mbalimbali. Bajeti yetu katika kuchochea utafiti ni ndogo mno, na sidhani kuna bajeti yoyote ya kuhamasisha ubunifu na uvumbuzi nchini miongoni mwa wasomi na wasiokuwa wasomi.

Wakati vijana wa Kenya wanagundua njia mbalimbali za kuzalisha umeme ikiwemo wa kutumia magurudumu ya baiskeli, umeme kwa upepe na sasa umeme kwa chupa ya cocacola na maji, vijana wa Kitanzania wamezungushiwa kitanzi shingoni mwao kinachowatia uoga katika kuanzisha au kuunda kitu chochote kinachoweza kuwa na manufaa kwa jamii yao. Na sio suala la ujinga au kutokujua. Ni kwamba wazazi wao na serikali yao haijakaa mkao wa kudai na kupata kutoka kwa kizazi hiki kipya zaidi ya muziki wa kuiga toka Marekani au kuvaa katakei!

Kati ya vijana wasiosoma sana ni wale ambao wameshawahi kuunda redio, kompyuta, gari, ndege, helikopta, transmita za redio na kadhalika. Lakini kwa kuwa baba na mama zao sio watu wakubwa, vijana hawa wameishia kutishiwa na vyombo vya dola hadi kujenga uoga mkubwa wa kuwa wabunifu na wavumbuzi wa kitu chochote katika maisha yao yaliyobakia. Ni nani anayekosa hapa. Tanzania au mtoto anayehusika?

Hebu, chunguza wewe mwenyewe katika nchi ambayo magazeti yametoa habari za watoto au vijana waliovumbua vitu mbalimbali, je, leo hao watoto wako wapi. Wamesaidiwa au wamehujumiwa, kwa kuwa tu ni watoto wa watu wasiokuwa na uwezo?

No comments:

Post a Comment