Nchi zetu za Kiafrika zimejenga utaratibu unaowafanya wananchi waamini kwamba bila serikali matatizo yao hayawezi kutatuliwa. Serikali inaonekana kujua kila kitu,kuwa na fedha zote duniani na kuwa bila mkono au mguu wa serikali hakuna anayeweza kusogea kwenda popote. Na serikali kwa upande wake inaelekea kuamini na kudhani ndiyo peke yake yenye majibu ya matatizo yote ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kiteknolojia. Kitu ambacho si kweli.
Guru wa Menejimenti, Profesa Peter Drucker anasema meneja mzuri na anayefanya kazi kwelikweli, hafanyi kazi yoyote. Ndivyo ilivyo pia kwa serikali nzuri na inayofanya kazi kwelikweli. Haifanyi kazi. Tunaposema haifanyi kazi hatuna maana haifanyi chochote au inategea tu. La hasha. Meneja na serikali bora na mfano wa kuigwa hufnaya kazi kwa kupitia watu, idara na taasisi nyingine. Unapoingilia kufanya kazi za watu wengine, idara na taasisi nyingine badla aya wao kuzifanya wenyewe kuna uwezekano mkubwa wa wewe kuvuruga kazi hizo au kutokuwa na tija linganifu wala ufanifu na ufanisi. Ni vizuri viongozi na mameneja wetu walielewe hili na wajipime na kuona kama kweli wanafanya kile ambacho kiongozi au meneja anachotakiwa kukifanya na sio kufanya anayoweza kufanya karani au tarishi. Kama sio waziri au mbunge au mkuu wa mkoa kama sio mkuu wa wilaya.
Tujiulize ni nini nafasi ya jamii katika ufumbuzi wa tatizo la umeme nchini Tanzania. Hivi leo, Benki ya dunia inamwaga misaada kwa ajili ya uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya kijamii, jambo linaloashiria uwezekano wa kushirikiana na benki hiyo kuziwezesha jamii mbalimbali kuja na mawazo na mapendekezo kuhusiana na jinsi wanajamii wenyewe wanavyoweza kuchangia katika uzalishaji umeme nchini bila ya kutegemea sana wawekezaji toka nje. Maana wawekezaji hawaji kujenga miundombinu bali kuwekeza katika biashara au uzalishaji mali kwenye eneo walilojikita. Mjenzi wa miundombinu yetu ni lazima awe Mtanzania mwenyewe, mwanajamii katika jamii husika.
Wanajamii wa maeneo mbalimbali nchini hivi leo wanasita kujiunga na shughuli yoyote inayonukia ujamaaujamaa au ushirka ushrika kwani dhana hizo zilichakachuliwa vibaya mno na viongozi waliokuwa chini ya Mwalimu Nyerere. Ni yeye tu inaelekea alikuwa na nia safi na nzuri ya kubadili maisha ya Watanzania na sio wengine, na kama walikuwepo walikuwa wachache sana na walisakamwa kupita kiasi na mafisadi na walilia ubepari wa wakati huo.
Ni vyema pia kuzijua njia mbalimbali za kuzalisha umeme. Kisha kuainisha ni ipi au zipi ambazo zinaweza katika muda mfupi kutupa nafuu katika tatizo hili na zile ambazo zinahitaji muda na uwekezaji mkubwa zaidi.
Ziko njia mbalimbali za kuzalsha umeme zinazojulikana kufikia sasa. Njia hizo ni pamoja na mchakato wa nyuklia; samadi na takataka mbalimbali; mvuke; mashamba ya umeme wa solar; mashamba ya umeme wa upepo; mafuta ya petroli au dizeli na maji.
Tanzania inasemekana haijafikia hali ya kujitosheleza kiuwezo na kiusalama kuzalisha umeme kwa mchakato wa uranium ijapo tumejaliwa madini hayo. Kwa hiyo, hii sio njia ya kutusaidia katika siku za karibu.
Umeme kwa maji ndio huo ambao unatuongezea umaskini, maafa na dhiki zisizokweisha.
Nao huu unaweza kurudia hali yake ya kawaida endapo mipango yetu ya uoteshai miti, utunzaji mazingira na vilivyomo na hususan kwenye maeneo ya vyanzo vya maji milimani au chini ardhini itafanikishwa.
Uzalishaji umeme kwa kutumia samadi na takataka mbalimbali; upepo; mafuta ya petroli au dizeli ndio njia zinazoweza kuchangia haraka zaidi kumaliza tatizo hili.
Kwa jiji kama Dar es salaam uzalishaji umeme kwa kutumia takataka ni kitu kinachowezekana. Na njia hii itaua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza, utaongeza megawati za umeme kwenye mtandoa wa umeme na pili utafanya jiji hili kuwa safi daima.
Mashamba ya umeme wa solar na upepo kwenye mikoa yenye jua na upepo wa kutosha yanaweza kuchangia gridi ya taifa kwa megawati kadhaa.
Kwenye miji na wilaya ambazo zina upepo wa kutosha ni dhahiri tukishirikiana na nchi kama Denmark na Netherlands tunaweza kupata 'shortcut' za kupata mitambo na vifaa vinavyohitaji na kuzalisha umeme chini ya mwaka mmoja.
Umeme wa jenereta zinazotuchafulia hali ya hewa, mazingira na kutupigia makelele unastahili kudhibitiwa na kuvumuliwa tu kutokana na ukweli kuwa hakuna ujanja mwingine.
Mitaani ili tusichafue zaidi hali ya hewa ni vyema maduka au makampuni kadhaa yakaungana na kununua jenereta kubwa zinazoweza kutosheleza maduka au makampuni yote yaliyo sehemu hiyo badala ya kila mmoja kuwa na kijenereta chake na hivyo kusababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira kwa moshi, kelele na hewa ya carbon monoxide.
Inafaa pia kuuliza kama nchi zilizotuzunguka, yaani, Msumbiji, Malawi, Zambia, Kongo Kinshasa, Rwanda (ambayo imefanya kazi nzuri sana katika upatikanaji umeme kwa watu wake), Burundi, Uganda na Kenya zina hali gani kiumeme na tunaweza kushirikiana nazo vipi ili tuzalishe umeme kwa pamoja utakaotusaidia sote kupunguza au kumaliza kabisa tatizo letu la umeme.
Maendeleo ni vigumu kupatikana bila kuwa na mipango mizuri inayotekelezeka. Ni heri nchi kupiga maktaimu kwa mwaka mmoja hata zaidi ili kwanza ihakikishe imejipanga vizuri kabla ya kuwa na mpango wowote wa maendeleo usiotekelezeka.
Katika hili ni muhimu kuona kwamba viongozi mbalimbali wa nchi hii wanawekwa kwa misingi ya kujenga na kuendeleza sehemu husika. Hii ina maana kazi ya mkuu wa shrika fulani, mathalani, TANESCO, lazima iwe ni kulitoa shirika hilo kwenye ngazi ya chini kwenda ngazi ya juu kiutendaji na kiufanisi.
Ndivyo ilivyo pia kwa mwenyekiti wa kijiji, katibu kata, kiongozi wa tarafa, mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa wanavyotakiwa kuwa. Baadhi ya matatizo yetu kama hili la umeme kama watu hawa wangeliachiwa kufanya kazi kama watu huru labda linaweza kumalizwa huko huko kwani wao wanajua eneo lao vyema zaidi kuliko viongozi wa kitaifa na mbunge asiyewatembelea hadi uchaguzi mkuu ujao.
Nilishawahi kuzungumzia kwamba ukiwa na kiongozi halafu kiongozi huyo hana tatizo analolitatua, wala haichangamkii fursa yoyote ili kuongeza kipato au kuyafanya maisha ya walio chini yake kuwa bora zaidi-ni sawa na kuwa na watu bila kiongozi.
Kadhalika, kama una shirika, wilaya, mkoa au wizara ambayo haijulikani inashughulikia tatizo gani au kuchangamkia fursa gani za kimaendeleo katika eneo husika, basi mahala hapo hakuna kiongozi. Kuna mtawala. Na kwa bahati mbaya viongozi wengi tuliokuwa nao hawastahili kuitwa viongzi bali watawala au magavana.
Tofauti ya kiongozi na mtawala ni kwamba, mtawala kazi yake ni kusimamia tu kile kilichopto, yaani, kile ambacho kimeshaanzishwa na wengine. Na sio jukumu lake kubadili chochote au kufanya kazi zaidi ya usimamizi na kutoa taarifa kwa wakubwa wake. Wakati kiongozi, ni mtu mwenye dhamana za kuleta mabadiliko toka hali duni kwenda hali bora zaidi. Kiongozi huonyesha kwa vitendo, hushauri, huelekeza, huelimisha, huwezesha na hutoa motisha ili walioko chini yake walete mabadiliko tarajiwa katika eneo husika.
Kiongozi tofauti na mtawala, huona mbali na mbele zaidi. Ni mtabiri wa namna fulani. Hufahamu fika kwamba haya ya kawaida watu walio chini yake wanayajua na wanaweza kuyashughulikia. Lakini yale ya mbele na yajayo na yasiyo tabirika ndio eneo la kuonesha uongozi wake.
Mathalani, mtawala huwaza jinsi ya kuwalisha watu wake leo leo. Wakati kiongozi anatakiwa kuwaza, kupanga na kuweka mikakati ya watu wake kupata chakula bila tatizo miaka mitano au kumi ijayo.
Mtawala huwaza kutatua tatizo la umeme leo leo, lakini kiongozi hutafakari, hupanga na kuweka mikakati inayouliza maswali ya msingi na yasiyo na majibu ya haraka. Kwa mfano, kama tutakuwa na ukame, yaani, mvua hazitanywesha na umeme wetu unategemea maji, ni njia gani mbadala tutakuwa nazo ili ukame na kukosa mvua kuisisababishe matatizo ya upatikanaji umeme.
Kiongozi mzuri huwatumia walio chini yake kutokana na uwezo na utalaamu walio nao bila kujali watokako wala udhaifu wao. Ubora na kile mtu anachoweza kukifanya katika kutimiza lengo lililoko mbele yake ndio kitu muhimu kuliko vyote. Na kiongozi bora, hatokei hata mara moja, kuwalaumu walio chini yake kwamba wameshindwa kazi fulani. Wakishindwa ina maana ni yeye ameshindwa na sio walio chini yake. Aghalabu, kiongozi mzuri na bora, huwaongoza watu kwa namna ambayo watu wao wanapofanikisha malengo fulani basi watu hao kwa pamoja husema, 'tumeweza, tumeshinda!' na sio kiongozi wetu ameweza, ameshinda!
Kiongozi bora na hususan akiwa wa wilaya au mkoa au nchi hupaswa kujua mambo ambayo mkoa wenyewe unastahili kutengeneza au kuzalisha na yale ambayo kwa muda fulani yapasa kuyapata toka kwa wengine.
Ni kichekesho kwa nchi kuwa na mpango unaotaka kuongeza asilimia ya nyumba zinazopata umeme toka asilimia 5 hadi asilimia ishirini na tano au hamsini, bila ya kuwa na mpango wa uzalishaji mashine, vifua umeme, mitambo na zanatepe mbalimbali zinazohitajika ili nchi yenyewe ijitegemee angalau kwa asilimia 80 kwa vitu vinavyohitajika kuzalisha, kusambaza na kuunganisha umeme nchini.
Kama nilivyodokeza huko nyuma, jambo hili sasa ni rahisi na jepesi kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu na maendeleo yetu. Maana, hakuna sheria inayosema ili tuendelee lazima tuwatumie tu Watanzania au raia wetu hata kama hawajui na hawajasomea kazi inayotaka kufanyika. Na eti, hata kama kuna wahandisi au mafundi wa umeme,, maprofesa wa umeme, washauri, wanafunzi na watafiti wa masuala ya uzalishaji umeme wasio na kazi wala mafunzo kwa vitendo nchini na nchi za nje lazima tutegemee shirika moja tu nchini kutunusuru na balaa na maafa yanayoikumba nchi na watu wetu leo.
Kutokuona na kutozithamini na kutozitumia rasilimali watu zilizotapakaa huko Marekani, Ulaya Magharibi, Ulaya Mashariki, Russia ya zamani na kwingineko kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia
ni jambo ambalo tutakaa na kuja kulijutia baada ya muda si mrefu kutoka sasa.
Miaka mingi iliyopita kulikuwa na Baba Baa na Baba Waa. Wote wawili walikuwa na mashamba makubwa yenye mimea ya kila aina pamoja na maeneo wazi, yaani, yasiyopandwa chochote. Msimu wa kilimo ulivyofika, Baba Baa alikuwa akiwatafuta vibarua wa kikwao tu, hakutaka wageni walime shamba lake. Aliamini hawajui kulima.Lakini mwenziwe Baba Waa aliwamwagia ajira Warundi, wamakonde, wasafwa, Wanyarandwa bila kubagua. Katika mchanganyiko huu wa watu wenye asili mbalimbali shamba la Baba Waa sio tu lililimwa vizuri bali lilinufaika na mimea mipya, njia mpya za kilimo, kama vile kupiga matuta na kadhalika. Hivi leo wajukuu wa Baba Baa hawana lolote maana shamba lilimshinda na hatimaye akaliuza. Wajukuu wa Baba Baa wangali na shamba la babu yao, na Mungu kawaongezea zaidi kwa kuwa na viwanda, maduka na mahoteli ya kitalii! Tafakari! Akili kichwani mwako!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment