Sunday, November 25, 2012

Kwanini Ushirika, Vijiji na Miradi ya Pamoja Inakwama ?


AGHALABU husemwa kwamba anayeumwa na nyoka akiona jani hustuka. Hii ndiyo hadithi ya shughuli za Ushirika, vijiji na miradi ya pmoja katika sehemu mbalimbali za nchi.
 Baada ya shughuli hizo kuingiliwa na siasa na wanasiasa na hatimaye kuchafuliwa kama sio kuharibiwa kwa kiasi kikubwa, Watanzania wengi walikatishwa tamaa na shughuli zozote zilizohitaji kufanzwa na mtu zaidi ya mmoja. Kila mmoja akawa ameamua kwenda kipweke pweke, hata pale ilipoonekana dhahiri kuwa jambo linalofanywa haliwezi kufanikiwa bila umoja au  ushirikiano wa namna moja au nyingine kati ya watu wawili au zaidi.
 Katika uchambuzi wake wa kisayansi kuhusu nadharia za ushirikishwaji umma nchini, Bi. Rebecca Maarsland (2006) alibainisha kwamba ushirika na ushirikishwaji watu Tanzania kumeathirika kwa kiasi kikubwa na mapambano  kati ya walio nacho na wasio nacho. Serikali ya awamu ya kwanza kwa nia njema kabisa iliamini na kutekeleza dhana ya ushirikishwaji umma kwa  lengo la kuwanasua  Watanzania na umaskini wa kupindukia. Hata hivyo. viongozi wa vikundi vya  ushirika walijikuta wakiwa na uwezo na fedha chungunzima na hapakuwa na njia nyingine ya kuutumia ila kwa kuingia katika siasa. Wanasiasa kwa upande wao walitegemea kodi iliyolipwa na wananchi nayo haikutosha pia kuwapa na fungu la kujiimarisha kisiasa. Hivyo, ushirika na viongozi wake wakawa ni tishio kwa viongozi wengine wa kisiasa. Mkwara ndipo ulipoanza. Wanasiasa na mangimeza hawakuwa tena na nia ya kuendeleza ushsirika bali kuua ushirika.
 Ushirikwa na ushirikishwaji ulistawi tu kati ya Uhuru na kabla ya kuanzishwa kwa CCM. Kuna wanaoamini kwamba hayo yalikuwa hivyo kwa sababu ni mtu mmoja tu aliyekuwa na nia ya kweli ya kuwasaidia Watanzania mafukara kupitia ushirika. Huyo hakuwa mwingine ila Mwalimu Nyerere. Inaelekea katika timu yake nzima ya uongozi hakuna aliyefahamu dhana ya ushirikishwaji achilia mbali kuamini katika nadharia hiyo  na kuitekeleza kwa vitendo.
 Wakati Tanzania ilisifika sana kimaneno kwa ushirika, yakini, ushirika wa kweli kwa vitendo  ulikuwepo Kenya japo kuwa wakati huo tukiwazomea kuwa wao ni wanyama au ubepari ni unyama ! Kweli ubepari ni unyama, lakini tofauti na ilivyo hivi leo Tanzania, Kenya wana kimbilio la kujihifadhi kama vyama vyao vya ushirika na vinawasaidia si haba. Tanzania hawana pa kukimbilia.
 Walioathirika sana ni wananchi ambao walifikia kuona ushirika ni baba na mama kwao. Ushirika ghafla ukawa ni wizi na unyonyaji wa masikini na wala sio mwokozi na kimbilio lao tena. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa kufa kwa ushirika nchini na imani ya wananchi kwa kitu kiitwacho ushirika. Hadi wa leo jeraha hilo kubwa halijapona.
 Nyerere alipowaachia viongozi wake wajenge na kuendeleza vijiji vya kijamaa ili nchi iwe na mfano unaong'aa kwa Afrika yote na dunia, maofisa wake walioona hiyo ni nafasi ya kuwakomoa wanavijiji tajiri na jeuri na hivyo wakawatoa kuliko na ardhi nzuri na yenye rutuba na kuwapeleka kwenye mawe na mchanga. Huo ukawa ni mwanzo wa kifo cha vijiji Tanzania, sambamba na  kufanikiwa kwa vijiji vya Uyahudi Kibutz  huko Uyahudi, ambavyo, hivi leo ni mfano kwa dunia nzima.
 Miji ilionekana kuwa na mameneja wazuri na hivyo kuiendesha miji yao vizuri  ikatuhumiwa kuwatajirisha na kuwapa kichwa mameneja na viongozi wake wengine, hivyo mkwara ukatafutwa na CCM  wa kumaliza nguvu pia halmashauri za mji nchini. Huo ukawa ni mwanzo wa kuwa na miji dhaifu na michafu Tanzania.

Kukosekana na ukweli na dhati pamoja na wanasiasa na mangimeza kuona miradi ya pamoja kama ni kazi ya kusadia masikini na watu walio nyuma kimaendeleo na sio kazi ya kuonesha uwezo wao kama viongozi ulichangia si haba....
 Utafiti usio rasmi nilioufanya unaonyesha kwamba hivi leo Watanzania hawana imani kabisa na kitu kinachoitwa ushirika wala miradi inayofanywa na watu wengi wasioshabihiana kwa mengi. Nalo hili kwa kiasi limechangiwa na siasa na sera za chama tawala ambacho  kwa makusudi ziliua moyo sio tu wa kujitegemea bali dhana nzima ya ushirika na ushirikishwaji nchini. Hata hivyo, ukweli haukanushiki kuwa ushirika na uendeshwaji wa vijiji kama makampuni ndio njia pekee ya kuwatoa kwenye umasikini watu walio wengi na hakuna njia nyingine rahisi kama mbadala.
 Nadharia mpya juu ya ushirika na ushirikishwaji watu zimeweza kutanabaisha kwamba kuna ngazi mbalimbali za ushirikishwaji watu na upelekaji madaraka kwenye ngazi za chini iwezekanavyo kwa faida ya walio wengi na sio wachache.
 Ukiipandikiza nadharia hii katika sehemu za mashambani au vijijini Tanzania utaona kwamba  katika miaka yetu yote ya kusumbuka na Ushirika na ushirikishwaji wananchi Tanzania haikuwa imekwenda popote. Ilikuwa chini kabisa katika modeli za nadharia ya ushsikishwaji watu na mgawanyo wa mamlaka au madaraka kwa wananchi.
 Kuna ngazi zipatazo nane katika nadharia hiyo ya ushirikishwaji. Ngazi hizo ni ile ya mwisho au ya chini kabisa, ambayo ndiyo ile iitwayo ya hila, ujanja, uzaini au kuchezea (manipulation)  ushirika na ushirikishwaji watu katika masuala mbalimbali. Katika hatua hii serikali kuu, serikali za mitaa, NGOs, makundi ya kiimani na mengineyo kwa kuwatumia watu iwe mjini au vijijini wanatafuta kunufaika wao kwanza na sio kuwastawisha walengwa. Ndio maana inaiitwa pia kuchezea watu au kucheza na maisha ya watu. Ni mzaha na utani mtupu. Kwa bahati mbaya hii ndiyo hatua ya chini na ya mwisho kabisa na masikini Watanzania hapo ndipo ushirika na ushirikishwaji wao ulipo kwa hivi leo.
 Ngazi ya saba ni ile ya kuganga (therapy) ambayo hutokea pale watu fulani wanapokuwa na tatizo basi tatizo hilo huhitaji ushirikishwaji wao ili kulitatua. Kwa hiyo ushiriki wao huanzia na kuishia hapo. Kwa mfano, kikizuka kipindukipindu ushirikishwaji huu huwa unatumika zaidi kuliko wa aina nyinigne yoyote.
 Ngazi ya sita ni ule ushirikishwaji wa kuarifiwa au kupewa habari au taarifa kwamba mnafanyiwa hili au lile. Wanaohusishwa zaidi ni viongozi wa kijiji au mtaa au sehemu husika. Kwa mfano, huu ndio mtindo maarufu zaidi unaotumiwa na TANAPA na washirika wake katika kulinda na kutunza hifadhi za wanyama kwa kuwashirikisha wananchi. Wananchi hawana sauti yoyote ya maana isipokuwa kugawia ambacho wenyewe tayari pia wamekwishajigawia.
 Tuliza au bembeleza ndio ngazi ya tano ambayo kama neno linavyoonyesha watu fulani wanabembelezwa kama sio kudekezwa au kutulizwa kwa kufanyiwa hili au lile halafu wenye mradi wakaendelea na shughuli zao kama kawaida bila kusumbuliwa na wanaowazunguka. Hilo hutokea sana katika miradi ya uchimbaji madini, gesi na mafuta.
 Kwenye ngazi ya nne sio tu watu wanabembelezwa na kutulizwa na kitu kidogo au miundombinu na zawadi hizi na zile bali pia wenye uwezo wanatafuta ushauri toka kwa wasio na uwezo. Mathalani, serikali kuomba ushauri wa raia, au mwneye mradi wa uchimbaji tanzanite kuomba ushauri wa watu wa Merelani. Lakini bado, watu wanakuwa hawana uwezo wa hali na mali katika mradi husika.
 Hatua yenye afadhali zaidi ni hatua ya tatu. Katika hatua hii ambayo inaitwa UBIA, raia au wananchi au wakazi wa sehemu husika wanakuwa ni wana hisa katika mradi husika. Mathalani, katika kilimo mwekezaji anapokubali kushirikiana na wanakijiji ili kuzalisha mazao fulani kwa ajili ya kuuza nchi za n je na kisha faida ikagawanywa kama ilivyokubaliwa katika mkataba ulioridhiwa na wanajiji wote kwa pamoja.
 Ngazi ya pili na ya kwanza ndio za juu kabisa katika ushirika na ushirikishwaji wananchi. Ya saba ni ile ya kukaimishiwa madaraka au mamlaka, mathalani, mkoa kuwa na gavana badala ya kiongozi wa kuteuliwa na kuruhusiwa kusimamia mambo yake ya kiuchumi na kijamii bila kuingiliwa nas erikali kuu katika utendaji shughuli zake za kila siku ili kuharakisha maendeleo ya mkoa na nchi nzima.
 Ngazi ya nane ni ile ya mamlaka au madaraka kuhodhiwa na wanakijiji au wanamtaa au wananchi wa eneo husika. Hii ndiyo ngazi ya juu kabisa katika ushirika na ushirikishwaji umma, ikiashiria pamoja na mambo mengine uhuru kamili wa watu kuendesha mambo yanayohusu maisha yao ya kila siku bila kuingiliwa na watu wanaokaa na kufanya kazi mbali kabisa na wao.
 Ni dhairi kuwa Tanzania  katika suala hili la ushirika na  ushirikishwaji umma ndio kama vile  tena tumeanza. Inasikitisha sana. Lakini ndio ukweli. Wenye niia ya kuufufua ushirika na moyo wa ushirikishwaji na kujitegemea kwa watu wetu ni lazima waanze kwanza kwa kazi ya kuwadhihirishia kwamba yaliyofanyika huko nyuma ni mkaosa na bado ushirika na mchango wao katika miradi ya kiuchumi na kijamii ni nunu yenye thamani kubwa na haiwezi  kuwa na ushindani wa aina n yingine.
 

Sunday, November 4, 2012

Tunajifunza kitu gani toka Utajiri wa Bakhressa ?


BIDHAA, viwanda na magari ya Bakhressa yanajulikana kuliko mwenyewe anavyojulikana. Somo la kwanza, umaarufu wa mtu unaotokana sio na kujisifia mwenyewe ila kile anachokizalisha na kukiuza au kukifanya na kukileta sokoni ni bora zaidi.
Moja kwa moja hili pamoja na mambo mengine ninayoyajua linanifanya kuamini kwamba bwana huyu amebahatika kuwa mtu mwenye kujitambua na anayejua anahitajiwa afanye nini katika dunia hii. Watu kama hawa huwa ni wachache sana duniani. Wengi wetu tupo, tupo tu, hata pale tunapopewa dhamana za juu katika makampuni au nchi. Na huwa tunaishi zaidi kwa kujinufaisha sisi na jamaa zetu na sio zaidi ya hapo. Wakati Bakhressa anaishi ili kuinufaisha nchi na sehemu kubwa ya Afrika na dunia. Haishi ili kuonekana ila anaishi ili anachokifanza kionekane na Mungu wake na dunia.
Ukubwa na utajiri sio ubwana bali ni utwana ni funzo jingine muhimu tunaloweza kujifunza tokana na utajiri wa mtu huyu mashuhuri asiyekimbiza sifa ila sifa zinazomkimbiza.
Taarifa za hivi karibuni zinazofichua utajiri wa Bakhressa na yeye kama mmojawapo wa matajiri wakubwa Afrika hazikuja kwa wengi kama kitu cha kushangaza. Watu walijua, wanajua, na wameendelea kujua kuwa Bakhressa ni tajiri asiye na makelele wala vishindo.
Kutokana na kutopenda sifa kwake ni kazi kweli kukutana au kukutanishwa naye. Lakini kutoka kwa watu wa karibu naye na uchambuzi binafsi wa maisha yake nimefanikiwa kuokota vitu viwili vitatu nitakavyowapatia.
Bwana huyu ni mchamungu nalo hili linaonekana wazi si katika vitendo na kauli zake tu bali pia katika bei ya bidhaa zake. Nina hakika uchamungu wake kwa kiasi fulani una mchango mkubwa katika utajiri alionao. Hii ni tofauti kabisa na viongozi na matajiri wetu walio wengi ambao wanadhani walichokipata na walichonacho kinatokana na akili na uwezo wao na sio mapenzi ya mungu.
Habari toka ndani zaidi zinasema kwamba bwana huyu huwa anaanza kazi baada tu ya swalati alfajiri na hatoki ofisini hadi saa nne usiku kama sio zaidi ya hapo. Hivi nani katika viongozi na matajiri wetu wengine anaweza akakipa kile anacholipwa mshahara au kinachomwingizia kipato zaidi ya masaa sita kwa siku? Ninaamini ni wachache sana. Na muda mwingi utakuwa unatumika kwa kujionyesha au kuzungumza mambo yasiyohusiana kabisa na kitu anachotakiwa kuwajibika.
Nikiikamata sifa hii hii, utagundua kuwa huyu bwana zaidi ya kusali sala 5 au zaidi kwa siku huwa hana muda na kitu kingine. Kwa hiyo, moja kwa moja gharama zake kimaisha ni ndogo mno, tofauti na viongozi na matajiri wetu wengi walivyo. Hana matanuzi, lakini si mchoyo wa zaka na sadaka na kodi ya serikali.
Kama ningeliikuwa shehe Saidi ninadhani ningeishia hapa. Ila nina hakika mtu wa kwanza kunikosoa atakuwa mhariri wangu. Makala yangu haitajaza nafasi iliyowekewa. Kwa hiyo, kwa kuwa kazi yetu ni kubwabwaja na hapa tunasifia sio mtu bali matunda ya mtu hebu tuendelee kidogo.
Huyu ni mmojawapo wa Watanzania wachache ambao wakati wanasiasa wetu wanapoteza muda kugombea nani atakuwa rais 2015/6; yeye yuko 'bize tu' na mananga kuhakikisha kwamba kila nyumba, kila duka, kila shule, kila hoteli na kila taasisi iwayo inakipata inachokihitaji kwa wakati.
Haiwezekani kila Mtanzania kuwa rais. Lakini inawwezekana kila mtu kuwa na mchango maalum wa kutoa kwa jamii ya Kitanzania. Bakhressa anaonesha kwa vitendo kuwa hili linawezekana. Na kwamba uongozi sio wa kisiasa tu, bali pia biashara ni uongozi na pengine bora zaidi.
Pamoja na kuwaachia wengine kukamata nafasi mbalimbali muhimu, bado ana muda na nguvu tosha ya kufuatilia na kudhibiti mambo pengine kutokana na uwezo wake binafsi au muundo wa kampuni au mfumo anaoutumia katika biashara zake.
Ili kuwa na huduma na bidhaa kama anazozalisha bwana huyu ni lazima uwe na rasilimali watu au wafanyakazi unaowajali na unaoangalia maslahi yao kwa kulhali. Wafanyakazi hao ndio wanaomuwezesha kufanikiwa katika mambo yake mbalimbali.
Tofauti na matangazo ya bidhaa za makampuni na watu wengine nchini upo ukweli kwa kiasi kikubwa kuhusu bidhaa za bwana huyu, hili likiwa na maana kwamba na yeye pia ni mkweli.

Wasifu wake unatufikisha wapi ?

Kwa kifupi tumeorodhesha sifa za Bakhresa kuwa ni pamoja na asiyetaka sifa binafsi; mchamungu; mkarimu; mpenda watu; mkweli; muadilifu; anatambua anachotakiwa kukifanya duniani; anaishi kutumikia wengine; mchapa kazi; ana iktisadi au mchache wa israfu na meneja au kiongozi daraja la kwanza.
Kwa maoni yangu,, bwana huyu ni kitabu kinachoishi cha menejimenti kinachostahili kutumiwa na viongozi wa kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiteknolojia na kiutamaduni ili Tanzania kupitia mfano wake iweze kuondokana na umaskini. Kama utajiri wake umetokana na Tanzania, basi kwanini Tanzania iwe maskini ikiwa angalau watu 1,000 tu watapatikana kuiga mfano wake?
Utajiri mkubwa wa bwana huyu umepatikana kutokana na mazao na bidhaa zinazotoka au zinazokuzwa hapahapa nchini. Vitu hivyo ni pamoja na nafaka, matunda, maji, maziwa, sukari na vitu kama hivyo. Nina hakika tungekuwa na sera nzuri za kodi, fedha na uchumi katika uchukuzi na usafirishaji pengine bwana huyu angetuwezesha pia kuwa na usafiri wa ndege, meli na mabasi ulio bora zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. Aanaonekana kuwa mbele zaidi ya wanasiasa na viongozi wetu kiuchumi na kiuongozi. Kiasi kwamba inabidi wamwekee breki hata pale breki hizo zinapokuwa sio kwa manufaa ya nchi na watu wake.
Je, viongozi wetu wa kisiasa wakizitazama sifa za kiongozi huyu wa kiuchumi na bila kuhofu wao ni vichuguu na yeye ni mlima Kilimanjaro hatuwezi kuambulia chochote hapa ?
Nina hakika mia kwa mia kwamba kama wilaya na mikoa yetu inaongozwa kama vile ni kampuni huru ndogo chini ya kampuni kubwa (nchi) na sio kama ofisi za chama tawala mapinduzi haya ya kiuchumi yaliyoasisiwa na Said Salim Bakhressa wa Tanzania ni kitu kinachoweza kupanuliwa zaidi na yakaishia sio kuifaa tu Tanzania bali Afrika na dunia nzima.
Sera inayohitajika hapa ni kuenzi vitu na watu wa ndani kwanza na sio kuchukuliwa na upepo wa uwekezaji ambao leo kwa mfano kwenye migodi ya dhahabu tunaona jinsi wanavyodanganya hata kwenye kile kidogo wanachotakiwa kutulipa. Kwa maneno mengine, ni muhali kwa nchi kujengwa na wawekezaji au watu kutoka nchi za nje bila kushirikishwa kikamilifu mzawa katika uleteaji nchi yake maendeleo ambaye na yeye pia ni mwanahisa.

Uchumi mikoani, wilayani

Kwa kukosa neno la kufaa pengine tunahitaji sera ya kuupelekea uchumi wetu mkoani na wilayani. Ukichukulia ule mfano wa kampuni niliouainisha hapo j uu ni kwamba kila wilaya na mkoa utaangalia rasilimali ilizonazo na kisha kuamua ni uzalishaji, huduma, biashara au shughuli gani zinazoweza kuukomboa mkoa au wilaya kiuchumi.
Hiki sio kitu kipya. Mikoa ya Nyanda za Juu kusini, mathalani iliaminika kwamba inaweza kulisha sio tu Tanzania bali Afrika Kusini na ya kati kwa nafaka za aina mbalimbali. Hata h ivyo, hadi wa leo miundombinu na mikakati ya kiuchumi na kibiashara inayoweza kufanikisha hilo bado haipo.
Kwa kifupi ni kwamba kuna mikoa na wilaya hapa nchini ambayo inaweza kutajirika na uvuvi tu au kilimo cha mboga na matunda tu au uchimbaji madini tu au sekta ya elimu (msingi, sekondari hadi vyuo) tu au mahospitali yanayopokea wagonjwa toka nchi za nje tu au kuwa na masoko na maduka ya mipakani na viwanja vya ndege, treni na mabasi tu au kwa utalii na huduma za hoteli tu. Hivi sasa tunajitawanya na kutapanya rasilimali chache tulizonazo ambazo badala ya kutusogeza mbele kimapato kunatukwamisha na kutuacha tusiojitosheleza hata kwa mahitaji yetu ya msingi.
Bakhressa hajajiingiza katika kila sekta ya uchumi. Amechagua. Na hizo alizochagua zimemfanya awe tajiri anayetambulika na dunia. Vivyo kila wilaya, kila mkoa, kila nchi (Tanganyika na Zanzibar ) inaweza kuchagua eneo moja la kiuchumi kama ndilo eneo lake la kuukimbia umaskini na kuanzia hapo ikawa hakuna kurudi nyuma tena ila kwa nchi nzima kuiga mfano wa Bakhressa-Inshallah!

Tutathmini Upya Mchango wa Taasisi za Fedha na Mikopo Nchini

MZAZI anayetambua kwamba mwanaye ana tabia mbaya, akamuachia vivyo hivyo bila kumkanya, huwa hajitendei haki wala hamtendei mwanawe haki.
                Umekuwa ni wimbo wa kurudiwa rudiwa kuwa Watanzania hawakopesheki. Ukiwakopa kulipa ni kazi. Lakini kwa wanaomuelewa binadamu wanafahamu fika kwamba tabia yoyote hujengwa na malezi na mazingira yaliyopo.
                Na inaeleweka pia kuwa asilimia kubwa ya wanadamu hawana tabia mbaya na ni idadi ndogo tu ambayo  haiaminiki na hailekezeki.
                Nitakuwa mchache wa shukrani bila kusifu kazi nzuri iliyofanzwa na taasisi za fedha hapa nchini. Lakini kutokana na ukweli kuwa bado tuna kazi ngumu ya kupigana na umaskini, ninaamini hata wao wanajua zipo changamoto za zamani na mpya ambazo twapasa kuzikabili ili nafuu katika umaskini ipatikane nchini.
                Nina wasiwasi pia kwamba baadhi ya taasisi husika zisipojiangalia upya zitajikuta zinachangia badala ya kupunguza umaskini. Na hili linatokea kutokanana kanuni na taratibu zilizopo na maombwe katika  masuala mbali mbali        ya kiudhibiti na kiufuatiliaji.
                Katika kutoa mchango wangu kuimarisha sekta hii muhimu nitabainisha mambo kadhaa ambayo yanastahili kuzingatiwa na taasisi za kifedha na mikopo nchini ili ziwe na mavuno bora na makubwa zaidi.
                Kwanza, taasisi zikopeshe biashara au mradi na sio mtu. Hali ilivyo hivi sasa ni kwamba Ali au Agnes ndiye anayekopeshwa. Na taasisi nyingi humuangalia na kumtathmini Ali au Agnes na sio biashara au mradi husika. Ali au Agnes huwa hafundishwi wala kufahamishwa juu ya tofauti yake yeye kama mtu na biashara au mradi wake kama mtu kisheria. Hii ni kasoro inayochangia si haba kushindwa kwa watu wengi  kurudisha fedha wanazozikopa.
                Wafanyakazi na wadhamini wafanze kazi kiurasimu na kiufundi zaidi. Pale wafanyakazi na wadhamini wanapokuwa na roho ya huruma na kutaka kusaidia mtu badala ya kumuwezesha mtu kiuchumi/kimkopo ndipo penye kiungo dhaifu kuliko vyote katika mlolongo mzima wa mikopo na ulipwaji wake. Ni muhimu tukajifunza kwamba nia, dhamira na uwezo wa mtu kujiondoa toka kwenye umaskini kwa juhudi na maarifa yake mwenyewe ni jambo kubwa kama ulivyo msaada wa fedha kumuwezesha kufanya hilo. Lakini yule anayeona ni rahisi kukopa na asifanye la maana na kisha kuirusha taasisi husika hachangii vita vyetu dhidi ya umaskini bali anaongeza umaskini wetu. Na watu wa namna hiyo kila kona ni watu wa kupigwa vita na kutangazwa kama maadui wa maendeleo.
                Pasiwe na mikopo isiyo na akiba.  Baadhi ya taasisi husika kwa kudhania kwamba zinawasaidia maskini, zimeamua kutoa mikopo bila sharti la mpewa mkopo kuwa na akiba katika akaunti yake. Ninaamini hili ni kosa na lina hatari kubwa zaidi ya kuchangia umaskini kuzidi badala ya kupungua kwa wale wanaokopeshwa.
                Akiba na uwekaji na utunzaji wake ni sehemu muhimu na isiyoonekana katika mfumo wowote wa kibenki na kifedha. Usipokuwepo chochote kinaweza kutokea ndani au nje ya uwezo wa wahusika na kuleta hasara na majuto makubwa zaidi. Ninaamini, wakati umefika wa Benki Kuu kuhakikisha kuwa taasisi zote za fedha ndogo kwa kubwa zinazotoa mikopo sio tu hazitoi mikopo kwa  mtu asiyekuwa na akiba hai bali pia na taasisi zenyewe zinakuwa na akiba kiasi fulani katika benki za biashara na benki kuu.
                Uwekezaji unaonufaisha wanachama wa taasisi za Kifedha.  Wakati umefika sasa ili kupunguza gharama na riba kwa wajasiriamali, taasisi za fedha kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika miradi sahihi inayochangia kumuendeleza mwananchi na kupunguza umaskini kiujumla nchini. Ubia ukianzishwa na mabenki makubwa, mifuko ya hifadhi, bima,makampuni na  watu binafsi ndani na nje ya nchi wenye uwezo na wanaotaka kutoa mchango wao katika vita dhidi ya umaskini kuna mengi yanaweza kufanyika tena kibiashara na taasisi husika na hivyo mwisho wa siku gharama na kiasi cha riba kinacholipwa (na wale ambao kwao riba si haramu) isiwe kikwazo bali kichocheo cha kukopa na kujiendeleza.
                Kuwashirikisha wanafamilia kiuwazi na kimkakati zaidi. Hali ilivyo hivi sasa ni kwamba baba au mama na jamaa wa familia husika wanahusishwa kama vile ni amana ambayo itadaiwa pindi mkopaji anaposhindwa kulipa deni lake.
                Ninaamini njia nzuri zaidi ni kumshirikisha baba au mama kama sehemu ya mkopo ili kuondoa hatari za baba au mama wanaokopa bila mume au mke kuwa na habari ya hili au lile. Aidha, kwa wale ambao  mikopo yao inatolewa bila mtu kuwa na akiba kwa upande wangu ninahofu kuwa utaratibu wao unaziongezea familia umaskini zaidi badala ya kuupunguza.
                Uchunguzi wangu binafsi umebaini kwamba kuna tabia ambazo pia zinawakera wakopaji ambazo ingelifaa zikomeshwe ili kujenga mahusiano bora zaidi kati ya taasisi husika na wakopaji wake. Ya kwanza, ni ile ya taasisi kutuma 'jeshi zima' kukabili mkopaji na familia yake pale panapotokea tatizo. Hili linaonesha kuwa mawasiliano kati ya wadhamini wa mkopaji na taasisi bado ni duni na yanastahili kuimarishwa toka siku ya awali. Hii ina maana kwamba mkopaji anaweza akapewa fedha na kuzitumia bila wadhamini kujua kinachoendelea. Na anakuja kushtuliwa pale tu ambapo mkopaji kaingia kwenye matatizo.
Laiti wadhamini wangelitambua toka awali wangeliweza kuweka njia zao wenye za kufuatilia au kujiandaa kwa lolote litakalotokea kuliko kushtuliwa na makomandoo wa mikopo mitaani.
                Jambo lingine ni tabia ya baadhi ya taasisi kuwafungia wakopaji wake ndani (kifungo cha muda) eti kwa kuwa huo ni utaratibu wa kuwalazimisha kumlipia mwanachama mwenzao aliyekwama kurejesha marejesho. Katika sheria za asili (natural justice) hili ni kosa, maana kama ilivyokwisemwa na wahenga kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe!
                Badala ya majeshi ya kudai mikopo kuwa ndiyo kitu kinachoonekana mara kwa mara mitaani, ninapendekeza kuwe na majeshi ya kuwasomesha na kuendeleza biashara za wakopaji.
                Endapo patakuwa na vijana mahiri katika menejimenti, oganaizesheni, usimamizi, udhibiti  na uongozi wa masuala ya biashara na taasisi hizi zikaja pamoja na kuwa na vitabu vya menejimenti na uongozi kwa Kiswahili nina hakika kasoro zinazotia hofu na uoga mabenki na taasisi za fedha nchini kumkopesha Mtanzania baada ya muda sio mrefu zitakuwa ni historia.
                Katika miaka ya 60 Japani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia ilianza kuzaliwa upya. Mkunga aliyetegemewa katika mazazi hayo hakuwa mwingine ila benki zilizoona mbali na mbele za Kijapani. Marehemu Matsushita (National na Panasonic), Akio Morita (Sony) achilia mbali wakina Toyoda na wengineo walibebwa si haba kutoka utoto wa ujasiriamali hadi kufikia makampuni makubwa tunayoyaona duniani leo. Siri ya mafanikio yao ilikuwa ni kwamba benki zilikuwa zikiwafuata wao kule waliko na wala sio wao kuzifata benki.
                Benki zilikuwa kwa Wajapani wakati huo kama baadhi yake zilivyo leo ni wabia wa wafanyabiashara, wenye viwanda na wajasiriamali. Wakati mwingine huyu akimbeba yule, na yule naye kwa wakati wake akimbeba huyu.
                Tanzania sio masikini tu kwa sababu inashindwa kuchimbua utajiri ulio katika ardhi yake, lakini kubwa zaidi ni kuwa umaskini wetu unatokana  pia na mabilioni ya fedha kufungiwa ndani badala ya kuwa mitaani kuendesha injini ya uchumi wa taifa letu. Wakati umefika wa taasisi za fedha na mikopo kwanza kutoa elimu na mafunzo yanayohitajika, kisha wakawa wabia na wajasiriamali na makampuni madogo na kisha wakawa wateketezi muhimu katika sera zinazochangia kukuza na kupanua uchumi badala ya kulea na kudekeza uchumi unaochangia kuwa na matajiri wachache lakini maskini wengi.
                Nionavyo mimi, muamko mpya wa serikali katika kuwatumikia Watanzania kwa njia bora zaidi hususan katika sekta za fedha na kodi kunaashiria kuwa serikali itakuwa mbele kuwasaidia wale wote watakaotaka kuwasaidia makini wa Tanzania.
Baada ya kumalizia tu makala haya, nilitazama mdahalo wa Barrack Obama (Democrats) dhidi ya Mitt Ronney (Republicans). Kinachodhihirika  hapa ni kwamba changamoto za kiuchumi, kibiashara na kimaendeleo ni sehemu ya maisha.  Tunastahili kujipanga, kujifunza na kujiendeleza kila siku ili kufanya vizuri katika masomo hayo ya maisha. Elimu, mafunzo, utafiti na ushauri viwe ni vitu vya mazoea na kawaida na sio vitu vya kukurupuka kukurupuka tu. Asiyejiendeleza hawezi kujiendeleza, wasiojiendeleza  hawawezi kuendelea.

JKT karne ya 22 inatakiwa iwe vipi ?




Watanzania  wanatarajia kwamba hadi inafikia mida hii ambayo JKT litayari kufungua milango yake kwa wanaJKT wa kizazi kipya kwamba kuna mipnago dhahiri ya muda mfupi na mrefu kuhusu uendeshaji wake; kuna mikakati-mipango sadifu, kuna sera tambuzi na shirikishi na kuna masahihisho kadhaa yaliyofanzwa ili kuoanisha  malengo mapya katika nyakati mpya kwa uendeshwaji wa JKT ijayo. Na kwamba JKT ikisaidina na majeshi yetu mengine itakuwa ndio kichwa cha garimoshi au injini ya kuiendesha Tanzania mpya itakayokuwa inatengeneza na kujenga karibu kila kitu kwa kutegemea rasilimali zetu wenyewe ikiwemo rasilimali watu.
                Kufanya hili lazima pawepo na mpango wa uendeshaji wa mwaka mmoja; mpango wa miaka mitatu - mitano (hususan kuhusu rasilimali mbalimbali)  na mpango wa muda mrefu wa miaka 25-50 inayolenga kuingiza nchi kwenye mabadiliko makubwa kila baada ya muongo mmoja.
                Mipango hii itarahisisha kufahamu ni kwa namna gani JKT itaoanisha matumizi na mapato yake katika uendeshaji wake. Lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa inakuwa ni taasisi inayojiendesha yenyewe bila kutegemea ufadhili toka nje au ndani ya nchi.
                JKT ikiweza kujiendesha yenyewe bila ufadhili na kwa  hiyo kujitegemea itazalisha vijana wanaoweza kujiajiri wenyewe na kujitegemea bila kutegemea kuajiriwa kama njia ya mtu kujipatia riziki yake ya kila siku.
                Mpango-mkakati ni muhimu kwa kuwa mpango huu ndio unaoisadia taasisi yoyote ile iwayo kujua mahala ilipo na inakotaka iwe baada ya miakafulani.
                Ili kufanikisha hili ni lazima tubainishe wazi malengo ya JKT. Bila shaka katika mustakabali wa sasa lengo moja litakuwa ni kuwaunganisha vijana  wenye itikadi tofauti na wanaounga mkono vyama tofauti vya kisiasa kujenga utamaduni wa ushindani-shirikishi, ushindani unaojenga badala ya kubomoa kwa kuheshimu misingi ya haki na usawa kwa kila Mtanzania. Na kwamba vijana wa Kitanzania kuanzia sasa hawatatiwa upofu wa kuchagua kilichooza na kuacha kilicho bora kwa namna yoyote ile.                  Na juu ya yote mtu yeyote mwenye kupiga vita mfumo wa vyama vingi na demokrasia ni adui na sio rafiki wa Watanzania. Na kwamba mtu yeyote anayetumia hila, hadaa, rushwa, fedha na ujanja wowote ule uwao ili kupata cheo au uongozi ni mtu wa kutliwa mashaka makubwa katika safu za uongozi wa taasisi na maeneo mbalimbali nchini.
                Tofauti na huko nyuma katika miaka hii ya upasho na uamsho upo umuhimu wa makambi ya JKT mpya kuheshimu imani  za wanakambi na uhuru wa watu kuabudu na kufuata maamrisho ya dini zao bila kukwazwa na kitu au mtu. Hili likifanyika litawaondoa wazazi hofu kuwa watoto wao wanaweza kwenda kuharibiwa au kupotoshwa JKT.
                Ninategemea pia kuwa JKT itafafanua dhana ya uzalendo iwe pana na wazi zaidi na ianyoendana na wakati. Kwangu mimi Uzalendo sio kukubali kuwa kondoo na kutii au kuridhia kila jambo linaloanzishwa au kuamriwa na wakubwa hata kama ni kosa au uovu; na wala uzalendo sio mavazi, ulimbwende na mapambo yenye rangi za bendera ya taifa.
                Uzalendo ninavyouelewa mimi ni hali ya juu ya utu na ubinadamu inayofikiwa katika nchi fulani. Uzalendo ni juu ya familia, urafiki, ukoo, kabila, imani, uchama na uwana- kikundi wowote ulekatika jamii husika. Mzalendo kwa maneno mengine ni mtu aliye juu ya mambo yake binafsi na ya kifamilia, juu ya masuala ya ukoo na ukabila, juu ya dini au imani yake na ni juu ya siasa za kichama pale utaifa unapohitajika kuwa juu ya kitu kingine chochote.             Aidha, mzalendo ni mtu anayefahamu katiba na sheria za nchi yake na ni mwepesi wa kuhoji na kuuliza ili kupata majibu sahihi kabla ya ya kufanya maamuzi yoyote ya kisiasa, kijamii au kiuchumi, aghalabu, akiliweka taifa lake na utaifa wake mbele ya mtu au kitu chochote kile kiwacho.
                Ili kudadavua na kuibua melengo yanayofaa ni kitu muhimu tuanze kwa kuangalia matatizo au changamoto zinazowakabili Watanzania mijini na vijijini.
                Changamoto hizo ni pamoja na umaskini unaotufanya tushindwe kulipa ujira unaokidhi mahitaji ya wafanyakazi mbalimbali na hivyo kuzusha matatizo ya rushwa, migomo, mitafutano na mengine kama hayo; aibu ya watu wetu kukosa nyumba, maji na umeme na mahitaji mengine ya msingi katika karne hii; mbinu duni katika kilimo na uzalishaji na biashara ya chakula;  kushindwa kutumia bahari, kushindwa kuunda vyombo vya kisasa ili kutajirika na rasilimali bahari na rasilimali kwa ujumla;  kukosa uwezo wa kuchimba na kuuza madini yetu sisi wenyewe na hivyo kuachia wageni kutuibia mali asili zetu kushoto na kulia; ushirikishwaji duni wa Watanzania katika maamuzi na uendeshaji wa nchi yao na mambo yake; kuweza kuwa na mashirika ya umma lakini tukashindwa kuwawezesha Watanzania wengi zaidi na hususan vijijini kumiliki kampuni, biashara a miradi yao yenye kuingiza kipato cha uhakika; kufulia kiteknolojia na  kiviwanda na hivyo kusababisha  kununuliwa kwa kila zana au kifaa toka nchi za nje;  Kushindwa kuitumia teknohama na mifumo ya kidijito kuharakisha maendeleo ya nchi kwa kasi kubwa zaidi;  kushindwa kutoa matunzo na  malezi kwa wazee, masikini, watoto wa mitaani na wajane;  kushindwa kuendeleza miundombinu na mahitajio mengine ambayo yangeweza kumuwezesha kijana wa Kitanzania kung'aa katika soka, riadha, michezo mbalimbali, filamu, maigizo, muziki na sanaa mbalimbali.
                Pasina ushirikishwaji wa dhati na uhakika wa masikini nchini ambao ndio idadi kubwa ya watu wetu hatutakwenda popote.                                Lazima JKT mpya iwe na kitengo mahsusi kinachokaa, kufikiri na kutekeleza hatua mbalimbali zitakazochangia kupiga vita umaskini nchini kwa vitendo na sio kwa nadharia na maneno.
                Kuna wakati JKT iliwakawaka katika kilimo. Nina hakika hali hii inaweza kurejeshwa pakiwa na ushirikiano kati ya JKT, vijiji na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi hasa kilimo na uzalishaji wake kitakapolenga matakwa ya wahitaji binafsi na kile wanachoagiza kikazalishwa kwa viwando vinavyokubalika.
                Ili mapinduzi ya kilimo yafanikiwe JKT inastahili kuzalisha zana mbalimbali za kilimo ikiwemo matrekta, kombaini havesta, malori na mitambo ya kuhifadhi na kusindika vyakula. Ni aibu miaka 50 baada ya uhuru kushindwa kutengeneza vitu kama hivyo sisi wenyewe.
                Aidha, katika mikoa inayopakana na bahari, maziwa na mito mikubwa nitategemea kuiona JKT katiika maeneo hayo sio tu ikijiingiza katika uvuvi na uvunaji rasilimali maji bali pia ikiunda vyombo vinavyohitajika na sekta hiyo ili kuisasaisha au kuifanya ya kileo zaidi.  
                Katika maeneo yenye madini ninatarajia kuona vitengo ndani ya JKT vinavyoharakisha kuwawezesha vijana wa Kitanzania kuwa wachimbaji madini na waendeshaji na wasimamizi wa migodi yetu ili tuonokane na kuibiwa waziwazi.
                Ninaamini makambi mbalimbali ya JKT yatakuwa na vyuo kwa vitendo vitakavyowafundisha vijana sio tu ujasiriamali bali taaluma zote za uongozi na utawala ikiwa ni pamoja na ubingwa wa kupanga, kusimamia rasilimali, kudhibiti mambo, kutafuta masoko na uzalishaji na uuzaji wa kile kinachozalishwa. Chuo hicho kwa kufanya mambo yake kwa vitendo ninakitarajia kuwa kitakuwa ndio eneo la  kupanda mbegu za kuzlisha makampuni ya kijamii kwa watu wa maeneo mbalimbali nchini.           
                JKT ijayo haiwezi kukwepa kuwa na kitendo cha teknolojia na teknohama ili kuiwezesha nchi na hususan vijana kwenda na wakati. Nitategemea watu hodari katika masuala ya kompyuta, simu, tovuti na mawasiliano watakuwa vijana waliopitia na kusomea mambo haya kwa vitendo na sio nadharia tu. JKT kwa maneno mengine itakuwa wadi ya uzalishaji miradi mbalimbali ya kiteknolojia na kiteknohama itakayochangia kuharakisha maendeleo ya Tanzania. Hususan katika matumizi ya tovuti yatakayosaidia kuwakutanisha watu kiteknohama toka Ulaya, Asia, Amerika na kwingineko Afrika wakaanzisha na kuendesha mradi hapa nchini.
                JKT ijayo lazima iwe na kitengo cha ustawi wa Jamii na kufanya kazi ambayo wizara ya afya na ustawi wa jamii meshindwa kwa kiasi kikubwa kuifanya inavyostahili.
                Kama ilivyo kwa makundi hayo hapo juu wanamichezo na wasanii wa Tanzania nao wamejikuta ni mayatima. Ninaamini JKT tena kwa faida kubwa sana inaweza kuingilia kati katika hili na kugeuza hali ya mambo ilivyo leo na Tanzania ikaanza kunufaika vilivyo na vipaji vya vijana wake.
                Hayo hapo juu yana maana kwamba JKT inastahili kuwa na mafunzo ya muda mfupi katika masuala ya matumizi sahihi ya silaha, ulinzi na uasktari (pengine miezi mitatu tu) na kisha vijana wakagawanywa katika idara mbalimbali  zenye majukumu ya kutekeleza changamoto hizo hapo juu (kwa miezi sita -tisa au hata zaidi)  kwa ufanifu na ufanisi mkubwa kila mwaka kuanzia pale itakapoanza rasmi.

Katiba iweke sawa udhibiti fedha, hazina na maliasili za nchi


BILA shaka wachangiaji kwenye uandaaji wa katiba mpya wamezungumza mengi juu ya katiba waitakayo. Binafsi, hata hivyo, ninaamini kwamba yote yanayozungumzwa yatakuwa hayana maana kama udhibiti fedha za serikali, hazina/benki kuu na mali asili za nchi havitakuwepo.
Kwa namna fulani kila tatizo, kubwa kwa dogo, linalosababishwa na serikali, watumishi wake na vyombo vyake hapa nchini linahusiana kwa namna moja au nyingine na udhaifu katika udhibiti fedha za walipa kodi, hazina/benki kuu na mali asili za nchi kama vile madini, misitu, maji, wanyama na vitu kama hivyo.
Ninasema udhibiti kwa sababu vitu hivyo kama vilivyo havina tatizo. Tatizo linakuja mkono wa mtu ukishaingia kwa kutumia cheo, nafasi au wadhifa wake katika taifa. Kwa maneno mengine, tatizo la Watanzania linatokana na vitu vilevile Mwalimu Nyerere alivyosema tunastahili kuwa navyo ili TUENDELEE.
Kwani watu wamezunguka ardhi, siasa na uongozi na kugeuza nyenzo za kutusaida kuendelea kuwa nyenzo za kutusaidia kuhujumiana, kufisadiana, kuminyiana, kutambiana na wengi wetu kuzidi kubaki nyuma kimaendeleo vijijini na mjini.
Hii ina maana tatizo la Tanzania leo ni watu. Sio vitu. Vitu havina matatizo. Ardhi haina tatizo kama ilivyo mistiu au wanyama pori au gesi au peteroli au barabara au bandari au TTCL au TANESCO au TAZARA au TRC au kiwanja cha ndege na kadhalika. Watu wanaosimamia au wanaotakiwa kuendesha vitu hivi ndio wenyewe matatizo. Watu ndio tatizo.
Na matatizo yenyewe yanakuja kwa njia mbili. Aidha watu hawana uwezo wa kuviendesha kwa sababu hawajawahi kusimamia vitu kama hivyo na wamepewa zawadi kuviendesha au wapo wenye uwezo wa kuvisimamia na kuviendesha lakini mifumo na muundo wa serikali na vyombo vyake kama ulivyo vinachangia kuua tassisi husika kuliko kuzisaidia kuendelea mara nyingi kwa kukosa usimamizi na udhibiti wa kutosha.
Majibu ya matatizo mengi ya kikatiba na uendeshaji kwa bahati nzuri yapo katika mafunzo ya uandishi wa habari.
Hususan somo la kwanza tu katika uandishi wa habari linamtaka mwanahabari kuuliza na kujibu maswali ya NANI, NINI, KWANINI, WAPI, LINI na KWA NAMNA GANI ? Maswali haya yakijibiwa kwa kiwango kinachokubalika mtu huwa na taarifa kamili inayomrahisishia kufanya maamuzi sahihi. Kinyume chake, aghalabu, utakuta ni maamuzi mabovu na dhaifu.
Kwa mfano, wale wanaozungumzia rais kupunguziwa madaraka ni kwamba wanauliza NANI au NINI kilichompa madaraka hayao; KWANINI kapewa madaraka hayo wakati huo na kwa NAMNA GANI? Na madaraka hayo wakati wa mfumo wa chama kimoja yalitumika vipi na wapi na kama katika mfumo wa vyama vipi yanatumika kwa usahihi? Na wakati huo (LINI) yalipotumika yalisaidia au kuchangia kitu gani na kama katika wakati wetu bado anastahili kuwa nayo? Na kama ni kumpunguzia tumpunguzie kwa NAMNA GANI na kwa faida na hasara ya NANI?
Umuhimu, uzito na uzuri wa maswali haya ya kiasili katika uandishi yanasaidia si haba kupata taarifa toshelevu kufanza maamuzi mbalimbali na kuwa na ukamilifu au uyakini wa kile kinachoandikwa. Isitoshe kila NANI inaweza kuzaa nini, kwanini, wapi, lini na kwa namna gani zake kama hizo nazo pia zinavyoweza kuzaa nani na hao ndugu zake katika muktadha na mustakabali wa kila jambo ?
Binafsi ninajikita zaidi leo na suala la katiba na umuhimu wa udhibiti wa fedha, hazina na maliasili za nchi, jambo ambalo kwa upande wangu ninaamini limeifanza katiba yetu leo kuonekana na walakini na serikali na uongozi mzima kuonekana dhaifu na usiotimiza ipasavyo wajibu wake.
Uzuri wa katiba kwa maneno mengine hautokani na katiba kuwa nzuri kimaandishi na kinadharia lakini kiwango cha udhibiti wa vitu muhimu vinavyofanya kuwepo na nchi inayoendelea au isiyoendelea; masikini au tajiri, yenye ukweli au uongo katika takwimu zake na yenye ungozi imara au u0ngozi dhaifu. Kwa maneno mengine hadhi ya kiwango fedha za mlipa kodi na kipato cha nchi kinavyotumika kumfaa mlipa kodi ndicho kiwango cha ubora wa katiba ya watu na nchi husika. Fedha na hazina ya nchi inavyotumika kuwafaa zaidi wananchi wote kwa umoja wao ni ushahidi wa katiba bora, na fedha za walipa kodi zinavyotumika kuwafaa walioko uongozini na maswahiba zao tu ndio dalili na ushahidi wa katiba mbovu na utawala dhaifu.
Ili kuona kana kwamba tuna katiba mbovu au nzuri tuyatumie maswali yale ya NANI, , NINI, KWANINI, WAPI, LINI na KWA NAMNA GANI kujiuliza kwa namna moja au nyingine baadhi ya maswali yaliyomo katika mtiririko huo hapo juu. Njia mbalimbali zinaweza kutumika, na ha hakuna njia iliyo bora kuliko nyingine ila ile inayomsadiai mtu kujenga uelewa na ufahamu bora zaidi wa jambo husika na hivyo kumuweka mahala anap;oweza kutoa majibu sahihi zaidi na kufanya maamuzi bora kuliko kama atakuwa ameshindwa kuuliza maswali hayo hapo awali.
Maswali haya ya NANI, NINI, KWANINI, LINI, WAPI NA KWA NAMNA GANI yanaweza kuulizwa kwa njia mbalimbali lakini azma kubwa ikiwa ni kupata majibu sahihi ya kututwezesha kuwa na vifungu tambuzi, bainifu na vinavyoona mbali katika katiba mpya ili katiba hiyo kiukweli iweze kutufaa kwa miaka 50 kama sio mia.
Binafsi kama kichwa cha insha yangu kinavyoonyesha nitajikita zaidi kwenye udhibiti na ufuatiliaji masula niliyoorodhesha hapa chini, kwa maana, ya kuuliza maswali ambayo yatatusaidia kupunguza kama sio kuondosha kabisa mapungufu yalipo hivi leo. Narudia tena, hii ni njia moja tu, ya kuuliza maswali kama haya nawe ukiwa na muktadha na mustakabali tofauti unaweza kuyauliza kwa njia tofauti na ile ninayoitumua mimi.
. Hali ilivyo hivi sasa. Je, ni NANI na amefanya kitu gani au NINI kutufikisha hapa tulipo leo? Je, imejitokea kwa ajali au kwa kukosa uongozi mzuri au kutokana na watu kushindwa kujua wanatakiwa wafanye NINI? KWANINI tunataka mabadiliko. Ni WAPI kuna umuhimu wa mabadiliko kwa NAMNA GANI na kwa kiasi gani. Je, hayo yakishafanyika kutakuwa na mabadiliko yanayohitajika hivi leo? Ni NANI, tofauti na huko nyuma atakayepewa jukumu la kuisimamia na kudhibiti KATIBA MPYA ili yote tunayokubaliana yasiwe yanaonekana tu yamekubalika kufanyika lakini yanafanyika KIKWELI KWELI.
. Chama, vyama na siasa. Katiba iliyopo ina nasaba na mfumo wa chama kimoja, je, Katiba mpya itakuwa inafanana na kutosheleza mahitaji ya mfumo wa vyama vingi na demokrasia au siasa za uwazi na ushindani. NANI atahakikisha kuwa VYAMA na Watanzania wote kwa ujumla wananufaika na mabadiliko katika katiba mpya? Ni kwa kiasi gani rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala anaweza akadhibiti serikali kutokipa chama chake fedha wakati kinazihitaji? Na, je, Gavana wa benki kuu atakataa pale chama kinapomuamrisha kukilipa kwa jambo lisiloeleweka ili mambo yake yafanikiwe? Katiba itatusaidia WAPI, KWANINI, LINI, VIPI na KWA NAMNA GANI ili hili liwe ni historia katika nchi yetu?
. Serikali, viongozi, wizara na watumishi wake. Je, viongozi walioppo madarakani ni akina NANI, wanapata NINI, na wanachokipata wanakipata KWA NINI. Haki waliyo nayo ilianza WAPI, LINI na KWANINI. Je, katika katiba mpya tutegemee mabadiliko gani chanya?
. Mikoa. Je, mikoa hivi leo inaongozwa na NANI na wanaongoza na wanaowachagua wanapata nini. Uhalali wao na wanachokipata unatoka WAPI ? LINI wanakipata na KWANINI wanakipata. Na KWANINI wanaogoza mikoa wasiwe watu wa kuchaguliwa badala ya wa kuteuliwa?
. TRA. Je, watumishi wa TRA wanalipwa tofauti na watu wengine? Uhalali wa hili ni NINI ? Umeanzia WAPI, LINI, KWANINI na kwa NAMNA GANI ? Hili linasaidia kuwa chachu katika maendeleo ya sekta nyingine au ni chanzo cha matatizo kwa watumishi wengine wa serikali? Na zaidi ya rais mwenyew, je, ni kina nani wanaodhibiti TRA na watumishi wake? Na, je, hao waliopewa kazi ya kuidhibiti TRA wanapata ujira na maduhuli sawa na watumishi hao?
. Benki Kuu, Hazina na taasisi nyingine za fedha. NANI anasimamia na kudhibiti mali zilizoko Benki Kuu? Kwa mfano kukiwa na dhahabu huko gavana peke yake anaweza akaamua kuiuza bila kumuarifu mtu yeyote? Je, hakuna uwezekano wa mtu toka kwenye serikali au chama tawala kuilazimisha benkii hiyo kulipa kisichostahili kulipwa? Benki kuu inatakiwa iendeshweje ili kuzuia mianya ya UFISADI na malipo yenye mashaka na wakati huo huo benki hiyo kuwa chachu kwa vijana na hususan wajasiramali kuanzisha miradi na makampuni yatakayotutoa toka kwenye umaskini?
. Mifuko ya pensheni na hifadhi za jamii. NANI anamiliki mifuko ya pensheni na hifadhi za jamii. Kama serikali ilishajaribu kumiliki makampuni na kisha ikashindwa KWANINI serikali isiwawezesha Watanzania mmoja mmoja na katika vikundi wao kuanzisha makampuni hivi leo. Na KWANINI wanachama wa mifuko kama hiyo wasiwe na haki ya kupewa HISA na mifuko hiyo?
. Kilimo na dada zake na mchango yao katika maendeleo yetu. NANI anastahili kusimamia shughuli za KILIMO. Na NINI kinachotokea sasa. KWANINI yanayofanyika sasa yanafanyika. Ndio kwanza yameanza au yalianza LINI na WAPI na KWA NAMNA gani na yanamfaa NANI?
. Viwanda na Uzalishaji mali na nafasi ya vipengele muhimu kubadili hali iliyopo. NANI alitaifisha viwanda, KWANINI akatii WB/IMF na sio kuiga mfano wa Uchina na ilivyobadili muundo na mfumo wa umilikaji wa makampuni ya umma ya Kichina na kushirikiana na sekta binafsi? Je, ni kweli makampuni ya umma yalitushinda kuendesha au waliochaguliwa walikuwa ni uozo na walichaguliwa kichama zaidi na sio kiutaalamu zaidi?
. Migodi, mali asili na michango yake na katiba ifanye nini ili kuongeza michango hiyo. NANI aliyetoa ruhusa ya kubinafsisha sekta ya madini. Katika kufanya hivyo serikali Ilipata NINI na yeye akapata NINI ? Je, leo tunapata NINI na kitu gani kifanyike WAPI, LINI NA KWA NAMNA GANI ili tupate sio tu manufaa zaidi bali tuweze kujifunza sisi wenyewe kuchimba na kumiliki migogi yetu kama Venezuela, Uchina na nchi kama hizo? . Mikopo ya ndani na toka nje ya nchi. Je, mikopo ambayo serikali inakopa toka kwenye mabenki na vyombo vya fedha vya ndani pamoja na ile inayokopwa toka nchi za nje inamfaa NANI, na anayenufaika anapata NINI, na KWANINI ni huyo au hao ndio wanaopata na sio mwingine au watu wengine?
Hili linahusu pia misaada na jinsi nchi inavyonufaika au inavyoathirika na misaada kama hiyo. . Elimu na Vijana. NINI kimetokea katika elimu toka kufa Azimio la Arusha. ? NANI ananufaika na NANI anahasirika. KWANINI kinatokea kinachotokea? WAPI wanaangaliwa na wapi wanasahauliwa? Watu watavumilia hadi LINI na mabadiliko yataletwa na nani na yanaweza kuja KWA NAMNGA GANI? Katiba itachangia nini katika hili, ilikuhakikisha aina na mfumo wa elimu tulionao ni ule unaowanufaisha wengi na sio wachache?
. Mahitaji ya Msingi na vyanzo vya uhai. Je, pamoja na baadhi yetu kuelezea na kuelezea umuhimu wa mahitaji ya msingi kutangulia kwanza vitu vyote, yaani, watu wapate kwanza hakika ya kupata chakula, maji, tiba, usalama wao na mali zao, hewa safi, mazingira bora, nyumba, ndoa, elimu hadi sekondari, ajira ni NANI anayepuuza hili. Anapata NINI kwa kupuuza ? KWANINI mahjitaji ya msingi kama vile nyumba kwa viongozi wetu wengine eti yanaonekana ni anasa? Na wanamtupia mgonjwa kutibu wagonjwa na masikini wenzie?
. Tofauti ya kipato. Je, NANI amefanyia utafiti wa kina juu ya tofauti ya kipato nchini? Anayeruhusu au wanaoruhusu tofauti hizi kuanza na kuendelea kukua anapata faida GANI na ni NANI na yeye anapata NINI. KWANINI tunakosa sera ya kitaifa (siyo ya kichama) katika hili? WAPI kuna watu wenye mtazamo na msimamo tofauti. Wanachgaia yepi, LINI tutawasikia na tutarajie mabadiliko yaje katika njia gani? IKiwa hapatakuwa na uwazi na udhibiti katika mambo haya, je, haitatokea kuwa nchi au serikali inaweza kushindwa kuendesha mambo yake kwa kuwa imejipanga kufanya mambo kiujanja ujanja na kutumia mabavu na sio busara na hekima katika maamuzi yake mbalimbali ? Je, Katiba mpya inawezakuzuia vipi jambo kama hili kutokea na kuhakikisha wakati wote kuna mipaka dhahiri kati ya serikali na vyama vya siasa, viongozi na watumishi wa serikali, na kwamba watu kwa umoja wao wanakuwa ndio waamuzi wa mwisho kuhusu hatima ya nchi yao na sio chama cha siasa au kikundi chochote kiwacho?

Tuna Uhuru wa Bendera, bado Uhuru wa Aina Zingine…


NCHI nyingi za Kiafrika zitakuwa zinafikisha nusu karne mwaka huu au mwaka ujao kama nchi huru. Uhuru huo wa kisiasa au uhuru wa  bendera au uhuru kutoka kutawaliwa na mgeni na kutawaliwa na mwenyeji ni mchakato wa asili kama vile watoto wa kiume au wakike wanapofikia umri wa kuoa au kuolewa na wanavyotoka nyumbani kuanzisha nyumba yao mpya.
                Bila shaka wengi wanajiuliza je, uhuru tuliopigania ulikuwa ni uhuru mmoja au uhuru wa aina nyingi? Jibu lake ni wazi hapa litakuwa kwamba uhuru tuliopigania sio uhuru wa aina moja, bali uhuru wa aina nyingi. Hapa tunachukulia neno uhuru kuwa ni pamoja na staha, heshima, kiwango stahilivu, uwazi na uwajibikaji wanaopewa majukumu mbalimbali kieneo na kitaifa.
                Watu wanajiuliza je, hivi, Watanzania na Waafrika kwa ujumla wakipata uhuru wa kujifunza na kuelewa na hata kuigeuza nadharia kuwa vitendo katika elimu na maarifa mbalimbali  ya dunia ikiwemo kujifahamu na kufanyia kazi kwa vitendo lugha yao ya asili, katiba na sheria za nchi yao ?
                Je, nini kitakachotokea ikiwa kama Watanzania na Waafrika watapata uhuru na demokrasia pana, kiasi cha kuwa na uhuru wa kukichagua chama chochote cha kisiasa kuingia madarakani na pale kinapoboronga iwe rahisi kukiondoa kama walivyokichagua bila mikwara kutoka vyombo vya dola vikiwemo vile vya usalama ? Tutakwenda mbele kijamii na kiuchumi au tutarudi nyuma ?
                Je, hivi hapa Afrika viongozi na watawala wetu wanaridhia, kuchangia na kusaidia
kuona kwamba watu wao wanakuwa na uhuru wa kuiwajibisha serikali na vyombo vya dola au wanawazuia kupata uhuru huo ?
                Je, ni nini kitakachotokea kama Watanzania na Waafika kwa ujumla wanakuwa na uhuru wa  kunufaika kwa mapana na marefu kutokana na ardhi yao na mali asili zao na isiwe ni viongozi na wageni tu ndio wanaonufaika na vitu hivyo ?
                Mathalani, hivi sasa wanaonufaika na ardhi ambayo chini yake kuna madini au vito vya thamani ni viongozi, wanasiasa na wale wanaopewa leseni kuvichimba vitu hivyo. Je, inapojulikana ardhi ya kijiji fulani iko juu ya mgodi wa dhahabu kwanini watu hao wasitajirike kutokana na kuwa wenyeji asili wa ardhi yao wakanufaika tu watu wengine?
                Je, uhuru wa kuzungumza,  kuchanganyika na watu, kuandamana, kufanya mikutano na kuwa na uhuru wa kuabudu na kuwa na mawazo tofatuti na watu wengine ni kitu kinachoheshimiwa na kuvumiliwa au kinashambuliwa na kinapigwa vita kwa kila hali ? Dhahiri au kwa siri ?
                Hivi kweli Waafrika walio wengi wana haki  ya kusafiri na kutembelea nchi nyingine za Kiafrika na ulimwengu. Upo au kuna usanii na porojo kwa kuwa mazingira yameandaliwa kumfanza Mwafrika asiwe na uhuru kama huo?  Na ni wachache wenye uwezo wa kutembea na kuona mikoa mingine ya nchi yao, achilia mbali uhuru wa kuona nchi za nje na huku watu wanataka kukuza utalii wa ndani? Nini kinachofanzwa ili watu wawe na uhuru wa kweli wa kusafiri ikiwa ni kuwepo kwa vyombo vyenye staha na heshima, gharama nafuu na ubora wa kuridhisha?
                Hivi Waafrika ni kati ya watu ambao wanahesabika kuwa na uhuru wa maji na  chakula. Nikiwa na maana ya uhuru huo kuwa ni pamoja na haki ya kupata maji safi na chakula chenye lishe tosha ukiwa mjini au kijijini? Au mahitaji haya ya msingi wanayapata wachache na linachukuliwa kama jambo la kuwaringia na kuwakoga wasiovipata?
                Je, Afrika kuna uhuru wa kusikilizwa na kusikia yote yakuhusuyo na yanayoihusu dunia? Au hali ilivyo ni kuwa sio tu raia bali pia viongozi kuna watu kati yao wanaokaa mkao wa kuwafanza wasikie yale tu wao wanayotaka wayasikie? Hivi vyombo vyetu vya habari, intaneti na mawasiiano mengine yako katika mkao wa kuruhusu uhuru wa mawasiliano wakati wote na kwa watu weote? Na kama uhuru huo haupo au unachezewa ni nini athari kwa nchi yetu na maendeleo yake ?
                Tanzania itafika wapi endapo tutaamua kutumia madini na utajiri wa mali asili ya nchi hii ili watoto wetu wawe na uhuru wa kusoma. Uhuru hapa ikiwa na maana kwamba mtoto anayetaka kusoma na kujiendeleza asinyimwe au asizuiwe kufanya hivyo kwa kuwa tu mzazi wake au jamaa zake hawana uwezo wa kumlipia ada na gharama nyingine za masomo?
                Je, itakuwaje kama Watanzania watachagua uhuru wa afya na tiba bora na wakachagua kuishi na sio kufa ? Ni nini serikali yao iwayo itatakiwa kulifanza na kuhakikisha kwamba uhuru huu unapatikana bila mizungu wala mikwara?
                Je, mikoa yetu inaweza kuwa huru toka serikali kuu na hususan katika masuala ya mipango, mikakati na utekelezaji wake huria bila kuingiliwa na serikali kuu ili kuharakisha kasi ya maendeleo ya mikoa yote nchini ? Kuna wanaoamini wakuu wa mikoa wanastahili kuchaguliwa na sio kuteuliwa, je, hili litaongeza uhuru wa mikoa kwa kiasi gani?
                Tumeona katika nchi kama Cuba, Cape Verde na Malaysia kwamba nyumba sio jambo la anasa. Na kwamba nyumba ni hitaji la msingi kwa binadamu wote. Wapo wanaoamini watu wakiwa na nyumba wanakuwa huru na tayari zaidi kutafuta maendeleo makubwa kuliko ikiwa kinyume cha hivyo. Huwezi ukawa na taifa la wajenga nyumba na waendaao saiti mwaka rudi kila mwaka na nchi ikaendelea!
                Je katika mambo kama vile ujenzi na uendeshaji viwanda, uendelezaji vijiji, mapainduzi ya kilimo, ajira ugenini, ushiriki wenye mafanikio katika michezo ndani na nje ya nchi, maendeleo ya riadha, maendeleo katika tafiti na ufumbuzi, maendeleo na ustawi wa mikoa, uendeshaji mashirika ya umma, yaliyo hai na vitu kama hivyo, je, kukiwa na ushindani na uhuru zaidi wa kuyaendesha Tanzania itapiga hatua mbele au itarudi nyuma ?
                Ni dhahiri kutokana na hayo hapo juu kuwa kuna aina nyingi za uhuru. Na ule wa kwanza, yaani, uhuru wa bendera hauwezi ukawa ni alfa na omega wa aina hizo za uhuru. Aidha, bila kupata uhuru wa aina hizo nyingine ule uhuru w mwanzo wenyewe hauwezi kukamilika.
                Kama hili lasadifu ni muhimu kwamba wakati huu tunapoangalia upya katiba yetu ya zamani kwa madhumuni ya kuwa na katiba mpya ni muhimu sana kuvinjari aina zote za uhuru zinazostahili kuwepo ili tuweze kuwa na mwananchi kamili na sio mwananchi nusunusu.
                Endapo, wabia wote wa nchi wataridhia njia iliyo bora zaidi ni kujaribu kuona tunakuwa na demokrasia pana na yenye kina kirefu kama njia ya kwanza yakuhakikisha kuwa aina nyingine za uhuru kwa njia moja au nyingine kila siku zinapatikana kwa watu wa sehemu na tasnia mbalimbali nchini.
                Matatizo mengi yanayotokea nchini mwetu hivi leo yanatokana na kuwa na demokrasia nusunusu, demokrasia ambayo wakati mwingine inaona kulia,  lakini haioni kushoto; wakati mwingine inasikiliza juu, ikaacha kusikiliza chini; na wakati mwingine inayojali ya mbele, pasina kujali ya nyuma. Hii ni demokraia rojorojo na ambayo ina hatari ya kuvuruga na kusambaratisha zaidi kuliko ya kujenga umoja na kuwa chachu ya kufanikisha maendeleo ya kweli ya kiuchumi na kijamii katika nchi zetu.
                                Nina hakika Tanzania ina kila sababu ya kuwa nyota, lulu na nuru ya Afrika endapo tu dhamira ya kujenga demokrasia ya kweli itakuwepo. Tukitangulia maslahi ya umma kwanza na kuzika ubinafsi, uchama, rushwa za kijinga na upendeleo vitu vilivyoanza kuchipua. Maana sisi tuna mfano wa kuiga na kuigwa. Nyerere. Raia wengine tunaweza tusiwe sawa na Nyerere, lakini kiongozi wetu kuanzia sasa tufanye juu chini awe ni mfano wa Nyerere. Tumtafute. Tumuenzi ili tunusuru nchi yetu, mtu kama huyo !