NCHI nyingi za Kiafrika zitakuwa zinafikisha nusu karne
mwaka huu au mwaka ujao kama nchi huru. Uhuru huo wa kisiasa au uhuru wa bendera au uhuru kutoka kutawaliwa na mgeni
na kutawaliwa na mwenyeji ni mchakato wa asili kama vile watoto wa kiume au
wakike wanapofikia umri wa kuoa au kuolewa na wanavyotoka nyumbani kuanzisha
nyumba yao mpya.
Bila
shaka wengi wanajiuliza je, uhuru tuliopigania ulikuwa ni uhuru mmoja au uhuru
wa aina nyingi? Jibu lake ni wazi hapa litakuwa kwamba uhuru tuliopigania sio
uhuru wa aina moja, bali uhuru wa aina nyingi. Hapa tunachukulia neno uhuru
kuwa ni pamoja na staha, heshima, kiwango stahilivu, uwazi na uwajibikaji
wanaopewa majukumu mbalimbali kieneo na kitaifa.
Watu
wanajiuliza je, hivi, Watanzania na Waafrika kwa ujumla wakipata uhuru wa
kujifunza na kuelewa na hata kuigeuza nadharia kuwa vitendo katika elimu na
maarifa mbalimbali ya dunia ikiwemo
kujifahamu na kufanyia kazi kwa vitendo lugha yao ya asili, katiba na sheria za
nchi yao ?
Je,
nini kitakachotokea ikiwa kama Watanzania na Waafrika watapata uhuru na
demokrasia pana, kiasi cha kuwa na uhuru wa kukichagua chama chochote cha
kisiasa kuingia madarakani na pale kinapoboronga iwe rahisi kukiondoa kama
walivyokichagua bila mikwara kutoka vyombo vya dola vikiwemo vile vya usalama ?
Tutakwenda mbele kijamii na kiuchumi au tutarudi nyuma ?
Je,
hivi hapa Afrika viongozi na watawala wetu wanaridhia, kuchangia na kusaidia
kuona kwamba watu wao wanakuwa na uhuru wa kuiwajibisha
serikali na vyombo vya dola au wanawazuia kupata uhuru huo ?
Je, ni
nini kitakachotokea kama Watanzania na Waafika kwa ujumla wanakuwa na uhuru
wa kunufaika kwa mapana na marefu
kutokana na ardhi yao na mali asili zao na isiwe ni viongozi na wageni tu ndio
wanaonufaika na vitu hivyo ?
Mathalani,
hivi sasa wanaonufaika na ardhi ambayo chini yake kuna madini au vito vya
thamani ni viongozi, wanasiasa na wale wanaopewa leseni kuvichimba vitu hivyo.
Je, inapojulikana ardhi ya kijiji fulani iko juu ya mgodi wa dhahabu kwanini
watu hao wasitajirike kutokana na kuwa wenyeji asili wa ardhi yao wakanufaika
tu watu wengine?
Je,
uhuru wa kuzungumza, kuchanganyika na
watu, kuandamana, kufanya mikutano na kuwa na uhuru wa kuabudu na kuwa na
mawazo tofatuti na watu wengine ni kitu kinachoheshimiwa na kuvumiliwa au
kinashambuliwa na kinapigwa vita kwa kila hali ? Dhahiri au kwa siri ?
Hivi
kweli Waafrika walio wengi wana haki ya
kusafiri na kutembelea nchi nyingine za Kiafrika na ulimwengu. Upo au kuna
usanii na porojo kwa kuwa mazingira yameandaliwa kumfanza Mwafrika asiwe na
uhuru kama huo? Na ni wachache wenye
uwezo wa kutembea na kuona mikoa mingine ya nchi yao, achilia mbali uhuru wa
kuona nchi za nje na huku watu wanataka kukuza utalii wa ndani? Nini
kinachofanzwa ili watu wawe na uhuru wa kweli wa kusafiri ikiwa ni kuwepo kwa
vyombo vyenye staha na heshima, gharama nafuu na ubora wa kuridhisha?
Hivi
Waafrika ni kati ya watu ambao wanahesabika kuwa na uhuru wa maji na chakula. Nikiwa na maana ya uhuru huo kuwa ni
pamoja na haki ya kupata maji safi na chakula chenye lishe tosha ukiwa mjini au
kijijini? Au mahitaji haya ya msingi wanayapata wachache na linachukuliwa kama
jambo la kuwaringia na kuwakoga wasiovipata?
Je,
Afrika kuna uhuru wa kusikilizwa na kusikia yote yakuhusuyo na yanayoihusu
dunia? Au hali ilivyo ni kuwa sio tu raia bali pia viongozi kuna watu kati yao
wanaokaa mkao wa kuwafanza wasikie yale tu wao wanayotaka wayasikie? Hivi
vyombo vyetu vya habari, intaneti na mawasiiano mengine yako katika mkao wa
kuruhusu uhuru wa mawasiliano wakati wote na kwa watu weote? Na kama uhuru huo
haupo au unachezewa ni nini athari kwa nchi yetu na maendeleo yake ?
Tanzania
itafika wapi endapo tutaamua kutumia madini na utajiri wa mali asili ya nchi
hii ili watoto wetu wawe na uhuru wa kusoma. Uhuru hapa ikiwa na maana kwamba
mtoto anayetaka kusoma na kujiendeleza asinyimwe au asizuiwe kufanya hivyo kwa
kuwa tu mzazi wake au jamaa zake hawana uwezo wa kumlipia ada na gharama
nyingine za masomo?
Je,
itakuwaje kama Watanzania watachagua uhuru wa afya na tiba bora na wakachagua
kuishi na sio kufa ? Ni nini serikali yao iwayo itatakiwa kulifanza na
kuhakikisha kwamba uhuru huu unapatikana bila mizungu wala mikwara?
Je,
mikoa yetu inaweza kuwa huru toka serikali kuu na hususan katika masuala ya
mipango, mikakati na utekelezaji wake huria bila kuingiliwa na serikali kuu ili
kuharakisha kasi ya maendeleo ya mikoa yote nchini ? Kuna wanaoamini wakuu wa
mikoa wanastahili kuchaguliwa na sio kuteuliwa, je, hili litaongeza uhuru wa
mikoa kwa kiasi gani?
Tumeona
katika nchi kama Cuba, Cape Verde na Malaysia kwamba nyumba sio jambo la anasa.
Na kwamba nyumba ni hitaji la msingi kwa binadamu wote. Wapo wanaoamini watu
wakiwa na nyumba wanakuwa huru na tayari zaidi kutafuta maendeleo makubwa
kuliko ikiwa kinyume cha hivyo. Huwezi ukawa na taifa la wajenga nyumba na
waendaao saiti mwaka rudi kila mwaka na nchi ikaendelea!
Je
katika mambo kama vile ujenzi na uendeshaji viwanda, uendelezaji vijiji,
mapainduzi ya kilimo, ajira ugenini, ushiriki wenye mafanikio katika michezo
ndani na nje ya nchi, maendeleo ya riadha, maendeleo katika tafiti na ufumbuzi,
maendeleo na ustawi wa mikoa, uendeshaji mashirika ya umma, yaliyo hai na vitu
kama hivyo, je, kukiwa na ushindani na uhuru zaidi wa kuyaendesha Tanzania
itapiga hatua mbele au itarudi nyuma ?
Ni
dhahiri kutokana na hayo hapo juu kuwa kuna aina nyingi za uhuru. Na ule wa
kwanza, yaani, uhuru wa bendera hauwezi ukawa ni alfa na omega wa aina hizo za
uhuru. Aidha, bila kupata uhuru wa aina hizo nyingine ule uhuru w mwanzo
wenyewe hauwezi kukamilika.
Kama
hili lasadifu ni muhimu kwamba wakati huu tunapoangalia upya katiba yetu ya
zamani kwa madhumuni ya kuwa na katiba mpya ni muhimu sana kuvinjari aina zote
za uhuru zinazostahili kuwepo ili tuweze kuwa na mwananchi kamili na sio
mwananchi nusunusu.
Endapo,
wabia wote wa nchi wataridhia njia iliyo bora zaidi ni kujaribu kuona tunakuwa
na demokrasia pana na yenye kina kirefu kama njia ya kwanza yakuhakikisha kuwa
aina nyingine za uhuru kwa njia moja au nyingine kila siku zinapatikana kwa
watu wa sehemu na tasnia mbalimbali nchini.
Matatizo
mengi yanayotokea nchini mwetu hivi leo yanatokana na kuwa na demokrasia
nusunusu, demokrasia ambayo wakati mwingine inaona kulia, lakini haioni kushoto; wakati mwingine
inasikiliza juu, ikaacha kusikiliza chini; na wakati mwingine inayojali ya
mbele, pasina kujali ya nyuma. Hii ni demokraia rojorojo na ambayo ina hatari
ya kuvuruga na kusambaratisha zaidi kuliko ya kujenga umoja na kuwa chachu ya kufanikisha maendeleo ya kweli ya
kiuchumi na kijamii katika nchi zetu.
Nina hakika
Tanzania ina kila sababu ya kuwa nyota, lulu na nuru ya Afrika endapo tu
dhamira ya kujenga demokrasia ya kweli itakuwepo. Tukitangulia maslahi ya umma
kwanza na kuzika ubinafsi, uchama, rushwa za kijinga na upendeleo vitu
vilivyoanza kuchipua. Maana sisi tuna mfano wa kuiga na kuigwa. Nyerere. Raia
wengine tunaweza tusiwe sawa na Nyerere, lakini kiongozi wetu kuanzia sasa
tufanye juu chini awe ni mfano wa Nyerere. Tumtafute. Tumuenzi ili tunusuru
nchi yetu, mtu kama huyo !
No comments:
Post a Comment