Watanzania
wanatarajia kwamba hadi inafikia mida hii ambayo JKT litayari kufungua
milango yake kwa wanaJKT wa kizazi kipya kwamba kuna mipnago dhahiri ya muda
mfupi na mrefu kuhusu uendeshaji wake; kuna mikakati-mipango sadifu, kuna sera
tambuzi na shirikishi na kuna masahihisho kadhaa yaliyofanzwa ili
kuoanisha malengo mapya katika nyakati
mpya kwa uendeshwaji wa JKT ijayo. Na kwamba JKT ikisaidina na majeshi yetu
mengine itakuwa ndio kichwa cha garimoshi au injini ya kuiendesha Tanzania mpya
itakayokuwa inatengeneza na kujenga karibu kila kitu kwa kutegemea rasilimali
zetu wenyewe ikiwemo rasilimali watu.
Kufanya
hili lazima pawepo na mpango wa uendeshaji wa mwaka mmoja; mpango wa miaka
mitatu - mitano (hususan kuhusu rasilimali mbalimbali) na mpango wa muda mrefu wa miaka 25-50
inayolenga kuingiza nchi kwenye mabadiliko makubwa kila baada ya muongo mmoja.
Mipango
hii itarahisisha kufahamu ni kwa namna gani JKT itaoanisha matumizi na mapato
yake katika uendeshaji wake. Lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa inakuwa ni
taasisi inayojiendesha yenyewe bila kutegemea ufadhili toka nje au ndani ya
nchi.
JKT
ikiweza kujiendesha yenyewe bila ufadhili na kwa hiyo kujitegemea itazalisha vijana wanaoweza
kujiajiri wenyewe na kujitegemea bila kutegemea kuajiriwa kama njia ya mtu
kujipatia riziki yake ya kila siku.
Mpango-mkakati
ni muhimu kwa kuwa mpango huu ndio unaoisadia taasisi yoyote ile iwayo kujua
mahala ilipo na inakotaka iwe baada ya miakafulani.
Ili
kufanikisha hili ni lazima tubainishe wazi malengo ya JKT. Bila shaka katika
mustakabali wa sasa lengo moja litakuwa ni kuwaunganisha vijana wenye itikadi tofauti na wanaounga mkono
vyama tofauti vya kisiasa kujenga utamaduni wa ushindani-shirikishi, ushindani
unaojenga badala ya kubomoa kwa kuheshimu misingi ya haki na usawa kwa kila
Mtanzania. Na kwamba vijana wa Kitanzania kuanzia sasa hawatatiwa upofu wa
kuchagua kilichooza na kuacha kilicho bora kwa namna yoyote ile. Na juu ya yote mtu yeyote
mwenye kupiga vita mfumo wa vyama vingi na demokrasia ni adui na sio rafiki wa
Watanzania. Na kwamba mtu yeyote anayetumia hila, hadaa, rushwa, fedha na
ujanja wowote ule uwao ili kupata cheo au uongozi ni mtu wa kutliwa mashaka
makubwa katika safu za uongozi wa taasisi na maeneo mbalimbali nchini.
Tofauti
na huko nyuma katika miaka hii ya upasho na uamsho upo umuhimu wa makambi ya
JKT mpya kuheshimu imani za wanakambi na
uhuru wa watu kuabudu na kufuata maamrisho ya dini zao bila kukwazwa na kitu au
mtu. Hili likifanyika litawaondoa wazazi hofu kuwa watoto wao wanaweza kwenda
kuharibiwa au kupotoshwa JKT.
Ninategemea
pia kuwa JKT itafafanua dhana ya uzalendo iwe pana na wazi zaidi na ianyoendana
na wakati. Kwangu mimi Uzalendo sio kukubali kuwa kondoo na kutii au kuridhia
kila jambo linaloanzishwa au kuamriwa na wakubwa hata kama ni kosa au uovu; na
wala uzalendo sio mavazi, ulimbwende na mapambo yenye rangi za bendera ya
taifa.
Uzalendo
ninavyouelewa mimi ni hali ya juu ya utu na ubinadamu inayofikiwa katika nchi
fulani. Uzalendo ni juu ya familia, urafiki, ukoo, kabila, imani, uchama na
uwana- kikundi wowote ulekatika jamii husika. Mzalendo kwa maneno mengine ni
mtu aliye juu ya mambo yake binafsi na ya kifamilia, juu ya masuala ya ukoo na
ukabila, juu ya dini au imani yake na ni juu ya siasa za kichama pale utaifa unapohitajika
kuwa juu ya kitu kingine chochote. Aidha,
mzalendo ni mtu anayefahamu katiba na sheria za nchi yake na ni mwepesi wa
kuhoji na kuuliza ili kupata majibu sahihi kabla ya ya kufanya maamuzi yoyote
ya kisiasa, kijamii au kiuchumi, aghalabu, akiliweka taifa lake na utaifa wake
mbele ya mtu au kitu chochote kile kiwacho.
Ili
kudadavua na kuibua melengo yanayofaa ni kitu muhimu tuanze kwa kuangalia
matatizo au changamoto zinazowakabili Watanzania mijini na vijijini.
Changamoto
hizo ni pamoja na umaskini unaotufanya tushindwe kulipa ujira unaokidhi
mahitaji ya wafanyakazi mbalimbali na hivyo kuzusha matatizo ya rushwa, migomo,
mitafutano na mengine kama hayo; aibu ya watu wetu kukosa nyumba, maji na umeme
na mahitaji mengine ya msingi katika karne hii; mbinu duni katika kilimo na
uzalishaji na biashara ya chakula;
kushindwa kutumia bahari, kushindwa kuunda vyombo vya kisasa ili
kutajirika na rasilimali bahari na rasilimali kwa ujumla; kukosa uwezo wa kuchimba na kuuza madini yetu
sisi wenyewe na hivyo kuachia wageni kutuibia mali asili zetu kushoto na kulia;
ushirikishwaji duni wa Watanzania katika maamuzi na uendeshaji wa nchi yao na
mambo yake; kuweza kuwa na mashirika ya umma lakini tukashindwa kuwawezesha
Watanzania wengi zaidi na hususan vijijini kumiliki kampuni, biashara a miradi
yao yenye kuingiza kipato cha uhakika; kufulia kiteknolojia na kiviwanda na hivyo kusababisha kununuliwa kwa kila zana au kifaa toka nchi
za nje; Kushindwa kuitumia teknohama na
mifumo ya kidijito kuharakisha maendeleo ya nchi kwa kasi kubwa zaidi; kushindwa kutoa matunzo na malezi kwa wazee, masikini, watoto wa mitaani
na wajane; kushindwa kuendeleza
miundombinu na mahitajio mengine ambayo yangeweza kumuwezesha kijana wa
Kitanzania kung'aa katika soka, riadha, michezo mbalimbali, filamu, maigizo,
muziki na sanaa mbalimbali.
Pasina
ushirikishwaji wa dhati na uhakika wa masikini nchini ambao ndio idadi kubwa ya
watu wetu hatutakwenda popote. Lazima
JKT mpya iwe na kitengo mahsusi kinachokaa, kufikiri na kutekeleza hatua
mbalimbali zitakazochangia kupiga vita umaskini nchini kwa vitendo na sio kwa
nadharia na maneno.
Kuna
wakati JKT iliwakawaka katika kilimo. Nina hakika hali hii inaweza kurejeshwa
pakiwa na ushirikiano kati ya JKT, vijiji na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
hasa kilimo na uzalishaji wake kitakapolenga matakwa ya wahitaji binafsi na
kile wanachoagiza kikazalishwa kwa viwando vinavyokubalika.
Ili
mapinduzi ya kilimo yafanikiwe JKT inastahili kuzalisha zana mbalimbali za
kilimo ikiwemo matrekta, kombaini havesta, malori na mitambo ya kuhifadhi na
kusindika vyakula. Ni aibu miaka 50 baada ya uhuru kushindwa kutengeneza vitu
kama hivyo sisi wenyewe.
Aidha,
katika mikoa inayopakana na bahari, maziwa na mito mikubwa nitategemea kuiona
JKT katiika maeneo hayo sio tu ikijiingiza katika uvuvi na uvunaji rasilimali
maji bali pia ikiunda vyombo vinavyohitajika na sekta hiyo ili kuisasaisha au
kuifanya ya kileo zaidi.
Katika
maeneo yenye madini ninatarajia kuona vitengo ndani ya JKT vinavyoharakisha
kuwawezesha vijana wa Kitanzania kuwa wachimbaji madini na waendeshaji na
wasimamizi wa migodi yetu ili tuonokane na kuibiwa waziwazi.
Ninaamini
makambi mbalimbali ya JKT yatakuwa na vyuo kwa vitendo vitakavyowafundisha
vijana sio tu ujasiriamali bali taaluma zote za uongozi na utawala ikiwa ni
pamoja na ubingwa wa kupanga, kusimamia rasilimali, kudhibiti mambo, kutafuta
masoko na uzalishaji na uuzaji wa kile kinachozalishwa. Chuo hicho kwa kufanya
mambo yake kwa vitendo ninakitarajia kuwa kitakuwa ndio eneo la kupanda mbegu za kuzlisha makampuni ya
kijamii kwa watu wa maeneo mbalimbali nchini.
JKT
ijayo haiwezi kukwepa kuwa na kitendo cha teknolojia na teknohama ili
kuiwezesha nchi na hususan vijana kwenda na wakati. Nitategemea watu hodari
katika masuala ya kompyuta, simu, tovuti na mawasiliano watakuwa vijana
waliopitia na kusomea mambo haya kwa vitendo na sio nadharia tu. JKT kwa maneno
mengine itakuwa wadi ya uzalishaji miradi mbalimbali ya kiteknolojia na
kiteknohama itakayochangia kuharakisha maendeleo ya Tanzania. Hususan katika
matumizi ya tovuti yatakayosaidia kuwakutanisha watu kiteknohama toka Ulaya,
Asia, Amerika na kwingineko Afrika wakaanzisha na kuendesha mradi hapa nchini.
JKT
ijayo lazima iwe na kitengo cha ustawi wa Jamii na kufanya kazi ambayo wizara
ya afya na ustawi wa jamii meshindwa kwa kiasi kikubwa kuifanya inavyostahili.
Kama
ilivyo kwa makundi hayo hapo juu wanamichezo na wasanii wa Tanzania nao
wamejikuta ni mayatima. Ninaamini JKT tena kwa faida kubwa sana inaweza
kuingilia kati katika hili na kugeuza hali ya mambo ilivyo leo na Tanzania
ikaanza kunufaika vilivyo na vipaji vya vijana wake.
Hayo hapo juu yana maana kwamba
JKT inastahili kuwa na mafunzo ya muda mfupi katika masuala ya matumizi sahihi
ya silaha, ulinzi na uasktari (pengine miezi mitatu tu) na kisha vijana
wakagawanywa katika idara mbalimbali
zenye majukumu ya kutekeleza changamoto hizo hapo juu (kwa miezi sita
-tisa au hata zaidi) kwa ufanifu na
ufanisi mkubwa kila mwaka kuanzia pale itakapoanza rasmi.
No comments:
Post a Comment