Sunday, November 4, 2012

Katiba iweke sawa udhibiti fedha, hazina na maliasili za nchi


BILA shaka wachangiaji kwenye uandaaji wa katiba mpya wamezungumza mengi juu ya katiba waitakayo. Binafsi, hata hivyo, ninaamini kwamba yote yanayozungumzwa yatakuwa hayana maana kama udhibiti fedha za serikali, hazina/benki kuu na mali asili za nchi havitakuwepo.
Kwa namna fulani kila tatizo, kubwa kwa dogo, linalosababishwa na serikali, watumishi wake na vyombo vyake hapa nchini linahusiana kwa namna moja au nyingine na udhaifu katika udhibiti fedha za walipa kodi, hazina/benki kuu na mali asili za nchi kama vile madini, misitu, maji, wanyama na vitu kama hivyo.
Ninasema udhibiti kwa sababu vitu hivyo kama vilivyo havina tatizo. Tatizo linakuja mkono wa mtu ukishaingia kwa kutumia cheo, nafasi au wadhifa wake katika taifa. Kwa maneno mengine, tatizo la Watanzania linatokana na vitu vilevile Mwalimu Nyerere alivyosema tunastahili kuwa navyo ili TUENDELEE.
Kwani watu wamezunguka ardhi, siasa na uongozi na kugeuza nyenzo za kutusaida kuendelea kuwa nyenzo za kutusaidia kuhujumiana, kufisadiana, kuminyiana, kutambiana na wengi wetu kuzidi kubaki nyuma kimaendeleo vijijini na mjini.
Hii ina maana tatizo la Tanzania leo ni watu. Sio vitu. Vitu havina matatizo. Ardhi haina tatizo kama ilivyo mistiu au wanyama pori au gesi au peteroli au barabara au bandari au TTCL au TANESCO au TAZARA au TRC au kiwanja cha ndege na kadhalika. Watu wanaosimamia au wanaotakiwa kuendesha vitu hivi ndio wenyewe matatizo. Watu ndio tatizo.
Na matatizo yenyewe yanakuja kwa njia mbili. Aidha watu hawana uwezo wa kuviendesha kwa sababu hawajawahi kusimamia vitu kama hivyo na wamepewa zawadi kuviendesha au wapo wenye uwezo wa kuvisimamia na kuviendesha lakini mifumo na muundo wa serikali na vyombo vyake kama ulivyo vinachangia kuua tassisi husika kuliko kuzisaidia kuendelea mara nyingi kwa kukosa usimamizi na udhibiti wa kutosha.
Majibu ya matatizo mengi ya kikatiba na uendeshaji kwa bahati nzuri yapo katika mafunzo ya uandishi wa habari.
Hususan somo la kwanza tu katika uandishi wa habari linamtaka mwanahabari kuuliza na kujibu maswali ya NANI, NINI, KWANINI, WAPI, LINI na KWA NAMNA GANI ? Maswali haya yakijibiwa kwa kiwango kinachokubalika mtu huwa na taarifa kamili inayomrahisishia kufanya maamuzi sahihi. Kinyume chake, aghalabu, utakuta ni maamuzi mabovu na dhaifu.
Kwa mfano, wale wanaozungumzia rais kupunguziwa madaraka ni kwamba wanauliza NANI au NINI kilichompa madaraka hayao; KWANINI kapewa madaraka hayo wakati huo na kwa NAMNA GANI? Na madaraka hayo wakati wa mfumo wa chama kimoja yalitumika vipi na wapi na kama katika mfumo wa vyama vipi yanatumika kwa usahihi? Na wakati huo (LINI) yalipotumika yalisaidia au kuchangia kitu gani na kama katika wakati wetu bado anastahili kuwa nayo? Na kama ni kumpunguzia tumpunguzie kwa NAMNA GANI na kwa faida na hasara ya NANI?
Umuhimu, uzito na uzuri wa maswali haya ya kiasili katika uandishi yanasaidia si haba kupata taarifa toshelevu kufanza maamuzi mbalimbali na kuwa na ukamilifu au uyakini wa kile kinachoandikwa. Isitoshe kila NANI inaweza kuzaa nini, kwanini, wapi, lini na kwa namna gani zake kama hizo nazo pia zinavyoweza kuzaa nani na hao ndugu zake katika muktadha na mustakabali wa kila jambo ?
Binafsi ninajikita zaidi leo na suala la katiba na umuhimu wa udhibiti wa fedha, hazina na maliasili za nchi, jambo ambalo kwa upande wangu ninaamini limeifanza katiba yetu leo kuonekana na walakini na serikali na uongozi mzima kuonekana dhaifu na usiotimiza ipasavyo wajibu wake.
Uzuri wa katiba kwa maneno mengine hautokani na katiba kuwa nzuri kimaandishi na kinadharia lakini kiwango cha udhibiti wa vitu muhimu vinavyofanya kuwepo na nchi inayoendelea au isiyoendelea; masikini au tajiri, yenye ukweli au uongo katika takwimu zake na yenye ungozi imara au u0ngozi dhaifu. Kwa maneno mengine hadhi ya kiwango fedha za mlipa kodi na kipato cha nchi kinavyotumika kumfaa mlipa kodi ndicho kiwango cha ubora wa katiba ya watu na nchi husika. Fedha na hazina ya nchi inavyotumika kuwafaa zaidi wananchi wote kwa umoja wao ni ushahidi wa katiba bora, na fedha za walipa kodi zinavyotumika kuwafaa walioko uongozini na maswahiba zao tu ndio dalili na ushahidi wa katiba mbovu na utawala dhaifu.
Ili kuona kana kwamba tuna katiba mbovu au nzuri tuyatumie maswali yale ya NANI, , NINI, KWANINI, WAPI, LINI na KWA NAMNA GANI kujiuliza kwa namna moja au nyingine baadhi ya maswali yaliyomo katika mtiririko huo hapo juu. Njia mbalimbali zinaweza kutumika, na ha hakuna njia iliyo bora kuliko nyingine ila ile inayomsadiai mtu kujenga uelewa na ufahamu bora zaidi wa jambo husika na hivyo kumuweka mahala anap;oweza kutoa majibu sahihi zaidi na kufanya maamuzi bora kuliko kama atakuwa ameshindwa kuuliza maswali hayo hapo awali.
Maswali haya ya NANI, NINI, KWANINI, LINI, WAPI NA KWA NAMNA GANI yanaweza kuulizwa kwa njia mbalimbali lakini azma kubwa ikiwa ni kupata majibu sahihi ya kututwezesha kuwa na vifungu tambuzi, bainifu na vinavyoona mbali katika katiba mpya ili katiba hiyo kiukweli iweze kutufaa kwa miaka 50 kama sio mia.
Binafsi kama kichwa cha insha yangu kinavyoonyesha nitajikita zaidi kwenye udhibiti na ufuatiliaji masula niliyoorodhesha hapa chini, kwa maana, ya kuuliza maswali ambayo yatatusaidia kupunguza kama sio kuondosha kabisa mapungufu yalipo hivi leo. Narudia tena, hii ni njia moja tu, ya kuuliza maswali kama haya nawe ukiwa na muktadha na mustakabali tofauti unaweza kuyauliza kwa njia tofauti na ile ninayoitumua mimi.
. Hali ilivyo hivi sasa. Je, ni NANI na amefanya kitu gani au NINI kutufikisha hapa tulipo leo? Je, imejitokea kwa ajali au kwa kukosa uongozi mzuri au kutokana na watu kushindwa kujua wanatakiwa wafanye NINI? KWANINI tunataka mabadiliko. Ni WAPI kuna umuhimu wa mabadiliko kwa NAMNA GANI na kwa kiasi gani. Je, hayo yakishafanyika kutakuwa na mabadiliko yanayohitajika hivi leo? Ni NANI, tofauti na huko nyuma atakayepewa jukumu la kuisimamia na kudhibiti KATIBA MPYA ili yote tunayokubaliana yasiwe yanaonekana tu yamekubalika kufanyika lakini yanafanyika KIKWELI KWELI.
. Chama, vyama na siasa. Katiba iliyopo ina nasaba na mfumo wa chama kimoja, je, Katiba mpya itakuwa inafanana na kutosheleza mahitaji ya mfumo wa vyama vingi na demokrasia au siasa za uwazi na ushindani. NANI atahakikisha kuwa VYAMA na Watanzania wote kwa ujumla wananufaika na mabadiliko katika katiba mpya? Ni kwa kiasi gani rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala anaweza akadhibiti serikali kutokipa chama chake fedha wakati kinazihitaji? Na, je, Gavana wa benki kuu atakataa pale chama kinapomuamrisha kukilipa kwa jambo lisiloeleweka ili mambo yake yafanikiwe? Katiba itatusaidia WAPI, KWANINI, LINI, VIPI na KWA NAMNA GANI ili hili liwe ni historia katika nchi yetu?
. Serikali, viongozi, wizara na watumishi wake. Je, viongozi walioppo madarakani ni akina NANI, wanapata NINI, na wanachokipata wanakipata KWA NINI. Haki waliyo nayo ilianza WAPI, LINI na KWANINI. Je, katika katiba mpya tutegemee mabadiliko gani chanya?
. Mikoa. Je, mikoa hivi leo inaongozwa na NANI na wanaongoza na wanaowachagua wanapata nini. Uhalali wao na wanachokipata unatoka WAPI ? LINI wanakipata na KWANINI wanakipata. Na KWANINI wanaogoza mikoa wasiwe watu wa kuchaguliwa badala ya wa kuteuliwa?
. TRA. Je, watumishi wa TRA wanalipwa tofauti na watu wengine? Uhalali wa hili ni NINI ? Umeanzia WAPI, LINI, KWANINI na kwa NAMNA GANI ? Hili linasaidia kuwa chachu katika maendeleo ya sekta nyingine au ni chanzo cha matatizo kwa watumishi wengine wa serikali? Na zaidi ya rais mwenyew, je, ni kina nani wanaodhibiti TRA na watumishi wake? Na, je, hao waliopewa kazi ya kuidhibiti TRA wanapata ujira na maduhuli sawa na watumishi hao?
. Benki Kuu, Hazina na taasisi nyingine za fedha. NANI anasimamia na kudhibiti mali zilizoko Benki Kuu? Kwa mfano kukiwa na dhahabu huko gavana peke yake anaweza akaamua kuiuza bila kumuarifu mtu yeyote? Je, hakuna uwezekano wa mtu toka kwenye serikali au chama tawala kuilazimisha benkii hiyo kulipa kisichostahili kulipwa? Benki kuu inatakiwa iendeshweje ili kuzuia mianya ya UFISADI na malipo yenye mashaka na wakati huo huo benki hiyo kuwa chachu kwa vijana na hususan wajasiramali kuanzisha miradi na makampuni yatakayotutoa toka kwenye umaskini?
. Mifuko ya pensheni na hifadhi za jamii. NANI anamiliki mifuko ya pensheni na hifadhi za jamii. Kama serikali ilishajaribu kumiliki makampuni na kisha ikashindwa KWANINI serikali isiwawezesha Watanzania mmoja mmoja na katika vikundi wao kuanzisha makampuni hivi leo. Na KWANINI wanachama wa mifuko kama hiyo wasiwe na haki ya kupewa HISA na mifuko hiyo?
. Kilimo na dada zake na mchango yao katika maendeleo yetu. NANI anastahili kusimamia shughuli za KILIMO. Na NINI kinachotokea sasa. KWANINI yanayofanyika sasa yanafanyika. Ndio kwanza yameanza au yalianza LINI na WAPI na KWA NAMNA gani na yanamfaa NANI?
. Viwanda na Uzalishaji mali na nafasi ya vipengele muhimu kubadili hali iliyopo. NANI alitaifisha viwanda, KWANINI akatii WB/IMF na sio kuiga mfano wa Uchina na ilivyobadili muundo na mfumo wa umilikaji wa makampuni ya umma ya Kichina na kushirikiana na sekta binafsi? Je, ni kweli makampuni ya umma yalitushinda kuendesha au waliochaguliwa walikuwa ni uozo na walichaguliwa kichama zaidi na sio kiutaalamu zaidi?
. Migodi, mali asili na michango yake na katiba ifanye nini ili kuongeza michango hiyo. NANI aliyetoa ruhusa ya kubinafsisha sekta ya madini. Katika kufanya hivyo serikali Ilipata NINI na yeye akapata NINI ? Je, leo tunapata NINI na kitu gani kifanyike WAPI, LINI NA KWA NAMNA GANI ili tupate sio tu manufaa zaidi bali tuweze kujifunza sisi wenyewe kuchimba na kumiliki migogi yetu kama Venezuela, Uchina na nchi kama hizo? . Mikopo ya ndani na toka nje ya nchi. Je, mikopo ambayo serikali inakopa toka kwenye mabenki na vyombo vya fedha vya ndani pamoja na ile inayokopwa toka nchi za nje inamfaa NANI, na anayenufaika anapata NINI, na KWANINI ni huyo au hao ndio wanaopata na sio mwingine au watu wengine?
Hili linahusu pia misaada na jinsi nchi inavyonufaika au inavyoathirika na misaada kama hiyo. . Elimu na Vijana. NINI kimetokea katika elimu toka kufa Azimio la Arusha. ? NANI ananufaika na NANI anahasirika. KWANINI kinatokea kinachotokea? WAPI wanaangaliwa na wapi wanasahauliwa? Watu watavumilia hadi LINI na mabadiliko yataletwa na nani na yanaweza kuja KWA NAMNGA GANI? Katiba itachangia nini katika hili, ilikuhakikisha aina na mfumo wa elimu tulionao ni ule unaowanufaisha wengi na sio wachache?
. Mahitaji ya Msingi na vyanzo vya uhai. Je, pamoja na baadhi yetu kuelezea na kuelezea umuhimu wa mahitaji ya msingi kutangulia kwanza vitu vyote, yaani, watu wapate kwanza hakika ya kupata chakula, maji, tiba, usalama wao na mali zao, hewa safi, mazingira bora, nyumba, ndoa, elimu hadi sekondari, ajira ni NANI anayepuuza hili. Anapata NINI kwa kupuuza ? KWANINI mahjitaji ya msingi kama vile nyumba kwa viongozi wetu wengine eti yanaonekana ni anasa? Na wanamtupia mgonjwa kutibu wagonjwa na masikini wenzie?
. Tofauti ya kipato. Je, NANI amefanyia utafiti wa kina juu ya tofauti ya kipato nchini? Anayeruhusu au wanaoruhusu tofauti hizi kuanza na kuendelea kukua anapata faida GANI na ni NANI na yeye anapata NINI. KWANINI tunakosa sera ya kitaifa (siyo ya kichama) katika hili? WAPI kuna watu wenye mtazamo na msimamo tofauti. Wanachgaia yepi, LINI tutawasikia na tutarajie mabadiliko yaje katika njia gani? IKiwa hapatakuwa na uwazi na udhibiti katika mambo haya, je, haitatokea kuwa nchi au serikali inaweza kushindwa kuendesha mambo yake kwa kuwa imejipanga kufanya mambo kiujanja ujanja na kutumia mabavu na sio busara na hekima katika maamuzi yake mbalimbali ? Je, Katiba mpya inawezakuzuia vipi jambo kama hili kutokea na kuhakikisha wakati wote kuna mipaka dhahiri kati ya serikali na vyama vya siasa, viongozi na watumishi wa serikali, na kwamba watu kwa umoja wao wanakuwa ndio waamuzi wa mwisho kuhusu hatima ya nchi yao na sio chama cha siasa au kikundi chochote kiwacho?

No comments:

Post a Comment