Sunday, November 4, 2012

Tutathmini Upya Mchango wa Taasisi za Fedha na Mikopo Nchini

MZAZI anayetambua kwamba mwanaye ana tabia mbaya, akamuachia vivyo hivyo bila kumkanya, huwa hajitendei haki wala hamtendei mwanawe haki.
                Umekuwa ni wimbo wa kurudiwa rudiwa kuwa Watanzania hawakopesheki. Ukiwakopa kulipa ni kazi. Lakini kwa wanaomuelewa binadamu wanafahamu fika kwamba tabia yoyote hujengwa na malezi na mazingira yaliyopo.
                Na inaeleweka pia kuwa asilimia kubwa ya wanadamu hawana tabia mbaya na ni idadi ndogo tu ambayo  haiaminiki na hailekezeki.
                Nitakuwa mchache wa shukrani bila kusifu kazi nzuri iliyofanzwa na taasisi za fedha hapa nchini. Lakini kutokana na ukweli kuwa bado tuna kazi ngumu ya kupigana na umaskini, ninaamini hata wao wanajua zipo changamoto za zamani na mpya ambazo twapasa kuzikabili ili nafuu katika umaskini ipatikane nchini.
                Nina wasiwasi pia kwamba baadhi ya taasisi husika zisipojiangalia upya zitajikuta zinachangia badala ya kupunguza umaskini. Na hili linatokea kutokanana kanuni na taratibu zilizopo na maombwe katika  masuala mbali mbali        ya kiudhibiti na kiufuatiliaji.
                Katika kutoa mchango wangu kuimarisha sekta hii muhimu nitabainisha mambo kadhaa ambayo yanastahili kuzingatiwa na taasisi za kifedha na mikopo nchini ili ziwe na mavuno bora na makubwa zaidi.
                Kwanza, taasisi zikopeshe biashara au mradi na sio mtu. Hali ilivyo hivi sasa ni kwamba Ali au Agnes ndiye anayekopeshwa. Na taasisi nyingi humuangalia na kumtathmini Ali au Agnes na sio biashara au mradi husika. Ali au Agnes huwa hafundishwi wala kufahamishwa juu ya tofauti yake yeye kama mtu na biashara au mradi wake kama mtu kisheria. Hii ni kasoro inayochangia si haba kushindwa kwa watu wengi  kurudisha fedha wanazozikopa.
                Wafanyakazi na wadhamini wafanze kazi kiurasimu na kiufundi zaidi. Pale wafanyakazi na wadhamini wanapokuwa na roho ya huruma na kutaka kusaidia mtu badala ya kumuwezesha mtu kiuchumi/kimkopo ndipo penye kiungo dhaifu kuliko vyote katika mlolongo mzima wa mikopo na ulipwaji wake. Ni muhimu tukajifunza kwamba nia, dhamira na uwezo wa mtu kujiondoa toka kwenye umaskini kwa juhudi na maarifa yake mwenyewe ni jambo kubwa kama ulivyo msaada wa fedha kumuwezesha kufanya hilo. Lakini yule anayeona ni rahisi kukopa na asifanye la maana na kisha kuirusha taasisi husika hachangii vita vyetu dhidi ya umaskini bali anaongeza umaskini wetu. Na watu wa namna hiyo kila kona ni watu wa kupigwa vita na kutangazwa kama maadui wa maendeleo.
                Pasiwe na mikopo isiyo na akiba.  Baadhi ya taasisi husika kwa kudhania kwamba zinawasaidia maskini, zimeamua kutoa mikopo bila sharti la mpewa mkopo kuwa na akiba katika akaunti yake. Ninaamini hili ni kosa na lina hatari kubwa zaidi ya kuchangia umaskini kuzidi badala ya kupungua kwa wale wanaokopeshwa.
                Akiba na uwekaji na utunzaji wake ni sehemu muhimu na isiyoonekana katika mfumo wowote wa kibenki na kifedha. Usipokuwepo chochote kinaweza kutokea ndani au nje ya uwezo wa wahusika na kuleta hasara na majuto makubwa zaidi. Ninaamini, wakati umefika wa Benki Kuu kuhakikisha kuwa taasisi zote za fedha ndogo kwa kubwa zinazotoa mikopo sio tu hazitoi mikopo kwa  mtu asiyekuwa na akiba hai bali pia na taasisi zenyewe zinakuwa na akiba kiasi fulani katika benki za biashara na benki kuu.
                Uwekezaji unaonufaisha wanachama wa taasisi za Kifedha.  Wakati umefika sasa ili kupunguza gharama na riba kwa wajasiriamali, taasisi za fedha kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika miradi sahihi inayochangia kumuendeleza mwananchi na kupunguza umaskini kiujumla nchini. Ubia ukianzishwa na mabenki makubwa, mifuko ya hifadhi, bima,makampuni na  watu binafsi ndani na nje ya nchi wenye uwezo na wanaotaka kutoa mchango wao katika vita dhidi ya umaskini kuna mengi yanaweza kufanyika tena kibiashara na taasisi husika na hivyo mwisho wa siku gharama na kiasi cha riba kinacholipwa (na wale ambao kwao riba si haramu) isiwe kikwazo bali kichocheo cha kukopa na kujiendeleza.
                Kuwashirikisha wanafamilia kiuwazi na kimkakati zaidi. Hali ilivyo hivi sasa ni kwamba baba au mama na jamaa wa familia husika wanahusishwa kama vile ni amana ambayo itadaiwa pindi mkopaji anaposhindwa kulipa deni lake.
                Ninaamini njia nzuri zaidi ni kumshirikisha baba au mama kama sehemu ya mkopo ili kuondoa hatari za baba au mama wanaokopa bila mume au mke kuwa na habari ya hili au lile. Aidha, kwa wale ambao  mikopo yao inatolewa bila mtu kuwa na akiba kwa upande wangu ninahofu kuwa utaratibu wao unaziongezea familia umaskini zaidi badala ya kuupunguza.
                Uchunguzi wangu binafsi umebaini kwamba kuna tabia ambazo pia zinawakera wakopaji ambazo ingelifaa zikomeshwe ili kujenga mahusiano bora zaidi kati ya taasisi husika na wakopaji wake. Ya kwanza, ni ile ya taasisi kutuma 'jeshi zima' kukabili mkopaji na familia yake pale panapotokea tatizo. Hili linaonesha kuwa mawasiliano kati ya wadhamini wa mkopaji na taasisi bado ni duni na yanastahili kuimarishwa toka siku ya awali. Hii ina maana kwamba mkopaji anaweza akapewa fedha na kuzitumia bila wadhamini kujua kinachoendelea. Na anakuja kushtuliwa pale tu ambapo mkopaji kaingia kwenye matatizo.
Laiti wadhamini wangelitambua toka awali wangeliweza kuweka njia zao wenye za kufuatilia au kujiandaa kwa lolote litakalotokea kuliko kushtuliwa na makomandoo wa mikopo mitaani.
                Jambo lingine ni tabia ya baadhi ya taasisi kuwafungia wakopaji wake ndani (kifungo cha muda) eti kwa kuwa huo ni utaratibu wa kuwalazimisha kumlipia mwanachama mwenzao aliyekwama kurejesha marejesho. Katika sheria za asili (natural justice) hili ni kosa, maana kama ilivyokwisemwa na wahenga kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe!
                Badala ya majeshi ya kudai mikopo kuwa ndiyo kitu kinachoonekana mara kwa mara mitaani, ninapendekeza kuwe na majeshi ya kuwasomesha na kuendeleza biashara za wakopaji.
                Endapo patakuwa na vijana mahiri katika menejimenti, oganaizesheni, usimamizi, udhibiti  na uongozi wa masuala ya biashara na taasisi hizi zikaja pamoja na kuwa na vitabu vya menejimenti na uongozi kwa Kiswahili nina hakika kasoro zinazotia hofu na uoga mabenki na taasisi za fedha nchini kumkopesha Mtanzania baada ya muda sio mrefu zitakuwa ni historia.
                Katika miaka ya 60 Japani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia ilianza kuzaliwa upya. Mkunga aliyetegemewa katika mazazi hayo hakuwa mwingine ila benki zilizoona mbali na mbele za Kijapani. Marehemu Matsushita (National na Panasonic), Akio Morita (Sony) achilia mbali wakina Toyoda na wengineo walibebwa si haba kutoka utoto wa ujasiriamali hadi kufikia makampuni makubwa tunayoyaona duniani leo. Siri ya mafanikio yao ilikuwa ni kwamba benki zilikuwa zikiwafuata wao kule waliko na wala sio wao kuzifata benki.
                Benki zilikuwa kwa Wajapani wakati huo kama baadhi yake zilivyo leo ni wabia wa wafanyabiashara, wenye viwanda na wajasiriamali. Wakati mwingine huyu akimbeba yule, na yule naye kwa wakati wake akimbeba huyu.
                Tanzania sio masikini tu kwa sababu inashindwa kuchimbua utajiri ulio katika ardhi yake, lakini kubwa zaidi ni kuwa umaskini wetu unatokana  pia na mabilioni ya fedha kufungiwa ndani badala ya kuwa mitaani kuendesha injini ya uchumi wa taifa letu. Wakati umefika wa taasisi za fedha na mikopo kwanza kutoa elimu na mafunzo yanayohitajika, kisha wakawa wabia na wajasiriamali na makampuni madogo na kisha wakawa wateketezi muhimu katika sera zinazochangia kukuza na kupanua uchumi badala ya kulea na kudekeza uchumi unaochangia kuwa na matajiri wachache lakini maskini wengi.
                Nionavyo mimi, muamko mpya wa serikali katika kuwatumikia Watanzania kwa njia bora zaidi hususan katika sekta za fedha na kodi kunaashiria kuwa serikali itakuwa mbele kuwasaidia wale wote watakaotaka kuwasaidia makini wa Tanzania.
Baada ya kumalizia tu makala haya, nilitazama mdahalo wa Barrack Obama (Democrats) dhidi ya Mitt Ronney (Republicans). Kinachodhihirika  hapa ni kwamba changamoto za kiuchumi, kibiashara na kimaendeleo ni sehemu ya maisha.  Tunastahili kujipanga, kujifunza na kujiendeleza kila siku ili kufanya vizuri katika masomo hayo ya maisha. Elimu, mafunzo, utafiti na ushauri viwe ni vitu vya mazoea na kawaida na sio vitu vya kukurupuka kukurupuka tu. Asiyejiendeleza hawezi kujiendeleza, wasiojiendeleza  hawawezi kuendelea.

No comments:

Post a Comment