Sunday, November 4, 2012
Tunajifunza kitu gani toka Utajiri wa Bakhressa ?
BIDHAA, viwanda na magari ya Bakhressa yanajulikana kuliko mwenyewe anavyojulikana. Somo la kwanza, umaarufu wa mtu unaotokana sio na kujisifia mwenyewe ila kile anachokizalisha na kukiuza au kukifanya na kukileta sokoni ni bora zaidi.
Moja kwa moja hili pamoja na mambo mengine ninayoyajua linanifanya kuamini kwamba bwana huyu amebahatika kuwa mtu mwenye kujitambua na anayejua anahitajiwa afanye nini katika dunia hii. Watu kama hawa huwa ni wachache sana duniani. Wengi wetu tupo, tupo tu, hata pale tunapopewa dhamana za juu katika makampuni au nchi. Na huwa tunaishi zaidi kwa kujinufaisha sisi na jamaa zetu na sio zaidi ya hapo. Wakati Bakhressa anaishi ili kuinufaisha nchi na sehemu kubwa ya Afrika na dunia. Haishi ili kuonekana ila anaishi ili anachokifanza kionekane na Mungu wake na dunia.
Ukubwa na utajiri sio ubwana bali ni utwana ni funzo jingine muhimu tunaloweza kujifunza tokana na utajiri wa mtu huyu mashuhuri asiyekimbiza sifa ila sifa zinazomkimbiza.
Taarifa za hivi karibuni zinazofichua utajiri wa Bakhressa na yeye kama mmojawapo wa matajiri wakubwa Afrika hazikuja kwa wengi kama kitu cha kushangaza. Watu walijua, wanajua, na wameendelea kujua kuwa Bakhressa ni tajiri asiye na makelele wala vishindo.
Kutokana na kutopenda sifa kwake ni kazi kweli kukutana au kukutanishwa naye. Lakini kutoka kwa watu wa karibu naye na uchambuzi binafsi wa maisha yake nimefanikiwa kuokota vitu viwili vitatu nitakavyowapatia.
Bwana huyu ni mchamungu nalo hili linaonekana wazi si katika vitendo na kauli zake tu bali pia katika bei ya bidhaa zake. Nina hakika uchamungu wake kwa kiasi fulani una mchango mkubwa katika utajiri alionao. Hii ni tofauti kabisa na viongozi na matajiri wetu walio wengi ambao wanadhani walichokipata na walichonacho kinatokana na akili na uwezo wao na sio mapenzi ya mungu.
Habari toka ndani zaidi zinasema kwamba bwana huyu huwa anaanza kazi baada tu ya swalati alfajiri na hatoki ofisini hadi saa nne usiku kama sio zaidi ya hapo. Hivi nani katika viongozi na matajiri wetu wengine anaweza akakipa kile anacholipwa mshahara au kinachomwingizia kipato zaidi ya masaa sita kwa siku? Ninaamini ni wachache sana. Na muda mwingi utakuwa unatumika kwa kujionyesha au kuzungumza mambo yasiyohusiana kabisa na kitu anachotakiwa kuwajibika.
Nikiikamata sifa hii hii, utagundua kuwa huyu bwana zaidi ya kusali sala 5 au zaidi kwa siku huwa hana muda na kitu kingine. Kwa hiyo, moja kwa moja gharama zake kimaisha ni ndogo mno, tofauti na viongozi na matajiri wetu wengi walivyo. Hana matanuzi, lakini si mchoyo wa zaka na sadaka na kodi ya serikali.
Kama ningeliikuwa shehe Saidi ninadhani ningeishia hapa. Ila nina hakika mtu wa kwanza kunikosoa atakuwa mhariri wangu. Makala yangu haitajaza nafasi iliyowekewa. Kwa hiyo, kwa kuwa kazi yetu ni kubwabwaja na hapa tunasifia sio mtu bali matunda ya mtu hebu tuendelee kidogo.
Huyu ni mmojawapo wa Watanzania wachache ambao wakati wanasiasa wetu wanapoteza muda kugombea nani atakuwa rais 2015/6; yeye yuko 'bize tu' na mananga kuhakikisha kwamba kila nyumba, kila duka, kila shule, kila hoteli na kila taasisi iwayo inakipata inachokihitaji kwa wakati.
Haiwezekani kila Mtanzania kuwa rais. Lakini inawwezekana kila mtu kuwa na mchango maalum wa kutoa kwa jamii ya Kitanzania. Bakhressa anaonesha kwa vitendo kuwa hili linawezekana. Na kwamba uongozi sio wa kisiasa tu, bali pia biashara ni uongozi na pengine bora zaidi.
Pamoja na kuwaachia wengine kukamata nafasi mbalimbali muhimu, bado ana muda na nguvu tosha ya kufuatilia na kudhibiti mambo pengine kutokana na uwezo wake binafsi au muundo wa kampuni au mfumo anaoutumia katika biashara zake.
Ili kuwa na huduma na bidhaa kama anazozalisha bwana huyu ni lazima uwe na rasilimali watu au wafanyakazi unaowajali na unaoangalia maslahi yao kwa kulhali. Wafanyakazi hao ndio wanaomuwezesha kufanikiwa katika mambo yake mbalimbali.
Tofauti na matangazo ya bidhaa za makampuni na watu wengine nchini upo ukweli kwa kiasi kikubwa kuhusu bidhaa za bwana huyu, hili likiwa na maana kwamba na yeye pia ni mkweli.
Wasifu wake unatufikisha wapi ?
Kwa kifupi tumeorodhesha sifa za Bakhresa kuwa ni pamoja na asiyetaka sifa binafsi; mchamungu; mkarimu; mpenda watu; mkweli; muadilifu; anatambua anachotakiwa kukifanya duniani; anaishi kutumikia wengine; mchapa kazi; ana iktisadi au mchache wa israfu na meneja au kiongozi daraja la kwanza.
Kwa maoni yangu,, bwana huyu ni kitabu kinachoishi cha menejimenti kinachostahili kutumiwa na viongozi wa kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiteknolojia na kiutamaduni ili Tanzania kupitia mfano wake iweze kuondokana na umaskini. Kama utajiri wake umetokana na Tanzania, basi kwanini Tanzania iwe maskini ikiwa angalau watu 1,000 tu watapatikana kuiga mfano wake?
Utajiri mkubwa wa bwana huyu umepatikana kutokana na mazao na bidhaa zinazotoka au zinazokuzwa hapahapa nchini. Vitu hivyo ni pamoja na nafaka, matunda, maji, maziwa, sukari na vitu kama hivyo. Nina hakika tungekuwa na sera nzuri za kodi, fedha na uchumi katika uchukuzi na usafirishaji pengine bwana huyu angetuwezesha pia kuwa na usafiri wa ndege, meli na mabasi ulio bora zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. Aanaonekana kuwa mbele zaidi ya wanasiasa na viongozi wetu kiuchumi na kiuongozi. Kiasi kwamba inabidi wamwekee breki hata pale breki hizo zinapokuwa sio kwa manufaa ya nchi na watu wake.
Je, viongozi wetu wa kisiasa wakizitazama sifa za kiongozi huyu wa kiuchumi na bila kuhofu wao ni vichuguu na yeye ni mlima Kilimanjaro hatuwezi kuambulia chochote hapa ?
Nina hakika mia kwa mia kwamba kama wilaya na mikoa yetu inaongozwa kama vile ni kampuni huru ndogo chini ya kampuni kubwa (nchi) na sio kama ofisi za chama tawala mapinduzi haya ya kiuchumi yaliyoasisiwa na Said Salim Bakhressa wa Tanzania ni kitu kinachoweza kupanuliwa zaidi na yakaishia sio kuifaa tu Tanzania bali Afrika na dunia nzima.
Sera inayohitajika hapa ni kuenzi vitu na watu wa ndani kwanza na sio kuchukuliwa na upepo wa uwekezaji ambao leo kwa mfano kwenye migodi ya dhahabu tunaona jinsi wanavyodanganya hata kwenye kile kidogo wanachotakiwa kutulipa. Kwa maneno mengine, ni muhali kwa nchi kujengwa na wawekezaji au watu kutoka nchi za nje bila kushirikishwa kikamilifu mzawa katika uleteaji nchi yake maendeleo ambaye na yeye pia ni mwanahisa.
Uchumi mikoani, wilayani
Kwa kukosa neno la kufaa pengine tunahitaji sera ya kuupelekea uchumi wetu mkoani na wilayani. Ukichukulia ule mfano wa kampuni niliouainisha hapo j uu ni kwamba kila wilaya na mkoa utaangalia rasilimali ilizonazo na kisha kuamua ni uzalishaji, huduma, biashara au shughuli gani zinazoweza kuukomboa mkoa au wilaya kiuchumi.
Hiki sio kitu kipya. Mikoa ya Nyanda za Juu kusini, mathalani iliaminika kwamba inaweza kulisha sio tu Tanzania bali Afrika Kusini na ya kati kwa nafaka za aina mbalimbali. Hata h ivyo, hadi wa leo miundombinu na mikakati ya kiuchumi na kibiashara inayoweza kufanikisha hilo bado haipo.
Kwa kifupi ni kwamba kuna mikoa na wilaya hapa nchini ambayo inaweza kutajirika na uvuvi tu au kilimo cha mboga na matunda tu au uchimbaji madini tu au sekta ya elimu (msingi, sekondari hadi vyuo) tu au mahospitali yanayopokea wagonjwa toka nchi za nje tu au kuwa na masoko na maduka ya mipakani na viwanja vya ndege, treni na mabasi tu au kwa utalii na huduma za hoteli tu. Hivi sasa tunajitawanya na kutapanya rasilimali chache tulizonazo ambazo badala ya kutusogeza mbele kimapato kunatukwamisha na kutuacha tusiojitosheleza hata kwa mahitaji yetu ya msingi.
Bakhressa hajajiingiza katika kila sekta ya uchumi. Amechagua. Na hizo alizochagua zimemfanya awe tajiri anayetambulika na dunia. Vivyo kila wilaya, kila mkoa, kila nchi (Tanganyika na Zanzibar ) inaweza kuchagua eneo moja la kiuchumi kama ndilo eneo lake la kuukimbia umaskini na kuanzia hapo ikawa hakuna kurudi nyuma tena ila kwa nchi nzima kuiga mfano wa Bakhressa-Inshallah!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment